MAKALA: USHAIRI WA KISWAHILI KATIKA NJIA PANDA: KUTUMIA AU KUTOTUMIA METHALI
Na
Joseph Nyehita Maitaria
Mwanafunzi wa Ph.D
Idara ya Kiswahili na Lugha za Kiafrika
Chuo Kikuu cha Kenyatta
Ikisiri
Makala hii inahakiki
mabadiliko ya kimtindo katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili.
Kwa mfano, hapo awali utungo huu ulitungwa kwa kuzingatia utamaduni wa Waswahili
kama jamii. Kwa wakati wa sasa unatungwa na wasanii kutoka jamii pana ya Afrika
Mashariki. Kipengele cha methali ni miongoni mwa zile maarufu katika tungo zilizozingatia
mno arudhi za kimapokeo. Aidha, baadhi ya wasanii wanawasilisha tungo zao kwa
kuzingatia zaidi kauli mahususi wanazobuni wanatumia kwa kadri au zile teule zinazopatikana
katika mapokeo ya jamii. Katika muktadha huu, ushairi wa Kiswahili una sifa
anuwai ambazo huweza kutumiwa kuubainisha. Kwa kuzingatia au kutozingatia matumizi
ya methali katika uwasilishaji, tungo hizi zinaweza kuainishwa kimakundi.
Kwa hivyo, ushairi wa
kisasa wa Kiswahili unaweza kuwa ni ule unaozingatia methali zaidi, chache au
ule unaoasi kabisa matumizi hayo. Swali ni kwamba, kati ya tungo zinazotumia au
zile zisizotumia methali katika uwasilishaji wake ni zipi zilizo bora?
USHAIRI
WA KISWAHILI KATIKA NJIA PANDA: KUTUMIA AU
KUTOTUMIA
METHALI
Na
Joseph
Nyehita Maitaria
Utangulizi
Makala hii inatathmini
mabadiliko katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili, hususan
ushairi huru. Tungo zinazozingatia arudhi za kimapokeo zimekuwa zikishirikisha
mno kipengele cha methali katika uwasilishaji wake kinyume na ushairi huru
ambao umekuwa hautumia sana matumizi hayo. Kadhalika, ushairi wa Kiswahili umepitia
mabadiliko mbalimbali ya kihistoria, kitamaduni na kijamii hadi kufikia hali yake
kwa wakati huu wa sasa. Kwa mfano, hapo awali ulikuwa ni utanzu maarufu miongoni
mwa waswahili kama jamii. Kwa wakati wa sasa ni utungo wa jamii pana ya Afrika
Mashariki na kwengineko kunakutumiwa lugha ya Kiswahili kama chombo cha mawasiliano.
Kutokana na maenezi ya
lugha ya Kiswahili kutoka Pwani ya Afrika Mashariki hadi bara, ushairi wa
Kiswahili umeweza kuenea na kupata umaarufu miongoni mwa jamii za Afrika
Mashariki. Kwa hivyo, watunzi wa ushairi wameweza kutunga tungo zao zinazoshirikisha
utamaduni mpana wa Afrika Mashariki kutokana na umaarufu wa maenezi ya lugha ya
Kiswahili. Kabla ya miaka ya sabini, ushairi wa Kiswahili ulitungwa kwa
kuzingatia zaidi arudhi za kimapokeo kama vile uzingativu wa idadi maalumu ya mizani,
mishororo, urari wa vina na ukariri wa vibwagizo. Baada ya miaka ya sabini, baadhi
ya washairi waliweza kujitupa ugani na kutunga tungo zao bila ya kuzingatia
zaidi arudhi za kimapokeo (Babusa 2005 na Chacha 1987). Kwa wakati huu wa sasa,
ushairi wa Kiswahili unawakilisha tungo unaozingatia zaidi arudhi za kimapokeo,
ule zilizozingatia sana arudhi hizo na zile zisizongatia kabisa arudhi hizo
katika utunzi na uwasilishaji wa utanzu huu. Hata hivyo, hizi ni tanzu za
ushairi wa Kiswhaili. Kwa hivyo, sura hii inafafanua jinsi matumizi ya methali
yanavyoweza kutumika kama kipengele muhimu cha kuainishia mabadiliko hayo
katika ushairi wa kisasa wa Kiswahili.
Uainishaji wa awali wa
Ushairi wa Kiswahili
Mpaka sasa utanzu wa
ushairi wa Kiswahili umeweza kuainishwa na baadhi ya wahakiki na waandishi wa
kifasihi kwa kuzingatia mitazamo tofauti tofauti. Maainisho hayo yanatokana na
baadhi ya tafiti zilizofanywa, kauli zinazotolewa na waandishi au watunzi wa
tungo wa Kiswahili. Miongoni mwa wainishaji hao ni kama: Babusa (2005), Masinde
(2003), Njogu na Chimerah (1999), Sanka (1995), Mazrui (1994), Noor (1988), Senkoro
(1988), Kandoro (1983), Kahigi na Mulokozi (1979), Kezilahabi (1974) na Abedi
(1954).
Kwa mfano, Masinde
(ibid), ameuainisha ushairi kwa kuzingatia kipengele cha mabadiliko ya maudhui
katika muktadha wa mpito wa kihistoria. Kwa kufanya hivyo, ameweza kuyaweka
mashairi hayo katika vipindi mahususi vya kihistoria. Kimsingi, ushairi wa
Kiswahili una tungo anuwai zenye kuwasilisha mada mbalimbali zinazotokana na
utamaduni na uhalisi wa maisha ya watu. Katika uwasilishaji wa sanaa hii, kuna matumizi
ya kauli mahususi za kauli za kimapokeo au zile zinazobuniwa kimakusudi na washairi
ili kuuathiri moyo na yanayochochea tafakuri ya msomaji.
Kwa kuzingatia kauli
teule za lugha, mshairi anaweza kuibusha masuala ambayo yanachoma au
yanayozindua moyo kupitia kwa taswira na istiari zinazoibushwa. Kwa hivyo,
uainishaji wa ushairi haupo tu katika kiwango cha maudhui, bali pia kwa kuzingatia
vipengele vya fani kama vile miundo, na maumbo, lugha mahsusi inayotumika na
usanii kwa jumla. Kulingana na nadharia ya semiotiki, mada au maudhui yale yale
yanaweza kusawiriwa upya kwa kuzingatia miundo badalia ya lugha (Jacobson 1960)
Zaidi ya maudhui katika
mkabala huu, Masinde amependekeza kuwa ushairi wa Kiswahili unaweza kuainishwa
kimakundi kama ifuatavyo:
Ø Ushairi
wa Kiswahili kabla ya kuja kwa wakoloni.
Ø Ushairi
wa Kiswahili wakati wa utawala wa kiarabu.
Ø Ushairi
wa Kiswahili wakati wa utawala wa kizungu.
Ø Ushairi
wa Kiswahili baada ya uhuru.
Ø Kuzingatia
kipengele cha muundo.
Ø Kuzingatia
kipengele cha mtindo.
Ø Kuzingatia
utendakazi wake.
Uhakiki wa Masinde
umebainisha kuwa ushairi wa Kiswahili unaweza kuainishwa kimakundi kwa
kuzingatia maudhui yanayoibushwa katika miktadha mbalimbali ya kiwakati au
kihistoria. Mwelekeo huu unajitokeza wazi katika makundi manne ya kihistoria
(Taz. Vipengele i, ii, iii na iv) ambapo amevitolea ufafanuzi wa kina kurejelea
vipindi hivyo mahususi. Hata hivyo, uainishaji huo umegusia pia vipengele
muhimu kama vile umuundo, mtindo na utendakazi wa ushairi (Taz. Vipengele v, vi
na vii).
Vipengele hivi vitatu
pia vya msingi na vinavyohitaji kutolewa maelezo na ithibati Kwa ambavyo ni
mapendekezo yanayohusu vigezo vya kijumla vinavyoweza kuzingatiwa, Masinde
hakuvitolea ufafanuzi wala kueleza jinsi vinavyoweza kutumiwa katika uainishaji
wa ushairi wa Kiswahili Kwa kurejelea mwelekeo na mapendekezo ya Masinde,
Babusa (2005) ameyaainisha mashairi ya Kiswahili kimaudhui na pia kudhihirisha
kwa kiwango fulani kuwa, kipengele cha muundo kinaweza kutumiwa katika uainishaji
wa mashairi hayo. Kwa kuzingatia kipengele cha muundo, Babusa amebainisha sura
mbalimbali zinazoibuka na ameyaweka mashairi hayo katika maumbo au bahari mbalimbali
za ushairi. Kulingana na bahari hizo ni kwamba, ushairi wa Kiswahili unawakilishwa
kwa miundo maalumu ya lugha kama vile uzingativu wa msamiati teule, sajili za
lugha na lahaja. Hata hivyo, kinachobainika katika maelezo ya Babusa ni kwamba,
umbo au muundo katika ushairi wa Kiswahili unajibainisha zaidi kupitia kwa wa
uwasilishaji.
Naye Kezilahabi (1973),
ameonyesha jinsi ushairi wa Kiswahili unavyoweza kuainishwa kwa kuzingatia
nyakati tatu maalumu za urasmi kama ifuatavo:
Ø Wakati
wa urasmi-mkongwe (1728-1885)
Ø Wakati
wa urasmi-mpya (1945-1960)
Ø Wakati
wa usasa (1967 hadi sasa)
Kulingana na
Kezilahabi, urasimi ni wakati ambapo misingi maalumu ya kazi za sanaa huwekwa
na kukubalika kuwa vipimo bora vya kazi nyinginezo za kisanaa. Katika muktadha
wa Waswahili, ushairi ulipasa kutungwa na kuwasilishwa kwa uelekezi wa baadhi
ya vipengele vifuatavyo:
Ø Idadi
maalumu ya mizani
Ø Urari
wa vina
Ø Umbo
Ø Maudhui
yanayojikita katika maadili
Ø Lugha
isiyo na utusani
Ø Mtiririko
au ushikamano wa mawazo kutoka ubeti hadi ubeti
Ø Kuimbika
kutokana na matumizi ya vina na mizani
Ø Utaratibu
wa uwasilishaji: mwanzo, kati na mwisho.
Basadhiya vipengele
hivyo viliidhinishwa na vilichukuliwa kuwa „roho‟ ya ushairi wa Kiswahili
katika kipindi cha urasmi. Mashairi ambayo yalikiuka utaratibu huo yalikemewa
na kupuuzwa (Kandoro 1983, Abedi 1954). Katika miaka ya sabini hapa Afrika ya
Mashariki, baadhi ya watunzi kutoka bara pia walianza kuwasilisha tungo zao kwa
kuziasi baadhi ya kaida hizo (Senkoro 1988 na Kahigi na Mulokozi 1979). Huu ulichukuliwa
na baadhi ya washairi wa kimapokeo kuwa ni dosari na uchafuzi wa ushairi wa
Kiswahili uliokuwepo. Mwelekeo huu unaweza kupata uelekezo kupitia kwa mihimili
ya nadharia ya Fomula ya kisimulizi ambapo kinachopendekezwa ni uzingativu wa
kauli teule za kimapokeo na maudhui yanayojikita katika uhalisi na utamaduni wa
jamii (Fowler 1966). Kuhusu ukiushi wa kaida, nadharia ya semiotiki inatoa
mwelekeo kwamba, kazi ya fasihi inaweza kuwasilishwa kwa mitindo tofauti
tofauti ilimradi ujumbe umefasiriwa kwa uzingativu wa utamaduni wa jamii
(Barthes 1981 na Eco 1976).
Hapo awali, Kiswahili
kilikuwa ni lugha ya wakaziwa pwani ya Afrika Mashariki na baadaye kuenea bara
kadhalika ushairi wa Kiswahili umeweza kuwekwa katika makundi mawili mahususi:
ushairi unaowasilishwa katika mazingira ya pwani na ule unaozingatia mazingira
ya bara. Mwelekeo huu usipozingatiwa hauwezi kuuchukulia ushairi wa Kiswahili
kwa upana wake. Kwa sababu hivi sasa utanzu huu unashirikisha tungo zinazotungwa
na jamii pana ya Afrika Mashariki na popote pale ambapo Kiswahili kinatumika
kama chombo cha mawasiliano. Vile vile, kutokana na kiumbiumbi cha mgogoro wa
ushairi kuhusu kutumia au kutokutumia baadhi ya arudhi za kimapokeo kama vile
vina na urari wa mizani ushairi wa Kiswahili umeweza kuwekwa katika matapo
mawili: ushairi unaozingatia arudhi za kimapokeo na ule usiozingatia arudhi za kimapokeo
katika utunzi na uwasilishaji wake (Sanka 1995 na Gibbe 1990)
Pia, ushairi kama
utungo wa fasihi umeainishwa kwa kuzingatia idadi maalumu ya mishororo katika
beti (Noor 1988, Kandoro 1983 na Abedi 1954). Zaidi ya kuzingatia idadi
mahususi ya mishororo, mizani na urari wa vina katika ubeti, ushairi wa
Kiswahili uliainishwa katika tanzu mbalimbali kutokana na:
Ø Urari
wa vina katika mistari au mishororo katika beti.
Ø Mpangilio
wa maneno katika mistari au mishoro katika beti.
Ø Idadi
ya vipande katika mistari au mishororo katika beti.
Ø Idadi
maalumu ya mizani katika mistari au mishororo katika beti.
Katika muktadha wa
vipengele hivyo vinne, muundo na maumbo ya ushairi huweza pia kuainishwa zaidi
kama ifuatavyo:
Ø Tathnitha
– shairi ambalo lina mishororo miwili katika kila beti.
Ø Tathlitha
– shairi ambalo lina mishororo mitatu katika kila beti.
Ø Tarbia
– shairi ambalo lina mishororo minne katika kila beti.
Ø Takhmisa
– shairi ambalo lina mishororo minne katika kila beti.
Ø Tashlita
– shairi ambalo lina mishororo sita katika kila beti.
Ø Ushairi
ambao una zaidi ya mishororo sita.
Masivina – shairi
ambalo lina mlingano wa mizani katika mishororo lakini si urari wa vina.
Ukawafi
– shairi ambalo lina vipande vitatu katika kila mshororo.
Msuko
– shairi ambalo lina kibwagizo kifupi.
Sakarani
– shairi ambalo linashirikisha bahari mbalimbali.
Kikwamba
–
shairi ambalo linarudia neno moja katika kila mwanzo wa beti.
Kulingana na Wafula na
Njogu (2007) na Mohamed (1990), ni katika kipindi cha urasimi mpya katika
fasihi ya Kiswahili ambapo palizuka istilahi maalumu za kuelezea dhana mbalimbali
za ushairi wa Kiswahili. Istilahi hizo zilizotumika zaidi ni kama:
Mshororo
– ambao ni mstari katika shairi
Mwanzo
– mstari au mshororo wa kwanza katika ubeti
Mloto
– mstari au mshororo wa pili katika ueti
Mleo
– Mstari au mshororo wa tatu katika ubeti
Kipokeo
– Mstari au mshororo wa mwisho katika ubeti
Ukwapi
– Sehemu ya kwanza katika mshororo
Utao
– Sehemu ya pili kaitka mshororo
Mwandamizi
– Sehemu ya tatu katika mshororo
Tabdila
– Kifupisho cha sauti kaitka neno linalotumika katika mshororo bila ya
kubadilisha maana ya msingi.
Inkisari
– Kunga ya kufupisha maneno katika mshororo
Mazida
– Kunga ya kurefusha neno bila ya kupotosha maana ya asili.
Kimsingi, istilahi hizi
zilitumika kimakusudi kwa malengo ya kuutambulisha ushairi wa Kiswahili. Katika
muktadha wa nadharia ya Fomula ya kisimulizi ni kwamba, uwepo wa bahari na
istilahi maalumu zinazotumika katika ushairi ni njia mojawapo ya kubainisha tanzu
za ushairi na fasihi kwa ujumla. Uainishaji huo unazingatia zaidi ushairi wa Kiswahili
unaotungwa katika muktadha wa arudhi za kimapokeo (King‟ei na Kemoli 2001).
Hata hivyo, inabainika kuwa ushairi wa Kiswahili usiozingatia arudhi hizo
katika utunzi na uwasilishaji haushirikishwi katika uainishaji. Zaidi ya hayo,
makala hii inapendekeza matumizi ya methali kama kipengele kinachoweza kutumika
katika kuainishia mabadiliko ya kiutunzi yanayobainika katika ushairi wa kisasa
wa Kiswahili.
Hii ni kwa sababu, kwa
wakati huu wa sasa kuna mashairi ambayo yanazingatia zaidi arudhi za kimapokeo,
yale yasiyozingatia mno arudhi za kimapokeo na yale yasiyozingatia kabisa arudhi
za kimapokeo katika utunzi na uwasilishaji wake. Makundi hayo matatu katika
ushairi wa Kiswahili yanadhihirisha kuwa:
Ushairi wa kimapokeo
unajitenga kwa kiasi fulani na ushairi huru lakini una ukuruba na ushairi wa
kati. Ushairi wa kati unazingatia zaidi mbinu za utunzi zinazopatikana katika ushairi
wa kimapokeo na ule wa ushairi huru.
Ushairi huru unajitenga
zaidi na ushairi wa kimapokeo kwa upande wa umuundo na kiumbo.
Kwa hivyo, ushairi wa
Kiswahili una tanzu zake ambazo zinawiana katika utunzi na uwasilishaji wake.
Hata hivyo, tofauti zinazobainika si za msingi zinazoweza kuzifanya tanzu hizo
kutalikiana. Kwa mfano, tungo hizi huzingatia zaidi lugha ya kimafumbo, kitaashira,
kiistiari, kitashbiha, kitashihisi miongoni mwa kunga zingine za uwasilishaji. Kimsingi,
kauli za lugha zinazotumika mno katika uwasilishaji ni zile zinazojibainisha katika
tamathali za usemi.
Kwa maoni ya Mwandishi
ni kwamba, matumizi ya methali yanapozingatiwa, ushairi andishi wa kisasa wa
Kiswahili unaweza kuainishwa kwa mwafaka zaidi. Hapa ieleweke kuwa, ushairi wa
Kiswahili umepitia mabadiliko mbalimbali hadi kufikia hali yake ya sasa (Kimaro
2008, Masinde 2003, Momanyi 1998 na Sanka 1995). Aidha, ushairi wa Kiswahili
unaweza kutumia methali nyingi, chache ama kutokutumia kabisa katika utunzi na
uwasilishaji wake kutegemea mahitaji ya kimtindo na mwelekeo wa mtunzi. Katika misingi
hii ya kurunzi tatu (ushairi wa kimapokeo kati na huru) za kimuundo, ushairi wa
Kiswahili unakuwa katika njia panda. Kwa kuzingatia namna methali zinavyotumiwa
katika utunzi na uwasilishaji wa utungo huu, upanda wake unaweza kubainishwa
Uainishaji wa Ushairi
wa Kiswahili unaopendekezwa
Matumizi ya methali
yanapozingatiwa, ushairi wa Kiswahili unaweza kuainishwa zaidi kwa kuzingatia
kutumiwa au kutotumiwa kwa methali kama ifuatayo:
Ushairi wa Kiswahili
unaotumia methali kama anwani
Ushairi wa Kiswahili
unaotumia methali moja
Ushairi wa Kiswahili
unaotumia methali nusu
Ushairi wa Kiswahili
unaotumia methali mbili (au zaidi)
Ushairi wa Kiswahili
unaotumia methali kama kauli
Ushairi wa Kiswahili
unaotumia methali kama kibwagizo (au kiishilio)
Ushairi wa Kiswahili
uso methali
Zaidi ya hayo, kila
kikundi cha ushairi kinaweza kupendekezewa jina mahususi kuwa kitambulisho
chake. Mbinu iliyotumika katika uundaji wa istilahi hizo za majina ni ile ya kuunganisha
viambishi awali vya maneno yanayopatikana katika kila kikundi. Majina hayo
yanayopendekezwa ni kama yafuatayo:
Ukimea –
Ushairi wa Kiswahili unaotumia methali kama anwani.
Ukimemo –
Ushairi wa Kiswahili unaotumia methali moja.
Ukimenu –
Ushairi wa Kiswahili unaotumia methali nusu.
Ukimembi –
Ushairi wa Kiswahili unaotumia methali mbili (au zaidi).
Ukimeka –
Ushairi wa Kiswahili unaotumia methali kama kauli.
Ukimeki –
Ushairi wa Kiswahili unaotumia kama kibwagizo (au kiishilio).
Ukimeso –
Ushairi wa Kiswhaili uso methali.
Kwa uelekezi wa
mihimili ya nadharia ya Fomula ya Kisimulizi, uainishaji huu unazingatia
kwamba, utunzi na uwasilishaji wa ushairi hushirikisha kauli teule zinazopatikana
katika mawasiliano ya jamii (Propp 1968). Vile vile, kwa kuzingatia mihimili ya
nadharia ya Semiotiki, methali kama ishara mahususi zinazotumika katika utunzi
na uwasilishaji wa tanzu mahsusi za kifasihi huweza kubadilika, kufifia au kutoweka
kulingana na mabadiliko ya utamaduni wa jamii (Nagler 1974) Katika muktadha
huu, methali kama ishara zinazotumika katika ushairi wa Kiswahili huweza kufasirika
au kufafanuliwa zaidi katika miktadha mahususi ya utamaduni wa jamii. Kwa hivyo,
matumizi ya methali katika ushairi wa kisasa wa Kiswahili huweza kutekelezwa kwa
kuzingatia kauli zingine zinazobuniwa kimakusudi na watunzi.
Ushairi wa Kiswahili
uso Methali
Katika makala hii
kitengo hiki cha ushairi wa Kiswhaili kitajumuisha tungo ambazo hazina kabisa
matumizi ya methali katika uwasilishaji wake. Kama ilivyokwisha kuelezwa hapo
awali „mgogoro‟ katika ushairi wa Kiswahili uliweza kuendelezwa rasmi wakati
ambapo baadhi ya watunzi wa ushairi walipoanza kutunga tungo ambazo hazikujikita
katika arudhi za kimapokeo. Kwa mfano, katika miaka ya sabini walitokea “watundu”
watatu: Hussein (1970), Kezilahabi (1974) na Angira (1970). Baadaye kikundi
hiki kilipata wafuasi wengine kama vile: Mulokozi na Kahigi (1973) na Mberia (1997).
Hawa walitunga na kuwasilisha kimaandishi tungo zao za mashairi bila kujali au kuzingatia
arudhi za kimapokeo ambazo zilichukuliwa kuwa ni „uti wa mgongo‟ katika uwasilishaji
wa ushairi wa Kiswahili (Njogu na Chimerah 1999 na Senkoro 1988).
Kimsingi, “mgogoro” huu
ulijikita katika kutumia au kutokutumia vipengele vya arudhi za kimapokeo kama
vile mizani na urari wa vina kuwa ni uti mgongo katika utunzi na uwasilishaji
wa ushairi wa Kiswahili (Walibora 2007 na Njogu 1998). Hii ni kwa sababu,
baadhi ya wahakiki na waandishi katika wakati huu wa sasa wana mawazo kwamba
ushairi wa Kiswahili haupaswi kuelekezwa kwa uzingativu wa vina na mizani maalumu
katika uwasilishaji wa tungo hizi.
Mawazo hayo yaliibua
hisi na mielekeo tofauti tofauti miongoni mwa baadhi ya watunzi na wahakiki wa
fasihi ya Kiswahili. Mitazamo hii ilizua mirengo miwili ya kimwelekeo: wale
wanaoshikilia mno na wale wasioshikilia zaidi kuwa urari wa vina na idadi maalumu
ya mizani ni mambo ya lazima katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili.
Kila kikundi cha washairi kilishikilia msimamo wake (Sanka 1995 na Mulokozi na
Kahigi 1979). Kwa hivi sasa, mashairi yanayotungwa kwa mitindo na mitazamo hii
miwili yamekubalika kuwa ni tanzu za ushairi wa kisasa wa Kiswahili.
Kulingana na Babusa
(2005) na Gibbe (1998), tungo hizi ni tanzu za ushairi wa Kiswahili.
Athari ya Maenezi ya Lugha
ya Kiswahili kutoka Pwani hadi Bara ya
Afrika Mashariki
Kwa wakati huu wa sasa,
ushairi wa Kiswahili unatungwa na kuwasilishwa kwa kuzingatia arydhi au
kutozingatia arudhi za kimapokeo. Hata hivyo tungo hizi ni sura mbili za sarafu
moja ambazo zinajengana na kukamilishana ingawa kwa uzingativu wa mitindo
tofauti tofauti. Kimsingi, hii leo Kiswahili si lugha ya Waswahili kama jamii
ya pwani tu kama ilivyokuwa katika karne mbili zilizopita ila matumizi yake
yameimarika na kuwa chombo cha kuwasilishia utamaduni wa jamii ya Afrika
Mashariki kwa ujumla (Kimaro 2008, Masinde 2003 na Momanyi 1998. Kwa hivyo,
mabadiliko hayo pia yaliweza kuwa na athari kubwa katika utunzi na uwasilishaji
wa tanzu za fasihi ya Kiswahili, hususan ushairi wa Kiswahili (Wafula na Njogu
2007, Chacha 1987).
Katika muktadha wa
uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili ni utungo wa jamii ya Afrika Mashariki na
kwa jamii zote zinazotumia lugha ya Kiswahili kama chombo cha mawasiliano
miongoni mwao. Ingawa kwa sasa makabiliano hayo hayapo au yanaendelezwa
kichinichini, utungo huu umekubalika na unaendelea kuzishughulisha kalamu za
watunzi wa pwani na hata bara ya Afrika Mashariki. Kama chombo kisuluhishi cha
uponda katika uwasilishaji wa utungo huu,methali zinaweza kutumika kama
kipengele cha kushirikishia mielekeo hiyo miwili katika ushairi wa kisasa wa
Kiswahili. Katika
muktadha wa nadharia ya semiotiki ni kwamba, dhima ya ishara moja huweza kupata
mshabaha au utekelezaji wake unaweza kupitia kwa ishara nyingine zinazopatikana
kwa urahisi katika jamii (Hawkes 1977).
Kulingana na mtazamo wa
wahakiki wa fasihi, utunzi na uwasilishaji wa mashairi huweza kuwa yenye maumbo
na miundo inayotofautiana lakini yenye kutekeleza dhima sawa ya kuuimarisha na
kuustawisha utanzu huu wa fasihi. (King‟ei 2007). Hoja hii ina mshabaha wake
katika maelezo ya Khan (1975) kwamba, mshairi anapotunga utungo huwa na lengo
la kumvutia msomaji wake. Kwa hivyo, msanii huwa na hadhari zaidi katika kuteua
kauli za lugha anazozishirikisha ili shairi lake lisije likakinaisha wasomaji wake.
Kwamba anapokabiliwa na hatari hii ya kuichosha hadhira yake, huanza kulipamba
shairi lake kwa kutumia kunga mbalimbali za lugha zinazotokana na tamathali za
usemi Andrzejewski 2011). Katika mantiki hii, mtunzi anaweza kwa hiari
kutotumia methali na kuibua matumizi ya kauli zingine mahususi za lugha ambazo
zinajibainisha zaidi katika tamathali za usemi. Kwa hivyo, matumizi ya methali
yanaweza kuwa si ya lazima katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi.
Matumizi ya kauli
zinazoibuliwa kibinafsi na mshairi huweza pia kujenga msingi wa kuuwasilishia
tungo kijazanda, kiistiari, kitaashira kitaswira na kimafumbo (Akporobaro 1994).
Kwa sababu uwasilishaji wa ujumbe katika utanzu wa fasihi, hususan ule wa ushairi
huwa hauna fasiri moja. Kimsingi, matumizi ya methali huwa yana maana ya kijuujuu
na batini (Wamitila 2005) Hata hivyo, maana inayokusudiwa huweza kubainishwa
kupitia kwa muktadha mahususi unaoibuliwa na mtunzi. Kwa hivyo, ufasiri huu
hutegemea jinsi mtunzi alivyoufumba ujumbe na jinsi mpokezi anavyolikabili
shairi hilo tangu mwanzo; mradi tu aweze kuthibitishia hoja zake kwa mifano
dhahiri inayotokana na miktadha halisi katika utamaduni wa jamii. Kwa hivyo,
ushairi wa Kiswahili unaweza kuwasilishwa kupitia kwa kauli au miundo tofauti
tofauti ya lugha ambayo si lazima ziwe za kimethali. Isitoshe, usomaji wa
ushairi wa Kiswahili haukamiliki pasipo hadhira maalum ya kuupokea ujumbe au
maana inayokusudiwa katika utungo. Kwa sababu kauli zinazotumika katika uwasilishaji
wa ushairi huifinya au huipanua maana inayowasilishwa.
Suala la Lugha ya
kawaida katika Ushairi wa Kiswahili
Baadhi ya watunzi wa
ushairi wa kisasa wa Kiswahili wana mawazo kwamba lugha wanayoitumia katika
uwasilishaji wao ni ya „kawaida‟ ili kuuleta ushairi huo karibu na watu wa kawaida
katika jamii (Kezilahabi 1974). Dhana ya „kawaida‟ hapa kama inavyotumiwa na
baadhi ya watunzi na wahakiki wa kifasihi ina utata. Kwa sababu baadhi ya
mashairi yanayotungwa na „watundu‟ au „wanamabadiliko‟ yana kiwango fulani cha
ugumu katika ufasiri wake Kwa mfano,mshairi Kezilahabi katika shairi “Mafahari
Wapigana”, ametumia kauli za kawaida kama vile: Mafahali wanono, kichunguu
mchwa kivumbi hicho ndio askari na kilikuwa kivumbi hicho.Kauli hizi ni za kawaida
lakini ni za kustiari ambapo msomaji anahitaji kupiga bongo katika utafakari wa
ujumbe. Kimsingi, mashairi haya yanakusudiwa kusomwa na tabaka la wasomi
hususan wanafunzi wa vyuo vikuu au wenye uwezo wa juu wa kiufasiri. Kimatumizi,
mpangilio usio wa kawaida ni kivutio cha udadisi zaidi kuliko lugha ya kawaida
(Mulokozi 2008).
Hii inatokana na ukweli
kwamba, kauli zinazoteuliwa na kutumiwa katika mawasiliano ya jamii husisitiza
zaidi vipengele fulani vya hisi na mawazo ya mwasilishaji (Maitaria 1991 na
Parker 1974). Katika muktadha wa utunzi na uwasilishaji wa shairi ujumbe unaowasilishwa
si wa kidhahania bali pia ni kauli zinazotumika hubainisha hisi za mtunzi kuhusu
yale aliyoathirika nayo katika uhalisi wa maisha.
Ushairi unaotumia
methali huuweka ujumbe unaowasilishwa katika muktadha wa utamaduni unaozoeleka
katika jamii. Kwa mfano, Abdalla (1973:19) ametumia methali ya Mpiga ngumi
ukuta , huumiza mkonowe katika ubeti ufatao: Ndipo kunipiga vita nisivyojua
mwanzowe ulotafuta mepata , hasara ni kwwako wewe mpiga ukuta huumiza mkonowe
wapigiyani mayowe? (Ubeti wa 17). Matumizi ya methali hii yanadhirisha ukiukaji
wa maadili katika jamii. Kwamba, binadamu wanapasa kuonekana imami wa kusaidiana
lakini mwafaka huu unakiukiwa na baadhi ya watu. Hii ni kwa sababu, methali
zinazotumika katika uwasilishaji wa ushairi ni kauli ambazo zimesheheni hekima na
busara ya jamii. Kama alivyo mtunzi mahiri wa fasihi, mshairi asiyetumia
methali huwa haridhiki katika kutumia miundo ya lugha ambayo imekuwepo tu
katika mapokeo ya jamii. Kwa hivyo, mshairi huhiari kushirikisha miundo mipya
na kwa uelekezo wa hisi zake ili kuutoa utungo huu kutoka kwa miundo ya lugha
inayozowewa. Kwa kufanya hivyo, huupa utungo huu upya wa kimaono na kimtazamo
katika uwasilishaji wake.
Kadhalika, wa mtafiti,
miundo ya lugha iliyozoweleka katika jamii huweza kuwa chakavu, ambapo
kimatumizi hupuuzwa au huweza kuvyazwa upya ili mtumizi yake yawe yenye uhai
unaostahili. Jambo la muhimu linalopaswa kwa watunzi na wahakiki wa ushairi
huru wa Kiswahili ni kubainisha zaidi sifa za kimsingi katika uwasilishaji wa utungo
huu. Kwa mfano, ushairi wa kimapokeo una sifa zake zinazoubainisha kinyume na
hali ilivyo katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi huru. Swali linaloweza
kuulizwa ni kwamba; iwapo mtunzi wa ushairi anapouwasilisha utungo wake pasi na
kuzingatia arudhi za kimapokeo ni ushairi huru? 3 Kimsingi, ushairi kama utanzu
wa fasihi ni sanaa iliyo hai. Kwa hivyo, mabadiliko ya kijamii huweza kuathiri
maudhui yanayoibushwa na fani inayotumika katika uwasilishaji wa utunzu huu.
Hata hivyo, ugumu au wepesi wa uwasilishaji na ufasiri katika ushairi wa
Kiswahili hutegemea kauli mahususi zinazotumiwa na mshairi. Katika muktadha
huu, ushairi unaweza ama kutumia au kutotumia methali na wakati uo huo ujumbe
huweza kuwasilishwa kwa mshindo unaostahili. Isitoshe, uwasilishaji wa ushairi
wa Kiswahili usiotumia methali, hutumia kauli teule za lugha ambazo pia
hujikita zaidi katika tamathali za usemi.
Kutotumia Methali
katika uwasilishaji wa Ushairi
Sawia na matumizi ya
methali katika mawasiliano ya jamii na pia katika uwasilishaji wa ushairi huu
wa ukimeso, ujumbe unaoibushwa huweza kufasiriwa kwa uzingativu wa utamaduni
na uhalisi wa jamii husika. Vilevile, lugha ya ushairi wa Kiswahili hutumia vipengele
ambavyo hujenga na huchochea usaili na utafakari katika akili ya hadhira. Japo
ushairi huru hautumii kwa uangavu methali mahususi, maudhui yanayoibushwa huwa
yana mwangwi wa methali unaotawala na unaohisika.
Shairi la „Mruko wa
Nyuki‟ katika Bara Jingine (Mberia 2001:20-25) ni mfano wa utungo
usiotumia methali yoyote katika uwasilishaji wake. Hali hii inatokana na muundo
na mtindo wa kiuwasilishaji au kutokana na mwelekeo wa mtunzi. Hata hivyo,
mwangwi wa methali unatawala katika uwasilishaji wa maudhui. Shairi hili
limewasilishwa kimchoro ambapo taswira ya kimaono inayoibushwa ni ile ya jamii
ambayo hapo awali ilikuwa yenye ushikamano na ushirikiano. Baadaye, ushikamano
huo uliathirika kutokana na utamaduni wa kigeni. Hatimaye wanajamii
walihamasishana na kuurejelea msingi wa utamaduni wao wa awali. Kwa hivyo,
mshairi anadhihirisha suala hili kwa uelekezo wa mchoro na hata kupitia kwa
jinsi anavyoandika maneno kama vile kupitia kwa maelezo yanayozingatiwa, hadhira
inaweza kujenga mwelekeo fulani kwa kurejelea methali yoyote inayostahiki. Kwa
mfano methali kama: „Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu‟ au „kidole kimoja
hakivunji chawa, zinaweza,‟ kusadifu katika kuupatanisha ujumbe unaowasilishwa.
Hata hivyo, eleweke kuwa upatanisho huu unahitaji utafakari na uzingativu wa
methali zilizopo katika utamaduni wa jamii. Kwa njia hii hadhira inashirikishwa
kiustadi katika upokezi wa ujumbe.
Kwa ambavyo methali ni
kauli ambazo zimezoweleka katika jamii na pia zimetumika mno katika utunzi na
uwasilishaji wa mashairi mengi ya kimapokeo, mtunzi wa ushairi usiotumia
methali humwachia msomaji wake kuupatanisha ujumbe unaoibuliwa na methali
yoyote maarufu anayoitaka. Katika muktadha huu, msomaji anashirikishwa kikamilifu
katika harakati za upokezi wa ujumbe. Hii ni mbinu ya msingi katika uwasilishaji
wa tanzu za fasihi simulizi.(Kunemah 2008). Hapa ieleweke kuwa, methali ni
misemo au kauli fupi yenye hekima fulani na hudhihirisha mkusanyiko na mafunzo waliyoyapata
watu wa vizazi vingi vya jumuiya fulani katika maisha yao (Mazrui na Syambo
1992). Kwa mintarafu hii, methali inakuwa ni sehemu moja ya lugha inayoweza
kusawiri na kubaini falsafa na matamanio ya jamii kuhusu maisha kwa jumla; hadhira
nayo huweza kuichopoa yoyote na kuipatanisha na ujumbe anaowasilishwa
katika shairi.
Kimaudhui, methali
zimesheheni tajriba ya jamii ambapo kila tamko au tendo linaloshuhudiwa katika
jamii huweza kupatanishwa na kauli mahususi ya methali.
Kadhalika, uhalisi huu
unadhihirisha kwamba, uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili unaweza kuzingatia
au kutozingatia baadhi ya kauli ambazo zimekuwa zikirithishwa kimapokeo kutoka
kizazi kimoja hadi kingine. Kwa hivyo, si shuruti kwamba ushairi wa Kiswahili
uweze kuwasilishwa kwa maumbo, miundo na mitindo ya lugha ile ile ya miaka
nenda miaka rudi. Kimsingi, kauli ambazo zimekuwepo katika mawasiliano ya jamii
kwa muda mrefu huweza kuwa chakavu na kushosha. Kwa hivyo watu hupendelea mno
kauli mpya kama zile zinazobuniwa kibinafsi na wanafunzi wa ushairi. Kauli hizi
ni maarufu miongoni wa vijana na zinaweza kuwasilishia mawazo mapya na yenye mielekeo
ya kisasa.
Katika muktadha wa
uwasilishaji, mitindo na miundo hiyo mipya ya kisanaa kama vile; kutokutumia
methali, haizingatiwi ili iwe mbadala wa zile za zamani au zilizozowewa bali
ziwe nyongeza kwa zile zilizopo. Kutotumiwa kwa methali katika utunzi na uwasilishaji
wa ushairi wa Kiswahili kuchukuliwe kuwa ni mchango wa kizazi hiki cha sasa
katika kuutajirisha utungo huu uliorithiwa kutoka kwa kizazi kilichotangulia.
Dhana ya kutotumiwa kwa
methali katika baadhi ya tungo za ushairi wa Kiswahili ni ushuhuda kwamba,
ushairi wa kisasa wa Kiswahili umebadilika kwa kiasi fulani hasa kifani na kimaudhui
(Masinde 2003 na Chacha 1987) Kando na hayo, busara katika ushairi wa kisasa wa
Kiswahili huweza kuwasilishwa kupitia kwa kauli nyinginezo za lugha zinazobuniwa
kibinafsi na watunzi kulingana na hisi au mchomo walionao katika uelekezi wa
uhalisi wa maisha yao. Hii ni kwa sababu, dhana ya busara au hekima huwa katika
mabadiliko yanayoathiri mielekeo ya jamii hususan katika ushairi wa kisasa wa Kiswahili.
Kwa hivyo, ushairi wa Ukimeso,
unadhihirisha mwelekeo kwamba; hakuna ulazima wowote wa kutumia methali
katika uwasilishaji wake. Kama ilivyo katika sanaa yoyote ya fasihi, utungo au
ushairi unaelekezwa kwanza kwa hisi au mchomo wa msanii kisha baadaye kufanyiwa
uteuzi wa fani mahususi ili kujenga mwafaka wa kuwasiliana na hadhira (Jilala
2008 na Njogu na Chimerah 1999).
Katika muktadha wa
uwasilishaji wa utungo wa Ukimeso ushairi wa kisasa wa Kiswahili huweza
ama kuimarisha au kudhoofisha baadhi ya vipengele vya lugha au kauli ambazo zimekuwa
zikithaminiwa mno katika mawasiliano ya jamii. Endapo baadhi ya matumizi hayo
ya miundo, mitindo au kauli za lugha zilizozoweleka itafifia, ile maarufu inayobuniwa
kibinafsi na kimakusudi na wasanii kwa wakati wa sasa, itastawishwa na itatumiwa
zaidi katika uwasilishaji wa tungo za kifasihi hususan ushairi wa Kiswahili.
Kwa mujibu wa nadharia
ya Fomula ya kisimulizi ni kwamba, mbinu au fani mahususi zinazotumika katika
uwasilishaji wa utanzu wa fasihi huweza kubadilika lakini mwanzoni mabadiliko
hayo hukabiliwa vikali na baadaye huzowewa na hukubalika
(Woods 1971 na Whallon
1969).
Sawia na kutotumiwa kwa
methali katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili, kunaashiria
mabadiliko ya kimtindo. Hivi sasa mabadiliko hayo ya kiutunzi yanakubalika shongo
upande. Hii ndio sababu, hapo awali katika miaka ya sabini hapa Afrika
Mashariki, ushairi huru
wa Kiswahili ulichukuliwa kuwa ni utungo wenye mikiki na usiofaa. Ingawa kwa
sasa „mgogoro‟ katika ushairi wa Kiswahili haupo au unaendelezwa chini kwa
chini kwa kiwango fulani. Kadhalika, „mgogoro‟ huenda ulitokana na kuasi baadhi
ya kauli za kimapokeo ambazo ni pamoja na matumizi ya methali ambazo
zimekuwa zilichukuliwa
kuwa ni muhimu katika jamii. Aidha, ushairi wa Kiswahili si sugu na hauna budi
kubadilika kifani na kimaudhui ili uweze kukabiliana na mabadiliko yaliyopo ya
kitamaduni katika jamii za Afrika Mashariki. Katika mkabala huu, ushairi usiotumia
methali unaweza pia kuwasilisha maudhui ambayo ni ya kidhahania lakini yenye
chemichemi ya ufasiri katika jamii.
Sifa Bainifu za Ushairi
Usiotumia methali
Kutokana na maelezo
yaliyozingatiwa katika makala hii ushairi wa Kiswahili usiotumia
methali wa Ukimeso unaweza
kuwa na sifa za kijumla zifuatazo:
a)
Mbinu za uwasilishaji kama vile fani si
sugu bali huweza kubadilika kulingana na mabadiliko ya mfumo wa utamaduni na
maisha ya jamii.
b)
Mabadiliko ya kijamii pia huweza
kuathiri mitazamo ya watunzi kuhusu mitindo mahususi ya lugha inayotumika na
maudhui yanayoibuliwa na kuwasilishwa katika ushairi.
c)
Hakuna ulazimu wa kutumia fani moja au
kauli mahususi kama vile methali katika uwasilishaji wa ushairi. Hii ni kwa
sababu, baadhi ya kauli msingi ambazo zinaeleweka katika jamii huweza kujengewa
mwangwi wake.
d)
Sura au vitanzu vya ushairi huweza kuwa
ni njia ya kubainisha mitindo mbalimbali inayotumika katika utunzi na
uwasilishaji wa ushairi.
e)
Matumizi ya kauli za lugha
zilizozoweleka katika jamii huweza kuchakaa na kupisha miundo mipya katika
utunzi wa ushairi.
f)
Usaili na utafakari unakuwa ni nyenzo
muhimu katika uwasilishaji na upokezi wa ujumbe.
g)
Hakuna njia moja mahususi inayoweza
kutumika katika kuwasilisha hisi na mchomo wa msanii wa ushairi.
Katika ushairi wa
Kiswahili kuna mifano ya anuwai ya mashairi yasiozingatia methali katika utunzi
na uwasilishaji wake. Hata hivyo baadhi ya sifa hizo zinaweza kubainika kwa
kuzingatia mashairi yafuatayo.
Diwani
ya Kichomi
(i) Shairi la Mafahali
wapigana (uk. 5)
(ii) Shairi la Nimechoka
(uk. 34 – 35)
(iii) Shairi la Kuchambua
Mchele (uk. 63)
(iv) Shairi la Hadithi
ya Mzee (Uk. 69 – 72)
Diwani
ya Bara Jingine
(i) Shairi la Hatujaaga
Ndoto (Uk. 4 – 5)
(ii) Shairi la Bara
Jingine (Uk. 10 – 16)
(iii) Shairi la Mruko
wa Nyuki (Uk. 20 – 25)
Hitimisho
Makala hii imebainisha
kuwa ushairi wa kisasa wa Kiswahili umebadilika mno kwa
upande wa fani msingi
zinazotumika na maudhui yanayowasilishwa. Kutokana na
maenezi ya lugha ya
Kiswahili kutoka pwani hadi bara ya Afrika Mashariki, ushairi
umekuwa ukitungwa na
jamii mbalimbali za Afrika Mashariki na kwingineko. Kwa
ambavyo utungo huu
umestawishwa na umeimarishwa kimatumizi, umeweza
kushirikisha mitindo
mbalimbali katika utunzi na uwasilishaji wake. Kwa hivyo, ushairi
wa Kiswahili ni utungo
ambao unahifadhi na unawasilisha utamaduni wa jamii ya Afrika
Mashariki. Isitoshe,
matumizi ya methali bado yana nafasi muhimu katika utunzi na
uwasilishaji wa ushairi
wa kisasa wa Kiswahili. Kwamba, matumizi ya methali
yanaweza kuwa angavu
zaidi au matumizi yake hudhihirika kama mwangwi wa
kurejelea.
Kuhusu mashairi
yanayojitoa nje ya arudhi za kimapokeo, (au yale yasiyotumia methali)
si kwamba tungo hizo
ndio bora zaidi. Kile kinachofanyika ni kuutoa utungo katika
mazoea ambayo
yanaelekea kuichosha hadhira. Vile vile, kinachobainika katika mitindo
inayotumika katika
uwasilishaji ni upenu mwingine wa kuukuza ushairi; la sivyo kizazi
cha sasa na kijacho
kitakuwa na mwelekeo finyu kuhusu ruwaza nzima ya sanaa hii ya
Kiswahili. Pamoja na
kwamba ukale (ushairi unaozingatia arudhi za kimapokeo) una
uzuri wake; usasa
(ushairi usiozingatia arudhi za kimapokeo) haupasi kudharauliwa.
Kwa sababu, kizazi cha
sasa kitahisi kuwa hakipewi uhuru katika kujumuika katika sanaa
hii.
Jambo lililo la muhimu
kuuliza ni: kwa nini watunzi wamezuka na mitindo badilia katika
uwasilishaji wa utungo
huu? Kimsingi, ushairi wa kisasa wa Kiswahili ni utungo ambao
ni kongamano la matini
za lugha na kunga mbalimbali zinazotumika katika utunzi na
uwasilishaji. Kwa
hivyo, methali kama ishara au matini zinazotumika katika ushairi wa
Kiswahili zichukuliwe
kuwa ni miongoni mwa kauli msingi zinazoshirikishwa na zenye
uzito sawia katika
utungo huu.
MAREJELEO
Abdalla, A. (1973):
“Ushairi wa Kiswahili na Uhuishwe Usiuliwe”, katika Zinduko. Dar
es Salaam: Jarida la
Chama cha Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Abedi, A. (1954): Sheria
za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri. Nairobi: East African
Literature Bureau.
Akporobaro, F. B. O. na
Emovon, J. A. (1994): Nigerian Proverbs: Meaning and
Relevance Today. Lagos:
Department of Culture.
Andrzejejewski, B.W
(2011)
Babusa, H. O. (2005):
“Vigezo badilia kuhusu uanishaji wa Mashairi ya Kiswahili”,
Tasnifu ya M. A., Chuo
Kikuu cha Kenyatta. (Haijachapishwa).
Barthes, R. (1981):
“Theory of the Text”, Ian Macleod (Mt.), katika Young, R. (Mh.)
Untying the Text. London:
Routledge.
Chacha, C. N. (1987):
“Meaning and Interpretation of Swahili Poetry: A Portrayal of
Changing Society”,
Tasnifu ya Ph.D, Yale University (Haijachapishwa)
Eco, U. (1976): A
Theory of Semiotics. Bloomington: Indiana University Press.
Fowler, R. (1966): “The
Formalaic Theory and its Application to English Alliterative
Poetry”, katika Fowler,
R. (Mh.) Essays on Style and Language. London:
Routledge & Kegan.
Gibbe, A. G. (1990):
“Ufumbaji katika Ushairi wa Kiswahili”, katika Gibbe, A. G. (Mh.)
Jarida la KISWAHILI,
Juzuu 1. Dar es Salaam: Education Services Centre.
Hawkes, T. (1977): The
Structuralism and Semiotics. London: Methuen.
Hussein, E. N. (1971): Mashetani.
Nairobi: Oxford University Press.
Jacobson, J. W. (1960):
“Concluding Statement: Linguistics and Poetics”, katika Seboek,
J. (Mh.) Style and
Language. Cambridge: MIT.
Kahigi, K. K. na
Mulokozi, M. M. (1979)
Kandoro, S. A. (1983):
“Hatua Mbalimbali za Kubuni na Kutunga Shairi la Kiswahili”,
katika Makala za
Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili III, Fasihi.
Dar es Salaam. TUKI.
Kezilahabi, E. (1973):
“Diwani ya Massamba”, katika MULIKA Na. 13. Dar es Salaam:
TUKI.
Khan, M. K. (1975)
Kimaro, K. (2008):
“Washairi huru Wamefilisika kimawazo na kisanaa”, katika Taifa
Leo Novemba
10, 2008 Uk. 21. Nairobi: Nation Media Group.
King‟ei, G. K. (2007):
“Athari za Washairi Wakongwe juu ya Washairi wa Kisasa:
Mfano wa Muyaka bin
Haji na Ahmed Nassir”, katika Kioo cha Lugha, Juzuu la
5. Dar es Salaam: TUKI.
King‟ei, G. K. na
Kemoli, A. (2001): Taaluma za Ushairi. Nairobi: Acacia Stantex
Publishers.
Maitaria, J. N. (1991):
“Methali za Kiswahili kama Chombo cha Mawasiliano: Mtazamo
wa Kiisimu-Jamii”.
Tasnifu ya M.A., Chuo Kikuu cha Kenyatta.
(Haijachapishwa)
Masinde, E. (2003):
“Ushairi wa Kiswahili Maendeleo na Mabadiliko ya Maudhui”.
Tasnifu ya Ph.D., Chuo
Kikuu cha Kenyatta. (Haijachapishwa)
Mazrui, A. (1994)
Mazrui na Syambo, B.K.
(1992): Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi: East African
Educational Publishers.
Mberia, K. wa (2001): Bara
Jingine. Nairobi: Marimba Publications Ltd.
___________ (1997): Natala.
Nairobi: Marimba Publications Ltd.
Mohamed, S.A. (1990): Mbinu
na Mazoezi ya Ushairi. Nairobi: Evans Brothers (Kenya)
Ltd.
Momanyi C. (1998):
“Usawiri wa Mwanmke Muislamu katika Jamii ya Waswahili kama
Inavyobainika katika
Ushairi wa Kiswahili”. Tasnifu ya Ph.D, Chuo Kikuu cha
Kenyatta.
(Haijachapishwa)
Mulokozi, M. M (2008):
“Nadharia ya Jadi ya Ushairi wa Kiswahili: Je Upo?” katika
Ogechi N.O, Shitemi,
N.L. na Simala, K.I. (Wah.) Nadharia ya Kiswahili na
Lugha za Kiafrika. Eldoret:
Moi University Press.
Mulokozi, M.M. na
Kahigi, K. K. (1973): Mashairi ya Kisasa. Dar es Salaam: Tanzania
Publishing House.
Nagler, M.N. (1967): Towards
a Generative View of Formula. TAPA 98.
Njogu, K.(1998):
Njogu, K. na Chimerah,
R. (1999 Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi:
Jomo Kenyatta
Foundation.
Noor, I.S. (1988): Tungo
Zetu. New Jersey: The Red Sea Press Inc.
Parker, C.A. (1974):
“Aspects of A Theory of Proverb”, Tasnifu ya Ph.D, Chuo Kikuu
cha Washington.
(Haijachapishwa)
Sanka, S. M. (1994): Semantic
Deviation in Iraqw Oral Poetry. Tasnifu ya M.A., Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam
(Haijachapishwa)
Senkoro, F. E. M.
(1988): Ushairi, Nadharia na Tahakiki. Dar es Salaam: Dar es Salaam
University Press.
Wafula, R.M. na Njogu
(2007): Nadharia na Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Jomo Kenyatta
Foundation.
Walibora, K. (2007): Malenga
wa Karne Mpya. Nairobi: Phoenix Publishers Ltd.
Wamitila, K. W. (2005):
Wood, R. (1971): An
Essay on the Original genus and Writing of Homer. New York:
Garland Publishing.
|