MUSWADA wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2021, unaoruhusu sasa lugha ya Kiswahili kutumika kama lugha ya Sheria na Mahakama umepitishwa rasmi na Bunge.
Waziri wa Katiba na Sheria Dk Mwigulu Nchemba, ndiye aliyewasilisha muswada huo bungeni leo unaopendekeza kufanyiwa marekebisho katika sheria tatu ambazo ni Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura ya 1, Sheria ya Mahakama za Migogoro ya Ardhi, Sura ya 216 na Sheria ya Mahakama za Mahakimu, Sura ya 11.
Alisema katika Sheria ya Tafsiri ya Sheria, Sura ya 1 inapendekezwa kufanya marekebisho katika kifungu cha 84 ili kuondoa matumizi ya lugha ya Kiingereza kama lugha ya sheria na lugha ya Mahakama na badala yake kutumia lugha ya Kiswahili.
Waziri huyo alieleza kuwa lugha hiyo ya Kiswahili ndiyo lugha ya taifa inayoeleweka na inatumika katika shughuli zote za maendeleo nchini.
Alisisitiza kuwa kutumika kwa lugha hiyo kisheria na kimahakama kutasaidia upatikanaji wa haki nchini.
“Marekebisho haya yanakusudia kuimarisha mfumo wa upatikanaji haki kwa wananchi ambao ndio watumiaji wa sheria husika. Mapendekezo haya yamezingatia marekebisho yaliyofanywa kwenye Sheria ya tafsiri za Sheria ambayo imeweka msingi wa lugha ya mahakama, mabaraza na vyombo vingine vyenye jukumu la kutoa haki kuwa ni Kiswahili," alieleza.
Alisema kwa mujibu wa marekebisho hayo, pia yanapendekeza vyombo vya utoaji haki kutumia lugha ya Kiingereza pale itakapoonekana ni muhimu kufanya hivyo kwa maslahi ya utoaji haki kwa mashauri husika..
“Hata hivyo, endapo chombo cha utoaji haki kitalazimika kutumia Kiingereza tafsiri ya mwenendo na uamuzi kuhusu shauri husika itatolewa mara moja," alisema.
Waziri huyo alisema kuwa kupitia marekebisho hayo Waziri wa Sheria anapewa mamlaka ya kutunga kanuni ili kubainisha mazingira ambayo lugha nyingine zinaweza kutumika katika kutunga sheria au katika mfumo wa utoaji haki.
Alisema pia Jaji Mkuu anapewa Mamlaka ya kutunga kanuni kwa ajili ya kutoa mwongozo ili kubainisha mazingira ya lugha ya kiingereza inaweza kutumika katika utoaji wa haki.
Waziri huyo alisema muswada huo pia unapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Mahakama za Migogoro ya Ardhi, Sura ya 216 na Sheria ya Mahakama za Mahakimu, Sura ya 11 kwa kufuta vifungu vinavyoweka sharti kuhusu lugha ya Mahakama na sasa itatumika kiswahili.
Mapendekezo hayo yamezingatia marekebisho yaliyofanywa kwenye Sheria ya Tafsiri za Sheria ambayo imeweka msingi wa lugha ya Mahakama, mabaraza na vyombo vingine vyenye jukumu la kutoa haki kuwa ni Kiswahili.
Kwa upande wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, kupitia Mwenyekiti wa kamati hiyo Mohammed Mchengerwa, ailishauri serikali kuweka kifungu kinachompa mamlaka Waziri ya kutangaza tarehe ya kuanza kutumika sheria hiyo.
Pia, kamati hiyo ilishauri kuwepo kwa mwongozo maalumu utakaobainisha namna ya kushughulikia mashauri yanayoendelea kwa sasa mahakamani.
Posted by: MwlMaeda - 10-18-2021, 07:53 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
RWANDA NI KABILA MOJA.
--------------------------------------
1.
Wasalam-aleikumu, hadhira hini azizi,
ninawagea nudhumu, yakinifu tena wazi,
n'kipenda mzifahamu, habari za pande hizi,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
2.
Nchi hii 'lijaliwa, na Rabana Maulana,
miaka elfu 'mekuwa, nchi 'metulia sana,
jamii 'likaa sawa, tena imeshikamana,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
3.
Aliishi mwananchi, popote nchini Rwanda,
kila sehemu ya nchi, lugha 'kiwa Kinyarwanda,
utamaduni wa nchi, ukiwa mmoja Rwanda,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
4.
Shughuli kuu za jadi, kufuga walimaizi,
wakiwa tena weledi, wakulima chapakazi,
walikuwa ni sitadi, mafundi wa ufinyanzi,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
5.
Hizi shughuli za jadi, na zilitegemeana,
ikiwa ndiyo miradi, ya babu zetu wa'ngwana,
jamii yetu ya jadi, kwazo ikielewana,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
6.
Waliishi kijamaa, kwa ukaribu wa sana,
kwa upendo na heshima, na wakithaminiana,
tangu za azali zama, 'kiwa wajamiiana,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
7.
Wakafika Wakoloni, walikuta ni wamoja,
'kaona utamaduni, na lugha yao ni moja,
hili liliwakwazweni, wakauvunja umoja,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
8.
''Gawanya na utawale," ilikuwa mbinu yao,
wakaziasisi shule, hasa kwa mafao yao,
waliyafundisha yale ya kugawa janja yao.
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
9.
Ninawaenzi wahenga, wali wa'sisi wa Rwanda,
utamaduni kujenga, kwa ari wakaulinda,
lugha iliyowaunga, Kinyarwanda waliunda,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
10.
Siasa za kikoloni, ziliyaleta madhara,
ukabila na udini, ni nguzo zao imara,
kuujenga ufitini, zilikuwa zake sera,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
12.
Maana za jadi yetu, kuelewesha shughuli,
zile za jamii yetu, Wazungu walibadili,
'ti ni makabila yetu, Dunia ikakubali,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
13.
Hebu weye tafakari, watu ulimi mmoja,
mila pia desituri, waishi aridhi moja,
jibu lake ni dhahiri, hawa ni watu wamoja,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
14.
Ilipofika nyakati, za uhuru kuutaka,
zilikuwa harakati, ukoloni kuutoka,
Wazungu 'kawa shariti, kutafuta vibaraka,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
15.
Ilikuwa ni rahisi, kuwapata vibaraka,
sababu 'weshanajisi, umoja wetu hakika,
ukoloni ibilisi, pisha mbali Mtajika,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
16.
Vibaraka walijaza, mifarakano nchini,
sana wakasheheneza, ukabila na udini,
yale walopandikiza, mahasidi Wakoloni,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
17.
Uhuru ulipofika, kote kote Afurika,
Rwanda tunasikitika, kusambaratika kote,
pande zote Afurika, tulikimbilia kote,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
18.
Mamboleo ukoloni, na wake vibarakala,
ulijikita nchini, pamwe na wake wakala,
kwa mtindo ja shetani, Rwanda wakaitawala,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
19.
Imetosha ! imetosha !, yametosha matokeo,
yalikotupelekesha, tunakojutia leo,
sana yametujulisha, ''Ukoloni mamboleo".
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
20.
Shukurani Maanani, kuniwezesha fikia,
ubeti wa ishirini, tungo ninamalizia,
nikiweka hadharani, fikira zangu sawia,
RWANDA NI KABILA MOJA, JINALE NI BANYARWANDA.
**********
Rwaka rwa Kagarama, (Mshairi Mnyarwanda)
Jimbo la Mashariki, Wilaya ya Nyagatare, JAMHURI YA RWANDA.
Beti sita hazifiki, wa tano ninakomea,
Niiweke yangu maki,hapo nije kuanzia,
Tunza siwe mtaliki, ufe hujajizalia,
Tunza unachomiliki, nadama hitokujia.
Mwalimu Nyakundi
Malenga Tembo mla nyama
Shule ya upili ya Amabuko, Keroka.
11. 10. 2021.
?
ITIKADI YA UJAMAA.
************************
Itikadi ya Ujamaa,
wengi hawakuelewa,
si ya Wachina jamaa,
si ya Warusi jamaa,
siasa ya Ujamaa,
ya Wafurika jamaa.
*******
N'jaribu kuelewesha,
Ujamaa kumaanisha,
ni mfumo wa maisha,
vema uliowezesha,
ya babu zetu maisha,
haswa kuyaneemesha.
*******
Wa binadamu usawa,
msingi wa ujamaa,
kazi kwa kila mjamaa,
na mapato ya wajamaa,
kugawana kwa usawa,
ni misingi ya ujamaa.
*******
Misingi ye nainena,
haswa kuthaminiana,
maana'ke kupendana,
pia kuheshimiana,
na walikaribiana,
tena kushirikiana.
*******
Mjamaa alikuwa,
ni haki kuthaminiwa,
ana haki ya kupendwa,
na tena kuheshimiwa,
alipaswa kuelewa,
ya jamii kushirikishwa.
*******
Ilikuwa mila yetu,
ni desituri ya kwetu,
kumjali jamaa yetu,
mtu 'kiugua kwetu,
huyo ni mgonjwa wetu,
anauguzwa kiutu.
*******
Kama mzazi 'lizaa,
alituzwa na jamaa,
arusi ikitokeaa,
inafanywa kijamaa,
mjamaa 'kilemaa,
alitunzwa na jamaa.
*******
Huko kuthaminiana,
jamaa wakipendana,
pia kuheshimiana,
mema walifanyiana,
huku wakishirikiana,
Wajamaa kufaana.
*******
Na pale mifarakano,
i'pokuwa jamii ino,
ulifanywa mkutano,
na hata makongamano,
ya kuleta mapatano,
sawa kwa ushirikiano.
*******
Hini ya Ujamaa mi'ko
uongo na rushwa mwiko,
umimi 'likuwa mwiko,
sisi kwa sisi ni mwiko,
uvivu wizi ni mwiko,
utengano uli mwiko.
*******
Jama ninakumbukia,
jamaa wa'vyochangia,
mambo yote ya jamia,
kwa pamwe ninawambia,
ya shari walichangia,
na shwari kufurahia.
*******
Jamii ya Wanyarwanda,
Ujamaa tuliutenda,
Wasukuma na Waganda,
Wakikuyu na Wamanda,
jamii zote zilipenda,
Ujamaa kuulinda.
*******
Na siwezi kuyamala,
ya Ujamaa yetu mila,
marefu si masihala,
ja 'lufu lela ulela,
Wazungu kututawala,
yetu waliyakatala.
*******
Waliyakatala yetu,
wakaosha bongo zetu,
eti ya kishenzi yetu,
tukawacha mila zetu,
na Ujamaa wa kwetu,
Mkoloni hana utu.
*******
Rwaka rwa Kagarama,
Mshairi Mnyarwanda,
Jimbo la Mashariki,
Wilaya ya Nyagatare,
JAMHURI YA RWANDA.
????????????
UMASKINI WA MAWAZO
*****************************
Hini la Nyerere wazo, ni tamko'le makini,
wa umaskini mawazo, mbaya mno jameni,
unapita si mchezo, wowote hii yakini,
umaskini wa mawazo, umasikini mbaya.
------------------
Busara'ye h'itakufa, na itadumu milele,
maneno'ye yatufaa, yakigonga ja kengele,
fikira'ze zina sifa, Mwalimu mbele kwa mbele,
umaskini wa mawazo, umasikini mbaya.
-------------------
Kale hadi enzi hizi, umasikini tatizo,
wa halisi ukombozi, ni ule wa kimawazo,
kama haupo ni wazi, kinakuwa ni kikwazo,
umaskini wa mawazo, umasikini mbaya.
------------------
Kula kiundwacho kitu, huanza waza malengo,
vyombo tumizi kwa watu, hutokana na ubongo,
tunapata zana zetu, kwa kufinyanga udongo,
umaskini wa mawazo, umasikini mbaya.
-------------------
Na hauwezi kushinda, bila ushindi ku'waza,
huwezi kitu kuunda, pasi kwanza kukiwaza,
huwezi safari kwenda, uendako hukuwaza,
umaskini wa mawazo, umasikini mbaya.
-------------------
Uongozi bora upo, ikiwa safi siasa,
ardhi ya kutosha ipo, watu salama kabisa,
zahanati shule zipo, miundombinu h'ijakosa,
umaskini wa mawazo, umasikini mbaya.
-------------------
Fikiria uno baba, mwenyi shamba kubwa sana,
linayo nyingi rutuba, na mvua yapatikana,
siha'ye ni marhaba, 'ti ni fukara anena,
umaskini wa mawazo, umasikini mbaya.
--------------------
Wa mawazo mkosefu, na huwa hajiamini,
hujisikia dhaifu, hajuwi yake thamani,
m'endeleo ayahofu, ya duni ndo atamani,
umaskini wa mawazo, umasikini mbaya.
-------------------
Bongo tuzitumikishe, mbele tuweze kusonga,
ili tuzikamilishe, njozi zetu kuzijenga,
uzembe Mola tupishe, tuachane na ujinga,
umaskini wa mawazo, umasikini mbaya.
-------------------
Za mwalimu ninakiri, fikira'ze ni makini,
sana tuzitafakari, tuzienzi wajameni,
Nyerere ni mshauri, zama zote wa thamani,
umaskini wa mawazo, umasikini mbaya.
_________________________________
Rwaka rwa Kagarama, Mshairi Mnyarwanda.
Jimbo la Mashariki, Wilaya ya Nyagatare,
JAMHURI YA RWANDA.
????????????