MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MAADHIMISHO SIKU YA KISWAHILI DUNIANI

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
MAADHIMISHO SIKU YA KISWAHILI DUNIANI
#1
KISHINDO SHAMRASHAMRA MAADHIMISHO  SIKU YA KISWAHILI DUNIANI, TAASISI, MABARAZA NA WADAU WAJIPANGA KUADHIMISHA KILA KONA, RAIS SAMIA KUONGOZA. UCHAMBUZI WA MATUKIO 10 MUHIMU

Anaaandika PhD Dkt.Ahmad Sovu

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania-kazi iendelee

Tarehe 7, Julai itakuwa ni siku ya maadhimisho ya Kiswahili Duniani (MASIKIDU). Kiswahili kinakuwa lugha ya kwanza ya Kiafrika na ya saba duniani kutengewa siku yake mahsusi ya kuadhimishwa.

Hatua hii ilifikiwa mnamo tarehe 23/Novemba/2021 nchini Ufaransa katika mkutano wake wa 41 wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO  ya kuipa hadhi na heshima ya kuwa na siku maalum lugha ya Kiswahili kila mwaka.
Ambapo kwa mwaka  huu tarehe 7, Julai Kiswahili kitaadhimishwa kwa mara ya kwanza duniani kote.

Maadhimisho haya yamepangwa kuadhimishwa kwa kishindo na bila shaka mambo yatasena kwelikweli.

Taasisi, mabaraza, vyama vya Kiswahili, Vyuo Vikuu na wadau anuwai vimejipanga kubeleghesha maadhimisho hayo makubwa ya kidunia.

Ufuatao ni uchambuzi wa baadhi ya Taasisi namna zilivyojipanga kuenzi na kukiadhimisha Kiswahili Ulimwenguni:

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Baraza la Kiswahili la Zanzibar, (BAKIZA), na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI)

Baraza la Kiswahili kupitia Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, BAKIZA na TATAKI zimejipanga kuadhimisha siku hiyo kwa mtindo wa aina yake. Asasi hizi mama zimeandaa mfulilizo wa matukio kuanzia tarehe mosi na sio tarehe moja kama wengine wanavyopenda kuita?? hadi tarehe 7 itakapofikia kilele cha maadhimisho hayo.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa BAKITA Bi.Consolatha Mushi, amesema tarehe mosi hadi tarehe 3 kutakuwa na tamasha kabambe la utamaduni na muziki litakofanyika katika uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam. Tarehe 3 kutakuwa na usiku wa Taarab katika viunga vya fukwe za Koko.

Tarehe 4 ni matembezi ya hisani kutoka uwanja wa Mwembe Yanga hadi uwanja wa Uhuru, tarehe 5 ni siku ya mijadala kwa wanafunzi, wadau, wasanii na tarehe 6 siku ya mdahalo motomoto kuhusu namna Kiswahili kilivyosaidia ukombozi wa wa nchi mbalimbali za Kusini mwa Afrika na tarehe 7 ndio kilele ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA)

Tume hii adhimu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki nayo ipejipanga kuadhimisha siku ya tarehe 6 na 7. Maadhimisho hayo yatafanyika Zanzibar na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Dkt.Hussein Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Kongamano hilo la aina yake nalo litawajumuisha wapenzi na mashabiki wa Lugha ya Kiswahili kutoka nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Koja la Walumbi wa Kiswahili Duniani (KOWAKIDU)

Jukwaa hili lenye umaarufu mkubwa nalo limeandaa Jioni ya Mswahili tukio la jioni ya Mswahili litafanyika katika viunga vya ufukwe wa BARAKUDA Kigamboni jijini Dar es Salaam. Ambapo, wadau watajumuika pamoja kwa ajili ya chajio, kusomwa kwa tenzi, mashairi, vitushi na Burudani mbalimbali. Tukio hilo litafanyika tarehe 7 baada ya kumalizika shughuli ya maadhimisho katika ukumbi wa Julius Nyerere.

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania

Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam wao ndio hata hawakutaka kuchelewa. Walikuwa wa kwanza kufanya maadhimisho ya Kiswahili Duniani. Tarehe 29 mwezi wa 6 walifanya maadhimisho hayo ambayo yalibebwa na mada kuu

Kusambaa kwa lugha ya Kiswahili kwa Wamarekani  kulivyoweza kuimarisha uhusiano wa kiutamaduni, kielimu, kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani

Kongandao (kongamano la Mtandaoni) na kusanyiko hilo lilihudhuriwa na Bi.Consolatha Mushi Katibu Mtendaji wa BAKITA akiwa mgeni rasmi na mwenyeji wake Mheshimiwa Balozi wa Marekani Tanzania Ndugu Donald Wright. Pamoja na mambo mengine buraha ilikuwa Mheshimiwa Balozi huyo alipotongoa hotuba yake kwa Kiswahili fasaha kabisa?? Ambapo alisema

Naipongeza hatua hii ya lugha ya Kiswahili kutengewa siku yake maalum duniani. Mimi ni Balozi lakini ni mwanafunzi wa Kiswahili??

Ubalozi wa Tanzania nchini Italia
Akihojiwa na idhaa ya Redio One ya Tanzania Mheshimiwa Balozi wa Tanzania nchini Italia Ndugu Mahmoud Thabiti Kombo alisema, wao wamejipanga vilivyo kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani huko nchini Italia.

Matukio waliyoandaa ni pamoja na mada zitakazowasilishwa na walimu mbalimbali wa Kiswahili wa Tanzania  na Waitalia.
Pia, kutakuwa na maonesho ya kivazi  cha Mswahili (fashion show) ambapo zitavaliwa Kanga, seruni, vikoi, msuli, kanzu, Madera, vijora n.k.
Vilevile, maadhimisho hayo yatapambwa na vyakula vya asili, manukato ya Mswahili na mambo mengine mazuri ikiwamo kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania. Hiki ndio kishindo cha MASIKIDU.

Wadau wa Kiswahili Marekani

Wadau wa Kiswahili nchini Marekani nao wamejipanga kuibelegesha siku hii ya Kiswahili Duniani. Akisailiwa na kituo cha Redio One Bi.Zaynab Mnubi anayeishi jimbo la Michigan. Alinena kuwa wao wamejipanga kuonesha bidhaa mbalimbali za Kiswahili. Bidhaa hizo ni pamoja na makawa, mkeka wa chembe, nguo, vitabu.

Aidha, wataonesha aina mbalimbali za mitindo ya misuko ya Kiswahili. Misuko kama twende kilioni, tatu kichwa n.k✍️✍️ Shughuli hiyo itafanyika katika moja ya maktaba kubwa ya mji huo. Hiki ndi Kishindo cha Kiswahili.

Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere

Chuo hiki ambacho kinabeba jina la mwasisi wa Taifa nacho hakikubaki nyuma.

Kupitia idara yake ya Lugha na Fasihi kwa kushirikiana na uongozi wa Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili Vyuo Vikuu Tanzania chuoni hapo kiliandaa siku mahsusi ya Kiswahili tarehe 18/6/2022. Pamoja na maudhui mengine ililenga kuwaandaa Wanafunzi wanaosoma Kiswahili chuoni hapo kujipanga kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani.

Bi.Consolatha Mushi na wadau wengine wa Kiswahili kina Masau Bwire, Maulid Kambaya, Majid Mswahili na wengine tele walibeleghesha siku hiyo ambapo kaulimbiu ilikuwa Lumba Kiswahili, Jiandae kuhesabiwa na Kazi Iendelee

Chuo cha Sumait Zanzibar

Chuo cha Kumbukumbu ya Abdurahman Sumait Zanzibar nao wamejipanga kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani. Mkuu wa Idara ya lugha chuo hapo Bi.Ulfat Ibrahim amesema wao wameandaa kongandao, yaani kongamano la Kimataifa la Mtandaoni leo tarehe mosi kuelekea maadhimisho ya siku hiyo adhimu ya Kiswahili Duniani.

Mada kuu ni hadhi na fursa ya Kiswahili Duniani. Wataalamu kutoka Ujerumani, Tanzania, Marekani, Afrika Kusini, Zanzibar watashiriki. Hiki ndio kishindo cha MASIKIDU.

Chuo cha KwaZulu Natal Afrika Kusini

Nako Bondeni tayari shamrashamra zimeanza. Nimefanya mazungumzo na Mwalimu Kiswahili chuoni hapo Ndugu Edwel Dzomba anaeleza kuwa wao tayari wamekwishaandaa fulana zao kwa ajili ya MASIKIDU ili kuichagiza siku hiyo.

Hata hivyo, wameona ila utamu unoge watakuja kwenye kitovu cha Kiswahili TANZANIA kwa ajili ya kuungana na Watanzania wote kuadhimisha siku hii adhimu ya Kiswahili.
Kaka Sovu ujumbe wa watu wa 4 viongozi wa Chuo Kikuu cha Kwa Zulu Natal tunakuja kwenye MASIKIDU TANZANIA alisema Mwalimu Dzomba. Hiki ndio kishindo cha MASIKIDU.

Chuo cha Saint John's Dodoma

Makao makuu ya nchi nako kutarindima. Wao wameandaa kongandao babkubwa litakalofanyika Mtandaoni. Shabaha ya kongandao hilo ni kutathimini hali ya utafiti wa Kiswahili ilivyo. Mhadhiri mwandamizi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Dkt.Athumani Ponera anatarajiwa kuwa mtoa mada mkuu katika kongandao hilo. Mudiri wa idara ya Kiswahili chuoni hapo, Dkt.Shadidu Ndossa amesema wao wanalenga kuzitia shime taasisi, wataalamu na watafiti anuwai wa Kiswahili kuongeza bidii ya kutafiti zaidi lugha ya Kiswahili hasa ukizingatia kwa sasa Kiswahili kimebeba majukumu ya kidunia. Ametoa wito kwa wadau na wapenzi kushiriki kongandao  hilo.

Haya ni baadhi tu ya matukio muhimu ambayo yatabeleghesha maadhimisho ya siku ya Kiswahili Duniani.

Ni burdani kila pahala Kiswahili kinakwenda kuisimamisha dunia.?

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ataja faida ya siku hii kwa Tanzania

Jamadari Mkuu, Amiri jeshi mkuu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan mbali ya kuwa anatarajiwa kuongoza kilele cha maadhimisho haya, amedokeza faida za hatua hii ya Kiswahili kutengewa siku yake maalum duniani. Ambazo ni:

-Kuongeza heshima kwa Taifa letu la Tanzania ambalo ndilo chimbuko la lugha ya Kiswahili.

-Itanyanyua hadhi ya Kiswahili Tanzania ??, Afrika Mashariki na maeneo yote kinamozungumzwa.

-Kiswahili kitaendelea kusemwa kwa upana.

-Idadi ya wanaotaka kusoma Kiswahili itaongezeka.

-Itaongeza fursa zaidi kwa Watanzania

-Itaongeza utangamano wa dunia.

-Itakuza uzalendo na thamani ya lugha ya Kiswahili.
Kongole Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kwa kuienzi lugha yetu adhimu na aushi ya Kiswahili.

Nimalizie kwa maneno ya mdau aitwaye Mwebesa anasema:

macho, masikio na hisia za walimwengu (waungwana) takriban wote wanayaelekeza Afrika Mashariki na hasa nchini Tanzania kuelekea JULAI SABA. Sherehe zinaswihi ila kubwa kuliko yote leo hii na kesho tuendako Kiswahili kilete fedha, pato binafsi na la umma (serikali), fursa kwa Watanzania, Waafrika na hata Waghaibu (diaspora) wote. KISWAHILI NI MALI KULIKO ZOTE AFRIKA

MWITO
Mwisho napenda kutoa mwito kwa Watanzania wote kushiriki katika shamrashamra za maadhimisho haya hususan kwa wale walioko DSM na maeneo mbalimbali kunakofanyika maadhimisho haya.

IFIKAPO TAREHE 7/7 TUISIMAMISHE DUNIA JAPO KWA DAKIKA TANO. KILA MMOJA ASHEREKEE HATA KWA KUWEKA WIMBO WA KISWAHILI AU JAMBO LOLOTE LILE LIHUSULO KISWAHILI.

Lumba Kiswahili, Jiandae kuhesabiwa, Kazi IENDELEEE

Mwandishi ni Mhadhiri na Mshititi kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kigamboni DSM.
sovu82@gmail.com
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)