Posted by: MwlMaeda - 11-14-2021, 08:41 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
UTU
Siku hizi ukitaka kupona utapona kwa pesa,
Utakufa bure,
Kufa ni rahisi kuliko kupona!
Wakati ukipambana na afya ya mwili,
Wao hupambana na afya ya mifuko yao,
Heri ufe kuliko kudhoofisha mifukoni!
Pesa ndio huongoza hatua za binadamu,
Bila pesa hufiki popote,
Ukitaka kupumua huulizwa una bei gani?
Pesa huamua upumue au ufe,
Na ikisema kufa utakufa.
Watu hawajali vyeti na ujuzi wako,
unamjua nani ndio mpango,
Humjui mtu, rudi na vyeti vyako panya wakafanye mazalia
Ndivyo yalivyo maisha,
Kila jambo limeshapigiwa mstari,
Ukibishana nalo unagonga ngumi ukutani lazima utachubuka.
Wanasema sisi watakatifu
Hatuna chembe ya ukabila
Bado hamjatembea, Kuna watu maarufu wa kubebana.
Eti hizo ni konekisheni,
haina haja uzoefu wako,
Umesoma wapi na lini utaambiwa kajiajiri
Wanatangaza watu wajiajiri
Wao wameajiriwa
Wanabadilisha VAT hawana karaha Kama zetu
Basi wanazidi kuhubiri jiajirini!
Wengine hawana vyeo, Wala ukiranja
Ila matendo ya kinyama yamewatawala,
Hao huparamia vichanga na kuvibaka
Maagizo ya waganga wa jadi kuwa watatajirika
Wengine hawalali hupita huku na kule kuvizia mikoba ya Wanawake
Kila mtu huwaza mkono unaendaje kinywani!
Wengine hukata tamaa na kukatisha maisha yao,
Wanaona haiwezekani, Bora nife nikapumzike
Wengine wamejenga mahekalu Sasa tuwaibie watu sadaka,
Mambo ni mengi!
Wanaookota makopo,
Wanaouza miili
Watu hawajali
Wakati ukipambana umshinde adui umasikini,
Mwanga anakuwangia,
Raha yake uendelee kujitundika viraka mwilini,
Yupo radhi asilale
Usiku kucha aje akatike viuno katika chumba chako
ukiamka umetenguliwa mgongo.
Wengine huweka kando jitihada zao
Mume na mke vitani
Wapendanao huuana
Mara tunasikia mke ameuawa na mumewe
Hapo madhila yanawaangukia watoto
Baba jela mama kaburini
Watoto mtaani!
Binadamu hatupendani
Yupo radhi kumtesa mtoto wa mwenzake eti hakumzaa
Atamchubua kwa bakora
Na kumchoma Moto
bila faida ni chuki
1. Kalamu yangu nashika, kuelezea kanuni,
Hisabati kuishika, tuweze kuwa makini,
Eneo mzingo fika, nataka mufahamuni,
Kanuni kuelezea, za maumbo ya hesabu.
2. Tukianza na mraba, Duara mstatili,
Pembetatu msambamba, tuweze kuyajadili,
Na trapeza si haba, la sita si la awali,
Za maumbo ya hesabu, kanuni kuelezea.
3. Awali hapa MRABA, eneo lake sikia,
Pande mara pande kiba, jibu utajipatia,
Mzingo wake mraba, pande mara nne pia,
Kanuni kuelezea, za maumbo ya hesabu.
4. Pili ni MSTATILI, Tujue eneo hili,
Refu mara pana jali, ni rahisi afadhali,
Pana ngeza refu pili, uzidishe mara mbili,
Mzingo wake hakika, hapo unamalizia.
5. PEMBETATU pia limo, tusije kulisahau,
Nusu uzidishe kimo, zidisha kitako dau,
Utapata vyema humo, eneo sio nahau,
Kanuni za hisabati, majibu kujipatia.
6. Tuende mzingo huo, kanuni ipi jamani,
Tajumlisha vipimo, vilivyo umboni,
Ei, B, na C kikomo, jumlisha vyote hani,
Majibu kujipatia, kanuni za hisabati.
7. MSAMBAMBA eneo lake, ni urefu mara kimo,
Muhimu mzingo wake, kanuni kuijuamo,
Refu ngeza kimo chake, uzidishe kwa mbilimo,
Kanuni za hisabati, majibu kujipatia.
8. TRAPEZA fuatilia, eneo kukujulisha,
Nusu mabano sikia, A na B jumlisha,
Kisha mabano wekea, pia kimo kuzidisha,
Majibu kujipatia, kanuni za hisabati.
9. Mzingo wa Trapeza, tunakuja kukujuza,
A, B, C, na D kuweza, hizo pamoja ongeza,
Jumlisha ni ongeza, hilo muhimu kuwaza,
Kanuni za hisabati, majibu kujipatia,
10. Sasa DUARA kanuni, Ya eneo angalia,
Chukua pai jamani, kipenyo kuzidishia,
Zidisha kwa umakini, fanya kipenyo skwea,
Kanuni za hisabati, majibu kujipatia.
11. Duara mzingo wake, sio mgumu jamani,
Sikiliza kanuni yake, pai mara kipenyoni,
Naomba fanya makeke, kujikumbusha kanuni,
Kanuni za hisabati, Majibu kujipatia.
12. Anaomba msamaha, iwapo amekosea,
Mwalimu wetu Twaha, Shairi katutungia,
Kanuni kwa ufasaha, kuweza kujifunzia,
Majibu kujipatia, Kanuni za hisabati.
MANENO MBADALA
1. Ngeza = Kujumlisha
2. Pande= upande
3. Refu= urefu
Titi la mama litamu, hata likiwa la mbwa,
kiswahili naazimu, sifayo inayofumbwa,
kwa wasiokufahamu, niimbe ilivyo kubwa,
toka kama chemchemu, furika palipozibwa,
titi la mama litamu, jingine halishi hamu.
Toka kama mlizamu, juu kwa wingi furika,
Mfano wa zamzamu, yenye rutuba Makka,
Uonyeshe na muhimu, kwa wasiokutamka,
Hata waanye hamu, mapajani kukuweka,
Titi la mama litamu, jingine halishi hamu.
Lugha yangu ya utoto, hata leo nimekua,
Tangu ulimi mzito, sasa kusema najua,
Sawa na manukato, moyoni mwangu na pua,
Pori bahari na mito, napita nikitumia,
Titi la mama litamu, jingine halishi hamu.
Sababu ya kupenda, lafidhi yangu natoa,
Natumia toka ganda, na kiini chanelea,
Lugha nyingine nakonda, wakati nikitumia,
Mbele nikitaka kwenda, ulimi wangu hukwaa,
Titi la mama litamu, jingine halishi hamu.
Ujira mwema napewa, kwa lugha za kigeni,
Na bidii natoa, nyingi nisiwekwe chini,
Lakini juu ya haya, nawaza mwangu moyoni,
Mwasi wa kutumia, lugha yake maskini,
Titi la mama litamu, jingine halishi hamu.
Usemi na akili, nip ambo vikilingana,
Kwa lugha ya Kiswahili, sina cha kunibana,
Kama natoa kauli, na fikira hufanana,
Lugha nyingine bahili, ujima kwangu hazina,
Titi la mama litamu, jingine halishi hamu.
Lugha kama kiarabu, kirumi na kingereza,
Kwa wingi zimeratibu, mambo ya kupendeza,
Na mimi nimejaribu, kila hali kujifunza,
Lakini sawa na bubu, nikizisema nabezwa,
Titi la mama litamu, jingine halishi hamu.
Posted by: MwlMaeda - 11-12-2021, 10:04 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
WALIMU SHIKENI HAYA
walimu zingatieni, kushika habari hizi,
mwenendo mwema shikeni, kuifanya yenu kazi,
tena kuweni makini, hasa kwenye siku hizi,
leo nawambia wazi, hasira zipunguzeni.
Leo nawaambia wazi, ushauri ushikeni,
atayeona upuzi, huyo bwana muacheni,
siku madhara kihozi, nitajiweka pembeni.
Hasira zipunguzeni, leo nawambia wazi.
Bakora sawa chapeni, Ila siwe kwa mashazi,
Si kucharaza mwilini, ukamzidisha dozi,
tabia hiyo acheni, huu utungo ni kozi,
Leo nawambia wazi, hasira zipunguzeni.
Jua wageuka mbuzi, kujitia hasirani,
kujiuzuia huwezi, upige namna gani,
sawa amekosa kwizi, lake kosa tathimini,
hasira zipunguzeni, leo nawambia wazi.
Kiwa si leo mwakani, taniweka kumbukizi,
Kuna huyu Athumani, yupo jela siku hizi,
niliposema acheni, yeye kajitia chizi,
hasira zipunguzeni, leo nawambia wazi.
chanzo Cha habari hizi, sijui likuwa nini,
Kama anapiga mwizi, huku kiwa darasani,
kupumua akasizi, mwanafunzi kijijini,
hasira zipunguzeni, Leo nawambia wazi.
Athumani matatani, huku atokwa machozi,
akatiwa gerezani, mwalimu loenda kozi,
kifungo cha maishani, kutoka huko hawezi,
Leo nawambia wazi, hasira zipunguzeni.
Kuna walimu jamani, zao kauli maudhi,
kumwita mtoto nyani, au ngedere na chizi,
Hilo halileti shani, ulienda wapi kozi?
leo nawambia wazi, hasira zipunguzeni.
Kumwambia mwanafunzi, maneno ya kisirani,
kusema hili hawezi, unamtia tamani,
Ila waambie wazi, jitihada ongezeni,
hasira zipunguzeni, Leo nawambia wazi.
Sasa natoka shuleni, pokeeni yangu dozi,
ingawa yangu kwinini, chungu peke huimezi,
naomba badilikeni, walimu muwe walezi,
Leo nawambia wazi, hasira zipunguzeni.
Mama yetu - Kiswahili anayetulea kwa hali na mali amepata pigo kwa kufa mmoja wa watoto wake - Profesa Pete Mhunzi.
Nilifahamiana na Profesa Pete Mhunzi, aliyelibadili kuwa la Kiswahili jina Peter Smith zaidi ya miaka 30 pale alipozuru Tanzania na kutembelea ofisi ya Waswahili - Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA), eneo la Anartoglo, Mnazimmoja, Dar es Salaam mwishoni mwa miaka ya 80.
Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kumuona Mmarekani mwenye asili ya Afrika aliyempenda Mama Kiswahili na kumtendea haki baada ya kukutana na John Mtembezi (Bwana Punda).
Profesa Pete Mhuzi alipenda sana kujifunza mambo mbalimbali kuhusu Kiswahili na Taaluma zake na tulikuwa na vikao maalum, tukiwa na gwiji la Kiswahili Marehemu Mzee Hamis Akida (Allaah Amrehemu), pale nyumbani kwa mwanadada (bila shaka sasa ni Bibi mwenye wajukuu) Irene (aliyekuwa mfanyakazi wa Kampuni ya TPH - Tanzania Publishing House, eneo la Kota za Misheni, Kariakoo, Dar es Salaam.
Anapofika Profesa Pete Mhuzi huwa ni hekaheka nguo kuchanika kwa waswahili waliokuwa na raghba ya kufanikisha ziara yake ya utalii wa Kiswahili.
Hapa namkumbuka Kaka Mswahili Mohamed Mwinyi (Bwana Jasho), Marehemu Ramadhani Stumai (Allaah Amrehemu), Marehemu Sihiyana Swalehe Mandevu (Mtenda Mema) na mradi wake wa alfabeti za Kiswahili zinazowakilisha vinavyopatikana Uswahilini kama upawa, mwiko, chungu na kadhalika.
Huchoki unapomsikiliza Mswahili Pete Mhunzi na juhudi zake za kumuenzi Mama Kiswahili.
Kuondoka kwake ni pigo kubwa kwa Mama yetu na ukoo mzima wa Mama Kiswahili.
Mama Kiswahili ana huzuni kubwa anapokumbuka maumivu ya tumbo la udele linalouma mno.
Makiwa Mama Kiswahili!
Makiwa watoto wa Mama Kiswahili!
Tunamuomba Mola wetu Ampokee.
Bwana Ametoa, Bwana Ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe.