SHAIRI: MABONDENI WAHAME - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: MABONDENI WAHAME (/showthread.php?tid=1290) |
SHAIRI: MABONDENI WAHAME - MwlMaeda - 10-01-2021 TANGAZO GAZETINI ULAMAA HEMED Shikeni hili gazeti, kuna tangazo msome, Kurasa za katikati, wa mabondeni wahame. MFAUME HAMISI Sababu hasa ni nini, tuache makazi yetu, Tueleze tubaini, au eneo la mtu? ULAMAA HEMED Imesema serikali, watu wahamie juu, Mvua itakuwa kali, masika ya mwaka huu. MFAUME HAMISI Kauli hiyo si kweli, serikali imezusha, Wataka eneo hili, lengo ni kutuondosha. ULAMAA HEMED Hebu acheni ubishi, fateni mnoambiwa, Mkiona ni uzushi, kwa nguvu mtatolewa. MFAUME HAMISI Mvua tangu azali, mbona huwa inanyesha?, Na tena zilizo kali, wala sio rasharasha. ULAMAA HEMED Wataalamu wasema, kumechafuka angani, Hivyo hameni mapema, kabla ya tafarani. MFAUME HAMISI Hiyo ni danganya toto, hapa haondoki mtu, Nayatufike mazito, ila hatung’oki katu. ULAMAA HEMED Juwa ni hasara kwenu, mafuriko yakifika, Zapotea mali zenu, kupata mlisumbuka. MFAUME HAMISI Hayo uloelimisha, yaweza kuwa huwenda, Ili wakituondosha, ni wapi tutapokwenda? ULAMAA HEMED Hilo wala usijali, kujuwa wapi muende, Kumbuka wale awali, walikwenda Mabwepande. MFAUME HAMISI Najua sio mjini, watatupeleka shamba, Ila twataka baini, watatujengea nyumba? ULAMAA HEMED Kujengewa sitaraji, ila viwanja mwapewa, Pia huduma za maji, na umeme mwawekewa. MFAUME HAMISI Hapo bila ya kupinga, naiona ahueni, Pili nimepata mwanga, hakufai mabondeni. ULAMAA HEMED Kwa kuwa umeelewa, athari utaepuka, Nishamaliza kahawa, kwa herini naondoka. MFAUME HAMISI Asante ndugu yangu, sina cha kusubiria, Naacha ubishi wangu, bondeni napakimbia. Watunzi: 1: Mfaume Hamisi (Mshairi Machinga) 0716541703 2: Ulamaa Hemed (Fundi wa tungo) 0717 501557 |