ETIMOLOJIA YA MANENO 'PUNGUANI, HAYAWANI ' NA 'MAJNUNI' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA MANENO 'PUNGUANI, HAYAWANI ' NA 'MAJNUNI' (/showthread.php?tid=2612) |
ETIMOLOJIA YA MANENO 'PUNGUANI, HAYAWANI ' NA 'MAJNUNI' - MwlMaeda - 06-27-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO 'PUNGUANI, HAYAWANI ' NA 'MAJNUNI' Maneno *punguani, hayawani na majnuni* yanatumika kwa maana ya mtu ambaye akili zake zina hitilafu; mwendawazimu, chizi, kichaa, mwehu. Neno *punguani* katika lugha ya Kiswahili ni nomino [ *Ngeli: a-/wa-]* yenye maana ya mtu ambaye akili zake zina hitilafu; mwendawazimu, chizi, majnuni. Neno *punguani* pia ni kivumishi chenye maana ya '-enye akili zisizotimia; pungufu wa akili. Neno hili *punguani* etimolojia yake ni Kibantu na linatokana na kitenzi si elekezi *pungua* ambacho moja ya maana zake ni *kuwa na hitilafu; kutotimia.* Neno *hayawani* katika lugha ya Kiswahili ni nomino [ *Ngeli: a-/wa-, wingi: mahayawani]* yenye maana zifuatazo: 1. Mnyama. 2. Mtu anayefananishwa na mnyama aghalabu asiye na adabu. 3. Mtu asiye na nidhamu. 4. Mwendawazimu, mwehu, kichaa, chizi. 5. Shetani. Katika lugha ya Kiarabu, neno *hayawani* limetokana na neno la Kiarabu *hayawaanun* (soma: *hayawaanun/hayawaanan/hayawaanin حيوان* ) lenye maana zifuatazo: 1. Kiumbe hai kinachojipambanua kwa kuwa na uhai, hisi na harakati; kila kilicho hai chenye kinachosema ( mwanadamu ambaye huitwa *hayawaanun naatwiqun حيوان ناطق* mnyama mwenye kusema) na mnyama asiyesema (baki ya wanyama wengineo). 2- Mnyama mwenye sifa ya mmea *hayawaanun nabaatiy* *حيوان نباتي* mnyama anayefanana na umbo la mmea kama *sifongo*. 3- Mnyama wa medula *hayawaanun nakhaaiyun حيوان نخاعي* mnyama wa uti wa mgongo, mwenye uti wa mgongo lakini hana ubongo. 4- Mbegu ya uzazi: manii. Kinachodhihiri ni kuwa neno hili ( *hayawaanun/hayawaanan/hayawaanin حيوان*) lilipoingia katika lugha ya Kiswahili na kutoholewa kuwa neno *hayawani* lilichukua katika lugha ya asili - Kiarabu maana za mnyama na mwendawazimu, kulipa maana mpya ya mtu asiye na aibu/nidhamu na kuacha maana zingine. Neno *majinuni* katika lugha ya Kiswahili ni nomino [ *Ngeli: a-/wa-]* yenye maana ya mtu asiye na akili. Neno hili *majinuni* linatokana na neno la Kiarabu *majnuun* (soma: *majnuunun/majnuunan/majnuunin محنون* ) lenye maana ya mtu asiye na akili. Kinachodhihiri ni kuwa maana za maneno ya Kiarabu *hayawanun* na *majnuunun* yalipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa hayawani na majinuni hayakubadili maana ya mtu asiye na akili. *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |