SHAIRI: BINTI WA AFRIKA - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: BINTI WA AFRIKA (/showthread.php?tid=1139) |
SHAIRI: BINTI WA AFRIKA - MwlMaeda - 09-06-2021 Binti wa Afrika Na Anna S. Manyanza (@annasamwel7) 1 Mara ngapi umenyanyasika? Mara ngapi umedhalilishwa? Mara ngapi umedharaulika? Mara ngapi umeteseka? Binti wa Afrika 2 Historia imekutesa Historia imekusahau Historia imekufuta Historia haikutambui Binti wa Afrika 3 Siasa imekulaani Siasa imekuasi Siasa imekukebehi Siasa imekukufuru Binti wa Afrika 4 Karne ya 1500, historia imekutia utumwani Karne ya 1700, historia imekutia ukoloni Karne ya 1800, historia imekutia aibu Karne ya 1900, historia imekuvunja moyo Binti wa Afrika 5 Utumwa umekusambaza dunia Mashariki Utumwa umekusambaza dunia Magharibi Ukoloni umekusambaza dunia Kaskazini Ukoloni umekusambaza dunia Kusini Binti wa Afrika 6 Mashamba ya katani umehenyeshwa Mashamba ya miwa umemenyeshwa Mashamba ya pamba umetaabishwa Mashamba ya karafuu umesoteshwa Binti wa Afrika 7 Jua limekuwamba Mvua imekulowesha Njaa imekudhoofisha Kiu imekuvyausha Binti wa Afrika 8 Moyo wa damu Mwili wa damu Roho ya damu Uke wa damu Binti wa Afrika 9 Kisu rohoni Kisu moyoni Kisu mwilini Kisu ukeni Binti wa Afrika 10 Roho ya majuto Roho ya machungu Roho ya majonzi Roho ya hofu Binti wa Afrika 11 Roho ya maombolezo Roho ya utumwa Roho ya mashaka Roho ya wasiwasi Binti wa Afrika 12 Binti mkimbizi Binti wa kupekua Binti wa mateso Binti wa kuchakaa Binti wa Afrika 13 Umezaa Umelea Umezika Umeomboleza Binti wa Afrika 14 Umejua vita Umejua mauaji Umejua maradhi Umejua ufukara Binti wa Afrika 15 Umebakwa, wana umezalishwa Umebakwa, maradhi umeambukizwa Umebakwa, moyo imedhalilishwa Umebakwa, roho imeumizwa Binti wa Afrika 16 Hulalamiki, nani atakuamini? Hulisemi, nani atakuafiki? Huripoti, nani atakusaidia? Huliongelei, nani atakutetea? Binti wa Afrika 17 Umenyimwa elimu Umenyimwa amani Umenyimwa penzi Umenyimwa haki Binti wa Afrika 18 Ukabila umekubagua Utamaduni umekulemaza Mila imekupumbaza Dasturi imekufunga Binti wa Afrika 19 Lolote baya, sababu ni wewe Lolote baya, shutuma ni wewe Lolote baya, lawama ni wewe Lolote baya, adhabu ni wewe Binti wa Afrika 20 Si kitu, hufi moyo Si kitu, hufi roho Si kitu, hufi faraja Si kitu, hufi taraja Binti wa Afrika 21 Weye u kisima cha majonzi na furaha Weye u mto wa majonzi na furaha Weye u ziwa la majonzi na furaha Weye u bahari ya majonzi na furaha Binti wa Afrika 22 U waridi jangwani U waridi kondeni U waridi nyikani U waridi milimani Binti wa Afrika 23 Malkia sawa na Miriam Makeba Malaika sawa na Waris Dirie Shupavu sawa na Michelle Obama Shujaa sawa na Wangari Maathai Binti wa Afrika 24 Mithili ya mbuyu, mkakamavu umesimama Mithili ya mpingo, mweusi umesimama Mithili ya mwembe, mpana umesimama Mithili ya mnazi, mrefu umesimama Binti wa Afrika 25 Binti wa Afrika umetoka mbali Binti wa Afrika bado uko safarini Binti wa Afrika usife tumaini Binti wa Afrika siku moja utafika Binti wa Afrika 26 Kuwa binti wa Afrika, si utumwa tena Kuwa binti wa Afrika, si ukoloni tena Kuwa binti wa Afrika, si kuambukizwa tena Kuwa Binti wa Afrika, si kubakwa tena Binti wa Afrika 27 Kuwa binti wa Afrika, si kisu ukeni tena Kuwa binti wa Afrika, si kufa njaa tena Kuwa binti wa Afrika, si hofu tena Kuwa binti wa Afrika, si kufa upesi tena Binti wa Afrika 28 Kuwa binti wa Afrika, si laana tena Kuwa binti wa Afrika, si kosa tena Kuwa binti wa Afrika, si lawama tena Kuwa binti wa Afrika, si aibu tena Kuwa binti wa Afrika, si shutuma tena Binti wa Afrika 29 Binti wa Afrika ana haki ya kuthaminiwa Binti wa Afrika ana haki ya kupendwa Binti wa Afrika ana haki ya uhuru Binti wa Afrika ana haki ya kuishi Binti wa Afrika 30 Binti Afrika una haki ya kufurahi Binti Afrika una haki ya kuelimika Binti Afrika una haki ya kutibiwa Binti Afrika una haki ya kuajiriwa Binti wa Afrika 31 Zaa wanao upendavyo Lea wanao upendavyo Elimisha wanao upendavyo Tetea wanao upendavyo Binti wa Afrika 32 Fundisha wanao upendo Fundisha wanao amani Fundisha wanao hekima Fundisha wanao kuwajibika Binti wa Afrika 33 Ni haki yako kukubali Ni haki yako kukataa Ni haki yako kukosoa Ni haki yako kupinga Binti wa Afrika 34 Ni haki yako kutaka ndoa Ni haki yako kufunga ndoa Ni haki yako kukataa ndoa Ni haki yako kuchoka ndoa Binti wa Afrika 35 Pinga ukame Pinga UKIMWI Pinga ufukara Pinga umasikini Binti wa Afrika 36 Pinga ubaguzi wa rangi Pinga ubaguzi wa jinsia Pinga ubaguzi wa wazee Pinga ubaguzi wa watoto Binti wa Afrika 37 Yako sauti paza Wako moyo paza Wako mori paza Yako roho paza Binti wa Afrika 38 Sifa yako simulia Elimu yako simulia Hisia yako simulia Maisha yako simulia Binti wa Afrika 39 Jitahidi binti wa Afrika Jaribu binti wa Afrika Wajibika binti wa Afrika Pambana binti wa Afrika Binti wa Afrika 40 Ruka milima, upendo peleka Vuka bahari, ujasiri peleka Vuka mito, amani peleka Vuka mabonde, furaha peleka Binti wa Afrika |