Aina za Maana
Maana msingi
Ni maana tunayoipata katika kamusi. Ni ile maana halisi. Mfano, Kupe – mdudu anayenyonya damu.
Udhaifu wa nadharia inayotokana na maana msingi
i. Inajikita katika viumbe hai tu.
ii. Inashindwa kutoa sifa za maneno dhahania.
iii. Inashindwa kutofautisha polisemia na homonimia.
iv. Inashindwa kutoa unyume wa mwanamume na mwanamke kama ni jinsi au vipi?
v. Kuna utata katika kubainisha sifa za maana husika kwani kuna baadhi ya maneno si rahisi kutambua sifa zake, mfano; la.
Maana dokezi
Inaweza ikatokana na maana msingi. Mfano: tabaka la juu ni majipu, mirija, kupe. Pia inatokana na mitazamo ya jamii. Wafaransa humchukulia mwanamke kama kiumbe dhaifu, hivyo magari madogo huyaita kwa kuanzia na herufi ‘la’ ikimaanisha jinsia ya kike.
Mfano, anahuruma kwa sababu ni mwanamke.
Maana dokezi hutokana na sifa kuu tatu
i. Sifa za kiungo cha kitu. Sifa hizi zinatokana na umbo la kitu fulani. Mfano, mwonekano wa mwanamke.
ii. Sifa za kisaikolojia za kitu husika.
iii. Mtazamo wa watu kuhusu kitu hicho. Mfano; mwanamume anachukuliwaje katika jamii? Mwanamke anachukuliwaje?
Maana hisia
Inahusu hisia. Mwandishi anapoandika anakuwa na hisia gani? Unapokuwa jukwaani unakuwa na hisia gani?
Kanisani watu hutoa sadaka kwa sababu ya hisia.
Maana hisia huweza kuwasilishwa kwa njia mbalimbali
i. Kutumia maana msingi au dokezi. Mfano; wewe ni mwanamume kwelikweli. Neno mwanamume limetumika kuonyesha ni kuwa jinsi gani mwanamume anatazamwa kama mwenye nguvu katika jamii.
ii. Kutumia njia isiyo ya moja kwa moja. Katika usemaji mtu anaweza kuibua hisia. Mfano; hongera, leo umependeza kwelikweli. Mtu aliyechelewa anaweza akaambiwa, hongera wewe ni mtu wa kuwahi siku zote.
Maana ambatani
Maneno unayotamka na kuyaandika yawe na maana na mantiki. Hayo maneno yaendane na mitazamo ya jamii. Maneno hayo yanateuana na yanaenda pamoja.
Mfano, mwanamume mtanashati, nyeusi tii, nyeupe pee…
Maana ya kidhima
Maana inakuwa ndani ya neno ambalo limewekewa msisitizo. Mfano, Mauaji ya binadamu hayatakiwi.
Maana akisi/ mwangwi
Inatokana na maana ambayo watu walikuwa wanamaanisha kitu kingine watu wakahamisha.
Mfano, Chomeka, Chomoa.
Maana kimtindo/ kijamii
Huhusiana na muktadha wa matumizi ya mitindo ya lugha. Mitindo ya lugha inaweza kubainishwa kama:
i. Mitindo ya kilahaja.
ii. Mitindo ya kiwakati.
iii. Mitindo ya kihadhi/ kitabaka. Mfano; anapoishi rais panaitwa ikulu.
Dhana ya utajo
Neno utajo linatokana na neno taja. Hivyo utajo ni kitu chochote kinachotajwa. Kwa mfano; Stella, Mussa…
Wakati mwingine wanaisimu na wanafalsafa wanachanganya dhana hizi. Kwa mfano; utajo umechanganywa na urejeleo.
Crystal 1991, anasema maana ya kitajo ni sawa na maana ya kiurejeleo.
Urejeleo
Ni uhusiano baina ya kiyambo cha kiisimu na viwakilishi vyake duniani kwa wakati maalumu wa somo katika muktadha maalumu.
Mfano wa viyambo virejelezi ni: Juma, mtoto yule, kijana aliyekuja leo n.k
Sifa bainifu ya viyambo hivi vyote ni kwamba vinarejelea kitu mahususi na kwamba vitu hivi vina ukilia muktadha.
Fahiwa
Fahiwa ya kiyambo ni seti ya mahusiano yaliyopo baina ya kiyambo hicho na viyambo vingine katika lugha. Mahusiano hayo huitwa mahusiano ya kifahiwa au kisemantiki.
Mfano; usawe, fedha, pesa.
Nadharia za maana ya maana
Ni miongozo inayojaribu kutafsiri maana katika lugha. Kutokana na kuwa ni vigumu kutoa fasili ya maana, wataalamu mbalimbali wamejaribu kutoa nadharia mbalimbali zinazoweza kutumika ili kutoa fasili ya maana. Zipo fasili mbalimbali zinazoelezea maana ya maana.
Fodor 1980, anaainisha nadharia tisa za maana
i. Maana kama kitajwa au kirejelewa.
ii. Maana kama dhana.
iii. Nadharia ya maana kama mwitikio.
iv. Nadharia ya maana kama matumizi.
v. Nadharia ya maana kama ukweli.
vi. Maana kama tendo uneni.
vii. Maana kama uthibitifu.
viii. Maana kama uchanganuzi.
Kati ya nadharia hizo, ni nadharia nne tu ndizo zimejadiliwa sana na wataalamu wa isimu na ndizo zinazopambanua zaidi maana katika ngazi ya neno. Nadharia hizo ni:
i. Maana kama kitajwa.
ii. Maana kama matumizi.
iii. Maana kama mwitiko.
iv. Maana kama dhana.
Maana kama kitajwa/ kirejelewa
Inasemekana kuwa ya mwanzo zaidi ikilinganishwa na nadharia nyingine. Hoja ya msingi ya nadharia hii ni:
Maana ya umbo la kiisimu hurejelea kitu fulani kinachotajwa na umbo hilo la kiisimu katika ulimwengu wa masilugha.
Umbo la kiisimu kama sentensi, kirai, kishazi n.k
Kwa mujibu wa Palmer 1976, viashiria ni dhana inayotumika kuonyesha uhusiano uliopo baina ya vipashio vya lugha kama vile maneno, sentensi n.k vinavyohusiana na vipashio masilugha katika ulimwengu halisi.
Kwa mfano; jina John ni kipashio cha kiisimu ambacho kiitikio chake katika ulimwengu halisi ni mtu anayejulikana kwa jina hilo. Kwa hiyo, nadharia hii inahusu zaidi majina maalumu ambayo hutokea kipekee na kuwakilisha kitu halisi.
Karlgren & Holn wanaeleza maana kinaweza kuwa kilichotajwa au uhusiano kati ya jina na kitajwa. Hivyo, ili kugundua maana ni lazima mtu atafute kinachorejelewa katika mazingira halisi. Kwa mfano; mtu akitaja embe, ili kuelewa ni lazima itakubidi ulijue hilo tunda halisi liitwalo embe.
Kwa mujibu wa nadharia hii, umbo la kiisimu lisilo na kitu halisi kinachorejelewa basi umbo hilo halina maana. Hali kadhalika, iwapo maumbo mawili au zaidi ya kiisimu yanarejelea kitu halisi kimoja, basi maumbo hayo yote yana maana moja.
Ubora wa nadharia ya maana kama kitajwa
i. Maneno yanachukuliwa kuwa ni dhana zinazotumika kutaja vitu, watu au viumbe wengine, ambapo ni kweli kuwa katika ulimwengu halisi kuna vitu mbalimbali tajiri vinavyoweza kutajwa kama kutumia maneno ya lugha mathalani kuku, daktari n.k. vilevile ni kweli kuwa, maneno mengi katika lugha huwa na kiwakilishi cha vitu halisi katika lugha. Kwa mfano; nomino pekee. Pia kuna vitenzi ambavyo huonyesha matendo halisi katika ulimwengu halisi.
ii. Nadharia hii inabainisha uwezo wake wa kuonyesha uhusiano uliopo baina ya neno na kitu ambacho neno hilo linarejelea au kuashiria. Ni dhahiri kuwa,lugha zina vipashio au viyambo ambavyo dhima yake ni kutaja au kurejelea vitu. Ushahidi wa nadharia hii unadhihirishwa na jinsi mtoto anavyo amilia lugha ya kwanza au kujifunza lugha ya pili, ambapo mtoto huyo huhusisha vitu anavyoviona, kuvisikia na kuvihisi kama dhana za kumsaidia kuamilia lugha.
Mapungufu ya nadharia ya maana ya neno kama kirejelewa
i. Nadharia hii inatilia mkazo aina moja ya neno yaani nomino. Kuna maneno ya kategoria nyingine ambayo hayana chochote yanachorejelea. Maneno kama, Looh, ala!
ii. Si kila neno katika lugha lina kirejelewa katika ulimwengu halisi. Kwa mfano; maneno dhahania kama njaa, upendo, chuki n.k
iii. Kiashiria kimoja kinaweza kuwa na maana nyingi. Kwa mfano neno kaa lina maana zaidi ya moja.
iv. Nadharia hii haina uwezo wa kuelezea maana za nahau ambazo kimsingi zinatawaliwa na utamaduni wa wazungumzaji wa lugha. Kwa mfano, vaa miwani.
v. Matumizi ya maneno kurejelea kitu kinachotajwa ingawa hutumia tamko au jina la kitu hicho. Kwa mfano, kupe ni mdudu mdogo anyonyaye damu ya wanyama. Hivyo kuitambua sentensi kama Hamis ni kupe kuwa na maana tofauti ya kile kitajwa ambacho ni mdudu.
Nadharia ya Maana kama Matumizi
Nadharia ya maana kama matumizi inahusishwa na mwanafalsafa Ludwig Wittgenstein. Anasema kuwa, ni kosa kubwa kuweka mipaka ya maana kama nadharia za maana kama dhana, mwitiko, na kitajwa zinavyofanya kwani kwa kufanya hivyo ni sawa na kuweka mipaka ya zamani ya umbo lenyewe la kiisimu na hivyo kinachopaswa ni kuzingatia matumizi yake.
Nadharia hii inasisitiza kuwa, hakuna haja ya kuuliza neno fulani au neno hili lina maana gani. Badala yake huulizwa swali kuwa, neno hili limetumikaje? Hii ni kwa sababu maneno kama yalivyo hayana maana isipokuwa maana yake hueleweka katika muktadha wa matumizi. Hivyo matumizi ya maneno ndiyo yanayoamua maana ya maneno hayo.
Nadharia hii pia hushughulika na mabadiliko ya maana za maneno.
Ubora wa Nadharia ya Maana kama Matumizi
i. Inasaidia kuondoa utata wa maneno yenye maana zaidi ya moja kwa sababu maneno hayo yanazingatia muktadha. Neno mbuzi linategemea muktadha. Kwa mfano, tumechinja mbuzi kwa ajili ya kitoweo. Hivyo, kupitia nadharia hii, utata wa neno hilo unaweza kuondolewa.
ii. Inasaidia kutupa maana ya maneo yasiyo na ujazo wa kisemantiki. Kwa mfano: na, ni, kwa… yanapotumika katika sentensi na si kusimama peke yake kwani yakisimama peke yake hayatoi maana yoyote ile.
iii. Nadharia hii inasaidia pale watoto wanapojifunza lugha. Kujifunza kwa kusikiliza na kuangalia maneno mbalimbali yanavyotumiwa.
Udhaifu wa Nadharia ya Maana kama Matumizi
i. Kupotosha maana kwa msikilizaji. Kwa mfano, wakati wa sherehe ukimwambia mtu alete mbuzi. Itakuwa vigumu kwa mtu huyo kutambua kama mbuzi kifaa au mbuzi mnyama ndiye anayetakiwa na mwagizaji.
ii. Maana ni zaidi ya matumizi. Huwezi kupata maana ya maneno katika matumizi kama huna dhana au uzoefu kuhusu manano hayo. Kwa mfano, Juma amebwia unga. Hapa si rahisi kujua maana ya maneno bwia na unga kama huyafahamu.
iii. Nadharia hii inaweka uhuru kupindukia kwani haijaweka wazi mipaka ya matumizi hayo.
Nadharia ya Maana kama Mwitiko au Uchocheo
Waasisi wa nadharia ya maana kama mwitiko ni Bloomfield 1935, na Lyons 1987. Nadharia hii imejengeka katika elimu nafsi. Inaonyesha kuwa, maana ya maana ni mwitiko wa ubongo. Maana ya neno ipo katika uitikio wake. Uitikio unajitokeza pale mtu akisikiliza neno fulani na hiyo ndiyo inayokuwa maana ya neno hilo.
Mwitikio hutokea pale mtu anaposikia neno lenye kuamsha hisia kama vile: nyoka, chatu, simba n.k
Ubora wa Nadharia ya Maana kama Mwitiko
i. Inajaribu kutazama jinsi lugha inavyomgusa mtu na jinsi anavyoitika.
ii. Mwitiko halisi juu ya maana hutambuliwa kutokana na mwitiko. Maana hii humsaidia mtu kutenda jambo fulani. Kwa mfano, mtu akiona mnyama asababishaye madhara huchukua tahadhari.
Udhaifu wa Nadharia ya Maana kama Mwitiko
i. Yapo maneno katika lugha ambayo ni vigumu kupata mwitiko wake.
ii. Kila neno lina mwitiko, lakini ni vigumu kupima mwitiko wa mtu kwa kila neno katika lugha kwani sayansi bado haijafikia uwezo huo. Pia ni vigumu kupima ni kwa jinsi gani ubongo huitikia kwa kila neno katika kutafuta maana ya neno hilo.
iii. Nadharia hii huchukulia kuwa, binadamu wote wana mwitikio sawa kutokana na kitu walichokisikia au kukiona, jambo ambalo si sahihi. Ukweli ni kwamba, kila mwanadamu ana kiwango chake cha mwitiko kulingana na mazingira tamaduni na uzoefu wake.
iv. Watu hupata mwitiko mkubwa zaidi katika vitu wanavyoviona kuliko wanavyovisikia. Mtu atakuwa na mwitiko mkubwa akimuona nyoka kuliko akisikia nyoka.
Nadharia ya Maana kama Dhana
Mtazamo huu uliasisiwa na kutumiwa na wanafalsafa wa kale kama: Edward Sapire, De Sassure, Ogden na Richard. Pia wanaisimu: Ullman 1964, Godon 1980 na wengineo waliutumia.
Wataalamu hawa wanafasili maana kama dhana kuwa ni jumla ya mawazo yanayotokana na wazungumzaji wa lugha katika ulimwengu wao. Kutokana na nadhari hii, maneno ni alama ya mawazo yaliyo ndani ya akili ya mzungumzaji.
Ubora wa Nadharia ya Maana kama Dhana
i. Maana ina uhusiano wa karibu na uwezo wa fikra ya mwanadamu ki mantiki na ki ufahamu. Hivyo, tunapochambua maana, tunachambua uwezo wetu wa kufikiria na kufahamu. Richard alisisitiza kuwa,hakuna kamusi yenye uwezo wa kufasili maana ya neno.
ii. Maana ya neno inahusishwa na sifa za ziada ambazo wazungumzaji wa lugha wanazihusisha na kitu kingine hata kama hakina sifa ya kisemantiki.
Mapungufu ya Nadharia ya Maana kama Dhana
i. Si kweli kwamba, wasimaji kwa wakati mmoja wanaweza kuwa na dhana moja juu ya kiumbe, kitu au jambo linalotajwa. Ni vigumu sana kupata maana ya neno linalotamkwa kuhusiana na viumbe au kitu kinachotamkwa. Dhana ya uzuri inakupa maana gani? Kila mtu ana matazamo wako kuhusiana na uzuri au ubaya wa kitu.
ii. Nadharia hii inaeleza kuwa, dhana ni jumuisho la sifa pambanuzi zinazotumika kutambulisha kitu. Inadai kuwa, kuna hitajio la sifa bainifu zinazokisahilisha kitu fulani kupata sifa na uwezo wa kuitwa kinavyopaswa kuitwa. Ili mwanamke aitwe mwanamke ni lazima awe na sifa baifu za kumfanya aitwe hivyo.
Vikoa vya Maana
Vikoa vya maana ni yale maneno yanayokuwa na uhusiano. Ni seti yoyote ile ya msamiati ambayo memba wake huhusiana kimlalo na kiwima hivyo msamiati wa lugha haukupangwa kiholela kutoka vichwa vya watumiaji wa lugha.
De – Ssassure anabainisha aina mbili za mahusiano
i. Mahisiano ya kiwima.
ii. Mahusiano ya kimlalo.
Mahusiano ya Kiwima
Haya ni mahusiano yanayohusu neno kubadilishana nafasi na neno jingine bila kupoteza maana au uelewekaji wake. Kwa mfano:
Huyu ni mtoto
Wale ni wezi
Mahusiano ya Kimlalo
Haya ni mahusiano ya maneno kimfuatano au kwa jinsi yanavyopangwa katika tungo kuzingatia kanuni za kisarufi za lugha husika. Kwa mfano:
Kitabu changu kimepotea katika mazingira ya kutatanisha.
Nampenda sana mama yangu kwa sababu alinilea vizuri.
Sifa za Vikoa vya Maana
i. Leksimu au maneno katika kikoa kimoja, yanaweza kuwa na uhusiano kwa msingi wa usiganifu yaani maneno kuwa na ufanano wa kimaana na wakati huohuo kutofautiana. Kwa mfano, rangi. Maneno haya yanafanana, lakini kuna usiganifu, rangi nyekundu, rangi nyeusi, njano n.k
ii. Kikoa kimoja kikibwa au kipana huweza kujumuisha vikoa vidogovidogo kadhaa au vingi. Katika kikoa cha matunda kuna kikoa kidogo cha aina ya matunda hayo, kama vile, machenza, machungwa n.k
iii. Leksimu katika kikoa kimoja huwa hazina mpangilio maalumu
iv. Hata hivyo, upo mpangilio maalumu, kwa mfano: siku za wiki, miezi,miaka na vipimo.
Mahusiano ya Kifahiwa
Mahusiano ya kifahiwa ni mahusiano yaliyopo baina ya maneno yanayoanza kikoa fulani cha maana yaani jinsi memba wa kikoa kimoja wanavyohusiana.
Hiponimia
Hiponimia ni uhusiano kati ya vitu na aina zake. Kwa mfano: katika matunda kuna maembe, machungwa, mananasi na matunda mengineyo.
Melonimia
Melonimia ni uhusiano uliopo baina ya maneno mawili au zaidi ambayo huonyesha sehemu ya kitu kizima. Au ni uhusiano wa kitu na sehemu zake. Kwa mfano, mkono, kiganja kidole n.k.
Polisemia
Polesemia ni hali ya maana nyingi zinazokaribiana au kuhusiana. Uhusiano huu hutokana na mnyumbuliko wa maana hizo katika maana moja ya msingi. Lyons anasema kuwa, upolisemia ni kuwa na maana nyingi zinazohusiana. Kwa mfano, mpira kifaa cha michezo. Mpira wa kujikinga na maradhi. Mpira wa kumwagilia.
Homonimia
Homonimia ni maneno katika lugha yenye muundo sawa. Maneno haya huandikwa na kutamkwa sawa lakini yana maana tofauti. Kwa mfano: kaa mnyama mdogo aishie majini. Kaa kipande cha mti kilichochomwa. Kaa kitendo cha kuweka makalio chini.
Baadhi ya wanasemantiki hutofautisha homonimia kwa kutumia maandishi na matamshi ya maneno. Katika kigezo hiki tunapata aina mbili za homonimia.
i. Homofoni. Ni maneno yenye matamshi sawa lakini yanahitilafiana katika maandishi yake. Hata hivyo ni vigumu kupata homofoni katika lugha ya kiswahili kwa sababu tunatamka kama tunavyoandika. Katika kiingereza miongoni mwa mifano ya homofoni ni; see na sea. Bear na bare. Hear na here.
ii. Homografu. Ni maneno yenye maandishi sawa lakini yanatofautiana katika utamkaji wake. Kwa mfano, barabara yaani njia ya kupita watu na magari. Au barabara yaani sawasawa ama kukubaliana na jambo fulani.
Aina za Sinonimia
Sinonimia ni maneno mawili au zaidi yenye maumbo tofauti lakini maana zake zinalingana na kukaribiana. Kwa mfano: fedha, hela, pesa, shimo, tundu, tobo. Kuna aina mbili za sinonimia:
i. Sinonimia za kimantiki. Hutokea pale ambapo leksimu mbili au zaidi huweza kubadilishana nafasi katika sentensi taarifu zote pasipo kuathiri masharti ya ukweli wake. Kwa mfano: aina, kategoria, shimo, tundu, tobo… n.k
ii. Sinonimia kuntu. Lyons 1987, anasema aina hii ya sinonimia hutokea pale ambapo leksimu mbili au zaidi huweza kubadilishana nafasi katika miktadha yote bila athari yoyote katika maana. Wanaisimu wengi wanakubaliana kuwa, hakuna lugha yoyote yenye sinonimia kuntu.
Vyanzo vya Sinonimia
i. Jinsia. Tofauti ya wanawake na wanaume hudhihirika kupitia asasi mbalimbali ikiwemo lugha. Lugha nyingi za binadamu zina maneno ambayo hutofautisha jinsi ya wanawake na wanaume. Kwa mfano: shoga na rafiki, shosti na besti, mtanashati na mrembo, ugumba na utasa… n.k
ii. Matabaka. Kwa mfano, marehemu, kasri, tembe, banda. Nyumba ya tajiri inaweza kuitwa kasri na nyumba ya masikini ikaitwa banda.
iii. Dini. Baadhi ya visawe hutumika katika muktadha wa dini fulani tofauti na dini nyingine. Kwa mfano, msikiti, kanisa, hekalu, Kwarezma, Ramadhani… n.k
iv. Eneo. Msamiati huweza kuongezeka kutokana na kuenea kwa lugha. Lugha ambayo hukua kwa kasi na kuenea hutokea kuwa na lahaja mbalimbali za kieneo. Lahaja hizi za kieneo hutofautiana katika matumizi ya maneno, lakini kwa kuwa ni lahaja za lugha moja, ni rahisi kupata msamiati ambao ni visawe. Kwa mfano: katika lugha ya Kiswahili tuna neno mti, katika kimvita tuna nti. Pia, macho na mato. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuna maneno kama: desa, kimbweta n.k
v. Sayansi na teknolojia. Televisheni (TV), flash (kinyonyi), laptop (kipakato), calculator (kikokotozi), keyboard (kicharazo), password (nywila)… n.k
vi. Taaluma. Taaluma mbalimbali huwa na maneno tofauti yanayorejelea dhana ileile au dhana zinazokaribiana. Kwa mfano: mshororo na msitari huchukuliwa kuwa na maana ileile isipokuwa mshororo ni istilahi ya kishairi na msitari hutumika katika lugha ya kawaida.
vii. Wakati au mabadiliko ya kiwakati. Kipindi cha nyuma soko lilijulikana kama utupu. Nayo macho yaliitwa maozi.
viii. Ukopaji wa msamiati. Neno shule limekopwa kutoka lugha ya kijerumani
ix. Umri. Chapa na charaza huambiwa mtoto. Piga na kichapo huambiwa wakubwa.
x. Shughuli za kijamii. Askari usalama, shushushu, mpelelezi, askari kanzu… n.k
Antonimia
Ni hali katika lugha ambapo maneno mawili au zaidi yana maana zinazopingana (unyume).
Aina za Antonimia
i. Unyume kadilifu. Onyesha viwango mbalimbali, kwa mfano: Juma ni mweusi sawasawa na John.
ii. Unyume kamilishani/ unyume wa kiutoano. Ni unyume wenye mpaka usiopitika ambapo hukanusha upande mmoja maana yake na kukubaliana na upande wa pili. Antonimia moja inapotumiwa huondoa nyingine. Kwa mfano: mwanamke – mwanamume, kifo – uhai, faulu – feli
iii. Unyume elekeani. Ni ule unaotokea pale ambapo uhusiano baina ya leksimu mbili katika jozi huwa ni wa kiuelekeano. Hii ina maanisha leksimu moja huwa ni kinyume cha leksimu nyingine kutegemeana na uelekeo yaani upande tendo linapoelekezwa. Kwa mfano: mwajiri – mwajiriwa, daktari – mgonjwa, mzazi – mtoto.
iv. Unyume tenduzi (rejezi). Vitenduzi vingi vina uhusiano unaoeleza hali ya kutendua. Kwa mfano: anika – anua, jenga – bomoa, kunja – kunjua, funga – fungua.
Semantiki ya Sentensi au Tungo
Kuna aina mbalimbali za maneno katika kiwango cha sentensi. Katika kiwango cha sentensi, tunaangalia uhusiano unaotokana na uhusiano wa neno moja na maneno mengine katika sentensi. Uhusiano wa maneno katika sentensi huchanuza maana iliyokusudiwa.
Mahusiano ya Kimaana
Usawe
Ni uhusiano baina ya sentensi mbili au zaidi ambapo sentensi hizo huwa na maana moja ya msingi.
Hali ya sentensi zaidi ya moja kuwa na maana moja.
Kwa mfano: ilikuwa vigumu kwake kupata uhamisho.
Haikuwa rahisi kwake kuweza kuhamishwa.
Sentensi hizo zinahusiana kwa misingi ya maana ileile na zinahusiana kwa misingi ya usawa.
Aina za Usawe
i. Usawe wa kileksika
ii. Usawe wa kimuundo.
Usawe wa Kileksika
Ni ule ambao unahusu sentensi mbili au zaidi ambazo zina maneno yenye maana ileile ya msingi katika nafasi ileile.
Kwa mfano: John alitupa jiwe likampiga Juma.
John alivurumisha jiwe likamnasa Juma.
Alivurumisha liko katika nafasi ileile na likamnasa nayo imebaki katika nafasi ileile. Katika sentensi hizi vitenzi tupa na vurumisha vina maana ileile na vitenzi piga na nasa vina maana sawa.
Usawe wa kimuundo
Usawe huu unatokana na maana ya msingi ya sentensi mbili au zaidi kubaki ileile japo sentensi hizo zinakuwa na mpangilio tofauti.
Usawe huu huitwa usawe wa kimuundo kwa sababau hauhusiani na maana za maneno au kirai kwani maneno ni yaleyale au ni maneno yanayotofautiana sana.
Mfano:
Maelezo yake yalikuwa magumu kueleweka.
Ilikuwa vigumu kuelewa maelezo yake.
Hakuna aliyeelewa maneno yake ya ajabu.
Maneno yake ya ajabu hayakueleweka.
Sentensi hizi zina maana ileile ya msingi.
Sentensi za namna hii hutokana na mchakato ambao kiisimu huitwa uhamishaji. Mchakato huu huhamisha vipashio kadhaa ama kutoka mwishoni kuja mwanzoni au vya mwanzoni viakawa mwishoni mwa sentensi.
Utata katika tungo
Utata ni kipengele kinachodhihirisha tafsiri zaidi ya moja. Sentensi huwa na mana zaidi ya moja au hueleweka kwa namna zaidi ya moja.
Aina za utata
1. Utata wa kileksika
Ni utata unaotokana na matumizi ya maneno au leksimu yenye maana zaidi ya moja iliyotumika ndani ya tungo. Utata huu kwa kawaida hutokana na matumizi ya hinonimia au polisemia.
Mfano:
Baba alimleta papa kazini kwake.
Nilinunua kanga kwa bei ya shilingi elfu ishirini.
Katika sentensi ya kwanza: papa anaweza kuwa mnyama, au anaweza kuwa papa mkuu wa kanisa katoliki.
Sentensi ya pili: kanga aina ya ndege au kanga nguo.
Utata wa kimuundo
Hutokana na jinsi sentensi ilivyopangiliwa. Hizi hutokana na jinsi sentensi ilivyoundwa au mpangilio wa sentensi na siyo neno moja.
Mfano
Alimkuta daktari na mgonjwa wake.
Utata
Alimkuta daktari na mgonjwa wa daktari.
Alimkuta daktari na mgonjwa wa mtu huyu aliyemtembelea daktari.
Anampenda zaidi kuliko wewe.
Utata
Anampenda kuliko unavyompenda wewe.
Anampenda yeye kuliko wewe.
Usawe na utata
Vina uhusiano linganuzi. Katika usawe, tungo kadhaa hupewa tafsiri moja, wakati katika utata, tungo moja hupewa tafsiri zaidi ya moja.
Mfano
Janga la UKIMWI ni la Dunia nzima.
Janga la UKIMWI ni la ulimwengu mzima.
Mimi ni mzuri.
Mimi ni mrembo.
Katika utata, sentensi ni moja.
Mfano
Albert ni kichwa.
Tungo ni moja lakini ina chanuza maana zaidi ya moja.
Ukinzani
Kuna vitu viwili ambavyo vinakuwa vinakinzana.
Mfano
Hapo juu ndipo chini.
Mpandangazi ndiye mshuka ngazi.
Kiambo kinzani ni kile kinachodhihirisha vigambe viwili siganifu kwa wakati mmoja. Kiyambo cha namna hii hunena kwamba, fulani ana kitu fulani, kinazosifa fulani na wakati huohuo hakina sifa hizo.
Mifano ya viyambo kinzani:
Hapo juu ndiyo chini.
Huyu mzee ni mtoto kabisa.
Huo uchungu ndiyo utamu wenyewe.
Chungu tamu.
Walikwenda mbele lakini wakabaki nyuma.
Vigambe vinavyotokana na sentensi hizo, havikubalini na ujuzi wetu wa malimwengu.
Mfano, huwezi ukawa mwanaume na wakati huo huo mwanamke.
Ukinzani huo hutumika sana kwa baadhi ya washairi wanaotaka kueleza jambo ambalo lina ukinzani ndani yake.
Upotoo
Ni ukiushi wa kimantiki unaotokea pindi vijenzi semantiki viwili siganifu vinapounganishwa kueleza jambo fulani. Kwa mfano,
Alichora barua kwa mguu wa kushoto.
Mjomba wangu ni mjamzito.
Uziada dufu
Ni urudiaji usiohitajika. Usio wa lazima.
Mifano
Mke wangu ni mke wangu.
Rafiki yangu ni msichana wa kike.
Mahusiano ya ukweli
Dhana ya uchopezi
Kufanya vitu viwe na mwingiliano. Mfano, maana ya kitu kimoja kuwekwa sawa na maana ya kitu kingine. Mfano, majangili wamemuua simba. Simba ameuawa na majangili.
Uchopezi unakuwa na uhiponimia. Mfano, tuliwaona wanyama mbugani. Tuliwaona simba mbugani.
Mahusiano ya ukweli yapo ya aina mbili yanayochunguzwa na semantiki.
Uchopezi
Udhanilizi
Uchopezi
Ni dhana itumiwayo na wanaisimu maana katika kutoa ufafanuzi juu ya uhusiano wa sentensi mbili au zaidi. Pia hufasiri maana za sentensi hizo kutokana na mtiririko wa mantiki baina ya sentensi moja na nyingine.
Mahusiano ya uchopezi baina ya sentensi ni wa kimaana. Hudaiwa kuwepo pasipo kuzihusisha sentensi hizo na muktadha.
Katika dhana hii, maana ya sentensi moja huweza kuhusishwa na sentensi nyingine pasipo kurejelea muktadha.
Mfano
A. Mwanamuziki ameuawa na majambazi.
B. Mwanamuziki amefariki.
A. Daktari amemponya mgonjwa.
B. Mgonjwa amepona.
Njia ya kawida ya kueleza uhusiano baina ya a na b hapo juu ni kwamba, mtu huweza kuchukulia kuwa a ni kweli kutokana na b yaani kama a ni kweli, basi hata b ni kweli.
Kwa mujibu wa sentensi a na b, tunaweza kusema kuwa, wa sabbu mwanamuziki ameuawa, basi bila shaka amefariki. Vivyo hivyo kwa sentensi ya pili.
Aina za uchopezi
Huweza kuwa wa kileksika au wa kisintaksia. Uchopezi wa kisintaksia hujumuisha miundo ambayo huwa na maana ileile ya msingi. Dhana ya kutendea na kutendwa.
Mifano
A. Ngedele amekula mahindi yangu.
B. Mahindi yangu yameliwa na ngedele.
Kwa mtazamo wa uchopezi, a na b, zinachopezana.
Uchopezi wa kileksika
Jambazi amemuua mwanamke.
Mwanamke amefariki.
Maana yake ni kwamba, mtu anaposema ameuawa, lazima kitu hicho kife, kama hakijafa, basi hajauawa.
Hiponimia imejikita kwenye ujumuizi ambao unafanana na uchopezi. Tofauti ikiwa tu ni kwamba, uchopezi unahusika na mahusiano baina ya sentensi na hiponimia huangalia uhusiano baina ya maneno.
Mfano
A. Tunashauriwa kula matunda mara kwa mara.
B. Tunashauriwa kula mananasi mara kwa mara.
A. Tuliwaona simba mbugani.
B. Tuliwaona wanyama mbugani.
Hapa sentensi B imechopezwa katika sentensi A kwa sababu simba ni aina ya mnyama.
Sifa za uchopezi
1. Sentensi zote hutegemeana kimantiki ili kubainisha ukweli.
2. Uwepo wa sentensi ya pili hutegemea sentensi ya kwanza ambayo inaweza kuwa jumuishi au mahususi.
3. Uchopezi hutokana na uhusiano baina ya sentensi, kwa hiyo hautegemei muktadha.
Udhanilizi
Hiki ni kipengele kilicho katikati ya mpaka wa semantiki na pragmatiki. Kimejadiliwa sana na wanasemantiki pamoja na wana pragmatiki. Hivyo ni kitengo ambacho wataalamu wengi wanakiweka katika kitengo cha pragmatiki.
Mifano ya udhanilizi
A. Umenunua gari jingine?
B. Ulikuwa na gari kabla ya hili?
A. Nyumba ya heri ni nzuri.
B. Heri ana nyumba.
Kwa hiyo sentensi a inadhaniliza sentensi b. Jambo linalodhanilizwa huchukuliw kuwa linafahamiwa na msemaji pamoja na msikilizaji. Katika sentensi a, kuidhaniliza sentensi b, ina maanisha kwamba, ukweli wa sentensi a lazima utokane na ukweli wa sentensi b.
Pragmatiki
Ni maana kulingana na muktadha ila ni maana zaidi ya muktadha. Taaluma hii iliandikwa na wanafalsafa a wanaisimu miaka ya 1980. walisema pragmatiki inaweza kutoa maana yake kulingana na muktadha.
Thomas 1997, pragmatiki ni zaidi ya matumizi, muktadha na matumizi. Anasema huu ni mtagusano na mchakato uliopo baina ya msikilizaji na msemaji.
Skema
Unaweza kuwa na skema ya awali kuhusu jambo fulani. Mfano: mtu fulani si mwizi, lakini ukikuta anaiba, skema yako inabadilika.
Maana ya pragmatiki itaangaliwa kupitia awamu au vipindi mbalimbali.
1. Kabla ya 1980
2. 1980
3. Miaka ya hivi karibuni.
Kabla ya 1980
Masuala ya pragmatiki yalishughulikiwa katika falsafa na siyo kama kipengele cha isimu. Hivyo wataalamu waliojishughulisha na pragmatiki walikuwa wanafalsafa zaidi kuliko wanaisimu.
1980
Pragmatiki ilianza kuandikwa katika vitabu vya kiisimu mwanzoni mwa miaka ya 1980. mwanzoni mwa miaka hiyo, fasili zake zilikuwa mbili:
– Pragmatiki ina maana katika matumizi.
– Pragmatiki ni maana katika muktadha.
Fasili hizi zina dosari
Vipengele hivi vinajumuisha baadhi ya vipengele vya kisemantiki ndani yake na hivyo kutufanya kushindwa kutofautisha kati ya pragmatiki na semantiki. Hii ni kwa sababu fasili ya kuwa pragmatiki ni maana katika matumizi inachukuliwa kuwa msingi wa pragmatiki ni matumizi na fasili ya pili isemayo kuwa pragmatiki ni maana katika muktadha inachukuliwa ni msingi wa pragmatiki ni muktadha.
Wataalamu waliojitokeza mwishoni mwa miaka ya 1980, waliboresha fasili hizo na kuhusisha pragmatiki na:
Maana ya msemaji.
Tafsiri ya kilichosemwa.
Pamoja na uboreshaji huo, bado kulikuwa na walakini. Mfano, fasili ya pragmatiki kuhusishwa na maana ya msemaji, inamwangalia zaidi msemaji au mtoa ujumbe na kusahau kwamba, upatikanaji wa maana ni mchakato shirikishi ambao umepitia ngazi kadha wa kadha kuanzia katika maana dhahania hadi katika maana ya ki muktadha.
Fasili hiyo imeletwa na wataalamu wanaochukulia kuwa, mawasiliano ni kitendo cha kijamii.
Fasili ya kuhusisha pragmatiki na fasili ya kilichosemwa yaani maana ya msikilizaji inajikita kwa mpokea ujumbe na kuzingatia mpokea ujumbe pekee na kupuuza vikwazo vya kijamii vinavyoweza kuwepo wakati wa mazungumzo au wakati ujumbe unapotolewa.
Fasili hii inatetewa na wataalamu wanaochukulia mawasiliano kuwa kitendo cha kiuchambuzi.
Maana ni ya nani kati ya mzungumzaji na msikilizaji? Hii ni changamoto.
Pragmatiki katika miaka ya hivi karibuni (1990)
Zimeibuka fasili kadhaa za pragmatiki ambazo ingawa bado zina dosari, walau zinaelekea kukidhi haja.
Fasili ya pragmatiki ni maana katika mtagusano (Thomas, 1995).
Fasili hii inaonesha kuwa, maana haijikiti katika maneno pekee wala haikaliwi na msemaji pekee na wala mana haitegemei utashi wa msikilizaji peke yake, isipokuwa yote yanategemeana. Hivyo kujenga maana ni mchakato changamani unaohusisha mwafaka baina ya wasemaji, msikilizaji, muktadha wa mazungumzo pamoja na maana ya msingi ya kile kinachosemwa.
(Leech, 1981), pragmatiki huchunguza uhusiano baina ya viyambo vya lugha na watumiaji wa vyombo hivyo.
Mawazo hayo yanaungwa mkono na (Yule, 1996) anaposema kuwa, pragmatiki ni taaluma inayohusu yaliyopo baina ya maumbo au alama za lugha na watumiaji wa maumbo au alama hizo.
Muktadha
Tunapozungumzia muktadha hatumaanishi tu sehemu, mahali au mazingira ambamo mazungumzo yanafanyika. Kwa hakika sehemu au mahali mazungumzo yanapofanyika ni kipengele kimojawapo cha muktadha miongoni mwa vipengele vingi.
Muktadha kamili hujumuisha:
– Nani anazungumza?/msemaji.
– Anazungumza na nani?/msikilizaji.
– Anazungumza na mtu huyo akiwa na watu gani?
– Wanazungumza nini?
– Wanazungumzia wapi?
– Wakati gani?
– Wanazungumza kwa lengo gani?
– Wanamtazamo gani kuhusu wao wenyewe na kuhusu wengine?
– Wapo katika hali gani?
– Nini kilitanguliwa kusemwa kabla ya kinachosemwa sasa?
– Je wanauzoefu sawa wa historia au wako tofauti?
Skema
Ni ramani dhahania zilizomo akilini mwa binadamu ambazo hutusaidia kupata, kupokea na kuelewa maarifa mapya.
Ni ramani majumui ya maarifa au utambuzi ambayo kila mtu anayo akilini mwake.
Kwa kawaida tunatumia skema mwanzoni tupatapo habari mpya, hivyo skema zetu huboreshwa pindi tupatapo habari au maarifa mapya. Skema ya mtu mmoja hutofautiana na ya mtu mwingine.
Jambo linalosisitizwa, skema hujengwa kutokana na utambuzi: akili ya mtu na uzoefu alionao mtu huyo.
Ni vigumu kuelewa jambo linaloongelewa kama huna ramani yake akilini. Kama jambo linazungumziwa ni lile ulilonalo akilini, huzua mgogoro.
Mifano:
Kwa kaka zangu, tukio hilo lilimaanisha kupata mtu wa kusaidiana naye kuchunga ng’ombe. Kwa baba yangu ilimaanisha kupata mtu mwingine anayeweza kutunza familia. Lakini kwa mama yangu ili maanisha kuwapo kwa kipindi kifupi cha kusubiri kabla ya kupata mkwe wa kusaidiana naye kazi mbalimbali…
|