ETIMOLOJIA YA MANENO 'SUGAR/SUKARI' NA 'KAGERA' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA MANENO 'SUGAR/SUKARI' NA 'KAGERA' (/showthread.php?tid=2318) |
ETIMOLOJIA YA MANENO 'SUGAR/SUKARI' NA 'KAGERA' - MwlMaeda - 01-26-2022 KWA HESHIMA YA DAKTARI SOVU NATEKELEZA AMRI YA MKUBWA WANGU... HII NDIYO ETIMOLOJIA YA MANENO ' SUGAR/SUKARI' NA 'KAGERA' Neno sugar/sukari katika lugha ya Kiswahili neno sukari ambalo ni tafsiri ya neno la Kiingereza 'sugar' lina maana zifuatazo: 1. Nomino: [Ngeli: i-/zi-] chembechembe ndogo aghalabu zenye ladha ya utamu zinazotiwa aghalabu kwenye chai au kwenye kitu kingine pale unapohitaji ladha ya utamu kwa mfano kwenye keki, juisi au maandazi. 2. Ladha ya utamu wa kitu. Kuna msemo : Sihadaike na rangi tamu ya chai ni sukari : usipumbazwe au kuhadaika na mapambo au uzuri wa nje wa kitu, kilicho muhimu ni faida au uzuri wa ndani/uzuri halisi. Katika lugha ya Kiarabu, mzizi SKR unatengeneza maneno matatu ambayo ni nomino nayo ni sukkarun/sukkaran/sukkarin, sakkarun/sakkaran/sakkarin, sikrun/sikran/sikrin سكر yenye maana zifuatazo: 1. Kila chenye kulewesha; kilevi; pombe. 2. Siki. 3. Kitu kitamu kinachotokana na juisi ya miwa; kitu kitamu kinachopatikana kwenye matunda mbalimbali. 4. Kilevi kinachopoteza akili kinapotiwa katika kinywaji. 5. Hali inayomfanya mtu kuhamasika kufanya jambo bila ya kutafakari hatima yake; jeuri. Kuna msemo : Akhadhahu Sukkarush Shabaab أخذه سكر الشباب imemchukua sukari (jeuri) ya ujana; Sukkarul Maal سكر المال, Sukari (jeuri) ya mali; Sukkarus Sultwaan,سكر السلطان Sukari (jeuri) ya Utawala. 6. Kingo ya mto na mfano wake. Neno kagera katika lugha ya Kiswahili ni jina la kipekee lenye asili ya Kibantu lenye maana ya utelezi, na pia kitenzi chenye maana ya ameteleza. Neno Kagera limekuwa maarufu kwa kutumiwa kutambulisha mto maarufu 'Mto Kagera', vita vilivyopiganwa baina ya Tanzania na Uganda wakati wa utawala wa Iddi Amini 'Vita vya Kagera' na mkoa maarufu magharibi mwa Tanzania 'Mkoa wa Kagera'. Wana-Etimolojia wa Kiarabu wanakiri kuwa neno 'sukari' (soma: sukkarun/sukkaran/sukkarin سكر) wameliarabisha baada ya kulikopa kutoka Kiajemi. Kinachodhihiri ni kuwa maneno haya SUGAR/SUKARI na KAGERA yanabeba uwezo maalumu wa kulewesha na pia kumfanya mtu aangukie pua kutokana na utelezi. Shukran sana. Neno Maalumu: Watani waniwie radhi, nimetumwa na wakubwa zangu. Chambilecho, mshenga hauwawi. Khamis S.M. Mataka. |