VIJANA JENGENI KWENU - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: VIJANA JENGENI KWENU (/showthread.php?tid=2805) |
VIJANA JENGENI KWENU - MwlMaeda - 08-21-2022 VIJANA JENGENI KWENU Yananipata mashaka, kwa vijana wa mijini, Kwenu mlikoondoka, hivi kuna hali gani? Nadhani kuna vichaka, nyoka yake masikani, Kwenu jengeni jamani, nawausia vijana. Kuna vijana wajanja, ukiwakuta mjini, Nyumbani hana kiwanja, japo hukesha baani, Si nyumba hata kichanja, kijana unafanyani? Kwenu jengeni jamani, nawausia vijana. Kiatu chake thamani, na mavazi ya fasheni, Utadhani Sultani, kumbe kwao kichakani, Kutazame kijijini, kijana aibu gani? Kwenu jengeni jamani, nawausia vijana. Kijana acha aibu, rudi kwenu ukajenge, Usitafute majibu, hoja yangu uichenge, Ninaona maajabu, hizo akili za kenge, Kwenu jengeni jamani, nawausia vijana. Nikitiwa hatiani, kudhani nimepotoka, Mambo kuwa hadharani, mseme nimeropoka, Mtunzi nishitakini, mahabusu kuniweka, Kwenu jengeni jamani, nawausia vijana. Kiwa ni njema kauli, kazi kaifanyieni, Mlao mbuzi kwa wali, hali kwenu taabani, Fikirini mara mbili, jipimeni kwa mzani, Kwenu jengeni jamani, nawausia vijana. Kama kwenu hukujenga, nawe raha unaponda, Wala hujapata kinga, kupona hiki kidonda, Shairi likupe mwanga, kwenu ukajenge nenda, Kwenu jengeni jamani, nawausia vijana. Sasa shairi nafunga, haya shime kijijini, Dhamira kwetu kujenga, initiayo huzuni, Japo mkono napunga, hatua zikuchueni, Kwenu jengeni jamani, nawausia vijana. Mtunzi: Filieda Sanga Mama B Mabibo Dsm 0753738704 |