SHAIRI : TUCHEKE TUNGALI HAI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI : TUCHEKE TUNGALI HAI (/showthread.php?tid=1940) |
SHAIRI : TUCHEKE TUNGALI HAI - MwlMaeda - 01-03-2022 Yana ufupi maisha, si marefu ja zamani Muda wake wa kuisha, u karibu na mwanzoni Yanayotushughulisha, si mambo yenye thamani Tuipatapo nafasi, tucheke tungali hai Dunia yataabisha, asiyejuwa ni nani? Mambo ya kutishatisha, ndiyo mengi duniani Hayo hutuhuzunisha, tukawa wenye huzuni Basi ijapo nafasi, tucheke tungali hai Mambo ya kufurahisha, sasa hayaonekani Mengi hututia presha, tudhoofike milini Hali yanazidunisha, japo tayari zi duni Iwapo moja nafasi, tucheke tungali hai Watu hujiongelesha, tupishanapo njiani Thubutu kuwatingisha, tatukanwa juu chini Hili linathibitisha, tumejawa visirani Nduyangu kwenye nafasi, tucheke tungali hai Dhiki zetu zimetosha, na huu umasikini Si vyema kuyaamsha, mengine yaso maani Tukawa twajinunisha, na kuvunja ujirani Tusipoteze nafasi, tucheke tungali hai Aliyeukamilisha, ujamaa ni Manani Kutaka kuuangusha, ni kuzikiuka dini Si vyema kujitunisha, na kupimana uzani Bali iwapo nafasi, tucheke tungali hai Muda tukishafikisha, wa kurejea nyumbani Juweni hatutovusha, japo sekunde sitini Wenzetu watatuosha, tuingie kaburini Ombi palipo nafasi, tucheke tungali hai Utungo naukatisha, peni naweka mezani Kama nilijikosesha, nakuomba samahani Japo hukunijulisha, kosa nikalibaini Ni finyu hii nafasi, tucheke tungali hai Elenzian_jk(Kalamu Ndogo) elenzianjohns@gmail.com +255625947688| 0655210909 Julai 26, 2019 Dar es salaam-Tanzania |