HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO 'ABTADI' NA 'ABTALI'
Neno *abtadi* katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo:
1. *Nomino: [Ngeli: a-/wa-]* shujaa wa vita.
2. *Kitenzi elekezi* fanya jambo kwa mara ya kwanza ili wengine wafuate; tangulia, anza.
3. *Kitenzi elekezi* alika kitu au shughuli *_Ninaabtadi safari yangu kwa kumuomba Mola; Bismillaahi n'abtadi*_ ninaanza kwa jina la Mwenyeezi Mungu.
Katika lugha ya Kiarabu, neno *abtadi* ni kitenzi cha Kiarabu *abtadiu ابتدئ* chenye maana ya 'ninaanza'.
Neno *abtali* katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo:
1. *Nomino: [Ngeli: a-/wa-, wingi: maabtali]* yenye maana ya askari au mpiganaji ambaye ni shujaa na mzoefu wa kupigana.
2. *Nomino: [Ngeli: i-/zi-]* yenye maana ya *wapiganaji.*
Katika lugha ya Kiarabu, neno *abtali* (soma: *abtwaalun/abtwaalan/abtwaalin ابطال* ) ni nomino iliyo wingi wa neno la Kiarabu *batwalun/batwalan/batwalin بطل* lenye maana zifuatazo:
1. *Batwalun fil Maarik* *بطل في المعارك* askari wa mstari wa mbele vitani; shujaa.
2. Mshindi wa kwanza katika mashindano ya michezo kama ndondi, riadha, mieleka na mingineyo.
3. Muhusika mkuu katika riwaya, tamthilia au filamu.
Kinachodhihiri ni kuwa neno *abtadi* linalotokana na kitenzi cha Kiarabu *abtadiu ابتدئ)* *ninaanza*, lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa *abtadi* maana yake katika lugha ya asili - Kiarabu haikubadilika ingawa iliongezwa maana ya kufanya jambo kwa mara ya kwanza ili wengine wafuate.
Kuhusu neno abtali (soma: *abtwaalun/abtwaalan/abtwaalin ابطال*) lenye maana ya wapiganaji nalo halikuacha maana yake katika lugha ya asili - Kiarabu ingawa lilipewa maana mpya ya askari au mpiganaji ambaye ni shujaa na mzoefu wa kupigana na kuziacha maana zingine katika lugha ya asili - Kiarabu.
Ni muhimu kuzingatia kuwa neno *abtadi* *ninaanza* limesajiliwa kamusini kwa maana ya *shujaa wa vita* na jambo hili yumkini ni kosa lililotokana na kukaribiana kwa maneno *abtadi* na *abtali* .
Neno *rubaa* katika lugha ya Kiswahili ni *nomino: [Ngeli: i-/zi-]* yenye maana zifuatazo:
1. Jumuiya ya watu wanaoishi na wanaofanya kazi pamoja kwa sababu wana uhusiano fulani unaowaunganisha; Watu wengi wanaofanya kazi pamoja kwa kuunganishwa na uhusiano fulani.
2. Kitendo cha kuweka mguu mmoja juu ya mwengine hali ukiwa umekaa.
*Mfano* : Mgeni alipopewa kiti alikaa rubaa.
3. Uwanja au uga wa shughuli fulani.
*Mfano* : Jangala siku hizi ni maarufu katika rubaa za michezo.
4. Kikundi cha askari wanaopangiwa na kutekeleza majukumu yao chini ya kiongozi mmoja.
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *rubaa*( *soma: rubaau/rubaa-a رباع )* ni nomino ya Kiarabu yenye maana ya kukariri namba 4: nne nne/wanne wanne. Kwa mfano: *Hum Jaauu Rubaa-a هم جاءوا رباعا* Wamekuja wanne wanne.
Kinachodhihiri ni kuwa neno la Kiarabu *rubaa-a رباعا* lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa nomino ya Kiswahili ' *rubaa* ' lilibeba maana mpya.
1. Nomino: [Ngeli: i-/zi-] idadi maalumu ya wajumbe inayoruhusu mkutano kufanyika na uamuzi kuweza kutolewa katika vikao.
5 . Nomino: [Ngeli: i-/i-] uchache wa watu au vitu.
Neno akdi katika lugha ya Kiswahili Nomino: [Ngeli: i-/zi-] yenye maana ya makubaliano rasmi ya watu kuishi pamoja wakiwa mume na mke.
Katika lugha ya Kiarabu, maneno akidi na akdi ni nomino inayotokana na neno aqdun/aqdan/aqdin عقد) lenye maana zifuatazo:
1. Ahadi; makubaliano ya kufunga ndoa au kufanya biashara.
2. Mkataba kama vile mkataba wa kufanya kazi kwa ujira fulani au kwa kujitolea.
3. Makumi: Hesabu inayojumuisha kumi, ishirini hadi tisini.
4. Suluhu; mapatano baina ya waliohasimiana.
5. Kifungu cha maneno kinachoashiria kukubaliana, kama vile kusema: Nimekuoza...., Nimenunua kutoka kwako.
Kinachodhihiri ni kuwa maneno akidi na akdi yanatokana na neno la Kiarabu aqdun/aqdan/aqdin عقد) na neno hili lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa akidi na akdi lilichukua kutoka Kiarabu maana ya makubaliano rasmi ya wawili kuishi pamoja wakiwa mume na mke na kubeba maana mpya.
KWA HESHIMA YA DAKTARI SOVU NATEKELEZA AMRI YA MKUBWA WANGU...
HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO ' SUGAR/SUKARI' NA 'KAGERA'
Neno sugar/sukari katika lugha ya Kiswahili neno sukari ambalo ni tafsiri ya neno la Kiingereza 'sugar' lina maana zifuatazo:
1. Nomino: [Ngeli: i-/zi-] chembechembe ndogo aghalabu zenye ladha ya utamu zinazotiwa aghalabu kwenye chai au kwenye kitu kingine pale unapohitaji ladha ya utamu kwa mfano kwenye keki, juisi au maandazi.
2. Ladha ya utamu wa kitu.
Kuna msemo : Sihadaike na rangi tamu ya chai ni sukari : usipumbazwe au kuhadaika na mapambo au uzuri wa nje wa kitu, kilicho muhimu ni faida au uzuri wa ndani/uzuri halisi.
Katika lugha ya Kiarabu, mzizi SKR unatengeneza maneno matatu ambayo ni nomino nayo ni sukkarun/sukkaran/sukkarin, sakkarun/sakkaran/sakkarin, sikrun/sikran/sikrin سكر yenye maana zifuatazo:
1. Kila chenye kulewesha; kilevi; pombe.
2. Siki.
3. Kitu kitamu kinachotokana na juisi ya miwa; kitu kitamu kinachopatikana kwenye matunda mbalimbali.
4. Kilevi kinachopoteza akili kinapotiwa katika kinywaji.
5. Hali inayomfanya mtu kuhamasika kufanya jambo bila ya kutafakari hatima yake; jeuri.
Kuna msemo : Akhadhahu Sukkarush Shabaab أخذه سكر الشباب imemchukua sukari (jeuri) ya ujana; Sukkarul Maal سكر المال, Sukari (jeuri) ya mali; Sukkarus Sultwaan,سكر السلطان Sukari (jeuri) ya Utawala.
6. Kingo ya mto na mfano wake.
Neno kagera katika lugha ya Kiswahili ni jina la kipekee lenye asili ya Kibantu lenye maana ya utelezi, na pia kitenzi chenye maana ya ameteleza.
Neno Kagera limekuwa maarufu kwa kutumiwa kutambulisha mto maarufu 'Mto Kagera', vita vilivyopiganwa baina ya Tanzania na Uganda wakati wa utawala wa Iddi Amini 'Vita vya Kagera' na mkoa maarufu magharibi mwa Tanzania 'Mkoa wa Kagera'.
Wana-Etimolojia wa Kiarabu wanakiri kuwa neno 'sukari' (soma: sukkarun/sukkaran/sukkarin سكر) wameliarabisha baada ya kulikopa kutoka Kiajemi.
Kinachodhihiri ni kuwa maneno haya SUGAR/SUKARI na KAGERA yanabeba uwezo maalumu wa kulewesha na pia kumfanya mtu aangukie pua kutokana na utelezi.
Shukran sana.
Neno Maalumu: Watani waniwie radhi, nimetumwa na wakubwa zangu. Chambilecho, mshenga hauwawi.
Neno rakadha katika lugha ya Kiswahili ni nomino: [Ngeli: i-/zi-] yenye maana zifuatazo:
1. Hali ya kung'ang'ania jambo: Fanyia rakadha.
2. Ulazima wa/shurutisho la kukamilisha jambo.
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili rakadha( soma: rakadhwa ركض ) ni kitenzi cha Kiarabu chenye maana zifuatazo:
1. Amekwenda mbio.
2. Amekita mguu chini.
3. Ametetea.
4. Amempiga mnyama mbavuni ili kumuhimiza aongeze mwendo.
5. Amerusha mshale.
6. Nyota zimetembea angani.
7. Ndege amepigapiga mabawa yake.
8. Amekimbia.
Kinachodhihiri ni kuwa kitenzi cha Kiarabu rakadhwa ركض kilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa nomino ya Kiswahili ' rakadha ' lilibeba maana mpya ya hali ya kung'ang'ania jambo na ulazima wa/shurutisho la kukamilisha jambo.