USHAIRI WA KISWAHILI KATIKA NJIA PANDA: KUTUMIA AU KUTOTUMIA METHALI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: USHAIRI WA KISWAHILI KATIKA NJIA PANDA: KUTUMIA AU KUTOTUMIA METHALI (/showthread.php?tid=726) |
USHAIRI WA KISWAHILI KATIKA NJIA PANDA: KUTUMIA AU KUTOTUMIA METHALI - MwlMaeda - 08-01-2021 MAKALA: USHAIRI WA KISWAHILI KATIKA NJIA PANDA: KUTUMIA AU KUTOTUMIA METHALI Na
Joseph Nyehita Maitaria
Mwanafunzi wa Ph.D
Idara ya Kiswahili na Lugha za Kiafrika
Chuo Kikuu cha Kenyatta
Ikisiri
Makala hii inahakiki
mabadiliko ya kimtindo katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili. Kwa mfano, hapo awali utungo huu ulitungwa kwa kuzingatia utamaduni wa Waswahili kama jamii. Kwa wakati wa sasa unatungwa na wasanii kutoka jamii pana ya Afrika Mashariki. Kipengele cha methali ni miongoni mwa zile maarufu katika tungo zilizozingatia mno arudhi za kimapokeo. Aidha, baadhi ya wasanii wanawasilisha tungo zao kwa kuzingatia zaidi kauli mahususi wanazobuni wanatumia kwa kadri au zile teule zinazopatikana katika mapokeo ya jamii. Katika muktadha huu, ushairi wa Kiswahili una sifa anuwai ambazo huweza kutumiwa kuubainisha. Kwa kuzingatia au kutozingatia matumizi ya methali katika uwasilishaji, tungo hizi zinaweza kuainishwa kimakundi. Kwa hivyo, ushairi wa
kisasa wa Kiswahili unaweza kuwa ni ule unaozingatia methali zaidi, chache au ule unaoasi kabisa matumizi hayo. Swali ni kwamba, kati ya tungo zinazotumia au zile zisizotumia methali katika uwasilishaji wake ni zipi zilizo bora? USHAIRI
WA KISWAHILI KATIKA NJIA PANDA: KUTUMIA AU KUTOTUMIA
METHALI Na
Joseph
Nyehita Maitaria Utangulizi
Makala hii inatathmini
mabadiliko katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili, hususan ushairi huru. Tungo zinazozingatia arudhi za kimapokeo zimekuwa zikishirikisha mno kipengele cha methali katika uwasilishaji wake kinyume na ushairi huru ambao umekuwa hautumia sana matumizi hayo. Kadhalika, ushairi wa Kiswahili umepitia mabadiliko mbalimbali ya kihistoria, kitamaduni na kijamii hadi kufikia hali yake kwa wakati huu wa sasa. Kwa mfano, hapo awali ulikuwa ni utanzu maarufu miongoni mwa waswahili kama jamii. Kwa wakati wa sasa ni utungo wa jamii pana ya Afrika Mashariki na kwengineko kunakutumiwa lugha ya Kiswahili kama chombo cha mawasiliano. Kutokana na maenezi ya
lugha ya Kiswahili kutoka Pwani ya Afrika Mashariki hadi bara, ushairi wa Kiswahili umeweza kuenea na kupata umaarufu miongoni mwa jamii za Afrika Mashariki. Kwa hivyo, watunzi wa ushairi wameweza kutunga tungo zao zinazoshirikisha utamaduni mpana wa Afrika Mashariki kutokana na umaarufu wa maenezi ya lugha ya Kiswahili. Kabla ya miaka ya sabini, ushairi wa Kiswahili ulitungwa kwa kuzingatia zaidi arudhi za kimapokeo kama vile uzingativu wa idadi maalumu ya mizani, mishororo, urari wa vina na ukariri wa vibwagizo. Baada ya miaka ya sabini, baadhi ya washairi waliweza kujitupa ugani na kutunga tungo zao bila ya kuzingatia zaidi arudhi za kimapokeo (Babusa 2005 na Chacha 1987). Kwa wakati huu wa sasa, ushairi wa Kiswahili unawakilisha tungo unaozingatia zaidi arudhi za kimapokeo, ule zilizozingatia sana arudhi hizo na zile zisizongatia kabisa arudhi hizo katika utunzi na uwasilishaji wa utanzu huu. Hata hivyo, hizi ni tanzu za ushairi wa Kiswhaili. Kwa hivyo, sura hii inafafanua jinsi matumizi ya methali yanavyoweza kutumika kama kipengele muhimu cha kuainishia mabadiliko hayo katika ushairi wa kisasa wa Kiswahili. Uainishaji wa awali wa
Ushairi wa Kiswahili Mpaka sasa utanzu wa
ushairi wa Kiswahili umeweza kuainishwa na baadhi ya wahakiki na waandishi wa kifasihi kwa kuzingatia mitazamo tofauti tofauti. Maainisho hayo yanatokana na baadhi ya tafiti zilizofanywa, kauli zinazotolewa na waandishi au watunzi wa tungo wa Kiswahili. Miongoni mwa wainishaji hao ni kama: Babusa (2005), Masinde (2003), Njogu na Chimerah (1999), Sanka (1995), Mazrui (1994), Noor (1988), Senkoro (1988), Kandoro (1983), Kahigi na Mulokozi (1979), Kezilahabi (1974) na Abedi (1954). Kwa mfano, Masinde
(ibid), ameuainisha ushairi kwa kuzingatia kipengele cha mabadiliko ya maudhui katika muktadha wa mpito wa kihistoria. Kwa kufanya hivyo, ameweza kuyaweka mashairi hayo katika vipindi mahususi vya kihistoria. Kimsingi, ushairi wa Kiswahili una tungo anuwai zenye kuwasilisha mada mbalimbali zinazotokana na utamaduni na uhalisi wa maisha ya watu. Katika uwasilishaji wa sanaa hii, kuna matumizi ya kauli mahususi za kauli za kimapokeo au zile zinazobuniwa kimakusudi na washairi ili kuuathiri moyo na yanayochochea tafakuri ya msomaji. Kwa kuzingatia kauli
teule za lugha, mshairi anaweza kuibusha masuala ambayo yanachoma au yanayozindua moyo kupitia kwa taswira na istiari zinazoibushwa. Kwa hivyo, uainishaji wa ushairi haupo tu katika kiwango cha maudhui, bali pia kwa kuzingatia vipengele vya fani kama vile miundo, na maumbo, lugha mahsusi inayotumika na usanii kwa jumla. Kulingana na nadharia ya semiotiki, mada au maudhui yale yale yanaweza kusawiriwa upya kwa kuzingatia miundo badalia ya lugha (Jacobson 1960) Zaidi ya maudhui katika
mkabala huu, Masinde amependekeza kuwa ushairi wa Kiswahili unaweza kuainishwa kimakundi kama ifuatavyo: Ø Ushairi
wa Kiswahili kabla ya kuja kwa wakoloni. Ø Ushairi
wa Kiswahili wakati wa utawala wa kiarabu. Ø Ushairi
wa Kiswahili wakati wa utawala wa kizungu. Ø Ushairi
wa Kiswahili baada ya uhuru. Ø Kuzingatia
kipengele cha muundo. Ø Kuzingatia
kipengele cha mtindo. Ø Kuzingatia
utendakazi wake. Uhakiki wa Masinde
umebainisha kuwa ushairi wa Kiswahili unaweza kuainishwa kimakundi kwa kuzingatia maudhui yanayoibushwa katika miktadha mbalimbali ya kiwakati au kihistoria. Mwelekeo huu unajitokeza wazi katika makundi manne ya kihistoria (Taz. Vipengele i, ii, iii na iv) ambapo amevitolea ufafanuzi wa kina kurejelea vipindi hivyo mahususi. Hata hivyo, uainishaji huo umegusia pia vipengele muhimu kama vile umuundo, mtindo na utendakazi wa ushairi (Taz. Vipengele v, vi na vii). Vipengele hivi vitatu
pia vya msingi na vinavyohitaji kutolewa maelezo na ithibati Kwa ambavyo ni mapendekezo yanayohusu vigezo vya kijumla vinavyoweza kuzingatiwa, Masinde hakuvitolea ufafanuzi wala kueleza jinsi vinavyoweza kutumiwa katika uainishaji wa ushairi wa Kiswahili Kwa kurejelea mwelekeo na mapendekezo ya Masinde, Babusa (2005) ameyaainisha mashairi ya Kiswahili kimaudhui na pia kudhihirisha kwa kiwango fulani kuwa, kipengele cha muundo kinaweza kutumiwa katika uainishaji wa mashairi hayo. Kwa kuzingatia kipengele cha muundo, Babusa amebainisha sura mbalimbali zinazoibuka na ameyaweka mashairi hayo katika maumbo au bahari mbalimbali za ushairi. Kulingana na bahari hizo ni kwamba, ushairi wa Kiswahili unawakilishwa kwa miundo maalumu ya lugha kama vile uzingativu wa msamiati teule, sajili za lugha na lahaja. Hata hivyo, kinachobainika katika maelezo ya Babusa ni kwamba, umbo au muundo katika ushairi wa Kiswahili unajibainisha zaidi kupitia kwa wa uwasilishaji. Naye Kezilahabi (1973),
ameonyesha jinsi ushairi wa Kiswahili unavyoweza kuainishwa kwa kuzingatia nyakati tatu maalumu za urasmi kama ifuatavo: Ø Wakati
wa urasmi-mkongwe (1728-1885) Ø Wakati
wa urasmi-mpya (1945-1960) Ø Wakati
wa usasa (1967 hadi sasa) Kulingana na
Kezilahabi, urasimi ni wakati ambapo misingi maalumu ya kazi za sanaa huwekwa na kukubalika kuwa vipimo bora vya kazi nyinginezo za kisanaa. Katika muktadha wa Waswahili, ushairi ulipasa kutungwa na kuwasilishwa kwa uelekezi wa baadhi ya vipengele vifuatavyo: Ø Idadi
maalumu ya mizani Ø Urari
wa vina Ø Umbo
Ø Maudhui
yanayojikita katika maadili Ø Lugha
isiyo na utusani Ø Mtiririko
au ushikamano wa mawazo kutoka ubeti hadi ubeti Ø Kuimbika
kutokana na matumizi ya vina na mizani Ø Utaratibu
wa uwasilishaji: mwanzo, kati na mwisho. Basadhiya vipengele
hivyo viliidhinishwa na vilichukuliwa kuwa „roho‟ ya ushairi wa Kiswahili katika kipindi cha urasmi. Mashairi ambayo yalikiuka utaratibu huo yalikemewa na kupuuzwa (Kandoro 1983, Abedi 1954). Katika miaka ya sabini hapa Afrika ya Mashariki, baadhi ya watunzi kutoka bara pia walianza kuwasilisha tungo zao kwa kuziasi baadhi ya kaida hizo (Senkoro 1988 na Kahigi na Mulokozi 1979). Huu ulichukuliwa na baadhi ya washairi wa kimapokeo kuwa ni dosari na uchafuzi wa ushairi wa Kiswahili uliokuwepo. Mwelekeo huu unaweza kupata uelekezo kupitia kwa mihimili ya nadharia ya Fomula ya kisimulizi ambapo kinachopendekezwa ni uzingativu wa kauli teule za kimapokeo na maudhui yanayojikita katika uhalisi na utamaduni wa jamii (Fowler 1966). Kuhusu ukiushi wa kaida, nadharia ya semiotiki inatoa mwelekeo kwamba, kazi ya fasihi inaweza kuwasilishwa kwa mitindo tofauti tofauti ilimradi ujumbe umefasiriwa kwa uzingativu wa utamaduni wa jamii (Barthes 1981 na Eco 1976). Hapo awali, Kiswahili
kilikuwa ni lugha ya wakaziwa pwani ya Afrika Mashariki na baadaye kuenea bara kadhalika ushairi wa Kiswahili umeweza kuwekwa katika makundi mawili mahususi: ushairi unaowasilishwa katika mazingira ya pwani na ule unaozingatia mazingira ya bara. Mwelekeo huu usipozingatiwa hauwezi kuuchukulia ushairi wa Kiswahili kwa upana wake. Kwa sababu hivi sasa utanzu huu unashirikisha tungo zinazotungwa na jamii pana ya Afrika Mashariki na popote pale ambapo Kiswahili kinatumika kama chombo cha mawasiliano. Vile vile, kutokana na kiumbiumbi cha mgogoro wa ushairi kuhusu kutumia au kutokutumia baadhi ya arudhi za kimapokeo kama vile vina na urari wa mizani ushairi wa Kiswahili umeweza kuwekwa katika matapo mawili: ushairi unaozingatia arudhi za kimapokeo na ule usiozingatia arudhi za kimapokeo katika utunzi na uwasilishaji wake (Sanka 1995 na Gibbe 1990) Pia, ushairi kama
utungo wa fasihi umeainishwa kwa kuzingatia idadi maalumu ya mishororo katika beti (Noor 1988, Kandoro 1983 na Abedi 1954). Zaidi ya kuzingatia idadi mahususi ya mishororo, mizani na urari wa vina katika ubeti, ushairi wa Kiswahili uliainishwa katika tanzu mbalimbali kutokana na: Ø Urari
wa vina katika mistari au mishororo katika beti. Ø Mpangilio
wa maneno katika mistari au mishoro katika beti. Ø Idadi
ya vipande katika mistari au mishororo katika beti. Ø Idadi
maalumu ya mizani katika mistari au mishororo katika beti. Katika muktadha wa
vipengele hivyo vinne, muundo na maumbo ya ushairi huweza pia kuainishwa zaidi kama ifuatavyo: Ø Tathnitha
– shairi ambalo lina mishororo miwili katika kila beti. Ø Tathlitha
– shairi ambalo lina mishororo mitatu katika kila beti. Ø Tarbia
– shairi ambalo lina mishororo minne katika kila beti. Ø Takhmisa
– shairi ambalo lina mishororo minne katika kila beti. Ø Tashlita
– shairi ambalo lina mishororo sita katika kila beti. Ø Ushairi
ambao una zaidi ya mishororo sita. Masivina – shairi
ambalo lina mlingano wa mizani katika mishororo lakini si urari wa vina. Ukawafi
– shairi ambalo lina vipande vitatu katika kila mshororo. Msuko
– shairi ambalo lina kibwagizo kifupi. Sakarani
– shairi ambalo linashirikisha bahari mbalimbali. Kikwamba
– shairi ambalo linarudia neno moja katika kila mwanzo wa beti. Kulingana na Wafula na
Njogu (2007) na Mohamed (1990), ni katika kipindi cha urasimi mpya katika fasihi ya Kiswahili ambapo palizuka istilahi maalumu za kuelezea dhana mbalimbali za ushairi wa Kiswahili. Istilahi hizo zilizotumika zaidi ni kama: Mshororo
– ambao ni mstari katika shairi Mwanzo
– mstari au mshororo wa kwanza katika ubeti Mloto
– mstari au mshororo wa pili katika ueti Mleo
– Mstari au mshororo wa tatu katika ubeti Kipokeo
– Mstari au mshororo wa mwisho katika ubeti Ukwapi
– Sehemu ya kwanza katika mshororo Utao
– Sehemu ya pili kaitka mshororo Mwandamizi
– Sehemu ya tatu katika mshororo Tabdila
– Kifupisho cha sauti kaitka neno linalotumika katika mshororo bila ya kubadilisha maana ya msingi. Inkisari
– Kunga ya kufupisha maneno katika mshororo Mazida
– Kunga ya kurefusha neno bila ya kupotosha maana ya asili. Kimsingi, istilahi hizi
zilitumika kimakusudi kwa malengo ya kuutambulisha ushairi wa Kiswahili. Katika muktadha wa nadharia ya Fomula ya kisimulizi ni kwamba, uwepo wa bahari na istilahi maalumu zinazotumika katika ushairi ni njia mojawapo ya kubainisha tanzu za ushairi na fasihi kwa ujumla. Uainishaji huo unazingatia zaidi ushairi wa Kiswahili unaotungwa katika muktadha wa arudhi za kimapokeo (King‟ei na Kemoli 2001). Hata hivyo, inabainika kuwa ushairi wa Kiswahili usiozingatia arudhi hizo katika utunzi na uwasilishaji haushirikishwi katika uainishaji. Zaidi ya hayo, makala hii inapendekeza matumizi ya methali kama kipengele kinachoweza kutumika katika kuainishia mabadiliko ya kiutunzi yanayobainika katika ushairi wa kisasa wa Kiswahili. Hii ni kwa sababu, kwa
wakati huu wa sasa kuna mashairi ambayo yanazingatia zaidi arudhi za kimapokeo, yale yasiyozingatia mno arudhi za kimapokeo na yale yasiyozingatia kabisa arudhi za kimapokeo katika utunzi na uwasilishaji wake. Makundi hayo matatu katika ushairi wa Kiswahili yanadhihirisha kuwa: Ushairi wa kimapokeo
unajitenga kwa kiasi fulani na ushairi huru lakini una ukuruba na ushairi wa kati. Ushairi wa kati unazingatia zaidi mbinu za utunzi zinazopatikana katika ushairi wa kimapokeo na ule wa ushairi huru. Ushairi huru unajitenga
zaidi na ushairi wa kimapokeo kwa upande wa umuundo na kiumbo. Kwa hivyo, ushairi wa
Kiswahili una tanzu zake ambazo zinawiana katika utunzi na uwasilishaji wake. Hata hivyo, tofauti zinazobainika si za msingi zinazoweza kuzifanya tanzu hizo kutalikiana. Kwa mfano, tungo hizi huzingatia zaidi lugha ya kimafumbo, kitaashira, kiistiari, kitashbiha, kitashihisi miongoni mwa kunga zingine za uwasilishaji. Kimsingi, kauli za lugha zinazotumika mno katika uwasilishaji ni zile zinazojibainisha katika tamathali za usemi. Kwa maoni ya Mwandishi
ni kwamba, matumizi ya methali yanapozingatiwa, ushairi andishi wa kisasa wa Kiswahili unaweza kuainishwa kwa mwafaka zaidi. Hapa ieleweke kuwa, ushairi wa Kiswahili umepitia mabadiliko mbalimbali hadi kufikia hali yake ya sasa (Kimaro 2008, Masinde 2003, Momanyi 1998 na Sanka 1995). Aidha, ushairi wa Kiswahili unaweza kutumia methali nyingi, chache ama kutokutumia kabisa katika utunzi na uwasilishaji wake kutegemea mahitaji ya kimtindo na mwelekeo wa mtunzi. Katika misingi hii ya kurunzi tatu (ushairi wa kimapokeo kati na huru) za kimuundo, ushairi wa Kiswahili unakuwa katika njia panda. Kwa kuzingatia namna methali zinavyotumiwa katika utunzi na uwasilishaji wa utungo huu, upanda wake unaweza kubainishwa Uainishaji wa Ushairi
wa Kiswahili unaopendekezwa Matumizi ya methali
yanapozingatiwa, ushairi wa Kiswahili unaweza kuainishwa zaidi kwa kuzingatia kutumiwa au kutotumiwa kwa methali kama ifuatayo: Ushairi wa Kiswahili
unaotumia methali kama anwani Ushairi wa Kiswahili
unaotumia methali moja Ushairi wa Kiswahili
unaotumia methali nusu Ushairi wa Kiswahili
unaotumia methali mbili (au zaidi) Ushairi wa Kiswahili
unaotumia methali kama kauli Ushairi wa Kiswahili
unaotumia methali kama kibwagizo (au kiishilio) Ushairi wa Kiswahili
uso methali Zaidi ya hayo, kila
kikundi cha ushairi kinaweza kupendekezewa jina mahususi kuwa kitambulisho chake. Mbinu iliyotumika katika uundaji wa istilahi hizo za majina ni ile ya kuunganisha viambishi awali vya maneno yanayopatikana katika kila kikundi. Majina hayo yanayopendekezwa ni kama yafuatayo: Ukimea –
Ushairi wa Kiswahili unaotumia methali kama anwani. Ukimemo –
Ushairi wa Kiswahili unaotumia methali moja. Ukimenu –
Ushairi wa Kiswahili unaotumia methali nusu. Ukimembi –
Ushairi wa Kiswahili unaotumia methali mbili (au zaidi). Ukimeka –
Ushairi wa Kiswahili unaotumia methali kama kauli. Ukimeki –
Ushairi wa Kiswahili unaotumia kama kibwagizo (au kiishilio). Ukimeso –
Ushairi wa Kiswhaili uso methali. Kwa uelekezi wa
mihimili ya nadharia ya Fomula ya Kisimulizi, uainishaji huu unazingatia kwamba, utunzi na uwasilishaji wa ushairi hushirikisha kauli teule zinazopatikana katika mawasiliano ya jamii (Propp 1968). Vile vile, kwa kuzingatia mihimili ya nadharia ya Semiotiki, methali kama ishara mahususi zinazotumika katika utunzi na uwasilishaji wa tanzu mahsusi za kifasihi huweza kubadilika, kufifia au kutoweka kulingana na mabadiliko ya utamaduni wa jamii (Nagler 1974) Katika muktadha huu, methali kama ishara zinazotumika katika ushairi wa Kiswahili huweza kufasirika au kufafanuliwa zaidi katika miktadha mahususi ya utamaduni wa jamii. Kwa hivyo, matumizi ya methali katika ushairi wa kisasa wa Kiswahili huweza kutekelezwa kwa kuzingatia kauli zingine zinazobuniwa kimakusudi na watunzi. Ushairi wa Kiswahili
uso Methali Katika makala hii
kitengo hiki cha ushairi wa Kiswhaili kitajumuisha tungo ambazo hazina kabisa matumizi ya methali katika uwasilishaji wake. Kama ilivyokwisha kuelezwa hapo awali „mgogoro‟ katika ushairi wa Kiswahili uliweza kuendelezwa rasmi wakati ambapo baadhi ya watunzi wa ushairi walipoanza kutunga tungo ambazo hazikujikita katika arudhi za kimapokeo. Kwa mfano, katika miaka ya sabini walitokea “watundu” watatu: Hussein (1970), Kezilahabi (1974) na Angira (1970). Baadaye kikundi hiki kilipata wafuasi wengine kama vile: Mulokozi na Kahigi (1973) na Mberia (1997). Hawa walitunga na kuwasilisha kimaandishi tungo zao za mashairi bila kujali au kuzingatia arudhi za kimapokeo ambazo zilichukuliwa kuwa ni „uti wa mgongo‟ katika uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili (Njogu na Chimerah 1999 na Senkoro 1988). Kimsingi, “mgogoro” huu
ulijikita katika kutumia au kutokutumia vipengele vya arudhi za kimapokeo kama vile mizani na urari wa vina kuwa ni uti mgongo katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili (Walibora 2007 na Njogu 1998). Hii ni kwa sababu, baadhi ya wahakiki na waandishi katika wakati huu wa sasa wana mawazo kwamba ushairi wa Kiswahili haupaswi kuelekezwa kwa uzingativu wa vina na mizani maalumu katika uwasilishaji wa tungo hizi. Mawazo hayo yaliibua
hisi na mielekeo tofauti tofauti miongoni mwa baadhi ya watunzi na wahakiki wa fasihi ya Kiswahili. Mitazamo hii ilizua mirengo miwili ya kimwelekeo: wale wanaoshikilia mno na wale wasioshikilia zaidi kuwa urari wa vina na idadi maalumu ya mizani ni mambo ya lazima katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili. Kila kikundi cha washairi kilishikilia msimamo wake (Sanka 1995 na Mulokozi na Kahigi 1979). Kwa hivi sasa, mashairi yanayotungwa kwa mitindo na mitazamo hii miwili yamekubalika kuwa ni tanzu za ushairi wa kisasa wa Kiswahili. Kulingana na Babusa
(2005) na Gibbe (1998), tungo hizi ni tanzu za ushairi wa Kiswahili. Athari ya Maenezi ya Lugha
ya Kiswahili kutoka Pwani hadi Bara ya Afrika Mashariki
Kwa wakati huu wa sasa,
ushairi wa Kiswahili unatungwa na kuwasilishwa kwa kuzingatia arydhi au kutozingatia arudhi za kimapokeo. Hata hivyo tungo hizi ni sura mbili za sarafu moja ambazo zinajengana na kukamilishana ingawa kwa uzingativu wa mitindo tofauti tofauti. Kimsingi, hii leo Kiswahili si lugha ya Waswahili kama jamii ya pwani tu kama ilivyokuwa katika karne mbili zilizopita ila matumizi yake yameimarika na kuwa chombo cha kuwasilishia utamaduni wa jamii ya Afrika Mashariki kwa ujumla (Kimaro 2008, Masinde 2003 na Momanyi 1998. Kwa hivyo, mabadiliko hayo pia yaliweza kuwa na athari kubwa katika utunzi na uwasilishaji wa tanzu za fasihi ya Kiswahili, hususan ushairi wa Kiswahili (Wafula na Njogu 2007, Chacha 1987). Katika muktadha wa
uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili ni utungo wa jamii ya Afrika Mashariki na kwa jamii zote zinazotumia lugha ya Kiswahili kama chombo cha mawasiliano miongoni mwao. Ingawa kwa sasa makabiliano hayo hayapo au yanaendelezwa kichinichini, utungo huu umekubalika na unaendelea kuzishughulisha kalamu za watunzi wa pwani na hata bara ya Afrika Mashariki. Kama chombo kisuluhishi cha uponda katika uwasilishaji wa utungo huu,methali zinaweza kutumika kama kipengele cha kushirikishia mielekeo hiyo miwili katika ushairi wa kisasa wa Kiswahili. Katika
muktadha wa nadharia ya semiotiki ni kwamba, dhima ya ishara moja huweza kupata mshabaha au utekelezaji wake unaweza kupitia kwa ishara nyingine zinazopatikana kwa urahisi katika jamii (Hawkes 1977). Kulingana na mtazamo wa
wahakiki wa fasihi, utunzi na uwasilishaji wa mashairi huweza kuwa yenye maumbo na miundo inayotofautiana lakini yenye kutekeleza dhima sawa ya kuuimarisha na kuustawisha utanzu huu wa fasihi. (King‟ei 2007). Hoja hii ina mshabaha wake katika maelezo ya Khan (1975) kwamba, mshairi anapotunga utungo huwa na lengo la kumvutia msomaji wake. Kwa hivyo, msanii huwa na hadhari zaidi katika kuteua kauli za lugha anazozishirikisha ili shairi lake lisije likakinaisha wasomaji wake. Kwamba anapokabiliwa na hatari hii ya kuichosha hadhira yake, huanza kulipamba shairi lake kwa kutumia kunga mbalimbali za lugha zinazotokana na tamathali za usemi Andrzejewski 2011). Katika mantiki hii, mtunzi anaweza kwa hiari kutotumia methali na kuibua matumizi ya kauli zingine mahususi za lugha ambazo zinajibainisha zaidi katika tamathali za usemi. Kwa hivyo, matumizi ya methali yanaweza kuwa si ya lazima katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi. Matumizi ya kauli
zinazoibuliwa kibinafsi na mshairi huweza pia kujenga msingi wa kuuwasilishia tungo kijazanda, kiistiari, kitaashira kitaswira na kimafumbo (Akporobaro 1994). Kwa sababu uwasilishaji wa ujumbe katika utanzu wa fasihi, hususan ule wa ushairi huwa hauna fasiri moja. Kimsingi, matumizi ya methali huwa yana maana ya kijuujuu na batini (Wamitila 2005) Hata hivyo, maana inayokusudiwa huweza kubainishwa kupitia kwa muktadha mahususi unaoibuliwa na mtunzi. Kwa hivyo, ufasiri huu hutegemea jinsi mtunzi alivyoufumba ujumbe na jinsi mpokezi anavyolikabili shairi hilo tangu mwanzo; mradi tu aweze kuthibitishia hoja zake kwa mifano dhahiri inayotokana na miktadha halisi katika utamaduni wa jamii. Kwa hivyo, ushairi wa Kiswahili unaweza kuwasilishwa kupitia kwa kauli au miundo tofauti tofauti ya lugha ambayo si lazima ziwe za kimethali. Isitoshe, usomaji wa ushairi wa Kiswahili haukamiliki pasipo hadhira maalum ya kuupokea ujumbe au maana inayokusudiwa katika utungo. Kwa sababu kauli zinazotumika katika uwasilishaji wa ushairi huifinya au huipanua maana inayowasilishwa. Suala la Lugha ya
kawaida katika Ushairi wa Kiswahili Baadhi ya watunzi wa
ushairi wa kisasa wa Kiswahili wana mawazo kwamba lugha wanayoitumia katika uwasilishaji wao ni ya „kawaida‟ ili kuuleta ushairi huo karibu na watu wa kawaida katika jamii (Kezilahabi 1974). Dhana ya „kawaida‟ hapa kama inavyotumiwa na baadhi ya watunzi na wahakiki wa kifasihi ina utata. Kwa sababu baadhi ya mashairi yanayotungwa na „watundu‟ au „wanamabadiliko‟ yana kiwango fulani cha ugumu katika ufasiri wake Kwa mfano,mshairi Kezilahabi katika shairi “Mafahari Wapigana”, ametumia kauli za kawaida kama vile: Mafahali wanono, kichunguu mchwa kivumbi hicho ndio askari na kilikuwa kivumbi hicho.Kauli hizi ni za kawaida lakini ni za kustiari ambapo msomaji anahitaji kupiga bongo katika utafakari wa ujumbe. Kimsingi, mashairi haya yanakusudiwa kusomwa na tabaka la wasomi hususan wanafunzi wa vyuo vikuu au wenye uwezo wa juu wa kiufasiri. Kimatumizi, mpangilio usio wa kawaida ni kivutio cha udadisi zaidi kuliko lugha ya kawaida (Mulokozi 2008). Hii inatokana na ukweli
kwamba, kauli zinazoteuliwa na kutumiwa katika mawasiliano ya jamii husisitiza zaidi vipengele fulani vya hisi na mawazo ya mwasilishaji (Maitaria 1991 na Parker 1974). Katika muktadha wa utunzi na uwasilishaji wa shairi ujumbe unaowasilishwa si wa kidhahania bali pia ni kauli zinazotumika hubainisha hisi za mtunzi kuhusu yale aliyoathirika nayo katika uhalisi wa maisha. Ushairi unaotumia
methali huuweka ujumbe unaowasilishwa katika muktadha wa utamaduni unaozoeleka katika jamii. Kwa mfano, Abdalla (1973:19) ametumia methali ya Mpiga ngumi ukuta , huumiza mkonowe katika ubeti ufatao: Ndipo kunipiga vita nisivyojua mwanzowe ulotafuta mepata , hasara ni kwwako wewe mpiga ukuta huumiza mkonowe wapigiyani mayowe? (Ubeti wa 17). Matumizi ya methali hii yanadhirisha ukiukaji wa maadili katika jamii. Kwamba, binadamu wanapasa kuonekana imami wa kusaidiana lakini mwafaka huu unakiukiwa na baadhi ya watu. Hii ni kwa sababu, methali zinazotumika katika uwasilishaji wa ushairi ni kauli ambazo zimesheheni hekima na busara ya jamii. Kama alivyo mtunzi mahiri wa fasihi, mshairi asiyetumia methali huwa haridhiki katika kutumia miundo ya lugha ambayo imekuwepo tu katika mapokeo ya jamii. Kwa hivyo, mshairi huhiari kushirikisha miundo mipya na kwa uelekezo wa hisi zake ili kuutoa utungo huu kutoka kwa miundo ya lugha inayozowewa. Kwa kufanya hivyo, huupa utungo huu upya wa kimaono na kimtazamo katika uwasilishaji wake. Kadhalika, wa mtafiti,
miundo ya lugha iliyozoweleka katika jamii huweza kuwa chakavu, ambapo kimatumizi hupuuzwa au huweza kuvyazwa upya ili mtumizi yake yawe yenye uhai unaostahili. Jambo la muhimu linalopaswa kwa watunzi na wahakiki wa ushairi huru wa Kiswahili ni kubainisha zaidi sifa za kimsingi katika uwasilishaji wa utungo huu. Kwa mfano, ushairi wa kimapokeo una sifa zake zinazoubainisha kinyume na hali ilivyo katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi huru. Swali linaloweza kuulizwa ni kwamba; iwapo mtunzi wa ushairi anapouwasilisha utungo wake pasi na kuzingatia arudhi za kimapokeo ni ushairi huru? 3 Kimsingi, ushairi kama utanzu wa fasihi ni sanaa iliyo hai. Kwa hivyo, mabadiliko ya kijamii huweza kuathiri maudhui yanayoibushwa na fani inayotumika katika uwasilishaji wa utunzu huu. Hata hivyo, ugumu au wepesi wa uwasilishaji na ufasiri katika ushairi wa Kiswahili hutegemea kauli mahususi zinazotumiwa na mshairi. Katika muktadha huu, ushairi unaweza ama kutumia au kutotumia methali na wakati uo huo ujumbe huweza kuwasilishwa kwa mshindo unaostahili. Isitoshe, uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili usiotumia methali, hutumia kauli teule za lugha ambazo pia hujikita zaidi katika tamathali za usemi. Kutotumia Methali
katika uwasilishaji wa Ushairi Sawia na matumizi ya
methali katika mawasiliano ya jamii na pia katika uwasilishaji wa ushairi huu wa ukimeso, ujumbe unaoibushwa huweza kufasiriwa kwa uzingativu wa utamaduni na uhalisi wa jamii husika. Vilevile, lugha ya ushairi wa Kiswahili hutumia vipengele ambavyo hujenga na huchochea usaili na utafakari katika akili ya hadhira. Japo ushairi huru hautumii kwa uangavu methali mahususi, maudhui yanayoibushwa huwa yana mwangwi wa methali unaotawala na unaohisika. Shairi la „Mruko wa
Nyuki‟ katika Bara Jingine (Mberia 2001:20-25) ni mfano wa utungo usiotumia methali yoyote katika uwasilishaji wake. Hali hii inatokana na muundo na mtindo wa kiuwasilishaji au kutokana na mwelekeo wa mtunzi. Hata hivyo, mwangwi wa methali unatawala katika uwasilishaji wa maudhui. Shairi hili limewasilishwa kimchoro ambapo taswira ya kimaono inayoibushwa ni ile ya jamii ambayo hapo awali ilikuwa yenye ushikamano na ushirikiano. Baadaye, ushikamano huo uliathirika kutokana na utamaduni wa kigeni. Hatimaye wanajamii walihamasishana na kuurejelea msingi wa utamaduni wao wa awali. Kwa hivyo, mshairi anadhihirisha suala hili kwa uelekezo wa mchoro na hata kupitia kwa jinsi anavyoandika maneno kama vile kupitia kwa maelezo yanayozingatiwa, hadhira inaweza kujenga mwelekeo fulani kwa kurejelea methali yoyote inayostahiki. Kwa mfano methali kama: „Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu‟ au „kidole kimoja hakivunji chawa, zinaweza,‟ kusadifu katika kuupatanisha ujumbe unaowasilishwa. Hata hivyo, eleweke kuwa upatanisho huu unahitaji utafakari na uzingativu wa methali zilizopo katika utamaduni wa jamii. Kwa njia hii hadhira inashirikishwa kiustadi katika upokezi wa ujumbe. Kwa ambavyo methali ni
kauli ambazo zimezoweleka katika jamii na pia zimetumika mno katika utunzi na uwasilishaji wa mashairi mengi ya kimapokeo, mtunzi wa ushairi usiotumia methali humwachia msomaji wake kuupatanisha ujumbe unaoibuliwa na methali yoyote maarufu anayoitaka. Katika muktadha huu, msomaji anashirikishwa kikamilifu katika harakati za upokezi wa ujumbe. Hii ni mbinu ya msingi katika uwasilishaji wa tanzu za fasihi simulizi.(Kunemah 2008). Hapa ieleweke kuwa, methali ni misemo au kauli fupi yenye hekima fulani na hudhihirisha mkusanyiko na mafunzo waliyoyapata watu wa vizazi vingi vya jumuiya fulani katika maisha yao (Mazrui na Syambo 1992). Kwa mintarafu hii, methali inakuwa ni sehemu moja ya lugha inayoweza kusawiri na kubaini falsafa na matamanio ya jamii kuhusu maisha kwa jumla; hadhira nayo huweza kuichopoa yoyote na kuipatanisha na ujumbe anaowasilishwa katika shairi.
Kimaudhui, methali
zimesheheni tajriba ya jamii ambapo kila tamko au tendo linaloshuhudiwa katika jamii huweza kupatanishwa na kauli mahususi ya methali. Kadhalika, uhalisi huu
unadhihirisha kwamba, uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili unaweza kuzingatia au kutozingatia baadhi ya kauli ambazo zimekuwa zikirithishwa kimapokeo kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Kwa hivyo, si shuruti kwamba ushairi wa Kiswahili uweze kuwasilishwa kwa maumbo, miundo na mitindo ya lugha ile ile ya miaka nenda miaka rudi. Kimsingi, kauli ambazo zimekuwepo katika mawasiliano ya jamii kwa muda mrefu huweza kuwa chakavu na kushosha. Kwa hivyo watu hupendelea mno kauli mpya kama zile zinazobuniwa kibinafsi na wanafunzi wa ushairi. Kauli hizi ni maarufu miongoni wa vijana na zinaweza kuwasilishia mawazo mapya na yenye mielekeo ya kisasa. Katika muktadha wa
uwasilishaji, mitindo na miundo hiyo mipya ya kisanaa kama vile; kutokutumia methali, haizingatiwi ili iwe mbadala wa zile za zamani au zilizozowewa bali ziwe nyongeza kwa zile zilizopo. Kutotumiwa kwa methali katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili kuchukuliwe kuwa ni mchango wa kizazi hiki cha sasa katika kuutajirisha utungo huu uliorithiwa kutoka kwa kizazi kilichotangulia. Dhana ya kutotumiwa kwa
methali katika baadhi ya tungo za ushairi wa Kiswahili ni ushuhuda kwamba, ushairi wa kisasa wa Kiswahili umebadilika kwa kiasi fulani hasa kifani na kimaudhui (Masinde 2003 na Chacha 1987) Kando na hayo, busara katika ushairi wa kisasa wa Kiswahili huweza kuwasilishwa kupitia kwa kauli nyinginezo za lugha zinazobuniwa kibinafsi na watunzi kulingana na hisi au mchomo walionao katika uelekezi wa uhalisi wa maisha yao. Hii ni kwa sababu, dhana ya busara au hekima huwa katika mabadiliko yanayoathiri mielekeo ya jamii hususan katika ushairi wa kisasa wa Kiswahili. Kwa hivyo, ushairi wa Ukimeso,
unadhihirisha mwelekeo kwamba; hakuna ulazima wowote wa kutumia methali katika uwasilishaji wake. Kama ilivyo katika sanaa yoyote ya fasihi, utungo au ushairi unaelekezwa kwanza kwa hisi au mchomo wa msanii kisha baadaye kufanyiwa uteuzi wa fani mahususi ili kujenga mwafaka wa kuwasiliana na hadhira (Jilala 2008 na Njogu na Chimerah 1999). Katika muktadha wa
uwasilishaji wa utungo wa Ukimeso ushairi wa kisasa wa Kiswahili huweza ama kuimarisha au kudhoofisha baadhi ya vipengele vya lugha au kauli ambazo zimekuwa zikithaminiwa mno katika mawasiliano ya jamii. Endapo baadhi ya matumizi hayo ya miundo, mitindo au kauli za lugha zilizozoweleka itafifia, ile maarufu inayobuniwa kibinafsi na kimakusudi na wasanii kwa wakati wa sasa, itastawishwa na itatumiwa zaidi katika uwasilishaji wa tungo za kifasihi hususan ushairi wa Kiswahili. Kwa mujibu wa nadharia
ya Fomula ya kisimulizi ni kwamba, mbinu au fani mahususi zinazotumika katika uwasilishaji wa utanzu wa fasihi huweza kubadilika lakini mwanzoni mabadiliko hayo hukabiliwa vikali na baadaye huzowewa na hukubalika (Woods 1971 na Whallon
1969). Sawia na kutotumiwa kwa
methali katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi wa Kiswahili, kunaashiria mabadiliko ya kimtindo. Hivi sasa mabadiliko hayo ya kiutunzi yanakubalika shongo upande. Hii ndio sababu, hapo awali katika miaka ya sabini hapa Afrika Mashariki, ushairi huru
wa Kiswahili ulichukuliwa kuwa ni utungo wenye mikiki na usiofaa. Ingawa kwa sasa „mgogoro‟ katika ushairi wa Kiswahili haupo au unaendelezwa chini kwa chini kwa kiwango fulani. Kadhalika, „mgogoro‟ huenda ulitokana na kuasi baadhi ya kauli za kimapokeo ambazo ni pamoja na matumizi ya methali ambazo zimekuwa zilichukuliwa
kuwa ni muhimu katika jamii. Aidha, ushairi wa Kiswahili si sugu na hauna budi kubadilika kifani na kimaudhui ili uweze kukabiliana na mabadiliko yaliyopo ya kitamaduni katika jamii za Afrika Mashariki. Katika mkabala huu, ushairi usiotumia methali unaweza pia kuwasilisha maudhui ambayo ni ya kidhahania lakini yenye chemichemi ya ufasiri katika jamii. Sifa Bainifu za Ushairi
Usiotumia methali Kutokana na maelezo
yaliyozingatiwa katika makala hii ushairi wa Kiswahili usiotumia methali wa Ukimeso unaweza
kuwa na sifa za kijumla zifuatazo: a)
Mbinu za uwasilishaji kama vile fani si sugu bali huweza kubadilika kulingana na mabadiliko ya mfumo wa utamaduni na maisha ya jamii. b)
Mabadiliko ya kijamii pia huweza kuathiri mitazamo ya watunzi kuhusu mitindo mahususi ya lugha inayotumika na maudhui yanayoibuliwa na kuwasilishwa katika ushairi. c)
Hakuna ulazimu wa kutumia fani moja au kauli mahususi kama vile methali katika uwasilishaji wa ushairi. Hii ni kwa sababu, baadhi ya kauli msingi ambazo zinaeleweka katika jamii huweza kujengewa mwangwi wake. d)
Sura au vitanzu vya ushairi huweza kuwa ni njia ya kubainisha mitindo mbalimbali inayotumika katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi. e)
Matumizi ya kauli za lugha zilizozoweleka katika jamii huweza kuchakaa na kupisha miundo mipya katika utunzi wa ushairi. f)
Usaili na utafakari unakuwa ni nyenzo muhimu katika uwasilishaji na upokezi wa ujumbe. g)
Hakuna njia moja mahususi inayoweza kutumika katika kuwasilisha hisi na mchomo wa msanii wa ushairi. Katika ushairi wa
Kiswahili kuna mifano ya anuwai ya mashairi yasiozingatia methali katika utunzi na uwasilishaji wake. Hata hivyo baadhi ya sifa hizo zinaweza kubainika kwa kuzingatia mashairi yafuatayo. Diwani
ya Kichomi (i) Shairi la Mafahali
wapigana (uk. 5) (ii) Shairi la Nimechoka
(uk. 34 – 35) (iii) Shairi la Kuchambua
Mchele (uk. 63) (iv) Shairi la Hadithi
ya Mzee (Uk. 69 – 72) Diwani
ya Bara Jingine (i) Shairi la Hatujaaga
Ndoto (Uk. 4 – 5) (ii) Shairi la Bara
Jingine (Uk. 10 – 16) (iii) Shairi la Mruko
wa Nyuki (Uk. 20 – 25) Hitimisho
Makala hii imebainisha
kuwa ushairi wa kisasa wa Kiswahili umebadilika mno kwa upande wa fani msingi
zinazotumika na maudhui yanayowasilishwa. Kutokana na maenezi ya lugha ya
Kiswahili kutoka pwani hadi bara ya Afrika Mashariki, ushairi umekuwa ukitungwa na
jamii mbalimbali za Afrika Mashariki na kwingineko. Kwa ambavyo utungo huu
umestawishwa na umeimarishwa kimatumizi, umeweza kushirikisha mitindo
mbalimbali katika utunzi na uwasilishaji wake. Kwa hivyo, ushairi wa Kiswahili ni utungo
ambao unahifadhi na unawasilisha utamaduni wa jamii ya Afrika Mashariki. Isitoshe,
matumizi ya methali bado yana nafasi muhimu katika utunzi na uwasilishaji wa ushairi
wa kisasa wa Kiswahili. Kwamba, matumizi ya methali yanaweza kuwa angavu
zaidi au matumizi yake hudhihirika kama mwangwi wa kurejelea.
Kuhusu mashairi
yanayojitoa nje ya arudhi za kimapokeo, (au yale yasiyotumia methali) si kwamba tungo hizo
ndio bora zaidi. Kile kinachofanyika ni kuutoa utungo katika mazoea ambayo
yanaelekea kuichosha hadhira. Vile vile, kinachobainika katika mitindo inayotumika katika
uwasilishaji ni upenu mwingine wa kuukuza ushairi; la sivyo kizazi cha sasa na kijacho
kitakuwa na mwelekeo finyu kuhusu ruwaza nzima ya sanaa hii ya Kiswahili. Pamoja na
kwamba ukale (ushairi unaozingatia arudhi za kimapokeo) una uzuri wake; usasa
(ushairi usiozingatia arudhi za kimapokeo) haupasi kudharauliwa. Kwa sababu, kizazi cha
sasa kitahisi kuwa hakipewi uhuru katika kujumuika katika sanaa hii.
Jambo lililo la muhimu
kuuliza ni: kwa nini watunzi wamezuka na mitindo badilia katika uwasilishaji wa utungo
huu? Kimsingi, ushairi wa kisasa wa Kiswahili ni utungo ambao ni kongamano la matini
za lugha na kunga mbalimbali zinazotumika katika utunzi na uwasilishaji. Kwa
hivyo, methali kama ishara au matini zinazotumika katika ushairi wa Kiswahili zichukuliwe
kuwa ni miongoni mwa kauli msingi zinazoshirikishwa na zenye uzito sawia katika
utungo huu. MAREJELEO
Abdalla, A. (1973):
“Ushairi wa Kiswahili na Uhuishwe Usiuliwe”, katika Zinduko. Dar es Salaam: Jarida la
Chama cha Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Abedi, A. (1954): Sheria
za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri. Nairobi: East African Literature Bureau.
Akporobaro, F. B. O. na
Emovon, J. A. (1994): Nigerian Proverbs: Meaning and Relevance Today. Lagos:
Department of Culture. Andrzejejewski, B.W
(2011) Babusa, H. O. (2005):
“Vigezo badilia kuhusu uanishaji wa Mashairi ya Kiswahili”, Tasnifu ya M. A., Chuo
Kikuu cha Kenyatta. (Haijachapishwa). Barthes, R. (1981):
“Theory of the Text”, Ian Macleod (Mt.), katika Young, R. (Mh.) Untying the Text. London:
Routledge. Chacha, C. N. (1987):
“Meaning and Interpretation of Swahili Poetry: A Portrayal of Changing Society”,
Tasnifu ya Ph.D, Yale University (Haijachapishwa) Eco, U. (1976): A
Theory of Semiotics. Bloomington: Indiana University Press. Fowler, R. (1966): “The
Formalaic Theory and its Application to English Alliterative Poetry”, katika Fowler,
R. (Mh.) Essays on Style and Language. London: Routledge & Kegan.
Gibbe, A. G. (1990):
“Ufumbaji katika Ushairi wa Kiswahili”, katika Gibbe, A. G. (Mh.) Jarida la KISWAHILI,
Juzuu 1. Dar es Salaam: Education Services Centre. Hawkes, T. (1977): The
Structuralism and Semiotics. London: Methuen. Hussein, E. N. (1971): Mashetani.
Nairobi: Oxford University Press. Jacobson, J. W. (1960):
“Concluding Statement: Linguistics and Poetics”, katika Seboek, J. (Mh.) Style and
Language. Cambridge: MIT. Kahigi, K. K. na
Mulokozi, M. M. (1979) Kandoro, S. A. (1983):
“Hatua Mbalimbali za Kubuni na Kutunga Shairi la Kiswahili”, katika Makala za
Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili III, Fasihi. Dar es Salaam. TUKI.
Kezilahabi, E. (1973):
“Diwani ya Massamba”, katika MULIKA Na. 13. Dar es Salaam: TUKI.
Khan, M. K. (1975)
Kimaro, K. (2008):
“Washairi huru Wamefilisika kimawazo na kisanaa”, katika Taifa Leo Novemba
10, 2008 Uk. 21. Nairobi: Nation Media Group. King‟ei, G. K. (2007):
“Athari za Washairi Wakongwe juu ya Washairi wa Kisasa: Mfano wa Muyaka bin
Haji na Ahmed Nassir”, katika Kioo cha Lugha, Juzuu la 5. Dar es Salaam: TUKI.
King‟ei, G. K. na
Kemoli, A. (2001): Taaluma za Ushairi. Nairobi: Acacia Stantex Publishers.
Maitaria, J. N. (1991):
“Methali za Kiswahili kama Chombo cha Mawasiliano: Mtazamo wa Kiisimu-Jamii”.
Tasnifu ya M.A., Chuo Kikuu cha Kenyatta. (Haijachapishwa)
Masinde, E. (2003):
“Ushairi wa Kiswahili Maendeleo na Mabadiliko ya Maudhui”. Tasnifu ya Ph.D., Chuo
Kikuu cha Kenyatta. (Haijachapishwa) Mazrui, A. (1994)
Mazrui na Syambo, B.K.
(1992): Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi: East African Educational Publishers.
Mberia, K. wa (2001): Bara
Jingine. Nairobi: Marimba Publications Ltd. ___________ (1997): Natala.
Nairobi: Marimba Publications Ltd. Mohamed, S.A. (1990): Mbinu
na Mazoezi ya Ushairi. Nairobi: Evans Brothers (Kenya) Ltd.
Momanyi C. (1998):
“Usawiri wa Mwanmke Muislamu katika Jamii ya Waswahili kama Inavyobainika katika
Ushairi wa Kiswahili”. Tasnifu ya Ph.D, Chuo Kikuu cha Kenyatta.
(Haijachapishwa) Mulokozi, M. M (2008):
“Nadharia ya Jadi ya Ushairi wa Kiswahili: Je Upo?” katika Ogechi N.O, Shitemi,
N.L. na Simala, K.I. (Wah.) Nadharia ya Kiswahili na Lugha za Kiafrika. Eldoret:
Moi University Press. Mulokozi, M.M. na
Kahigi, K. K. (1973): Mashairi ya Kisasa. Dar es Salaam: Tanzania Publishing House.
Nagler, M.N. (1967): Towards
a Generative View of Formula. TAPA 98. Njogu, K.(1998):
Njogu, K. na Chimerah,
R. (1999 Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi: Jomo Kenyatta
Foundation. Noor, I.S. (1988): Tungo
Zetu. New Jersey: The Red Sea Press Inc. Parker, C.A. (1974):
“Aspects of A Theory of Proverb”, Tasnifu ya Ph.D, Chuo Kikuu cha Washington.
(Haijachapishwa) Sanka, S. M. (1994): Semantic
Deviation in Iraqw Oral Poetry. Tasnifu ya M.A., Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(Haijachapishwa) Senkoro, F. E. M.
(1988): Ushairi, Nadharia na Tahakiki. Dar es Salaam: Dar es Salaam University Press.
Wafula, R.M. na Njogu
(2007): Nadharia na Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Walibora, K. (2007): Malenga
wa Karne Mpya. Nairobi: Phoenix Publishers Ltd. Wamitila, K. W. (2005):
Wood, R. (1971): An
Garland Publishing.
Essay on the Original genus and Writing of Homer. New York: |