SHAIRI: NYUMBA IKIKOSA MAMA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: NYUMBA IKIKOSA MAMA (/showthread.php?tid=1136) |
SHAIRI: NYUMBA IKIKOSA MAMA - MwlMaeda - 09-04-2021 NYUMBA IKIKOSA MAMA ? Nyumba ikikosa mama, inapungua salama, Nyumba ikikosa mama, zaongezeka lawama, Nyumba ikikosa mama, inapungua heshima, Nyumba ikikosa mama, kuta zote huinama. Wao huleta heshima, maadili kuwa mema, Mama alo na huruma, anoitambua dhima, Dunia akiihama, inaenea nakama, Nyumba ikikosa mama, kuta zote huinama. Mkiishi kwa salama, naye baba pia mama, Baba akikusakama, kwa mama utatuama, Wapo kinababa kima, misituni walohama, Lakini 'kiwepo mama, dunia yote salama. Malezi yake si haba, mama anayo mahaba, Hapa simtusi baba, huu ukweli si haba, Mama kamshinda baba, thamani aloibeba, Nyumba ikikosa mama, kuta zote huinama. Wako baba visirani, udikteta vichwani, Hudhani wako vitani, wana hukosa amani, Kinamama huwa chini, ipatikane amani, Nyumba ikikosa mama, kuta zote huinama. Yeye mama masikini, mbawa zake ziko chini, Huruma pasi kifani, wana wawe salamani, Furaha au shidani, utakuwa mikononi, Nyumba ikikosa mama, kuta zote huinama. Malezi yake makini, asubuhi na jioni, Ni mwepesi kubaini, mtoto kapatwa nini, Mapenzi na umakini, mama apaswa nishani, Nyumba ikikosa mama, kuta zote huinama. Pole mlokosa mama, huzuni kuwasakama, Muombeni ya karima, peponi wende simama, Nanyi mlobaki nyuma, muwafikie salama, Nyumba ikikosa mama, kuta zote huinama. Pole kwako wewe Chiku, kaka Omi na Siwema, Kwa mchana na usiku, Mola awape neema, Sylvia dada Siku, Hantama na Halima, Hindu pia kaka Chaku, Mola awape tuama, Nyumba ikikosa mama, kuta zote huinama. Shaaban Mwinyikayoka (Mwanaupwa) Iringa |