MISEMO YA VYOMBO VYA USAFIRI (2) - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Semi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=49) +---- Thread: MISEMO YA VYOMBO VYA USAFIRI (2) (/showthread.php?tid=731) |
MISEMO YA VYOMBO VYA USAFIRI (2) - MwlMaeda - 08-02-2021 Misemo yenye Ujumbe kuhusu Maisha kwa Ujumla 1. “Ajali sio kugongwa na gari tu, hata kukosea kuoa au kuolewa pia ni ajali”
Maana:
· Kuoa au
kuolewa ni jambo linalopaswa kufanywa kwa umakini sana. · Ndoa njema
ni kiini cha furaha na mafanikio; ndoa mbaya ni kiini cha faraka na maangamio ya kimaisha. · Waoaji au
waolewa wanapaswa kuzingatia vigezo vya msingi katika kutafuta wenza wa kuishi nao. · Mwenza akiwa
mkorofi ndani ya ndoa, maisha kwa ujumla huwa magumu na machungu. 2. “Asili haipotei”
Maana:
· Mambo ambayo mtu aliwahi kuyafanya katika maisha
yake ya awali hayawezi kubadilika yote hata kama atabadilisha mfumo au mtindo wa maisha au utamaduni. · Mtu hawezi kusahau kwao.
· Hata mtu awe katika maeneo ya mbali na kwao bado
vitu vya asili yake vitaendelea kubakia katika kumbukumbu zake; hivyo atavitamani avipate. 3. “Bora uzima”
Maana:
· Vitu vyote ukose (kiuchumi, kielimu au kijamii)
lakini uzima (na uhai) uwepo. · Mtu hata akiwa na ulemavu wa namna yoyote, bado
sio tatizo ili mradi yuko hai. · Mengine yote ni ziada, kilicho muhimu ni uhai.
4. “Born to suffer”
Maana:
· Duniani ni sehemu ya kuchakarika, siyo kulegea.
· Maisha ni kazi
· Kiumbe yeyote anayeishi hapaswi kutetereka hata
kidogo. · (Mwandishi) Amezoea matatizo, shughuli ngumu,
shida na madhila mengine ya hali ngumu ya maisha. · (Mwandishi) hatishwi na lolote linaloambatana na
harakati za maisha. 5. “Chanda chema….?
Maana:
· Mtu anayetenda mema hutuzwa.
· Ni vema tutende mema ili tuhifadhiwe au majina
yetu yatajwe vema hata baada ya kuondoka duniani. · Mambo mema huhifadhiwa vizuri na kwa fahari.
6. “Bora uzee kuliko uzembe”
Maana:
· Ni afadhali Mzee (ambaye mara nyingi nguvu huwa
zimemwishia) hufanya mambo yake taratibu na kwa umakini mkubwa, lakini hufanikiwa au hufika mwisho; kuliko mtu mzembe ambaye huacha au husita kufanya jambo kwa makusudi na mwisho haambulii chochote au hupata madhara. · Uvivu hauna faida katika maisha.
· Vema kujitahidi katika jambo fulani lenye
mafanikio kuliko kuliacha kabisa. 7. “Hakuna tuzo ya ngono zaidi ya UKIMWI”
Maana:
· Uzinzi na Uasherati una hasara kubwa kwa mtu na
jamii; hasara kubwa ni kwa mhusika kupata maradhi kama vile UKIMWI. 8. “Butua uwakomboe wenzako”
Maana:
· Tujenge tabia ya kuwasaidia wenzetu.
· Fanya lolote uwezalo ili kuwasaidia walio chini yako.
· Kumbuka kutumia kile ulichoruzukiwa na Mola kwa
kuwasaidia masikini. 9. “Hata bibi alikuwa binti”
Maana:
· Maisha ni mapito yanayomtokea binadamu hatua kwa
hatua, hivyo, kuwa makini na kila hatua ya maisha. · Uhai, umri au utajiri huwa havidumu milele, bali
huisha au hubadilika baada ya muda. · Fanya ufanyalo lakini jua kuna kesho.
· Kila jambo lina wakati wake.
10. “Bosi hanuniwi”
Maana:
· Bosi (kiongozi) hata akikosea kwa waajiriwa wake
hawezi kuchukiwa, kwani yeye ndiye aliyeshinda maisha yao kiuchumi. · Mwenye mali au pesa anaweza kufanya chochote kwa
asiye nazo. · Katika kutafuta maisha tunaaswa kupambana na
changamoto mbalimbali zinazojitokeza. 11. “Bora lawama kuliko hasara”
Maana:
· Ni bora mtu kumweleza ukweli wa jambo hata kama
hapendi, kuliko kukaa kimya na baadaye kitu kibaya kikatokea kutokana na huo ukimya. · Hasara ni adui wa maendeleo.
· Ni bora ulaumiwe kuliko kuingia matatizoni.
· Kabla ya kukubali kufanya jambo au kitu
chochote, ni vema kuangalia na kupima matokeo yake. . Mtu anapaswa kuchukua uamuzi unaoleta madhara
madogo kuliko ule unaoleta madhara makubwa. Chanzo:
Ponera, A. S na Kikula, I.S, (2017) Misemoya Vyombo vya Usafiri. UDOM. Afroplus Industries, Ltd. |