Historia ya Kiswahili Nchini Rwanda: Kielelezo cha Nafasi ya Utashi wa Kisiasa katika Ustawi wa Lugha ya Kiswahili
Wallace Mlaga
Ikisiri
Makala hii inajikita kuonesha namna ambavyo utashi wa kisiasa umekuwa na umuhimu katika ustawi wa lugha ya Kiswahili nchini Rwanda. Ili kuonesha vema kuwapo kwa utashi wa kisiasa, hususan katika zama za sasa, makala inaitalii historia fupi ya Kiswahili nchini Rwanda, kuanzia kipindi cha ukoloni mpaka sasa. Makala inatambua zama za sasa kuwa zinaanzia mara baada ya mauaji ya kimbari (mwaka 1994) dhidi ya Watutsi hadi sasa. Ni katika kipindi hiki, ndipo mdhihiriko wa utashi wa kisiasa unabainishwa kwa mifano. Makala inabainisha pia kuwa ili kuwe na utashi wa kisiasa, lazima ziwepo sababu za msingi za kuleta utashi huo wa kisiasa. Pia inabainisha kuwa hata baada ya utashi wa kisiasa kuwapo, lazima kuwe na sababu zitakazohakikisha utashi huo wa kisiasa unaendelea kuwapo. Mwishoni kabisa makala inaonesha changamoto zinazokabili ustawi wa Kiswahili nchini Rwanda pamoja na mapendekezo ya nini kifanyike katika kutatua changamoto hizo.
1.0 Utangulizi
Kiswahili ni lugha ya taifa ya nchi za Tanzania na Kenya. Pia, ni lugha ya mawasiliano mapana ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ni lugha ambayo imeenea katika maeneo mbalimbali duniani. Kiswahili pia ni mojawapo ya lugha kuu nne zinazotumika katika nchi ya Rwanda; lugha nyingine ni Kinyarwanda, Kifaransa na Kiingereza. Mohochi (2011) anaeleza kuwa lugha ya Kiswahili bado inakabiliwa na vipingamizi vingi kikiwemo kutothaminiwa na viongozi wa serikali. Hiki ni kiashiria muhimu cha kukosekana kwa utashi wa kisiasa. Utashi wa kisiasa ni nini? Kabla hatujajibu swali hili ni muhimu kubainisha muundo wa makala hii. Makala hii imegawanyika katika sehemu kuu sita: utangulizi, nadharia na mbinu za utafiti, historia fupi ya Kiswahili nchini Rwanda, utashi wa kisiasa hivi sasa na sababu za kuwapo kwake, kudhihirika kwa utashi wa kisiasa nchini Rwanda, na hitimisho. Pia, baadhi ya sehemu hizi kuu zimegawanyika katika vijisehemu vidogovidogo.
Utashi wa kisiasa kwa mujibu wa Post na wenzake (2008) ni uungwaji mkono na viongozi wa kisiasa ambao husababisha mabadiliko ya kisera. Pia, wanaeleza zaidi kwamba utashi wa kisiasa hudhihirishwa na uungwaji mkono mpana wa viongozi kwa ajili ya mabadiliko. Aidha, wataalamu hawa pamoja na Charney (2009), wanabainisha kuwa utashi wa kisiasa ni dhana telezi. Kwa mujibu wa Post na wenzake (2008), wananadharia na watafiti mara nyingi huitumia dhana ya utashi wa kisiasa pale tu wanapomulika vipengele vinavyohusiana na utayari, kujihusisha, au kutojihusisha kwa serikali. Katika makala hii utashi wa kisiasa unatumika pia kumulika vipengele vinavyohusiana na utayari, kujihusisha, au kutojihusisha kwa serikali kuhusiana na ustawishaji wa lugha ya Kiswahili.
Charney (2009) anaelezea kwamba utashi wa kisiasa ni nguvu isiyoonekana iliyopo katika vikundi vinavyoongoza vyama vya siasa au serikali, na nguvu hii ndiyo husukuma na kusababisha maamuzi ya kisiasa. Anaona kuwa utashi wa kisiasa ni muunganiko wa mambo matatu: maoni, mkazo, na umuhimu. Hii ina maana kwamba lazima yawepo maoni kuhusiana na suala fulani. Ijapokuwa sio maoni yote yanahusika na utashi wa kisiasa, maoni hayo lazima yawe yenye nguvu miongoni mwa jamii. Maoni yanaweza kuwa yenye nguvu au kuwekewa mkazo sana lakini bado yasifanikishe utashi wa kisiasa. Ili yafanikishe utashi wa kisiasa ni lazima yawe na umuhimu katika maamuzi ya umma. Maelezo haya ni ya muhimu hususan katika kubainisha sababu zinazoshikilia kuwapo kwa utashi wa kisiasa kuhusiana na lugha ya Kiswahili nchini Rwanda. Kutokana na utelezi wa dhana ya utashi wa kisiasa, ni vema kujiegemeza katika nadharia mahususi itakayotuongoza, sio tu katika namna ya kuielewa dhana hiyo, bali pia katika kuona udhihirikaji wa utashi wa kisiasa.
Katika kufanikisha utafiti huu, data zilikusanywa kwa kufanya uchambuzi matini pamoja na mahojiano na Afisa wa ukuzaji mitaala, mwalimu wa Kiswahili mzoefu katika shule za sekondari na chuo kikuu, na wanafunzi 5 wa programu ya Kiswahili Hatua ya Awali.
2.0 Nadharia ya Utashi wa Kisiasa na jinsi Inavyohusiana na Sera ya Lugha na Upangaji Lugha
Ili kubainisha kuwapo au kutokuwapo kwa utashi wa kisiasa tunaweza kutumia mojawapo ya nadharia tatu kuhusiana na ufanyaji wa maamuzi wa serikali. Nadharia hizi zinafafanuliwa na Graham Allison na Philip Zelikow (1999) katika andiko lao la Essence of Decision: Explaining the Cuban Missile Crisis, kama wanavyonukuliwa na Post na wenzake (2008). Nadharia tatu wanazozijadili ni: Nadharia ya Mtendaji Razini, Nadharia ya Siasa za Kiserikali, na Nadharia ya Tabia ya Kitaasisi. Kati ya nadharia hizi tatu, Nadharia ya Mtendaji Razini, ndiyo tunayoona inafaa. Katika nadharia hii, ufanyaji wa maamuzi ya serikali hutazamwa kuwa ni kitendo cha kirazini; kikiegemea katika uelewa wa mtendaji wa hali iliyopo, malengo ya mtendaji, na matokeo tarajiwa ya uchaguzi wa sera.
Fasili za sera ya lugha na upangaji lugha1 zinadhihirisha kufaa kwa nadharia hii. Weinstein (1990:6) akirejelewa na Niyibizi (2014) anafasili sera ya lugha na upangaji lugha kuwa hurejelea “uchaguzi na maamuzi ya kimakusudi ya muundo wa lugha na/au matumizi ya lugha yanayofanywa na taasisi (serikali) ili kutatua matatizo ya lugha.” Katika kutofautisha sera ya lugha na upangaji lugha, Cooper (2009) akirejelewa na Niyibizi (2014), anabainisha kuwa sera ya lugha mara nyingi hurejelea malengo ya upangaji wa lugha. Pia, Niyibizi (2014) anaona kuwa upangaji lugha ni jitihada za muda mrefu na za makusudi zinazoendelezwa na kuidhinishwa na serikali kubadilisha matumizi ya lugha katika jamii kwa malengo ya kutatua matatizo ya mawasiliano.
Hii ina maana kwamba hakuna uamuzi wowote kuhusiana na lugha unaofanyika pasipo uamuzi wa kimakusudi wa serikali. Hii ndiyo sababu ya kuonesha namna ambavyo historia ya Kiswahili nchini Rwanda ni kielelezo sahihi cha nafasi ya utashi wa kisiasa katika ustawi wa lugha ya Kiswahili. Utashi huu wa kisiasa katika lugha ya Kiswahili nchini Rwanda unadhihirika vema tunapojiegemeza katika aina mbili kati ya nne za upangaji lugha2. Aina hizo mbili ni upangaji wa lugha kihadhi na upangaji wa upataji lugha. Upangaji wa lugha kihadhi hufasiliwa kama utaratibu wa kuzipatia lugha zilizopo dhima mbalimbali. Upangaji wa upataji lugha ni uwekaji wa mikakati mbalimbali ya kufanikisha uongezaji wa idadi ya watumiaji wa lugha. Hii ni tofauti na upangaji wa lugha kihadhi ambao hujikita zaidi katika kuongeza matumizi ya lugha. Upangaji wa upataji wa lugha huhusisha serikali kuongeza fursa zitakazochochea watu kujifunza lugha husika. Pia, upangaji wa upataji lugha huweza kujitokeza kupitia uanzishwaji wa programu mbalimbali za kufundisha lugha.
Utashi wa kisiasa juu ya lugha ya Kiswahili uliopo sasa nchini Rwanda unaweza kufahamika vema zaidi kwa kuitalii kwa kifupi historia ya Kiswahili nchini humo. Hii itatuwezesha kutambua vipindi ambavyo utashi wa kisiasa kwa Kiswahili haukuwapo na kubaini kuwapo kwa utashi wa kisiasa katika kipindi hiki cha sasa. Sehemu inayofuatia inaelezea historia fupi ya Kiswahili nchini Rwanda.
3.0 Historia Fupi ya Kiswahili nchini Rwanda
Historia ya Kiswahili nchini Rwanda inaweza kutazamwa katika vipindi vikuu viwili: wakati wa ukoloni na baada ya ukoloni. Kipindi cha ukoloni kimegawanyika pia katika vipindi viwili ambavyo ni wakati wa utawala wa Wajerumani na utawala wa Wabelgiji. Kipindi cha baada ya ukoloni nacho kimegawanyika katika vipindi viwili ambavyo ni kuanzia mwaka 1979 – 1994 na baada ya mauaji ya kimbari. Vipindi hivi vyote vinaonesha ama kuwapo au kutokuwapo kwa utashi wa kisiasa dhidi ya Kiswahili. Pale ambapo kuna utashi wa kisiasa, lugha ya Kiswahili inaonekana kustawi sana.
3.1 Kipindi cha Ukoloni
Nchi ya Rwanda ilitawaliwa na watawala wawili wa kikoloni: Mjerumani kuanzia mwaka 1898 – 1916 na Mbelgiji kuanzia mwaka 1916 – 1962. Serikali hizi mbili kila moja ilikuwa na uamuzi wa kipekee kuhusiana na lugha ya Kiswahili pamoja na lugha nyingine nchini Rwanda. Uamuzi huo ndiyo msingi wa kuwapo au kutokuwapo kwa utashi wa kisiasa katika kipindi hiki.
3.1.1 Wakati wa Utawala wa Wajerumani
Mtawala huyu ndiye aliyeitumia lugha ya Kiswahili kwa mara ya kwanza kama lugha rasmi na lugha ya utawala nchini Rwanda (Kimenyi, 2003; MINEDUC, 2010; Niyibizi, 2014). Hii haina maana kwamba Kiswahili kililetwa Rwanda kwa mara ya kwanza na Wajerumani kwani lugha ya Kiswahili ilikuwapo nchini humo hata kabla ya utawala wa Wajerumani. Hii ni kutokana na ukweli kwamba misafara ya biashara kutoka pwani ya Afrika Mashariki ilifika Rwanda na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo kabla ya utawala wa Mjerumani (Niyibizi, 2014).
Kutokana na Kiswahili kuwa lugha rasmi na lugha ya kiutawala, shule nyingi katika kipindi hiki zilifundisha lugha ya Kiswahili na masomo mengine (Republic of Rwanda, 1999; Kimenyi, 2003)3. Lugha za Kiswahili na Kijerumani ndizo pekee zilizofundishwa kama somo katika shule ya kwanza kabisa nchini Rwanda iliyojulikana kama Shule ya Nyanza. Shule hii ilianzishwa na Wajerumani katika eneo la Nyanza kwenye Jimbo la Kusini (Niyibizi, 2014). Utashi wa kisiasa wa utawala wa Wajerumani unaonekana katika kuipangia lugha ya Kiswahili dhima maalumu. Pia serikali hii ya kikoloni ilishiriki katika kuongeza idadi ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili nchini humo. Hili lilifanyika kwa kuhakikisha kuwa Kiswahili kinafundishwa pia katika shule zilizokusudiwa kwa ajili ya watoto wa viongozi. Jitihada hizi ziliifanya lugha ya Kiswahili kupata hadhi kubwa miongoni mwa watumiaji wake na jamii yote kwa ujumla katika koloni hili la Mjerumani. Utashi huu wa kisiasa uliopendelea lugha ya Kiswahili ulichochewa zaidi na Rwanda kuwa sehemu ya koloni la Mjerumani la Afrika Mashariki. Katika makoloni mengine, hususan Tanganyika, lugha ya Kiswahili ilikuwa imestawi zaidi na hivyo kumlazimisha Mjerumani aitumie kama lugha ya utawala na mawasiliano rasmi.
3.1.2 Wakati wa Utawala wa Wabelgiji
Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, Mjerumani alipoteza himaya zake. Hii ilitokana na kushindwa vita. Hivyo, Rwanda ilikoma kuwa chini ya utawala wa Wajerumani baada ya vita hivi, na utawala wa Ubelgiji ukachukua nafasi. Mfalme wa Ubelgiji akawa mtawala mpya wa Rwanda kuanzia mwaka 1916 – 1962. Mabadiliko haya yalikuwa na athari kubwa kwa lugha ya Kiswahili. Athari hiyo ilitokana na marufuku iliyowekwa dhidi ya lugha ya Kiswahili. Marufuku hii ilihusu kukataza lugha ya Kiswahili kutumika kama lugha rasmi na lugha ya utawala. Kufikia mwaka 1929, Kiswahili kiliondolewa kuwa lugha ya kufundishia katika shule za msingi na sekondari. Hoja hii inadhihirishwa na Ntawigira (1997) kama anavyonukuliwa na Kimenyi (2003: 4) akisema:
Mnamo mwaka wa 1929 Kiswahili kilifutwa kama lugha ya kufundishia katika shule za msingi na zile za upili… Mnamo mwaka 1929, mkaguzi wa ufundishaji wa kikoloni kutoka Leopordiville (Kinshasa), alisema kwamba hakukuwepo fursa ya kuendelea kutumia Kiswahili.
Dondoo hili linaonesha namna Wabelgiji walivyoshiriki kurudisha nyuma ustawi mkubwa wa lugha ya Kiswahili uliokuwa umefikiwa katika kipindi cha utawala wa Wajerumani. Dondoo hili pia linaonesha kwamba ndani ya miaka 13 ya utawala wao Wabelgiji waliweza kukiondoa Kiswahili kama lugha ya kufundishia. Je, kwa nini utawala wa Wabelgiji ulikosa utashi wa kisiasa wa kustawisha Kiswahili nchini Rwanda?
Marufuku hii inaweza kutokana na mambo mawili. Jambo la kwanza ni kutaka kuonesha kwa vitendo mabadiliko ya kiutawala. Hivyo huenda ilikusudiwa kuonesha kuwa sasa kuna mabadiliko ya kiutawala ili kuleta utii zaidi kwa utawala mpya. Utaratibu huu wa mabadiliko ya lugha, kupitia sera za lugha, umejitokeza katika nchi nyingi, kwa nia ya kujitenga na kale na kujenga taswira mpya ya mwanzo mpya (Steflja, 2012). Jambo la pili linahusiana na kuihusisha au kuifungamanisha lugha ya Kiswahili na dini ya Kiislamu (Bujra, 2002). Wabelgiji kwa kiwango kikubwa walifungamana na dini ya Kikristo, hususan madhehebu ya Kikatoliki. Jambo hili lilitosha kuwa sababu ya msingi ya kuipiga marufuku lugha ya Kiswahili.
Baada ya Kiswahili kuondoshwa katika mfumo wa elimu, Kifaransa kilipewa hadhi ya juu na kuwa lugha rasmi na lugha ya kiutawala. Lakini pia kilianza kutumika kama lugha ya kufundishia katika shule (taz. Niyibizi, 1980 katika Niyirora, 2013:5). Hivyo lugha ya Kiswahili ilianza kupoteza hadhi yake na ilianza kutumiwa na watu duni au watu wa chini kama vile Waislamu, vibarua, na wafanyabiashara (Kimenyi, 2003). Waislamu katika kipindi cha utawala wa Wabelgiji walikuwa katika kipindi kigumu kutokana na Uislamu wao. Hawakupata fursa ya kupata elimu na hivyo kukosa kuajiriwa katika kazi mbalimbali za serikali ambazo zilionekana kuwa na hadhi ya juu. Kutokana na matumizi ya Kiswahili kushamiri miongoni mwa Waislamu, ambao walitazamwa kama watu duni, lugha ya Kiswahili pia ikajikuta ikitazamwa kama lugha duni.
Sababu nyingine ya kushuka kwa hadhi ya Kiswahili ni ukatili wa “Abasemyi” (Wanyarwanda wachache waliokuwa na uwezo wa kuzungumza lugha ya Kiswahili). Watu hawa walitumiwa na watawala wa Kibelgiji kama wakalimani kufanikisha mawasiliano kati ya watawala na wenyeji. Wakalimani hawa walitumiwa na Wabelgiji kuanzia mwaka 1916 hadi 1919. Katika kipindi hiki, walijipatia utajiri mkubwa kutokana na marupurupu yao; pia, walijihusisha katika kuwapiga na kuwaibia raia (Republic of Rwanda, 1999). Hivyo basi, kwa mazingira haya ilikuwa ni rahisi lugha ya Kiswahili kuhusishwa na unyang’anyi. Kutokana na uamuzi wa kimakusudi wa serikali ya Wabelgiji kuhusiana na sera ya lugha, lugha ya Kiswahili haikupata nafasi ya kustawi. Ijapokuwa Kiswahili kiliendelea kuwapo Rwanda kutokana na Uislamu, biashara, na kuzungukwa na watumiaji wa lugha ya Kiswahili, kipindi hiki kinatajwa kama kipindi cha udumavu wa Kiswahili nchini humo.
3.2 Kipindi cha baada ya Uhuru
Kipindi cha baada ya uhuru kinaweza kugawanywa katika vipindi vikuu viwili: kipindi cha kuanzia mwaka 1979 – 1994, na kipindi cha baada ya mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994. Tunaangalia historia hii ya Kiswahili kuanzia mwaka 1979 na wala sio kuanzia mwaka 1962, ambapo Rwanda ilipata uhuru, kutokana na ukweli kuwa Kiswahili hakikupewa nafasi yeyote katika nchi ya Rwanda huru kabla ya mwaka 1979 (Niyibizi, 2014). Kipindi cha baada ya mauaji ya kimbari kinaanza kuanzia baada ya mwaka 1994 – 2016. Hivyo basi, kipindi hiki cha pili ndicho tunachokitazama kama kipindi cha zama hizi za sasa. Makala hii inakiangazia kipindi hiki kama kielelezo cha nafasi ya utashi wa kisiasa katika ustawi wa lugha ya Kiswahili nchini Rwanda.
3.2.1 Kipindi cha Kuanzia 1979 – 1994
Kipindi cha mwaka 1979 – 1994 kinaweza kutazamwa kama kipindi cha mvuvumko wa ustawi wa Kiswahili nchini Rwanda. Baada ya Kiswahili kutokupewa kipaumbele kwa muda mrefu, kipindi hiki kinashuhudiwa kuwapo kwa kustawi na kuchipuka upya kwa lugha hii. Mathalani, kuliibuka jitihada za makusudi za kustawisha Kiswahili katika nchi nzima ya Rwanda kama vile kuanzishwa kwa ushirikiano baina ya serikali ya Rwanda na ya Tanzania. Ushirikiano huu ulifanikisha kupatikana kwa walimu wa Kiswahili kutoka Tanzania. Makubaliano ya serikali za nchi hizi mbili yalifanyika mwaka 1977 na utekelezaji wake ulionekana kwa vitendo kuanzia mwaka 1979. Utekelezaji wa makubaliano haya ulihusisha kubadilishana walimu ambao walifanikisha Kiswahili kuanza kufundishwa nchini Rwanda kuanzia kidato cha pili mpaka kidato cha nne kwa wanafunzi wote. Baada ya hapo, wanafunzi waliosoma mchepuo wa lugha waliendelea na Kiswahili kuanzia kidato cha tano hadi kidato cha sita (Kimenyi, 2003). Pamoja na hayo, serikali ya Rwanda iliweka mkazo katika ufundishaji wa lugha ya Kiswahili. Somo la Kiswahili lilipewa saa nne kwa wiki. Wanafunzi walijifunza masuala ya sarufi, isimu, pamoja na ukalimani na tafsiri. Ukalimani na tafsiri ulihusisha lugha ya Kiswahili dhidi ya Kifaransa, Kiingereza, na Kinyarwanda.
Mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hiki ni pamoja na kuandikwa kwa vitabu mbalimbali vya Kiswahili4. Vitabu hivi viliendelea kutumiwa na baadhi ya walimu hadi miaka ya 2000 kabla ya Bodi ya Elimu ya Rwanda (REB) kufanikisha upatikanaji zaidi wa vitabu vya kufundishia na kujifunzia.
Jambo jingine la muhimu katika kipindi hiki ni kupatikana kwa wataalamu wazawa wa lugha ya Kiswahili ambao ni matunda ya kwanza ya walimu wa Kiswahili kutoka Tanzania. Wataalamu hawa wamekuwa na manufaa makubwa katika ustawi wa lugha ya Kiswahili nchini Rwanda.
3.2.2 Wakati wa baada ya Mauaji ya Kimbari
Kama tulivyobainisha katika sehemu iliyotangulia, kipindi hiki tunakitazama kama kielelezo cha utashi wa kisiasa katika kustawisha lugha ya Kiswahili. Serikali ya Rwanda katika kipindi hiki, hususan mwaka 1996 – 2016, imechukua hatua mbalimbali ambazo zimechangia ustawi wa lugha ya Kiswahili nchini humo. Hivyo basi, historia ya Kiswahili katika kipindi hiki inafafanuliwa kwa namna tofauti na sehemu zilizotangulia kama inavyobainika hapa chini.
4.0 Utashi wa Kisiasa Hivi sasa na Sababu za Kuwapo kwake
Tunaporejelea utashi wa kisiasa katika kipindi hiki (1996 -2016) tunajikita kuangalia namna serikali inavyoshiriki au kujihusisha na ustawishaji wa lugha ya Kiswahili nchini Rwanda. Kipengele cha pili katika sehemu hii kinahusika na sababu za kuwapo kwa utashi huo wa kisiasa. Tunakusudia kuonesha kwamba utashi wa kisiasa hauji tu kwa bahati mbaya bali hujengwa na mazingira sahihi.
4.1 Utashi wa Kisiasa 1996 – 2016
Katika kipindi hiki serikali inayoongozwa na chama cha RPF (Rwanda Patriotic Front) imefanya maamuzi mengi ya kisiasa yaliyochangia ustawi wa lugha ya Kiswahili nchini Rwanda. Tunasema ni maamuzi ya kisiasa kwa sababu masuala yote yanayohusiana na sera ya lugha na upangaji wa lugha huwa hayatenganishiki na maamuzi ya kisiasa. Katika kipindi hiki, serikali ilifanya mabadiliko ya sera ya lugha katika elimu mara mbili. Licha ya nyaraka za mabadiliko ya kisera kutoitaja lugha ya Kiswahili ni muhimu kujiegemeza katika miktadha ya mabadiliko hayo ili kuona ni hatua gani zilichukuliwa kuhusiana na Kiswahili.
Katika mabadiliko ya kwanza, serikali iliasili sera ya utatu lugha mnamo mwaka 1996. Lugha zilizohusika katika sera hii zilikuwa ni Kinyarwanda, Kifaransa na Kiingereza. Pia mgawanyo wa matumizi ya lugha hizi katika elimu ulibainishwa. Kwani ilikusudiwa kuwa, lugha hizi tatu zifundishwe kama masomo lakini pia kama lugha za kufundishia kuanzia shule za awali hadi vyuo vikuu. Ilikusudiwa kuwa Kinyarwanda kitakuwa lugha ya kufundishia katika shule za msingi wakati Kiingereza na Kifaransa zitakuwa lugha za kufundishia katika shule za sekondari na vyuo vikuu (Niyibizi, 2014). Ni bayana kuwa Kiswahili hakitajwi kabisa katika sera hii. Si hivyo tu, bali pia hata katiba ya Rwanda ya mwaka 1996, haihitaji lugha ya Kiswahili. Katiba hii inatambua lugha rasmi kuwa ni Kinyarwanda, Kiingereza na Kifaransa.
Hata hivyo si kwamba Kiswahili kilikuwa hakitumiki kabisa au hakipewi umuhimu katika baadhi ya maeneo. Mathalani, Kimenyi (2003:10) anabainisha umuhimu wa Kiswahili nchini Rwanda mara baada ya 1994; anaeleza kwamba “tangu mwaka 1996, shule nyingi za msingi kwenye mikoa inayopakana na Tanzania zilikuwa zikifundisha kwa lugha ya Kiswahili, na baadaye watoto walitahiniwa kwa lugha hiyo ili wachaguliwe kuendelea na elimu ya sekondari.” Dondoo hili linaonesha namna ambavyo serikali ilikuwa inatambua nafasi ya Kiswahili kwa watu wake. Licha ya kutokuwa lugha rasmi, wala lugha ya taifa, serikali iliruhusu baadhi ya shule zitumie lugha ya Kiswahili kama somo na kama lugha ya kutahinia wanafunzi. Aidha, mwaka huohuo wa 1996, serikali iliandaa muhtasari mpya wa kufundisha somo la Kiswahili kwa wanafunzi wa kidato cha nne hadi kidato cha sita5. Hii ni tofauti na Kiswahili kilivyokuwa kikifundishwa kabla ya kipindi hiki kama tulivyoona hapo awali (1979 -1994). Licha ya changamoto hii, jambo la muhimu ni kuonekana kwa utashi wa kisiasa katika kuiendeleza lugha ya Kiswahili zaidi ya maeneo yaliyopakana na Tanzania. Muhtasari huu ulidumu kuanzia mwaka 1996 hadi 2008. Baada ya hapo, yalifanyika mabadiliko ya elimu yaliyogusa pia lugha kuu nne zilizopo nchini Rwanda ambazo ni Kinyarwanda, Kiingereza, Kiswahili na Kifaransa (Steflja, 2012).
Ieleweke kwamba, katika muhtasari wa mwaka 1996, lugha ya Kiswahili ilikuwa inafundishwa kama somo kuanzia kidato cha nne hadi cha sita. Hivyo basi, wanafunzi walimaliza ngazi ya chini ya sekondari (kidato 1 – 3) bila kujifunza lugha ya Kiswahili. Katika mabadiliko ya pili ya sera ya lugha, ambayo yalifanyika Oktoba 2008, serikali ya Rwanda ilifanyia marekebisho sera ya utatu lugha iliyokuwapo. Katika mabadiliko haya, lugha tatu zilitambulika kama lugha za kufundishia. Kiingereza kwa mara ya kwanza kikatambulika kama lugha pekee ya kufundishia masomo yote na katika ngazi zote za elimu (elimu ya awali hadi chuo kikuu). Lugha za Kinyarwanda na Kifaransa zilifundishwa kama masomo kuanzia chekechea, shule za msingi na shule za sekondari (Niyibizi, 2014). Sera hii ilipaswa kutekelezwa kwa awamu, hususan katika kuhakikisha Kiingereza kinakuwa lugha ya kufundishia katika viwango vyote vya elimu hadi kufikia mwaka 2011. Ijapokuwa, utekelezaji ulienda tofauti na matarajio, kwa Kiingereza kuanza kutumika kama lugha ya kufundishia mara moja kuanzia mwaka 2009.
Licha ya sera ya lugha katika elimu wakati wa kipindi hiki kuongelea lugha tatu tu, bado serikali haikuacha kujihusisha na lugha ya Kiswahili. Kwa mfano, baada ya maboresho ya elimu mwaka 2008, serikali iliufanyia mabadiliko muhtasari wa Kiswahili wa mwaka 1996, na hivyo muhtasari mpya wa Kiswahili ulianza kutumika kuanzia wakati huo mpaka sasa kwa baadhi ya madarasa. Ni kwa baadhi ya madarasa kwa kuwa kuanzia Januari 2016 madarasa mengine yameanza kutumia muhtasari mpya wa 2015. Muhtasari huu umetokana na mtaala ulioegemezwa katika umahiri au uwezo. Ikiwa na maana kwamba, baada ya kufundishwa Kiswahili wanafunzi hao wanaweza kufanya au kutenda nini kutokana na hicho walichojifunza. Hivyo basi, kila somo linapimwa kufanikiwa au kutofanikiwa kwa kuangalia wanafunzi wanaweza kutenda nini na sio kuishia tu katika kile wanachojua au nadharia. Muhtasari huu mpya umepangwa kutekelezwa kwa awamu kwa kuanza na kidato cha kwanza na kidato cha nne.
Katika muhtasari wa mwaka 2008, Kiswahili kilipaswa kufundishwa kuanzia kidato cha kwanza mpaka kidato cha tatu; na pia katika kidato cha nne hadi kidato cha sita kwa wanafunzi wanaochukua mkondo wa lugha mchepuo wa Kiingereza, Kifaransa na Kiswahili (EKK). Mwaka 2013, serikali kupitia Bodi ya Elimu Rwanda (REB), ilianza mchakato wa kufanya mabadiliko makubwa ya mtaala wa elimu kwa shule za msingi na sekondari. Mchakato huu, umehitimishwa kwa kufanikisha uandaaji wa mtaala mpya wa elimu nchini Rwanda. Mtaala huu mpya umeegemezwa katika umahiri au uwezo wa mwanafunzi; ikiwa na maana ya kumjengea uwezo mwanafunzi ili aweze kutumia maarifa aliyoyapata. Muhtasari mpya wa Kiswahili ulipatikana mwaka 2015 na kuanza kutekelezwa kuanzia muhula wa kwanza wa masomo wa mwaka 2016, kwa kidato cha kwanza na kidato cha nne. Matarajio ni kwamba mwaka 2017 muhtasari huu mpya utaanza pia kutumika kwa kidato cha pili na cha tano. Kisha utaanza kutekelezwa kwa viwango vyote vya elimu mwaka 2018 pale ambapo kidato cha tatu na kidato cha sita vitakapoanza kuutumia muhtasari huu.
Kwa mtaala huu mpya, tunaweza kusema kuwa Kiswahili kimezidi kupiga hatua kwa kuongezewa idadi ya vipindi, kutoka kimoja kwa wiki mpaka vipindi viwili kwa kidato cha kwanza hadi cha tatu. Kwa upande wa kidato cha nne na sita, vipindi sasa vimekuwa ni vinane kutoka vile vinne vilivyokuwepo. Si hivyo tu, bali sasa, Kiswahili kinaanza kuwa somo la lazima ambapo litatahiniwa kwa wanafunzi wote kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha tatu. Hivyo basi, kutokana na hatua hizi ambazo serikali ilizichukua au kuidhinisha kuhusiana na Kiswahili, Kiswahili kimepata msukumo wa kisiasa wa kuweza kustawi kwa kiasi chake. Je, nini hasa sababu ya msukumo au utashi huu wa kisiasa mara baada ya mauaji ya kimbari?
4.2 Mambo Yaliyosababisha kuwapo kwa Utashi wa Kisiasa Kipindi hiki
Utashi huu wa kisiasa katika kipindi hiki unaweza kuelezwa kuwa ulisababishwa na mambo muhimu matatu: nguvu ya kundi la watu waliorejea Rwanda baada ya mwaka 1994, ushirikiano wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sababu hizi tatu zinafungamana pia na ustawi wa kijamii, kisiasa, na kiuchumi wa nchi ya Rwanda. Hivyo basi, serikali ilichukua uamuzi wa kuunga mkono jitihada za kustawisha Kiswahili kutokana na misukumo hiyo. Sababu hizi zinafafanuliwa kama ifuatavyo:
4.2.1 Nguvu ya Kundi la Watu Waliorejea Rwanda baada ya 1994
Katika mwaka wa 1959 na 1973 idadi kubwa ya Wanyarwanda walienda uhamishoni katika nchi mbalimbali. Nchi walizoenda ni pamoja na zile zinazotumia lugha ya Kiingereza, Kifaransa, na Kiswahili. Baada ya mwaka 1994, idadi kubwa ya Wanyarwanda waliokuwa nje ya Rwanda walirejea Rwanda. Hali hii ilisababisha kuwapo kwa mchanganyiko wa watu wanaotumia lugha tofauti. Staflja (2012) anakadiria idadi ya watu waliorudi mwanzoni ni kati ya 500,000 na 800,000. Katika kueleza msingi wa lugha ya Kiingereza kupata nafasi nchini Rwanda, Samuelson na Freedman (2010) wanaihusisha na harakati za ukombozi wa chama cha RPF6 kutoka uhamishoni katika nchi kama Uganda, Kenya, na Tanzania. Pia wanaelezea suala la kurejea nyumbani kwa Wanyarwanda waliokuwa uhamishoni katika nchi za Kenya, Burundi, Kongo na Tanzania. Licha ya kujiegemeza katika lugha ya Kiingereza, ni dhahiri kuwa Kiswahili pia kilipata nafasi miongoni mwa Wanyarwanda hawa waliporejea nyumbani. Hivyo basi, idadi kubwa ya watumiaji wa Kiswahili baada ya mwaka 1994 ilichangia sana katika kuisukuma serikali kufanya uamuzi wa kujihusisha na lugha ya Kiswahili nchini Rwanda.
4.2.2 Ushirikiano wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu
Ni muhimu ikafahamika kuwa, kabla Rwanda haijajiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2007, tayari serikali ya Rwanda ilikuwa imeshashiriki au kushirikishwa kwa namna mbalimbali katika mikakati ya ustawishaji wa lugha ya Kiswahili7. Mikutano ya Kikanda ya Nchi za Maziwa Makuu (yaani Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, na Burundi) iliyofanyika Kampala, Uganda mwaka 2002, na ule wa Dar es Salaam mwaka 2004, ni muhimu katika kueleza sababu ya kuwapo kwa utashi wa kisiasa katika ustawishaji wa lugha ya Kiswahili nchini Rwanda. Inaelezwa kuwa mkutano wa Kampala ulitanguliwa na kongamano lililoandaliwa na Mfuko wa Mwalimu Nyerere lenye anwani “Uimarishaji wa Mashirikiano ya Kikanda na Kuweka Agenda ya Millennia ya Utamaduni wa Amani, Umoja na Maendeleo ya Watu” (Kiango, 2002). Hivyo basi, maazimio ya kongamano hili yalisomwa mbele ya wakuu wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu. Miongoni mwa maazimio hayo ni “Kiswahili kinaweza kuchukua dhima ya kuwaunganisha watu katika kiwango cha kikanda. Hivyo Kiswahili kipewe hadhi ya kuwa lugha mawasiliano (lingua franca) ya kikanda. Pia, lugha nyingine zitakuwa na dhima katika kiwango cha kieneo, kitaifa, au kimataifa” (Kiango, 2002).
Maazimio haya huenda yalichochea utashi wa kisiasa, miongoni mwa viongozi wa ukanda huu wa Maziwa Makuu na Rwanda ikiwamo. Kwani katika mkutano wa mwaka 2004 wa Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu, viongozi walipendekeza kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha zinazotumika katika shughuli zote za mashirikiano katika ukanda huu. Hivyo basi, kuna uwezekano kabisa kuwa maazimio ya kongamano lililoandaliwa na Mfuko wa Mwalimu Nyerere 2002, na kusomwa mbele ya wakuu wa nchi katika mkutano wa Kampala, yalikuwa ni chachu ya lugha ya Kiswahili kupata nafasi ya kipekee kuingia katika mjadala, na hatimaye kuwa miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa wakuu wa nchi na serikali za Ukanda wa Maziwa Makuu mnamo mwaka 2004. Makubaliano yanafikiwa na wakuu wa nchi kwa kuridhia Azimio la Dar es Salaam. Azimio hili ni matokeo ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu uliofanyika tarehe 19 – 20, Novemba, 2004. Katika mkutano huu, wakuu wa nchi waliazimia kuweka jitihada zao kuhakikisha uwezeshaji wa kukifanya Kiswahili kuwa lugha tumizi au lugha ya mawasiliano katika Ukanda wa Maziwa Makuu. Azma hii ya wakuu wa nchi inapatikana katika kifungu namba 64 cha Azimio la Dar es Salaam8. Jambo jingine muhimu lililojitokeza katika mkutano huu ni azimio la uwekaji wa mikakati ya utekelezaji wa maazimio yote yaliyofikiwa. Kifungu namba 67 cha Azimio la Dar es Salaam kinaeleza kuundwa kwa Kamati ya Wizara Mtambuka ya Kanda, ikisaidiwa na Kamati ya Maandalizi ya Kanda, iliyosheheni uwakilishi kutoka makundi mbalimbali kama vile wanawake, vijana, wataalamu waliobobea, na wanachama mbalimbali wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali. Miongoni mwa majukumu ya kamati hii ni kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa maazimio mbalimbali yaliyofikiwa katika mkutano huu, hii ikiwa ni pamoja na yale yanayohusu lugha ya Kiswahili.
Si hivyo tu, utekelezaji wa kivitendo wa makubaliano kuhusu ustawishaji wa lugha ya Kiswahili unajitokeza katika Programu ya Kikanda ya Utekelezaji wa Masuala ya Kiutamaduni na Kijamii ya mwaka 2006. Katika programu hii, kazi mradi namba 4.2.3 inaeleza programu ya utekelezaji wa ustawishaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kama lugha ya mawasiliano au tumizi katika Ukanda wa Maziwa Makuu. Utangulizi wa programu hii unarejelea Azimio la Dar es Salaam kama msingi wa programu yenyewe lakini pia unatambua utashi wa kisiasa wa viongozi wa ukanda huu katika ustawishaji wa lugha ya Kiswahili. Ili kufanikisha azma iliyobainishwa na wakuu wa nchi, kazi mradi inabainisha lengo la jumla la mradi kuwa ni ukuzaji wa Kiswahili kama lugha ya mawasiliano katika Ukanda wa Maziwa Makuu. Hivyo basi, ushiriki wa rais wa Rwanda pamoja na viongozi wengine katika kuweka maazimio ya kuistawisha lugha ya Kiswahili unafaa kutazamwa kama sababu mojawapo ya kuwapo kwa utashi wa kisiasa katika kustawisha Kiswahili nchini Rwanda.
4.2.3 Ushirikiano wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
Jumuiya ya Afrika Mashariki inastahili kutazamwa kama nguzo kuu ya kuwapo kwa utashi wa kisiasa katika ustawishaji wa Kiswahili nchini Rwanda katika kipindi cha sasa. Utashi huu wa kisiasa unajitokeza zaidi baada ya Jamhuri ya Rwanda kuruhusiwa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki mnamo mwaka 2007. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mara baada ya kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ndipo pia utekelezaji wa ufundishaji wa Kiswahili kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha tatu kwa wanafunzi wote wa shule za serikali ukaanza kutekelezwa kuanzia mwaka 2008. Pia, inaelezwa kuwa mojawapo ya masharti ya Rwanda kukubaliwa kujiunga katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kukubali kutumia lugha ya Kiswahili (Kawoya, 2009:7).
Mukuthuria (2006) anaeleza kuwa kifungu cha 19 (d) cha mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kinasisitiza suala la ukuzaji na uendelezaji wa lugha za asili hususan Kiswahili kama lugha ya mawasiliano ya ukanda (lingua franca). Hii ina maana kwamba, wakati Rwanda inakusudia kuingia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, tayari ilikuwa inajua umuhimu na nafasi ya Kiswahili kama lugha mawasiliano katika ukanda huu. Utashi wa kisiasa katika masuala ya lugha, unaambatana na masuala ya faida za kijamii, kisiasa, na kiuchumi kwa lugha husika. Katika kuweka mkazo wa faida za kiuchumi, Steflja (2012) anaeleza kuwa maafisa wa Rwanda wanaeleza kuwa lugha yoyote yenye manufaa ya kiuchumi hata kama ni Kihispaniola itapewa kipaumbele. Katika sehemu inayofuatia, mdhihiriko wa utashi wa kisiasa katika ustawishaji wa lugha ya Kiswahili unajadiliwa.
5.0 Mdhihiriko wa Utashi wa Kisiasa nchini Rwanda
Sehemu hii inajadili mambo muhimu manne ambayo ni: mdhihiriko wa kisiasa, sababu za kuendelea kuwapo kwa utashi wa kisiasa, changamoto zilizopo kuhusiana na lugha ya Kiswahili, na mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto hizo.
5.1 Mambo Yanayodhihirisha Utashi wa Kisiasa
Mdhihiriko wa utashi wa kisiasa unajitokeza katika hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ya Rwanda kuhusiana na lugha ya Kiswahili. Hatua hizi zinaweza kutazamwa kuanzia mwaka 1996. Kuanzia mwaka 1996, kama ilivyoelezwa hapo awali, Kiswahili kilianza tena kufundishwa nchini Rwanda. Katika kipindi hiki, Kiswahili kilifundishwa kuanzia kidato cha nne. Hii ilileta changamoto kubwa kutokana na ugumu uliopo katika kumfundisha mwanafunzi anayekutana na Kiswahili kwa mara ya kwanza katika kiwango hiki.
Maboresho ya elimu ya mwaka 2008 yaliwezesha lugha ya Kiswahili kuanza kufundishwa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tatu. Pia kukawapo na mchepuo unaohusisha somo la Kiswahili kwa wanafunzi wa kidato cha nne mpaka cha sita. Hatua hii isingewezekana kutekelezwa bila ya kuwapo kwa utashi wa kisiasa.
Uamuzi huu chanya katika ustawi wa lugha ya Kiswahili nchini Rwanda ulihitaji utashi zaidi wa kisiasa. Hivyo, ilibidi serikali ihakikishe kuwa walimu wa kufundisha somo la Kiswahili katika shule za sekondari wanapatikana. Kwa hiyo serikali ikaanza kufundisha somo la Kiswahili katika vyuo vya ualimu9. Kutokana na maboresho ya elimu ya 2008 (yaliyotekelezwa kuanzia mwaka 2009) mpaka sasa nchini Rwanda kuna vyuo vya ualimu zaidi ya kumi10. Vyuo hivi vinafundisha fani ya ualimu katika ngazi ya stashahada na vina mchepuo wa lugha unaojumuisha pia somo la Kiswahili.
Zaidi ya hayo, serikali ililazimika kuandaa walimu wenye digrii kwa ajili ya kufundisha Kiswahili katika vyuo vya ualimu na katika shule za sekondari. Kutokana na mahitaji hayo, Chuo Kikuu cha Rwanda, Koleji ya Elimu, pamoja na chuo chake kishiriki cha elimu Rukara (walimu wa ngazi ya stashahada), kina programu mojawapo ya elimu inayohusisha Kiswahili kama somo mojawapo la kufundishia. Athari chanya nyingine ni pamoja na mahitaji ya uandishi wa vitabu vya Kiswahili. Serikali kupitia Bodi ya Elimu Rwanda (REB) imefanikiwa kuandika vitabu vya Kiswahili kwa ajili ya kidato cha kwanza hadi cha sita kwa kuegemea kwenye muhtasari wa 2008. Pia kwa wakati huu, REB imefanikisha uandishi wa vitabu kwa kufuata muhtasari mpya wa Kiswahili wa mwaka 2015. REB imekusudia kuhakikisha kuwa kila kidato kinapata vitabu kutoka kwa wachapishaji watatu tofauti. Pia, Bodi hii inahusika na utengenezaji wa mtaala wa Kiswahili. Hili ni jambo zuri kwa sababu Kiswahili kinafundishwa kwa kufuata mtaala rasmi. Kwa sasa, Bodi hii ya elimu imekamilisha kuandaa muhtasari mpya wa Kiswahili ulioanza kutumika kuanzia Januari 2016.
Katika muhtasari mpya wa sasa vipindi vya Kiswahili vimeongezeka. Kwa kidato cha kwanza hadi kidato cha tatu, kutakuwa na vipindi viwili. Mgawanyo huu wa muda wa kujifunza Kiswahili ni sawa kabisa na muda wa kujifunza Kifaransa. Kwa upande wa kidato cha nne hadi kidato cha sita, Kiswahili kwa wiki kina vipindi vinane. Si hivyo tu, Kiswahili pia kimekuwa ni somo la lazima ambapo kila mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule inayofundisha Kiswahili atatahiniwa katika mtihani wa taifa wa kidato cha tatu.
Jambo jingine muhimu kuhusu REB, katika Kurugenzi yake ya mitaala, kuna ofisi ya mkuzaji mtaala wa Kiswahili. Hili ni jambo muhimu katika maendeleo ya Kiswahili. Afisa huyu anayehusika na mtaala wa Kiswahili ndiye anayeratibu na kusimamia mambo mbalimbali yanayohusiana na ufundishaji wa Kiswahili. Pia kuna wakaguzi wa elimu wanaohusika na ubora wa ufundishaji na ujifunzaji wa lugha ya Kiswahili. Aidha, Bodi hii ya elimu imeajiri maafisa wanaoratibu mitihani ya kitaifa ya lugha ya Kiswahili. Maafisa hawa wana wajibu wa kuona malengo ya ufundishaji na ujifunzaji yanapimwa kama inavyopaswa. Sehemu inayofuata inabainisha sababu za kuendelea kuwapo kwa utashi wa kisiasa nchini Rwanda katika kustawisha lugha ya Kiswahili. Hii ina maana ya kwamba bila kuwapo kwa sababu hizi utashi wa kisiasa uliopo sasa ungeweza kuwa umetoweka.
5.2 Sababu Zinazoendeleza Kuwapo kwa Utashi wa Kisiasa nchini Rwanda
Katika sehemu hii tunajadili mambo yanayosababisha utashi wa kisasa katika ustawishaji wa lugha ya Kiswahili kuendelea kuwapo. Hii ina maana kwamba utashi wa kisiasa unatengenezwa lakini baada ya kutengenezwa unapaswa kujengewa mazingira ya kuendelea kuwapo ili usitoweke. Zifuatazo ni sababu mbili za msingi katika kuendelea kuwapo kwa utashi wa kisiasa nchini Rwanda.
5.2.1 Kuongezeka kwa Mahitaji na Matumizi ya Kiswahili nchini Rwanda
Lugha ya Kiswahili imekuwa na idadi kubwa ya watumiaji katika nchi ya Rwanda. Makadirio yaliyofanywa na Wizara ya Elimu (1984) yanaonesha kwamba wazungumzaji wa Kiswahili walikuwa 500,000. Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2002 kwa upande wa mijini wazungumzaji wa Kiswahili walikadiriwa kufikia asilimia 12.2 na wale wa vijijini ilikuwa ni asilimia 2.1. Sensa ya mwaka 2012 iliiweka lugha ya Kiswahili katika kundi la lugha nyinginezo (Niyibizi, 2014). Aidha, tarehe 12/10/ 2016, Baraza la Mawaziri nchini Rwanda liliamua kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi nchini humo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mahitaji ya lugha hii katika nchi hii yameendelea kuongezeka kila siku. Kuongezeka kwa mahitaji ya lugha ya Kiswahili ni nguvu muhimu pia katika kushikilia kuwapo wa utashi wa kisiasa katika kuhitaji kuistawisha lugha ya Kiswahili. Zifuatazo ni sababu za kuongezeka kwa mahitaji ya Kiswahili nchini Rwanda:
Mosi, ni kuongezeka kwa maingiliano ya kibiashara kati ya Rwanda na nchi nyingine wanachama, hususan Kenya na Tanzania. Hii ni kutokana na ukweli kwamba msisitizo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kuona uchumi ukiendeshwa zaidi na sekta binafsi kuliko kuendeshwa na serikali (Kawoya, 2009). Hali hii imewafaya wafanyabiashara au wafanyakazi wao kulazimika kwenda katika nchi nyingine kwa ajili ya shughuli za biashara. Katika safari hizi, lugha ya Kiswahili ndiyo inayotumika zaidi kuliko lugha nyingine yoyote. Hali hii inadhihirishwa na Kiango (2002) pale anapobainisha matumizi ya Lugha ya Kiswahili na Kiingereza katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Vilevile, Steflja (2012 akiwarejelea Rosendal (2009), LeClerc (2008), Munyankesha (2004) na Samuelson na Freedman (2010) anaeleza kuwa nchini Rwanda, asilimia 100 wanazungumza Kinyarwanda, asilimia 8 wanazungumza Kifaransa na asilimia 4 wanazungumza Kiingereza. Takwimu hizi zinaonesha kuwa katika ukanda huu watu wengi hawajui Kiingereza wala Kifaransa. Hivyo, lugha pekee inayoweza kutumika zaidi ni Kiswahili.
Wafanyabiashara na watu mbalimbali wasiojua lugha ya Kiswahili wanajikuta wakiwa na wakati mgumu wanapotoka nje ya Rwanda.
Pili, ni suala la kufungua mipaka kwa ajili ya watu kwenda kufanya kazi mbalimbali nchini Rwanda. Hali hii pia imechangia kwa kiwango kikubwa sana kuwa na watu wengi kutoka katika nchi mbalimbali zikiwamo nchi wanachama za Afrika Mashariki. Hali hii inalazimisha wenyeji wakati mwingine watumie lugha ya Kiswahili ili kufanikisha mawasiliano na wageni wanaojua lugha ya Kiswahili tu.
Tatu, ni kurudi kwa wingi kwa watu waliokuwa uhamishoni baada ya hali ya usalama na utulivu kurejea nchini Rwanda. Kundi hili la watu wanaoendelea kutumia Kiswahili linaendelea kuwapo kutokana na kujikuta likikaa sehemu moja. Pia, kundi hili la watu limekuwa na mahusiano ya muda mrefu na watu wa maeneo mbalimbali ya nchi walizokuwa uhamishoni. Watu hawa wanawasiliana kwa simu na kutembeleana. Katika mawasiliano yao lugha inayotumiwa zaidi ni Kiswahili. Pia, watu hawa wanashirikiana pamoja katika matukio ya misiba, harusi na ugonjwa.
Nne, ni mahitaji ya mtu binafsi kutokana na watu waliomzunguka kuwa wanatumia lugha ya Kiswahili. Hii pia ni sababu mojawapo ya kuwapo kwa hamasa kwa baadhi ya watu kujifunza lugha ya Kiswahili ili waweze kuwasiliana na watu wao wa karibu. Katika mahojiano na mwanafunzi mmoja wa Kiswahili, alieleza kwamba yeye anajifunza Kiswahili kwa sababu mume wake anazungumza Kiswahili.
5.2.2 Kuwapo kwa Matumizi ya Kiswahili katika Maeneo mbalimbali nchini Rwanda
Hii pia ni sababu nyingine muhimu katika kuushikilia utashi wa kisiasa katika lugha ya Kiswahili. Nchini Rwanda lugha ya Kiswahili inatumika katika maeneo mbalimbali: mosi ni eneo la Gikondo au Magerwa. Hili ni eneo la kibiashara yaani kituo muhimu kwa biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Eneo hili ni mahususi katika upakuaji wa mizigo mbalimbali, hususan ile inayotoka katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki. Kimsingi katika eneo hili lugha inayotumiwa sana ni Kiswahili. Pili ni sehemu ya Nyamirambo. Sehemu hii, mbali na kukaliwa na wazungumzaji wengi wa Kiswahili, pia inatambulika kama kitovu cha Waswahili asili na dini ya Kiislamu katika nchi ya Rwanda. Toka zamani, Nyamirambo ni eneo linalokaliwa na watu mchanganyiko, na mchanganyiko huu umeendelezwa zaidi baada ya mwaka 1994 kutokana na watu waliotoka uhamishoni14. Inaelezwa kwamba wakati wa machafuko ya mwaka 1994 eneo hili halikuathiriwa sana kutokana na wakazi wa eneo hili kujiona kuwa wote ni ndugu kutokana na matumizi ya lugha ya Kiswahili. Umuhimu wa lugha ya Kiswahili katika eneo hili unadhihirishwa na uamuzi wa Rais Paul Kagame wa Rwanda kuzunguamza Kiswahili katika kampeni za uchaguzi wa mwaka 201015. Hii inaonesha pia namna ambavyo lugha ya Kiswahili ilivyostawi nchini Rwanda kiasi cha kuweza kutumika hata katika shughuli za kisiasa.
Tatu, ni maeneo ya mipakani hususan Rusumo kwa upande wa mpaka wa Rwanda na Tanzania na Gisenyi kwa upande wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo. Katika maeneo haya, kuna matumizi makubwa sana ya lugha ya Kiswahili.
Nne, ni sokoni, madukani, na migahawani. Haya ni maeneo mengine muhimu sana ambapo lugha ya Kiswahili inatumika ipasavyo kutokana na mahitaji ya kibiashara. Hivyo basi, Kiswahili kinaonekana kutekeleza vema jukumu la kuwa lugha ya mawasiliano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Tano, ni katika vyombo vya usafiri hususan teksi, bodaboda (pikipiki), mabasi yaendayo nje ya Rwanda na katika vituo vya mabasi. Hii ni sehemu nyingine muhimu ambayo ina matumizi makubwa ya lugha ya Kiswahili ukilinganisha na lugha nyingine za kigeni kama Kiingereza na Kifaransa. Sita ni katika nyumba za ibada na vyombo vya habari vya kidini. Eneo hili linahusika kutokana na ukweli kuwa baadhi ya taasisi za kidini zinamiliki vyombo vya habari ambavyo baadhi ya vipindi vyake vya dini hutangazwa kwa lugha ya Kiswahili. Hata taasisi za kidini ambazo hazimiliki vyombo vya habari huandaa vipindi maalumu na kuvirusha katika vyombo vingine vya habari kwa kutumia lugha ya Kiswahili.
Saba ni katika vyombo mbalimbali vya habari kama vile redio za masafa ya FM. Kushamiri kwa redio hizi kumefanya kuwapo na vipindi vinavyotangazwa kwa lugha ya Kiswahili. Aidha, Redio ya Taifa pamoja na Televisheni ya Taifa zinatumia Kiswahili katika vipindi mbalimbali kama vile taarifa ya habari, vipindi vya kufundisha Kiswahili, na hata matangazo ya mpira.
Eneo la nane lenye matumizi makubwa ya lugha ya Kiswahili ni muziki wa kizazi kipya. Wapenzi wengi wa muziki huu katika nchi ya Rwanda wanazifahamu nyimbo nyingi za wasanii wa muziki wa kizazi kipya kama vile bongo fleva, hip hop n.k. kutoka Uganda, Kenya na Tanzania ambazo zinaimbwa kwa Kiswahili. Baada ya kubainisha sababu kuu mbili zinazoshikilia kuendelea kuwapo kwa utashi wa kisiasa katika kustawisha lugha ya Kiswahili nchini Rwanda, kuna haja pia ya kubainisha changamoto zinazoikabili lugha hii nchini humo.
5.3 Changamoto Zinazoikabili Lugha ya Kiswahili nchini Rwanda
Licha ya kubainisha kuwapo kwa utashi wa kisiasa ambao umefanikiwa vema kuistawisha lugha ya Kiswahili nchini Rwanda, bado kuna changamoto kadhaa ambazo pia zinapaswa kubainishwa na kutatuliwa ili kufanikisha zaidi ustawi wa lugha hii nchini humo. Changamoto hizi ni: Mosi, lugha ya Kiswahili kutokufundishwa katika shule zote za sekondari nchini Rwanda. Kutokana na uamuzi huu mwanafunzi anapata fursa ya kujifunza Kiswahili pale tu ambapo shule aliyopo inafundisha Kiswahili. Pili, Kiswahili kutokufundishwa katika shule za msingi. Hali hii inawafanya wanafunzi kujifunza lugha ya Kiswahili katika umri mkubwa. Kwa kuwa katika shule za msingi mwanafunzi anakutana na lugha tatu, yaani Kiingereza, Kifaransa na Kinyarwanda, kuna uwezekano wa kujenga mtazamo hasi kuhusiana na lugha ya Kiswahili. Hivyo kuna uwezekano wa baadhi ya wanafunzi kuamua kutosoma Kiswahili hata kama lugha hiyo inafundishwa katika shule yake.
Tatu ni kuhusiana na utaratibu unaotumika kuwaweka wanafunzi katika mchepuo wenye somo la Kiswahili. Hadi sasa, kuna wanafunzi wanaowekwa kusoma katika mchepuo wa Kiswahili kidato cha nne (kiwango cha sekondari ya juu kinaanzia hapa) hata kama hawakusoma kabisa Kiswahili kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tatu. Utaratibu huu unaleta changamoto kubwa hususan kwa walimu, kwani walimu wanajikuta wana aina mbili za wanafunzi: waliosoma Kiswahili kutoka kidato cha kwanza hadi cha tatu na wale ambao wanakutana na Kiswahili kwa mara ya kwanza katika kidato cha nne. Tatizo hili halijatatuliwa hata na mtaala mpya wa mwaka 2015 kwani wanafunzi wote hawa walio katika viwango tofauti wanalazimika kufundishwa maudhui sawa.
Nne, ni kukosekana kwa mafunzo ya mara kwa mara ya uboreshaji wa mbinu za ufundishaji na ujifunzaji wa lugha ya Kiswahili. Hii inakwamisha uwezekano wa kutumia mbinu na maarifa mapya yaliyopatikana katika stadi za Kiswahili. Changamoto ya mwisho ni uhaba wa walimu wa kufundisha Kiswahili katika shule za sekondari. Huenda hii ndiyo sababu ambayo inaifanya serikali kutofanya uamuzi wa kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inafundishwa katika shule zote za serikali nchini humo.
5.4 Mapendekezo
Kutokana na changamoto mbalimbali ambazo tumezibainisha, tunaona kwamba iwapo mapendekezo yafuatayo yakitekelezwa yanaweza kutatua changamoto hizo. Tunapendekeza kwamba, mosi, serikali ifanye uamuzi wa kuanza kufundisha Kiswahili katika shule zote za sekondari na shule za msingi. Hii itaongeza ustawi wa lugha ya Kiswahili nchini Rwanda. Hili linaweza kufanikishwa kwa kuingia makubaliano na serikali za nchi nyingine za Afrika Mashariki zilizopiga hatua zaidi katika lugha ya Kiswahili. Nchi hizi zinaweza kukubaliana kubadilishana walimu wa Kiswahili na Kifaransa.
Pili, serikali ikomeshe utaratibu wa kuruhusu wanafunzi kuingia katika mchepuo wenye somo la Kiswahili hata kama hawakuwahi kusoma Kiswahili katika viwango vilivyotangulia. Hii itaepusha mkanganyiko katika ufundishaji na ujifunzaji. Mwalimu akifundisha mambo yanayohusu mwanafunzi anayeanza kusoma Kiswahili kwa mara ya kwanza, haitawavutia wanafunzi wanaoifahamu lugha ya Kiswahili. Vivyo hivyo, mwalimu akizingatia wale wanaofahamu tayari lugha ya Kiswahili, atawaathiri wanaokutana na lugha hii kwa mara ya kwanza.
Tatu, ni kuweka mkazo katika mafunzo ya walimu wa Kiswahili. Mafunzo haya yanaweza kufanikishwa kwa njia ya uendeshaji wa semina za ufundishaji na ujifunzaji wa lugha ya Kiswahili. Hii inaweza kufanikishwa kwa ushirikiano kati ya REB na Koleji ya Elimu iliyopo Chuo Kikuu cha Rwanda.
Mwisho, ni kuhusiana na utekelezaji wa mtaala mpya ulioegemezwa katika umahiri. Ni muhimu sana serikali ikaangalia kwa ukaribu iwapo walimu wameelewa maana ya mabadiliko ya mtaala wa elimu nchini Rwanda. Licha ya mafunzo yaliyotolewa, bado uangalizi wa karibu unahitajika ili mtaala mpya utekelezwe kama inavyopaswa.
6.0 Hitimisho
Lugha ya Kiswahili imefanikiwa kustawi nchini Rwanda kutokana na utashi wa kisiasa uliopo. Tumeona kuwa katika vipindi mbalimbali vya historia ya Kiswahili nchini Rwanda, Kiswahili kilistawi pale tu utashi wa kisiasa ulipokuwapo. Pia, Kiswahili kilisinyaa pale ambapo utashi wa kisiasa ulipokosekana. Licha ya hivyo, tumeona kuwa utashi wa kisiasa ili uwepo lazima kuwe na sababu zitakazola- zimisha kuwapo kwa utashi wa kisiasa. Hii ina maana kwamba utashi wa kisiasa huja kutokana na hali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi iliyopo katika kipindi husika. Pamoja na hayo, utashi wa kisiasa unapokuwapo ni lazima pia kuwe na sababu zitakazofanya utashi huo wa kisiasa uendelee kuwapo. Hii ina maana kwamba utashi wa kisiasa unaweza ukawa upo na baada ya muda ukatoweka iwapo sababu za kuendeleza utashi huo zitakoma. Aidha, tumeona kwamba licha ya utashi wa kisiasa kuwapo katika kustawisha lugha ya Kiswahili, bado kuna changamoto kadhaa ambazo zinaikabili lugha ya Kiswahili. Hivyo basi, ili ustawi wa Kiswahili uzidi kuwa endelevu nchini Rwanda, kuna haja ya kutatuliwa kwa changamoto zilizobainishwa.
Marejeleo
Aime, M. U. (2013). Usanifishaji wa Ikiryogo kwenye Shule ya Groupe Scolaire Kabusunzu: Mfano wa Kidato cha Tatu. Tasnifu ya Utafiti wa Kivitendo (Haijachapishwa). Taasisi ya Elimu Kigali, Kigali.
Bujra, A. (2002). Islam in Eastern Africa: Historical Legacy and Contemporary Challenges. kutoka
Charney, C. (2009). Political Will: What is It? How is It Measured? kutoka
International Conference of the Great Lakes Region (2004). Dar Es-Salaam Declaration on Peace, Security, Democracy and Development In The Great Lakes Region. Dar es Salaam
International Conference of the Great Lakes Region (2006). Regional Programme of Action for Humanitarian and Social Issues: Promotion of the Use of Kiswahili as a Working language in the Great Lakes Region.
Kawoya, V. (2009). The Case of Kiswahili as a Regional Broadcasting Language in East Africa. The Journal of Pan African Studie, 8 (3): 1 -35.
Kiango, J. C. (2002). Nafasi ya Kiswahili katika Ujenzi wa Jamii Mpya Afrika Mashariki.
Nordic Journal of African Studies, 11 (2): 185 – 197.
Kimenyi, T. (2003). Hali ya Kiswahili nchini Rwanda. Tasnifu ya Digrii ya Umahiri Katika Sanaa (Haijachapishwa). Chuo Kikuu cha Egerton, Nakuru.
Mekacha, K. D. R. (2011). Isimujamii: Nadharia na Muktadha wa Kiswahili. Dar es Salaam: TUKI.
MINEDUC (2010). History Program for Advanced Level Secondary School. Kigali:
MINEDUC.
Mohochi, S. (2011). Mielekeo ya Wasomi wa Kiswahili na Viongozi wa Afrika Mashariki
kuhusu Lugha ya Kiswahili. Swahili Forum, 18:24 -36.
Msanjila, P.Y na wenzake (2009). Isimujamii: Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: TATAKI.
Mukuthuria, M. (2006). Kiswahili and its Expanding Roles of Development in East African Cooperation: A Case of Uganda. Nordic Journal of African Studies, 15 (2): 154 – 165.
Niyibizi, E. (2014). Foundation Phase Learner’s and Teacher’s Attitudes and Experiences with the Rwandan Language- in- Educatition Policy Shifts. Tasnifu ya Digrii ya Uzamivu (Haijachapishwa). University of Witwatersrand, Johannesburg.
Niyirora, E. (2013). Utumiaji wa Mazungumzo na Ufahamu kama Mbinu za Kuboresha
Ufundishaji wa Kiswahili cha Maongezi. Tasnifu ya Utafiti wa Kivitendo (Haijachapishwa). Taasisi ya Elimu Kigali, Kigali.
Post, A. L. na wenzake (2008). Using Public Will to Secure Political Will. in Governance
Reform under Real – World Conditions: Citizens, Stakeholders, and Voice. Washington DC: The World Bank. pp. 113 -124
Republic of Rwanda. (1999). The Unity of Rwandans: Before Colonial Period, Under the
Colonial Rule, and Under the First Republic. A Report of the President’s Commitee on the Unity of Rwandans, Office of the President of the Republic, Kigali.
Samuelson, B. L. & Freedman, S. W. (2010). Language Policy, Multilingual Education, and Power in Rwanda. Language Policy, 9 (3): 191-215.
Steflja, I. (2012). The High Costs and Consequences of Rwanda’s Shift in Language Policy from French to English in Africa Portal Backgrounder. Montreal: CGI.
|