Lugha ya Kiswahili imeanza takriban miaka 1000 iliyopita kwenye pwani ya Afrika ya Mashariki. Neno Swahili lina asili ya Kiarabu: Sahil ina maana ya pwani; sawahil ’’ a-sawāhilī’’ ni wingi wake kwa kumaanisha yote yanayohusiana na pwani, watu au utamaduni na lugha ya eneo la pwani. Kiswahili kilianza kama lugha ya miji na bandarini wakati wa biashara ya kimataifa kwenye pwani ya Afrika ya mashariki.
Tuna historia jinsi gani miji kama vile Kilwa, Lamu na mingine kadhaa iliyoanzishwa na wafanyabiashara Waarabu au Wajemi waliooa wenyeji. Idadi ya wahamiaji kutoka Uarabuni haikuwa kubwa sana, hivyo lugha ya wenyeji ilitumika kila mahali ila tu maneno mengi yameingia kutoka katika lugha ya Kiarabu. Utamaduni mpya ulijitokeza uliokuwa wa Kiafrika Kiswahili kilizaliwa kuwa lugha ya Kibantu kilichopokea maneno mengi ya asili na ya nje.
Kiswahili kiliandikwa muda mrefu kwa herufi za Kiarabu kama inavyosomeka kwenye sanamu ya askari huko Dar es Salaam, Tanzania. Maandishi Yanasema: "Huu ni ukumbusho wa askari wenyeji Waafrika waliopigana katika Vita Kuu."
Lugha iliandikwa kwa herufi za Kiarabu tangu karne ya 13 kabla ya kristo. Kwa bahati mbaya leo hatuna tena maandiko ya kale sana, kutokana na hali ya hewa kwenye pwani isiyosaidia kutunza karatasi na kurasa zenyewe zinaweza kuoza kutokana na unyevu hewani pamoja na wadudu wengi walioko katika mazingira ya pwani ya Tanzania.
Kuna Maandiko ya kale yanayopatikana kutoka karne ya 17 huonyesha ya kwamba tenzi na mashairi vinafuata muundo uliotangulia maandiko yenyewe kwa karne kadhaa. Sehemu kubwa ya maandiko ya kale ni tenzi yaani mashairi yenye aya maelfu. Tenzi ndefu kabisa inahusu kifo cha Mtume Muhamad ikiwa na aya 45,000.
Kiswahili kilipokelewa kirahisi na wenyeji kwa sababu walikosa lugha ya pamoja kati yao, lugha za Kibantu ziko karibu sana na athira ya Kiarabu ilikuwa kilekile kote pwani. Haya yote yalisaidia kujenga umoja wa Kiswahili katika eneo kubwa la pwani ya Afrika ya Mashariki. Kiajemi pia kilichangia maneno mbalimbali, kama vile "bibi" na "cherehani".
Kufika kwa Wareno huko Afrika ya Mashariki kuanzia mwaka 1500 kulileta athira mpya ikiwa maneno kadhaa ya Kireno yameingia katika Kiswahili kama vile "bendera", "gereza" na "meza".
Kuwepo kwa wafanyabiashara Wahindi katika miji mikubwa ya pwani kuliingiza pia maneno ya asili ya Kihindi katika lugha kama vile "lakhi", "gunia" n.k. Athira ya lugha za Kihindi iliongezeka kiasi baada ya Waingereza kutumia Wahindi wengi kujenga reli ya Uganda.
Kiswahili kama Lugha ya biashara.
Kiswahili kilitumika kama lugha ya biashara baina ya watu wa pwani na bara katika kanda ndefu sana kutoka Somalia hadi kasikazini mwa Msumbiji,
Wafanyabiashara Waswahili waliendeleza biashara ya misafara hadi Kongo. Kiswahili kiliendelea kuenea kwenye njia za misafara hii. Kila msafara ulihitaji mamia ya watu hadi maelfu wa kubeba mizigo ya biashara kutoka pwani hadi pale msafara ulipolenga Ziwa Tanganyikan. katika mkoa wa Kigoma.
Watu hawa wote walisambaza matumizi ya Kiswahili katika sehemu za ndani ya Tanzania.
Kiswahili wakati wa ukoloni
Karne ya 19 ilileta utawala wa kikoloni. Wakoloni walitangulia kufika katika bandari za pwani wakatumia makarani, askari na watumishi kutoka eneo la pwani wakijenga vituo vyao Pwani wakitumia lugha ya kiswahili. Watu hao walipeleka
Kiswahili pande za bara.
Wajerumani waliamua kutumia Kiswahili kama lugha ya utawala katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Hapo waliweza kutumia kazi ya wamisionari Wakristo wa awali, hasa Ludwig Krapf, waliowahi kufanya utafiti wa lugha na kutunga kamusi na sarufi za kwanza mwaka 1879 na kuchapishwa Jijini London Uingereza Mwaka 1882 pamoja na kuunda mfumo wa kuandika Kiswahili kwa herufi za Kilatini.
Utawala wa kikoloni ulirahisisha mawasiliano kati ya wenyeji kwa kuzungumza Kiswahili wakati wote wa Ujenzi wa Reli ya kati ilijengwa na wafanyakazi kutoka makabila mbalimbali wakishirikiana.
Waafrika walilazimishwa kulipa kodi kwa wakoloni, hivyo walitafuta kazi ya ajira katika mashamba makubwa yaliyolimwa mazao ya biashara na katika migodi ya madini huko Kongo ambako watu wa makabila mengi walichanganyikana wakitumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano.
Namna Lugha ya Kiswahili ilivyoenea zaidi.
Waingereza baada ya kuchukua Tanganyika kutoka kwa Wajerumani waliendela kutumia Kiswahili kama lugha ya utawala. Kuanzia mwaka 1930 waliunda kamati yenye shabaha ya kuunganisha lahaja mbalimbali na kuunda Kiswahili cha pamoja kwa ajili ya Afrika ya Mashariki (Inter-territorial Language (Swahili) committee for the East African Dependencies).
Mwenyekiti alikuwa Frederick Johnson, makatibu R. K. Watts, P. Mzaba na Seyyid Majid Khalid Barghash. Kamati hiyo iliamua kutumia lahaja ya Kiunguja kuwa msingi wa Kiswahili cha pamoja kilichoendela kufundishwa shuleni. Leo hii ndicho Kiswahili rasmi kinachofunzwa na wanafunzi na kuandikwa magazetini na vitabuni.
Miaka ya ukoloni ilisababisha kupokelewa kwa maneno mapya katika Kiswahili. Kijerumani kiliacha maneno machache kama "shule" (Kijerumani Schule) na "hela" (Heller) lakini maneno mengi sana ya asili ya Kiingereza yalipokelewa.
Kiswahili kimeonyesha uwezo mkubwa wa kupokea maneno kutoka lugha tofauti, kikitumia maneno haya kufuatana na sarufi ya Kibantu ya Kiswahili.
Mwalim Nyerere alivyochangia kukua kwa Kiswahili
HAYATI Mwalimu Julius Nyerere, ni miongoni mwa viongozi wanaokumbukwa kwa kuwa watetezi wa lugha na falsafa za Kiafrika, akiheshimika kwa juhudi kubwa za kukuza na kuendeleza Kiswahili katika jitihada za kuwaunganisha Watanzania na Waafrika pia.
Mchango wake ulianza wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Hii inajidhihirisha kwa kuangalia jinsi alivyotumia lugha ya Kiswahili kama chombo muhimu cha mawasiliano ambacho kiliwaunganisha Watanganyika kupigania na kudai uhuru.
MWALIMU Nyerere alitumia Kiswahili katika kampeni za kisiasa ambapo siasa na sera za TANU zilienezwa sehemu mbalimbali nchini kwa kutumia kiswahili. Matumizi ya lugha ya Kiswahili ni sababu mojawapo ya Tanganyika kupata Uhuru mapema na bila vikwazo vingi wale waliokuwa hawaifahamu na waliokuwa hawajui kusoma walipata nafasi ya kujifunza na kuelewa hatua za kudai uhuru zinavyokwenda na zilipofikia. Baada ya Uhuru,
Mwalimu Nyerere akiwa Waziri Mkuu wa kwanza alitangaza Kiswahili kuwa Lugha ya Taifa na kuagiza itumike katika shughuli zote rasmi za umma. Kwa kuonyesha msisitizo wa matumizi ya lugha hii, Nyerere alitoa hotuba ya kusherekea sikukuu ya Jamhuri tarehe 10, Desemba 1962, kwa Kiswahili.
Hatua hiyo ilidhihirisha na kukionyesha Kiswahili kama lugha asilia ambayo ilitumika ili kuondoa uwezekano wowote wa mafarakano yanayohusiana na mitafaruku ya kimatamshi.
Aidha, Mwalimu Nyerere alihutubia hafla nyingi kwa Kiswahili, hatua ambayo ilifanya kila mwananchi kuelewa mipango na mikakati ya serikali katika kuwaletea maendeleo yao. Kuanzia wakati huo Kiswahili kilianza kutumika katika shughuli zote za nyanja mbalimbali nchini kwa kuimarisha mahusiano ya makabila na kuifanya nchi kuwa kama kabila moja licha ya kuwa na zaidi ya makabila 120.
Hatua ya pili iliyochukuliwa na Mwalimu Nyerere ilikuwa ni kupitisha Azimio la Arusha mwaka 1967, aliposema kuwa ni mfumo wa “ujamaa na kujitegemea ndiyo sera ya taifa, hii ilikuwa ni njia muhimu ya kuwaunganisha Watanzania wote.
Matumizi ya Kiswahili yaliendelea kupanuka ambapo mnamo 1962, lugha hii ilianza kutumika rasmi bungeni na kwa upande wa elimu kilianza kutumika kufundishia masomo yote katika shule za msingi nchini huku Kiingereza kikibaki kufundishwa kama somo.
Mwalimu Nyerere alianzisha mpango wa Elimu ya Watu wazima, waliofundishwa kusoma na kuandika kwa Kiswahili, pia alianzisha maktaba za vijiji ambazo zilitumia vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili. Aidha kampeni mbalimbali za kitaifa zilizotangazwa na viongozi na kutekelezwa na wananchi zilitumia kaulimbiu za Kiswahili.
Mfano wa kampeni hizi ni ‘Siasa ni Kilimo’, ‘Mtu ni Afya’, ‘Kilimo cha Kufa na Kupona’ na ‘Madaraka Mikoani’.
Mwalimu Nyerere aliandika vitabu kwa Kiswahili, baadhi ya vitabu hivyo ni ‘TANU na Raia’ ‘Elimu Haina Mwisho’ na ‘Tujisahihishe’. Pia Mwalimu Nyerere alitafsiri kitabu cha ‘The Merchant of Venice’ cha William Shakespear kama ‘Mabepari wa Venis’ kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili.
Juhudi za Mwalimu Nyerere katika kukiendeleza Kiswahili zilikwenda mbali kwa kutoa idhini ya kuanzishwa kwa asasi mbalimbali za kushughulikia maendeleo ya Kiswahili nchini, zikiwamo Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (Tuki), Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) na Umoja wa Kiswahili na Ushauri Tanzania (UKUTA).
Kiswahili leo Nchini Tanzania Kiswahili lugha rasmi ya serikali na taifa. Shule za msingi hutumia. Kiswahili lakini shule za sekondari na vyuo bado zinaendelea kufundisha kwa Kiingereza. Kiswahili kimezidi kuenea sehemu mbalimbali duniani na kuongeza idadi ya watumiaji. Juhudi za kukiendeleza zinapata msukumo kutoka marais walioongoza Tanzania baada ya Mwalimu kwa kusisitiza matumizi ya Kiswahili.
Kiswahili kwa sasa kinatumika katika nchi za Afrika Mashariki, kati na pembe ya Afrika. Baadhi ya nchi zinazotumia lugha hiyo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Malawi Msumbiji, Zambia, Visiwa vya Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kiswahili ni miongoni mwa lugha zinazozungumzwa sana hata Mashariki ya Mbali, na Ulaya na Marekani. Kiswahili barani Afrika ni lugha ya pili ya Kiafrika inayotumiwa na watu wengi ikitanguliwa na Kiarabu. katika eneo kubwa la Afrikakiswahili ina utajiri mkubwa wa misamiati, misemo, methali, mashairi, mafumbo, vitendawili na nyimbo. Kiswahili kinatumika kufundishia shuleni na kuna vitabu vingi vilivyotungwa kwa lugha ya kiswahili, vikiwa pamoja na vile vya hadithi, hekaya na riwaya.
Kiswahili ni lugha ya utawala serikalini Tanzania na mahakamani amabko mashauri yote husikilizwa kwa lugha ya Kiswahili,
Kiswahili kinatumika kote nchini, makanisani, misikitini, redioni, kwenye runinga na idadi kubwa ya magazeti.
Nchini Kenya:
Sera ya elimu ya mwaka 2015 imechagua Kiswahili katika miaka 10 ijayo kiwe lugha ya kufundishia katika ngazi zote, ikiwemo ile ya chuo kikuu Kenya: ni lugha ya taifa tena lugha rasmi, sawa na Kiingereza, baada ya rasimu ya katiba mpya kupitishwa tarehe 4 Agosti 2010;
Kiswahili ni lugha ya kwanza ya mawasiliano kati ya wananchi wakikutana nje ya eneo lenye kabila moja tu; ni lugha inayofundishwa lakini si lugha ya kufundisha mashuleni; ni lugha inayotumika na polisi na jeshi, ni lugha ya kuhutubia wananchi mjini na kitaifa; sehemu za ibada makanisani zinatumia Kiswahili; kuna gazeti moja tu la Kiswahili; sehemu za vipindi redioni na kwenye runinga ni kwa Kiswahili. Hata hivyo mara nyingi, lugha ya Kiswahili inachanganywa na Kiingereza na lugha za maeneo au za kikabila.
Nchini Uganda:
Kiswahili kimetangazwa kuwa lugha ya taifa tangu 2005; iliwahi kuwa lugha ya taifa wakati wa utawala wa Idi Amin; wakati wa ukoloni ilifundishwa mashuleni ikaelekea kuwa lugha rasmi pamoja na Kiingereza lakini matumizi haya yalipingwa hasa na Waganda hivyo Waingereza waliacha mipango hiyo.
Ni lugha ya polisi na jeshi, hali ambayo imeleta ugumu kwa lugha kukubalika na wananchi wengi kutokana na historia ya utawala wa kijeshi Uganda; watu wengi bado hukumbuka hasa matusi ya wanajeshi waliowatesa wakizungumza Kiswahili. Lakini kuna maeneo ya Uganda ambako Kiswahili kinatumiwa na watu wengi kama lugha ya sokoni na barabarani. Wona UBC, WBS tv.
Mwaka 2005 bunge lilipiga kura kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya pili kwa kuwa kinazungumzwa zaidi (nje ya Buganda).
Nchini Rwanda:
Tarehe 8 Februari 2017 bunge la Rwanda lilifanya Kiswahili lugha rasmi ya nne baada ya Kinyarwanda, Kifaransa na Kiingereza.
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo:
Kiswahili ni kati ya lugha nne za kitaifa (pamoja na Kilingala, Kiluba na Kikongo), pia lugha ya jeshi. Kiswahili kilifika mashariki ya nchi ya DRC kupitia misafara ya wafanyabiashara ya watumwa na pembe za ndovu kutoka Zanzibar na pwani ya Tanganyika. Imeenea zaidi kati ya mchanganyiko wa wafanyakazi kwenye migodi ya Shaba.
Kimataifa
Lugha hii leo imekuwa na umuhimu mkubwa duniani kwa jumla, hasa Afrika, kwa sababu ya kuenea kwake nchi mbali mbali za ulaya zimeanzisha idhaa mbalimbali za Kiswahili zinazorusha matangazo yake Dunia nzima kwa lugha ya Kiswahili. ambazo zinachukuwa mahala pa lugha za kigeni za Wakoloni, kama Kiarabu, Kiurdu, Kiebrania, Kireno na kadhalika.
Leo Kiswahili kimekuwa kinatumiwa katika kusambaza habari katika vituo mbali mbali ulimwenguni kama vile Sauti ya Amerika, BBC, Deutsche velle, Monte Carlo, RFI, na nchi nyinginezo kama vile Uchina, Urusi, Irani.
Kiswahili kimekuwa ni mojawapo ya lugha muhimu zinazofundishwa katika vyuo vikuu nchini Marekani, Uingereza, Ulaya bara, Urusi, Uchina, na Nchi nyingi barani Afrika.
Maendeleo ya Kiswahili
Lugha ina maendeleo: inaweza kukua, kukwama au kufa. Athira nyingi hutokea bila mpangilio pale ambako wasemaji wanapokea maneno mapya, wanaacha kutumia maneno mengine au hubadilisha kawaida ya matamshi au sarufi. Haya yote hutokea pia katika uwanja wa Kiswahili.
Taasisi zinazokuza Kiswahili Tanzania
Kuna taasisi zinazolenga kukuza na kuimarisha Kiswahili kama vile Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na idara za Kiswahili katika vyuo vikuu vingine vya Kenya na pia Uganda.
Nchini Tanzania kuna Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) ilhali nchini Kenya kuna Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA). BAKITA na CHAKITA pamoja na wawakilishi kutoka Uganda wanaandaa kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la
Afrika Mashariki (BAKAMA)
Uchunguzi wa Kiswahili huendelea pia katika idara za vyuo vikuu vingi duniani, kwa mfano katika Institute National des Langues et Civilisations Orientales, jijini Paris, Ufaransa. Matumizi yake ni kwa njia ya lahaja za Kingwana.
Faida za kutumia lugha ya Kiswahili zinatajwa kama ifuatavyo:
1. Husaidia kuleta umoja wa bara zima.
2. Hudumisha utamaduni wa Kiafrika kuliko kufuata kasumba.
3. Hufanya Waafrika waamini zaidi mambo yao kuliko kutegemea tu ya kigeni.
4. Hurahisisha mawasiliano baina ya watu wa Afrika Mashariki.
5. Husaidia kuwa na mahusiano ya kibiashara na watu mbalimbali.
6. Ni ishara ya kuwa huru na kushikamana.
7. Ni utambulisho wa jamii husika (utaifa).
8. Husaidia kukuza na kuendeleza sanaa.
9. Husaidia kuimarisha ulinzi na usalama katika taifa husika.
10. Husaidia kupata ajira katika vyuo na shule mbalimbali zinazofundisha lugha ya Kiswahili hata nje ya nchi.
11. Husaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wa lugha hiyo watakaofanya vizuri katika masomo kwa kuyaelewa zaidi.
12. Husaidia kuikuza na kuieneza ndani na nje ya jamii.
Kamusi za Kiswahili
Kati ya shughuli muhimu za taasisi hizo, mojawapo ni kazi ya kukuza misamiati ya Kiswahili yaani kutafuta maneno mapya au kupanua matumizi ya maneno yaliyopo ili kutaja mambo ya maisha ya kisasa yaliyobadilika. Utunzi wa kamusi za Kiswahili hupanua elimu hiyo.
Zifuatazo ni baadhi ya Kamusi za lugha ya Kiswahili
Kamusi ya Kiswahili ya Kwanza ya mwaka 1882
Kamusi ya Kiswahili Sanifu (imetungwa na TATAKI, awali TUKI)
Kamusi la Kiswahili Fasaha (KKF), (imetungwa na BAKIZA
Kamusi ya Karne ya 21 (KK21). Nairobi, Kenya
Kamusi Teule ya Kiswahili (KTK).
Kamusi Kuu ya Kiswahili (KKK). (imetungwa na BAKITA)
Kamusi Sanifu ya Kompyuta (KSK),
Kamusi Sanifu ya Biolojia, Fizikia na Kemia
Kamusi ya Tiba (KyT),
Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha
Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha,
Kamusi ya Tashbihi, Vitendawili, Milio na Milingano,
Kamusi ya Fasihi. Istilahi na Nadharia,
Kamusi ya Historia - TUKI,
Kamusi ya Methali,
Kamusi Fafanuzi ya Methali,
Kamusi ya Biashara na Uchumi
Kamusi ya Tiba (TUKI)
Kamusi ya Ndege kwa Picha, TUKI
Kamusi ya Wanyama - TUKI
Kamusi ya Semi,
Kamusi ya Semi,
Kamusi ya Visawe,
Kamusi ya Ukristo, Mkuki na Nyoka,
Kamusi ya Kiswahili - Kiingereza
Kamusi Awali ya Sayansi na Tekinolojia (
A Standard Swahili-English Dictionary
Mafanikio ya Kiswahili nchini yametokana na juhudi kubwa za Mwalimu Nyerere ambaye mpaka leo anakumbukwa kwa kukienzi. Katika kuunga mkono jitihada zake, Watanzania wanapaswa kujivunia juhudi hizi na kuwa mstari wa mbele katika kukiendeleza na kukitumia kama utambulisho wao ili kukieneza pamoja na kutangaza utamaduni wa taifa. Lugha ya Kiswahili.
Rais wa Tanznaia Dkt John Pombe Magufuli amekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili Afrika na Duniani. Akitambua kwamba Tanzania ndipo Kiswahili kilipoanzia na asili ya Kiswahili ni nchini Tanzania.
Neno *baghami* katika lugha ya Kiswahili ni *nomino: [Ngeli: a-/wa-*] yenye maana ya mtu aliyepungukiwa akili.
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *baghami* limechukuliwa kutoka neno la Kiarabu *'baghama* ambalo ni kitenzi cha Kiarabu chenye maana zifuatazo:
1. (Kwa mnyama Paa) amempigia mwanawe kelele kwa sauti nyembamba.
2. (Kwa mnyama Ngamia) ameacha kutoa sauti.
3. (Kwa mazungumzo) hakufafanua na hakubainisha maana yake.
4. (Nomino) koja au mkufu anaouvaa mwanamke.
Kinachodhihiri ni kuwa neno *'baghama بغم* lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *baghami* lilichukua maana mpya ya *mtu aliyepungukiwa na akili* na kuacha maana zake katika lugha ya asili - Kiarabu.
Posted by: MwlMaeda - 07-02-2022, 07:50 PM - Forum: Je, wajua ?
- No Replies
Kwa faida ya wengine....
Ijumaa iliyopita, nilikuwa darasani nikiwafundisha wanafunzi wangu ndipo mwanafunzi mmoja wa kike akainua mkono kuuliza swali. Nilimruhusu na akauliza swali rahisi sana ambalo nilidhani anapaswa kujua jibu lake maana tayari nilikuwa nimezungumzia mada hiyo wiki iliyopita.
*"Kaa chini, tafadhari! Na sura yako mbaya! Muone!"* ndilo jibu pekee nililompa. Darasa zima liliangua kicheko na alionekana kufedheheka sana.
Niliendelea na somo langu lakini nilihisi kuwa na hatia kwa sababu ya kile nilichokuwa nimesema. Nilimaliza kipindi changu na kuondoka.
Siku ya Jumapili, nilienda Kanisani. Mhubiri alikuwa akiongea juu ya *nguvu ya ulimi*.
Alizungumza juu ya jinsi unavyoweza *kuwavunja moyo, kuwakatisha tamaa na kuwaangusha kabisa wengine kwa kile unachosema*. Nilikumbuka kile kilichotokea Ijumaa na nikajiona ni mwenye hatia zaidi. Niliapa kuwa nitaenda kumuomba msamaha Jumatatu nikifika darasani.
Jumatatu alasiri, nilienda darasani lakini sikumuona yule mwanafunzi. Nilimuulizia kwa wenzake lakini hawakuonekana kujua ni nani hasa niliyekuwa nikimzungumzia.
Ndipo nikasema *"ninamtafuta mtu niliyemtukana Ijumaa".*
*"Aah, huyo ni Furaha, mwalimu! Hayuko darasani leo"* walijibu.
*Rafiki yake ni nani?* Niliuliza.
*"Aisha",* walijibu. *Lakini Aisha pia hayupo darasani.*
Ghafla, msichana aliye na Hijab aliingia. *"Mwalimu, huyo ni Aisha"* wanafunzi wangu walinijulisha.
*Yuko chumba cha kuhifadhia maiti.* Alijibu.
Jibu hilo lilinishtua! *Chumba cha kuhifadhia maiti ????? Kufanya nini hapo ??* Niliuliza.
*"Alikufa Ijumaa"* Aisha alijibu.
*Imekuaje ??????* Niliuliza.
Baadaye niligundua kuwa baada ya kipindi changu Ijumaa, Furaha aligongwa na gari lililokuwa likienda kwa kasi. Alikuwa akivuka barabara bila tahadhari, labda kwa sababu ya kile nilichosema.
*"Mazishi yake ni Jumamosi na umealikwa pia, mwalimu"* Aisha aliendelea.
Wakati nilikuwa nimesimama nilijaribu kuudhibiti mshtuko niliokuwa nao, Aisha alisema huku akilia, *"Mwalimu, umemuua rafiki yangu".*
Alikuwa sahihi! Ninapaswa kuwa muuaji! Wasichana wengine darasani walikuwa tayari wanalia! Sikujua niseme nini, ikiwa ni kuomba msamaha kwa rafiki wa Furaha au kwa roho ya Furaha.
Niliwasilisha barua yangu ya kujiuzulu siku iliyofuata ikiwa na maneno haya: *Wapendwa Wahadhiri na Walimu, tafadhali acheni kutukana wanafunzi wenu. Wako shuleni ili kujifunza kutoka kwenu. Ingekuwa tayari wanajua, wasingekuwa shuleni!*
Tafadhali fikiria kile unachosema kwa watu wengine. Je! Maneno yako yanaleta uhai au kifo kwa wasikilizaji?
ZINGATIO: HADITHI HII NI LAZIMA ISOMWE NA HAIWAHUSU WALIMU TU BALI SISI SOTE TUNAPOKUWA TUNAWASILIANA NA BINADAMU WENZETU: *WATEJA, WANAFUNZI, WAZAZI, WENZIO, MARAFIKI NA KADHARIKA*
Yatupasa tuwe waangalifu sana juu ya jinsi tunavyosemezana.
FAFANUA KWA UFUPI NA KWA KUTOLEA MIFANO MAANA NA DHIMA YA KILA MOJAWAPO WA VITANZU HIVI:- SOGA, MAJIGAMBO, VICHEKESHO, NGONJERA, MICHONGOANO NA, WAADHI.
KISHINDO SHAMRASHAMRA MAADHIMISHO SIKU YA KISWAHILI DUNIANI, TAASISI, MABARAZA NA WADAU WAJIPANGA KUADHIMISHA KILA KONA, RAIS SAMIA KUONGOZA. UCHAMBUZI WA MATUKIO 10 MUHIMU
Anaaandika PhD Dkt.Ahmad Sovu
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania-kazi iendelee
Tarehe 7, Julai itakuwa ni siku ya maadhimisho ya Kiswahili Duniani (MASIKIDU). Kiswahili kinakuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika na ya saba duniani kutengewa siku yake mahsusi ya kuadhimishwa.
Hatua hii ilifikiwa mnamo tarehe 23/Novemba/2021 nchini Ufaransa katika mkutano wake wa 41 wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO ya kuipa hadhi na heshima ya kuwa na siku maalum lugha ya Kiswahili kila mwaka.
Ambapo kwa mwaka huu tarehe 7, Julai Kiswahili kitaadhimishwa kwa mara ya kwanza duniani kote.
Maadhimisho haya yamepangwa kuadhimishwa kwa kishindo na bila shaka mambo yatasena kwelikweli.
Taasisi, mabaraza, vyama vya Kiswahili, Vyuo Vikuu na wadau anuwai vimejipanga kubeleghesha maadhimisho hayo makubwa ya kidunia.
Ufuatao ni uchambuzi wa baadhi ya Taasisi namna zilivyojipanga kuenzi na kukiadhimisha Kiswahili Ulimwenguni:
Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Baraza la Kiswahili la Zanzibar, (BAKIZA), na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI)
Baraza la Kiswahili kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, BAKIZA na TATAKI zimejipanga kuadhimisha siku hiyo kwa mtindo wa aina yake. Asasi hizi mama zimeandaa mfulilizo wa matukio kuanzia tarehe mosi na sio tarehe moja kama wengine wanavyopenda kuita?? hadi tarehe 7 itakapofikia kilele cha maadhimisho hayo.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa BAKITA Bi.Consolatha Mushi, amesema tarehe mosi hadi tarehe 3 kutakuwa na tamasha kabambe la utamaduni na muziki litakofanyika katika uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam. Tarehe 3 kutakuwa na usiku wa Taarab katika viunga vya fukwe za Koko.
Tarehe 4 ni matembezi ya hisani kutoka uwanja wa Mwembe Yanga hadi uwanja wa Uhuru, tarehe 5 ni siku ya mijadala kwa wanafunzi, wadau, wasanii na tarehe 6 siku ya mdahalo motomoto kuhusu namna Kiswahili kilivyosaidia ukombozi wa wa nchi mbalimbali za Kusini mwa Afrika na tarehe 7 ndio kilele ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA)
Tume hii adhimu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki nayo ipejipanga kuadhimisha siku ya tarehe 6 na 7. Maadhimisho hayo yatafanyika Zanzibar na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Dkt.Hussein Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Kongamano hilo la aina yake nalo litawajumuisha wapenzi na mashabiki wa Lugha ya Kiswahili kutoka nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Koja la Walumbi wa Kiswahili Duniani (KOWAKIDU)
Jukwaa hili lenye umaarufu mkubwa nalo limeandaa Jioni ya Mswahili tukio la jioni ya Mswahili litafanyika katika viunga vya ufukwe wa BARAKUDA Kigamboni jijini Dar es Salaam. Ambapo, wadau watajumuika pamoja kwa ajili ya chajio, kusomwa kwa tenzi, mashairi, vitushi na Burudani mbalimbali. Tukio hilo litafanyika tarehe 7 baada ya kumalizika shughuli ya maadhimisho katika ukumbi wa Julius Nyerere.
Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania
Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam wao ndio hata hawakutaka kuchelewa. Walikuwa wa kwanza kufanya maadhimisho ya Kiswahili Duniani. Tarehe 29 mwezi wa 6 walifanya maadhimisho hayo ambayo yalibebwa na mada kuu
Kusambaa kwa lugha ya Kiswahili kwa Wamarekani kulivyoweza kuimarisha uhusiano wa kiutamaduni, kielimu, kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani
Kongandao (kongamano la Mtandaoni) na kusanyiko hilo lilihudhuriwa na Bi.Consolatha Mushi Katibu Mtendaji wa BAKITA akiwa mgeni rasmi na mwenyeji wake Mheshimiwa Balozi wa Marekani Tanzania Ndugu Donald Wright. Pamoja na mambo mengine buraha ilikuwa Mheshimiwa Balozi huyo alipotongoa hotuba yake kwa Kiswahili fasaha kabisa?? Ambapo alisema
Naipongeza hatua hii ya lugha ya Kiswahili kutengewa siku yake maalum duniani. Mimi ni Balozi lakini ni mwanafunzi wa Kiswahili??
Ubalozi wa Tanzania nchini Italia
Akihojiwa na idhaa ya Redio One ya Tanzania Mheshimiwa Balozi wa Tanzania nchini Italia Ndugu Mahmoud Thabiti Kombo alisema, wao wamejipanga vilivyo kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani huko nchini Italia.
Matukio waliyoandaa ni pamoja na mada zitakazowasilishwa na walimu mbalimbali wa Kiswahili wa Tanzania na Waitalia.
Pia, kutakuwa na maonesho ya kivazi cha Mswahili (fashion show) ambapo zitavaliwa Kanga, seruni, vikoi, msuli, kanzu, Madera, vijora n.k.
Vilevile, maadhimisho hayo yatapambwa na vyakula vya asili, manukato ya Mswahili na mambo mengine mazuri ikiwamo kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania. Hiki ndio kishindo cha MASIKIDU.
Wadau wa Kiswahili Marekani
Wadau wa Kiswahili nchini Marekani nao wamejipanga kuibelegesha siku hii ya Kiswahili Duniani. Akisailiwa na kituo cha Redio One Bi.Zaynab Mnubi anayeishi jimbo la Michigan. Alinena kuwa wao wamejipanga kuonesha bidhaa mbalimbali za Kiswahili. Bidhaa hizo ni pamoja na makawa, mkeka wa chembe, nguo, vitabu.
Aidha, wataonesha aina mbalimbali za mitindo ya misuko ya Kiswahili. Misuko kama twende kilioni, tatu kichwa n.k✍️✍️ Shughuli hiyo itafanyika katika moja ya maktaba kubwa ya mji huo. Hiki ndi Kishindo cha Kiswahili.
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
Chuo hiki ambacho kinabeba jina la mwasisi wa Taifa nacho hakikubaki nyuma.
Kupitia idara yake ya Lugha na Fasihi kwa kushirikiana na uongozi wa Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili Vyuo Vikuu Tanzania chuoni hapo kiliandaa siku mahsusi ya Kiswahili tarehe 18/6/2022. Pamoja na maudhui mengine ililenga kuwaandaa Wanafunzi wanaosoma Kiswahili chuoni hapo kujipanga kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani.
Bi.Consolatha Mushi na wadau wengine wa Kiswahili kina Masau Bwire, Maulid Kambaya, Majid Mswahili na wengine tele walibeleghesha siku hiyo ambapo kaulimbiu ilikuwa Lumba Kiswahili, Jiandae kuhesabiwa na Kazi Iendelee
Chuo cha Sumait Zanzibar
Chuo cha Kumbukumbu ya Abdurahman Sumait Zanzibar nao wamejipanga kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani. Mkuu wa Idara ya lugha chuo hapo Bi.Ulfat Ibrahim amesema wao wameandaa kongandao, yaani kongamano la Kimataifa la Mtandaoni leo tarehe mosi kuelekea maadhimisho ya siku hiyo adhimu ya Kiswahili Duniani.
Mada kuu ni hadhi na fursa ya Kiswahili Duniani. Wataalamu kutoka Ujerumani, Tanzania, Marekani, Afrika Kusini, Zanzibar watashiriki. Hiki ndio kishindo cha MASIKIDU.
Chuo cha KwaZulu Natal Afrika Kusini
Nako Bondeni tayari shamrashamra zimeanza. Nimefanya mazungumzo na Mwalimu Kiswahili chuoni hapo Ndugu Edwel Dzomba anaeleza kuwa wao tayari wamekwishaandaa fulana zao kwa ajili ya MASIKIDU ili kuichagiza siku hiyo.
Hata hivyo, wameona ila utamu unoge watakuja kwenye kitovu cha Kiswahili TANZANIA kwa ajili ya kuungana na Watanzania wote kuadhimisha siku hii adhimu ya Kiswahili.
Kaka Sovu ujumbe wa watu wa 4 viongozi wa Chuo Kikuu cha Kwa Zulu Natal tunakuja kwenye MASIKIDU TANZANIA alisema Mwalimu Dzomba. Hiki ndio kishindo cha MASIKIDU.
Chuo cha Saint John's Dodoma
Makao makuu ya nchi nako kutarindima. Wao wameandaa kongandao babkubwa litakalofanyika Mtandaoni. Shabaha ya kongandao hilo ni kutathimini hali ya utafiti wa Kiswahili ilivyo. Mhadhiri mwandamizi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Dkt.Athumani Ponera anatarajiwa kuwa mtoa mada mkuu katika kongandao hilo. Mudiri wa idara ya Kiswahili chuoni hapo, Dkt.Shadidu Ndossa amesema wao wanalenga kuzitia shime taasisi, wataalamu na watafiti anuwai wa Kiswahili kuongeza bidii ya kutafiti zaidi lugha ya Kiswahili hasa ukizingatia kwa sasa Kiswahili kimebeba majukumu ya kidunia. Ametoa wito kwa wadau na wapenzi kushiriki kongandao hilo.
Haya ni baadhi tu ya matukio muhimu ambayo yatabeleghesha maadhimisho ya siku ya Kiswahili Duniani.
Ni burdani kila pahala Kiswahili kinakwenda kuisimamisha dunia.?
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ataja faida ya siku hii kwa Tanzania
Jamadari Mkuu, Amiri jeshi mkuu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan mbali ya kuwa anatarajiwa kuongoza kilele cha maadhimisho haya, amedokeza faida za hatua hii ya Kiswahili kutengewa siku yake maalum duniani. Ambazo ni:
-Kuongeza heshima kwa Taifa letu la Tanzania ambalo ndilo chimbuko la lugha ya Kiswahili.
-Itanyanyua hadhi ya Kiswahili Tanzania ??, Afrika Mashariki na maeneo yote kinamozungumzwa.
-Kiswahili kitaendelea kusemwa kwa upana.
-Idadi ya wanaotaka kusoma Kiswahili itaongezeka.
-Itaongeza fursa zaidi kwa Watanzania
-Itaongeza utangamano wa dunia.
-Itakuza uzalendo na thamani ya lugha ya Kiswahili.
Kongole Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kwa kuienzi lugha yetu adhimu na aushi ya Kiswahili.
Nimalizie kwa maneno ya mdau aitwaye Mwebesa anasema:
macho, masikio na hisia za walimwengu (waungwana) takriban wote wanayaelekeza Afrika Mashariki na hasa nchini Tanzania kuelekea JULAI SABA. Sherehe zinaswihi ila kubwa kuliko yote leo hii na kesho tuendako Kiswahili kilete fedha, pato binafsi na la umma (serikali), fursa kwa Watanzania, Waafrika na hata Waghaibu (diaspora) wote. KISWAHILI NI MALI KULIKO ZOTE AFRIKA
MWITO
Mwisho napenda kutoa mwito kwa Watanzania wote kushiriki katika shamrashamra za maadhimisho haya hususan kwa wale walioko DSM na maeneo mbalimbali kunakofanyika maadhimisho haya.
IFIKAPO TAREHE 7/7 TUISIMAMISHE DUNIA JAPO KWA DAKIKA TANO. KILA MMOJA ASHEREKEE HATA KWA KUWEKA WIMBO WA KISWAHILI AU JAMBO LOLOTE LILE LIHUSULO KISWAHILI.
Lumba Kiswahili, Jiandae kuhesabiwa, Kazi IENDELEEE
Mwandishi ni Mhadhiri na Mshititi kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni DSM.
sovu82@gmail.com
Neno bakaa katika lugha ya Kiswahili ni nomino: [Ngeli: li-/ya-, wingi: mabakaa] yenye maana zifuatazo:
1. Salio linalobaki baada ya matumizi ya kitu.
2. Kiasi cha fedha kinachobaki baada ya matumizi.
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili bakaa limechukuliwa kutoka neno la Kiarabu 'baqaa( soma: baqaaun/baqaa-an/baqaain بقاء ) ambalo ni nomino ya Kiarabu yenye maana zifuatazo:
1. Kukaa mahali, kudumu.
2. Kuendelea na jambo.
3. Kukaa milele, daarul baqaai دار البقاء nyumba ya milele; kuzimu.
4. Tendo-jina la kitenzi cha Kiarabu baqiya بقي chenye maana ya kudumu, kilichothibiti, kilichobakia kutokana na kitu.
Kinachodhihiri ni kuwa neno 'baqaaun بقاء lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno bakaa lilichukua kutoka lugha ya asili - Kiarabu maana ya kilichobakia kutokana na kitu na likapewa maana ya salio linalobaki baada ya matumizi ya kitu, kiasi cha fedha kinachobaki baada ya matumizi.
TANBIHI:
Katika Kiarabu neno linalotumiwa kwa maana ya salio linalobaki baada ya matumizi ya kitu, kiasi cha fedha kinachobaki baada ya matumizi ni neno raswiid (soma: raswiidun/raswiidan/raswiidin رصيد).
Neno *bairi* katika lugha ya Kiswahili ni *nomino: [Ngeli: a-/wa-*] yenye maana ya *mnyama mkubwa mwenye nundu mgongoni abebaye mizigo wakati wa safari ndefu aghalabu jangwani; ngamia.*
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *bairi* limechukuliwa kutoka neno la Kiarabu *'baiiru*( *soma: baiirun/baiiran/bairiin بعير )* ambalo ni nomino ya Kiarabu yenye maana zifuatazo:
1. Mnyama afaaye kumpanda kwa usafiri au kumbebesha mizigo miongoni mwa ngamia wa kiume na wa kike baada ya kutimia umri wa miaka minne.
2. Punda atumikaye kubeba mizigo.
Waarabu wana msemo maarufu: *Alba-aratu Tadullu Alal Baiiri البعرة تدل على البعير* kinyesi cha ngamia ni dalili ya kupita kwake hapo.
Kinachodhihiri ni kuwa neno *'baiirun بعير* lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *bairi* lilichukua maana ya jumla ya mnyama *ngamia* na kuacha maana halisi ya mnyama aliyefikisha miaka minne akafaa kubeba watu na mizigo aghalabu kwa safari za jangwani.
HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO 'PUNGUANI, HAYAWANI ' NA 'MAJNUNI'
Maneno *punguani, hayawani na majnuni* yanatumika kwa maana ya mtu ambaye akili zake zina hitilafu; mwendawazimu, chizi, kichaa, mwehu.
Neno *punguani* katika lugha ya Kiswahili ni nomino [ *Ngeli: a-/wa-]* yenye maana ya mtu ambaye akili zake zina hitilafu; mwendawazimu, chizi, majnuni.
Neno *punguani* pia ni kivumishi chenye maana ya '-enye akili zisizotimia; pungufu wa akili.
Neno hili *punguani* etimolojia yake ni Kibantu na linatokana na kitenzi si elekezi *pungua* ambacho moja ya maana zake ni *kuwa na hitilafu; kutotimia.*
Neno *hayawani* katika lugha ya Kiswahili ni nomino [ *Ngeli: a-/wa-, wingi: mahayawani]* yenye maana zifuatazo:
1. Mnyama.
2. Mtu anayefananishwa na mnyama aghalabu asiye na adabu.
3. Mtu asiye na nidhamu.
4. Mwendawazimu, mwehu, kichaa, chizi.
5. Shetani.
Katika lugha ya Kiarabu, neno *hayawani* limetokana na neno la Kiarabu *hayawaanun* (soma: *hayawaanun/hayawaanan/hayawaanin حيوان* ) lenye maana zifuatazo:
1. Kiumbe hai kinachojipambanua kwa kuwa na uhai, hisi na harakati; kila kilicho hai chenye kinachosema ( mwanadamu ambaye huitwa *hayawaanun naatwiqun حيوان ناطق* mnyama mwenye kusema) na mnyama asiyesema (baki ya wanyama wengineo).
2- Mnyama mwenye sifa ya mmea *hayawaanun nabaatiy* *حيوان نباتي* mnyama anayefanana na umbo la mmea kama *sifongo*.
3- Mnyama wa medula *hayawaanun nakhaaiyun حيوان نخاعي* mnyama wa uti wa mgongo, mwenye uti wa mgongo lakini hana ubongo.
4- Mbegu ya uzazi: manii.
Kinachodhihiri ni kuwa neno hili ( *hayawaanun/hayawaanan/hayawaanin حيوان*) lilipoingia katika lugha ya Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *hayawani* lilichukua katika lugha ya asili - Kiarabu maana za mnyama na mwendawazimu, kulipa maana mpya ya mtu asiye na aibu/nidhamu na kuacha maana zingine.
Neno *majinuni* katika lugha ya Kiswahili ni nomino [ *Ngeli: a-/wa-]* yenye maana ya mtu asiye na akili.
Neno hili *majinuni* linatokana na neno la Kiarabu *majnuun* (soma: *majnuunun/majnuunan/majnuunin محنون* ) lenye maana ya mtu asiye na akili.
Kinachodhihiri ni kuwa maana za maneno ya Kiarabu *hayawanun* na *majnuunun* yalipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa hayawani na majinuni hayakubadili maana ya mtu asiye na akili.
HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO 'FAKIRI/FUKARA' na 'MASKINI'
Neno *fakiri* katika lugha ya Kiswahili ni nomino [ *Ngeli: a-/wa-]* yenye maana ya mtu asiye na mali, maskini sana.
Neno *fakiri* pia ni kivumishi chenye maana ya: - enye umaskini, -a kuhitaji.
Neno *fukara* katika lugha ya Kiswahili ni nomino [ *Ngeli: a-/wa-, wingi: mafukara]* yenye maana ya mtu maskini sana.
Katika lugha ya Kiarabu, neno *fakiri* limetokana na neno la Kiarabu *faqiir* (soma: *faqiirun/faqiira/faqiirin فقير* ) lenye maana zifuatazo:
1. Muhitaji asiyemiliki cha kumtosha yeye na familia yake.
2. Mtu mwenye maumivu ya uti wa mgongo kutokana na kuvunjika au maradhi.
3. Shimo lililochimbwa kwa ajili ya kupanda mche au mbegu.
4. Mkondo wa maji kutoka katika mdomo wa mfereji kama vile Mfereji wa Suez, nchini Misri.
Kinachodhihiri ni kuwa neno hili ( *faqiirun/faqiiran/faqiirin فقير*) lilipoingia katika lugha ya Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *fakiri* lilichukua katika lugha ya asili - Kiarabu maana ya mtu asiye na mali, masikini sana na kuacha maana zingine.
Waswahili walilichukua neno fukara linalotokana na nomino ya Kiarabu *fuqaraau فقراء* ambalo ni wingi wa neno *faqiirun (fakiri)* na kulipa pia maana ileile ya neno *fakiri*.
Neno *maskini* katika lugha ya Kiswahili ni nomino [ *Ngeli: a-/wa-]* yenye maana ya mtu au nchi isiyojitosheleza kimapato.
Neno hili *maskini* linatokana na neno la Kiarabu *miskiin* (soma: *miskiinun/miskiinan/muskiinin مسكين* ) lenye maana zifuatazo:
1. Fakiri muhitaji sana.
2. Mtu ambaye hamiliki chochote katika mali.
3. Mtu dhalili, mnyonge.
Kinachodhihiri ni kuwa maana za maneno fakiri *(fukara)* na *maskini* , katika Kiswahili na Kiarabu, zinashabihiana na kukurubiana kiasi cha kuona maneno yote yana maana moja.
*TANBIHI:*
Katika muktadha wa Sharia ya Kiislamu maneno *fakiri* na *maskini* yametumika kwa maana kuwa *fakiri ni yule asiye na kipato maalumu* na *maskini ni yule mwenye kipato kisichomtosha.*