MUHADHARA WA TATU: FASIHI SIMULIZI NA UANDISHI
Tangu kutawala kwa fasihi andishi Ulaya,Asia na kutumiwa na wenye nguvu za kisiasa na kiuchumi fasihi simulizi ilidharauliwa ikatwezwa,ikadunishwa na kushushwa hadhi huku fasihi andishi ikitukuzwa na kuendelezwa.
Taaluma ya fasihi simulizi hivi leo inashughulikiwa kwa nguvu nyingi ili kuondokana na fikra duni zilizorithiwa toka kwa wataalamu wa kigeni kuwa sanaa kongwe ya fasihi simulizi ni ya kishenzi.
Pamoja na dharau juu ya fasihi simulizi bado ukweli unabaki kuwa sanaa hii ndiyo ghala halisi la fasihi andishi.
Hata sasa imebainika kuwa tenzi za Kigiriki zinazodaiwa kutungwa na manju aitwaye “Home” hazikuwa zimeandikwa kwa zaidi ya miaka miatano (500) ndipo baadaye zikaja kuhifadhiwa katika maandishi.
Hivi majuzi pia wanateknolojia wameanza kukubali kuwa sehemu kubwa ya Biblia ni fasihi simulizi ya Wayahudi walioishi zama mbalimbali. Wanazidi kueleza kuwa imebainika kuwa fasihi hiyo haikutoka mbinguni bali mizizi yake ni katika jamii ya Wasumuri (Mesopotamia),Waajemi na Wagiriki.
Hoja ya msingi ni kuwa na fasihi andishi haijaibua dhamira mpya zote ni zilezile ambazo zilijitokeza katika masimulizi.
Mfano:
Mapenzi, siasa, unyonge wa wanawake, ukombozi, uchawi na ushirikina, uzazi, ndoa na migogoro ya kitabaka.
Misemo ya fasihi simulizi haijapitwa na fasihi andishi wala fani yake haijabadilika mpaka leo.
Kimsingi fasihi simulizi na fasihi andishi kitu kimoja isipokuwa njia zinazotumiwa na fanani na hadhira katika kuwasilisha ujumbe.
(i) Fanani wa fasihi simulizi hutumia mdomo,sauti,vitendo na muziki wakati fanani wa fasihi andishi hutumia karatasi na wino.
(ii) Fasihi simulizi huweza kuwasilishwa kupitia maandishi na fasihi andishi huweza kutumia ala za fasihi simulizi kunogesha kazi yake na kufikisha ujumbe wake. Hivyo maandishi sio kigezo cha kuitenganisha kabisa fasihi simulizi na fasihi andishi.
(iii) Matumizi ya taarabu na nyimbo za kiasili kayika fasihi andishi ni uthibitisho kuwa fasihi simulizi bado inapendwa na haiwezi kufa bali kubadilika umbo tu ili kuiwezesha kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
(iv) Ukichunguza kazi mbalimbali za fasihi andishi utabaini kila mwandishi ameathiriwa na fasihi simulizi kwa namna fulani. Wapo walioathiriwa kifani na wengine kimaudhui.
Kifani
Hapa tunao watunzi kama Ibrahim Hussein (Mashetani na KInjeketile), Penina MHando (Pambo na Lina Ubani), Shaaban Robert (Adili na Nduguze), Mohamed Said Abdullah (Mzimu wa Watu wa Kale).
Waandishi wote hao wametumia wahusika wa kifasihi simulizi kama wanyama,majitu,mazimwi na mapango.
Kimaudhui
Ukichunguza kazi nyingi za fasihi andishi utagundua kuwa maudhui yake ni ya kifasihi simulizi. Vichwa vya hadithi zao ni methali fulani toka fasihi simulizi.
Mfano:
– Mwerevu hajinyoi
– Baada ya dhiki faraja
– Lila na fila havitangamani
– Mwana umleavyo ndivyo akuavyo, n.k
Tanzu za fasihi simulizi za kihadithi
Kuna makundi mawili makuu ya tanzu za fasihi simulizi.
– Kundi moja linahusika na tanzu zenye mwelekeo wa kishairi na kundi lingine ni lile linaloshughulikia tanzu za kinathari zenye sifa za kihadithi.
Tanzu za kinathari ni zile zote zinazojumuisha matumizi ya lugha ya kawaida ya maongezi na yenye mjazo.
Mfano:
Hadithi yoyote iliyotungwa kwa mpangilio wa visa na matukio katika namna inayochukuana na kuleta muwala (mtiririko).
NGANO
Ngano zinaelezwa kuwa ni hadithi za “paukwa pakawa” wakaishi raha mustarehe. Maana hii imezingatia zaidi mianzo na miisho ya ngano kutokana na tanzu nyingine za fasihi simulizi.
Mara nyingi ngano huambatana na nyimbo ambazo hutumiwa kuwasilisha ujumbe, kubadili mandhari ya wahusika au kuchapuza hadithi kinachotendeka. Vilevile nyimbo huweza kutumiwa kama kiliwazo katika kulegeza mtiririko na upeo wa matukio yanayotambwa katika ngano.
AINA ZA NGANO
Ngano hugawanywa katika aina mbalimbali kulingana na vigezo vitumikavyo.
v Kwa kigezo cha wahusika tunapata aina mbili ambazo ni Hekaya na Kharafa/Khurafa.
Hekaya – ni ngano ambazo wahusika wakuu na muhimu ni binadamu. Hekaya hutumiwa kuonesha jinsi watu wa tabaka fulani walivyo na hekima na busara kwa kiasi kikubwa. Mfano: Hekaya za Abunuwasi.
Khurafa/Kharafa- ni hadithi ambazo wahusika wake wakuu ni wanyama na wahusika wasio na uhai kama miti,mawe,majitu,n.k.
v Kwa kigezo cha matukio tunapata ngano kama vile:
– Ngano zinazohusu matukio ya kijamii, mfano Waluya na Wapangwa ni makabila yenye historia zinazoelekeana sana. Ngano yoyote toka jamii hizi huchukuliwa kuwa ni ngano za aina moja kwa sababu zinahusu matukio yanayogusa historia za jamii hizo.
Tatizo la kuzingatia kigezo hiki ni tofauti ya mtiririko kama mizani ya kutambulia ngano kwa kuwa ngano hizo zinaweza kuwa na matukio na mtiririko unaoelekeana lakini zikatofautiana katika mianzo na miisho yake.
v Kigezo kingine ni kutumia wahusika vikale, dhanna hii inahusu aina fulani ya mtiririko. Wahusika au picha kongwe inayojitokeza mara nyingi hutumika kama kigezo. Mfano: mtu kunyanyaswa na kufaulu baadaye. Hawa huitwa wahusika vikale. Kwa namna ingine wahusika vikale ni wale ambao hawategemei nguvu za miili yao katika kushinda bali hutumia akili,ujuzi na maarifa kwa kiasi kikubwa na hatimaye hushinda. Mifano ya wahusika hawa ni Sungura,Kobe,Nyoka, n.k
UAINISHAJI WA NGANO KWA MUJIBU WA VLADMIR PROPP
Propp aliainisha ngano kwa kuzingatia muundo wa ngano yenyewe akitumia Nadharia ya urasimi, nadharia hii iliasisiwa na Vladimir Propp (1928,1968) katika kitabu chake cha “The Morphology of the folktale.” Nadharia hii ilizuka ili kupinga mawazo ya wanamsambao hususani katika ugawaji wa ngano bila kuchunguza kwa umakini sifa ya kila kundi. Propp anaamini kuwa ili kuchunguza asili ya ngano ni vyema kuanza kuchunguza aina za ngano kwa kuangalia maumbo ya ngano. Hivyo mtazamo huu unaangalia asili ya ngano kwa kuchunguza maumbo ya ngano husika.
Ubora wa nadhairia hii, nadharia hii inasaidia kujua aina za ngano kutokana na dhima zake, mfano ngano za urafiki, miadi, ukatili, ugunduzi na mwisho wa urafiki, (Alan Dunde’s)
Udhaifu wa nadharia, nadharia hii inaonekana kutomzingatia mtambaji ambaye ni sehemu ya ngano yenyewe ambaye anaweza kubadilisha umbo la ngano kadri ya utendaji wake.
Nafasi ya nadharia hii katika ngano za Kiswahili, nadharia hii inatusaidia kuziweka ngano katika makundi kutokana na kazi zake. Mfano tunapata ngano zinazohusu wahusika wajanja mfano sungura na wahusika wasiowaerevu/wajinga mfano fisi.