MUHADHARA WA TATU : FASIHI YA KISWAHILI NI NINI? - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Chuo (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=3) +---- Forum: Shahada (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=20) +----- Forum: Nukuu (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=22) +----- Thread: MUHADHARA WA TATU : FASIHI YA KISWAHILI NI NINI? (/showthread.php?tid=1268) |
MUHADHARA WA TATU : FASIHI YA KISWAHILI NI NINI? - MwlMaeda - 09-24-2021 MUHADHARA WA TATU
FASIHI YA KISWAHILI NI NINI?
Kuhusu dhanna ya fasihi ya Kiswahili kuna mjadala mkali sana miongoni mwa wanazuoni tangu miaka ya 1970-1990.
Mgogoro huu ulizuka kutokana na hofu ya baadhi ya watu kuwa kuna njama za kuwameza Waswahili au kukana juu ya kuwepo kwa kabila au jamii ya waswahili.
Ilidaiwa kwamba waswahili ni watu wenye asili ya Mwambao wa Afrika Mashariki nao wana fasihi yao ambayo huelezwa kwa lugha yao ya Kiswahili.
Kuna wale walioona kuwa waswahili ni kabila au taifa mahususi (Sengo 1987:217) na hivyo wanayo fasihi yao mahususi ambayo ndio inayostahili kuitwa Fasihi ya Kiswahili na zile nyingine zinazotumia Kiswahili ziitwe Fasihi kwa Kiswahili.
Kundi lingine linaamini kuwa hakuna kabila la waswahili na hivyo kwa mantiki hiyo hakuna fasihi ya waswahili (Senkoro 1988:11) anasema; Tunasema kuwa kazi fulani ni fasihi ya Kiswahili au la kutokana na jinsi inavyotambulisha utamaduni wa waswahili, hapa neno “waswahili” halimaanishi kabila la waswahili kwani kabila la namna hiyo halipo leo.
Waswahili hapa ni wananchi wote wa Afrika Mashariki na kati kwa ujumla na si watu wa Pwani tu.
Kundi lingine linaloona kuwa fasihi ya Kiswahili ni fasihi inayoelezwa kwa lugha ya Kiswahili ni kundi la Mazigwa (1991:18) pamoja na Syambo na Mazrui (1992)
Kwa ujumla kutokana na majadiliano hayo unaweza kupata maswali ya msingi kama vile:
– Mswahili ni nani?
Mswahili kama inavyoelezwa katika HISI ZETU cha Sengo na Kiango; ni: (mzaliwa wa pwani kwa asili, msemaji wa lugha ya Kiswahili kwa ufasaha, muislamu na kwa maana za utani mswahili ni mtu asiyetimiza miadi na mjanjamjanja)
– Mswahili yukoje?
Mswahili anaweza kujipambanua zaidi kwa nje kupitia mavazi, shughuli za uzalishaji mali, mahusiano yake ya kijamii na kupitia fasihi yake kwa ujumla.
– Uswahili ni nini?
Uswahili ni mfumo mzima wa maisha ya Mswahili unaomtofautisha na watu wa jamii nyingine, kama ilivyo uchaga kwa mchaga, umasai kwa mmasai au uhaya kwa muhaya.
– Kiswahili ni nini?
Ni lugha ya waswahili na ndiyo huitumia kuelezea mila zao.
Majibu ya maswali hayo ni nguzo muhimu sana katika kuamua kama kuna fasihi ya Kiswahili au la.
FASIHI YA KISWAHILI NI IPI?
Wataalamu wa fasihi walio wengi na hasa waswahili wanaamini kuwa jamii ya waswahili ipo ingawa yawezekana kuwa waliitwa au kujiita kwa majina mbalimbali kama vile (wa-amu, wapate, wamvita, wapemba au waunguja)
Watu hawa waliunganishwa na lugha moja ya utamaduni wa aina moja na wote ni wenyeji wa Mwambao wa Afrika Mashariki na visiwa vyake na ndio wajulikanao kwa jina la waswahili.
Kuwepo kwa watu hao ni ithibati kuwa wanayo fasihi yao ambayo yapaswa kuitwa fasihi ya Kiswahili ya waswahili na mifano yake ni pamoja na Utendi wa Fumo Liyongo na nyimbo mbalimbali za shughuli za kijamii kama harusi, uvuvi, unyago, misiba, n.k
Kuenea kwa lugha ya Kiswahili sehemu nyingi za Afrika Mashariki kumeifanya lugha hiyo kuwa chombo cha fasihi ya watu wote wanaoitumia lugha hiyo hasa baada ya kuingia kwa wakoloni.
Syambo na Mazrui (1992) wanasema; Hatuna budi kuichukulia fasihi ya Kiswahili kuwa ni ile iliyoandikwa kwa Kiswahili tu bila kujali inazungumzia utamaduni wa Kiswahili au mwingineo maadam imetumia lugha ya Kiswahili na inafuata mbinu za ufasa wa lugha hiyo basi ni fasihi ya Kiswahili.
Kuenea kwa Kiswahili ndani na nje ya Afrika Mashariki na hata nje ya bara la Afrika kumezua fungu la fasihi ya kigeni katika lugha ya Kiswahili mfano; tafsiri mbalimbali kama Biblia, Mabepari wa Venisi, Bwana Muyombekere na Bibi Bugonoka; Ntulanalwo na Bulihwali (Anicet Kitereza, 1980) zimeibua aina ya fasihi ijulikanayo kama Fasihi kwa Kiswahili.
Baadhi ya wanafasihi wanaamini kuwa fasihi ya Kiswahili ni ile iliyobuniwa na mswahili tu kwa kutumia lugha ya Kiswahili bila kujali inazungumzia utamaduni wa Mswahili au la.
Wapo wengine wanaoamini kuwa fasihi ya Kiswahili ya Waswahili ni ile iliyobuniwa na mswahili kuhusu utamaduni wa Waswahili.
Kundi la tatu ni lile linalodai kuwa fasihi kwa Kiswahili ni ile iliyobuniwa na kuandikwa na mtu asiye mswahili au kwa lugha nyingine na kisha ikafasiriwa kwa lugha ya Kiswahili.
Mfamo:
– Mfalme Edipode
– Takadini
– Barua Ndefu Kama Hii
– Mabepari wa Venisi
– Orodha, n.k
AINA ZA FASIHI YA KISWAHILI KWA JINSI YA UWASILISHAJI
Fasihi ya Kiswahili hugawanywa katika aina mbili kulingana na jinsi ya uwasilishaji.
– Fasihi simulizi
– Fasihi andishi
FASIHI SIMULIZI
Ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi. Hivyo fasihi simulizi ni tukio linalofungamana na muktadha fulani wa kijamii. Fasihi simulizi hutawaliwa na mambo yafuatayo:
– Fanani
– Hadhira
– Fani inayotendwa
– Mahali/mandhari
– Wakati
– Tukio lenyewe
Kwa kawaida fasihi simulizi hutungwa kichwani kabla au wakati uleule wa kutamkwa. Hata hivyo fanani huwa na uhuru wa kubadili matini ya utungo wakati wowote ili kukidhi mahitaji ya muktadha na hadhira yake.
Tanzu za fasihi simulizi ni nyingi na hutofautiana kulingana na jamii. Pamoja na wingi wake wataalamu wameziweka katika makundi yafuatayo:
(a) Mazungumzo
Tanzu zilizomo katika kundi hili ni hotuba, malumbano ya watani, soga na mawaidha.
(b) Masimulizi (yale yote yanayosimuliwa)
Hapa huingizwa tanzu mbalimbali za hadithi kama vile ngano, hekaya, hurafa, simulizi za kihistoria na kiasili kama vile visakale, mapisi, tarihi, kumbukumbu na visasili.
© Maigizo
Hapa huingizwa tanzu mbalimbali kutegemeana na shabaha na muktadha.
(d) Ushairi
Hubeba tanzu kama nyimbo, maghani, tenzi, ngonjera na mashairi.
(e) Semi
Huwa na misemo kama methali, vitendawili, simo, mafumbo, lakabu na mizungu.
(f) Ngomezi
Ni fasihi simulizi inayowasilishwa kwa kutumia mlio wa ngoma badala ya mdomo.
FASIHI ANDISHI
Ni sanaa itumiayo maneno teule ya lugha kufikisha ujumbe kwa njia ya maandishi. Kuwapo kwa fasihi andishi hutegemea;
– Mtunzi –anayetunga kazi ya fasihi
– Hadhira –mlengwa wa kuisoma kazi hiyo
– Mchapishaji – anayepiga chapa kazi husika
Fasihi andishi inagawanyika katika makundi mawili ambayo ni:
– Nudhumu – ushairi (hujumuisha tenzi,ngonjera na nyimbo)
– Nathari – masimulizi ya kimjazo yanayofuata kanuni za kimasimulizi
|