Kiswahili ni lugha ambayo huzungumzwa na zaidi ta watu milioni mia moja kote ulimwenguni. Aidha, ni lugha ya saba ulimwenguni na ya pili barani Afrika kwa kuwa na wazungumzaji wengi. Ni lugha ya kitaifa na rasmi nchini Kenya na Tanzania. Aidha, ni moja kati ya lugha rasmi katika vikao vya Umoja wa Afrika. Lugha hii ilizungumzwa mara ya kwanza pwani ya Afrika Mashariki. Asili ya lugha hii imetafitiwa na wanaisimu na wanahistoria na wamezuka na nadharia zinazokinzana.
Chimbuko la Kiswahili
Neno chimbuko lina maana ya mwanzo au asili ya kitu. Wanaisimu kadha wamejaribu kuchunguza asili ya lugha ya Kiswahili na kutuachia kumbukumbu za kutusaidia kukuza welewa wetu.
Nadharia ya lugha mseto/ lugha chotara
Baadhi ya watu wanaoshikilia kuwa Kiswahili ni lugha ya mseto ni pamoja na Fredrick Johnson, Carl Meinhof, G.W. Broomfield, W.E. Taylor, Askofu Dakta Steere, W. Broomfield, W.H. Whiteley miongoni mwa wengine.
Nadharia hii inadai kuwa kutokana na kuingiliana kwa lugha za kigeni kama Kiarabu, Kiajemi, Kihindi na lugha za makabila ya wenyeji wa pwani ya Afrika Mashariki, maneno yalichukuliwa na vizalia vya mazingira hayo ya maingiliano kutoka kwa lugha hizo. Kwa msemo mwingine, nadharia hii inadai kuwa wageni walioana na wenyeji na kwa hivyo lugha zao za akina baba, mama na wajomba zilitumiwa kuunda lugha ya Kiswahili.
Wanadai Kiswahili kilizuka ili kufanikisha mawasiliano katika shughuli za kibiashara na kwamba hakikuwepo kabla ya kuja kwa kwa wageni.
Madai haya ya lugha mseto vilevile hayana msingi. Kulingana na taaluma ya isimu, lugha chotara au pijini huwa tofauti sana na lugha zinazokutana au kuchanganyana ili kuibusha. Uchanganuzi wa lugha ya Kiswahili unaonyesha ni lugha yenye tabia na sifa za Kibantu.
Udhaifu mwingine wa nadharia hii ni kuwa inaegemea kwenye kipimo au kigezo kimoja tu: msamiati. Ni ukweli kuwa Kiswahili kina maneno mengi ya Kiarabu, Kiajemi, Kihindi, Kireno, Kiingereza lakini kigezo cha msamiati pekee hautoshi. Lazima muundo nasifa nyinginezo kama sauti zichunguzwe.
Nadharia kuwa Kiswahili ni lahaja ya Kiarabu
Kuna wataalamu wanaodai kuwa Kiswahili ni mojawapo ya lahaja za Kiarabu kwa sababu kuna idadi kubwa ya msamiati wa Kiarabu katika Kiswahili. Wanadai kuwa asili ya jina Kiswahili limetokana na neno la Kiarabu sahil kwa maana ya pwani. Wingi wake ni sawaahil. Isitoshe, wanadai kwamba idadi kubwa ya wenyeji wa pwani ni Waislamu, dini iliyoletwa na Waarabu. Kwa hivyo, ikiwa Kiswahili kilianza pwani na wasemaji wake ni Waislamu, basi hata nacho kilitoka Uarabuni. Aidha, wanaoshikilia nadharia hii wanasema kuwa Kiswahili ni tokeo la ndoa baina ya wanawake wa pwani ya Afrika Mashariki na Waarabu; kwamba watoto walozaliwa walizungumza Kiarabu!
Udhaifu unatokana hapa: Pana uwezekano gani, kwa mfano, wa mtu mwenye asili ya Kikuyu na Mluo kuoana na kisha mtoto wao aongee lugha ngeni. Na je, kwa nini lugha ya Kiingereza ambayo ina asilimia takribani 70% ya maneno ya Kilatini na Kiyunani (Kigiriki cha kale) hauitwi lugha ya vizalia?
Madai haya hayana mashiko kwani japo ni kweli kuwa takribani asilimia 30% za viini vya maneno ya Kiswahili inatokana na lugha ya Kiarabu, Zaidi ya asilimia 65% ya viini vya maneno yote ya Kiswahili inatokana na lugha ya Kibantu. Maneno yaliyoazimwa kutoka Kiarabu na lugha nyinginezo yalihusu utamaduni na vitu visivyopatikana katika utamaduni na mila wa Mwafrika, kwa hivyo, Kiswahili kinabakia kuwa lugha ya Kibantu.
Vilevile, hakuna uhusiano uliopo baina ya dini na lugha. Hata Kiarabu chenyewe kilikuwepo kabla ya kuja kwa dini ya Kiislamu ilioibuka katika karne ya sita Baada ya Kristo (BK).
Nadharia kuwa Kiswahili ni lugha ya Kibantu
Huu ndio msimamo unaokubaliwa na watu wengi. Mwasisi wa nadharia hii alikuwa Profesa Malcolm Guthrie. Wataalamu wanadhihirisha kuwa Kiswahili ni lugha ya Kibantu kwa kufafanua awamu zifuatazo za maenezi ya Wabantu. Kulingana na utafiti wa wataalamu hawa, chimbuko la Wabantu ni Afrika Magharibi, sehemu za nchi ya Kameruni. Kutoka huko, Wabantu walienea katika sehemu wanazokalia sasa. Maenezi haya yalifanyika katika awamu mbalimbali katika kipindi kirefu. Awamu ya kwanza kulingana na ushahidi wa kihistoria ilifanyika kati ya mwaka 40 hadi 10 Kabla ya Kristo (KK). Mtandao huu wa maenezi ulilipeleka kundi moja la Wabantu hadi ukanda wa Kusini mwa misitu ya Kongo na kundi jingine sehemu za Magharibi ya eneo la Ziwa Viktoria.
Mtawanyiko wa pili ulitokea mwaka 1 KK. Kundi la Wabantu lililokuwa na maskani Kusini mwa Msitu wa Kongo lilitawanyika na kuenea eneo kubwa la Afrika ya Kati.Kipindi kati ya mwaka 100 hadi 1100 BK kilishuhudia wimbi la tatu la mtawanyiko uliotokana na ongezeko la watu na msongamano uliotokana na upungufu wa ardhi ya kilimo – ulisababisha kutawanyika kwa Wabantu kutoka sehemu za Katanga kuelekea Kusini na Kaskazini-Mashariki. Kundi hili la Wabantu ndilo liliingia nyanda za kati ya Afrika ya Mashariki katika karne ya kwanza na pili BK.
Wabantu walioingia Afrika ya Mashariki waliendelea kugawanyika katika vikundi vidogovidogo kadiri walivyozagaa na muda kupita. Baadhi ya vikundi hivi vilielekea upande wa Mashariki (sehemu ambayo sasa ni Kenya) mpaka kufikia Shungwayaya. Kulingana na fasihi simulizi, sehemu hii ya mabonde yenye rutuba ilikuwa baina ya Mto Juba huko Somalia na Mto Tana nchini Kenya.
Mnamo karne ya 5BK,Wabantu waliosakini Shungwaya walisambaa sehemu mbalimbali hasa za pwani ya Bahari Hindi. Kuhama huko kulisababishwa na majanga mbalimbali yakiwemo njaa kutokana naukame, maradhi ya kuambukiza, ukosefu wa ardhi yenye rutuba na msongamano wa watu. Lakini, tukio lililoharakisha uhamaji ni mashambulizi ya kabila la Wagalla.
Uhamiaji kutoka Shungwaya ulitokea kwa mikondo na nyakati tofauti. Baadhi ya kikundi cha Wabantu walielekea upande wa Magharibi, huku wengine wakienda Kusini. Kikundi kinachounda makabila ya Gikuyu, Wameru, Waembu na Wakamba walifuata Mto Tana na kuanzisha makaazi katika eneo linalouzunguka Mlima Kirinyaga au Kenya kama unavyojulikana leo hii. Wasegeju nao walielekea Kusini na kukalia eneo baina ya pwani na milima ya Usambara. Kikundi kinachojiita Wataita kilianzisha makaazi kwenye milima ya Taita karibu na Mlima Kilimanjaro.
Kikundi kinachounda makabila ya Mijikenda kiliteremka Kusini kikifuata ukanda wa mwambao kama kilomita 40 upana kuelekea bara. Hatimaye kikundi hiki kilianzisha maskani baina ya mji wa Malindi na Kusini ya Mombasa. Kikundi kingine, kilichounda kabila la Wapokomo kilielekea Kusini ya Mto Tana na kuanzisha makaazi kati ya mito Tana na Galana au Athi.
Kikundi kiitwacho Wangozi kilianzisha makaazi sehemu mbalimbali za ufuo wa bahari kuanzia Kismayu (Kusini mwa Somalia) mpaka Sofala kule Msumbiji. Wengine walivuka bahari na kuishi katika visiwa vya Lamu, Pate, Faza, Pemba, Unguja, Ngazija na Bukini.
Waswahili wanadai kuwa Kiswahili kuwa Kiswahili cha asili kilitokana na Kingozi, lugha ya Wangozi. Katika mapokezi mengi ya zamani, maneno ngozi, ngozini, na Wangozi hutokea kwa wingi. Asili ya kuitwa Wangozi ni kwa kuwa walikuwa wakipima mashamba kwa kanda ya ngozi. Pia, walikuwa wakiishi katika mji wa zamani, Ngozi.
Mapokezi ya Bwana Abdallah Barua ni kuwa mashairi ya Hamziya ni Kingozi cha kati ya Kivumba na Kingozi cha mwisho. Kingozi cha kwanza hakipo tena. Kingozi chasemekana kilianza kaskazini katika penya za visiwa vya Magunyani, Pate, Faza na Lamu na kushukia mpaka mipaka ya Mto Tana.
Waarabu walipofika upwa wa Afrika Mashariki katika karne ya 10 BK, waliwakuta Wangozi waliokuwa wamestawi kijamii na kibiashara. Walizikuta lahaja za lugha zilizokuwa zinafanana wakaziita swahil, yaani lugha za pwani au watu wa pwani. Baadaye, neno hili lilitoholewa kuwa Swahili. Lugha ya wenyeji wa pwani ilianza kuitwa Kiswahili.
Maingiliano ya kibiashara na kijamii kati ya wenyeji wa pwani na wageni yaliendelea kwa karne nyingi. Maingiliano hayo yalileta athari kubwa kwa lugha na utamaduni wa Waswahili. Kwa mfano, Waswahili wengi walisilimu na kuwa Waislamu. Aidha, idadi kubwa ya maneno ya Kiarabu yaliingizwa katika lugha ya Kiswahili.
Uchunguzi wa isimu historia na isimu linganishi uliofanywa na Malcolm Guthrie mwaka wa 1948 unaonyesha kuwa Kiswahili kina uhusiano na lugha zingine za Kibantu hasa tunapotazama mashina na mizizi ya maneno mengi kutoka lugh mbalimnali za Kibantu. Maneno ya asili kama vile kichwa, mkono, maji, njia na majina ya wanyama katika lugha hizi yanahusiana, na hivyo kubainisha kuwa yalitoka kitovu kimoja.
Jambo lingine ni kuwa Kiswahili kina irabu (vokali) tano kama zilivyo lugha nyingi za Kibantu. Irabu hizi ni a, e, i, o, na u.
Hali kadhalika, muundo wa msamiati wa Kiswahili kimsingi huchukua konsonanti – irabu (KI). Kwa mfano; karatasi, baba, kamata. Hata hivyo konsonanti mbili, tatu au nne zinaweza kufuatana. Kwa mfano; pwani, nywele, mchwa.
Mpangilio wa nomino za Kiswahili huleta uwiano wa kisarufi na huitwa ngeli za nomino. Hujitokeza katika lugha zingine za Kibantu. Mfano wa mpangilio wa nomino hizi ni ngeli ya A-WA, KI-VI, U-I, LI-YA. Nomino hizi zinapotumiwa katika lugha ya Kiswahili huwa na uwiano na vitenzi. Jambo hili pia hutokea katika lugha zingine za Kibantu, na kudhihirisha kuwa Kiswahili ni mojawapo ya lugha za Kibantu.
Katika maoni ya fasihi simulizi, asili ya Kiswahili ni Kingozi. Mashairi ya Hamziya yaliyoandikwa katika karne ya 18 yaliandikwa kwa Kingozi. Kingozi kilikuwa kikizungumzwa sehemu iliyoitwa Uswahili, upande wa visiwa vya Magunyoni (Pate, Lamu, Faza) hadi bara kupakana na Mto Tana.
Asili ya neno Kiswahili inasemekana ilitokana na kijana wa Kingozi aliyeulizwa na wageni kutoka Uarabuni kuwa wao ni kina nani, naye akajibu kuwa ‘’Sisi ndio wenye siwa hili.’’Yaani wenyeji wa kisiwa hili. Kutegemea wakati na matamshi, jina hili lilibadilika na kuwa Waswahili.
Wazo la pili ni kuwa wageni waliuita upwa wa Afrika Mashariki Sahil, wingi wake Sawahili, yaani pwani. Kiambishi ‘’ki’’ kiliongezwa kuonyesha lugha na kuwa Kisuaili na hatimaye Kiswahili, jina ambalo lilianza kutumika Kaskazini mwa Kenya karibu na Lamu katika karne ya saba na nane baada ya kuzaliwa Kristo.
Ushahidi wa kihistoria unaonyesha kuwa katika karne ya kwanza ya Kristo, neno ‘Azania’’ limetajwa katika kitabu cha Maelezo ya Bahari Hindi (Periplus of Erythrean Sea) kutaja sehemu za Afrika Mashariki. Wasafiri wengine walozungumza juu ya lugha hii katika Afrika Mashariki ni Ibn Batuta, Ibn Masud na Al-Idris.
Baadhi ya wasafiri hao wa kale walinukuliwa kutaja maneno ya Kiswahili kama vile ‘mkono wa tembo’ na ‘kisukari’ yaliyokuwa majina ya ndizi. Majina haya hata sasa yanatumika.
Maenezi ya Kiswahili
Misafara ya biashara iliyokuwa ikitoka pwani ya Afrika Mashariki kwenda bara ilisaidia kueneza Kiswahili. Mwanzo kabisa safari hizi zilikuwa zikifanywa baina ya Waafrika wa pwani na wale wa bara. Kundi la pili lilikuwa la wafanya biashara wa Kiarabu walioingia bara kutafuta pembe za ndovu na watumwa. Waarabu hawa hawakuja na ujuzi wa lugha hii. Walifundishwa na wenyeji wa pwani na bara ambaowalikuwa wapagazi wao. Misafara hiyo ndio iliyoeneza Kiswahili Kongo na lahaja ya Kingwana ilizuka huko Kongo.
Maenezi ya pili yalifanywa na wamishenari. Dini za kigeni zina nafasi muhimu katika maenezi ya Kiswahili. Kwanza kabisa, Waarabu walipokuja iliwabidi kuhubiri dini lao (Kiislamu) katika lugha ya Kiarabu. Kwa vile wenyeji hawakujua Kiarabu, ilibidi wageni wajifunze Kiswahili ili waweze kueneza dini yao vilivyo. Mashehe na maulama wakaanzisha matumizi ya maandishi ya Kiswahili wakitumia abjadi za Kiarabu. Wamishenari kutoka Ulaya walipokuja hawakutumia Kiswahili sana kwa sababu kilihusishwa na dini ya Kiislamu. Wao walitumia zaidi lugha za kienyeji, lakini baadaye walibadilisha mtindo huo. Kwanza kabisa, ilionekana wangefanikiwa zaidi iwapo wangetumia lugha ya Kiswahili.
Pili, ilikuwa ghali kuchapisha vitabu katika lugha tofauti za kienyeji. Tatu, iliwabidi wajifunze lugha nyingi katika maeneo yao ya mahubiri. Wamishenari hawa walianzisha shule za dini kwa lugha ya Kiswahili. Walianzisha maandishi ya abjadi ya Kirumi ambayo yanatumika hadi sasa.
Baadhi ya wamishenari waliofanya bidii kuandika wakitumia maandishi hayo ni Askofu Edward Steere na Ludwig Krapf. Pia wamishenari walianzisha magazeti yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili. Baadhi ya magazeti haya ni Msimulizi (1888), Habari za Mwezi (1894), na Habari za Wakilindi (1905), Rafiki Yangu (1905) ilichapishwa Mombasa. Ufalme wa Mungu ilichapishwa Vuga, Pwani na Bara (1910).
Krapf alitoa tafsiri ya Injili ya Luka na Injili ya Yohana ili kuwasaidia wamishenenari wengine waliokuja katika janibu hii ya Afrika Mashariki. Hali kadhalika Krapf alishughulikia kamusi ya Kiswahili-Kiingereza. Uandishi huu ulitoa msingi wa maenezi ya Kiswahili.
Maenezi ya tatu yalifanywa na utawala wa kikoloni. Kwanza kabisa, utawala wa Sultani wa Zanzibar. Alipopewa sehemu ya maili kumi mraba kutoka ufuo wa bahari, Kiswahili kilitumika zaidi katika sehemu hii. Sehemu fulani katika pwani ya Kenya ilikuwa chini ya mraba huu.
Wajerumani walikuza Kiswahili kupitia kwa shughuli zao za utawala kwa sababu kilikuwa kimeenea zaidi. Walifanya Kiswahili kutumika katika shughuli mawasiliano . Ilibidi wafanyikazi wa serikali kumaizi lugha ya Kiswahili. Ili uajiriwe kama jumbe au afisa wa serikali lazima ungejua Kiswahili.
Shule za msingi zilifundisha Kiswahili nchini Tanganyika lakini nchini Kenya shule za msingi zilifundisha kwa lugha za kienyeji ingawa badhi yazo zilitumia Kiswahili, hasa zile zilizokuwa mijini. Sera ya Waingereza haikutilia maanani Zaidi matumizi ya Kiswahili kama lugha ya mafunzo bali Kiingereza kilitumiwa zaidi.
Wakati wa harakati zakupambana na ukoloni, Kiswahili kiltumiwa kama lugha ya mawasiliano. Mikutano mingi ilifanywa kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Waingereza waltanabahi kuwa Kiswahili kilikuwa kinatumiwa kama chombo cha umoja katika harakati za kudai uhuru nchini Kenya; walisitisha matumizi yake kama lugha ya kufundishia n hata ufundishaji wa lugha yenyewe na, badala yake, walitilia mkazo matumizi ya lugha za kienyeji. Hatua hii ilidhamiria kuvunja umoja wa Wakenya. Nchini Tanganyika, Kiswahili kilitumiwa sana hasa katika harakati za kupigania uhuru. Mikutano ya vyama tofauti ilihutubiwa kwa lugha ya Kiswahili.
Nchini Uganda, Kiswahili hakikuenea sana kwa sababu kilipigwa vita na wamishenari na Waganda wenyewe waliokifungamanisha na dini ya Uislamu.
Mwisho, rekodi zilizoimbwa na wanamuziki wa Afrika Mashariki kama Edward Masengo na Jimmy Mwenda Bosco (wote kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) zilisaidia katika kueneza Kiswahili.
Kwa sasa Kiswahili ni lugha rasmi na lugha ya taifa nchini Tanzania na Kenya. Baraza la Kiswahili la Tanzania (BAKITA) ni taasisi inayoshughulikia maswala ya Kiswahili. Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki ilibadilishwa na kuwa Taasisi ya Uchunguzi wa Lugha ya Kiswahili (TUKI).
Nchini Kenya, Kiswahili kilitangazwa kuwa Lugha ya taifa mwaka wa 1969. Mnamo 1975, kilianza kutumika katika shughuli za bunge.
Lugha ya Kiswahili ilifundishwa katika shule zote za msingi za umma nchini Kenya, na mwaka wa 1985 kilitahiniwa kwa mara ya kwanza katika mtihani wa kitaifa. Aidha, Kiswahili kama lugha imekuwa ikifunzwa na kutahiniwa katika shule za msingi na za upili kote nchini.
Mafunzo ya Kiswahili yanafanywa katika vyuo vya walimu na vyuo vikuu vyote vya umma nchini. Pia vyuo vya walimu wa shule za msingi hufunza Kiswahili kama somo la lazima.
Vyama vinavyoshughulikia masuala ya Kiswahili nchini Kenya ni Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) na Chama cha Waandishi wa Kiswahili wa Taifa (WAKITA) miongoni mwa mengine. Vyama hivi vimesaidia katika maenezi ya Kiswahili kwa kuandaa warsha mbalimbali za kuinua hadhi ya Kiswahili nchini.
Vyombo vya habari kama redio na runinga, hasa Shirika la Utangazaji wa Kenya (KBC) na vituo vingine vingi vilivyoibuka katika miaka za mwisho mwisho wa karne iliyopita vimesaidia katika kuendeleza na kusambaza Kiswahili.Vituo hivi hutangaza kupitia kwa redio na kwenye runinga.
Dhima ya magazeti haiwezi kusahauliwa. Kwa mfano, gazeti la Taifa Leo linalochapishwa kila siku nchini Kenya na mengine kama Majira, Nipashe, Kasheshe na kadhalika kutoka nchini Tanzania zinachangia kufunza na kueneza lugha ya Kiswahili kupitia makala mbalimbali na matumizi ya lugha yenyewe.
Katika mfumo wa elimu ya 8-4-4 (miaka minane katika shule ya msingi na minne katika shule za upili na mingine isiyopungua minne katika vyuo vikuu), Kiswahili ni somo la lazima kwa wanafunzi wa shule za msingi na wa shule za upili. Somo hili linatahiniwa katika viwango hivi. .
Matatizo ya kuenea kwa lugha ya Kiswahili nchini Kenya
Misafara iliyoanzia Mombasa na Malindi ya wafanyibiashara ilikuwa michache kutokana na hali ya vita ambavyo vilikuwepo Mombasa, Siyu na Pate. Wenyeji walipigana na tawala za kisultani, Kireno na watawala wa Shirazi.
Magonjwa ya malaria na malale yaliwashambulia wafanyibiashara waliojaribu kuelekea sehemu za bara.
Kulikuwa na ukame mkubwa ulioenea sehemu kubwa kuanzia Mombasa kupitia Sultan Hamud.
Mkazo mkubwa kuwapo katika ufundishaji wa lugha nyinginezo, hasa zile za kikabila katika shule za msingi
Misafara ya biashara haingeweza kupitia nchini Kenya kwa sababu waliogopa kupigwa vita na Wamaasai na baadaye kidogo Wanandi.
Simba wala watu katika maeneo ya Tsavo waliwashambulia wafanyibiashara waliojaribu kupitia kwenye nyika walimoishi.
Kuhusishwa kwa lugha ya Kiswahili na dini ya Kiislamu na eneo la pwani tu.
Wamishenari wa kwanza kupendelea kueneza dini zao kwa kuzitumia lugha za kikabila.
Kuwepo kwa kasumba ya kuamini kuwa lugha ya Kiingereza au lugha nyinginezo za kigeni zina hadhi kubwa.
Kutokuwepo kwa sera mwafaka kuhusiana na matumizi ya Kiswahili kwa muda mrefu.
Kutokuwepo kwa waandishi wa kutosha wanaoandika katika lugha ya Kiswahili.
Kuchukuliwa kwa Kiswahili kama lugha duni ambayo inahusishwa na watu wa ngazi fulani za kimaisha tu.
Ukosefu wa wataalamu wa kutosha kumaanisha kuwa ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa njia ifaayo unakabiliwa na tatizo kubwa.
Jambo lingine ni kuwa sehemu inayotumia Kiswahili ni kubwa sana. Eneo hili liliweza kufanya lahaja mbalimbali za Kiswahili kuchimbuka.
Uhaba wa magazeti au majarida ya Kiswahili ambayo ni msingi muhimu wa usambazaji wa lugha.
Mashirika ya uchapishaji kuelekea kukipa Kiingerea kipaumbele katika uchapishaji wao.
Licha ya pingamizi hizi, Kiswahili kiliweza kuenea katika nchi za Afrika Mashariki na Kati na kwingineko ulimwenguni.
Usanifishaji wa lugha ya Kiswahili
Kusanifisha ni kufikia uamuzi wa kufuata utaratibu fulani. Hivyo basi, usanifishaji wa lugha ni kuwa na kanuni maalumu zinzotawala matamshi na maandishi ya lugha. Msingi wa Kiswahili Sanifu tunachozungumza nchini Kenya na kwingineko ni Kiunguja. Hata hivyo, lugha hii imepiga hatua kubwa na kutofautiana kwa kiasi kikubwa na Kiunguja. Lugha yoyote ile inayokua lazima ikope kutoka lugha nyinginezo. Maneno hayo huweza kujadiliwa na kukubaliwa na hatimaye kusambazwa ili yatumiwe na wazungumzaji.
Kuna sababu kadha ambazo ziliwatia wakoloni shime na ghera ya kuchukua azma ya kusanifisha Kiswahili.
Kwanza, kuondoa utata wa kutumia lahaja tofauti katika mawasiliano.
Pili, walihitajika (Wakoloni) kupata lugha moja ya uandishi wa vitabu vya masomo katika nchi zote za Afrika Mashariki.
Tatu, palihitajika lugha ambayo ingetumiwa katika shughuli za kufundishia katika nchi zote za Afrika Mashariki.
Jambo lingine lilikuwa kusawazisha hati za Kirumi kwa matumizi ya Kiswahili badala ya hati za awali za Kiarabu.
Palihitajika pia usawazisho wa maendelezo (tahajia/hijai) ya lugha hii ili kuwe na sarufi moja iliyokubalika.
Aidha, palihitajika lahaja moja ambayo ingetumika kutafsiri vitabu vilivyokuwa vimeandikwa tayari.
Haya ni baadhi ya mambo yaliyochochea shughuli za usanifishaji miongoni mwa mengine. Lahaja iliyochaguliwa kwa usanifishaji wa Kiswahili ilikuwa ile ya Kiunguja, ingawa baadhi ya wataalamu walipendekeza Kimvita na wengine Kiamu. Kiunguja kilichaguliwa kwa sababu tayari kilikuwa kimeteuliwa kama lugha ya kutumiwa nchini Tanganyika mnamo mwaka wa 1925 katika mkutano wa Gavana wa Tanganyika.
Jambo la pili ni kuwa Kiunguja kilikuwa kimeenea sana kwa kuwa Unguja ndiko kulikuwa kitovu cha wafanyibiashara. Kwenye kamati hiyo hapakuwa na Mwafrika hata mmoja. Waafrika waliana kuchaguliwa kuwa washiriki mnamo mwaka 1939 kakini hawakushiriki katika mijadala hadi mwaka wa 1946.
Ingawa lahaja ya Kiunguja iliteuliwa kuwa msingi wa Kiswahili rasmi, udhaifu wa hatua hii bado unadhihirika. Kwanza, usanifishaji ulipuuza lahaja nyingine zenye utajiri wa msamiati. Huenda Kiswahili kingekuwa na ukwasi zaidi kama lahaja zote zingeshirikishwa tokea mwanzoni. Pili, walioongoza usanifishaji wa Kiswahili ni wageni na hawakuwashirikisha wenyeji.Hili lilimsukuma Broomfield, mmoja wa Wazungu aliyejihusisha na usanifishaji, kulalamikia hatua ya kuwatenga wenyeji katika ukuzaji wa lugha yao.
Mnamo Januari mosi, 1930, serikali za nchi nne za Afrika Masharikizilipata kibali kutoka kwa Waziri wa Kikoloni kuunda baraza ambalo lingeshughulikia usanifishaji wa Kiswahili. Kamati iliyoundwa iliitwa Inter-Territorial (Swahili) Language Committee (Kamati ya Lugha ya Kiswahili ya Afrika Mashariki).Kamati hii ilikuwa na majukumu haya:
Kusanifisha matumizi ya maandishi katika lugha ya Kiswahili kote Afrika Mashariki.
Kutunga kamusi za kutumia.
Kutafiti lahaja za Kiswahili ambavyo vingetumika katika masomo.
Kuboresha vitabu vya shule na vingine vilivyokuwa tayari vimechapishwa ilipohitajika.
Kusoma na kuhakiki vitabu vilivyoshughulikiwa na kamati. Kufanya tafsiri za vitabu vingine kwa lugha ya Kiswahili.
Kujibu maswali yanayohusu lugha ya Kiswahili na fasihi yake. Kuwatia moyo waandishi, hasa wenyeji wa lugha ya Kiswahili. Kuwapa watu wote walio na hamu ya uandishi motisha kwa
kuwashauri kuhusu uandishi wa vitabu wanaokusudia kuandika. Kusahihisha vitabu vya shule vilivyokwisha kuchapishwa.
Baadhi ya mafanikio ya kamati ni tafsiri ya vitabu vya Kiingereza kwa lugha ya Kiswahili. Kwa mfano: King Solomon’s Mine – Mashimo ya Mfalme Suleiman, Alice in Wonderland – Alice katika Nchi ya Ajabu, Guliver’s Travel – Safari za Guliva.
Jambo lingine ni kuchapishwa kwa kamusi za ‘A Standard English-Kiswahili Dictionary’ pamoja na Kamusi ya Kiswahili- Kiingereza zilizohaririwa na Fredrick Johnson.
Kamati ya usanifishaji ilipitia hatua mbalimbali kuanzia mwaka wa 1930 hadi 1962. Kwa mfano, ilibadilisha jina lake na kuwa East African Swahili Committee, kisha ikabadili na kuwa Institute of Swahili Research (Chuo cha Uchunguzi wa Lugha ya Kiswahili) na hatimaye Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) yenye makao yake nchini Tanzania katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Sasa hivi kinaitwa Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili (TATAKI).
Wakati huo huo, kampuni ya East African Literature Bureau (EALB) ilianzishwa ili kusaidia katika kazi ya kuendeleza na kueneza Kiswahili baada ya kamati kulemewa na kazi. Shirika hili lilikuwa na kibali cha kupitia na kupitisha miswada yote ya Kiswahili na kuthibitisha ubora wa lugha yake. Usanifishaji wa lugha ni harakati zinazoendelea lakini mwaka wa 1930 ndio ulioweka msingi wa usanifishaji.
Matatizo ya usanifishaji
Tatizo la kutafsiri moja kwa moja kutoka lugha ya Kiingereza hadi Kiswahili bila kuchunguza ikiwa yale maneno yanawza kupatikana katika lugha za Kibantu. Kwa mfano:
Speaker (Kiingereza) – Spika
Sister (Kiingereza) – Sista
Forward (Kiingereza) – Fowadi
Tatizo lingine lilikuwa ni wingi wa maneno yaliyoingizwa katika Kiswahili yanayotokana na lugha za Kibantu za Tanzania kama vile Kinyamwezi, Kizanaki, na kupuuza makabila ya Kibantu kutoka Kenya, Uganda.
Migogoro baina ya washiriki waliopendekeza kusanifishwa kwa lahaja ya Kimvita na wale waliopigia debe lahaja ya Kiunguja.
Aidha, kuna wale waliokuwa na maoni kuwa lugha wastani iliundwa na Wazungu. Waafrika hawakuhusishwa katika kamati hii.
Usanifishaji wa Kiswahili nchini Kenya
Ingawa nchi ya Kenya haina chombo rasmi kinachohusika na usanifishaji rasmi wa maneno na istilahi, zimekuwako juhudi kadha:
Vyombo vya habari vina nafasi kubwa kufanikisha juhudi hizi. Usanifishaji huu umewezesha kuwepo kwa Kiswahili kinachoweza kutumika katika mawasiliano na shughuli mbalimbali nyinginezo. Baadhi ya maneno ambayo yametokana na juhudi hizi ni kama: tarakilishi (computer), UKIMWI (AIDS), eneobunge (constituency), barua pepe (e-mail), kotokoto (calculator), utandawazi (globalization), wavuti (internet), tovuti (website).
Uchapishaji wa vitabu vya kisarufi vinavyohimiza matumizi ya lugha sanifu.
Juhudi za Taasisi ya Elimu ya Kenya (K.I.E.) ya kusambaza nyenzo za kufundishia lugha.
Juhudi za kutumia lugha ya Kiswahili katika viwango mbalmbali ikiwemo bunge.
Hali ya Kiswahili baada ya uhuru nchini Kenya - Tume ya Ominde iliyobuniwa mwaka wa 1963 na kuanza shughuli zake rasmi 1964 ilipendekeza Kiswahili kiwe somo la lazima katika shule za msingi. Tume hii pia ilipendekeza itahiniwe katika shule za msingi na za upili.
- Tume ya Gachathi (1976) ilipendekeza Kiswahili kitumiwe kufundishia darasa la kwanza hadi la tatu katika shule za msingi katika sehemu za mijini.
- Tume ya Mackay (1981) nayo ilipendekeza Kiswahili kiwe somo la lazima kwa wanafunzi wote katika shule za msingi, upili na vyuo vya walimu.
- Kiswahili kilitangazwa kuwa lugha ya taifa mnamo mwaka wa 1969.
- Kiswahili kilitangazwa kuwa lugha ya bunge mnamo mwaka wa 1975. Kinatumiwa pamoja na Kiingereza kama lugha rasmi katika shughuli za bunge la Seneti na bunge la wawakilishi
- Wanaowania viti vya kisiasa katika ngazi zote hulazimika kukijua Kiswahili kama sharti mojawapo.
- Kiswahili sanifu kimeendelea kukuzwa na kuimarika. Vitabu vingi vya lugha, riwaya, hadithi fupi, tamthilia na hata kamusi za semi mbalimbali vimeandikwa.
- Kiswahili kimepewa hadhi kubwa nchini Kenya. Ni somo la lazima katika mtaalu wa elimu nchini kuanzia shule za msingi hadi za upili.
- Mwaka wa 1985 Kiswahili kilitahiniwa kwa mara ya kwanza katika mtihani wa kitaifa na ,waka wa 1989 watahiniwa wote wa kidato cha nne walifanya Kiswahili kama somo la lazima.
- Isitoshe, lugha ya Kiswahili hutumiwa kufunzia fasihi na hata isimu ya Kiswahili kuanzia shule za upili hadi vyuo vikuu.
- Kiswahili ni lugha ya kimataifa. Inafunzwa katika vyuo vikuu vingi bara Uropa, Asia na Marekani na nyumbani bara Afrika, Kenya ikiwemo.
- Katika Afrika Mashariki, ni chombo muhimu cha kuunganisha nchi sita: Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ndiyo lingua franka katika eneo hili.
- Vyombo vya habari hususan redio na runinga vimechangia pakubwa katika kuimarisha Kiswahili. Gazeti la Taifa Leo huchapishwa kila siku katika lugha ya Kiswahili.
- Maigizo, nyimbo na ukariri wa mashairi katika tamasha za mashindano tofauti kuanzia ngazi za tarafa hadi ngazi za kitaifa hutumia lugha ya Kiswahili. Kadiri baadhi wanavyokariri kwa Kiingereza, wengi hukariri kwa Kiswahili.
- Lugha ya Kiswahili hutumika katika mahubiri ya dini. Wahubiri wasio na makao maalumu au wale ambao hupatikana katika sehemu za mabustani hutumia lugha ya Kiswahili.Wengine katika makanisa au mikutano ya injili hutumia Kiingereza lakini wana wakalimani ambao hutoa maelezo hayo kwa Kiswahili.
- Taasisi ya Utawala ya Kenya hufunza Kiswahili ili watawala waweze kuwasiliana na wananchi vizuri pindi wanapopata uhamisho kutoka sehemu moja ya nchi hadi nyingine.
- Kiswahili kinatumiwa kuendeleza shughuli mbalimbali za kisiasa na utawala. Kwa mfano, kampeni nyingi mijini na hata vijijini huendeshwa kwa lugha ya Kiswahili.
Matatizo yanayokumba Kiswahili nchini Kenya
Lugha kama kitu kingine kile kinachokuwa hukumbwa na matatizo aina aina. Hakuna kitu au mtu anayeweza kudai kuwa hakusongwa na matatizo yoyote katika kukua au hata katika utu uzima wake. Kiswahili kama lugha yoyote ile kina matatizo yanayokitanza, mengine yanashabihiana na yanayozitatiza lugha zingine, hali mengine ni ya kipekee kutokana na mazingira yanayokilea.
Baadhi ya matatizo yamezuiliwa na Wazungu watawala wa Afrika Mashariki wa hapo awali, hali mengine tumeyazua sisi.
Fikra finyu miongoni mwa watu kuwa Kiswahili ni somo na lugha ya watu duni na wasioelimika. Fikra kama hii bila shaka ni ya watu ambao wana kasumba ya kikoloni.
Kustawishwa kwa Kiswahili kumekwazwa kwa kiasi kikubwa na kuzuka kwa kilugha cha Sheng’. Matumizi ya mkorogo huu wa maneno ya Kiswahili na Kiingereza pamoja na lugha mama za jamii mbalimbali yameenea sana, hasa katika sehemu za mijini. Hasara kubwa ni kuwa, wengi hupapia yatokayo mjini eti ni dalili za kuendelea na kwenda na wakati.
Kuna wale ambao matatizo yao kuhusu kukitumia Kiswahili yanatokana na athari za lugha yao tangulizi. Athari hizi husababisha kukiukwa kwa kanuni za sarufi za Kiswahili fakaifa (sembuse) matamshi! Mwingiliano wa lugha ya kwanza na Kiswahili umesababisha kukosekana kwa lugha sanifu.
Walimu wa Kiingereza hufunza tu Kiingereza na fasihi ilhali wa Kiswahili huhitajika kufunza Kiswahili, fasihi na somo nyingine tofauti kabisa. Hapo tunaona kwamba mwalimu wa Kiingereza atanufaika kwa vile atakuwa na umilisi zaidi katika uwanja wake na pia kuwa na muda kufanya utafiti.
Isitoshe, masomo yote nchini yanafundishwa katika lugha ya Kiingereza ilhali ni Kiswahili tu ndicho hufundishwa kwa Kiswahili.
Shule nyingi huwahimiza wanafunzi kuwasiliana katika lugha ya Kiingereza. Kiswahili hutumika katika somo tu. Aidha, baadhi ya taasisi hupiga marufuku kuzunguma Kiswahili isipokuwa siku ya Kiswahili.
Kiswahili hupewa muda mchache katika vyombo vya habari, vipindi vinavyofunzwa shuleni na hata miongoni mwa viongozi katika mabunge yote, matumizi hayo ni nadra.
Aidha, Kiswahili kinakumbwa na ushindani mkubwa kutoka lugha nyinginezo, kwa mfano, Kiingereza na Kifaransa na sasa Kijerumani.
Baadhi ya wanafunzi hasa kutoka tabaka la juu hukiona Kiswahili kuwa kigumu.
Kunasibishwa kwa Kiswahili na watu wa pwani huzua mwelekeo hasi miongoni mwa watu wa bara.
Kiswahili inakumbwa na ukosefu wa ufadhili wa kufanya utafiti na kuendeleza usomi wake.
Mikutano mingi rasmi hufanywa katika lugha ya Kiingereza. Matukio muhimu kama kusomwa kwa makisio ya matumizi ya serikali na hotuba za kitaifa hufanywa kwa lugha ya Kiingereza.
Wakati mwingine vyombo vya habari havitumii Kiswahili sanifu. Hali hii hujitokeza katika runinga. redio, magazeti. Baadhi ya vyombo vya habari huvuruga Kiswahili kwa kuruhusu na kutumia Sheng’.
Kutohimizwa katika vyuo vya daraja la kati kama vile vyuo vya kufunzia mahazili.
Mashirika ya uchapishaji kuelekea kukipa Kiingereza kipaumbele katika uchapishaji wao.
Uhaba wa magazeti au majarida ya Kiswahili ambazo ni msingi muhimu wa usambazaji wa lugha.
Kutokuwepo kwa sera madhubuti kuhusu matumizi ya Kiswahili.
Kuzuka na kuenea kwa kilugha cha Sheng’ miongoni mwa wanajamii hasa vijana na ambao ndio wengi katika jamii.
Kutokuwepo kwa waandishi wa kutosha wanaoandika katika lugha ya Kiswahili.
Ukosefu wa chombo cha kuiendeleza lugha ya Kiswahili kama taasisi ya Kiswahili na kadhalika.
Suluhisho kwa matatizo yanayokumba Kiswahili
Kiswahili kimepiga hatua kubwa kimaendeleo tangu Kenya ilipopata uhuru.
Hata hivyo, bado ipo haja ya kupanga mikakati ya kitaifa kukiimarisha zaidi.
Hatua mojawapo ya kukiimarisha Kiswahili kupitishwa kwa sera nzuri inayoweka wazi malengo ya serikali kuihusu lugha hii na kutoa mwongozo ufaao hatima ya lugha yenyewe.
Kuanzishwa kwa tuzo zinazowatuza waandishi wanaoandika kazi nzuri zinazosaidia ukuzaji wa Kiswahili.
Wachapishaji wahimizwe kuchapisha machapisho ya lugha ya Kiswahili. Serikali inaweza kuzuka na agizo vya kuwafanya wachapishaji hao wasichelee kuchapisha vitabu hivyo.
Kuhimiza kuwapo kwa idara ya Kiswahili katika taasisi za juu ili kuendeleza utafiti wa Kiswahili.
Kuhimiza wananchi kutambua kuwa Kiswahili ni msingi wa kujitambulisha kama raia wan chi hii.
Kiswahili kifanywe lugha ya kimsingi katika taasisi za elimu. Kwa mfano, ili ufanye kozi ya uhandisi au udaktari, lazima uwe na umilisi mzuri wa lugha ya Kiswahili.
Kuandikwa kwa magazeti na majarida zaidi ya Kiswahili na yauzwe kwa bei ambayo wamanchi wanaweza kumudu.
Shughuli mbalimbali za kiserikali, kidini, kisiasa, ziendelezwe kwa lugha ya Kiswahili.
Watoao matangazo ya habari wawe waliohitimu vyema katika lugha ya Kiswahili na vipindi vinavyosaidia kukuza Kiswahili vipewe muda zaidi na wakati hu huo vinavyochangia katika matumizi mabaya viondolewe.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ishughulikie Kiswahili kwa njia sawa na Kiingereza, kwa mfano, vipindi viongezwe, walimu zaidi waajiriwe na baadhi ya masomo mengine yafunzwe kwa lugha ya Kiswahili.
Walimu wa Kiswahili wapewe au waongezewe marupurupu maalumu ili kuwahimiza wengi wasomee lugha hii.
Sheng’ ipigwe marufuku hasa shuleni na viongozi wawe katika msitari wa mbele katika kuzungumza Kiswahili sanifu.
Kuhimizwa kuwepo kwa magazeti mengi ya Kiswahili ambayo yatauzwa kwa bei inayowafanya wengi kuyamudu.
Kiswahili kitumike kwenye mtandao.
Wajibu wa Kiswahili kitaifa na kimataifa
Lugha ni chombo cha mawasiliano baina ya wanajamii. Jamii mbalimbali zimeunganishwa na lugha ya Kiswahili. Jamii zote arobaini na tatu za Kenya na mia na ishirini za Tanzania zimeunganishwa kwa lugha ya Kiswahili. Kiswahili sio tu lugha ya kitaifa katika mataifa haya bali pia ya kimataifa.
Magazeti, majarida mbalimbali huchapishwa katika lugha ya Kiswahili. Mifano ni kama vile gazeti la Taifa Leo (Kenya), Mulika (Tanzania), Urafiki (Ujerumani). Magazeti ni vyombo vya kusambaza habari.
Lugha ya Kiswahili inatumiwa kama lugha rasmi na ya taifa nchini Kenya na mataifa jirani kama vile Tanzania; na kwa njia hii kuhimiza matumizi yake zaidi.
Kwamba Kiswahili kinatumiwa katika mtandao ni jambo muhimu. Wageni huwajibika kujifunza Kiswahili ili kuweza kuwasiliana ipasavyo na wenyeji kwa kusudi la kufanikisha miradi yao mbalimbali.
Katika eneo la Mashariki na Kati pamoja na Kusini mwa Afrika, Kiswahili kinazidi kupanda hadhi kama lugha sambazi/ lingua franka.
Madereva wa safari ndefu za kusafirisha bidhaa katika maeneo haya wanazidi kutumia lugha ya Kiswahili zaidi ya nyingine.
Lugha ya Kiswahili hutumiwa katika utangazaji wa redio sio tu hapa Kenya au Tanzania bali katika mataifa mengi ulimwenguni kama vile Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Redio Beijing (Jamhuri ya Watu wa Uchina) mingoni mwa mengine mengi.
Lugha hii imeanza kutumiwa katika nyanja ambazo zamani haikutumiwa kwa mapana. Kwa mfano, siku hizi zipo filamu ambazo zinaigizwa kwa lugha ya Kiswahili.
Kama chombo cha mawasiliano kinachotumiwa na nchi na watu wengi, Kiswahili kimetangazwa kuwa moja kati ya lugha rasmi katika vikao vya baraza kuu la la Umoja wa Afrika, hivyo kuinua hadhi yake katika ngazi ya juu kiwango hiki.
Kiswahili ni mojawapo wa lugha zinazofunzwa kote ulimwenguni. Kinafunzwa katika Chuo Kikuu cha Bayreuth (Ujerumani), Chuo Kikuu cha Cairo (Misri), Chuo Kikuu cha Columbia na Chuo Kikuu cha Yale (Marekani), Chuo Kikuu cha Osaka (Ujapani), School of Oriental and African Studies (Uingereza), Chuo Kikuu cha Khartoum (Sudan).Mipaka yake imevuka chimbuko na asili yake na kuwa chombo cha mawasiliano ya kitaifa na kimataifa.
Matumizi ya Kiswahili kwenye mtandao ni jambo lingine muhimu. Jambo hili limefungamana na miradi tofauti ambayo huandaliwa na wageni. Wageni hawa huwajibika kujifunza Kiswahili ili waweze kuwasiliana vyema na wenyeji.
Lugha hii imepanuka kwa kuwa pia inatumiwa katika nyanja ya kisayansi.Siku hizi kampuni za kimataifa kama vile Linux na Microsoft zimeishirikisha lugha ya Kiswahili katika lugha ambazo zinatumiwa katika program zao.
Lugha ya Kiswahili imekuwa msingi muhimu wa kufanya biashara katika maeneo mbalimbali inakotumiwa lugha hii. Kwa njia hii, matumizi yenyewe yanapanuka.
Kamusi mbalimbali zimesaidia kuieneza na kukipatia Kiswahili hadhi zaidi Baadhi ya kamusi hizi ni English-Swahili, Kijerumani-Kiswahili, Russia-Kiswahili, Japanese-Kiswahili, Polandi-Kiswahili miongoni mwa zingine.
Umuhimu wa Kiswahili
Ni chombo cha mawasiliano katika kiwango cha kitaifa na hata kimataifa kama ilivyo katika Afrika Mashariki.
Ni kitambulisho muhimu cha utaifa na uzalendo wetu.
Ni chombo cha kuwaunganisha watu wa Afrika Mashariki.
Kiswahili kinawunganisha watu wa kutoka makabila tofauti Afrika Mashariki na Kati.
Ni lugha ya Kiafrika ambayo asili yake ni Afrika Mashariki wala si lugha kutoka ugenini kama vile Kiingereza, Kifaransa, Kireno.
|