NI NANI KAMA MWALIMU.
------------------------------------
1.
Naja nikiwakumbusha kuipitia nudhumu,
anayejenga maisha, laazizi maalimu,
yule alotufundisha, kwanza kushika kalamu,
NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI?
2.
Nalola siku ya kwanza, nikipelekwa shuleni,
na wakati nilianza, kuingia darasani,
mwalimu alinifunza, 'lufabeti kwa makini,
NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI?
3.
Sana nilizikariri, herufi alonifunda,
tena nikiwa mahiri, wa nyimboze nilopenda,
hadi leo ninakiri, nafaidi ye matunda,
NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI?
4.
Nakumbuka nikianza, kuandika mchangani,
kalamu yangu ya kwanza, ni kijiti wajameni,
Huyo aliyenifunza, mgee kheri Manani,
NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI?
5.
Nakumbuka kuhesabu, tangu moja hadi kenda,
wakati 'likuwa tabu, ikiwa inanishinda,
chonde chonde taratibu, mlezi akanifunda,
NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI?
6.
Leo miye mhasibu, taasisi ya takwimu,
mdogo wangu tabibu, jijini Darisalamu,
si kwa bahati nasibu, ni matunda ya mwalimu,
NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI?
7.
Wanoitwa wata'lamu, wa'zo maridhawa fani,
alowafunda mwalimu, leo wakuu nchini,
mlezi wangu mwalimu, sana ninakuthamini,
NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI?
8.
Kumbukeni ni mwalimu, wa mataifa mlezi,
alowagea elimu, wa dunia welekezi,
kiongozi ufahamu, yoyote uliyo ngazi,
NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI?
9.
Na wasifa wake jama, haumaliziki wala,
ndefu ja hadithi kama, alufu lela ulela,
namuombea salama, nipulike wangu Mola,
NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI?
10.
Subukhana shukurani, beti kumi kutimia,
yaliyokuwa moyoni, hadhira nimepatia,
na baraka maishani, walezi n'kiwatakia,
NI NANI KAMA MWALIMU, HUSUSAN WA MSINGI?
*********
Rwaka rwa Kagarama, (Mshairi Mnyarwanda).
Jimbo la Mashariki, Wilaya ya Nyagatare,
JAMHURI YA RWANDA.
Nna swali kuhusu neno 'mzungu' je maana yake haswa ni nini na kiasili laweza kuwa latoka wapi? Fursi?
Nami nikamjibu?
Waalaykum salaam. Asili yake ni Kiswahili; si Kifursi. Mzi(zi) wa neno hilo ni "zung-". Kutokana na mzi huo ndio twapata vitenzi: zungua, zunguana, zungulia, zunguliwa, zunguka, zungusha; na kadhalika. Na twapata nomino (majina): mzunguaji, mzunguliwa, mzunguka, mzungusha; au mzungu, kizungu, uzungu, na kadhalika.
Pengine utauliza: Vilikuwaje hata Mswahili akamwita huyu mtu "mweupe" kutoka Ulaya "mzungu"? Kuna nadharia tatu:
Ya kwanza ni kwamba mtu huyu alipokuja Uswahilini, au Afrika kwa jumla, hakutulia mahali pamoja, bali alizungukazunguka kutafuta mahali pamfaapo kukita hema lake au kukipata kile alichokuwa akikitafuta - khaswa utajiri wa nti zetu. Kwa hivyo, kutokana na kuzungukazunguka kwake, akaitwa mzungu; yaani mzungukaji.
Nadharia ya pili yatokana na maana ya pili ya neno "mzungu" (wingi wake ni "mizungu") - neno ambalo likitumika katika Kiswahili hata kabla ya mtu mzungu kuja pande za kwetu. Na maana hiyo ndiyo ambayo kwa Kiingereza huitwa "trick." Kwa vile mzungu alipokuja makwetu, mbali na kutumia nguvu za silaha, ndia nyengine aliyoitumia ili kutawala ilikuwa ni urongo na kuwahadaa wenyeji ili apate kuwatawala. Kwa hivyo, akaitwa "mzungu" kwa maana ya kwamba ni mtu wa kuhadaa watu - a man of tricks.
Nadharia ya tatu ya kwa nini aliitwa "mzungu" yatokana na neno la kale la Kiswahili, "mzungupule" ambalo maana yake ni mtu mwerevu; na uwerevu ni uzungupule. Kwa vile mzungu alipokuja makwetu watu walimuona kuwa ni mtu mwenye akili na ajuaye mambo mengi, basi wakamwita "mzungu"; yaani mtu mwerevu, mwenye akili. Sijui ni ipi kati ya hizo tatu ndiyo nadharia ya sawa.
Natumai nnafahamika, ingawa nnayaandika haya haraka haraka na bongo langu hivi sasa lashughulika zaidi na kujiuguza; halikutulia.
~ Abdilatif Abdalla
Hamburg, Ujarumani
6 Juni 2019
Posted by: MwlMaeda - 10-01-2021, 07:32 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
TANGAZO GAZETINI
ULAMAA HEMED
Shikeni hili gazeti, kuna tangazo msome,
Kurasa za katikati, wa mabondeni wahame.
MFAUME HAMISI
Sababu hasa ni nini, tuache makazi yetu,
Tueleze tubaini, au eneo la mtu?
ULAMAA HEMED
Imesema serikali, watu wahamie juu,
Mvua itakuwa kali, masika ya mwaka huu.
MFAUME HAMISI
Kauli hiyo si kweli, serikali imezusha,
Wataka eneo hili, lengo ni kutuondosha.
ULAMAA HEMED
Hebu acheni ubishi, fateni mnoambiwa,
Mkiona ni uzushi, kwa nguvu mtatolewa.
MFAUME HAMISI
Mvua tangu azali, mbona huwa inanyesha?,
Na tena zilizo kali, wala sio rasharasha.
ULAMAA HEMED
Wataalamu wasema, kumechafuka angani,
Hivyo hameni mapema, kabla ya tafarani.
MFAUME HAMISI
Hiyo ni danganya toto, hapa haondoki mtu,
Nayatufike mazito, ila hatung’oki katu.
ULAMAA HEMED
Juwa ni hasara kwenu, mafuriko yakifika,
Zapotea mali zenu, kupata mlisumbuka.
MFAUME HAMISI
Hayo uloelimisha, yaweza kuwa huwenda,
Ili wakituondosha, ni wapi tutapokwenda?
ULAMAA HEMED
Hilo wala usijali, kujuwa wapi muende,
Kumbuka wale awali, walikwenda Mabwepande.
MFAUME HAMISI
Najua sio mjini, watatupeleka shamba,
Ila twataka baini, watatujengea nyumba?
ULAMAA HEMED
Kujengewa sitaraji, ila viwanja mwapewa,
Pia huduma za maji, na umeme mwawekewa.
MFAUME HAMISI
Hapo bila ya kupinga, naiona ahueni,
Pili nimepata mwanga, hakufai mabondeni.
ULAMAA HEMED
Kwa kuwa umeelewa, athari utaepuka,
Nishamaliza kahawa, kwa herini naondoka.
MFAUME HAMISI
Asante ndugu yangu, sina cha kusubiria,
Naacha ubishi wangu, bondeni napakimbia.
Watunzi:
1: Mfaume Hamisi
(Mshairi Machinga)
0716541703
2: Ulamaa Hemed
(Fundi wa tungo)
0717 501557
Posted by: MwlMaeda - 10-01-2021, 07:08 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
NIJILE TAKA IDHINI
Nijile ndimi nijile, nijilepo pa kujiwa
Nami sijile na kele, zitazozusha beluwa
Nijile tuteze lele, na shingo tukizitowa
Kama idhini ‘tapawa
Nijile tuteze lele, na masogora wenzawa
Na ngoma hizi na zile, zipibwapo kutezewa
Nami ‘tateza vivile, midundo hiinyakuwa
Kama idhini ‘tapawa
Nami ‘tateza vivile, uwandani sitakawa
Na watezewa waole, wafurahi watezewa
Na ijapo mizingile, ‘tangiya kuizinguwa
Kama idhini ‘tapawa
Na ijapo mizingile, izingayo wazingiwa
Hata yangawa ni mile, ‘tajit’atuwat’atuwa
Nazo kumbi zilo tele, ‘tazingiya za kungiwa
Kama idhini ‘tapawa
Nazo kumbi zilo tele, ziso matango na t’uwa
‘Tazingiya nizikale, nikeleti kwa sitawa
Kwa hayano na hayale, nizishize zangu ngowa
Kama idhini ‘tapawa
Kwa hayano na hayale, na mengine sitotowa
Mhariri nikujile, ufanye vya kufanyiwa
Na ambavyo vilekele, ni hayano kuchapiwa
Kama idhini ‘tapawa
Na ambavyo vilekele, naweta wa kuwajuwa
Zuberi Lesso nijile, nawe nalishawishiwa
Ahadi nitimizile, ‘siwe mbwa kulaumiwa
Kama idhini ‘tapawa
Ahadi nitimizile, Shabani Gonga tambuwa
U miyongoni mwa wale, walio wana welewa
Numa numa ‘siketile, nikaja nikakutiwa
Kama idhini ‘tapawa
Numa numa ‘siketile, John Komba wagotewa
Mwandani wako ningile, nataraji kupokewa
Sambe nikusahawile, ukanipakaza towa
Kama idhini ‘tapawa
Sambe nikusahawile, J. Mayoka pumuwa
Hilino halilekele, la nami kusahawiwa
U mwenzangu mwenginele, upokee ujiliwa
Kama idhini ‘tapawa
U mwenzangu mwenginele, siwi mbwa kukuk’utuwa
Salim Ali yuyule, “Kibao” wafahamiwa
Ni mlangoni nikele, nangoja kufunguliwa
Kama idhini ‘tapawa
Ni mlangoni nikele, watunzi nawamkuwa
Wa Ngurumo musikile, salamu nyote mwapawa
Na ambako nitoshile, ‘tanena mupate juwa
Kama idhini ‘tapawa
Na ambako nitoshile, ni Mvita mwakwelewa
La zaidi sitashile, kwongeza mengi yakawa
Nikomilepo komele, nangoja kuchapishiwa
Kama idhini ‘tapawa
Nikomilepo komele, sendi nyengine hatuwa
Na ambalo lisalile, ni kwombeyana afuwa
Tupate liteza lele, mitima kufurahiwa
Kama idhini ‘tapawa
Abdilatif Abdalla
Dar es Salaam
Aprili 7, 1973
______________
Hili lilikuwa ni shairi langu la pili kulitunga Tanzania, tangu nilipohamia Dar es Salaam kutoka Mombasa, Kenya, mwezi wa Agosti 1972; na ambako nilifanya kazi Chuo cha Uchunguzi wa Kiswahili (baadaye Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mpaka mwaka 1979. Madhumuni yake yalikuwa ni kuwaomba idhini washairi wa Tanzania wanikubali mimi mgeni kuwa matengoni mwao. Maombi yangu yalikubaliwa, na nikakaribishwa kwa mashairi na washairi kadha wa kadha. Lilichapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Ngurumo la tarehe 12 Aprili, 1973, na gazeti la Uhuru la tarehe 19 Mei, 1973.
Fasihi simulizi ni utanzu mmojawapo wa fasihi ambao huwasilishwa kwa njia ya mdomo na hurithishwa toka kizazi kimoja hadi kingine. Tanzu za fasihi hii ni pamoja na ushairi, semi, sanaa za maonesho na hadithi. mambo yanayoifanya fasihi simulizi iwe hai ni kama ifuatavyo:
Kuwepo kwa hali ya utendaji ambapo hushirikisha hadhira na fanani.
Kubadilika kulingana na wakati na mazingira.
Kuwepo kwa mtendaji ambaye ndiye mtendaji mkuu wa fasihi simulizi. huyu ndiye anayerithisha kazi za fasihi simulizi toka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.
Kuwepo kwa hadhira tendi .
Kuwepo kwa utegemezi katika fasihi simulizi huifanya iwe hai.
Huzaliwa, hukua na mwisho hufa kulingana na maendeleo ya jamii.
Fasihi simulizi huweza kutumiwa kama burudani kwenye mkusanyiko wa jamii. Tanzu kama hadithi, ushairi, semi (methali, vitendawili, nk.) aghalabu hutumiwa ili kuwaburudisha waliokusanyika katika jamii. Kwa mfano, watoto
wanapokusanyika kucheza, aghalabu hutegeana vitendawili kama njia ya kujiburudisha. Hadithi, ngano, hekaya au hata hurafa huweza pia kutambwa kama njia ya burudani.
(ii) Kuelimisha
Kwa kutumia fasihi simulizi, wanajamii wanaweza kuzielimisha thamani za kijamii, historia yao, utamaduni na mtazamo wao kilimwengu kutoka kizazi kimoja hadi chengine.
(iii) Kuipa Jamii Muelekeo
Kwa njia ya kuelimishana kimawazo yanayohusiana na tamaduni na desturi za jamii husika, wanajamii wanahakikisha kwamba jamii, kwa kutumia fasihi simulizi, inapata muelekeo utakaowabainisha wao mbali na wengine.
(iv) Kuhifadhi Historia na Utamaduni
Katika kuhifadhi amali muhimu za kijamii, fasihi simulizi inakuwa nyezo muhimu. Aidha, wanajamii hufahamishwa kifasihi simulizi historia yao – wao ni nani na wanachimbukia wapi. Maarifa haya ni muhimu kwa kila mwanajamii, kwani yanamsaidia sio tu kujielewa, bali pia kujitambua.
(v) Kuunganisha Vizazi vya Jamii
Fasihi simulizi ni msingi mkubwa wa kuwaunganisha wanajamii waliopo na waliotangulia mbele ya haki. Kwa kutambiwa hadithi, vitendawili, methali na nyimbo zao, umbali wa kiwakati kati ya vizazi vilivyotangulia mbele ya haki, vilivyopo na vijavyo unafupishwa kwa kiasi kikubwa sana.
(vi) Kufundisha
Jamii ina jukumu la kuwafundisha vijana wake maadili ya jamii ile ambayo yana adili yaani funzo au ujumbe unaowaelekeza, kuwaadibu, kuwaonya na kuwaongoza kwenye matarajio ya jamii ile. Kwa hiyo, jamii nyingi hutumia fasihi simulizi kama njia ya kuwaelekeza na kuwafundisha vijana wake mwenendo mzuri, maadili na falsafa ifaayo ili kutunza jina na heshima ya jamii ile. Kwa mfano, katika vita dhidi ya Nduli Iddi Amini 1978/1979 nyimbo za kwaya, nyimbo za muziki wa dansi, tenzi, mashairi n.k. zilitumika kuongeza hamasa kwa askari wetu waliokuwa mstari wa mbele vitani kuwaongezea ari ya kumwadhibu adui yetu. Kitendo cha kushindwa kwa Iddi Amini katika vita vile tunaweza kusema kwamba kazi hizo za fasihi simulizi zimefaulu katika dhima yake ya kuelimisha ili
kuongeza hamasa kwa askari wetu. Umuhimu wa fasihi unaonekana katika kufaulu kutatua matatizo yetu katika jamii.
(vii) Kuukuza Ushirikiano
Ilivyo ni kwamba fasihi simulizi ni mali ya jamii wala sio ya mtu binafsi. Hadithi inaposimuliwa kwa hadhira kubwa, vitendawili vinapotegewa kundi pana, ni kwa sababu kimsingi fasihi simulizi ndivyo ilivyokusudiwa itumike katika muktadha wa kuvihusisha sio vikundi vidogo vidogo tu, bali pia, na hasa jamii nzima.kwa jumla.
(viii) Kuzikuza na Kuziendeleza Stadi za Lugha
Kwa kuwa fasihi simulizi hutegemea usemi na matamko, hatuwezi kushiriki katika kusimulia hadithi, kutegeana vitendawili, kuimba, nk. bila ya kuongea au kutamka au kuimba. Kwa sababu hii, fasihi simulizi ina mchango mkubwa wa kuboresha uwezo wetu wa kuzimiliki na kuzimudu stadi za lugha. Kwa mfano, tanzu za vitanza ulimi zilisaidia kuhakikisha kwamba utamkaji ni mzuri; utegeanaji wa vitendawili na majibu yake sahihi huukuza uwezo wa kuwaza haraka haraka na kwa usahihi. Hadithi huukuza ule uwezo wa kukumbuka maudhui.
PROF SAID AHMED MOHAMED: AMECHANGIA KWA TANZU ZOTE ZA FASIHI YA KISWAHILI; SI RIWAYA, SI TAMTHILIYA, SI HADITHI FUPI, SI USHAIRI
Msomi wa Kiswahili na mwandishi maarufu wa riwaya, tamthilia, mashairi, kazi za watoto na vitabu vya kiada Profesa Said Ahmed Mohamed Khamis
Kwa Mukhtasari
KUISHI kuna nafuu na gharama juu yake. Ingawa kila jambo maishani hustahili kugharimiwa, gharama kubwa zaidi ni ile ya amani.
Kuandika kazi yoyote ya fasihi kunahitaji wakati, utulivu na wito wa ndani ya nafsi. Huwezi kujilazimisha kutunga. Kila kazi ya fasihi katika utanzu wake ni kama mtoto uliyemzaa.
Haiwezekani mtoto mmoja awe sawa na mwingine wa tumbo moja. Huu siku zote utasalia kuwa ukweli katika uandishi wa kubuni.
Ingawa kila mwandishi ana msimamo na falsafa yake, mimi siwezi hata kidogo kuwafanya wahusika katika kazi zangu wakate tamaa. Bila ya tamaa binadamu hawezi kujikomboa.
Kukaa nje ya Zanzibar na Tanzania kumenipa uzoefu ambao umechangia pakubwa ubunifu wa mandhari, maudhui na fani katika kazi zangu.
Itakulazimu kupenda lugha, kusikiliza sana na kusoma kwingi ili uwe mwandishi bora wa Fasihi.
Ingawa si kosa kwa mtunzi kuiga baadhi ya mawazo kutoka kwa watangulizi wake, mwandishi lazima awe mweledi na mwepesi wa kutumia misemo ya kuvutia na kushangaza.
Huu ndio ushauri wa Profesa Said Ahmed Mohamed Khamis – msomi wa Kiswahili na mwandishi maarufu wa riwaya, tamthilia, mashairi, kazi za watoto na vitabu vya kiada.
MAISHA YA AWALI
Alizaliwa Pemba, Zanzibar mnamo Desemba 12, 1947. Hakubahatika kupata malezi ya baba na mama ipasavyo kwani wazazi wake walitengana akiwa na umri mdogo sana.
Alilelewa na mama zake “wakubwa”, Bi Jokha na Bi Rukia. Alisomea Wete Boys, Pemba kabla ya kuhamia Kiembe Samaki kisha Darajani, Unguja alikohitimu elimu ya shule ya msingi.
Baadaye alijiunga na shule ya upili ya Gulioni (awali ikiitwa King George The VI). Baada ya kuhitimu masomo ya sekondari, alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Nkurumah, Zanzibar mnamo 1966.
Hakujiunga na Kidato cha Tano na Sita kwa sababu wakati huo aliyekuwa kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi nchini Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume alipiga marufuku masomo ya kiwango hicho.
USOMI NA UTAALAMU
Baada ya kuhitimu Ualimu mnamo 1966, alifundisha katika shule ya msingi ya Kizimbani kwa wiki mbili tu, halafu akahitajika kwenda kufundisha Biolojia, Hisabati, Kemia na Kiswahili katika shule ya upili ya Utaani hadi 1974.
Alibahatika kujiunga na shule ya International Correspondence alikosomea masomo ya Sanaa katika kiwango cha Kidato cha Tano na Sita.
Mnamo 1976, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kusomea Shahada ya Kwanza katika Elimu. Alijikita katika Isimu na Fasihi ya Kiswahili.
Baada ya kufuzu, alirejea Zanzibar na kuwa Mwalimu Mkuu katika shule za msingi na upili za Hamamni kwa miaka mitatu.
Baadaye alirejea Chuo Kikuu cha Dar es salaam kusomea shahada ya Uzamili katika Isimu Tekelezi.
Upekee wa umilisi wake wa Kiswahili ulimvutia mwalimu Siegmund Brauner, Mjerumani aliyemfundisha kozi za Isimu Linganishi na Isimu Historia. Said alipata fursa ya kuelekea Ujerumani kusomea shahada ya Uzamifu (PhD).
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Karl Marx Leipzig, Ujerumani mwishoni mwa 1981 na kukamilisha masomo yake mnamo 1985.
Miezi michache baadaye, aliteuliwa na Rais wa Zanzibar wakati huo, Mzee Idris Abdul Wakil kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI) ambayo baadaye iliitwa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA).
Alielekea Kenya mnamo 1987 na kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Idara ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret na baadaye kufundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi hadi 1990.
Kisha alitua Japan kufundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Osaka akiwa Mkuu wa Idara ya Lugha za Kigeni. Alipata Uprofesa na kuhamia Chuo Kikuu cha Bayreuth, Ujerumani alikofundisha Kiswahili kati ya 1997 na 2012.
UANDISHI
Alipenda kusoma, kutunga mashairi na hadithi fupi tangu alipokuwa mwanafunzi wa darasa la tano. Alitunga mashairi ambayo mengi yalitumiwa na walimu kufundishia madarasa ya juu.
‘Nimfuge Ndege Gani Ili Nipate Salama’ ni shairi lake la kwanza alilolitunga mnamo 1960.
Mengi ya mashairi yake yalighaniwa katika Radio Zanzibar. Alipata motisha zaidi kutoka kwa walimu wake, Mohamed Abdallah na Kindi Abubakary waliomhamasisha pakubwa.
Anakiri kurithi kipawa cha usanii kutoka kwa mama yake “mkubwa” aliyekuwa nyakanga. Mama huyu alikuwa bingwa wa kuimba nyimbo za unyago.
Pia alikuwa mtunzi mzuri wa mashairi na alipenda sana hadithi za jadi za fasihi simulizi. Zaidi ya kurithi kipaji kutoka kwa mama yake, uandishi wa Said ulitokana na mafunzo ya elimu ya dini ya Kiislamu aliyopata katika madrassa.
Aliwahi kushiriki mashindano ya Uandishi wa Hadithi Fupi za Kiswahili yaliyodhaminiwa na Shirika la Habari la BBC katika miaka ya 90.
Nyingi za hadithi zake pia zilisomwa katika kituo cha Deutsche Welle (DW), Ujerumani. Hali hii ilimhimiza kuandaa diwani Sadiki Ukipenda na Hadithi Nyingine, kitabu kilichochapishwa na Jomo Kenyatta Foundation (JKF) mnamo 2002.
Said alidhihirisha uwezo alio nao katika kutunga visa bunilizi vilivyoelezea maisha halisi ya kila siku katika jamii.
Upekee wa kisanaa katika riwaya za Mohamed Suleiman Mohamed, Kiu (1972) na Nyota ya Rehema (1976) ulimpa Said hamu na shauku ya kuandika riwaya yake ya mwanzo, Asali Chungu (1977). Baadaye alitunga Utengano na Dunia Mti Mkavu vitabu vilivyochapishwa mnamo 1980.
Kazi hizo zilimzidishia umaarufu na kumfungulia milango ya kupokezwa tuzo za haiba kubwa ndani na nje ya Afrika.
Akiwa mshairi mahiri, Said ametunga diwani mbalimbali zikiwa ni pamoja na Sikate Tamaa (1980), Kina cha Maisha (1984) na Jicho la Ndani (2002), kazi zinazozamia masuala ya kisiasa, kiuchumi, mapenzi na utamaduni.
Ujuzi wa fani katika utunzi wa fasihi ni sifa iliyomfanya kufaulu kutumia mtindo wa uhalisia mazingaombwe katika Kivuli Kinaishi (1990), Amezidi (1995), Babu Alipofufuka (2001) na Sadiki Ukipenda (2002).
Ametumia kwingi mbinu za bunilizi, utomeleaji na taswira katika tamthilia za Pungwa (1988), Kitumbua Kimeingia Mchanga (2004) na Posa za Bi Kisiwa (2007) aliyoiandika kwa kumshirikisha Profesa Kitula King’ei wa Chuo Kikuu cha Kenyatta.
Nyuso za Mwanamke (2010) ni riwaya aliyoitunga Said miaka 36 baada ya kuchapishwa kwa Utengano (1980). Anajivunia pia riwaya Kiza Katika Nuru (1988), Tata za Asumini (1990), Dunia Yao (2006), Mhanga Nafsi Yangu (2012) na Mkamadume (2013).
Ameandika zaidi ya vitabu 60, cha karibuni zaidi kikiwa Mashetani Wamerudi,tamthilia iliyozinduliwa rasmi Oktoba 10, 2016 katika Tuzo za Kumi – Kumi za WASTA.
Gharama ya Amani (2014) ni kitabu chake cha hadithi kinachosisitiza umuhimu wa utu, uadilifu na utaifa miongoni mwa wanajamii.
Akiwa miongoni mwa waandishi wa riwaya za kimapinduzi na kifalsafa, baadhi ya kazi zake zimetafsiriwa kwa lugha za kigeni.
Ametajwa kuwa mwandishi mashuhuri zaidi Afrika Mashariki kutokana na ukamilifu wake katika kuandika riwaya, tamthilia, mashairi, hadithi fupi, kazi za watoto na hata vitabu vya kiada vya kufundishia shule za msingi, upili na vyuo.
Ameandika zaidi ya vitabu 60, cha karibuni zaidi kikiwa Mashetani Wamerudi, tamthilia iliyozinduliwa rasmi Oktoba 10, 2016 katika Tuzo za Kumi – Kumi ambazo hutolewa kila mwaka na mwasisi wa WASTA Kituo cha Kiswahili Mufti, Guru Ustadh Wallah Bin Wallah.
FAMILIA
Said ana mke mmoja, Rahma na watoto wawili. Msichana Najima, jina lenye maana ya nyota.
Jina la mvulana ni Mahir, neno la Kiarabu linalomaanisha mwenye ujuzi. Wote hawa wamemaliza kusomea Shahada ya Kwanza.