Posted by: MwlMaeda - 01-03-2022, 08:10 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
U N D U G U **** 1. Ndugu ni yule mwenzako, aliye karibu yako, hata akitoka huko, kunakoitwa Bamako, huyo naye nyota yako. 2. Kama ni Mmarekani, ni Mwafurika kusini, asili ye Warabuni, ama Mwese Ubendeni, wote wagee thamani. 3. Maadamu mshirika, mpo pamoja hakika, kokote anakotoka, kwako atahitajika, mfaane bila shaka. 4. Anayekukaribia, maisha mkachangia, pamwe mkifurahia, pamoja mkaumia, huyo ni ndugu sikia. 5. Nina ndugu siwaoni, nili’shi nao zamani, daima wako moyoni, hawatoki fikarani, kuwaona natamani. 6. Ndugu hao walikuwa, toka pande maridhawa, za mabara na visiwa, vema walinielewa, wakin’jali sawasawa. 7. Kwao somo nalipata, la busara nikachota, kuwa watu wote nyota, ‘sijali wanakotoka, sote ni ndugu hakika. 8. Rangi ya ntu ‘siijali, ukabila usijali, udini usiujali, kuwa ni ‘mtu’ ujali, akubariki Jalali. **** Rwaka rwa Kagarama, (Mshairi Mnyarwanda) Wilaya ya Nyagatare Jimbo la Mashariki,RWANDA.
Posted by: MwlMaeda - 01-03-2022, 08:02 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
Yana ufupi maisha, si marefu ja zamani
Muda wake wa kuisha, u karibu na mwanzoni
Yanayotushughulisha, si mambo yenye thamani
Tuipatapo nafasi, tucheke tungali hai
Dunia yataabisha, asiyejuwa ni nani?
Mambo ya kutishatisha, ndiyo mengi duniani
Hayo hutuhuzunisha, tukawa wenye huzuni
Basi ijapo nafasi, tucheke tungali hai
Mambo ya kufurahisha, sasa hayaonekani
Mengi hututia presha, tudhoofike milini
Hali yanazidunisha, japo tayari zi duni
Iwapo moja nafasi, tucheke tungali hai
Watu hujiongelesha, tupishanapo njiani
Thubutu kuwatingisha, tatukanwa juu chini
Hili linathibitisha, tumejawa visirani
Nduyangu kwenye nafasi, tucheke tungali hai
Dhiki zetu zimetosha, na huu umasikini
Si vyema kuyaamsha, mengine yaso maani
Tukawa twajinunisha, na kuvunja ujirani
Tusipoteze nafasi, tucheke tungali hai
Aliyeukamilisha, ujamaa ni Manani
Kutaka kuuangusha, ni kuzikiuka dini
Si vyema kujitunisha, na kupimana uzani
Bali iwapo nafasi, tucheke tungali hai
Muda tukishafikisha, wa kurejea nyumbani
Juweni hatutovusha, japo sekunde sitini
Wenzetu watatuosha, tuingie kaburini
Ombi palipo nafasi, tucheke tungali hai
Utungo naukatisha, peni naweka mezani
Kama nilijikosesha, nakuomba samahani
Japo hukunijulisha, kosa nikalibaini
Ni finyu hii nafasi, tucheke tungali hai
Elenzian_jk(Kalamu Ndogo)
elenzianjohns@gmail.com
+255625947688| 0655210909
Julai 26, 2019
Dar es salaam-Tanzania
Posted by: MwlMaeda - 01-03-2022, 07:57 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
Kalamu ninaandika,
Mioyo ya Wanawake, mwenzenu yanishangaza
Ina mapenzi lukuki, na huba za kutosheza
Kwa hili naipa heko, tena ninaipongeza
Mola ameiruzuku.
Ukweli usio shaka,
Mioyo ya Wanawake, Mungu ilimpendeza
Kuipunguzia chuki, na upendo kuongeza
Itutoe sononeko, pale linapotokeza
Kwenye za taabu siku.
Hili ninalianika,
Mioyo ya Wanawake, hodari kwa kuuguza
Hufanya kile na hiki, uwelewo kuupoza
Taabu na masumbuko, yenyewe huyapunguza
Na kurejesha shauku.
Kusema nalazimika,
Mioyo ya Wanawake, tulizo hututuliza
Japokuwa zao haki, sisi huzikandamiza
Hutupatia vicheko, japo tunaiumiza
Kwa mchana na usiku.
Tena nina uhakika,
Mioyo ya Wanawake, kwa kujali yaongoza
Kwenye faraja na dhiki, hutuondoshea kiza
Tuibebeni kwa mbeko, tuache kuipuuza
Na tuzo tuitunuku.
Elenzian_jk(Kalamu Ndogo) elenzianjohns@gmail.com
+255625947688| 0655210909
Julai 18, 2019
Dar es salaam-Tanzania
Posted by: MwlMaeda - 01-03-2022, 07:55 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
Kwaye mgawa bahati, ninaanza kuandika
Anitoe gatigati, neno liwe na baraka
Kila jambo na wakati, hakwepi aloumbika
Leo nimemkumbuka SHABANI BIN ROBERTI.
SHABANI BIN ROBERTI, leo nimekumbuka
Menoneye ni yakuti, hayawezi kunitoka
Hakuweka utondoti, kila alicho andika
Leo nimemkumbuka SHABANI BIN ROBERTI.
Mola huwa hamuwati, katika zake nyaraka
Aliusi kila goti, hakupata kupituka
Japo kafikwa mauti, nabati kisha atika
Leo nimemkubuka SHABANI BIN ROBERTI.
Mpambo wa mabanati, kiswahili kakivika
Kama wambeja na koti, vile wanavyo jivika
Sasa kinapewa hati, SHABANI kishaondoka
Leo nimemkumbuka SHABANI BIN ROBERTI.
Ulimliza wakati, nguvu zinavyokatika
Kutengwa na mabanati, matozi yalimtoka
Ujana jinale hati, haiwezi kupauka
Leo nimemkumbuka SHABANI BIN ROBERTI.
Akampamba na Siti, binti Sadi msifika
Alojaliwa sauti, iwezayo towa nyoka
Ni mja wa hasanati, kioo kiso vunjika
Leo nimemkumbuka SHABANI BIN ROBERTI.
Kilio cha zaujati, SHABANI kilimfika
Akaziandika beti, Amina ameondoka
Huwezi baki sukuti, machozi yatamwagika
Leo nimemkubuka SHABANI BIN ROBERTI.
Ujane hakwenda shoti, aliuona mashaka
Akaipaza sauti, malumbano yakazuka
Mambo yakawa halati, tungo zilimiminika
Leo nimemkubuka SHABANI BIN ROBERTI. Adili zakwe swifati, na akiraba kandika
Kahadithi aradhati, manyani wakitabika
Ni utungo madhubuti,kichwani siwakutoka
Leo nimemkumbuka SHABANI BIN ROBERTI
Kwa hapa kaditamati, kalamu naifutika
Nachelea utondoti, mbele nisende potoka
Alimopita ROBERTI,nyayo hazitofutika
Leo nimemkumbuka SHABANI BIN ROBERTI
Posted by: MwlMaeda - 01-03-2022, 07:50 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
Kunani huko jamani, nauliza nambieni,
Kunani humo vichwani, mtoapo mawazoni,
Kunani humo vitini, enzi yenu mketini,
Kwa kiti Cha kuzunguka, ninauliza kunani?
Kunani majaridani, mema’nu ndiyo foleni,
Kunani huko jamvini, vibaya vi daharauni,
Kunani mwenu kinywani, vizuri vi ahadini,
Kwa kiti cha kuzunguka, ninauliza kunani?
Kunani mkutanoni, mwatuzuga akilini,
Kunani mwenu machoni, jema mbona silioni,
Kunani kwenu ndimini, au nd’o sumu sirini,
Kwa kiti Cha kuzunguka, ninauliza kunani?
Kunani kwenu nyumbani, mbona njaa siioni,
Kunani kwetu jamani, mbona Kama jalalani,
Kunani barabarani, Shida kwenu sizioni,
Kwa kiti Cha kuzunguka, ninauliza kunani?
Kunani kwenu tumboni, kwani yamevimbia’ni,
Kunani kwangu mwilini, kwani ninakondeani,
Kunani kwangu jamani, Uhuru u mafichoni,
Kwa kiti cha kuzunguka, ninauliza kunani?
Kwa sita natamatiya, kukwea tena siwezi,
Haya nilo washushiya, si madafu ila nazi,
Usojuwa vumiliya, utapofika ulizi,
Usiyejuwa matozi, muole anayeliya.
‘Kinirudisha ujana, vema nitautumiya.
Sikuwi mvivu tena, yalopita najutiya.
Nitachapa kazi sana, nguvu nikizitumiya.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
Shuleni nikirudiya, masomo sin’tachezeya.
Hivi ninashuhudiya, baba alon’elezeya.
Kuwa somo n’kichukiya, mbele sintaendeleya.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
Sasa nimedhoofika, mwili wote watetema.
Moyo kama wapasuka, tumbo kichwa vyaniluma.
Ni mapombe yaninyuka, na tumbaku niso’koma.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
Rai za wangu wazazi, miye nilipuuziya.
Mwalimu mwema mlezi, yake sikuzingatiya.
Sasa ndiyo namaizi, yote waloniwambiya.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
Uliopita mlongo, mahela nililokota.
Yote nikanyweya gongo, sikujenga banda hata.
N’tatumiya kwa malengo, leo pesa nikipata.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
Nguvu za mwili zaisha, mawazo ndo yapevuka.
Ninaelewa maisha, nimefika mingi miaka.
Leo najisahihisha, bila hata pa kushika.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIYA VEMA.
Hivi ndiyo naelewa, ma’na ya kuwajibika.
Niliishi nikilewa, yangu vilewo kusaka.
Hadi sasa ninakuwa, jamii imenichoka.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
Nilikuwa sikujali, hata weye Mu’mba wangu.
Nikipuuza kauli, inayomtaja Mungu.
Sasa ‘meanza kuswali, n’kiwa na mwingi uchungu.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
Vema nitautumiya, ujana nikiurudi.
Mno nitakazaniya, kazini kuwa mshindi.
Maisha ‘menipatiya, masomo mengi zaidi.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
”Ni kama moshi ujana, uk’enda h’urudi chini”.
Ni tamko alinena, mshairi Shaabani,
Ila kwako Maulana, nini hakiwezekani?
NIRUDISHIE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
Hapa nimeufikiya, wa thenashara ubeti.
Mola umeyasikiya, maombi yangu ya dhati.
Jawabu ‘tanipatiya, naandaa mikakati.
NIRUDISHIYE UJANA, NITAUTUMIA VEMA.
************** Rwaka rwa Kagarama, (Mshairi Mnyarwanda)
Jimbo la Mashariki, Wilaya ya Nyagatare,RWANDA.
HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO ' JAALA', 'JALIA' 'JALI.A/JAALI.A' na 'MAJALIWA'
Neno jaala[ Ngeli: i-/i-] katika lugha ya Kiswahili ni nomino yenye maana ya' mambo yafanyikayo kwa mapenzi/uwezo wa Mwenyezi Mungu'.
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili jaala (soma: ja-a-la جعل) ni kitenzi cha Kiarabu chenye maana zifuatazo:
1. Amefanya kitu fulani kiwepo.
2. Ametoa kitu kumpa mtu mwengine.
3. Ameanza jambo fulani.
4. (Kwa Mwenyeezi Mungu tu) Ameumba.
5. Ametengeneza.
Neno jalia[ Ngeli: a-] katika lugha ya Kiswahili ni kisawe cha neno jalali [ Ngeli: a-] lenye maana ya 'jina la kumtaja Mwenyeezi Mungu kwa sifa yake ya kuwa utukufu mwingi'.
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili jalali (soma: jalaalun/jalaalan/jalaalin جلال) ni nomino ya Kiarabu yenye maana zifuatazo:
1. Utukufu. Mwenyeezi Mungu hutajwa kuwa Dhul Jalaali ذو الجلال mwenye utukufu.
2. -enye cheo/hadhi kubwa.
3. Kilicho kikubwa zaidi.
Maneno jali.a/jaali.a[ Vitenzi Elekezi ] katika lugha ya Kiswahili vina maana ya 'fanya uwezekano, saidia, wezesha: Mwenyeezi Mungu akitujalia/akitujaalia uhai tutaonana.
Neno hili linaponyambuliwa tunapata vitenzi: jaalika, jaalisha na jaaliwa.
Neno majaliwa[ Ngeli: ya-/ya-] katika lugha ya Kiswahili ni nomino yenye maana ya' mambo yafanyikayo kwa uwezo/mapenzi ya Mwenyezi Mungu'.
Maneno ' jaala ' na ' majaliwa ' ni visawe.
Neno ' majaliwa ' halina mfano wake kimatamshi katika lugha ya Kiarabu bali yumkini limebuniwa kutokana na nomino ' jaala ' au kitenzi ' jaalia/jaaliwa'.
Kitenzi ' jali.a/jaali.a' kinamhusu Mwenyeezi Mungu tu kwa maana ya kumpa mtu uwezo wa kupata au kuweza kufanya jambo fulani.
Kinachodhihiri ni kuwa neno jaala ( soma: ja-a-la جعل) ambalo ni kitenzi katika lugha ya Kiarabu lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno jaala limekuwa nomino kwa maana ya 'mambo yafanyikayo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu'.
Kiujumla, maneno yote haya hayakuepukana na maana zake katika lugha ya asili - Kiarabu.
Posted by: MwlMaeda - 01-03-2022, 07:16 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
TEZI NA OMO
Waume na nisiwani, duniyani tungalimo,
Hayano hatuyaoni, tunaifunga midomo,
Tumemuwacha Manani, tushenda tezi na omo,
Tushenda tezi na omo, naturejee ngamani.
Malezi ya kizamani, kichwani tena hayamo,
Wanetu ndiyo waneni, kila jambo wao wamo,
Ushapotea mzani, tushenda tezi na omo,
Tushenda tezi na omo, naturejee ngamani.
Mashibu tena sioni, kwa walozidi makamo,
Tumekuwa hayawani, ubinadamu haumo,
Zimetupotea soni, tushenda tezi na omo,
Tushenda tezi na omo, naturejee ngamani.
Tu asira wa shetani, kundini mwake tumumo,
Kama donda la kichani, hatulioni lilimo,
Zimeviza zetu mboni, tushenda tezi na omo,
Tushenda tezi na omo, naturejee ngamani.
Mvuli kuwekwa ndani, duniya yenda ukomo,
Akajivika gauni, ja banati mtazamo,
Hatuchukii moyoni, tushenda tezi na omo,
Tushenda tezi na omo, naturejee ngamani.
Kengele afungwe nani, tuhumu kama hatumo,
Tumeingia shimoni, kwakukosa misimamo,
Kitanzi kipo shingoni, tushenda tezi na omo,
Tushenda tezi na omo, naturejee ngamani.
Wakatabahu matini, huchezi bila mfumo,
Aliye mkongwe Nyani, amekwepa nyingi fumo,
Haitwishi mitihani, tushenda tezi na omo,
Tushenda tezi na omo, naturejee nhamani.
MKANYAJI
HAMISI A.S KISSAMVU
0715311590
kissamvujr@gmail.com
kutoka (Baitu shi’ri)