SEHEMU YA PILI: UANDISHI
7. Matatizo ya Waandishi Chipukizi
C.G. Mung’ong’o
Utangulizi
Uandishi, kama zilivyo sanaa nyingine nyingi, ni kazi ya wito. Ni kazi ambayo si kila atakaye huweza kuifanya. Ni kazi inayohitaji kipaji cha pekee. Tukitamka hivyo hatusemi kwamba kila mwenye kipaji cha uandishi huweza kuwa mwandishi mzuri. La hasha. Mifano tunayo si haba ya waandishi walioanza kwa kutoa kazi zenye kutia tumaini lakini wakaishia kukata tamaa na kuvia. Na hata wengine wakaishia kujihusisha na uandishi mamluki; uandishi wa kutafuta shibe.
Si lengo la makala haya kujihusisha katika mjadala wa kuwalaumu ama kuwatukuza waandishi wa jinsi hiyo. Lengo ni kutaka tu kufafanua na hatimaye ikiwezekana kuelezea kwa nini na kwa jinsi gani waandishi wetu wengi wenye kuinukia hukatishwa tamaa kiasi cha kushindwa kuendeleza vipawa vyao.
Kwa kuanzia makala haya nitapenda kutoa historia fupi tu ya uandishi na utoaji wa riwaya yangu ya awali kabisa kama mtano hai wa hayo nitakayoyajadili huko mbele.
Wale wachache wanaonifahamu katika maandishi yangu wananifahamu kwa kazi mbili tu zilizochapishwa, yaani Mirathi ya Hatari (1977) na Njozi Iliyopotea (1980). Lakini hizo si kazi pekee nilizoandika. Na wala si zote mbili ziliandikwa katika miaka hiyo ya 1970 kama tarehe za andiko zionyeshavyo.
Kulihali, hata hivyo, kazi yangu ya awali kabisa ilikuwa ni Mirathi ya Hatari. Kazi hii ilianza kuandikwa mapema mwaka 1966 nilipokuwa katika kidato cha pili katika shule ya Sekondari ya Kibaha. Lakini kwa sababu ya mzigo wa masomo na kwamba wakati ule sikuwa na mtu wa kunishauri katika maswala hayo ya utunzi sikuweza kuikamilisha kazi hiyo hadi mwaka 1969 nilipoingia kidato cha tano katika shule ya Sekondari ya Azania. Wakati huo mwalimu wangu wa shule ya msingi, Ndugu I.C. Mbenna, alikuwa ni mhariri katika shirika la East African Literature Bureau, mjini Dar es Salaam. Nikaamua kumpelekea maandishi yale ili ayasome na kutoa maoni yake.
Mwalimu Mbenna hakulimatia. Aliisoma hadithi ile akavutiwa nayo sana. Na hatimaye alinirudishia maandishi yale akanipa na mawaidha kadhaa juu ya marekebisho ambayo yangepasa kufanywa kabla muswada haujaweza kuwa katika hali ya kupelekwa kwa mchapishaji.
Niliupokea ushauri wake huo kwa moyo mkunjufu. Nikaurekebisha muswada ule kwa kadri nilivyoweza. Kisha nikampelekea tena ili auangalie kwa mara nyingine. Wakati huo mwalimu Mbenna alikuwa amekwisha hamia Tanzania Publishing House (TPH) kama mhariri vilevile. Basi aliipokea tena kazi ile; akaisoma na kuridhika nayo. Akaamua pia kuipokea rasmi kama muswada wa kuchapishwa na TPH. Huo ulikuwa ni mwaka 1971.
Lakini kwa bahati mbaya mwalimu Mbenna hakukaa sana TPH. Na alipoondoka tu maendeleo ya muswada ule yakaanza kuwa mashakani. Wengi wa wenye maamuzi katika TPH hawakuona thamani ya maandishi yale. Na mgogoro ukazuka juu ya jinsi ya kuushughulikia muswada ule. Kuna wale waliosema urudishwe kwa mwandishi na mkataba uvunjwe, kwani yamkini ulikuwa unalitazama swali ambalo kwa mawazo yao halikuwa la “kimaendeleo” – swala la uchawi. Lakini kwa upande mwingine kulikuwapo pia wale walioufahamu fika utamaduni wa Mtanzania na jinsi imam za uchawi zinavyotawala maisha ya watu. Hawa walisisitiza kwamba kazi ile ilikuwa ni muhimu; kwamba ilipasa ichapishwe baada ya marekebisho fulanifulani.
Ubishi uliendelea, lakini hatimaye kundi hilo la pili lilifanikiwa kujenga hoja kamambe. Na muswada ukarudishwa kwangu kwa ajili ya masahihisho na marekebisho. Huo ulikuwa ni mwaka 1974. Hata hivyo, muswada haukuweza kutoka kama kitabu hadi mwaka 1979.
Kutokana na maelezo hayo mafupi juu ya migogoro michache tu kati ya mingi iliyoikumba riwava ya Mirathi ya Hatari kabla va kuchapishwa, tunaweza kuchanganua makundi makuu mawili ya matatizo yanayomwathiri mwandishi chipukizi katika jamii yetu: matatizo yatokanayo na mwandishi mwenyewe; na yale yatokanayo na ukosefu wa udhamini, hasa kwa upande wa watoaji vitabu.
Matatizo Yatokanayo na Mwandishi
Matatizo yanayoshamiri katika kundi hili kwa kiasi kikubwa ni matatizo ya utunzi. Mwandishi huwa ana wazo analotaka kuliweka mbele ya hadhara katika muundo wa hadithi ama tamthiliya. Pengine huwa hata ameijenga hadithi yake vizuri akilini. Lakini hajui aanzie wapi au aendeleeje kuyaweka masimulizi yake katika maandishi. Kwa jumla matatizo ya hapa huwa ama ni ya kimaudhui ama ni ya kifani.
Kwa matatizo ya kimaudhui shida huwa haipo katika uchaguzi wa maudhui yenye maana kwa jamii ya Kitanzania. Wengi wa waandishi chipukizi, kama asemavyo Penina Mlama (1983:214), wanafahamu fika yapi ni maudhui sahihi na yenye maana kwa jamii hii. Ndiyo maana wengi wao huandika juu ya mapenzi, juu ya ujamaa, juu ya uhalifu, n.k., katika mazingira ya Kitanzania. Bali tatizo lipo katika kutambua viwango vya umuhimu, ama uzito, wa maudhui hayo kwa jamii yetu. Waandishi hawa aghalabu hupata shida kumaizi uzito wa jambo linalozungumziwa, siyo kwa mtu binafsi tu ila kwa taifa zima. Mara nyingi waandishi hawa hushindwa kujua ni vigezo vipi watumie kutambua ipi ni misingi sahihi ya kutumia katika kuchagua jambo la uzito zaidi kwa jamii. Je atumie matakwa gani? Ya kwake binafsi? Ya wachapishaji? Ya wasomaji? Ama ya taifa zima? (Mlama, 1983: 215). Na, mathalani, matakwa ya taifa zima ni yapi? Ni yale ya serikali? Ya Chama kinachotawala? Ama ya viongozi watajika nchini?
Kwa upande wangu mwenyewe, kwa mfano, tatizo lililonisumbua sana lilikuwa ni kutokuwa na itikadi maalumu juu ya maisha. Nilianza kuandika Mirathi ya Hatari wakati bado sijawa na welekevu mkubwa wa mfumo mzima wa harakati za kitabaka nchini. Sikujua ni nani walihusika na harakati hizo, mbinu zao, migogoro iliyopo, na kufanikiwa ama kutofanikiwa kwa pande zinazohusika, n.k. (Khamisi, 1983: 242-243). Kwa sababu hiyo, basi, jambo la uzito zaidi kwa jamii nililiona ni lile linalotamkwa na viongozi watajika majukwaani. Bila kupata ushauri na maongozi mathubuti nilikuwa katika hatari ya kuishia katika ukasuku wenye kudhalilisha hadhi yangu kama mwandishi (Kezilahabi, 1983: 232).
Kwa upande wa fani, matatizo yake kwa waandishi chipukizi ni mengi kiasi kwamba si rahisi kuyachambua yote kwa ufasaha katika makala kama haya. Hata hivyo, kwa mahitaji yetu hapa tunaweza kuyagawa matatizo hayo katika sehemu kuu mbili: matatizo yatokanayo na umbile la ndani la hadithi ama tamthiliya inayohusia, na yale yatokanayo na umbile la nje la kazi hizo.
Umbile la ndani la hadithi ama thamthiliya kwa kawaida huundwa kutokana na vitu vitatu muhimu: mtiririko wa matukio, jumuiya ya wahusika, na mandhari. Hebu basi na tuviangalie vitu hivi kimojakimoja ili tuone jinsi gani humtatiza mwandishi chipukizi.
Tukianza na mtiririko wa matukio tunaweza kusema huu ni mfululizo wa vituko vilivyopangwa kwa pamoja kufuatana na wakati – cha kwanza, cha pili, n.k. – kwa mahusiano sahihi ya migogoro inayojiri. Kwa jumla mtiririko huo wa matukio hutoa takriban ramani nzima ya hadithi ukionyesha waziwazi mwanzo, kati, na mwisho wake (Mung’ong’o, 1981). Kutokana na makala mengi ya waandishi chipukizi niliyosoma na kutokana na uchambuzi uliofanywa na Penina Mlama (1983: 218) tatizo kubwa hapa kwa waandishi chipukizi ni kwamba wengi hawapangi vituko vyao katika mfululizo wenye kujenga ama kuendeleza wazo maalumu. Badala yake huwaweka tu watu wakizungumza na kutenda mambo ambayo pengine hata hayana uwiano maalumu kimawazo, na wala hayana misukumo yoyote. Katika hadithi nyingi, kwa mfano, unaweza ukashtukia watu wanapigana risasi na kuuana bila kuwapo na hata misukumo sahihi inayoleteleza kupigana huko.
Kwa ujumla waandishi wa jinsi hii hulundika tu vituko katika maandishi bila kujali kama vinasaidia kujenga hoja ama wazo maalumu, au la. Hawajali kama vituko hivyo vina misukumo yenye kufanya migongano itokee ama la.
Matatizo hayo yatokanayo na mitiririko dhaifu ya matukio aghalabu huathiri pia uumbaji wa wahusika. Kwa vile wahusika ni sharti wajengwe kutokana na misukumo ya migongano itokanayo na vituko, basi mitiririko dhaifu ya vituko hufanya pia matendo, maneno na mawazo ya wahusika yakose uhalisi na uhusika wa kuaminika (Mlama, 1983: 219).
Swala la mandhari vilevile ni gumu sana kwa waandishi wengi chipukizi. Tanzania ni nchi kubwa yenye makabila mengi, kila kabila likiwa na mila na desturi zake. Hali hii aghalabu humkanganya mwandishi na kumnyang’anya ule uhuru wa kuwapeleka wahusika wake popote apendapo. Hivyo waandishi wengi huishia kuwaweka wahusika wao mijini kwenye utamaduni unaoeleweka kwa urahisi (Kezilahabi, 1983: 227). Lakini matatizo ya kitaifa na kijamii si ya mijini tu. Yapo pia vijijini, tena pengine kwa wingi zaidi huko kuliko hata mjini. Na waandishi chipukizi wajaribupo kuoanisha maisha ya mijini na yale ya vijijini ndipo wanapoingia katika migogoro mikubwa. Kama asemavyo Rajmund Ohly, wanakuwa kama mtu anayejaribu kucheza kamari pasi na utaalamu maalum wa mchezo wenyewe (Ohly, 1981: 82).
Binafsi niliweza kuepukana na matatizo haya kwa kwenda kuishi na marehemu nyanya yangu kijijini, kila likizo, wakati naandika riwaya zangu za vijijini, Mirathiya Hatari(1977) na Njozi Iliyopotea (1980). Ilipasa nifanye hivyo kwa vile nililazimika kuyaelewa vema mazingira ambayo ningeyatumia “kuweka hadharani tatizo la kitaifa” (Kezilahabi, 1983: 227) la uchawi (Mirathi) na uongozi potofu (Njozi).
Umbile la nje la hadithi, kwa upande mwingine, hutegemea sana jinsi mwandishi anavyozitumia nafsi katika usimulizi wake, na jinsi anavyotumia dhana ya wakati. Hapa mwandishi huweza kutumia nafsi ya kwanza ama ya tatu katika masimulizi yake. Huweza pia akaisimulia hadithi yake katika wakati uliopo, wakati uliopita, ama hata wakati ujao (Mbenna, 1971).
Hapa waandishi chipukizi wengi hutatanishwa hasa na matumizi ya nafsi ya kwanza katika masimulizi. Mbali tu ya kujikuta wanashindwa kufafanua zaidi matendo na falsafa za hadithi zao – kwa vile hawawezi kukiuka maono na maonjo ya mhusika anayesimulia hadithi – aghalabu hujikuta wamejiingiza katika masimulizi yenyewe. Katika harakati za kuandika waandishi hawa hujisahau kabisa kuwa wao ni waandishi tu na wala si wasimuliaji wa hadithi yenyewe. Kwa yakini huchukuliwa na mpwitompwito wa hadithi kiasi kwamba hatimaye masimulizi huwa hayatokani na maono na maonjo ya msimulizimhusika, bali ya mwandishi mwenyewe (Mung’ong’o, 1981). Simbamwene, kwa mfano, katika riwaya yake, Mwisho wa Mapenzi (Longman, 1971) amepatikana na tatizo hili kiasi cha kumalizia hadithi yake hivi:
Quote:Askari mmoja alikuwa karibu kabisa na mimi lakini alishindwa kunikamata kwani mguu wangu mmoja ulikuwa tayari baharini. Hapo yule askari alianguka kwa kishindo kikubwa na bunduki aliyoishika mkononi iliwaka moto na risasi yake ikapita juu ya kichwa changu na hapo nikatumbukia baharini.
Hapa msomaji ana haki kabisa ya kumwuliza msimulizi huyu: “Je uliponaje hata ukaishi kuisimulia mikasa iliyokusibu?”
Kwa kifupi basi haya ndiyo matatizo muhimu yampatayo mwandishi chipukizi kimaudhui na kifani. Lakini kwa bahati nzuri ni matatizo yawezayo kurekebika iwapo mwandishi atakuwa tayari kujifunza na hivyo kukuza sanaa yake. Ni matatizo ya kundi la pili, yaani matatizo ya watoaji vitabu na udhamini hafifu, yanayosababisha waandishi wengi chipukizi kukatishwa tamaa na hatimaye vipawa vyao kuvia.
Matatizo ya Udhamini
Kama asisitizavyo Penina Mlama “kuendelea kwa sanaa yoyote kunategemea udhamini wa jamii nzima au kundi la watu katika jamii, na mara nyingi kundi la wanaoshikilia madaraka” (Mlama, 1983: 220). Hapa nchini, basi, mtu angetarajia kwamba katika fani ya uandishi vyombo kama maskuli, vyuo na taasisi mbalimbali, umoja wa watoaji vitabu, umoja wa waandishi, jumuiya ya wahakiki, Chama na Serikali kwa jumla, vingekuwa mstari wa mbele katika kuwatambua waandishi chipukizi na kuwapa hamasa na nafasi ya kukuza vipawa vyao. Lakini hali halisi sivyo ilivyo.
Kwanza kabisa mfumo mzima wa elimu haujajishughulisha kabisa na swala la kufundisha mbinu za utunzi. Pale ambapo somo la fasihi limekuwa likifundishwa basi limejihusisha zaidi na kugogotoa na kuhakiki riwaya, tamthiliya na mashairi, badala ya utunzi wenyewe. Na hata vitabu vya fasihi vilivyotokana na mfumo huo wa elimu vimekuwa vikilengwa zaidi kwa hadhira ya wanazuoni kiasi kwamba haviwasaidii sana waandishi waanzao. Kwa jumla basi waandishi hawa hukosa mwongozo wa kutosha katika hatua muhimu sana ya uandishi wao (Mlama, 1983: 221).
Na hata wale wachache wanaofanikiwa kuokota mbinu za uandishi hapa na pale wakaweza kuandika kazi zao za awali hawaishiwi na matatizo. Shida kubwa kwao zamu hii huwa ni jinsi ya kumpata mtoaji bora wa vitabu vyao. Na hasa nyakati hizi ambapo kilio kutoka katika kila pembe ya dunia ni kilio cha hali ngumu ya uchumi, watoaji wengi wa vitabu – kama si wote – hawana kabisa nafasi ya kumdhamini mwandishi chipukizi. Wanachotafuta wao ni miswada yenye kutoa best sellers za kuwapatia fedha ya haraka haraka ya kuendeshea shughuli zao, basi. Mwandishi chipukizi kwao kwa kweli ni kiumbe wa kuepukwa.
Kwa sababu hiyo, basi, mtu angetarajia kwamba angalau waandishi na ‘wahakiki wenyewe kwa umoja wao wangejizatiti zaidi na kuanzisha udhamini wa aina fulani kwa waandishi hawa wanaoanza. Mtu angetarajia kwamba hata kama hakungekuwa na udhamini mahususi kwa maana ya kusimamia na kugharimia sehemu fulani ya uchapishaji wa miswada ya chipukizi hao, lakini walau kungekuwa na vijigazeti ambamo kazi za waandishi hao zingechapishwa na kuhakikiwa vilivyo. Magazeti katika mfumo wa Chinese Literature, Soviet Literature, n.k., ndiyo ambayo mtu angetarajia kuyaona yameshamiri hapa.
Lakini kwa bahati mbaya hali sivyo ilivyo. Kwa muda mrefu sasa chama cha waandishi hapa nchini kimekuwa katika hali ya kudumaa. Kwa sababu moja ama nyingine hakijaweza kukua kiasi cha kuweza kuchukua majukumu ambayo yanapasa kuchukuliwa nacho. Hapa tatizo la fedha limekuwa ndicho kipingamizi kikubwa katika ukuaji wa chama hiki; kiasi kwamba, mathalan, uanzishaji wa gazeti la chama umebakia tu katika maazimio. Japo binafsi padhani ukosefu wa uongozi mathubuti pia umefanya tatizo hili kuwa zito zaidi ya vile lilivyotegemewa liwe.
Katika hali hiyo waandishi chipukizi wengi wameishia kutumia nafasi zitolewazo na magazeti ya kawaida, kama vile Mzalendo, Mfanyakazi, n.k., kuchapisha hadithi zao. Lakini, kama inavyojulikana, haya si magazeti maalum kwa ajili ya fasihi, na aghalabu uchapaji wao hauzingatii vionjo vya kisanaa. Hivyo mara nyingi utakuta hadithi hizo zikitokea na makosa maridhawa ambayo pengine hayangekuwapo laiti magazeti hayo yangekuwa ni kwa ajili ya maswala ya fasihi tu. Tazama, kwa mfano, hali ya sehemu ya hadithi iliyoambatishwa mwishoni mwa makala haya.
Kwa jumla, basi, utaona kwamba matatizo haya yatokanayo na jamii yenyewe yana athari kubwa sana katika ukuzaji wa sanaa ya mwandishi anayeanza. Kwani, kama anavyosisitiza Penina Mlala, bila udhamini wa kutosha hakuwezi kuwepo na misukumo ya kutosha katika utunzi wa kuuwezesha kukua na kukomaa kiasi cha kuwa na manufaa kwa Taifa zima. Na hata wale watunzi wenye vipawa na ari wataendelea tu kupoteza nguvu zao katika utunzi usiokuwa na kanuni (Mlama, 1983: 221).
Hitimisho
Kwa kuhitimisha basi hatuna budi kujiuliza swali moja muhimu. Swali ni hili: Je baada ya kuyajua matatizo yote haya sasa tufanye nini ili angalau kuishikiza sanaa hii ya uandishi isiyumbe zaidi? Kama tulivyotamka hapo awali kabisa, utunzi ni kazi ya wito. Kuwepo ama kusiwepo na matatizo mwandishi mwenye kipawa na ari ataandika tu katika tumaini kwamba siku moja, inshallah, maandishi yake yatachapishwa. Kwa hiyo la muhimu kwetu hapa, pamoja na kuyajua matatizo, ni kuona jinsi gani mwandishi kama huyu anaweza kusaidiwa kutimiza ndoto yake.
Binafsi juhudi zangu za awali katika uandishi zilisaidiwa sana na juhudi na welekevu wa Mwalimu Mbenna. Lakini si kila mwandishi atakuwa na mdhamini wa jinsi ya Mwalimu Mbenna. Binafsi basi naona jawabu la awali tunalo sisi waandishi. Sisi kwa umoja wetu tunaweza kuanza kutoa mchango angalau mdogo, badala ya kuendelea tu kulalamika majukwaani kwamba utunzi hauna udhamini. Mchango huo nauona, kwanza kabisa ukijitokeza hususani katika UWAVITA, kama chama cha waandishi, kuchukua kikamilifu wajibu wa kuwalea waandishi wake kwa hali na mali, hasahasa katika maswala yafuatayo:
Quote:(a) UWAVITA iunde kamati ya uhariri katika sekretariati yake; kamati ambayo itashughulikia maswala ya ushauri kwa waandishi chipukizi.
(b) UWAVITA ikamilishe mipango yake ya utoaji wa gazeti la chama. Mbali ya kuwa tu uwanja wa kuchapishia hadithi na makala ya waandishi chipukizi, gazeti hilo litasaidia pia katika kutoa tahariri na mawaidha maridhawa muhimu juu ya hali ya fani nzima ya uandishi.
© UWAVITA ianzishe Yearbook yake yenyewe ikiwa katika mfano wa ile ya Authors’ Association ya Uingereza, ambamo maswala yote yanayomhusu na apasayo kujua mwandishi yatafafanuliwa kikamilifu.
Ni dhahiri kwamba mambo yote haya yatahitaji fedha na uwajibikaji mkubwa kwa upande wa uongozi wa UWAVITA. Lakini iwapo maandalizi ya semina hii yanaweza kuwa ni kipimo sahihi cha uwajibikaji huo binafsi, sioni kwa nini majukumu hayo machache yasiweze kukamilishwa.
Marejeo
Kezilahabi, E. (1983) “Utunzi wa Riwaya na Hadithi Fupi” katika TUKI, Makala za Semina… uk. 223 – 238.
Khamisi, S.A.M. (1983): “Hatua Mbalimbali za Kubuni na Kutunga Riwaya” katika TUKI, Makala za Semina… uk. 239 – 252.
Mbenna, I.C. (1970): Uandishi wa Vitabu. TPH, Dar es Salaam.
Mlama, P.O. (1983): “Utunzi wa Tamthiliya katika Mazingira ya Tanzania” katika TUKI, Makala ya semina… uk. 203-222.
Mung’ongo, C.G. (1981); “Fani ya Uandishi wa Hadithi”, Muswada usiochapishwa.
Ohly, R. (1981): Aggressive Prose: a Case Study in Kiswahili Prose of the Seventies. TUKI, Dar es Salaam.
The Writers’ and Artists’ Yearbook A Directory for Writers. Adam & Charles Black, London.
TUKI (1983): Makala za Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili III: Fasihi. TUKI, Dar es Salaam.
KIAMBATISHO I
Kusota Waya
Pamoja na kukutumia utangulizi huu kwa wasomaji wapya wa hadithi hii, ninashauri, kama upo uwezekano, hadithi hii ianze tena upya kwani sehemu kubwa ya maandishi yake katika Toleo lililopita haikusomeka, nadhani kutokana na matatizo ya uchapishaji.
Ninahisi basi, kuwa mtiririko wa hadithi haukupatikana kwa wasomaji walio wengi, kiasi kwamba hata utangulizi huu pengine hautasaidia sana.
UTANGULIZI KWA WASOMAJI WAPYA
MSOTA WAYA, ni fukara – fakiri wa mjini, mhitaji, aghalabu kupata kwake ni kwa mashaka yaliyokithiri.
Msota Waya, hana mpango wowote wa maisha. Kwake maisha ni wakati ule tu anaoooumua. mambo ya saa ijayo au kesho, hayamhusu, yatajijua yenyewe. Hata hivyo apange nini wakati maisha kwake ni seti yenye memba mmoja tu, isiyochagulika; ‘KUSOTA WAYA’?
Basi, kijana Kado Tangatanga ni msota waya.
Katika toleo lililopita tuliona jinsi Kado alivyobahatisha mlo wake wa siku baada ya kupora kapu la unga katika vurumai iliyosababishwa na ile ‘shikashika’ ya watu wa CITY, katika mtaa wa Congo jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, Kapu hilo linaishia mikononi mwa watoto wa mjini… Kidawa, Pili na Chikuwasota waya pia. Kado anaambulia mlo wa usiku.
Kesho yake linazuka tatizo la kulipana ushuru wa mkesha wao wa furaha. Kado hana hela na Kidawa, mtoto wa mjini haelewi wala hataki kuelewa.
Ni nini ada ya msota waya?
“Rudisha hiyo hela Kidawa”. Anamaka Kado, “ona na shati umenichania”.
“Sirudishi… jana tu ulikuwa umejaa kishenzi, sasa unanifunga kamba mwenzio.”
Hawaelewani. Uamuzi wa Kado kutumia nguvu ili kuipata tena noti ile, haufanikiwi. Anaishia tu kupandisha hasira na kumchapa vibao Kidawa. Kisha anatimua mbio… asichelewe kazini; la sivyo atakuta majina ya vibarua wa siku hiyo yamejaa.
Anapoikaribia barabara, analiona gari dogo jekundu. Analitambua mara moja. Ni gari la Meneja wa Kazi, kule kiwandani, Bwana Riziki. Ni mara nyingi sana Kado amekuwa akimsujudia meneja huyo ofisini mwake kuomba ajira ya kudumu, lakini daima huambulia jibu lile lile la – SUBIRI KIJANA”, na kisha Meneja huyo humpungia mkono, ule umwambiao, “Nipishe basi ofisini”.
Kado anakurupuka bila kufikiri. Anaifikia barabara sawia na lile gari jekundu. “Rift Mzee… anapaaza sauti. Kinachomjibu ni dhoruba la maji machafu yaliyorushwa na gari hilo kutoka kwenye dimbwi. Yamempata Kado barabara usoni na hata mdomoni yameingia. Anatema chini mara nyingi tu, huku akitukana na kumlaani bwana Riziki. Hata hivyo, Kado anakaza tu mwendo.
Anapofikia kwenye lango kuu la kiwanda ni saa mbili kamili: Yuko hoi, jasho linamvuja. Ghafla, macho yake yanakumbana na maandishi manene mekundu, yaliyobandikwa kwenye lango; “AJIRA ZA VIBARUA ZIMESIMAMISHWA.” Nguvu sasa zinamwishia Kado. Anatamani akae chim. Kwa muda wa miezi tisa sasa amekuwa akifanya kazi kiwandani hapo kama kibarua na kila mkupuo wa ajira ulipokuwa ukiisha amekuwa akibadilisha majina kwa maelewano maalum na karani ili aendelee kuajiriwa. Lakini sasa alikuwa kanyolewa bila hata kupewa nafasi ya kutia maji.
Kado, akiwa amekata tamaa kabisa, anaanza kurudi nyumbani kinyume nyume. Pengine kakumbwa na kihoro. Sasa yupo katika barabara kuu ya Pugu, pasipo kujua. Anazidi kwenda kinyumenyume tu huku akijisema mwenyewe. FEDHEHA YA FEDHA.
Honi kali ya gari ndiyo inayomshtua. Ikafuatia sauti kali ya matairi ya gari yakichunika kwenye lami. Kado kutanabahi tu, yuhewani. Sekunde chache baadaye anashtukia amelala chali katikati ya barabara. Umbo kubwa ajabu la mwanamme wa kihindi limemwinamia.
“Dugu mimi hapana gongo… yeye naruka kabla,” huyo mhindi mnene anasema kwa wasiwasi. “Kwa nini, bana yeye navuka hii ‘highway’ kwa ‘aboutwalk’… Nachezea kifo eeh…” Baada ya kusema hayo huyo mhindi anakimbilia kwenye gari lake. Kado naye anajizoazoa chini na kusimama, lakini anapoangalia chini, anachanganyikiwa; kuna damu juu ya lami.
“Wee mhindi usiondoke, umenigonga, umeniumiza… twende polisi,” sasa Kado tayari kalifikia lile gari na kumkaba koo yule mhindi kwa kulitumia shati lake.
Kado hana habari kuwa mtu aliyemkaba ni yule milionea wa kihindi jijini Bwana Patel Kumar, mtengenezaji na msambazaji maarufu wa mapochopocho nchini kote. Kati ya vitu aviogopavyo Bwana Patel duniani mbali na kifo, ni polisi na sheria. Baada ya yeye pia kuona ile damu barabarani, na sasa kutamkiwa neno POLISI, anaanza kuhisi hali ya hatari.
“Bana, wacha hii shingo yangu… naumiza mimi bure. Mimi najua veve naumia kidogo tu. Mimi sasa talipa veve pesa ya kwenda Hospitali. Hapana sema yule Kumar wa pochopocho nagonga mtu Pugu Road’… sema veve nateleza tu naanguka”. Hapo hapo ikafunguliwa ‘brief case’. Nusura Kado apofuke kwa kuziona tu pesa zilizokuwepo… Nyingi mno, Patel Kumar akamega neti kasi tu, na bila kuzihesabu akamkabidhi Kado.
Kado anasogea p’embeni mwa barabara huku akihema na Patel analiondoa gari lake kwa kasi.
Kumbe alikuwa kachubuka sana mgongoni. Hayo anayagundua Kado baada ya maumivu kuanza kujitokeza. Anapoanza kujisikia vibaya zaidi, anasimamisha ‘texi’.
“Nipeleke Muhimbili”, anamueleza dreva.
NG’OMBE WA MASKINI
Wakiwa safarini, Kado anafanya kazi ya kuhesabu zile pesa. Anapomaliza, anashangaa; Ni shilingi thelathini na saba elfu. Sasa anatabasamu. Ala… kumbe hata ng’ombe wa maskini huzaa pacha; sasa Kado anapanga mengi kichwani mwake. Anapanga kuanzisha biashara, kuoa na mengineyo. Anaangua kicheko na kunyamaza…
Wanapofika Muhimbili dreva anageuka nyuma.
“Hallo… Brother tumefika”: Kimya, “Aisee, Ndugu… umesinzia…” kimya.
Maskini, dreva anapomgusa Kado, ndipo anapogundua kuwa abiria wake ni mkavu wa jana; maiti.
TAARIFA YA DAKTARI
“Marehemu Kado Tangatanga, yaelekea aligongwa na kuanguka-Amekufa kwa kuvuja damu ndani kwa ndani.”
“Maskini, maiti ya Kado, haikupata mtu wa kuitambua. Alizikwa na watu wa CITY.
Ndiyo ada ya msota waya hiyo; kufa kama mbwa na kusahaulika.
|