MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MAKOSA YALIYOZOELEKA KATIKA KISWAHILI

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
MAKOSA YALIYOZOELEKA KATIKA KISWAHILI
#1
WASWAHILI MPO?
Imenukuliwa na John Wisse
Inasikitisha sana kuwaona walimu, waandishi na watangazaji wa Kenya na Tanzania wakijidai kuwa ni wataalamu wa Kiswahili eti ni wazawa wa Uswahilini wanadiriki kuitumia bila kuwa na ujuzi wa kutosha katika fasihi na isimu yake. Haya ndiyo makosa yanayotakiwa kurekebishwa kwa njia za semina na warsha hata katika hafla mbalimbali za kifasihi…Maneno na Miundo ya maneno ya Kiswahili inayokanganya.
Baada ya kuandika juu ya Asili na Chimbuko la Kiswahili katika Afrika Mashariki, nitaeleza kwa muhtasari matatizo yanayoikumba lugha hii hasa katika tahajia, matamshi, maana na matumizi yake. Kwa maneno mengine, lugha ya Kiswahili hivi sasa inawakanganya watumiaji wake hasa wanafunzi wa ndani na nje ya Afrika Mashariki. Mkanganyiko huu unasababishwa na udhaifu uliopo katika taaluma ya lugha ya Kiswahili kama mofolojia, fonolojia, sintaksia na semantiki kwa waandishi na watangazaji wa Kiswahili.
Nitatoa mifano ya mikanganyiko hii na kupendekeza njia bora ya kukitumia Kiswahili na kwa ufasaha.
Nianze kwa kutoka mifano michache:
Maneno yanayokanganya kwa mfuatano wa alfabeti.
A
Adhima na Azma
Lugha za asili zinachangia sana katika mkanganyiko huu hasa kwa kuchanganya herufi /dh/ na /z/. Kwa mfano maneno Adhima na Azma.
Adhima si neno la Kiswahili linalofahamika ijapokuwa kuna neno adhimu au adhimisha. Kuadhimisha ni kufanya sherehe ya kumbukumbu ya tukio fulani kama siku ya kuzaliwa, kufunga ndoa, kupata uhuru, n.k. Neno azma maana yake ni jambo linalokusudiwa kufanyika au makusudio ya jambo fulani. Hili ni neno sahihi la Kiswahili.
Ahirisha na hairisha
Kwa matumizi sahihi ya Kiswahili neno lililosadifu ni ahirisha maana yake ni kuchelewesha jambo kwa makusudi ili lifanyike baadaye. Neno hairisha si neno sanifu.
Aidha, ama, au
Maneno haya matatu yanatumiwa vibaya. Kwa mfano neno aidha lina asili ya Kiarabu na maana yake ni tena, basi, zaidi ya hayo, vilevile, n.k.
Wanaokosea kulitumia ni wale wenye misingi ya Kiingereza wanaofuata mtindo wa kutumia ‘either … or ’
Tunasoma katika magazeti kwa mfano:
“Wataalamu wa Kichina watabaki aidha Bara au Visiwani”. Kwa usahihi inatakiwa kuandikwa,” “Watalaamu wa Kichina watabaki ama Bara au Visiwani.”
Kwa matumizi sahihi ya ‘aidha’ tutakiwa kuandika: “Kabla ya kwenda sokoni nitapitia aidha benki ili kuchukua fedha.” Maana yake …nitapitia pia benki ili kuchukua fedha.
Ajali na ajari
Yako makabila ambayo hawawezi kutofautisha kati ya herufi /l/ na /r/. Kwa mfano neno ajali ni tukio lenye madhara yanayotokea ghafla lakini ajari ni malipo ya kazi ya ziada au ovataimu.
B
Baadaye na baadae
Neno sahihi hapa ni baadaye.
Budi
Kama neno budi litatumika peke yake maana yake ni hiari. Kwa kawaida hutumika likifuatana na maneno kama: Hapana budi, hatuna budi budi, sina, hawana, n.k.
Kwa mfano kama tukisema “Wakulima ni budi walime, tuna maana kuwa wakulima wana hiari ya kulima au kuacha. Lakini tukisema “Wakulima hawana budi walime” tuna maana ya kusema kuwa wakulima ni lazima walime.
D
Dahili na Sajili
Watumiaji wa maneno haya huyachanganya. Haya yanatofautiana katika maana.
Kudahili maana yake ni kudadisi, kutaka kujua jambo kwa kuulizauliza.
Sajili maana yake ni kuweka orodha ya kumbukumbu za vitu au watu kwa kuandika katika daftari maalumu. Kwa mfano wanachuo au wafanyakazi wapya hudahiliwa na hatimaye kama wanaonekana wanafaa huandikwa katika daftari la kudumu na hapo tunasema wamesajiliwa.
Digiti na Dijitali
Haya ni maneno mawili yanapatikana kutokana na neno la Kiingereza la ‘digit’. Neno hili ni nomino na kwa kawaida tunatohoa nomino badala ya kitenzi, kivumishi au kielezi. Kwa msingi huo neno sahihi ni ‘digiti’ badala ya digitali ambalo linatokana na ‘digital’ ambalo ni kisifa.
Darubini
Hiki ni chombo kinachowezesha kuona mbali … ‘kiona mbali’. Kwa lugha ya kigeni ni ‘telescope’ au ‘binocular’. Nneno hili ni tafauti na ‘hadubini’ ambalo ni ‘microscope’
Dhahama na Zahama
Neno sahihi ni zahama. Wanaotumia dhahama wameathirika kutokana na athari ya lugha yao ya asili ambapo herufi /dh/ na /z/ huchanganywa. Maana ya zahama ni vurugu, vurumai, fujo.
Durusu na durufu
Durusu ni kusoma na kupitia yale yaliyokwisha someshwa, kupitia tena maandishi yaliyoandikwa zamani kwa madhumuni ya kuyasahihisha au kuyaboresha ili kutoa chapisho jipya.
Durufu ni turubai.
Fedha, pesa, hela:
Haya ni maneno yenye maana moja lakini asili yake ni tofauti. Maneno yanayofanana na hayo ni kama fulusi, sarafu, faranga, dirihamu, ndarama. Hizi ni sarafu kwa ajili ya malipo zilizotumika siku za nyuma na baadaye noti zilichapishwa.
Maneno yaliyozoeleka zaidi ni fedha au pesa.
Fikiri, dhani:
Ijapokuwa maneno haya yanafanana kwa kiwango fulani, wako watu wanaoyachanganya na kuyatumia kama ni visawe. Tofauti kati ya maneno haya ni kuwa kufikiri ni kutumia akili ili kutatua jambo pia kutafakari au kuwaza. Kudhani ni kufikiri bila kuwa na uhakiki.
G
Ghairi:
Maana ya kughairi ni kubadili nia, acha mpango au jambo lililokusudiwa, bila kujali.
Ghushi/gushi: Neno sahihi ni ghushi kwa maana ya kudanganya kwa kuiga saini au maandishi. Maana nyingine ni bila kuzidi wala kupungua, tosha. Gushi si neno sahihi.
Gharamia, Gharimia:
Maneno haya yanatokana na neno gharama ni nomino. Kitenzi chake ni gharimia badala ya gharamia.
H
Hadubini
Hiki ni chombo kinachotumika kuona vitu visivyoonekana kwa macho. Neno la kigeni ni ‘microscope’. Watu wanalichanganya na darubini.
Hoteli, mahoteli:
Haya ni maneno yaliyokopwa kutoka neno ‘hotel’ lenye asili ya Kiingereza. Kwa misingi sahihi ya kisarufi hatuna wingi wa hoteli. Kwa hiyo kiambishi ma hakitakiwi. Hivyo sahihi ni hoteli kwa umoja na kwa wingi na wala si ‘mahoteli’
Hovyo, ovyo:
Wanaotumia neno hovyo wanakosea. Neno sahihi ni ovyo.
Hadhari, tahadhari:
Neno hadhari linachanganywa na tahadhari. Yanatofautiana katika matumizi. Hadhari ni uangalifu na tunasema kuchukua hadhari kabla ya athari/hatari. Maana yake ni kuepuka jambo ili usipatikane na matatizo, hatari au ubaya. Tahadhari linaweza kutumika kama kitenzi. Ni sahihi kusema, ‘Tunachukua hadhari” au tunatahadhari tusipatwe na janga.”
Hatima, hatma:
Katika kuandika tunatumia neno hatima ila tunapozungumza tunaweza kutumia hatma.
Harusi, arusi:
Maneno haya mawili yanakubalika kuwa sahihi ila kwa mazoea watu wengi hutumia zaidi neno harusi.
Hauhusiki; hautaki
Sahihi ni huhusiki; hutaki.
I
Idadi , nambari:
Idadi ni jumla ya mambo yanayohesabika. Nambari limetoholewa kutoka katika neno ‘number’. Namba lina maana ya tarakimu kama 1, 2, 3, 4, 5, n.k. Idadi ni namba au hesabu ya kujumlisha kwa mfano idadi kubwa ya Watanzania ni wakulima.
J
Jingine, lingine:
Maneno haya mawili ni sahihi na hutumika kulingana na muktadha. Aghalabu neno lingine hutumika zaidi.
Jinsi, jinsia:
Jinsi ni namna kitu kilivyo kama binadamu, wanyama, ndege, wadudu, n.k. Kwa lugha ya kigeni jinsi ni sex na jinsia ni gender. Tunasema ‘jinsi ya kike’ na wala si ‘jinsia ya kike’.
Zatiti, Dhatiti:
Neno sahihi ni zatiti ambapo dhatiti linatokana na athari ya lugha za kikabila. Kuzatiti maana yake ni kufanya kuwa madhubuti kwa shughuli fulani kama katika vita.
Kuwapo, kuwepo:
Neno sahihi ni kuwapo ijapokuwa kuwepo linatumika kimazoea.
Kiwanda, karakana:
Kiwanda ni mahali pa kuundia vitu mbalimbali. Katika kila sehemu ya kiwanda kuna sehemu zinazofahamika kama karakana. Kwa mfano kiwanda sehemu za kuundia samani, vioo, milango na madirisha. Sehemu hizi zinafahamika kama karakana. Kwa hiyo kiwanda ni mkusanyiko wa karakana mbalimbali.
Kampuni, makampuni:
Kampuni ni neno lililokopwa kutoka katika neno la Kiingereza ‘company’. Umoja na wingi ni kampuni. Kuweka kiambishi ma ni makosa.
Kurudufu:
Maana yake ni kunakili au kutoa nakala.
Kimbiza, wahisha :
Kukimbiza ni kufuata kitu au mtu kwa mbio nyuma yake au kufukuza.
Kuwahisha ni kutenda jambo mapema kabla halijaharibika. Kwa mfano majeruhi amewahishwa hospitali na wala siyo kukimbizwa hospitali.
Kuongea na kuzungumza:
Tofauti kati ya maneno haya ni ndogo sana. Kuongea ni kushiriki katika mazungumzo. Kuzungumza ni kujadili jambo kwenye mjadala, mkutano au baraza na kutoa hoja/maoni.
Kupeleka, kutuma:
Kupeleka ni kuchuka kitu au mtu na kumfikisha mahali fulani. Unaweza kumpeleka mtoto shuleni.
Kutuma ni kuagiza mtu kufanya jambo fulani. Mzazi anamtuma mtoto kwenda dukani. Kama tukiandika pelekea tunapata maana nyingine. Kwa mfano kupelekea ni kupeleka kwa niaba ya mtu mwingine. Mtoto amempelekea mzazi wake chakula shambani. Wakati mwingine waandishi huandika kupelekea kwa maana ya kusababisha. Haya ni makosa.
Kuyeyuka, kuyayuka:
Neno sahihi ni kuyeyuka kwa maana ya kugeuka kwa kitu kigumu kuwa kioevu.
Kengeuka:
Kumfanya mtu afuate njia mbaya, tabia mbaya, kupotosha au kumfanya mtu afuate njia mbaya.
Kutokana, kufuatia:
Maneno haya yanatumika kama vile yana maana moja kumbe ni tofauti kabisa. Wako wanaotumia maneno haya vibaya. Kwa mfano yako matumizi kama, “Kufuatia njaa kali inayowakabili wananchi wa Bariadi, serikali imepeleka magunia 200,000 ya mahindi’.
Sahihi ni, ‘Kutokana na njaa kali inayowakabili wananchi wa Bariadi, serikali imepeleka magunia 200,000 ya mahindi.’
Kwa jumla, kwa ujumla:
Matumizi ya maneno haya yanategemea maudhui. Tunasema,’kwa jumla maisha ni magumu’ lakini tunaweza kusema kwa ‘ujumla wake mvua imekithiri’.
M
Mazishi, maziko:
Maneno haya yanatokana na shina moja ambalo ni ‘zika’. Maana ya maneno haya ni tofauti.
Maziko ni kitendo cha kuzika maiti kwa maana ya kwenda makaburini kuzika. Mazishi ni matayarisho kabla ya maziko kwa mfano kutafuta sanda, kuchimba kaburi na pia shughuli nyingine za matanga na ada zake kama ufanyaji wa hesabu zilizotumika. Maziko yana muda maalumu ambapo mazishi hayana muda maalumu.
Masurufu, marupurupu:
Masurufu ni fedha anazopewa mtu aendaye safari ya kikazi kwa ajili ya matumizi ya huko aendako. Mhusika anaporudi hudaiwa stakabadhi ya kuonyesha jinsi alivyotumia fedha alizopewa. Kwa lugha ya kigeni ni imprest
Marupurupu ni fedha za ziada anazopewa mfanyakazi mbali na mshahara wake. Malipo ya marupurupu huweza kuwa ni malipo ya ajari na hudaiwi stakabadhi. Mifano ya malipo ya aina hii ni posho ya jamala, posho ya kujikimu, takrima au posho ya usumbufu. Kwa lugha ya kigeni ni allowance.
Majira:
Majira ni kipidi maalumu cha hali ya hewa. Neno lingine ni msimu. Yako majira ya mvua, kiangazi, ukame. Maana nyingine ni mwendo wa saa. Kwa mfano tunasema, ‘Saa yangu imepoteza majira’ lakini ni makosa kusema, ‘Nitawasili majira ya saa tano’. Sahihi ni kusema, nitawasili saa tano.’
Mkasa, maafa:
Maneno haya hudhaniwa kuwa ni sawa lakini yana maana tofauti. Maana ya mkasa ni tukio au jambo la huzuni au la kushtua.
Maafa maana yake ni janga, balaa au msiba. Kwa mfano, ‘Mji wetu umekumbwa na maafa ya mafuriko.’
Mtaalamu, mtaalam:
Sahihi ni mtaalamu.
Mtaala, mtalaa:
Watu wengu wamezoea kutumia neno mtaala lakini usahihi ni mtalaa.
Mashtaka, mashitaka:
Neno sahihi ni mashtaka na kama ni kitenzi ni shtaki.
Makala haya, makala hii.
Sahihi ni makala haya.
Mahali, mahari.
Mahali ni sehemu ambapo mtu au kitu huweza kukaa.
Mahari ni fedha au mali inayotolewa na mwanamume na kupewa mwanamke au wazazi wa mwanamke anayeolewa.
Maneno haya yanatofautiana kutokana na kuchanganya herufi /L/ na /r/
Mkongwe: nguli
Maana ya mkongwe ni mzee sana, aghalabu asiyejiweza. Nguli ni mtu jasiri au shujaa
Mkristo, Mkristu.
Maneno haya yana maana moja ila hutegemea na madhehebu. Madhehebu ya Kikatoliki hutumia Mkristu ambapo Waprotestanti hutumia Mkristo.
Mtazamo, mtizamo:
Neno sahihi ni mtazamo.
Maskini, msikini:
Neno sahihi ni maskini.
Muafaka, mwafaka:
Sahihi ni mwafaka
Makandarasi, wakandarasi:
Sahihi ni makandarasi.
Mwongozo, muogozo:
Neno sahihi ni mwongozo.
Mashaka, shaka:
Haya ni maneno mawili tofauti. Shaka maana yake wasiwasi, hali ya kutokuwa na uhakika wa jambo, hatihati.
Mashaka mambo magumu, tabu, dhiki au adha.
Masilahi , maslahi:
Neno sahihi ni masilahi.
Mjumbe: jumbe:
Sahihi ni mjumbe yaani mtu anayewakilisha mtu au watu wengine kama wakala au mwakilishi. Pia mtu anayewasilisha habari fulani. (Mjumbe hauawi).
N
Nyauka, kauka
Kunyauka ni kufifia kwa sababu ya jua au ukame.
Kauka nu kutoka maji na kuwa kavu au gungumka.
Najisi:
Uchafu unaoweza kumkirithi mtu. Pia kutengua tohara ya mtu au kitu kwa kukichafua. Vilevile kujamiiana na mtu bila ridhaa yake kama ni mtoto na kubaka kama ni mtu mzima.
O
Ofisa, afisa:
Neno sahihi ni ofisa linalotokana na utohozi wa neno kutoka lugha ya Kiingereza ‘officer’.
Onyesha onesha:
Kwa muda mrefu kumekuwa na mazoea ya kutumia neno onyesha badala ya onesha kwa maana ya kusababisha kuonekana. Hata hivyo onesha linatokana na neno ona kwa maana ya kutambua kitu kwa kutumia macho au kitu kwa hisia za mwili. Onyesha chimbiko lake ni ‘onya’ yaani kuasa ua kutahadharisha.
P
Pasa, pasha:
Maneno haya yanakaribiana katika matamshi lakini hayafanani. Pasa ni kuwajibika, kulazimika. Kwa mfano. ‘Inanipasa kuitunza familia yangu.
Pasha ni kusababisha kupata kitu au kuenea kwa kitu. Tunapasha habari au tunapasha moto. Kupashana habari ni kueneza taarifa au kuitangaza habari.
Pokea, pokelea:
Kupokea ni kitendo cha kupata kitu kutoka kwa mtu mwingine, kukaribisha au kulaki. Kumpokelea kitu au mtu ni kupokea kwa niaba ya mtu mwingine. Kwa hiyo mgeni hupokewa maana yake ni kukaribisha.
Pacha, mapacha:
Neno sahihi ni pacha ijapokuwa watu wamezoea neno mapacha.
Padri, padre:
Neno sahihi ni padri.
Runinga, luninga: Sahihi ni runinga
Rufaa, rufani:
Siku za nyuma maneno haya yalitofautishwa lakini siku hizi yanatumika kwa maana moja. Kwa hakika neno rufaa likitumika kama kisifa lina maana ya chombo cha juu cha kutoa uamuzi wa mwisho. Tuna hospitali za rufaa au mahakama za rufaa.
Njano, manjano:
Kwa mazoea tunatumia njano badala ya manjano na tofauti yake ni ndogo. Hata hivyo ipo rangi ya njano na pia ipo homa ya manjano.
R
Rundo, lundo:
Kutokana na athari za lugha za asili inakuwa vigumu kutofautisha maneno haya mawili kwani wanashindwa kutofautisha kati ya herufi /l/ na /r/.
Kwa usahihi neno rundo ndilo linalokubalika. Yapo maneno kama kurundika, kurundikana.
S
Saini, sahihi:
Neno saini limetokana na lugha ya Kiingereza sign. Tunasoma, ‘Tanzania na Uingereza wamesaini mkataba wa shilingi 300 milioni kuimarisha elimu.’ Hapa kuna makosa.Tunatakiwa kuandika,’Tanzania na Uingereza watiliana saini mkataba…’ au ‘wamewekeana saini’ na siyo wamesaini.
Swala, sala:
Maneno haya mawili yanatumika kulingana na ibada kwa madhehebu mbalimbali. Katika ibada kwa Waislamu wanatumia swala (Wanaswali). Kwa upande wa Wakristo wanatumia neno sala (wanasali).
Sheria, sharia:
Katika maandishi enzi za ukoloni neno lililotumika ni sharia lakini Kamati ya Kiswahili ya Afrika ya Mashariki ilisanifu neno hili na kuwa sheria. Hata hivyo wenzetu wa Visiwani wanaendelea kutumia sharia badala ya sheria.
Soko, gulio:
Soko maana yake ni mahali penye mkusanyiko wa watu wanaonunua na kuuza bidhaa za rejareja. Gulio ni soko linalofanya shughuli zake mara moja kwa juma. Liko neno chete lenye maana na gulio kwa hufanya shughuli zake mara moja kwa wiki.
Skuli, shule:
Haya ni maneno yenye maana moja ila tofauti ni asili ya maneno hayo. Neno shule linatokana na Kijerumani (Schule) na skuli linatokana na Kiingereza – (school). Tanzania Bara linatumika shule na Visiwani ni skuli.
Shaka, mashaka:
Shaka ni neno lenye maana ya kutokuwa na uhakika, kuwa na wasiwasi wa jambo, hatihati, wahaka.
Mashaka ni hali ya kuashiria mambo magumu yanayomfika mtu katika maisha, tabu, dhiki, adha, n.k.
Shehe, Shekhe, Sheikh:
Maneno haya matatu yana maana moja ila tahajia yake ni tofauti. Neno linalotumika zaidi ni ‘shekhe’.
T
Tuma, peleka:
Neno kutuma linatumika kwa maana ya kupeleka. Haya ni makosa. Maana ya kutuma ni kuagiza, kuamuru au kumtaka mtu afanye jambo. Kwa mfano mzazi huwatuma watoto kufanya jambo fulani. Naye Rais humtuma waziri wake kupeleka salamu au barua kwa kiongozi mwenzake.
Kupeleka ni kuwasilisha mtu au kitu mahali fulani. Mzazi anampeleka mwanaye shuleni.
Tangu, tangia:
Neno sahihi ni tangu. Neno tangia linatokana na lahaja mojawapo ya Kiswahili na halikusanifiwa.
Tahayari, tahayuri:
Tahayari ni kitenzi. Maana yake ni kuona haya au fedheha. Pia kuingiwa na hofu.
Tahayuri ni nomino na maana yake ni kuona haya baada ya kutenda jambo au kufikwa na jambo la fedheha.
Tegemea, tarajia, tazamia:
Kutegemea maana yake ni kushikilia, kuegemea au kuzuiliwa.
Kutarajia na kutazamia yana maana moja yaani kutumainia kupata au kufanya jambo.
Tazama, tizama:
Neno sahihi ni tazama.
U
Uamuzi, maamuzi:
Neno sahihi ni uamuzi
Uchaguzi, chaguzi:
Neno uchaguzi ndilo sahihi. Vivyo hivyo kwa utafiti na tafiti. Neno sahihi ni utafiti na si kinyume chake.
Ununuzi, manunuzi:
sahihi ni ununuzi
Upungufu, mapungufu
Neno sahihi ni upungufu.
Ujumbe, jumbe:
Neno sahihi ni ujumbe
Ushirikiano, mashirikiano:
Neno sahihi ni ushirikiano
Uzito, uzani:
Maneno haya yanayofanana katika maana. Hata hivyo, uzito una maana nyingine ya ziada yaani kuwa na umuhimu wa jambo. Kwa mfano tunasema, ‘Serikali imeweka uzito katika suala la kuongeza uchumi.’
Vyema, vema:
Neno sahihi ni vyema.
W
Waislamu, Waislam:
Tahajia sahihi ni Waislamu.
Warsha, kongamano.
Warsha ni mahali wataalamu wa fani fulani hujumuika na kujadili masuala kadhaa ya kitaaluma. Lengo ni kupata mwafaka wa jambo.
Kongamano ni mkusanyiko wa watu wanaojadili jambo fulani la kuelimishana.
Wakala, wakili:
Wakala ni chombo chenye madaraka ya kusimamia jambo fulani. Kwa mfano tuna wakala wa meli, wakala wa mazao, wakala wa biashara, n.k.
Wakili ni mwanasheria anayemtetea mshtaki au mshatakiwa au mtu anayepewa uwezo na mtu mwingine kusimamia mashauri yake. Pia anaweza kuwa ni dalali.
Wasilisha, wakilisha:
Kuwasilisha ni kufikisha kitu mahali fulani. Wakilisha ni kufanya jambo kwa niaba ya mtu mwingine. Ni makosa kusema kuwa, Juma amewakilisha barua ofisini. Sahihi ni kusema, Juma amewasilisha barua ofisini.
Wasia, wosia:
Neno sahihi ni wasia kwa maana ya maagizo anayotoa mtu kwa watu wake ili yazingatiwe baada ya kifo chake. Neno lingine ni usia.
Wehuka, weuka:
Neno sahihi ni wehuka na shina lake ni wehu. Maana ya wehu ni kutokuwa na akili timamu na na hali hii hukaribia kuwa uwenda wazimu.
Y
Yeyote, yoyote:
Maneno haya yanatofautiana katika maana.
Tunasema mtu yeyote na mazingira yoyote. Kwa hiyo hutegemea na muktadha.
Pamoja na tofauti katika matumizi ya maneno mbalimbali, ipo miundo au vifungu vya maneno ambavyo hutumika kwa makosa.
Angalia mifano ifuatayo:
Pembeni ya: pembeni na.
Sahihi ni kuandika pembeni ya: Gari jingine: gari lingine. Sahihi ni gari lingine.
Nyumba ingine: nyumba nyingine.
Sahihi ni nyumba nyingine.
Kwamba:ya kwamba.
Sahihi ni kwamba.
Kuelekea Arusha: Kwenda Arusha.
Sahihi ni kwenda Arusha.
Bila ya mashine: bila mashine.
Sahihi ni bila mashine.
Mbali ya: mbali na.
Sahihi ni mbali na.
Hajaja, hajafika, hajakuja.
Sahihi ni hajaja.
Hajaondoka: hakuondoka.
Sahihi ni hajaondoka. Soka la : soka ya.
Sahihi ni soka la.
Karibu nianguke: sahihi ni nusura nianguke au almanusura nianguke.
Mwisho wa siku: mwishowe.
Sahihi ni mwishowe, hatimaye.
Kusafiri na ndege:
Sahihi ni kusafiri kwa ndege.
Anayekwenda kwa jina la… Sahihi ni anayefahamika kwa jina la …
Akizungumza kwa njia ya simu.
Sahihi ni akizungumza kwa simu.
Mke wa Rais Kikwete, Salma: Sahihi ni Salma, mke wa Kikwete.
Maiti hizo: maiti hao
Sahihi ni maiti hao.
Majambazi hao: majambazi hayo.
Sahihi ni majambazi hao.
Mchezo wa ngumi: sahihi ni ngumi.
Mchezo wa soka: Sahihi ni soka.
Makinda ya Kiafrika yatikisa Ulaya:
Sahihi ni Makinda wa Kiafrika watikisa Ulaya.
Miamba 32 yapangiwa makundi: Sahihi ni miamba 32 wapangwa katika makundi.
Alisubiri mpaka jioni: Sahihi ni alisubiri hadi jioni.
Rais aliwasili na ndege: Sahihi ni Rais aliwasili kwa ndege.
ASANTE SANA Mwl Stephen Maina
Wasiliana naye kwa: stephenjmaina@yahoo.com
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 2 Guest(s)