DHANA YA MISEMO KWA UJUMLA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Semi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=49) +---- Thread: DHANA YA MISEMO KWA UJUMLA (/showthread.php?tid=729) |
DHANA YA MISEMO KWA UJUMLA - MwlMaeda - 08-02-2021 Misemo huweza kuelezwa kuwa ni vifungu vya maneno ambavyo hutumiwa ili kuleta maana fulani (Ponera, A.S na Kikula, I. S, 2017). Kwa kawaida, sura ya nje ya misemo siyo lazima iafikiane na maana halisi ya vifungu hivyo vya maneno. Hii hutokana na ukweli kuwa misemo hutumia lugha ambayo si ya moja kwa moja huku ikibeba mvuto na mnato maalumu kwa hadhira (Mng’aruthi, 2008; Kunemah, 2008; Wamitila, 2010; Kipacha, 2014; na Ponera, 2015. Ponera (2015) anabainisha sifa bainifu za misemo kuwa ni: a) Hushabihiana sana na vipengele vingine vya semi kama vile methali.
b) Hutamalakiwa na lugha isiyo ya moja kwa moja
c) Huchimbuka katika visa, mikasa, matukio na vitushi vitokeavyo katika maisha ya kila siku katika jamii
d) Huwa na unyumbufu mkubwa wa kimatumizi kuliko vipengele vingine vyote vya semi. Yaani, misemo hutumika hata katika mazingira au mazungumzo yasiyo rasmi.
e) Hubadilika (na hata kutoweka kulingana na wakati) kutokana na ukweli kwamba chimbuko lake kuu ni visa, mikasa, matukio na vitushi vya kila siku
f) Muundo wake wa kimatumizi huanzia kwa watu wa daraja la chini (watu wa kawaida; wasiokuwa wasomi, watu maarufu wala viongozi)
g) Hufanya kazi kama mwamvuli wa vipengele vingine vya semi. Yaani, misemo huruhusu kubeba sura mbalimbali za semi.
Mhamo wa Ruwaza katika Matumizi ya Misemo
Ruwaza zinazorejelewa hapa ni zile zinazohusisha misemo hiyo kuandikwa katika:
a) Mavazi kama vile khanga, fulana au kofia
b) Vifaa mbalimbali kama vile vikombe, makawa, na vipepeo
c) Maeneo ya umma kama vile vyoo vya umma (vituo vya mabasi, sokoni, shuleni), madarasani (kwenye mbao za paa au ukutani).
d) Vyombo vya usafiri kama vile mabasi, malori, na hivi sasa kwenye pikipiki (za kawaida na zile za magurudumu matatu – bajaji)
e) Kwenye mitandao ya kijamii kupitia nyenzo mbalimbali za kielektroniki. Hapa tunakusudia misemo itumiwayo na watumiaji wa mitandao ya kijamii kama kauli-hadhi (status) zao. Haya ni matokeo ya majilio na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Mathalani, mitandao ya kijamii kama vile facebook na WhatsApp imekuwa maarufu katika kuibua misemo mbalimbali inayowekwa kama kauli-hadhi ya mhusika.
|