Posted by: MwlMaeda - 10-09-2021, 09:44 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
MGAMBO
Nakuomba ndugu yangu, ninayonena sikiya,
Hako kamtaji kangu, uliko kashikiliya,
Jua mama na wanangu, ndiko kananitunziya,
Ni kweli wamekutuma, ela akili tumiya.
Mgambo hayo majungu, unayoyaangaliya,
Yanafanya mambo chungu, yatunza familiya,
Yanasomesha wanangu, mume aloniwachiya,
Ni kweli wamekutuma, ela akili tumiya.
Mgambo hicho kirungu, usije kukiachiya,
Kikapiga kichwa changu, maumivu kunitiya,
Tambua kuna wanangu, huko wanisubiriya,
Ni kweli wamekutuma, ela akili tumiya.
Ela likitanda wingu, kunyesha yakaribiya,
Utaponifunga pingu, hivi umefikiriya?
Wale wadogo wanangu, nani atahudumiya?
Ni kweli wamekutuma, ela akili tumiya.
Mgambo wasiya wangu, nakuomba zingatiya,
Niwache niende zangu, machinga sina hatiya,
Wanisubiri wanangu, chochote hawajatiya,
Ni kweli wamekutuma, ela akili tumiya.
Mshairi Machinga,
mfaumehamisi @gmail.com,
+255716541703/752795964,
Dar es salaam, Kkoo.
LIPO LA KUFANYA KWA AJILI YAKE (ABDULRAZAK GURNAH)
??Ni yeye Profesa Abdulrazak Gurnah. Jina kubwa kwenye ulimwengu wa Fasihi. Jina liliandikwa kwenye riwaya kumi za maisha yake. Ama kweli baada ya dhiki faraja. Mungu ametufariji kwa faraja hasa kupitia mkono wake. Itazame Dunia ilivyoimba Jina lake na letu ghafla tu limekuwa kubwa mno. Ametukuka Subuhana
??Mcheza kwao hutunzwa. Kwanini tusimtunze? Ametunyanyua waswahili. Hivi kumuenzi itakuwa dhambi?
??Hakika leo Tanzania hasa Zanzibar imekuwa midomoni mwa walimwengu. Watu wanaitaja kwa wema. Tena kwa wema uliotukuka. Ulimwengu juzi ulipofungua mdomo na kutamka." Tuzo ya Nobel ya Fasihi imekwenda kwa mzaliwa wa Zanzibar Profesa Abdulrazak Gurnah." Wengi walitaka kujua huyu ni nani?
??Kwa hakika Dunia imepata kumuelewa mtu huyu mpole,mcheshi, mjuzi wa mambo na mzalendo hasa. Kwenye hili utambuzi wake upo baina ya pua na mdomo.
Mara nyingi amelidhihirisha kupitia ulimi wake. Kalamu ilaliweka wazi tu. Mara ngapi amejinasibu kwa uzawa wake? Hii haitoshi? Msikilize alipoulizwa kuhusu tuzo hii. " Tuzo hii ni kwa ajili ya Afrika, Waaafrika na Wasomaji wangu." Allah akubariki kwa hili.
?? Binafsi amenishajihisha sana. Mimi ni mwanafasihi chipukizi. Acha niweke ndoto yake kwenye kichwa changu. Msururu wa vitabu miaka 40 baada ya uzawa wake. Vitabu kumi baada ya kile cha awali. Hakika amefanya kazi kubwa mno. Jitihada zake zimemuweka pale alipotaraji kuwa.
??Nikiri kwamba Jina lake niliwahi kulisikia kupitia kwa rafiki yangu mmoja. Ila kwa hakika hakuniambia wala kujiongeza kumtafuta kufahamu nasab yake. Ila tokea tangazo lilipotoka kwamba yeye ndio yeye. Nikasema "Hakika dutu imepata mpigaji." Kwani hili haliwafanyi Wanafasihi chipukizi kuongeza jitihada? Lipo la kujifunza kwalo.
??Nadhani ipo namna pia ya kushangiria hili.Si lake peke yake. "Mvyelewe harusi ngia uwanjani mtu lake hatendewa." Lazima tumuenzi. Na arudi kusitiri kitovu chake. Profesa karibu nyumbani tena. Mtaka nyingi nasaba hupata mingi misiba. Njoo tukuvishe joho na kukufuta machozi kwa safari tuliyokutima. Wewe ni askari uliyeipeperusha bendera yetu vyema. Umeshinda vita njoo tushangiriye. Wewe ni wetu itavyokuwa tena wetu hasa. Aliyemo yumo asiyekuwemo haingii.
"MEMORY OF DEPARTURE " ya ABDULRAZAK GURNAH.
Nimemaliza kusoma Riwaya ya Kitawasifu ya AbdulRazak Gurnah Mshindi wa Tuzo ya Nobel katika Fasihi 2021 inayoitwa "Memory of Departure".
Wakati wengine wakiendelea na mijadala yao ya ima yeye ni Mtanzania au Mwingereza,mimi nikaona nijikite kutazama yaliyompa hedaya duniani kote.Makubwa na machache niliyoyabaini ni yafuatayo katika Falsafa yake:
1.Nimeishuhudia nguvu kubwa ya Utamaduni katika kujenga aina ya kizazi tutachokitaka ama Utamaduni unavyoweza kuifuta jamii moja au hata Taifa moja na likabaki historia tu katika ndimi za watu.
2.Nimeshuhudia kuanzia mwanzo mpaka mwisho nguvu kubwa ya mama.Kwa namna mama anavyoweza kumfinyanga mwana na akawa vile atakavyo.Mama anavyoweza kuilinda familia.Mama anavyoweza kuifariji familia.
3.Nimeshuhudia kuwa AbdulRazak kifalsafa ni Mmajumui wa Afrika na haya hana katika hilo.Wanaobishana wabishane lakini yeye anaililia Afrika.
4.Nimeishuhudia safari inayoakisi kama yakwake.Laiti angalipata "Scholarships" za Serikali ambazo zilikuwa zinatolewa kwa upendeleo kipindi hiko,katu asingaliondoka Zanzibar kama mkimbizi.Mitihani alifaulu vizuri,alikuwa na malengo ya kusoma nje kama alivyomshawishi Mwalimu wake wa Kiingereza,alifanya harakati za kupata "passport" n.k.
5.Nimeishuhudia namna uchungu nao unavyoweza kumsukuma mtu katika maendeleo.Kwasababu kwa maoni yangu ukiniuliza hasa kilichomkimbiza AbdulRazak Zanzibar nitakwambia ni matendo ya kiutamaduni,kwa maana tabia za watu binafsi wachache,hali ya maisha ya kifamilia (umasikini) kuliko hata hizo vuguvugu za kisiasa zinazotajwa kwamba labda ni hofu ya kuuawa ama vinginevyo.
6.Nimeona jitihada na athari ya kukitambulisha Kiswahili kwa maneno tele ambayo angalitaka angaliyapata tu katika lugha ya Kiingereza.Utaona humo maneno kama:
a)Voti mpeni Jongo.
b)Mbatata
c)Mzambarau.
d)Rizki.
e)Buibui.
f)Khitma.
g)Muadhin.n.k.
Kwa hakika,ninaweza kusema kuwa, kwa uandishi wake na kwa namna nilivyowahi kuwaona waandishi wengine wa Kiswahili,laiti ingalikuwa kazi zetu za Kiswahili za waandishi wetu nguli hapa Tanzania hutafsiriwa katika lugha za kimataifa kama Kiingereza, basi huenda tuzo zenyewe za Nobel zingelikuwa zinatiririkia hapa kwetu tu na hivi sasa ingelikuwa tumeshazizoea huku tukiwashuhudia wenzetu wa nchi jirani zinazotuzunguka wakizimezea mate.Wasalam!.
Misingi katika kusoma
Kusoma ni nini?
Kusoma kunaelezwa katika ngazi nne
(i) uwezo wa kutambua maandishi katika maumbo yake mbalimbali kwa kuyahusisha maumbo hayo na kitu, jambo au tendo.
(ii) Uwezo wa kuyakabili maandishi kwa kasi na wepesi bila kupoteza kiini chake.
(iii) Uwezo wa kuelewa maana iliyomo bila vipingamizi.
(iv) Uwezo wa kuyahusisha maandishi na uzoefu wake wa kila siku.
(v) Uwezo wa kuzingatia na kuyatumia yale yote yaliyo muhimu na kuyafanya sehemu ya maisha.
kwa kifupi kusoma ni ufumbuzi wa maandishi anaofanya msomaji. Katika mawasiliano maandishi (fumbo) – kusoma ni mawasiliano na kikomo ni macho (mapokeo), utambuzi, tafsiri, maana, uzingatiaji kumbukumbu na kadhalika wa msomaji.
Posted by: John John - 10-05-2021, 07:00 PM - Forum: Ushairi
- No Replies
HONGERA MWALIMU
Nimeishika kalamu, ya moyoni kuongea,
Uyasikie mwalimu, kila kona ya dunia,
Wewe ni mtu muhimu, nani asiyelijua?
Hongera sana mwalimu, Rahmani akujalie.
Fani yako ni adhimu, werevu wanatambua,
Kuandaa watalamu, tena waliobobea,
Endeleza gurudumu, maarifa kuyatoa,
Hongera sana mwalimu, Rahmani akujalie.
Hakuna Wanasheria bila Mwalimu!
Hakuna Wahandisi bila Mwalimu!
Hakuna Wanahabari bila Mwalimu!
Hakuna Madaktari bila Mwalimu!
Hakuna Marais bila Mwalimu!
WALIMU NI MUHIMU.
Mlitufundisha!
Mlituelimisha
Mlitufurahisha!
Mlituhamasisha!
Mlituheshimisha!
WALIMU NI MUHIMU.
Mbarikiwe na Mungu Walimu!
Mlipwe na Mungu Walimu!
Muwe na maisha mema Walimu!
Tunawaombea daima mema Walimu!
Tunafurahia leo Siku ya Walimu!
WALIMU NI MUHIMU.