Posted by: MwlMaeda - 09-27-2021, 10:07 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
SIFA KAMA ZAKO
Ayi! Nanena dhahiri, leo kila mtu yuko,
Ili utambuwe siri, usipate tatiziko,
Na uwache kufikiri, ukalipata sumbuko,
Bado ninamsubiri, mwenye sifa kama zako.
Wala sifanyi kikiri, nipate badala yako,
Mwenye akili titiri, kama zilivyo za kwako,
Mtu mwenye umahiri, asiye na hangaiko,
Bado ninamsubiri, mwenye sifa kama zako.
Namngojea mzuri, mithili ya huo wako,
Ambaye asiye ghuri, jeuri na mcharuko,
Aliyekosa kiburi, choyo hila na vituko,
Bado ninamsubiri, mwenye sifa kama zako.
Tambua mie amiri, niliyeketi kitako,
Usiku alfajiri, naomba dua mwenzako,
Anipatie Qahari, kwenye kila kitu chako,
Bado ninamsubiri, mwenye sifa kama zako.
Hapano langu shairi, limefika tamatiko,
Usiumie sadiri, nakupata sikitiko,
Nitasubiri kadiri, ndio mana hivi niko,
Bado ninamsubiri, mwenye sifa kama zako.
Mshairi Machinga,
mfaumehamisi@gmail.com,
+255716541703/752795964,
Dar es salaam, Kkoo.
Posted by: MwlMaeda - 09-27-2021, 07:59 AM - Forum: Je, wajua ?
- No Replies
ACHA KUPENDA VYA BURE !!!!
(Pamoja na urefu wake nakusihi ujipe muda kusoma mpaka mwisho)
Makala aliyoandika Paul Mashauri siku chache kabla ya kifo cha Ally Mufuruki. (Mufuruki the legend).
Miaka 10 iliyopita nilimfuata Mr. Ally Mufuruki, Mwenyekiti, CEO, Round Table ofisini kwake. Nikamwambia Mr. Ally unajua tunavyojaribu kusaidia watanzania wenzetu wapate maarifa kupitia “East Africa Speakers Bureau”. Nakuomba sana uje uzungumze katika kongamano tunaloandaa kwa wafanyabiashara. Akaniambia Paul hakuna tatizo juu ya hilo, lakini ada yangu “speaker fee” ni Tsh. milioni 2. Sikumuelewa kabisa Mr. Mufuruki hasa ukizingatia ukweli kwamba anapenda maendeleo ya watanzania wenzake na angeweza kuongea bure.
Lakini haikunichukua muda kumuelewa Mr. Mufuruki. SIku moja mimi mwenyewe binafsi nikaandaa semina ya bure. Gharama zote nilibeba mwenyewe lakini walifika watu 5 tu. Nilistaajabu ya dunia. Semina ambayo hutoza mshiriki mmoja Tsh. 350,000/= na ukumbi unajaa wamekuja watu 5 tu angali semina hiyo hiyo ni bure. Nikagundua watu hawathamini kitu wanachopata bure. Ndiyo maana Mr. Mufuruki alikataa kuongea bure. Sio kwa sababu ya pesa, ni kwa sababu hana muda wa kupoteza. Vitu vya bure vingempotezea muda wake. Nikajifunza kitu kipya kwenye maisha yangu. Ukitaka jambo lako lithaminiwe acha watu walipe gharama.
Somo nililolipata kwa Mr. Mufuruki likawa sehemu ya maisha yangu. Miaka kadhaa ikapita nikafuatwa na binti mmoja na kaka mmoja. Walikuwa ni watu maarufu sana katika nchi hii. Wenye ushawishi mkubwa kwa vijana “celebrities”. Wote walikuwa na mawazo ya biashara na walitaka niwe “mentor” wao. Nikawaambia sawa. Lakini kabla sijaanza “mentorship” program hii, naomba kila mmoja wenu aandike hilo wazo katika “business plan” na atengeneze mfano au “demo” itokanayo na hilo wazo, kisha atafute angalau wateja 2 ndio tuanze “mentorship”. Waliondoka moja kwa moja hawakurudi tena.
Sikuwaambia wale vijana wafanye yote hayo kwa sababu nilikuwa siwezi kuwatengenezea “business plan” au kuwatafutia wateja. Saa 12 tu kwangu zingetosha kuwapa “business plan” yenye mashiko na ningepiga simu chache tu kwenye “network” yangu kuwaunganisha na wateja. Niliwaambia wafanye yale yote ili walipe gharama. Ili waone thamani ya “mentorship” program wanayoitaka. Ili watilie maanani kile wanachotaka kujifuna kutoka kwangu. Kama Mr. Mufuruki alivyotaka mimi na wale niliokuwa nawaandalia kongamano waone thamani ya muda wake na maarifa aliyonayo na mimi nilitaka hawa vijana waone thamani ya muda wangu na kile wanachohitaji ili kuishi ndoto zao.
Kupenda vitu vya bure, kupenda mteremko ni chanzo cha umasikini. Kwa sababu vitu vya bure vinakuja kirahisi. Hautumii nguvu, hautumii akili wala hautokwi jasho. Ukiangalia duniani jamii ambazo zimefanikiwa sana kiuchumi ni jamii ambazo ili uishi, ili upate chakula, ili upate mahala pa kulala ni lazima utumie nguvu zako, akili zako, maarifa yako. Hakuna vitu vya bure. Hakuna mteremko. Kwa kifupi ni lazima ulipe gharama. Ndiyo maana mataifa kama Uingereza na Marekani, huwezi kuishi kama huna kazi inayoeleweka. Wakati mwingine lazima ufanye kazi zaidi ya moja. Ndiyo maana nchi kama Japan, haina rasilimali nyingi lakini ni moja kati ya mataifa yenye uchumi wenye nguvu. Ni kwa sababu kuna changamoto nyingi sana kiasi kwamba kama huna ubunifu huwezi kuishi. Ndiyo maana watu kutoka nchi kama India na China wamesambaa dunia nzima. Ni kwa sababu huko kwao wako wengi sana kiasi kwamba ili utoke kimaisha ni lazima ufanye kitu cha tofauti.
Na kwa mtazamo huohuo ukiangalia jamii masikini sana duniani ni zile jamii ambazo watu wanapenda vitu vya bure. Wanapenda vya kupewa. Ni jamii ambazo hata kama hutaki kufanya kazi utaishi. Kwa sababu ukiumwa njaa utaenda kwa mjomba atakupa hela, utampiga mzinga shemeji yako atakupa hela, utatafuta mke kutoka familia bora utapata hela, utatafuta mume wa mtu akuweke nyumba ndogo upate hela, au utaingia barabarani kuwa ombaomba upate hela ya chakula. Ni jamii ambazo ombaomba wana akiba ya fedha “savings” kuliko wenye mishahara. Ni jamii ambazo maisha siyo magumu. Ni jamii ambazo watu wazembe wanaona ni wajibu wa wale wanaojituma na kutokwa jasho kuwapa hela za kujikimu angali wao wanakesha baa wanakunywa mbege na wanzuki. Ni maisha yasiyo na utofauti na chawa. Maisha ya kunyonyana damu.
Hakuna ubaya kwenye kusaidiana katika maisha. Wala hakuna ufahari kwenye kufanikiwa kwa kutokwa jasho. Lakini ukweli ni kwamba kula kwa jasho ni amri iliyotoka kwa Mungu mwenyewe. Kula kwa kutumia kazi za mikono mikono yako ni amri iliyotoka kwa Mungu mwenyewe. Asiyefanya kazi na asile ni amri iliyotoka kwa Mungu. Hatukatai! Unaweza ukapewa kitu cha bure lakini usifanye kuwa ni sehemu ya utamaduni wako. Kwa sababu akili yako ikifika hatua ikaona kupata vya bure ni haki yako, utachukia watu pasipo sababu za msingi na utaona ni bore ufe kuliko kuishi. Kumbe uwezo wa kupila gharama na kutoka kimaisha uko ndani yako.
Unapokataa kumpa mtu kitu cha bure haumnyanyasi unamsaidia. Hata mtoto mdogo ana umri wa kutafutiwa chakula na kulishwa. Lakini ukitaka umtafutie mtoto wako chakula na kumrisha maisha yake yote hata akishaota ndevu haumsaidii unamharibu. Hivyo ndivyo nilivyowafanyia wale vijana wawili waliokuja kwangu wanataka “mentorship”. Ningewatengenezea “business plan” na kuwatafutia “wateja” ningekuwa siwasaidii ningewaharibu. Kwa sababu “business plan” na “wateja” ni sehemu ndogo sana ya kufanya baishara. Kuna kuishi na wafanyakazi, kuna kuishi na mabenki, kuna kupambana na changamoto za kuibiwa nk. Zaidi ya hapo, mimi ni binadamu, nina matatizo yangu na ninafamilia inaniangalia. Siwezi kuwa sehemu ya maisha ya wale vijana milele hata kama nina roho nzuri kiasi gani. Lazima waonyeshe kiu na njaa ya kutaka kuishi ndoto yao kabla sijaingiza maarifa na muda wangu katika maisha yao.
Sio mimi tu na Mr. Mfuruki tulio na mtazamo huu. Nakumbuka pia siku moja nilikuwa na rafiki yangu, Partner wa KPMG. Akaniambia wanapotafuta wafanyakazi, moja kati ya vigezo ni kuona “attitude” zao. Hata kama huyu mtu ana akili kiasi gani kama “attitude” yake si nzuri wanaweza wakamuacha. Akasema wakati mwingine unaweza ukamuita mtu kwa ajili ya “interview” lakini unamuacha akae kwanza “reception” muda wa “appointment” yake upite tena sana ili uone uvumilivu wake. Sio kwamba unamtesa au unakuwa “unprofessional”. Hapana, ni sehemu ya “interview”. Kama mtu hawezi kuvumilia masaa 3 mbele ya muda aliopewa wa “interview” ataweza kuvumilia “etra hours” akiwa kazini?
Rafiki yangu wa KPMG akawa ameniongezea kitu ambacho Mr. Mfuruki alinifundisha. Kwamba ukipata kitu kwa mteremko huwezi kukithamini. Hata mtu anayepata kazi kwa mteremko hawezi kithamini ile kazi. Ingekuwa ukimaliza tu chuo unapigiwa simu njoo uanze kazi kwa mshahara wa milioni 30 inawezekana wengi wetu wasingethamini kazi zao. Lakini ule mchakato wa kutembea na bahasha ya kaki, kuomba “interview” na kukosa, kuitwa kwenye “interview”, kufanya “interview” ya kwanza na ya pili na ya tatu inakufanya uiheshimu kazi. Kwa sababu kufuatilia kazi miezi sita ni kulipa gharama. Ni sawa na kumlipa Mr. Mfuruki shilingi milioni 2 aje kuzungumza kwenye kongamano lako. Yale atakayofundisha utayatilia maanani. Kwa sababu umelipa gharama.
Mambo ya msingi kwenye maisha utakutana nayo kila mahali. Kulipa gharama ili utoke maishani ni jambo la msingi ukubali au ukatae. Hata wewe usikubali kutoa ulichonacho bure hata kama ni mawazo. Hata kama hauhitaji chochote weka gharama fulani anayehitaji ulichonacho alipe. Akikipata kwa jasho atakiheshimu. Nililiona hilo kwa Mfuruki, kwa rafiki yangu Partner wa KPMG na nikaja nikaliona tena kwa Dr. Reginald Mengi. Siku moja nikiwa ofisini kwake akaanza kulalamika. Akasema “hebu anagalia hawa vijana wa siku hizi walivyo wa ajabu. Kuna kijana hapo “reception” baba yake amemtuma kwangu nimpe kazi. Mimi nina vikao. Amekaa hapo masaa 2 ameshampigia simu baba yake kwamba mimi nimemueweka tu hapo reception masaa 2. Huyu ameshashindwa “interview”. “He is a baba’s boy”.
Kama ilivyokuwa kwa Mr. Mfuruki Dr. Reginald Mengi alitaka kuuthaminisha mchakato wa yule kijana kupata kazi. Sio kwa sababu baba wa yule kijana anafahamiana na Dr. Mengi basi kazi ipatikane kirahisi. Huo sio utamaduni wa mafanikio. Watu waliopitia michakato ya kufanikiwa kama Mr. Mfuruki na Dr. Mengi wanata
mbua hilo. Ndivyo nchi zilizoendelea zilipotokea. Wanatambua umuhimu wa kulipa gharama. Wanakimbia utamaduni wa kutaka vya bure. Wanaheshimu amri ya kula kwa jasho, kula kwa kazi za mikono yako na asiyefanya kazi na asile.
Nimeandika makala hii kwa sababu hii sio elimu ambayo utafundishwa darasani. Hata mimi sikufundishwa na Professor wangu wa uchumi. Nimefundishwa mtaani. Somo lilipoiingia vizuri na mimi nikaanza mchakato wa kufundisha wengine. Ndio maana hata mimi huwezi kunipata kirahisi. Huwezi kuandika tu msg. facebook naomba kukuona nikasema njoo kesho. Sio Mashauri huyu. Sio kwa sababu sina muda. Muda unatengenezwa na unapatikanika. Kama napata muda wa kuandika kwanini nikose muda wa kuonana na wewe? Lakini nataka nijirizishe kwamba uko tayari kulipa gharama. Nataka nijue kama kweli una njaa na hicho unachokitaka, una kiu ya kukifanikisha au unataka kunipotezea muda wangu.
Hata wale ninaofanya nao kazi au niliowahi kufanya nao kazi watakuambia. Wanalipa gharama. Ndio maana wapo vijana wengi leo hii wamesimama wao kama wao wakiwa na biashara zao lakini watakuambia nilijifunza nilipofanya kazi kwa Mashauri. Wengine ni wakuu wa wilaya na wengine ni mawaziri. Ni kwa sababu sikuwaacha wasubiri kulishwa kama watoto wadogo angali wameshaota meno. Nilihakikisha hawapati mteremko walipokuwa na mimi, nilihakikisha wanatoka jasho, wanapanda milima na mabonde. Nilikuwa nawafundisha kujitegemea. Hilo ndio somo ambalo wengi hawalitaki, lakini hilo ndio somo pekee mbalo linaweza likakuvusha kutoka hapo ulipo kuelekea kule unapotaka kufika.
kama umeweza kusoma makala hii ndefu namna hii na kuimaliza ina maana wewe hupendi mteremko na nataka nikutie moyo ya kwamba utafika mbali kwenye maisha yako. Wengi wakiona makala ndefu kama hii hawasomi. wanaandika chini kwenye-comments “gazeti”. Ni kwa sababu wanapenda mteremko. Wanapenda kusoma vile vitabu vya “How to Get Rich Quicker”. Wanapenda kusoma “tweets” yenye sentensi mbili. Bahati mbaya sana maisha siyo “twitter”, maisha hayana shortcut.
Ndio maana matangazo ya “tender” za biashara na kazi hayako “twitter” yako kwenye magazeti. Kwa sababu ili usome gazeti kama hii makala ni lazima uwe na njaa, uwe na kiu ya kufikia malengo yako. Ndio maana “page” kama zangu haziwezi kuwa na “followers” wengi kwenye “social media” ukilinganisha na “comedy”. Kwa sababu masomo yangu hayana mteremko. Lazima ufikiri ndio uelewe. Unaweza ukasoma “post” yangu usiku ukaitafakari usiku kutwa usielewe ukaelewa subuhi. Yes! Umelipa gharama.
Mungu akubariki sana na sambaza makala hii iwe baraka kwa mwenzako. Lakini ili imsaidie lazima alipe gharama. Lazima aende kinyume na utamaduni wa kutaka kusoma vitu vifupi vifupi. Aanze utamaduni mpya wa kulipa gharama kwa kusoma vitu virefu. Na mtihani wa kwanza na hii makala kama gazeti la Daily News-Paul R.K Mashauri
IMEMNAMBA DUNIA
21-09-2021
Kajitanua kifua, akatembea kwa ndaro
Mabega kuyanyanyua, asijitiye kasoro
Fahamu akajitoa, kwa watu kufanya kero
Azolewa kwa pauro, imemnamba dunia.
Imemnamba Dunia, muache agaregare
Mambo yamemfikia, acha roho yampare
Yale aliyoringia, sasa acha yamkere
Sasa aliwa ni chore, imemnamba dunia.
Imemnamba Dunia, kichwani sasa hanani
Mambo aliyavamia, kuyaweka kifuani
Sasa yamning'inia, hakika yu taabani
Hanani sasa hanani, imemnamba dunia.
Imemnamba Dunia, yamfundisha adabu
Wa vyele hakusikia, na hii ndio sababu
Njiani akapotea, jua likamsulubu
Sasa amekuwa bubu, imemnamba dunia.
Imemnamba Dunia, muacheni atuliye
Hakika kajichokea, kiasi ajililiye
Majuto ajijutia, acha leo aumiye
Akomeshwe akomaye, imemnamba dunia.
Kuhusu dhanna ya fasihi ya Kiswahili kuna mjadala mkali sana miongoni mwa wanazuoni tangu miaka ya 1970-1990.
Mgogoro huu ulizuka kutokana na hofu ya baadhi ya watu kuwa kuna njama za kuwameza Waswahili au kukana juu ya kuwepo kwa kabila au jamii ya waswahili.
Ilidaiwa kwamba waswahili ni watu wenye asili ya Mwambao wa Afrika Mashariki nao wana fasihi yao ambayo huelezwa kwa lugha yao ya Kiswahili.
Kuna wale walioona kuwa waswahili ni kabila au taifa mahususi (Sengo 1987:217) na hivyo wanayo fasihi yao mahususi ambayo ndio inayostahili kuitwa Fasihi ya Kiswahili na zile nyingine zinazotumia Kiswahili ziitwe Fasihi kwa Kiswahili.
Kundi lingine linaamini kuwa hakuna kabila la waswahili na hivyo kwa mantiki hiyo hakuna fasihi ya waswahili (Senkoro 1988:11) anasema; Tunasema kuwa kazi fulani ni fasihi ya Kiswahili au la kutokana na jinsi inavyotambulisha utamaduni wa waswahili, hapa neno “waswahili” halimaanishi kabila la waswahili kwani kabila la namna hiyo halipo leo.
Waswahili hapa ni wananchi wote wa Afrika Mashariki na kati kwa ujumla na si watu wa Pwani tu.
Kundi lingine linaloona kuwa fasihi ya Kiswahili ni fasihi inayoelezwa kwa lugha ya Kiswahili ni kundi la Mazigwa (1991:18) pamoja na Syambo na Mazrui (1992)
Kwa ujumla kutokana na majadiliano hayo unaweza kupata maswali ya msingi kama vile:
– Mswahili ni nani?
Mswahili kama inavyoelezwa katika HISI ZETU cha Sengo na Kiango; ni: (mzaliwa wa pwani kwa asili, msemaji wa lugha ya Kiswahili kwa ufasaha, muislamu na kwa maana za utani mswahili ni mtu asiyetimiza miadi na mjanjamjanja)
– Mswahili yukoje?
Mswahili anaweza kujipambanua zaidi kwa nje kupitia mavazi, shughuli za uzalishaji mali, mahusiano yake ya kijamii na kupitia fasihi yake kwa ujumla.
– Uswahili ni nini?
Uswahili ni mfumo mzima wa maisha ya Mswahili unaomtofautisha na watu wa jamii nyingine, kama ilivyo uchaga kwa mchaga, umasai kwa mmasai au uhaya kwa muhaya.
– Kiswahili ni nini?
Ni lugha ya waswahili na ndiyo huitumia kuelezea mila zao.
Majibu ya maswali hayo ni nguzo muhimu sana katika kuamua kama kuna fasihi ya Kiswahili au la.
FASIHI YA KISWAHILI NI IPI?
Wataalamu wa fasihi walio wengi na hasa waswahili wanaamini kuwa jamii ya waswahili ipo ingawa yawezekana kuwa waliitwa au kujiita kwa majina mbalimbali kama vile (wa-amu, wapate, wamvita, wapemba au waunguja)
Watu hawa waliunganishwa na lugha moja ya utamaduni wa aina moja na wote ni wenyeji wa Mwambao wa Afrika Mashariki na visiwa vyake na ndio wajulikanao kwa jina la waswahili.
Kuwepo kwa watu hao ni ithibati kuwa wanayo fasihi yao ambayo yapaswa kuitwa fasihi ya Kiswahili ya waswahili na mifano yake ni pamoja na Utendi wa Fumo Liyongo na nyimbo mbalimbali za shughuli za kijamii kama harusi, uvuvi, unyago, misiba, n.k
Kuenea kwa lugha ya Kiswahili sehemu nyingi za Afrika Mashariki kumeifanya lugha hiyo kuwa chombo cha fasihi ya watu wote wanaoitumia lugha hiyo hasa baada ya kuingia kwa wakoloni.
Syambo na Mazrui (1992) wanasema; Hatuna budi kuichukulia fasihi ya Kiswahili kuwa ni ile iliyoandikwa kwa Kiswahili tu bila kujali inazungumzia utamaduni wa Kiswahili au mwingineo maadam imetumia lugha ya Kiswahili na inafuata mbinu za ufasa wa lugha hiyo basi ni fasihi ya Kiswahili.
Kuenea kwa Kiswahili ndani na nje ya Afrika Mashariki na hata nje ya bara la Afrika kumezua fungu la fasihi ya kigeni katika lugha ya Kiswahili mfano; tafsiri mbalimbali kama Biblia, Mabepari wa Venisi, Bwana Muyombekere na Bibi Bugonoka; Ntulanalwo na Bulihwali (Anicet Kitereza, 1980) zimeibua aina ya fasihi ijulikanayo kama Fasihi kwa Kiswahili.
Baadhi ya wanafasihi wanaamini kuwa fasihi ya Kiswahili ni ile iliyobuniwa na mswahili tu kwa kutumia lugha ya Kiswahili bila kujali inazungumzia utamaduni wa Mswahili au la.
Wapo wengine wanaoamini kuwa fasihi ya Kiswahili ya Waswahili ni ile iliyobuniwa na mswahili kuhusu utamaduni wa Waswahili.
Kundi la tatu ni lile linalodai kuwa fasihi kwa Kiswahili ni ile iliyobuniwa na kuandikwa na mtu asiye mswahili au kwa lugha nyingine na kisha ikafasiriwa kwa lugha ya Kiswahili.
Mfamo:
– Mfalme Edipode
– Takadini
– Barua Ndefu Kama Hii
– Mabepari wa Venisi
– Orodha, n.k
AINA ZA FASIHI YA KISWAHILI KWA JINSI YA UWASILISHAJI
Fasihi ya Kiswahili hugawanywa katika aina mbili kulingana na jinsi ya uwasilishaji.
– Fasihi simulizi
– Fasihi andishi
FASIHI SIMULIZI
Ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi. Hivyo fasihi simulizi ni tukio linalofungamana na muktadha fulani wa kijamii. Fasihi simulizi hutawaliwa na mambo yafuatayo:
– Fanani
– Hadhira
– Fani inayotendwa
– Mahali/mandhari
– Wakati
– Tukio lenyewe
Kwa kawaida fasihi simulizi hutungwa kichwani kabla au wakati uleule wa kutamkwa. Hata hivyo fanani huwa na uhuru wa kubadili matini ya utungo wakati wowote ili kukidhi mahitaji ya muktadha na hadhira yake.
Tanzu za fasihi simulizi ni nyingi na hutofautiana kulingana na jamii. Pamoja na wingi wake wataalamu wameziweka katika makundi yafuatayo:
(a) Mazungumzo
Tanzu zilizomo katika kundi hili ni hotuba, malumbano ya watani, soga na mawaidha.
(b) Masimulizi (yale yote yanayosimuliwa)
Hapa huingizwa tanzu mbalimbali za hadithi kama vile ngano, hekaya, hurafa, simulizi za kihistoria na kiasili kama vile visakale, mapisi, tarihi, kumbukumbu na visasili.