MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
JE, KISWAHILI NI MALI YA NANI? - Printable Version
JIFUNZE KISWAHILI
JE, KISWAHILI NI MALI YA NANI? - Printable Version

+- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz)
+-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1)
+--- Forum: Maendeleo ya Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=11)
+--- Thread: JE, KISWAHILI NI MALI YA NANI? (/showthread.php?tid=1160)



JE, KISWAHILI NI MALI YA NANI? - MwlMaeda - 09-06-2021

Soma hapa pengine utapata kujua sababu za Wakenya kudai kuwa Kiswahili ni chao.
Swahili ni Taifa la makabila yaliyopo katika Pwani ya Afrika ya Mashariki na visiwa vyake tokea Barawa hadi Sofala. Baadhi ya makabila hayo ni Wabarawa, Wapate, Waamu, Wagiriama, Wadigo, Waduruma, Wakauma, Wakambe, Wachoni, Warabai, Waribe, Wajibana, Wakilindini, Wajomvu, Wamtwapa, Wachangamwe, Watangana, Wamvita, Wapokomo, Wavanga, Wamakunduchi, Wapemba na Wangazija. Kabila hizi zote zilikuwa zikizungumza lugha ilokuwa ikijulikana kama Kingozi. Hata hivyo, makabila yote haya yalikuwa na ndimi (lahaja/dialect) zao na miji yao; baadhi yao bado wangali na ndimi zao na miji yao. Ndimi zote hizi zina ukhusiano au ukuruba mkubwa wa maneno na maana zake. Kwa mfano, utakuta kwamba kuna ukuruba fulani baina ya Kipemba na Kiamu.
Kila kabila ina ndimi yake, dasturi zake, mila zake, tungo zake, na kadhalika. Haya yote ni kabla ya Waarabu na Washirazi hawajaanza kuhamia kimaisha katika Pwani ya Afrika ya Mashariki – takriba karne nane hadi kumi zilizopita (yaani baina ya miaka 800 hadi 1000).
Washirazi hawakuathiri mno mila, dasturi, mapisi, na lugha hiyo ya Watu wa Pwani. Waarabu ndiyo walioathiri sana, khususa Makabila ya Kati na Kati (kwa mfano, Wamvita, Watangana na Wakilindini). Makabila haya yaliathirika mno hadi ya kuwa majina haya yalipotea na ndimi zao za kiasili zilipotea vilevile. Ndimi ambazo bado zipo ingawa zimeazima maneno fulani ya Kiarabu (kama ambavyo pengine Kiarabu kimeazima kutoka Lugha ya Kingozi) ni ndimi za kaskazini na zile za kusini.
Ndimi za Kaskazini ambazo bado zipo na wenyewe wanatambuliwa ni kama vile Kibarawa, Kiamu, Kipokomo, na kadhalika. Ama Ndimi za Kusini ambazo hazikuathiriwa mno ni Kingazija, Kimakunduchi, Kipemba na Kivanga. Ndimi za Kati na Kati ambazo bado zikalipo ni kama vile, Kigiriama, Kiduruma, Kijibana; hizi ni miongoni mwa kabila ambazo leo zajiita au zatambuliwa kama Mijikenda (yaani miji tisia).
Utakuta ya kuwa katika makabila ya kati na kati, yale ambayo hayakuathiriwa sana ni yale ambamo watu wake hawakuwa Waislamu. Na ndiyo maana mpaka hii leo utaona ya kuwa makabila ya Mijikenda (isipokuwa Digo), ni makabila ambayo wengi katika watu wake si Waislamu. Hii ni kwa sababu makabila kama ya Mvita, Tangana na Changamwe hayakujitahidi au kujishughulisha kufanya usambazaji wa Risala ya U-Islam kwa makabila haya; Waarabu piya walipokuja hawakuwa na lengo hilo la kuingia vijijini kufanya Da’wah. Lengo lao kubwa ilikuwa ni biashara. Kama tujuavyo U-Islam ulifika Kaskazini Mashariki mwa Bara la Afrika kabla haujafika katika sehemu nyengine za bara Arabu kama vile, Yemen, Omani na hata katika mji wa Madina na sehemu nyingi za nchi tunayoijua leo kama Saudi Arabia. Yaani U-Islam ulifika Abisinia (Ethiopia ya leo) katika mwaka wa 615, miaka mitano tu baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.) kupewa risala (610). Mtume alizaliwa mwaka wa 570. Ingawa wale Waislamu waliokuja kuomba hifadhi Abisinia walikwenda zao Madina baada ya kutawazwa kwa serikali ya kwanza ya Islam mwaka wa 623 (huu ni mwaka wa kwanza wa Hijria), walikuwa washawasilimisha watu kadha wa kadha (akiwemo Mfalme wao, Najash); hii ndiyo ilikuwa ni sababu ya kuanza kusambaa kwa U-Islam katika bara la Afrika. Kwa hivyo ni muhimu kutambua na kuamini ya kuwa makabila fulani ya Afrika ya Mashariki yalisilimu kabla ya kuja kwa Waarabu hawa tuwajuwao leo, waliokuja kwa biashara katika pwani ya Afrika ya Mashariki kutoka Yemen, Omani, na kadhalika.
Na khususa ni Waarabu hao wa Yemen na Omani ndiyo waloowana na baadhi ya hao Wangozi, au wanaojulikana leo kama Waswahili. Kwa hivyo, baadhi ya Waswahili wana damu za Kiarabu na baadhi yao hawana damu ya Kiarabu. Katika dasturi za Kizungu za kufuata ukoo, mtu anapotanganya tu damu na asekuwa Mzungu, basi azaliwae katika mtanganyiko huo katu hakubaliwi kuwa ni Mzungu. Na ndiyo twaona ya kuwa ingawa kuna asili mia thalathini (30%) ya Wamarekani Weuse (African-Americans) ndani ya Marekani, lakini wanasibishwa na U-Afrika na U-weuse (Blacks) pekee, na katu hawanasibishwi na uzungu. Kwa Waarabu nao ni rahisi zaidi kunasibishwa na taifa hilo ikiwa mtu lugha yake ya kwanza ni Kiarabu. Ama kwa Waswahili tukati na kati, yaani aghlabu mtu hunasibishwa na Uswahili kwa lugha na asili. Kwa hivyo leo wako baadhi ya Waswahili wenye damu za Kiarabu ambao wametagua, kwa sababu mbalimbali, kujinasibisha zaidi na U-Arabu kuliko U-Afrika; kadhalika, kuna baadhi yao, kwa sababu moja au nyengine, wameamua kujinasibisha zaidi na U-Afrika kuliko U-Arabu.
Hakuna yoyote atakayekataa ya kuwa neno Swahili au Sawahel ni neno lenye asili ya Kiarabu, ambalo lina maana ya Pwani au Mwambao. Kwa hivyo, ni wazi kabisa kuwa jina au neno Swahili halikuapo kabla ya kuja kwa Waarabu. Hivyo basi, wema mmoja ambao Waarabu waliwafanyia wenyeji wa Mwambao wa Afrika ya Mashariki na visiwa vyake ni kuwabandikiza neno lililoanza kutumika kama jina la taifa la wenyeji hao, litambulikanalo leo hii kama Taifa La wa-Swahili, yaani Taifa La wa-Mwambao. Watu wa taifa hili ni Waswahili, yaani Wamwambao, au kwa jina la kiasili, Wangozi. Na hapo pao napo paitwa Uswahilini. Na mila na dasturi zao ndiyo Uswahili. Na lugha ya watu hawa ni Kiswahili. Ni lugha ambayo maneno yake zaidi yatokamana na ndimi za makabila ya kati – kama vile Kimvita, Kichangamwe na Kitangana; halafu ikatukua na maneno ya Kiamu, Kivanga, Kipemba, Kingazija, Kibarawa, Kigiriama, na kadhalika. Kwa hivyo, Kiswahili ni kile kile Kingozi, tofauti ni jina tu; timbuko lake ni mtanganyiko wa ndimi za makabila ya Pwani. Piya kuna maneno ya Kiarabu, Kishirazi, Kiingereza, Kireno, na lugha za bara ya Afrika ya Mashariki. Kiswahili kimeazima maneno ya lugha nyegine kama ambavyo lugha zote zimefanya hivyo. Wao na Wahindi piya wameazimiana katika Upishi. Yayumkinika kuwa katika Kireno, Kiarabu na lugha nyenginezo kuna maneno ya Kimvita, Kijomvu, Kiamu, na kadhalika. Hili ni suala ambalo halihitaji mjadala mkubwa kwani liko waziwazi. Ikiwa baba Adamu (a.s.) na mama Hawaa walizungumza lugha moja kwa nini leo tuwe na lugha, makabila na mataifa tungu nzima? Tazama katika Quraani [Al-Hujuraat aya 13 na Ar-Rum aya 22].
Kwa mfano ukiangalia namna mataifa ya Arabu na Yahudi yalivyoanza utaona ya kuwa ni kama mtezo. Historia na dini yatueleza kuwa Mayahudi na Waarabu wanatokamana na Mtume Yaaqub (a.s.) na Mtume Ismael (a.s.). Ikiwa hii ni kweli, kwa nini iwe hivi na wote wawili wanatokana na Mtume Ibrahim (a.s.) ambae taifa lake hatulijui wala hatukuelezwa. Kwa nini wajukuu, vitukuu, vilembwe, na vilembwekeza vya Nabii Ibrahim wawe na taifa tofauti na yeye? Tena tofauti yenyewe si ya taifa moja bali mataifa mawili, angalau!
Mwana Ismael azae Waarabu na mjukuu Yaaqub (mtoto wa Is-haka) azae Mayahudi. Hii yote hapa ni kuwa tunajaribu kuonyesha ya kuwa kunahitajika sababu ndogo mno (pengine hata isiyoingia akilini mwetu) kuzaliwa kwa taifa jipya au kabila mpya. Lakini hii ni kazi ya Allah (s.w.t.) kama aya za hapo juu zinavyoonyesha. Halafu isitoshe, baada ya kuzaliwa kwa Taifa la Arabu, kukaanza Makabila kama vile Qureish, Aws, Khazraj, na kadhalika. Bado haijatosha, kukazaliwa Koo mbali mbali, kama vile kwenye kabila ya Qureish kuna koo kama Umayya, Makhzum, Alawi, Hashim na kadhalika. Ikiwa haya yote yawezekana, kwa nini visiwezekani kuapo kwa taifa la Swahili na makabila kama vile Mvita, Ngazija, Giriama, na Makunduchi? Au kwa nini kusiwe na koo kama vile Mwinjaa, Wanyali, Wamuyaka, na kadhalika?
Hii leo ni jambo gani linalomuunganisha Muarabu kutoka Sudan na yule wa kutoka Lebanon na yule wa kutoka Hijaz? Sio dini, wala rangi, wala nywele, wala tabia, wala mapishi! Huenda moja au zaidi ya mambo haya yakafanana, lakini jambo kubwa linalowafanya wote wakaitwa Waarabu ni Lugha, na labuda Asili. Labuda na Mayahudi ni vile vile, mtukue Yahudi wa Palestine, na yule wa Habashi na yule wa Urusi; kitu kitakacho waunganisha ni Asili, na pengine lugha na dini.
Kwa hivyo Swahili ni taifa ambalo lipo, na lenye makabila yasiopungua kumi na tano, tokea mji wa Barawa (kaskazini) mpaka mji wa Sofala (kusini). Ni taifa ambalo makabila yake yametapakaa katika nchi sita: Somalia, Kenya, Tanganyika, Zanzibar, Ngazija (Comoro Islands), na Msumbiji (Mozambique). Kwa hiyo, nasema tena ya kuwa Swahili ni Taifa. Ni muhimu kufahamu ya kuwa mtu anaposema kuwa yeye ni Mswahili haimaanishi kuwa kabila yake ni Swahili bali ni kuwa anatokamana na Taifa La Waswahili. Na kitu kinachowaunganisha watu katika taifa hili ni: Asili na Lugha.