UMAARUFU WA KISWAHILI DUNIANI - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Maendeleo ya Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=11) +--- Thread: UMAARUFU WA KISWAHILI DUNIANI (/showthread.php?tid=1166) |
UMAARUFU WA KISWAHILI DUNIANI - MwlMaeda - 09-06-2021 UMAARUFU WA KISWAHILI DUNIANI
Na. Erasto Duwe
Mkurugenzi mshiriki wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dr Musa Hans anasema, “Huu ni uzalendo wa hali ya juu ulioonyeshwa na kiongozi mkuu wa nchi na ni dhahiri kwamba uzalendo huu unatoa heshima kwa Waafrika kwa jumla.”
Mdau na mhadhiri wa Kiswahili Jovieth Bulaya anasema,” Uamuzi wa Rais Magufuli kutumia Kiswahili katika hotuba yake kwa Rais wa Vietnam ni suala la kizalendo na linapaswa kuigwa na kuungwa mkono na wapenzi wote wa Kiswahili. Viongozi wakuu wa nchi kama marais wana mchango mkubwa katika kukiendeleza, kukikuza na kukifanya kiheshimike ndani na nje ya nchi hivyo tuunge mkono jitihada zao.”
Ule mzigo uliokuwa ukiwaelemea wadau na wapenzi wa lugha ya Kiswahili sasa wameutua. Ni mzigo wa kutaka Kiswahili kupewa msukumo wa kisiasa kama chachu ya kuiendeleza lugha hiyo ya taifa. Kwa muda mrefu wadau wa Kiswahili wamekuwa wakiwakosoa viongozi kwa kukosa utashi wa kukikuza, kukiendeleza na hata kukitangaza kimataifa. Ilifika wakati mgeni anatumia lugha mama akiwa katika ardhi ya Tanzania huku Watanzania tukiona fahari kutumia lugha za kigeni na kuipa kisogo Kiswahili.
Pongezi kwa Rais John Magufuli kwani katika uongozi wake tayari kuna kila dalili kuwa kuna kila dalili za kuzitetemekea lugha za kigeni kufikia tamati nchini.
Kiswahili katika mkutano wa viongozi wa EAC
Akiwa mwenyekiti mpya wa marais hao, Rais Magufuli alitaka Kiswahili kitumike katika Jumuiya hiyo kama lugha rasmi ili kuboresha utengamano.
Kwa mujibu wa Rais John Magufuli Kiswahili kinatambulika kama lugha rasmi , hivyo nchi za Afrika Mashariki haziwezi kukiweka kando.
“Lugha ni nyenzo na nguvu kubwa ya umoja na kuboresha mawasiliano katika jamii.” Alisema.
Ziara ya Rais wa Vietnam
Pia uamuzi wa Rais Magufuli kutumia Kiswahili katika hotuba zake wakati wa ziara ya Rais wa Vietnam Truong Tan Sang hivi karibuni umefungua ukurasa mpya wa maendeleo ya Kiswahili ndani na nje ya nchi. Tukio hilo limeibua hisia za aina yake miongoni mwa Watanzania na jamii ya wasomi . Kwa hakika ni tukio la aina yake linalovuta hisia kwa wapenzi wa Kiswahili na masuala ya utamaduni. Kwa walio wengi, hii ni hatua nzuri ya kukipa hadhi na kukiendeleza Kiswahili .
Kwa kuzungumza Kiswahili mbele ya vyombo vya habari vya kimataifa hatua hiyo imeitangaza lugha ya Kiswahili siyo kwa Wavietnam waliokuwa wakifuatilia ziara ya rais wao bali hata wananchi wa maeneo mbalimbali duniani.
Kwa hakika Rais Magufuli amepiga baragumu na kupaza sauti kwa watu wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam. Baragumu hilo halijaishia Vietnam pekee bali mwangwi wa sauti ya baragumu hilo umeenea kote duniani kwani mataifa yamesikia. Ndiyo maana Baraza la Kiswahli la Taifa (Bakita) halikuchelewa kumpa pongezi Rais Magufuli kwa uzalendo wake wa kuitumia lugha ya Kiswahili katika mikutano mikubwa na hafla mbalimbali za kitaifa na kimataifa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bakita Profesa Martha Qioro alisema msimamo huo wa Rais umewasaidia Watanzania kupata taarifa moja kwa moja kutoka katika matukio anayokuwapo.
“Uamuzi na msimamo wa Rais Magufuli wa kutumia Kiswahili katika mikutano mikubwa ukiwamo mkutano mkuu wa 17 wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepokewa kwa furaha kubwa na wananchi na wadau wengi wa Kiswahili ndani na nje ya Tanzania.” Alisema. Kwa mujibu wa Profesa Quoro Bakita linaamini kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza lugha ya Kiswahili na kutoa fursa za ajira kwa Watanzania kupitia tafsiri na ukalimani na hivyo kuwapelekea maendeleo wananchi wote wa Afrika Mashariki.
Wasemavyo wadau
Mkurugenzi mshiriki wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dr Musa Hans anasema, “Huu ni uzalendo wa hali ya juu ulioonyeshwa na kiongozi mkuu wa nchi na ni dhahiri kwamba uzalendo huu unatoa heshima kwa Waafrika kwa jumla.”
Mdau na mhadhiri wa Kiswahili Jovieth Bulaya anasema,” Uamuzi wa Rais Magufuli kutumia Kiswahili katika hotuba yake kwa Rais wa Vietnam ni suala la kizalendo na linapaswa kuigwa na kuungwa mkono na wapenzi wote wa Kiswahili. Viongozi wakuu wa nchi kama marais wana mchango mkubwa katika kukiendeleza, kukikuza na kukifanya kiheshimike ndani na nje ya nchi hivyo tuunge mkono jitihada zao.”
Mwisho.
|