MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
KISWAHILI KINA NAFASI YA KUTAMBULIKA DUNIANI ? - Printable Version
JIFUNZE KISWAHILI
KISWAHILI KINA NAFASI YA KUTAMBULIKA DUNIANI ? - Printable Version

+- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz)
+-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1)
+--- Forum: Maendeleo ya Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=11)
+--- Thread: KISWAHILI KINA NAFASI YA KUTAMBULIKA DUNIANI ? (/showthread.php?tid=1167)



KISWAHILI KINA NAFASI YA KUTAMBULIKA DUNIANI ? - MwlMaeda - 09-06-2021

WAKATI wazungumzaji wa Kiswahili wakiendelea kukibananga, watunga sera na watoa maamuzi wameisahau lugha hiyo.
Hivi ndivyo mtafiti na mtaalamu wa Kiswahili, Sheikh Khamis Mataka anavyoyatazama maendeleo ya lugha ya Kiswahili kama alivyohojiwa na mwandishi wetu Abeid Poyo
Swali: Unayatazamaje maendeleo ya lugha ya Kiswahili hivi leo?
Jibu: Maendeleo ya Kiswahili naweza kuyashabihisha na Nabii asiyekubalika kwao. Wakati Tanzania ikibeba sifa ya chimbuko la lugha ya Kiswahili iliyofikia hivi leo kuwa lugha mama na kuvuka vikwazo kadhaa na kukubalika Afrika na Ulimwenguni, juhudi za kukishugulikia, kukikuza na kukiendeleza zimefifia kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na kinavyoshughulikiwa nje ya mipaka ya Tanzania. Kwa mfano, walimu wengi wa Kiswahili Ulaya na Marekani si Watanzania, wengi ni Wakenya. Aidha niangalie maendeleo yake hususan upande wa wazungumzaji, hapa maendeleo yanasuasua; leo watu wanazungumza Kiswahili kibovu tofauti na miaka ya 1960.
Swali: Unadhani nini kinakwamisha juhudi za kukikuza Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya Tanzania?
Jibu: Kuna mambo kadhaa yanayokwamisha juhudi, kubwa kuliko yote ni kukosekana kwa utashi wa kisiasa.
Ukuzaji Kiswahili si katika vipaumbele vya watoa maamuzi, hili lipo dhahiri unapoangalia bajeti ya Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita). Bakita ni sawa na mtoto yatima asiye na ruhusa ya kudeka mbele ya mlezi wake. Leo Bakita haina jengo lake, kuna vyombo vimeundwa baada ya Bakita, leo vina majengo. Lakini Bakita liko tangu 1967 na hadi leo halina jengo. Serikali ilipaswa kuwa mlezi kwa kuwa baraza ni sawa na idara tu ya serikali. Kule kwenye utashi tunaona maendeleo. Hali ni hiyo hiyo unapoangazia mchango wa serikali katika kuwezesha tafiti mbalimbali ambazo ni uti wa mgongo katika ukuzaji wa Kiswahili. Tafiti zikifanyika basi ujue ni kwa ufadhili wa taasisi za nje hususan Wajerumani. Utashi wa kisiasa ndiyo pia unaokwamisha juhudi za Kiswahiili kuwa lugha ya kufundishia sekondari na elimu ya juu ingawa ukweli, moja ya sababu inayopelekea kushuka kwa kiwango cha elimu nchini ni tatizo la kutumia lugha ya Kiingereza linalowakabili walimu na hata wanafunzi.
Swali: Ukoje mchango wa vyama wadau wa Kiswahili kama Bakita na Ukuta katika kukikuza Kiswahili kwa sasa?
Jibu: Kama nilivyoeleza hali mbaya ya Bakita inayolikwaza kutoa mchango kuntu katika kukikuza Kiswahili, Chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (Ukuta) kimebaki historia hususan baada ya kufa au kukosa nguvu za kisiasa wale waliokuwa wakiwaonea haya waanzilishi wa Ukuta. Miaka ya mwishoni mwa 1980 nilikuwa miongoni mwa wanachama wa Ukuta chini ya Uenyekiti wa Sheikh Mohammed Ally Al-Bukhry. Wakati ule chama kilikuwa chumba cha wagonjwa mahututi na marehemu Mzee Saadani Kandoro kwa kumtumia Mzee Kawawa walifanya juhudi za makusudi kukihuisha lakini kilio chao hakikusikiwa. Kadhalika marehemu John Komba akiwa Katibu Mkuu wa Ukuta alijitahidi kuendesha kwa gharama binafsi shughuli za Ukuta. Walipokufa au kuchoka wale waliokuwa wakionewa haya, kama marehemu Mzee Khamis Akida aliyekuwa akifungua ofisi ya Ukuta pale Anartoglou na kufanya kazi zake binafsi za kitaaluma. Katika hali hii huwezi kutarajia mchango wa Ukuta katika kuikuza lugha ya Kiswahili.
Swali: Hivi Kiswahili kina nafasi katika dunia ya sasa?
Jibu: Nafasi ya lugha yoyote ni kupata fursa ya kuzungumzwa, lugha isiyozungumzwa ni lugha mfu. Kwa mantiki ya Kiswahili kupata fursa ya kuzungumzwa si tu Afrika Mashariki, Kati na Kusini bali hata duniani kiasi cha kufundishwa katika vyuo vikuu mbalimbali, ni dhahiri Kiswahili kina nafasi ya kuwa miongoni mwa lugha zinazotambuliwa Afrika na duniani kwa jumla. Faraja kubwa iliyopo ni kwa Kiswahili kukubalika kutumika Umoja wa Afrika na kuwapo dhana ya kuwa Kiswahili kina uwezo wa kuiunganisha Afrika kimawasiliano. Utashi wa kisiasa ukiwapo Kiswahili kina uwezo wa kuiunganisha Afrika.
Swali: Unadhani Kiswahili kinakidhi haja ya kuwa lugha ya kufundishia katika madaraja yote ya elimu nchini?
Jibu: Ndiyo. Ieleweke kuwa hakuna lugha maalumu ya elimu, na kwa dhati kabisa Kiswahili kwa kuweza kufanikisha mawasiliano baina ya wazungumzaji wake, kadhalika ina uwezo wa kuwa lugha ya kufundishia kama ilivyo Kiarabu katika ulimwengu wa Kiarabu, Kifaransa kwa nchi zinazozungumza Kifaransa, Kichina kule China na lugha kama vile Kijapan, Kikorea na kadhalika. Kelele unazozisikia ni kasumba iliyowakolea wapenda Kiingereza. Hata Waingereza wenyewe hapo awali waliingiwa na kasumba ya kukijali Kilatini hadi pale walipotambua umuhimu wa lugha yao kwa maendeleo. Tuache dhana kuwa kujua Kiingereza ndiyo kuwa na elimu, wapo wajinga wanaozungumza Kiingereza kama ilivyo Tanzania wajinga wanaozungumza Kiswahili.
Swali: Njia gani tutumie kama jamii kuwaenzi wale waliokipandisha chati Kiswahili?
Jibu: Njia bora ni kudumisha historia yao. Jamii inapaswa kuwajua vilivyo mashujaa hawa wa Kiswahili kama ambavyo angalau Sheikh Shaaban Robert alivyosaidiwa kubaki hai kama alama ya watu waliosaidia kuipandisha chati lugha ya Kiswahili. Sheikh Shaaban Robert hakuwa peke yake kama ambavyo Mwalimu Nyerere hakuwa peke yake katika kupigania uhuru wa nchi hii. Jamii haina budi kujua michango ya akina Sheikh Ali Mohamed Al-Bukhry, Mathias Mnyampala, Sheikh Abdulbari Diwani, Saadan Kandoro, Padro Joji Mbaruku, Juma Mnyibwe, Mohammed Suleiman, Akilimali Snowhite, Sheikh Shaaban Gonga, Mzee Hamdun Jitu Kali na wengineo.
Swali: Umewahi kufanya kazi na baadhi ya magwiji hawa, nini umejifunza kutoka kwao?
Jibu: Nimejifunza mengi hususan kutoka kwa marehemu Sheikh Khamis Akida na Mwalimu Pera Ridhiwani. Lakini jambo kubwa nililojifunza ni kudharauliwa kwa watu waliokishughulikia Kiswahili. Ninawafahamu watu kadhaa ambao marehemu Akida aliwasaidia kazi zao zilizosababisha kupata shahada na kupanda daraja za kitaaluma katika taaluma za Kiswahili. Aidha mzee huyu na mwenzake mwalimu Pera wana mchango mkubwa katika kazi za kamusi na fasihi zilizotolewa na taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (Tuki), lakini kwa uswahili wao wamekufa bila kutunukiwa japo shahada za heshima. Wapo watu wengi tu wanapata shahada za heshima, kwa nini wazee hawa wasipewe basi hata kumbukizi yao hakuna? Ni dhahiri Waswahili waliokitumikia Kiswahili wamesahauliwa.
Swali: Kuna madai kuwa wasomi wa Kiswahili ndiyo wanaochangia kukiua Kiswahili, wanakitetea mdomoni lakini si katika matendo, upi ukweli?
Jibu: Kuwavurumishia madai haya wasomi wote ni kuwaonea. Hata hivyo, upo ukweli baadhi ya wasomi ama kwa kukata tamaa au kuwaridhisha wapanga sera na watoaji wa maamuzi wamekuwa wakiyumba katika kukitetea Kiswahili. Lakini ukweli utabaki pale pale kuwa msomi mzalendo anayejua thamani ya lugha kwa maendeleo hatoyumba katika msimamo wake wa kukijenga, kukienzi na kukitetea Kiswahili.
Swali: Una ushauri wowote kwa serikali au jamii kuhusu Kiswahili
Jibu: Watanzania tunaongoza kwa kukibananga Kiswahili na kutotaka kujifunza tukijidanganya tunakijua. Hili linawakusanya wanasiasa, wasanii, wanahabari na jamii kwa jumla.Ni muhali kusoma gazeti lolote la Kiswahili na usikute makosa yanayojirudia. Tujifunze Kiswahili kwa dhati kabisa, na kwa wanahabari wawe mstari wa mbele katika hilo ili waepuke dhulma wanayoifanyia lugha yetu adhimu. Kwa naishauri serikali ichukue hatua madhubuti na kufanya maamuzi stahiki kuhusu namna bora ya kukikuza na kukiendeleza Kiswahili.