SHAIRI: UMASKINI WA MAWAZO - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Fasihi simulizi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=6) +---- Forum: Ushairi (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=50) +---- Thread: SHAIRI: UMASKINI WA MAWAZO (/showthread.php?tid=1317) |
SHAIRI: UMASKINI WA MAWAZO - MwlMaeda - 10-14-2021 UMASKINI WA MAWAZO ***************************** Hini la Nyerere wazo, ni tamko'le makini, wa umaskini mawazo, mbaya mno jameni, unapita si mchezo, wowote hii yakini, umaskini wa mawazo, umasikini mbaya. ------------------ Busara'ye h'itakufa, na itadumu milele, maneno'ye yatufaa, yakigonga ja kengele, fikira'ze zina sifa, Mwalimu mbele kwa mbele, umaskini wa mawazo, umasikini mbaya. ------------------- Kale hadi enzi hizi, umasikini tatizo, wa halisi ukombozi, ni ule wa kimawazo, kama haupo ni wazi, kinakuwa ni kikwazo, umaskini wa mawazo, umasikini mbaya. ------------------ Kula kiundwacho kitu, huanza waza malengo, vyombo tumizi kwa watu, hutokana na ubongo, tunapata zana zetu, kwa kufinyanga udongo, umaskini wa mawazo, umasikini mbaya. ------------------- Na hauwezi kushinda, bila ushindi ku'waza, huwezi kitu kuunda, pasi kwanza kukiwaza, huwezi safari kwenda, uendako hukuwaza, umaskini wa mawazo, umasikini mbaya. ------------------- Uongozi bora upo, ikiwa safi siasa, ardhi ya kutosha ipo, watu salama kabisa, zahanati shule zipo, miundombinu h'ijakosa, umaskini wa mawazo, umasikini mbaya. ------------------- Fikiria uno baba, mwenyi shamba kubwa sana, linayo nyingi rutuba, na mvua yapatikana, siha'ye ni marhaba, 'ti ni fukara anena, umaskini wa mawazo, umasikini mbaya. -------------------- Wa mawazo mkosefu, na huwa hajiamini, hujisikia dhaifu, hajuwi yake thamani, m'endeleo ayahofu, ya duni ndo atamani, umaskini wa mawazo, umasikini mbaya. ------------------- Bongo tuzitumikishe, mbele tuweze kusonga, ili tuzikamilishe, njozi zetu kuzijenga, uzembe Mola tupishe, tuachane na ujinga, umaskini wa mawazo, umasikini mbaya. ------------------- Za mwalimu ninakiri, fikira'ze ni makini, sana tuzitafakari, tuzienzi wajameni, Nyerere ni mshauri, zama zote wa thamani, umaskini wa mawazo, umasikini mbaya. _________________________________ Rwaka rwa Kagarama, Mshairi Mnyarwanda. Jimbo la Mashariki, Wilaya ya Nyagatare, JAMHURI YA RWANDA. ???????????? |