MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
HISTORIA YA LUGHA YA KISWAHILI

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
HISTORIA YA LUGHA YA KISWAHILI
#1
Lugha ya Kiswahili imeanza takriban miaka 1000 iliyopita kwenye pwani ya Afrika ya Mashariki. Neno Swahili lina asili ya Kiarabu: Sahil ina maana ya pwani; sawahil ’’ a-sawāhilī’’ ni wingi wake kwa kumaanisha yote yanayohusiana na pwani, watu au utamaduni na lugha ya eneo la pwani. Kiswahili kilianza kama lugha ya miji na bandarini wakati wa biashara ya kimataifa kwenye pwani ya Afrika ya mashariki.

Tuna historia jinsi gani miji kama vile Kilwa, Lamu na mingine kadhaa iliyoanzishwa na wafanyabiashara Waarabu au Wajemi waliooa wenyeji. Idadi ya wahamiaji kutoka Uarabuni haikuwa kubwa sana, hivyo lugha ya wenyeji ilitumika kila mahali ila tu maneno mengi yameingia kutoka katika lugha ya Kiarabu. Utamaduni mpya ulijitokeza uliokuwa wa Kiafrika Kiswahili kilizaliwa kuwa lugha ya Kibantu kilichopokea maneno mengi ya asili na ya nje.

Kiswahili kiliandikwa muda mrefu kwa herufi za Kiarabu kama inavyosomeka kwenye sanamu ya askari huko Dar es Salaam, Tanzania. Maandishi Yanasema: "Huu ni ukumbusho wa askari wenyeji Waafrika waliopigana katika Vita Kuu."

Lugha iliandikwa kwa herufi za Kiarabu tangu karne ya 13 kabla ya kristo. Kwa bahati mbaya leo hatuna tena maandiko ya kale sana, kutokana na hali ya hewa kwenye pwani isiyosaidia kutunza karatasi na kurasa zenyewe zinaweza kuoza kutokana na unyevu hewani pamoja na wadudu wengi walioko katika mazingira ya pwani ya Tanzania.

Kuna Maandiko ya kale yanayopatikana kutoka karne ya 17 huonyesha ya kwamba tenzi na mashairi vinafuata muundo uliotangulia maandiko yenyewe kwa karne kadhaa. Sehemu kubwa ya maandiko ya kale ni tenzi yaani mashairi yenye aya maelfu. Tenzi ndefu kabisa inahusu kifo cha Mtume Muhamad ikiwa na aya 45,000.

Kiswahili kilipokelewa kirahisi na wenyeji kwa sababu walikosa lugha ya pamoja kati yao, lugha za Kibantu ziko karibu sana na athira ya Kiarabu ilikuwa kilekile kote pwani. Haya yote yalisaidia kujenga umoja wa Kiswahili katika eneo kubwa la pwani ya Afrika ya Mashariki. Kiajemi pia kilichangia maneno mbalimbali, kama vile "bibi" na "cherehani".

Kufika kwa Wareno huko Afrika ya Mashariki kuanzia mwaka 1500 kulileta athira mpya ikiwa maneno kadhaa ya Kireno yameingia katika Kiswahili kama vile "bendera", "gereza" na "meza".

Kuwepo kwa wafanyabiashara Wahindi katika miji mikubwa ya pwani kuliingiza pia maneno ya asili ya Kihindi katika lugha kama vile "lakhi", "gunia" n.k. Athira ya lugha za Kihindi iliongezeka kiasi baada ya Waingereza kutumia Wahindi wengi kujenga reli ya Uganda.

Kiswahili kama Lugha ya biashara.

Kiswahili kilitumika kama lugha ya biashara baina ya watu wa pwani na bara katika kanda ndefu sana kutoka Somalia hadi kasikazini mwa Msumbiji,

Wafanyabiashara Waswahili waliendeleza biashara ya misafara hadi Kongo. Kiswahili kiliendelea kuenea kwenye njia za misafara hii. Kila msafara ulihitaji mamia ya watu hadi maelfu wa kubeba mizigo ya biashara kutoka pwani hadi pale msafara ulipolenga Ziwa Tanganyikan. katika mkoa wa Kigoma.

Watu hawa wote walisambaza matumizi ya Kiswahili katika sehemu za ndani ya Tanzania.

Kiswahili wakati wa ukoloni
Karne ya 19 ilileta utawala wa kikoloni. Wakoloni walitangulia kufika katika bandari za pwani wakatumia makarani, askari na watumishi kutoka eneo la pwani wakijenga vituo vyao Pwani wakitumia lugha ya kiswahili. Watu hao walipeleka

Kiswahili pande za bara.
Wajerumani waliamua kutumia Kiswahili kama lugha ya utawala katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Hapo waliweza kutumia kazi ya wamisionari Wakristo wa awali, hasa Ludwig Krapf, waliowahi kufanya utafiti wa lugha na kutunga kamusi na sarufi za kwanza mwaka 1879 na kuchapishwa Jijini London Uingereza Mwaka 1882 pamoja na kuunda mfumo wa kuandika Kiswahili kwa herufi za Kilatini.

Utawala wa kikoloni ulirahisisha mawasiliano kati ya wenyeji kwa kuzungumza Kiswahili wakati wote wa Ujenzi wa Reli ya kati ilijengwa na wafanyakazi kutoka makabila mbalimbali wakishirikiana.

Waafrika walilazimishwa kulipa kodi kwa wakoloni, hivyo walitafuta kazi ya ajira katika mashamba makubwa yaliyolimwa mazao ya biashara na katika migodi ya madini huko Kongo ambako watu wa makabila mengi walichanganyikana wakitumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano.

Namna Lugha ya Kiswahili ilivyoenea zaidi.
Waingereza baada ya kuchukua Tanganyika kutoka kwa Wajerumani waliendela kutumia Kiswahili kama lugha ya utawala. Kuanzia mwaka 1930 waliunda kamati yenye shabaha ya kuunganisha lahaja mbalimbali na kuunda Kiswahili cha pamoja kwa ajili ya Afrika ya Mashariki (Inter-territorial Language (Swahili) committee for the East African Dependencies).

Mwenyekiti alikuwa Frederick Johnson, makatibu R. K. Watts, P. Mzaba na Seyyid Majid Khalid Barghash. Kamati hiyo iliamua kutumia lahaja ya Kiunguja kuwa msingi wa Kiswahili cha pamoja kilichoendela kufundishwa shuleni. Leo hii ndicho Kiswahili rasmi kinachofunzwa na wanafunzi na kuandikwa magazetini na vitabuni.

Miaka ya ukoloni ilisababisha kupokelewa kwa maneno mapya katika Kiswahili. Kijerumani kiliacha maneno machache kama "shule" (Kijerumani Schule) na "hela" (Heller) lakini maneno mengi sana ya asili ya Kiingereza yalipokelewa.

Kiswahili kimeonyesha uwezo mkubwa wa kupokea maneno kutoka lugha tofauti, kikitumia maneno haya kufuatana na sarufi ya Kibantu ya Kiswahili.

Mwalim Nyerere alivyochangia kukua kwa Kiswahili
HAYATI Mwalimu Julius Nyerere, ni miongoni mwa viongozi wanaokumbukwa kwa kuwa watetezi wa lugha na falsafa za Kiafrika, akiheshimika kwa juhudi kubwa za kukuza na kuendeleza Kiswahili katika jitihada za kuwaunganisha Watanzania na Waafrika pia.

Mchango wake ulianza wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Hii inajidhihirisha kwa kuangalia jinsi alivyotumia lugha ya Kiswahili kama chombo muhimu cha mawasiliano ambacho kiliwaunganisha Watanganyika kupigania na kudai uhuru.

MWALIMU Nyerere alitumia Kiswahili katika kampeni za kisiasa ambapo siasa na sera za TANU zilienezwa sehemu mbalimbali nchini kwa kutumia kiswahili. Matumizi ya lugha ya Kiswahili ni sababu mojawapo ya Tanganyika kupata Uhuru mapema na bila vikwazo vingi wale waliokuwa hawaifahamu na waliokuwa hawajui kusoma walipata nafasi ya kujifunza na kuelewa hatua za kudai uhuru zinavyokwenda na zilipofikia. Baada ya Uhuru,

Mwalimu Nyerere akiwa Waziri Mkuu wa kwanza alitangaza Kiswahili kuwa Lugha ya Taifa na kuagiza itumike katika shughuli zote rasmi za umma. Kwa kuonyesha msisitizo wa matumizi ya lugha hii, Nyerere alitoa hotuba ya kusherekea sikukuu ya Jamhuri tarehe 10, Desemba 1962, kwa Kiswahili.

Hatua hiyo ilidhihirisha na kukionyesha Kiswahili kama lugha asilia ambayo ilitumika ili kuondoa uwezekano wowote wa mafarakano yanayohusiana na mitafaruku ya kimatamshi.

Aidha, Mwalimu Nyerere alihutubia hafla nyingi kwa Kiswahili, hatua ambayo ilifanya kila mwananchi kuelewa mipango na mikakati ya serikali katika kuwaletea maendeleo yao. Kuanzia wakati huo Kiswahili kilianza kutumika katika shughuli zote za nyanja mbalimbali nchini kwa kuimarisha mahusiano ya makabila na kuifanya nchi kuwa kama kabila moja licha ya kuwa na zaidi ya makabila 120.

Hatua ya pili iliyochukuliwa na Mwalimu Nyerere ilikuwa ni kupitisha Azimio la Arusha mwaka 1967, aliposema kuwa ni mfumo wa “ujamaa na kujitegemea ndiyo sera ya taifa, hii ilikuwa ni njia muhimu ya kuwaunganisha Watanzania wote.

Matumizi ya Kiswahili yaliendelea kupanuka ambapo mnamo 1962, lugha hii ilianza kutumika rasmi bungeni na kwa upande wa elimu kilianza kutumika kufundishia masomo yote katika shule za msingi nchini huku Kiingereza kikibaki kufundishwa kama somo.

Mwalimu Nyerere alianzisha mpango wa Elimu ya Watu wazima, waliofundishwa kusoma na kuandika kwa Kiswahili, pia alianzisha maktaba za vijiji ambazo zilitumia vitabu vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili. Aidha kampeni mbalimbali za kitaifa zilizotangazwa na viongozi na kutekelezwa na wananchi zilitumia kaulimbiu za Kiswahili.

Mfano wa kampeni hizi ni ‘Siasa ni Kilimo’, ‘Mtu ni Afya’, ‘Kilimo cha Kufa na Kupona’ na ‘Madaraka Mikoani’.

Mwalimu Nyerere aliandika vitabu kwa Kiswahili, baadhi ya vitabu hivyo ni ‘TANU na Raia’ ‘Elimu Haina Mwisho’ na ‘Tujisahihishe’. Pia Mwalimu Nyerere alitafsiri kitabu cha ‘The Merchant of Venice’ cha William Shakespear kama ‘Mabepari wa Venis’ kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili.

Juhudi za Mwalimu Nyerere katika kukiendeleza Kiswahili zilikwenda mbali kwa kutoa idhini ya kuanzishwa kwa asasi mbalimbali za kushughulikia maendeleo ya Kiswahili nchini, zikiwamo Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (Tuki), Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) na Umoja wa Kiswahili na Ushauri Tanzania (UKUTA).

Kiswahili leo Nchini Tanzania Kiswahili lugha rasmi ya serikali na taifa. Shule za msingi hutumia. Kiswahili lakini shule za sekondari na vyuo bado zinaendelea kufundisha kwa Kiingereza. Kiswahili kimezidi kuenea sehemu mbalimbali duniani na kuongeza idadi ya watumiaji. Juhudi za kukiendeleza zinapata msukumo kutoka marais walioongoza Tanzania baada ya Mwalimu kwa kusisitiza matumizi ya Kiswahili.

Kiswahili kwa sasa kinatumika katika nchi za Afrika Mashariki, kati na pembe ya Afrika. Baadhi ya nchi zinazotumia lugha hiyo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Malawi Msumbiji, Zambia, Visiwa vya Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kiswahili ni miongoni mwa lugha zinazozungumzwa sana hata Mashariki ya Mbali, na Ulaya na Marekani. Kiswahili barani Afrika ni lugha ya pili ya Kiafrika inayotumiwa na watu wengi ikitanguliwa na Kiarabu. katika eneo kubwa la Afrikakiswahili ina utajiri mkubwa wa misamiati, misemo, methali, mashairi, mafumbo, vitendawili na nyimbo. Kiswahili kinatumika kufundishia shuleni na kuna vitabu vingi vilivyotungwa kwa lugha ya kiswahili, vikiwa pamoja na vile vya hadithi, hekaya na riwaya.

Kiswahili ni lugha ya utawala serikalini Tanzania na mahakamani amabko mashauri yote husikilizwa kwa lugha ya Kiswahili,

Kiswahili kinatumika kote nchini, makanisani, misikitini, redioni, kwenye runinga na idadi kubwa ya magazeti.

Nchini Kenya:
Sera ya elimu ya mwaka 2015 imechagua Kiswahili katika miaka 10 ijayo kiwe lugha ya kufundishia katika ngazi zote, ikiwemo ile ya chuo kikuu Kenya: ni lugha ya taifa tena lugha rasmi, sawa na Kiingereza, baada ya rasimu ya katiba mpya kupitishwa tarehe 4 Agosti 2010;

Kiswahili ni lugha ya kwanza ya mawasiliano kati ya wananchi wakikutana nje ya eneo lenye kabila moja tu; ni lugha inayofundishwa lakini si lugha ya kufundisha mashuleni; ni lugha inayotumika na polisi na jeshi, ni lugha ya kuhutubia wananchi mjini na kitaifa; sehemu za ibada makanisani zinatumia Kiswahili; kuna gazeti moja tu la Kiswahili; sehemu za vipindi redioni na kwenye runinga ni kwa Kiswahili. Hata hivyo mara nyingi, lugha ya Kiswahili inachanganywa na Kiingereza na lugha za maeneo au za kikabila.

Nchini Uganda:
Kiswahili kimetangazwa kuwa lugha ya taifa tangu 2005; iliwahi kuwa lugha ya taifa wakati wa utawala wa Idi Amin; wakati wa ukoloni ilifundishwa mashuleni ikaelekea kuwa lugha rasmi pamoja na Kiingereza lakini matumizi haya yalipingwa hasa na Waganda hivyo Waingereza waliacha mipango hiyo.

Ni lugha ya polisi na jeshi, hali ambayo imeleta ugumu kwa lugha kukubalika na wananchi wengi kutokana na historia ya utawala wa kijeshi Uganda; watu wengi bado hukumbuka hasa matusi ya wanajeshi waliowatesa wakizungumza Kiswahili. Lakini kuna maeneo ya Uganda ambako Kiswahili kinatumiwa na watu wengi kama lugha ya sokoni na barabarani. Wona UBC, WBS tv.

Mwaka 2005 bunge lilipiga kura kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya pili kwa kuwa kinazungumzwa zaidi (nje ya Buganda).

Nchini Rwanda:
Tarehe 8 Februari 2017 bunge la Rwanda lilifanya Kiswahili lugha rasmi ya nne baada ya Kinyarwanda, Kifaransa na Kiingereza.

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo:
Kiswahili ni kati ya lugha nne za kitaifa (pamoja na Kilingala, Kiluba na Kikongo), pia lugha ya jeshi. Kiswahili kilifika mashariki ya nchi ya DRC kupitia misafara ya wafanyabiashara ya watumwa na pembe za ndovu kutoka Zanzibar na pwani ya Tanganyika. Imeenea zaidi kati ya mchanganyiko wa wafanyakazi kwenye migodi ya Shaba.

Kimataifa
Lugha hii leo imekuwa na umuhimu mkubwa duniani kwa jumla, hasa Afrika, kwa sababu ya kuenea kwake nchi mbali mbali za ulaya zimeanzisha idhaa mbalimbali za Kiswahili zinazorusha matangazo yake Dunia nzima kwa lugha ya Kiswahili. ambazo zinachukuwa mahala pa lugha za kigeni za Wakoloni, kama Kiarabu, Kiurdu, Kiebrania, Kireno na kadhalika.

Leo Kiswahili kimekuwa kinatumiwa katika kusambaza habari katika vituo mbali mbali ulimwenguni kama vile Sauti ya Amerika, BBC, Deutsche velle, Monte Carlo, RFI, na nchi nyinginezo kama vile Uchina, Urusi, Irani.

Kiswahili kimekuwa ni mojawapo ya lugha muhimu zinazofundishwa katika vyuo vikuu nchini Marekani, Uingereza, Ulaya bara, Urusi, Uchina, na Nchi nyingi barani Afrika.

Maendeleo ya Kiswahili
Lugha ina maendeleo: inaweza kukua, kukwama au kufa. Athira nyingi hutokea bila mpangilio pale ambako wasemaji wanapokea maneno mapya, wanaacha kutumia maneno mengine au hubadilisha kawaida ya matamshi au sarufi. Haya yote hutokea pia katika uwanja wa Kiswahili.

Taasisi zinazokuza Kiswahili Tanzania
Kuna taasisi zinazolenga kukuza na kuimarisha Kiswahili kama vile Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na idara za Kiswahili katika vyuo vikuu vingine vya Kenya na pia Uganda.

Nchini Tanzania kuna Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) ilhali nchini Kenya kuna Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA). BAKITA na CHAKITA pamoja na wawakilishi kutoka Uganda wanaandaa kuundwa kwa Baraza la Kiswahili la

Afrika Mashariki (BAKAMA)
Uchunguzi wa Kiswahili huendelea pia katika idara za vyuo vikuu vingi duniani, kwa mfano katika Institute National des Langues et Civilisations Orientales, jijini Paris, Ufaransa. Matumizi yake ni kwa njia ya lahaja za Kingwana.

Faida za kutumia lugha ya Kiswahili zinatajwa kama ifuatavyo:

1. Husaidia kuleta umoja wa bara zima.

2. Hudumisha utamaduni wa Kiafrika kuliko kufuata kasumba.

3. Hufanya Waafrika waamini zaidi mambo yao kuliko kutegemea tu ya kigeni.

4. Hurahisisha mawasiliano baina ya watu wa Afrika Mashariki.

5. Husaidia kuwa na mahusiano ya kibiashara na watu mbalimbali.

6. Ni ishara ya kuwa huru na kushikamana.

7. Ni utambulisho wa jamii husika (utaifa).

8. Husaidia kukuza na kuendeleza sanaa.

9. Husaidia kuimarisha ulinzi na usalama katika taifa husika.

10. Husaidia kupata ajira katika vyuo na shule mbalimbali zinazofundisha lugha ya Kiswahili hata nje ya nchi.

11. Husaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wa lugha hiyo watakaofanya vizuri katika masomo kwa kuyaelewa zaidi.

12. Husaidia kuikuza na kuieneza ndani na nje ya jamii.

Kamusi za Kiswahili
Kati ya shughuli muhimu za taasisi hizo, mojawapo ni kazi ya kukuza misamiati ya Kiswahili yaani kutafuta maneno mapya au kupanua matumizi ya maneno yaliyopo ili kutaja mambo ya maisha ya kisasa yaliyobadilika. Utunzi wa kamusi za Kiswahili hupanua elimu hiyo.

Zifuatazo ni baadhi ya Kamusi za lugha ya Kiswahili
  • Kamusi ya Kiswahili ya Kwanza ya mwaka 1882

  • Kamusi ya Kiswahili Sanifu (imetungwa na TATAKI, awali TUKI)

  • Kamusi la Kiswahili Fasaha (KKF), (imetungwa na BAKIZA

  • Kamusi ya Karne ya 21 (KK21). Nairobi, Kenya

  • Kamusi Teule ya Kiswahili (KTK).

  • Kamusi Kuu ya Kiswahili (KKK). (imetungwa na BAKITA)

  • Kamusi Sanifu ya Kompyuta (KSK),

  • Kamusi Sanifu ya Biolojia, Fizikia na Kemia

  • Kamusi ya Tiba (KyT),

  • Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha

  • Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha,

  • Kamusi ya Tashbihi, Vitendawili, Milio na Milingano,

  • Kamusi ya Fasihi. Istilahi na Nadharia,

  • Kamusi ya Historia - TUKI,

  • Kamusi ya Methali,

  • Kamusi Fafanuzi ya Methali,

  • Kamusi ya Biashara na Uchumi

  • Kamusi ya Tiba (TUKI)

  • Kamusi ya Ndege kwa Picha, TUKI

  • Kamusi ya Wanyama - TUKI

  • Kamusi ya Semi,

  • Kamusi ya Semi,

  • Kamusi ya Visawe,

  • Kamusi ya Ukristo, Mkuki na Nyoka,

  • Kamusi ya Kiswahili - Kiingereza

  • Kamusi Awali ya Sayansi na Tekinolojia (

  • A Standard Swahili-English Dictionary
Mafanikio ya Kiswahili nchini yametokana na juhudi kubwa za Mwalimu Nyerere ambaye mpaka leo anakumbukwa kwa kukienzi. Katika kuunga mkono jitihada zake, Watanzania wanapaswa kujivunia juhudi hizi na kuwa mstari wa mbele katika kukiendeleza na kukitumia kama utambulisho wao ili kukieneza pamoja na kutangaza utamaduni wa taifa. Lugha ya Kiswahili.

Rais wa Tanznaia Dkt John Pombe Magufuli amekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili Afrika na Duniani. Akitambua kwamba Tanzania ndipo Kiswahili kilipoanzia na asili ya Kiswahili ni nchini Tanzania.

MWISHO
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)