KIWANGO CHA FONETIKI NA OTHOGRAFIA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Sarufi na Utumizi wa lugha (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=9) +--- Thread: KIWANGO CHA FONETIKI NA OTHOGRAFIA (/showthread.php?tid=169) |
KIWANGO CHA FONETIKI NA OTHOGRAFIA - MwlMaeda - 06-21-2021 Mitindo mbalimbali pia inaweza kutofautishwa kwa kutumia kiwango cha fonetiki na othografia. Othografia ina maana ya tahajia iliyokubaliwa rasmi kuwa ni sanifu (Kamusi ya Kiswahili Sanifu, 1990). Unapochunguza mtindo kama unaotumika katika magazeti utaona waandishi wanaruhusiwa kutumia ufupisho wa maneno k.m. KCB badala ya ‘Kenya Commercial Bank’ mfano mwengine ni kama ‘waandamana kupinga kufungwa kwa KFA’. Jambo hili huruhusiwa katika magazeti kwa kuwa magazeti hulenga kubania nafasi ya karatasi. Mbali na kujaribu kupunguza utumizi wa karatasi,hii aidha ni mbinu inayoleta mvuto katika msomaji kutokana na kule kufupishwa kunakoipa lugha uzuri wa aina fulani.
Kwa upande mwengine hii mbinu ya kufupisha haiwezi kutumika katika mtindo kama wa kitaaluma au kirasmi. Katika kitabu cha taaluma fulani huwezi kwa mfano ukiwa unazungumzia mji wa Nairobi uandike Nrb. Pia kwa mfano unapoandika makala katika kitabu au unapotaka kufanya wasilisho fulani katika semina itakubidi uandike kila jambo kwa ukamilifu kwani hii ndiyo kaida ya mtindo huo. Yaani lazima ufuate zile kanuni au taratibu za kisarufi.
ZOEZI
Unatumia matamshi na uneni wa aina gani?
Tunapozungumzia fonetiki tunachunguza kipengele cha isimu kinachojishughulisha na sauti za vitamkwa za lugha. Utaona kuwa pia tunavyotamka kutatofautiana kutegemea na mtindo tunaotumia.
Unapokuwa unatamka au kuzungumza katika mazingira yanayohitaji mtindo wa kirasmi kwa mfano kama kuzungumza katika chombo cha umma kama redio au runinga au unapokuwa ni mwalimu na unafundisha au kutoa mhadhara, bila shaka utajaribu iwezekanavyo kuepuka matatizo yatokanayo na athari za lugha ya kwanza ikiwa una matatizo hayo. Pia kama ni mzungumzaji anayetumia lahaja fulani kwa mfano ya Kiswahili aidha katika mazingira kama hayo utajaribu kuepuka utumizi wa lahaja.
Katika mtindo wa kifasihi mwandishi wa kazi fulani huweza kuwapa wahusika wake lahaja fulani au tanakali ya lafudhi. Hizi huwa ni mbinu za kimtindo ambazo mwandishi hutumia kuwatofautisha wahusika kwani mwandishi anapoandika kazi ya kifasihi huwa anawaweka wahusika wake katika mazingira fulani ya kijamii au ya kieneo. Mfano mzuri ni katika tamthilia ya Kinjeketile ambapo E. Hussein anampatia mhusika wake mkuu tanakali ya lafudhi inayomjulisha kuwa si mzungumzaji asilia wa lugha ya Kiswahili Sanifu. |