SHAIRI : SHABANI BIN ROBERTI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI : SHABANI BIN ROBERTI (/showthread.php?tid=1938) |
SHAIRI : SHABANI BIN ROBERTI - MwlMaeda - 01-03-2022 Kwaye mgawa bahati, ninaanza kuandika Anitoe gatigati, neno liwe na baraka Kila jambo na wakati, hakwepi aloumbika Leo nimemkumbuka SHABANI BIN ROBERTI. SHABANI BIN ROBERTI, leo nimekumbuka Menoneye ni yakuti, hayawezi kunitoka Hakuweka utondoti, kila alicho andika Leo nimemkumbuka SHABANI BIN ROBERTI. Mola huwa hamuwati, katika zake nyaraka Aliusi kila goti, hakupata kupituka Japo kafikwa mauti, nabati kisha atika Leo nimemkubuka SHABANI BIN ROBERTI. Mpambo wa mabanati, kiswahili kakivika Kama wambeja na koti, vile wanavyo jivika Sasa kinapewa hati, SHABANI kishaondoka Leo nimemkumbuka SHABANI BIN ROBERTI. Ulimliza wakati, nguvu zinavyokatika Kutengwa na mabanati, matozi yalimtoka Ujana jinale hati, haiwezi kupauka Leo nimemkumbuka SHABANI BIN ROBERTI. Akampamba na Siti, binti Sadi msifika Alojaliwa sauti, iwezayo towa nyoka Ni mja wa hasanati, kioo kiso vunjika Leo nimemkumbuka SHABANI BIN ROBERTI. Kilio cha zaujati, SHABANI kilimfika Akaziandika beti, Amina ameondoka Huwezi baki sukuti, machozi yatamwagika Leo nimemkubuka SHABANI BIN ROBERTI. Ujane hakwenda shoti, aliuona mashaka Akaipaza sauti, malumbano yakazuka Mambo yakawa halati, tungo zilimiminika Leo nimemkubuka SHABANI BIN ROBERTI. Adili zakwe swifati, na akiraba kandika Kahadithi aradhati, manyani wakitabika Ni utungo madhubuti,kichwani siwakutoka Leo nimemkumbuka SHABANI BIN ROBERTI Kwa hapa kaditamati, kalamu naifutika Nachelea utondoti, mbele nisende potoka Alimopita ROBERTI,nyayo hazitofutika Leo nimemkumbuka SHABANI BIN ROBERTI MKANYAJI HAMISI A.S. KISSAMVU 0715311590 kissamvujr@gmail.com kutoka(Baitu Shi’ri MABIBO -DAR ES SALAAM |