ETIMOLOJIA YA MANENO 'ABTADI' NA 'ABTALI' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA MANENO 'ABTADI' NA 'ABTALI' (/showthread.php?tid=2380) |
ETIMOLOJIA YA MANENO 'ABTADI' NA 'ABTALI' - MwlMaeda - 01-30-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO 'ABTADI' NA 'ABTALI' Neno *abtadi* katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. *Nomino: [Ngeli: a-/wa-]* shujaa wa vita. 2. *Kitenzi elekezi* fanya jambo kwa mara ya kwanza ili wengine wafuate; tangulia, anza. 3. *Kitenzi elekezi* alika kitu au shughuli *_Ninaabtadi safari yangu kwa kumuomba Mola; Bismillaahi n'abtadi*_ ninaanza kwa jina la Mwenyeezi Mungu. Katika lugha ya Kiarabu, neno *abtadi* ni kitenzi cha Kiarabu *abtadiu ابتدئ* chenye maana ya 'ninaanza'. Neno *abtali* katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. *Nomino: [Ngeli: a-/wa-, wingi: maabtali]* yenye maana ya askari au mpiganaji ambaye ni shujaa na mzoefu wa kupigana. 2. *Nomino: [Ngeli: i-/zi-]* yenye maana ya *wapiganaji.* Katika lugha ya Kiarabu, neno *abtali* (soma: *abtwaalun/abtwaalan/abtwaalin ابطال* ) ni nomino iliyo wingi wa neno la Kiarabu *batwalun/batwalan/batwalin بطل* lenye maana zifuatazo: 1. *Batwalun fil Maarik* *بطل في المعارك* askari wa mstari wa mbele vitani; shujaa. 2. Mshindi wa kwanza katika mashindano ya michezo kama ndondi, riadha, mieleka na mingineyo. 3. Muhusika mkuu katika riwaya, tamthilia au filamu. Kinachodhihiri ni kuwa neno *abtadi* linalotokana na kitenzi cha Kiarabu *abtadiu ابتدئ)* *ninaanza*, lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa *abtadi* maana yake katika lugha ya asili - Kiarabu haikubadilika ingawa iliongezwa maana ya kufanya jambo kwa mara ya kwanza ili wengine wafuate. Kuhusu neno abtali (soma: *abtwaalun/abtwaalan/abtwaalin ابطال*) lenye maana ya wapiganaji nalo halikuacha maana yake katika lugha ya asili - Kiarabu ingawa lilipewa maana mpya ya askari au mpiganaji ambaye ni shujaa na mzoefu wa kupigana na kuziacha maana zingine katika lugha ya asili - Kiarabu. Ni muhimu kuzingatia kuwa neno *abtadi* *ninaanza* limesajiliwa kamusini kwa maana ya *shujaa wa vita* na jambo hili yumkini ni kosa lililotokana na kukaribiana kwa maneno *abtadi* na *abtali* . *Shukran sana.* *Khamis S.M. Mataka.* |