Kwa mujibu wa Mbonde katika kongamano la Jubilei ya Miaka 75 ya TUKI (2005) anafafanua maana ya methali pamoja na dhima/umuhimu au nafasi yake katika jamii kama ifuatavyo;
“Methali ni lugha nyepesi ipenyayo moja kwa moja katika mioyo ya wasikilizaji. Aidha, methali au misemo huondoa wingu au ukungu katika mawasiliano ya kisayansi na ya teknolojia nzito za kitaaluma. Pia, methali ni kielelezo cha utashi wa uhai wa jamii husika, historia na falsafa ya utu wa binadamu, hekima na busara. Mwanafasihi mashuhuri katika Afrika, Chinua Achebe, katika kitabu chake Things Fall Apart (1959: 7) anaandika, “Methali ni mafuta ya mawese ambayo kwayo maneno huliwa.” Kauli hii ikizingatiwa barabara huyafanya maandishi kukubalika kuwa ni fasihi, maana, matumizi ya methali na fani nyingine hukoleza simulizi kama tui la nazi na viungo mbalimbali kama vile vitunguu, nyanya, zinavyoifanya mboga iwe na riha na ladha tamu zaidi.
Dhima ya methali katika jamii. Mbonde anaendelea kufafanua dhima/umuhimu au nafasi ya methali katika jamii “Methali ni njia ya mkato ya kuelimisha, kuadilisha, kukosoa na kuelekeza jamii, hususani vijana katika kuzingatia tunu za jadi kwa kina ndani ya mazingira ya asili ya jamii”.
Vilevile Ngole na Honero wanafasili kuwa “methali ni aina ya usemi mzito na ambao unakusudiwa kusema jambo maalumu kwa njia ya fumbo. Usemi huu mzito mara nyingi hukusudiwa kumuonya, kumuongoza, na kumuadilisha mwanadamu. Kwa umbile la nje methali huwa na muundo maalumu, muundo wenye baadhi (pande) mbili. Upande mmoja wa methali huwa unaeleza mazoea au tabia ya mtu au kitu juu ya utendaji wa jambo; na upande wa pili unaeleza matokeo yatokanayo na mazoea hayo au tabia hiyo ambayo imeelezwa katika upande wa kwanza.
UCHAMBUZI WA METHALI ZA SHAABAN ROBERT
1. Cha mjinga huliwa na mwerevu.
– Asiyejua mara nyingi hudhulumiwa na mtu anayejua.
– Hutumiwa kuwatanabaisha watu wasiojua kwamba, haki zao siku zote hudhulumiwa na wale wanaojua, wajanja au wasomi.
2. Cha mlevi huliwa na mgema. (Tazama:1)
3. Cha mwivuo hulishwa na mgema.
– Ubaya hubainishwa kwa wema.
– Hutumika kuelezea kuwa daima watu wema ndiyo ambao hubainisha maovu katika jamii.
– Cha mwovuo hulishwa na mwemao.
– Sawa na “Cha mwivuo hulishwa na mwemao.” (tazama 3)
4. Cha nini kitu hiki kizuri? Punje moja ya mtama bora mara elfu.
– Si kila kisifiwacho ni kizuri kwani vipo visivyosifiwa ambavyo ni vizuri zaidi ya hivyo vinavyosifiwa.
– Hutumiwa kuonesha kuwa vitu vizuri (watu) siku zote havijibainishi kwamwonekano wake au umbile lake.
– Sawa na “Wamo lakini hawavumi.”
5. Cha kichwa kitamu, na cha mkia kitamu.
– Kila mtu anafurahia nafasi yake katika maisha.
– Hutumika kuonesha kuwa kila hali (cheo, uchumi nk.) inauzuri wake katika maisha.
6. Cha shina kitamu, cha kati kitamu na cha ncha kitamu. (tazama: 5)
7. Chachu ikichachuka, watu watatafutana.
– Amani itapotea punde mnyonge atakaposimama na kudai haki yake.
– Hutumiwa kwa lengo la kuwatahadharisha wale wawanyonyao wanyonge kuwasiku watakapotambua haki yao hapatatosha.
8. Chafi rasilimali yake utumbo.
– Kitu chochote chenye thamani hakiachwi/hakionekani waziwazi. Au tunaweza kusema uzuri wa mtu si umbo wala sura (mwonekano wa nje) bali ni tabia.
– hutumika kuwatahadharisha wale wanaoshadidia au kupapatikia vitu kwakuangalia umbile lake bila kujua undani wake.
9. Chafi rasilimali yake matumbo. (tazama: 8)
10. Chagua dogo katika maovu mawili.
– Heri kutenda kosa dogo kuliko kuliko kutenda kosa kubwa. Au ni afadhali kupata hasara kidogo kuliko kupata hasara kubwa.
– Hutumika kufariji endapo mtu anapatwa na tatizo dogo, hivyo anambiwa methali hii ili aone kwamba tatizo alilolipata huenda Mungu kamwepusha na janga kubwa zaidi ya hilo.
11. Chakula bora ni ukipendacho.
– Uzuri au ubora wa kitu anaujua mtumiaji au mlaji.
– Methali hii hutumika kueleza kuwa, katika maisha si vizuri kumlazimisha mtu kutenda jambo bila yeye mwenyewe kuridhia.
12. Chakula bora ni ulichonacho.(tazama:11)
13. Chakula ni wali, kiungo ni samli na mke ni mwanamwali.
– Kitu chenye thamani huthaminiwa na watu.
– Methali hii hutumika kuonesha kwamba katika maisha daima vitu vyenye thamani ndivyo vinavyothaminiwa na watu. Pia hata watu wazuri au wenye sifa nzuri ndiyo wanaopendwa na wengi.
14. Chanda na pete, ulimi na mate, uta na upote.
– Chanda: kidole; Uta: upinde wa kupigia mshale; Upote: kamba ya upinde.
– Kila kitu hutegemeana.
– Hukuna kitu ambacho kimekamilika katika maisha.
15. Cha ndugu hakiwi chako sharti upewe.
– Using’ang’anie vitu visivyo vyako.
– Methali hii hutumika kwa ajili ya kuwaonya na kuwakosoa wale wenye tabia ya kudhani kwamba kitu cha ndugu ni sawa na chakwake. Hivyo katika maisha haupaswi kijivunia vitu ambavyo si mali yako hata kama ni vya ndugu yako wa damu.
16. Changilizi ya chungu huua hata nduvu.
– Changilizi: kazi ya pamoja.
– Umoja au ushirikiano wa wanyonge huweza kufanya mapinduzi makubwa.
– Hutumiwa kuwa hamasisha watu hasa wa tabaka la chini (duni) kuwa endapo wataungana na kushirikiana wanaweza kutenda mambo makubwa katika maisha yao.
Changu si chetu.
– Kitu ambacho ni changu mwenyewe hakiwezi kuwa cha wote.
– Hutumika kuwa hamasisha watu kupenda kujishughulisha katika maisha iliwajipatie vitu vyao wenyewe badala ya kutegemea vitu vya wengine. Pia inawafundisha watu kutopenda kuishi kwa kutegemea migongo ya wengine.
17. Chatu anamvuto kwa mbwa na paka kama fedha kwa mtu.
– Jinsi fedha ilivyo na mvuto vivyo hivyo wabaya au wakorofi wana uzuri pia kwa watu wao.
– Methali hii hutumika kuwatanabaisha watu watambue kwamba katika maisha hakuna mtu asiye na rafiki hata kama mbaya kupita kiasi.
18. Chawa si nzito lakini husumbua.
– Matatizo madogo madogo yasipodhibitiwa tangu awali huweza kusumbua na kusababisha matatizo makubwa zaidi.
– Hutumika kuwatahadharisha wale wenye tabia ya kudharau matatizo madogo madogo kwani huweza kuongezeka na kushindwa kutatulika.
– Sawa na “mdharau mwiba guu huota tende, usipoziba ufa utajenga ukuta.”
19. Cheche huzaa moto.
– Kitu kidogo huweza kuleta madhara makubwa.
– Hutumika kuwatahadharisha wale wanaodharau mambo madogo kwani huweza kusababisha madhara makubwa yasiyotegemewa.
– Sawa na “mazoea hujenga tabia”
20. Cheche ndiyo moto.
– Tabia ya mtu huonekana kupitia matendo yake.
– Hutumika kuwatahadharisha watu katika maisha wanapaswa kufanya mambo kwa umakini kwani kupitia kwayo huweza kutambulika haraka.
21. Chechema utafika wendako.
– Hata ukitembea polepole utafika tu.
– Hutumika kuwafariji watu waliokata tamaa katika mambo mbalimbali kuwa na uvumilivu katika yote kwani uvumilivu ndiyo msingi wa mafanikio katika maisha.
22. Cheka uchafu, usicheke kilema.
– Usimdhalilishe binadamu mwenzako kwa lolote lile.
– Hutumika kuwaasa watu wenye tabia ya kuwanyanyapaa walemavu kwani hawakupenda kuwa hivyo na hata wao watambue kwamba wanaweza kupata ulemavu wakati wowote.
– Usimcheke mtu mwenye shida kwani hata wewe siku moja unaweza kupata shida kama hiyohiyo.
23. Chema chajiuza, kibaya chajitembeza.
– Siku zote kitu kizuri (watu wazuri) hujulikana tena bila hata kutangazwa. Lakini kitu kibaya hulazimu kutangazwa tena hata ikibidi kutia chuku ili kionekane kizuri.
– Methali hii hutumika kuwaambia watu wasio na wema katika jamii.
24. Chema hakikai, hakina maisha.
– Daima katika maisha kitu chema hakidumu kwa muda mrefu.
– Hutumiwa kuwafariji wale waliofiwa na wapendwa wao. Pia huweza kutumika wakati watu wanazungumza juu ya habari za mtu aliyekuwa mwema ambaye huenda amefariki dunia.
– Sawa na “Wema hauozi.”
25. Chema hakikai, hakina maisha.
– Daima kitu kizuri katika maisha hakiwezi kuishi kwa muda mrefu.
– Hutumika kuwatia moyo na kuwafajiri wale wote waliondokewa na ndugu, jamaa na marafiki zao.
26. Chema hujiuza, kibaya hujitembeza. (tazama: 23)
27. Chema hutakwa na Mungu na watu.
– Kitu kizuri hupendeza machoni mwa kila mtu pamoja na Mungu pia.
– Huasa watu kuwa na tabia nzuri kwani hupendeza mbele jamii na hata kwa Mungu pia.
28. Cheupe dawa, cheusi dalili hawa.
– Tabia na sifa nzuri huongeza utu na thamani ya mtu, lakini tabia mbaya huondoa utu na thamani ya mtu huyo pia huondoka katika jamii.
29. Chini kwetu juu kwa Mungu.
– Hakuna binadamu anayeweza kuingilia mamlaka ya Mungu.
– Huonya watu kuacha tabia ya kuingilia mamlaka ya Mungu.
30. Chini ya mdogo juu ya mkubwa.
– Usijiamini kwa nafasi uliyonayo na kujifanya wewe ndio wewe katika maisha kwani wapo watu ambao wamekuzidi.
– Hutolewa kwa watu ambao huringia nafasi na vyeo walivyo navyo katika maisha.
31. Chini yetu Juu ya Mungu. (tazama: 29).
32. Chipukizi ndio miti.
33. Vijana ndio taifa la kesho.
– Hutumika katika kuelimisha watu wasiwadharau vijana na kuwanyima haki zao kwa sababu vijana ndio taifa la kesho.
34. Chombo cha kuvunja (kuharibika hakina rubani)
– Kitu au jambo lililoharibika kamwe halina mwokozi.
– Hutolewa kwa watu wanaostaajabu na kulaumu kwa nini jambo limetokea na kutaka wajue kuwa jambo likisha tokea limetokea.
35. Chombo cha mwenye kiburi hakifiki bandarini.
– Watu wasiopokea ushauri daima hawafanikiwi.
– Hutumika kuonya watu wasiopenda kushauriwa ili wapende kufuata ushaurikwani si kila ushauri ni mbaya.
36. Chongo kwa msangu, kwa mswahili rehema ya Mungu.
– Kitu kisicho na thamani kwako kwa mwenzio kinathamani.
– Hutolewa kwa wale wanaodharau vya wenzao.
37. Chongo kwa mnyamwezi kwa mswahili rehema ya Mungu. (tazama: 36)
38. Choyo huweka mali mpaka ikaoza.
– Uchoyo husababisha uharibifu wa mali.
– Huonya watu ambao hawapendi kutoa vitu vyao kwa wahitaji mapaka vinaharibika
39. Chuchu mpya huangua chuchu ya zamani.
– Kitu kipya husababisha maendeleo ya kile cha zamani.
– huelimisha watu juu ya kutunza na kuthamini vya zamani kuwa vyote kwa pamoja ni sehemu ya maendeleo.
40. Chombo mpya huangua chombo ya zamani. (tazama: 39)
41. Chuki hupotoa watu.
– Daima chuki hupoteza watu mpaka wakashindwa kuaminiana, kupendana na hatA kushindwa kushirikiana katika mambo mbalimbali ya kimaendeleo.
– Hutolewa kwa watu ambao wanachukiana na kuwatahadharisha kuwa hali hiyo huleta athari mbalimbali katika maisha.
42. Chuki hupotoa haki na watu.
– Chuki hupoteza haki na huleta mfarakano baina ya watu.
– Hutumika kuwaelimisha watu juu ya athari za chuki kuwa hupoteza haki za watu na pia kufarakanisha watu hao.
43. Chuma kimetawala dunua.
– Watu wenye mamlaka wametawala dunia.
– Hutumika kuonesha kuwa watu wenye mamlaka ndio waamuzi wa kila kitu.
44. Chuma kipate kingali moto.
– Ni vyema kufanya mambo katika wakati mwaafaka.
– Kuhamasisha watu kufanya mambo katika wakati unaofaa bila kusubiri.
45. Chumvi ikizidi chakula huaribika.
– Uongo ukizidi hupoteza uaminifu.
– Huambiwa watu wapendao kusema uongo, kutoa ahadi bila kutekeleza (hasa kwa viongozi kuwa hupelekea jamii au watu wanaowaongoza kushindwa kuamini kabisa)
46. Chumvi ilihadaa watu kuja pwani kama sukari.
– Tamaa ya mali iliwashawishi wageni kuingia nchini mara kwa mara.
– Hujuza watu kuhusu historia ya uvamizi wa wageni nchini na lengo la kuja kwao ambalo lilikuwa ni kujipatia utajiri.
– Pia hutumika kutoa funzo kwamba ni vyema kutafiti jambo kabla ya kutenda.
47. Chungu huvunjika magae na mtu huharibika asifae.
– Hakuna kitu ambacho hakina mapungufu.
– Hujuza watu kuwa hata binadamu anaweza kuharibika na kupoteza thamani sawa na vitu vingine kama chumvi. Hakuna kitu ambacho kimekamilika.
8. Chungu kibovu kimekuwa magae.
– Kitu kilichoharibika huweza kukosa thamani kabisa.
– Hutahadharisha watu kuwa kilichoanza kuharibika kisipo chukuliwa hatua huharibika zaidi.
49. Chura hushangilia mvua wala hakina (hana mtungi).
– Watu wengi hufurahia mafanikio fulani bila kujua sababu za mafanikio hayo.
– Hutolewa kwa wale wote ambao hupenda kufurahia mafanikio bila kufuatilia hatima ya mafanikio hayo ikiwa wao ni sehemu ya jamii hiyo.
50. Chururu si ndondondo.
– Jambo kubwa si sawa na jambo dogo.
– Kuhamasisha watu ambao wanajuhudi katika kufanya kazi ndani ya jamii kuwa waongeze juhudi.
51. Dalili ya mpumbavu hupumbaa.
– Dalili ya mtu mwenye mienendo mibaya huonekana kutokana na matendo yake katika jamii.
– Hutumika kuwaonyesha watu ambao hawajali hususani mambo yaliyo ya msingi.
52. Dalili ya mvua mawingu.
– Mafanikio ya mtu katika maisha hutegemeana nay eye mwenyewe jinsi alivyoyaandaa.
– Hufundisha watu kuchukua taadhari.
53. Dalili ya vita matata.
– Kila matatizo yanayotokea katika jamii kuna chanzo chake.
– Tuondokane na migogoro inayochangia vita.
54. Damu nzito kuliko maji.
– Ndugu ni ndugu tu hata kama wakigombana watapatana hawataweza kutengana kamwe.
– Hutumika kuhamasisha ndugu kuthaminiana/kusaidiana.
55. Dau la mnyonge haliendi joshi,likenda joshi ni mungu kupenda.
– Shida au matatizo ya mtu hayawezi kumuathiri mtu mwingine
– Hutumika kuwaonya
56. Dawa ya deni kulipa
– Uaminifu katika maisha ni muhimu ili kuweza kuishi na jamii pasipo shaka.
– Huwaonya watu wanaokopa wanatakiwa wawe wanalipa kwa wakati.
57. Dawa ya moto ni moto.
– Ubaya hulipwa kwa ubaya.
– Usimwogope kumkabili mtu.
58. Dawa za wakurugenzi ni mizizi na makombe.
– Viongozi walio wengi ili waweze kutwaa madaraka au kushika nyadhifa, lazima wapitie katika mambo ya kishirikina.
– Kuwakosoa watu waendekezao imani potofu.
59. Dhahabu haina maana chini ya ardhi.
– Kukosa maarifa katika kazi ni sawa na hujafanya chochote.
– Maarifa yanahitajika katika kazi ili uweze kufanikiwa.
60. Dhambi hukimbiwa ,haikimbiwi.
– Kitu chochote chenye hatari na chenye kuleta madhara hakina urafiki.
– Huwataadharisha watu wenye mienendo mibaya.
61. Dhihaka ina ukweli nyingi.
– Si kila jambo lisemwalo kiutani halina ukweli ndani yake.
– Tusidharau mambo yoyote yanayokuwa yanasemwa na watu ili baadaye tusije juta.
62. Dhihaka ina kweli ndani. (tazama: 62)
63. Dhiki hukumbusha deni la zamani.
– Unapopatwa na matatizo au shida kwa mara nyingine lazima kukumbuka yaliyokufika kipindi cha nyuma.
– Hukumbusha kulipa deni kabla ya wakati ili uaminiwe zaidi.
64. Dini ni mali ya roho.
– Kila jambo lina wakati wake katika kupenda ambapo husukumwa na roho.
– Tupende vitu kutoka rohoni na wala tusilazimishwe.
65. Dunia duara huzunguka kama pia.
– Usimfanyie mwenzako ubaya pasi kutambua kwamba ipo siku huyo mtu atakusaidia.
– Hutumika kuonyesha namna maisha ambavyo hayatabiriki.
66. Dunia hadaa na walimwengu shujaa.
– Maisha ya duniani yamejaa hila na yanahitaji werevu na ushujaa.
– Dunia huitaji werevu na ujuzi kuikabili.
67. Dunia haidawamu,hudumu nayo.
– Mambo ya duniani ni ya kupita, hayadumu.
– Hutoa funzo kwa watu wasihadaike na mambo ya duniani.
68. Dunia haishi kupambwa na kuharibiwa.
– Wajengao ndo waharibuo au akupendaye kwa leo kutokana na fadhila zako kesho aweza kukua pasipo kutegemea.
– Huonyesha namna dunia inavyokuwa na vitu vibaya na vizuri.
69. Dunia haishi kupendwa na watu.
– Mambo mazuri hayaishi kupendwa na watu na hata kuharibiwa.
– Kuwa makini na vitu vilivyoko duniani si vyote ni dhahabu.
70. Dunia haishi upya ingawa ya zamani.
– Utu uzima au uzee hauwezi ukawa kizuizi kwa mtu kutokuwa na mawazo yanayojenga katika jamii (hekima,busara).
– Tuwaenzi watu wazima ili watupe mapya.
71. Dunia huleta jema na ovu.
– Kila binadamu anao wema wake na hata uovu pia.
– Tusitegemee mema maishani bali hata mabaya.
72. Dunia huzunguka kama pia.
– Dunia huitaji maarifa kuikabili na wala sio kuiamini moja kwa moja.
– Tusikurupukie mambo pasipo kuwa na maarifa au uelewa nayo.
73. Dunia ikupapo soni, kila utendalo huzuni.
– Walimwengu wakikuacha au kukugeuzia shingo, kutoshirikiana mambo utajisikia vibaya.
– Walimwengu twapaswa kuishi nao vyema.
74. Dunia kitu dhaifu.
– Hakuna mtu aliyemkamilifu katika dunia hii.
– Hatuna budi kusameheana katika mapungufu na madhaifu tuliyonayo.
75. Dunia kubwa mtakwisha hamu na kiu.
– Mambo ya dunia hii ni mengi huwezi kuyamudu yaliyo yote.
– Kuwa na kiasi katika maisha kwa kufanya uchaguzi ulio sahihi ili kuondokana na tamaa zisizo za lazima.
76. Dunia mapito haiweki alama wala nyayo.
– Wanadamu na mambo yao yanapita kila wakati,na siku husogea na mambomapya huibuka.
– Watu wanapaswa kujua kwamba hapa duniani mambo mengi yanapita, haina haja ya kushikilia sana yaliyopita hasa mabaya, twapaswa kuyasahau kwani hayaweki kumbukumbu yoyote nzuri katika maisha yajayo.
77. Dunia mti mkavu kiumbe siulemee.
– Dunia inafananishwa na kitu dhaifu kama mti mkavu ambao hauna nguvu hivyo mwanadamu hapaswi kutegemea sana.
– Walimwengu si watu wa kutegemea katika maisha waweza kukupoteza.
78. Dunia nzito kwa mtu mjinga.
– Mambo huwa magumu kwa mtu mjinga asiyeweza kutumia akili katika kujikwamua kutika hapo alipo hadi kwingineko.
– Inawafundisha watu kutumia akili katika kufanya mambo kwa bidii ili wasije wakalemewa na maisha .
79. Dunia pana msilie ngoa.
– Usilie na kuumia (wivu) unapoona mwenzako kapata kwani kila mmoja ana bahati yake.
– Inatupasa kutokuwa na wivu juu ya maendeleo ya mtu bali tujifunze kwa waliofanikiwa ili nasi tufanikiwe.
80. Dunia toto kwa mtaalamu.
– Hakuna mtu anayeweza kushindana na dunia.
– Huhamasisha watu kuwa makini na maisha ya duniani hususani katika kuzikabili changamoto zake.
81. Dua la kuku halimpati mwewe.
– Dharau na kiburi haviwezi kumuathiri mtu aliyeko juu yako katika maisha au laana ya mnyonge na malalamiko yake hayamtishi mwenye nguvu.
– Kulalamika sio ndio suluhisho la matatizo.
82. Eda ni ada yenye faida.
– Mwanamke kukaa eda ni muhimu na yenye mafunzo makubwa na faraja pia.
– Kuwaasa wanawake kuwa mila na desturi zinapaswa kuenziwa.
83. Eda ya mke hakuna eda yam me.
– Eda huwekwa wanawake waliofiwa na waume zao tu na sio wanaume.
– Mwanamke anaonwa kama mlezi mkuu wa familia hivyo anapoachiwa jukumu la kulea anapaswa kufundwa.
84. Ee huyu ana ndaro si ukali wa tumbili.
– Mtu anayetishia na kujitapa hana uwezo wa kufanya lolote. Mara nyingi anayejitapa mno kabla ya kufanya jambo hafanikiwi.
– Inatuasa kuwa ukitaka kutenda jambo onesha kweli kwa vitendo na sio matambo na vitisho.
85. Egemeo la mnyonge ni Mungu.
– Mungu ndiye muweza wa yote katika maisha ambapo mnyonge hukimbilia.
– Tuishi kwa kufuata mienendo miema impendezayo mungu ambaye ndiye kama kimbilio la mnyonge.
86. Elekeo la moyo hushindwa na la akili.
– Akili ndiyo hutawala na ndio mwongozo wa kila jambo.
– Kufundisha watu kuwa twapaswa kutumia akili kupambana na kuamua mambo.
87. Elimu haina mwisho.
– Elimu haina mwisho au haina kikomo.
– Tujielimishe pasipo kuwa na mwisho wake.
88. Elimu bahari haikaushiki. (tazama: 88)
89. Elimu bahari haiishi kwa kuchotwa.
– Penye maarifa na ujuzi hapaishiwi, watu hupenda kuchota pasipo kikomo.
– Tusitosheke kwa mambo yenye manufaa maishani kama elimu.
90. Elimu bila adabu ni uharabu.
– Unapokuwa na elimu na ukaitumia kinyume na ilivyotakiwa ni uharibifu
– Tuyatumie vizuri maarifa tuliyoyapata.
91. Elimu bila adili ni ujahili.
– Elimu bila hekima ni kazi bure.
– Hutumika kuhamasisha watu kuthamini elimu.
92. Elimu hushinda nguvu.
– Ukiwa na maarifa, weledi na ujuzi katika kazi utashinda nguvu ambazo ungezitumia.
– Tusipende kutumia nguvu nyingi katika kazi badala yake maarifa ndiyo yatumike.
93. Elimu hutaka adabu.
– Inamaana kuwa ili kufanya jambo zuri inatakiwa kuwa na uvumilivu.
– Tunatakiwa kuwa na nidhamu katika kufanya mambo yenye tija.
94. Elimu kidogo hatari.
– Mwenye elimu ya chini mara nyingi huwa na matatizo.
– Kuwa na kiwango fulani cha elimu husababisha usumbufu katika jamii hasa kwa yule aliyenayo elimu hiyo.
– Huonya wale ambao wana kiwango fulani cha elimu kutojisikia kuwa wao ndio kila kitu kwani wapo ambao wamewazidi katika hilo.
– Huhamasisha watu kujipatia elimu ya kutosha ili kuzikabili changamoto mbalimbali za maisha.
95. Elimu kidogo wazimu.
– Mwenye elimu ya chini mara nyingi huwa na matatizo.
– Kuwa na kiwango fulani cha elimu husababisha usumbufu katika jamii hasa kwa yule aliyenayo elimu hiyo.
– Huonya wale ambao wana kiwango fulani cha elimu kutojisikia kuwa wao ndio kila kitu kwani wapo ambao wamewazidi katika hilo.
– Huhamasisha watu kujipatia elimu ya kutosha ili kuzikabili changamoto mbalimbali za maisha.
96. Elimu mwangaza
– Elimu ndio njia ya kila kitu katika maisha.
– Huhamasisha watu kuwa na bidii katika kutafuta elimu kwani ndio kila kitu katika maisha.
97. Elimu ni nguvu kwa mwanadamu.
– Elimu ndio mkombozi katika maisha ya mwanadamu.
– Huhamasisha watu kuthamini elimu kwani ndio dira ya maisha.
98. Enda mwanakwenda usirudi tena.
– Nenda moja kwa moja usirejee tena.
– Hutumika katika migogoro baina ya watu huku wakijibizana lilikusisitiza kuwa hakuna haja ya kuonana tena.
99. Endaye ya akhera si wa marejeo.
– Mtu ambaye amepoteza kamwe harudi tena duniani.
– Hutumika katika kuhamasisha watu kupunguza masikitiko na kufanya shughuli nyingine, kwani mtu akishafariki hawezi kurudi tena.
100. Endaye hufika atakakokwenda.
– Kila mwenye juhudi ya kufikia mafanikio fulani daima hufanikiwa.
– Kuhamasisha watu kutokata tamaa katika harakati za maisha.
|