UMUHIMU WA FASIHI SIMULIZI KATIKA JAMII - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi kwa ujumla (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=73) +--- Thread: UMUHIMU WA FASIHI SIMULIZI KATIKA JAMII (/showthread.php?tid=1285) |
UMUHIMU WA FASIHI SIMULIZI KATIKA JAMII - MwlMaeda - 09-29-2021 (i) Kuburudisha
Fasihi simulizi huweza kutumiwa kama burudani kwenye mkusanyiko wa jamii. Tanzu kama hadithi, ushairi, semi (methali, vitendawili, nk.) aghalabu hutumiwa ili kuwaburudisha waliokusanyika katika jamii. Kwa mfano, watoto
wanapokusanyika kucheza, aghalabu hutegeana vitendawili kama njia ya kujiburudisha. Hadithi, ngano, hekaya au hata hurafa huweza pia kutambwa kama njia ya burudani. (ii) Kuelimisha
Kwa kutumia fasihi simulizi, wanajamii wanaweza kuzielimisha thamani za kijamii, historia yao, utamaduni na mtazamo wao kilimwengu kutoka kizazi kimoja hadi chengine.
(iii) Kuipa Jamii Muelekeo
Kwa njia ya kuelimishana kimawazo yanayohusiana na tamaduni na desturi za jamii husika, wanajamii wanahakikisha kwamba jamii, kwa kutumia fasihi simulizi, inapata muelekeo utakaowabainisha wao mbali na wengine.
(iv) Kuhifadhi Historia na Utamaduni
Katika kuhifadhi amali muhimu za kijamii, fasihi simulizi inakuwa nyezo muhimu. Aidha, wanajamii hufahamishwa kifasihi simulizi historia yao – wao ni nani na wanachimbukia wapi. Maarifa haya ni muhimu kwa kila mwanajamii, kwani yanamsaidia sio tu kujielewa, bali pia kujitambua.
(v) Kuunganisha Vizazi vya Jamii
Fasihi simulizi ni msingi mkubwa wa kuwaunganisha wanajamii waliopo na waliotangulia mbele ya haki. Kwa kutambiwa hadithi, vitendawili, methali na nyimbo zao, umbali wa kiwakati kati ya vizazi vilivyotangulia mbele ya haki, vilivyopo na vijavyo unafupishwa kwa kiasi kikubwa sana.
(vi) Kufundisha
Jamii ina jukumu la kuwafundisha vijana wake maadili ya jamii ile ambayo yana adili yaani funzo au ujumbe unaowaelekeza, kuwaadibu, kuwaonya na kuwaongoza kwenye matarajio ya jamii ile. Kwa hiyo, jamii nyingi hutumia fasihi simulizi kama njia ya kuwaelekeza na kuwafundisha vijana wake mwenendo mzuri, maadili na falsafa ifaayo ili kutunza jina na heshima ya jamii ile. Kwa mfano, katika vita dhidi ya Nduli Iddi Amini 1978/1979 nyimbo za kwaya, nyimbo za muziki wa dansi, tenzi, mashairi n.k. zilitumika kuongeza hamasa kwa askari wetu waliokuwa mstari wa mbele vitani kuwaongezea ari ya kumwadhibu adui yetu. Kitendo cha kushindwa kwa Iddi Amini katika vita vile tunaweza kusema kwamba kazi hizo za fasihi simulizi zimefaulu katika dhima yake ya kuelimisha ili
kuongeza hamasa kwa askari wetu. Umuhimu wa fasihi unaonekana katika kufaulu kutatua matatizo yetu katika jamii. (vii) Kuukuza Ushirikiano
Ilivyo ni kwamba fasihi simulizi ni mali ya jamii wala sio ya mtu binafsi. Hadithi inaposimuliwa kwa hadhira kubwa, vitendawili vinapotegewa kundi pana, ni kwa sababu kimsingi fasihi simulizi ndivyo ilivyokusudiwa itumike katika muktadha wa kuvihusisha sio vikundi vidogo vidogo tu, bali pia, na hasa jamii nzima.kwa jumla.
(viii) Kuzikuza na Kuziendeleza Stadi za Lugha
Kwa kuwa fasihi simulizi hutegemea usemi na matamko, hatuwezi kushiriki katika kusimulia hadithi, kutegeana vitendawili, kuimba, nk. bila ya kuongea au kutamka au kuimba. Kwa sababu hii, fasihi simulizi ina mchango mkubwa wa kuboresha uwezo wetu wa kuzimiliki na kuzimudu stadi za lugha. Kwa mfano, tanzu za vitanza ulimi zilisaidia kuhakikisha kwamba utamkaji ni mzuri; utegeanaji wa vitendawili na majibu yake sahihi huukuza uwezo wa kuwaza haraka haraka na kwa usahihi. Hadithi huukuza ule uwezo wa kukumbuka maudhui.
|