ETIMOLOJIA YA NENO "BINAMU'' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA NENO "BINAMU'' (/showthread.php?tid=2803) |
ETIMOLOJIA YA NENO "BINAMU'' - MwlMaeda - 08-14-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO "BINAMU'' Neno *binamu* katika lugha ya Kiswahili ni *nomino: [Ngeli: a-/wa-*] yenye maana ya mtoto wa kike au wa kiume wa shangazi au mjomba. Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *binamu* limechukuliwa kutoka maneno mawili ya Kiarabu *bun (ibnu) بن/ابن na ammi (soma: ammun/amman/ammin عم).* Neno *ibnu/bnu بن/ابن* lina maana ya mtoto wa kiume. Unaposema: Khamis bun Said, maana yake ni: Khamis mtoto wa kiume wa Said. Watu wa Mauritania badala ya neno *bun بن* wao hutumia neno *walad ولد* neno la Kiarabu lenye maana ya mtoto wa kiume. Yaani: *Khamis bun Said* Wa-Mauritania husema: *Khamis Walad Said.* Na neno *ammun عم* lina maana ya ndugu wa kiume wa baba. Neno hilo pia lina maana ya kundi la watu wengi, majani (nyasi) na mtende mrefu. Kinachodhihiri ni kuwa maneno ya Kiarabu *'ibnu ammi ابن عم* yenye maana ya mtoto wa kiume wa ndugu wa kiume wa baba yalipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *binamu* yalichukua maana mpya ya mtoto wa kike au wa kiume wa shangazi au mjomba. *TANBIHI:* Katika lugha ya Kiarabu neno *ibnu* hutumika katika lugha ya mafumbo kama vile: 1. *Ibnus Swulbi ابن الصلب* (mtoto wa uti wa mgongo) kwa maana ya mtoto halisi/mtoto halali kisheria. 2. *Ibnu Amsi/Albaariha ابن امس/البارحة* (mtoto wa jana) kwa maana ya mtu asiye na tajriba ya maisha. 3. *Ibnu Batwinihi ابن بطنه* (mtoto wa tumbo lake) kwa maana ya mchumia tumbo. 4. *Ibnu Jalaa ابن جلا* (mtoto wa wanja) kwa maana ya mtu mashuhuri maarufu. 5. *Ibnul Balad ابن البلد* (mtoto wa mjini) kwa maana ya mtu anayeishi katika mji aliozaliwa na kukulia. 6. *Ibnul Halaali ابن الحلال* (mtoto wa halali) kwa maana ya mtoto aliyezaliwa ndani ya ndoa ya kisheria. Katika lugha ya Kiarabu, shangazi huitwa *ammat عمة* na mtoto wa shangazi huitwa *ibnu ammat ابن عمة* na mjomba huitwa *khaalun خال* na mtoto wa mjomba huitwa *ibnu Khaalin ابن خال.* *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |