METHALI ZA KIUTANDAWAZI
Na. John P. Mbonde
Utangulizi
Katika kuziainisha methali, watu hupenda kuziita kuwa hizi ni za asili ya jamii fulani kama vile ya Kihispania na zile ni za Kiafrika au hizi ni za Kimaasai na hizo ni za Kingoni n.k. Aina hii ya methali, jamii huzidai kuwa ni za asili ya jamii yake (kabila fulani), na hivyo, huzifanya kuwa ni mali yake kiutamaduni kama zilivyo mila na desturi tofauti mbalimbali katika jamii hiyo husika. Kumbe kati ya methali hizo zote, baadhi yake hutumika mahali pote duniani. Aina hii ya methali zitumikazo mahali pengi duniani, ingawa huundwa katika lugha tofauti mbalimbali na wakati mwingine kwa mipangilio yake ya maneno hutofautiana, lakini maana yake huwa ni ileile.
Ni kwa mantiki hiyo, nimeamua kuziita Methali za Kiutandawazi. Nafahamu pia kwamba baadhi ya wanataaluma wangependa kuziita ni Methali za Kimataifa. Jina lolote linaloweza kutumika kuainisha methali hizo, halina utata wala mjadala kwa kuwa zinatumika miongoni mwa mataifa mengi duniani kote. Kamwe methali hizo siyo mpya wala za ajabu wala hazina hadhi ya milenia ya tatu kwa maumbile, bali ni zilezile ambazo zimezoeleka katika matumizi ya kila siku. Ila inawezekana kwamba zinaweza kuwa za asili ya jamii fulani zilizoanza kuzitumia, au hupendelea kuzitumia mara nyingi zaidi kuliko jamii nyingine kwa msukumo wa mazingira. Kwa mfano, lugha ya Kispanishi ina utajiri mkubwa sana wa methali kuliko lugha nyingi duniani. Hali kadhalika, Kichina kimefaulu kuhifadhi methali zake kwa wingi tangu karne na karne.
Madhumuni ya kuzikusanya na kuzihifadhi pamoja ni kurahisisha upatikanaji wake. Fauko ya hayo, huu ni wakati muafaka wa kuzijengea uhalali na hadhi yakinifu methali za kiutandawazi ili kwenda sambamba na maendeleo endelevu ya kisayansi na kiteknolojia. Ifahamike wazi kuwa bado suala hilo linahitaji kufanyiwa tafiti za kina kirefu ili kuboresha dhana hiyo.
Mwenendo wa methali za kiutandawazi hautofautiani na ule wa methali za kawaida. Ni dhahiri kuwa baadhi ya vigezo vya kubainisha methali za kiutandawazi ni ile tabia ya taswira za kimataifa zilizobebwa nazo. Baadhi ya methali huhusishwa na vitu vya eneo dogo la nchi, lakini zile za kiutandawazi hazina mipaka. Kwa mfano,Waarabu wa Pemba hujuana kwa vilemba. Pemba ni kisiwa katika bahari ya Hindi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilemba ni vitambaa wafungazo vichwani. Tabia ya kufunga vilemba vya aina hiyo, hujitokeza huko Pemba miongoni mwa Waarabu katika mashamba ya karafuu. Ingawa maana ya ndani ya methali hii yaweza kabisa kuwa ya kimataifa, yaani ya kiutandawazi. Mathalani, wazungu watawapendelea wazungu wenzao. Ufinyu wa methali za mahali ni sawa na jinsi aina fulani za mila hutawala jamii ndogo ya mahali hapo tu. Kumbe methali Wapiganapo tembo, nyasi huumia (When elephants fight, the reeds get hurt),hii ni methali ya kiutandawazi.
Kwa upande mwingine, baadhi ya methali huwa hazitumiki kila siku, katika ufinyu au utandawazi wake, badala yake huwa zimebaki katika vitabu tu. Ukweli ni kwamba hata baadhi ya misamiati katika kamusi za aina zote za lugha, hubaki katika vitabu kwani matumizi yake ni ya nadra mno kwa sababu au bila sababu za kimsingi. Na kila zinapotumika husikika kuwa ni ngeni katika masikio ya wasikilizaji wake. Hata nchini Tanzania ambako ni chimbuko la historia ya Kiswahili, hususan Zanzibar, kwa namna moja au nyingine, Waswahili hao, si hoja kama ni wasomi au watu wa kawaida, wanaposikia mtu akitumia msamiati au istilahi iwayo utawasikia wakishutumu, “Kiswahili cha siku hizi ni kigumu, jamani! Afadhali ya Kiingereza.” Vivyo hivyo, iwapo Mwiingereza msomi akitumia misamiati isiyotumika katika maisha ya kila siku ya jamii ya Waingereza, wanaposikia hayo hulaani na kusema, “Kiingereza cha wasomi wa siku hizi ni kigumu (bombastic).
- Nini maana ya methali?
Methali ni lugha nyepesi ipenyayo moja kwa moja katika mioyo ya wasikilizaji. Aidha, methali au misemo huondoa wingu au ukungu katika mawasiliano ya kisayansi na ya teknolojia nzito za kitaaluma. Pia, methali ni kielelezo cha utashi wa uhai wa jamii husika, historia na falsafa ya utu wa binadamu, hekima na busara. Mwanafasihi mashuhuri katika Afrika, Chinua Achebe, katika kitabu chake Things Fall Apart (1959: 7) anaandika, “Methali ni mafuta ya mawese ambayo kwayo maneno huliwa.” Kauli hii ikizingatiwa barabara huyafanya maandishi kukubalika kuwa ni fasihi, maana matumizi ya methali na fani nyingine hukoleza simulizi kama tui la nazi na viungo mbalimbali kama vile vitunguu, nyanya, zinavyoifanya mboga iwe na riha na ladha tamu zaidi. Methali ni njia ya mkato ya kuelimisha, kuadilisha, kukosoa na kuelekeza jamii, husuan vijana katika kuzingatia tunu za jadi kwa kina ndani ya mazingira ya asili ya jamii.
“Methali ni aina ya usemi nzito na ambao unakusudiwa kusema jambo maalumu lakini ya fumbo. Usemi huu mzito mara nyingi hukusudiwa kumuonya, kumuongoza, na kumuadilisha mwanadamu. Kwa umbile la nje methali huwa na muundo maalumu, muundo wenye baadhi (pande) mbili. Upande mmoja wa methali huwa unaeleza mazoea au tabia ya mtu au kitu juu ya utendaji wa jambo; na upande wa pili unaeleza matokeo yatokanayo na mazoea hayo au tabia hiyo ambayo imeelezwa katika upande wa kwanza.” (S. Y. A. Ngole na Lucas N. Honero, Fasihi- Simulizi Methali: Kitabu cha pili, (uk viii) TUKI, DUP 1981.
Lugha ya Kiswahili ni tajiri sana kwa semi zake. Licha ya methali, kuna misemo, misimu, nahau. Tofauti na methali misemo ni tungo zitumiazo picha, ishara na tamathali kueleza kitu au wazo kwa kifupi, ili litolewe maadili au maonyo au sifa fulani. Kumbe vitendawili ni semi fupifupi za fumbo zenye kutumia picha, tamathali na ishara kueleza wazo lililofichika ambalo ndilo jawabu la fumbo. Kwa mfano, Koti la mzee halikosi chawa.
Na kwa upande wa misimu ni semi ndogondogo za kuibuka na kufifia au kufa kabisa ambazo huzushwa katika mazingira fulani, hufa baada ya mazingira yale kutoweka. Kwa mfano, Klabu ya Simba ilishinda kwa kishindo cha tsunami.(This coinage was heard by the author while travelling in Dar es Salaam comuters known as “Daladala” hence I personally call such sayings as “Daladala Philosophy” which associate with contemporary events such as ‘tsunami’ impact in which Simba soccer club beat their long time rival, the Younger soccer club with such impact as that of tsunami). Pia, matumizi ya msimu, k.m. Mambo! Poa! Huu ni msimu uliochipua na kuchanua miaka hii ya karibuni, ambao nao siku itafika utanyauka na kufa. Hata Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa ameondokea kuupenda na kuutumia mara nyingi sana anaposalimiana na wananchi kabla ya kuzungumza au kuwahutubia. Akisha sema, “Mambo!” Hadhira humkubalia kwa mkupuo mmoja, “Poa!”
“Methali hutupa maarifa;
hutupa ukweli kwa kifupi;
hufanana katika lugha mbalimbali za nchi kadha za ulimwenguni;
hutumika hasa na wazee kufundisha vijana na watoto, hali ya maisha duniani.” Kutoka katika Utangulizi wa kitabu 500 Haya Proverbs kilichotungwa na Nestor, H. Byera, EALB (1978).
Aidha, kuna ufafanuzi wa aina mbalimbali kutoka kwa wanataaluma wa nyakati mbalimbali kuhusu dhana “methali”. Katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu 1981: 165 “Methali ni kifungu cha maneno yanayotumiwa pamoja kisanii kwa njia ya kufumba au kupigia mfano na ambacho kinachukua maana ndefu na pana kuliko maneno yenyewe yanayotumiwa; muhtasari wa maneno ya kisanii wenye maana pana k.v. Mcheza kwao hutunzwa.”Kuna baadhi ya hadithi nyingi huanza na methali na kumalizia kwa methali. Kwa mfano, katika kitabu kilichotungwa na Kayombo, Innocent Kapilima, Hadithi za Babu Zetu wa Tanganyika, TMP (1959), ametumia mtindo huo wa kuanza na ‘methali’ na kumalizia na methali katika kusimulia hadithi zake.
Zipo methali nyingi ni za Kiafrika pale zinapohusisha na ishara au vitu vipatikanazo katika mazingira yao. K.m. “Jifya moja haliinjiki chungu.”
- Nini Maana ya Utandawazi?
Dhana ya utandawazi ilizuka mwishoni mwa miaka ya 1980 na kushamiri miaka ya 1990 na kuwa changamoto katika nyanja mbalimbali. Utandawazi ni upanukaji kwa kina kirefu zaidi na kusambaa kwa masafa marefu mahusiano miongoni mwa jamii mbalimbali mintarafu uhalisia wa maisha, kuanzia yale ya ustawi wa jamii hadi yale ya harakati za kujikimu, kiuchumi, kiutamaduni, kiulinzi, kibiashara, kiuwekezaji, kimawasiliano, kiteknolojia na kuufanya mchakato mzima kuipelekea dunia iwe mithili ya kijiji kimoja kidogo. Mvuvumko huo wa kiutandawazi kiuchumi na kiutamaduni umeipa Marerkani nafasi ya kasi kubwa ya katika kuhodhi na kudhibiti mageuzi hayo.
“Kwa ufafanuzi wa jumla, dhana utandawazi inamaanisha kuifanya dunia nzima ionekane kama kijiji kimoja kwa kupanuka kwake kimawasiliano, kijamii na kiuchumi katika uhalisia wa mambo ulivyo katika nyanja mbalimbali kama vile uchumi, utamaduni, biashara, uwekezaji, kiteknolojia hata kiroho. Kutokana na welewa huu inadaiwa kwamba uchumi wa dunia umo katika mchakato wa kuoanishwa kwa kuvunja mipaka na nguvu za kiuendeshaji kuwa kitu kimoja.” S.M.Rugumamu, Globalization Demystified, DUP (2005).
Waandishi wengine, kama vile C.K. Omari, Prof. E. Kezilahabi na W.D. Kamera wanasisitiza katika vitabu vyao Misemo na MethaliToka Tanzania (Kitabu cha I&II):
“Misemo na Methali zimejaa wingi wa hekima na mafundisho yanayoweza kutumika katika kufafanua utamaduni wa jamii, muundo na mfumo wake, siasa yake, uchumi na mazingira yake.”
- Mantiki ya Methali za Kiutandawazi
Nimeorodhesha baadhi tu ya methali zenye hadhi ya utandawazi na kuelezea kwa kifupi kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, ingawa ingependeza sana kama tafsiri yake ingeweza kuwa katika lugha ya Kifaransa, Kijerumani, Kichina na katika lugha zingine za kimataifa. Ukweli huu wa methali za kiutandawazi unaenda sambamba kama alivyoandika Hellen Byera Nestor katika utangulizi: “…methali hufanana katika lugha mbalimbali za nchi kadha za ulimwenguni.” Hapa mwandishi huyo kwa kutumia dhana ‘hufanana’ kimsingi alimaanishwa kuwa baadhi ya methali hutumika mahali pengi duniani ingawa ni kwa lugha tofauti lakini maana iliyobebwa katika maudhui yake ni ileile.
Zimepangwa kwa kuzingatia alfabeti ya Kiswahili. Methali za kiutandawazi ni changamoto kwa upande wa maendeleo ya mawasiliano ya kiuhusiano miongoni mwa mataifa. Ikumbukwe kwamba madai kwamba methali za kiutandawazi asili yake ni Ulaya au Marekani kama inavyodaiwa katika masuala mengine mengi ya kiutamaduni na kihistoria. Utajiri uliomo katika methali za kiutandawazi kamwe usimithilishwe na utajiri au maendeleo mengine ya kisayansi na kiteknolojia kutoka katika nchi tajiri duniani na kwenda nchi maskini duniani!
Ni matumaini yangu kwamba mkusanyiko huu wa methali za kiutandawazi utatoa changamoto kwa wanataaluma kujenga wigo mpana na kukita katika kina kirefu cha uchambuzi na upembuzi yakinifu.
4.0 Changamoto
Watu binafsi, serikali na taasisi mbalimbali zinaendelea kupania katika kukikuza Kiswahili. Kutokana na hali halisi ya baadhi ya methali kuweza kupotea miongoni mwa jamii mbalimbali za Kiafrika, mpango maalumu umeanzishwa ili kuweza kuziandika na kuzitolea maelezo methali za makabila mbalimbali ya Afrika kwa kuandika vitabu kadha wa kadha. Mradi huo ambao kila mwezi hutoa methali moja kutoka nchi moja ya Kiafrika, unaweza kuwanufaisha wengi kwa kutumia mtandao kama ulivyo katika tovuti ifuatayo: African Proverbs, Sayings and Stories Website: www.afriprov.org.
Hali kadhalika, kuna vitabu vingi vya methali vilivyoandikwa na watunzi mbalimbali duniani. Katika mradi nilioutaja hapo juu, jitihada zimefanywa na kila mwandishi katika kukumekusanya methali zisizopungua mia moja za jamii yake kwa shabaha ya kuzihifadhi ili zisije zikapotea. Mradi wa methali adimu za Kiafrika ulioanza mwaka 1999 ilimradi kusalimisha methali na misemo ambayo iko hatarini kupotea, hadi 2004 ulikuwa umefaulu kuzikusanya na kurudufu vijitabu kumi na tatu. Kuna tegemeo kubwa kupata ongezeko kubwa kabla ya mwisho wa mwaka huu 2005.
5.0 Hitimisho
Tunaposherehekea Jubilei ya Miaka Sabini na Tano (75) ya mchakato wa kukistawisha Kiswahili (The Inter-Territorial Language [Swahili] Committee iliyoundwa 1930 hadi Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), iliyopandishwa hadhi mwaka 1964), bado safari ni ndefu. Juhudi mbalimbali zilifanywa na serikali hata ikaunda Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) 1967; Idara ya Kiswahili-Chuo Kikuu cha Dar es Salaam 1970; Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni, Zanzibar 1979. Na wakereketwa waasisi walianzisha Chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA) tangu miaka mingi kabla ya kupata Uhuru mwaka wa Tanganyika. Kiswahili hutumika katika nchi nyingi duniani; hufundishwa katika taasisi na vyuo vikuu kadha wa kadha duniani; hutumika katika vituo vya redio na televisheni nyingi duniani; aidha, ni moja ya lugha rasmi za Umoja wa Afrika (AU).
Zifuatazo ni baadhi tu ya methali za kiutandawazi:
METHALI ZA KIUTANDAWAZI
- Ada ya mja hunena muungwana ni kitendo
Kutokana na tabia ya kibinadamu, mtu hutambulika kwa uungwana wake kwa vitendo vyake wala siyo kwa mavazi, maumbile au maneno ayasemayo.
Public opinion maintains, a gentleman is judged by his actions. (Manners make man; or Handsome is as handsome does).
- Akili ni nywele kila mtu ana zake
Akili za watu ni za aina nyingi na ni tofauti kama vile nywele za kila binadamu ni tofauti. Brains are like hair, every humankind has her/his own kind.
- Baada ya dhiki faraja
Baada ya shida huja raha.
After hardship comes relief. (Every cloud has a silver lining; After storm comes a calm).
- Bandubandu huisha (humaliza) gogo
Hata gogo liwe kubwa namna gain, unapolichanachana mwisho gogo hilo humalizika.
Chip! Chip! Finishes the log. (Little strikes fell great oak. Constant dripping wears away a stone).
- Chanda chema hufikwa (huvishwa) pete
Jambo jema husifiwa na hushangiliwa ili liweze kufana zaidi. Ni wana kama kidole kizuri kinapovalishwa pete ili kizidi kupendeza.
A handsome finger gets a ring put round it.
- Chema chajiuza kibaya chajitembeza
Kitu kizuri huonekana bila ya kunadiwa, lakini kibaya hupigiwa debe ili kukitangaza.
A good thing sells itself, a bad thing advertises itself for sale. (Good wine needs no bush).
- Dalili ya mvua ni mawingu
Ishara ya kuwa mvua itanyesha hivi punde ni mawingu meusi makubwa. Na yasipokuwepo mawingu haiwezi kunyesha. Hali kadhalika, katika juhudi zako waweza kujua mapema kama utafanikiwa.
Clouds are the sign of rain. (Morning shows the day as the childhood shows the man. Cunning events cast their shadows before. No smoke without fire).
- Damu ni nzito kuliko maji
Watu wa ukoo mmoja husaidiana sana katika matatizo yao kuliko marafiki au jamaa wa mbali.
Blood is thicker than water.
- Elimu haina mwisho
Elimu ni za aina nyingi. Kila siku maarifa ya aina mpya yanagunduliwa na kuzuka, hivyo haiwezekani kuielewa elimu yote duniani.
Education has no limits. (One has to continue to learn all his/her life time).
- Elimu ni bahari
Elimu ni pana hivi sawa na upeo wa bahari ambayo huelezwa na kusambazwa miongoni mwa binadamu.
Education is like an ocean which spread all over the horizons of people’s life.
- Fadhili za punda ni mashuzi
Shukrani za mtu mjinga ni kumtukana yule aliyemtendea mema.
The gratitude of a donkey is a breaking of wind.
- Fimbo ya mbali haiuwi nyoka
Fimbo iliyo karibu nawe ndiyo ikufaayo wakati inapotokea shida. Methali hii inalenga kuwatanabaisha watu kuwa binadamu anapopata shida ni watu walio karibu naye ndio watakaomsaidia.
A stick in the hand is the one that kills a snake.
- Ganda la muwa la jana, chungu kaona kivuno
Ganda la jana la muwa huwa limekauka, lakini chungu anapolipata huona ni mavuno maridhawa. Maana asiyezoea kuwa nacho, akipatapo hata kama ni kitu duni au hafifu namna gani na kidogo, hushangilia. Mathalani, kukengeuka kwa maadili kwa vijana barani Afrika na kuzamia tamaduni za kigeni.
The skin of yesterday’s sugar-cane is a whole harvest of an ant.
- Gonga gogo usikie mlio wake
Ukitaka kujua mlio wa gogo, lipige na usikilize. Hili lina maana kuwa yakupasa kulichunguza jambo kwanza kabla ya kulihukumu (kulikabili).
Knock a log in order to hear the sound it makes.
- Haba na haba hujaza kibaba
Ukiweka akiba kidogo ya kitu kila mara, mwishoni utakuwa na akiba kubwa. Mwanzo wa makubwa ni madogo.
Little by little fills up the measure. (Little drops of water, little grains of sand, make a mighty ocean and a pleasant land).
- Harakaharaka haina baraka
Jambo lifanywalo harakaharaka, haliwezi kufana. Mambo lazima yaende kwa kuzingatia mchakato wenye mpango na taratibu madhubuti.
Hurry, hurry, has no blessing. (More haste, less speed).
- Iliyopita si ndwele, ganga ijayo
Mambo yaliyopita, yasishughulikiwe sana, bali tujizatiti kuyakabili na kuyadhibiti yale yajayo.
That which has passed is not a diease, cure what is coming.
- Iwapo nia, njia hupatikana
Mtu anapofanya dhamira ya dhati ya kutaka kulitekeleza jambo, hawezi kukosa njia ya utekelezaji.
Where there’s a will, there’s a way.
- Jambo usilolijua ni kama usiku wa giza
Chochote usichokifahamu vizuri huwezi kukieleza kwa ufasaha.
A matter of which you are ignorant is like a dark night.
- Jogoo la shamba haliwiki mjini
Jogoo lililozoea kuishi shamba, likihamishiwa mjini hushindwa kuwika kwa sababu ya mabadiliko ya mazingira yake. Maana, ye yote aliye ugenini yampasa kufanya mambo kwa tahadhari ili kulingana na mazingira ya hapo.
The country cock does not crow in the town.
- Kata pua uunge wajihi
Mtu akikata pua yake kwa ajili ya kujirembesha anakuwa anaiharibu sura yake zaidi.
Cut off your nose to mend your face. (Keep up appearances even at the price of losing your property. Cut off your nose to spite your face).
- Kidole kimoja hakivunji chawa
Mtu mmoja peke yake hawezi kutenda mengi. Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
One finger cannot kill a louse.
- Kuishi kwingi kuona mengi
Kuishi katika dunia kwa muda mrefu humpa mtu nafasi ya kujifunza mengi. Tuwaheshimu wazee kwa vile wanaweza kutushirikisha katika mang’amuzi mengi yenye hekima na busara.
To live long is to see much.
- La kuvunda halina ubani
Harufu mbaya ya kitu kilichooza haiwezi kufichika au kuzuiwa kwa kufukizia ubani. Hali kadhalika, jambo lililoharibika halifichiki.
There is no incense for something rotting (it is impossible to conceal its evil odour).
- Lililoandikwa ndilo liwalo
Lile aliloliweka Mungu litendeke, halishindwi kutendeka kama alivyolipanga. Hii ina maana kuwa Mwenyezi Mungu ni muweza wa yote, hivyo alipendalo hutokea vivyo hivyo. Hakuna awezaye kushindana na matakwa (mapenzi) ya Muumba.
That which is written (by God) is what is (i.e. must surely come to pass).
- Maji yaliyomwagika hayazoleki
Maji yakisha mwagika haiwezekani kuyazoa au kuyakusanya tena. Yaani, jambo likiharibika huwa limeharibika, hata kama likitengenezwa kamwe halitaweza kuwa kama lilivyokuwa hapo awali.
If water is spilt, it cannot be gathered up.
- Milima haikutani, lakini binadamu hukutana
Milima haina uwezo wa kukutana, lakini binadamu wakiwa hai huweza kukutana hata baada ya kuwa mbalimbali kwa muda mrefu. Hii ni methali inayotumika katika kutiana moyo wakati wanapoagana kwamba wakijaliwa watakutana. Pia hutumika katika kuwaonya watu kuacha tabia ya kuwatendea vibaya wengine kwani huenda wao pia wakatendewa hivyo siku za usoni.
Mountains do not meet, but people meet each other.
- Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo
Malezi umpatiayo mtoto huwa ni msingi wa mustakabali wake. Maisha ya mtu yanategemea sana msingi wa malezi aliyoyapata tangu angali mchanga. Ni vigumu kwa mtu kuacha tabia aliyoizoea katika makuzi yake.
As you bring up the child, so he/she will be.
- Njia mbili zilimshinda fisi
Kutokana na tamaa yake kubwa, fisi alijaribu njia mbili ya kushoto na kulia, lakini alishindwa. Mwangata mbili, moja humpokonya.
Two ways failed the hyena.
- Nyumba usiyolala ndani yake hujui ila zake
Mtu hufahamu tu mambo ya nyumba ambamo amelala. Ni jambo la kijinga kwa mtu kujifanya kuwa anaelewa mambo ambayo kwa yamkini hayaelewi.
You cannot know the defects of a house you have not slept in. It is the wearer who knows where the shoe pinches.
- Ombaomba huleta unyonge
Tabia ya kuombaomba vitu humfanya mwombaji kuwa mnyonge au duni. Mlegevu, mzembe, goigoi na mvivu kuwategemea watu wengine, maana hana bidii ya kujitafutia riziki yake kwa kufanya kazi mwenyewe. Mtegemea cha ndugu, hufa maskini.
Begging makes somebody become inferior.
- Ondoa dari uezeke paa
Acha kujenga dari mpaka umalize kuezeka. Mtu anatakiwa kwanza kufanya jambo lililo muhimu kwanza kabla ya mengine yasiyo muhimu.
Remove the ceiling in order to thatch the roof.
- Panapofuka moshi pana moto
Moshi ni ishara ionyeshayo uwepo wa moto. Watu wanaogombana mara kwa mara si ajabu kuwa siku moja wataingia vitani na kusababisha maafa.
Where there is smoke there is fire.
- Paka akiondoka, panya hutawala
Paka na panya ni maadui wakubwa. Paka hutishia sana uhai wa panya kwa kuwakamata na kuwala nyama. Kwa jinsi hiyo, paka anapoondoka, panya hupata nafasi ya kufanya vitu vyao bila ya kuwa na hofu yoyote. Ndivyo ilivyo kwa wafanyakazi, endapo mkubwa wao akiondoka, walio chini hujiona kuwa huru na hufanya mambo wapendavyo.
When the cat goes away, mice do reign. When the cat’s away, the mice do play.
- Penye watu wengi hapaharibiki neno
Mahali ambapo kuna watu wengi hapaharibiki neno. Walipo watu wengi hubadilishana mang’amuzi na hivyo fikira na nguvu zao hukusanywa pamoja ili kulitengeneza jambo. Penye wengi pana Mungu ambaye ni muweza wa yote.
Where there is a gathering of people nothing goes bad. Where there are many people, there God is (Vox populi vox Dei).
- Radhi ni bora kuliko mali
Kupata radhi ya wazazi ni bora kuliko kupata mali. Baraka ya wazazi haiwezi kupatikana hivihivi tu, lakini mtu anaweza kutafuta mali wakati na mahali popote. Kwa hiyo, yatupasa kuwatii wazazi (wakubwa) wetu ili watubariki ndipo hata tutafutapo mali au riziki huwa tumekwisha pata baraka ya mafanikio maishani kutoka kwa wazazi.
Blessings are better than wealth.
- Rahisi haihalisi
Kitu au bidhaa ipatikanayo kwa bei poa ni kitu hafifu hivyo huwa si kizuri na hakifai. Cheap things are not worthy spending money on them.
- Sikio halilali njaa
Hapana siku ipitayo bila ya sikio kusikia maneno fulanifulani yawe mabaya au mazuri. Hivyo sikio halilali bila ya kusikia neno.
An ear does not go to sleep hungry (there’s always plenty of gossip).
- Sumu ya neno ni neno
Moto huzimwa kwa maji na pia neno humalizwa na neno. Likizuka neno au jambo linalowafanya watu kulisema sana au uvumi fulani, ule uvumi huendelea hadi pale uvumi mwingine tofauti utakapotokea. Basi, hapo watu husahau ule uvumi wa kwanza wakaushika ule uvumi mpya.
The poison for a word is a word. Tit for tat.
- Tamaa mbele, mauti nyuma
Mtu mwenye tamaa nyingi mwishowe hupatwa na misiba mibaya. Anayetanguliza tamaa na ubinafsi mbele ajue hana mwisho mzuri.
Desire first, death afterwards (i.e. No one ever thinks of the possibility of death when concentrating on achieving a particular end). Man proposes, God disposes.
- Taratibu ndio mwendo
Mwendo wa polepole ndio ufaao. Yaani, jambo lolote lile halina budi kufanywa kwa kuzingatia kanuni.
Slowly is indeed the way to walk. He that goes slowly goes surely. Hasten slowly. Slow but sure.
- Uchungu wa mwana, aujua mzazi
Mzazi ndiye anayepata uchungu mwingi zaidi ya watu wote anapomzaa mtoto wake. Yaani mwenye kuthamini kitu chochote kile ni yule mwenye kitu hicho. Kwani ni yeye ndiye aliyetaabika katika kukitafuta na kukipata.
The labour of childbirth is known to the mother.
- Ukiona vinaelea, vimeundwa
Ukiviona vyombo vya kusafiria vinaelea juu ya maji, ujue kwamba ni matokeo ya juhudi na maarifa ya watu waliovitengeneza. Kizuri chochote ukionacho, ufahamu kimepatikana kwa bidii na jasho na siyo kwa miujiza.
If you see vessels afloat, remember that they have had to be built.
- Usipoziba ufa, utajenga ukuta
Usipoukarabati ufa kwenye ukuta mapema, ukuta utabomoka na hivyo utalazimika kuujenga ukuta tena. Usipolirekebisha kosa dogo tangu mwanzo, utapata hasara kubwa hatimaye.
If you do not fill up a crack, you will have to build a wall. A stitch in time saves nine.
- Vita havina macho
Wakati wa vita mtu ye yote yule anaweza kuumizwa, kuuawa au kupata madhara ya aina yoyote ile. Ni vema kujiepusha na vita.
War has no eyes (i.e. it kills indiscriminately).
- Vita vya panzi furaha ya kunguru
Panzi wanapopigana na kuuana kwa wingi ni furaha ya kunguru kwani hupata chakula chao kwa urahisi. Hali kadhalika, maafa ya wanyonge huweza kuwa furaha ya wakubwa.
A fight between grasshoppers is a joy to crows.
- Wapiganapo tembo, nyasi huumia
Ndovu wawili wakipigana, husababisha nyasi kukanyagwakanyagwa na kuharibika. Yaani viongozi wawili wanapopigana wanaoumia ni wafuasi au watu walio chini ya himaya zao. Wakati mataifa makuu mawili (k.m.Warusi na Marekani wakati wa vita baridi) yanapopigana, mataifa madogo ndiyo yanayoumia.
Where elephants fight, the reeds get hurt.
- Ya kale hayapo
Yale yaliyotokea zamani yamekwisha na yanapaswa kusahauliwa. Hapana haja ya mtu kuwa na kifundo cha moyo kwa ubaya aliofanyiwa hapo zamani.
The ancient (things) are no longer with us. Let bygones be bygones.
- Yote yang’aayo si dhahabu
Si kila kionekanavyo kinameremeta ni dhahabu. Kwani viko vingi ving’aavyo, lakini ambavyo si dhahabu na ni vya thamani ndogo mno kuliko dhahabu. Usikipende kitu kwa uzuri wake wa nje, bali ukichunguze sana ili ujue ubora wake. Uzuri wa mkakasi ndani kipande cha mti.
All that glitters, do not think it is gold.
- Ziba mwanya, asipite panya
Ukisha kugundua mwanya wa panya, fanya hima ili uuzibe ili panya wasifanye mazoea ya kuutumia mwanya huo. Mathalani, serikali ikisha gundua mwanya wa bidhaa za magendo haina budi kuharakisha kuuziba mwanya ili kuondokana na ugumu wa kulikabili tatizo hilo baada ya kuzoeleka na walanguzi seuze na wafanyabiashara ya magendo.
Seal the small path so that the rats should not create the habit of using it.
- Zimwi likujualo halikuli likakwisha
Shetani akujuaye hakuli akakumaliza. Watu wa jamii au ukoo moja hawadhuriani kabisa. Endapo wakifanya hivyo, basi huhesabika kuwa ni wachawi.
A devil that knows you will not devour you completely.
|