Neno bughudha katika lugha ya Kiswahili ni nomino: [Ngeli: i-/zi-] yenye maana ya mambo yanayomkasirisha au kumuudhi mtu, maneno na vitendo vinavyomfanya mtu audhike.
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili bughudha linatokana na tendo-jina la Karabu bugh-dhwun بغض lenye maana ya chuki linalotokana na kitenzi cha Kiarabu baghadhwa (soma: baghadhwa/yabghadhwu/bugh-dhwan بغض، يبغض، بغضا) chenye maana zifuatazo:
1. Kuchukia.
2. Kuchukiza.
3. Kuchukiwa.
Kinachodhihiri ni kuwa neno bugh-dhwun بغض lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno bughudha lilichukua maana mpya ya maneno na vitendo vinavyomfanya mtu audhike, mambo yanayomkasirisha au kumuudhi mtu.
Kwa tatizo yake dawa, uanze kulisakama,
Mwishowe kulitatatua, kwa busara na hekima,
Wako moyo utapowa, furaha ukiifuma,
Halina thamani chozi, aliniusia mama.
Wakati tukifiliwa, mfano baba na mama,
Moyo hutaki kutuwa, machozi hujaa pima,
Vipi wanafufuliwa? mwisho vichwa vyatuuma,
Halina thamani chozi, aliniusia mama.
Tupatapo mitihani, ya mabonde na milima,
Mikono huwa kichwani, tulie olele mama,
Mwisho tunapata Soni, kulia mtu mzima,
Halina thamani chozi, aliniusia mama.
Nilikuwa bado kinda, alipofariki mama,
Kilio sikukishinda, nililia Kama kinda,
Huku kule nilikwenda, yani aamke mama,
Halina thamani chozi, aliniusia mama.
Siku niliyoamini, chozi halina salama,
Yangu hapo sithamini, kulivisha koja jema,
Machozi ni kitu duni, aminj ninayosema,.
Halina thamani chozi, aliniusia mama.
Kwa heri wanazuoni, ndugu zangu maulama,
Nimefika ukingoni, ndiyo yangu kaditama,
Kulialia ya nini, bure kujitia homa?
Halina thamani chozi, aliniusia mama.
Neno budi katika lugha ya Kiswahili ni nomino: [Ngeli: i-/zi-] yenye maana zifuatazo:
1. Jambo la lazima.
Msemo:
Sina budi kusafiri: lazima nisafiri. (Kamusi Kuu ya Kiswahili).
2. Suala linalomlazimu mtu kulitimiza.
Msemo:
Sina budi kuwasilisha mada yangu leo. (Kamusi ya Karne ya 21)
3. Nomino (Msemo) Sina budi kuja kesho: Lazima nitakuja kesho; Hapana budi : lazima. (Kamusi ya Kiswahili Sanifu-TUKI).
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili budi linatokana na neno la Kiarabu buddun (soma: buddun/buddan/buddin بد) lenye maana zifuatazo:
1. Sehemu ya kitu, mbadala, kutengana.
Waarabu hulitumia neno hili pamoja na herufi laa (لا), yaani: Laa budda لا بد kwa maana ya: hakuna mbadala, hakuna hiari, hakuna pa kukimbilia.
2. Sanamu, nyumba ya kuhifadhi sanamu.
Kinachodhihiri ni kuwa neno buddun بد lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno budi lilichukua maana ya Laa budda inayoashiria 'ulazima' katika Kiarabu lakini wakalipa neno lenyewe ' budi ' maana ya 'lazima' ambayo ikitanguliwa na neno ' hapana ' linaleta maana kinyume na kilichokusudiwa.
Neno ' budi ' lilipaswa kupewa maana ya hiari au kitu mbadala ili linapotanguliwa na neno ' hapana/sina' lilete maana ya ulazima.
VIJANA JENGENI KWENU
Yananipata mashaka, kwa vijana wa mijini,
Kwenu mlikoondoka, hivi kuna hali gani?
Nadhani kuna vichaka, nyoka yake masikani,
Kwenu jengeni jamani, nawausia vijana.
Kuna vijana wajanja, ukiwakuta mjini,
Nyumbani hana kiwanja, japo hukesha baani,
Si nyumba hata kichanja, kijana unafanyani?
Kwenu jengeni jamani, nawausia vijana.
Kiatu chake thamani, na mavazi ya fasheni,
Utadhani Sultani, kumbe kwao kichakani,
Kutazame kijijini, kijana aibu gani?
Kwenu jengeni jamani, nawausia vijana.
Nikitiwa hatiani, kudhani nimepotoka,
Mambo kuwa hadharani, mseme nimeropoka,
Mtunzi nishitakini, mahabusu kuniweka,
Kwenu jengeni jamani, nawausia vijana.
Kiwa ni njema kauli, kazi kaifanyieni,
Mlao mbuzi kwa wali, hali kwenu taabani,
Fikirini mara mbili, jipimeni kwa mzani,
Kwenu jengeni jamani, nawausia vijana.
Kama kwenu hukujenga, nawe raha unaponda,
Wala hujapata kinga, kupona hiki kidonda,
Shairi likupe mwanga, kwenu ukajenge nenda,
Kwenu jengeni jamani, nawausia vijana.
Neno *binamu* katika lugha ya Kiswahili ni *nomino: [Ngeli: a-/wa-*] yenye maana ya mtoto wa kike au wa kiume wa shangazi au mjomba.
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *binamu* limechukuliwa kutoka maneno mawili ya Kiarabu *bun (ibnu) بن/ابن na ammi (soma: ammun/amman/ammin عم).*
Neno *ibnu/bnu بن/ابن* lina maana ya mtoto wa kiume. Unaposema: Khamis bun Said, maana yake ni: Khamis mtoto wa kiume wa Said.
Watu wa Mauritania badala ya neno *bun بن* wao hutumia neno *walad ولد* neno la Kiarabu lenye maana ya mtoto wa kiume. Yaani: *Khamis bun Said* Wa-Mauritania husema: *Khamis Walad Said.*
Na neno *ammun عم* lina maana ya ndugu wa kiume wa baba.
Neno hilo pia lina maana ya kundi la watu wengi, majani (nyasi) na mtende mrefu.
Kinachodhihiri ni kuwa maneno ya Kiarabu *'ibnu ammi ابن عم* yenye maana ya mtoto wa kiume wa ndugu wa kiume wa baba yalipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *binamu* yalichukua maana mpya ya mtoto wa kike au wa kiume wa shangazi au mjomba.
*TANBIHI:*
Katika lugha ya Kiarabu neno *ibnu* hutumika katika lugha ya mafumbo kama vile:
1. *Ibnus Swulbi ابن الصلب* (mtoto wa uti wa mgongo) kwa maana ya mtoto halisi/mtoto halali kisheria.
2. *Ibnu Amsi/Albaariha ابن امس/البارحة* (mtoto wa jana) kwa maana ya mtu asiye na tajriba ya maisha.
3. *Ibnu Batwinihi ابن بطنه* (mtoto wa tumbo lake) kwa maana ya mchumia tumbo.
4. *Ibnu Jalaa ابن جلا* (mtoto wa wanja) kwa maana ya mtu mashuhuri maarufu.
5. *Ibnul Balad ابن البلد* (mtoto wa mjini) kwa maana ya mtu anayeishi katika mji aliozaliwa na kukulia.
6. *Ibnul Halaali ابن الحلال* (mtoto wa halali) kwa maana ya mtoto aliyezaliwa ndani ya ndoa ya kisheria.
Katika lugha ya Kiarabu, shangazi huitwa *ammat عمة* na mtoto wa shangazi huitwa *ibnu ammat ابن عمة* na mjomba huitwa *khaalun خال* na mtoto wa mjomba huitwa *ibnu Khaalin ابن خال.*
Neno *biladi* katika lugha ya Kiswahili ni *nomino: [Ngeli: i-/zi-*] yenye maana ya *mji* .
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *biladi* limechukuliwa kutoka neno la Kiarabu *'bilaad* *(soma: bilaadun/bilaadan/bilaadin بلاد)** likiwa ni wingi wa neno la Kiarabu *baldah (soma: baldatun/baldatan/baldatin بلدة)* lenye maana zifuatazo:
1. Eneo kubwa la ardhi.
2. Eneo maalumu la ardhi wanalokaa watu fulani lenye miji, vijiji na mipaka inayotambulika; *nchi*.
*Yaa baladii, yaa bilaadii يا بلادي، يا بلدي* Ee nchi yangu!
3. Sehemu ya nchi au mji.
4. Mji mdogo.
5. Chanzo.
Kinachodhihiri ni kuwa neno la Kiarabu *'bilaadun بلاد* lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *biladi* lilichukua kutoka lugha ya Kiarabu maana ya *mji* na kuziacha maana nyingine.
Neno *shukurani* katika lugha ya Kiswahili ni *nomino: [Ngeli: i-/zi-*] yenye maana ya maneno yanayotolewa kuonesha kuupokea kwa mikono miwili wema uliotendewa; *ahsante/asante.*
*Nahau* : *Toa shukurani:* sema ahsante.
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *shukurani* limechukuliwa kutoka neno la Kiarabu *'shukraan* *(soma: shukraanun/shukraanan/shukraanin شكران)** tendo-jina *Masdar مصدر* la *kitenzi* cha Kiarabu *shakara شكر* chenye maana zifuatazo:
1. Amemsifu na kumtaja mtu mwengine kwa wema kutokana na hisani aliyomfanyia.
2. Amemlipa mtu mwengine malipo fulani kwa kuifanya vizuri kazi aliyomtuma.
Kinachodhihiri ni kuwa neno la Kiarabu *'shukraanun شكران* lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *shukurani* halikubadili maana katika lugha ya Kiarabu.
Neno *biashara* katika lugha ya Kiswahili ni *nomino: [Ngeli: i-/zi-*] yenye maana ya mchakato wa kununua na kuuza mali au vitu.
*Biashara sukutu*: aina ya uuzaji na ununuaji wa bidhaa bila maongezi.
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *biashara* limechukuliwa kutoka maneno mawili ya Kiarabu *'bay-un* *(soma: bay-un/bay-an/bay-in بيع)** na *'shiraau* *(soma: shiraaun/shiraa-an/shiraain شراء)** yenye maana zifuatazo:
*Bay-un* ni:
1. Tendo-jina *Masdar مصدر* ya kitenzi cha Kiarabu *baa-a باع* chenye maana ya *ameuza* .
2. Kitendo cha kuchukua kitu na kulipa thamani yake.
3. Kitendo cha kutoa kitu na kuchukua thamani yake.
4. Bidhaa za kuuzwa.
Na *shiraau شراء* ni:
1. Kitendo cha kutaka kununua kitu na kulipa thamani yake.
2. Mahali pa kuuza na kununua; *suuq سوق*, *soko* .
Kinachodhihiri ni kuwa maneno mawili ya Kiarabu *'bay-un wa shiraa بيع و شراء* yalipoingia katika Kiswahili na yalitoholewa kuwa neno *biashara* na neno hili la Kiswahili halikubadili maana ya msingi ya maneno hayo ya Kiarabu, kuuza na kununua.