AINA ZA MANENO - Nomino – majina, aina za nomino, uundaji wa nomino kutoka kwa maneno mengine, wingi
- Vitenzi – vitendo katika sentensi, aina za vitenzi, mnyambuliko wa vitenzi
- Viwakilishi – maneno yanayowakilisha nomino; aina za viwakilishi
- Vivumishi – aina za vivumishi k.v vivumishi vya sifa, n.k
- Vielezi – vielezi halisi, vielezi vya namna n.k
- Viunganishi – a-unganifu, kuonyesha tofauti, sababu, sehemu n.k
- Vihisishi – maneno ya kuonyesha hisia k.v hasira, mshangao n.k
- Vihusishi – uhusiano wa nomino na mazingira yake
Nomino (N)
Kiingereza
Nouns
Nomino ni maneno ambayo hutaja majina ya watu, vitu, hali n.k. Kuna nomino za kawaida na nomino za kipekee miongoni mwa aina nyingine za nomino. - AINA ZA NOMINO
- Nomino za Kawaida
- Nomino za Kipekee
- Nomino za Jamii
- Nomino za Wingi
- Nomino za Vitenzi Jina
- Nomino za Dhahania
Aina za Nomino
Kuna aina mbalimbali za nomino katika lugha ya Kiswahili - Nomino za Kipekee
- Nomino za Kawaida
- Nomino za Jamii/Makundi
- Nomino za Kitenzi-Jina
- Nomino za Dhahania
- Nomino za Wingi
Nomino za Kawaida
Haya ni majina ya kawaida yanayoweza kutumiwa kurejelea vitu mbalimbali, watu, wanyama, mahali na kadhalika. Nomino hizi zinaweza kuwa katika umoja au wingi kulingana na ngeli yake.
k.m: nyumba, mbuzi, daktari, soko, kalamu, jua
Nomino za Kipekee
Haya ni majina maalum ya watu, mahali, bidhaa, kampuni, na kadhalika. Herufi ya kwanza ya nomino hizi huwa ni herufi kubwa. Nomino za kipekee haziwezi kubadilika, na hivyo basi hazina wingi.
k.m: Tanzania, Nairobi, Anita, Gafkosoft, Athi, Kimbo,
Nomino za Jamii
Nomino za jamii hurejelea kundi la vitu au wanyama, kwa ujumla. Aghalabu vitu vinavyorejelewa hutokea kwa makundi ya vitu mbili au zaidi. Nomino hizi hutumia wingi tu tunaporejelea makundi zaidi ya moja.
k.m: jozi la viatu, umati wa watu, bustani la maua, bunga la wanyama
Nomino za Wingi
Nomino hizi hurejelea vitu ambavyo hutokea kwa wingi na haziwezi kuhesabiwa. Vitu kama hivyo hutumia aina nyingine ya vipimo ili kurejelea kiasi chake. Nomino za wingi hazina umoja.
k.m: maji, maziwa, changarawe, pesa, nywele
Nomino za Vitenzi Jina
Nomino hizi huundwa kutokana na vitenzi kwa kuongeza kiungo KU mwanzoni mwa mzizi wa kitenzi.
k.m: kulima, kuongoza, kucheza, kulala
Nomino za Dhahania
Haya ni majina ya hali au vitu ambavyo havionekani wale haviwezi kushikika.
k.m: upendo, furaha, imani, elimu, ndoto, mawazo, maisha, usingizi
Vitenzi (T)
Kiingereza
Verbs
Vitenzi ni maneno yanayosimamia kitendo. Kila kitenzi huwa na shina la kitenzi (sehemu ndogo zaidi ya kitenzi ambayo ndiyo huwakilisha tendo hilo). Shina la kitenzi huambatanishwa na viambishi ili kutoa maana iliyokusudiwa kama vile mtendaji, mtendewa, wakati kitendo kinafanyika na pia kauli ya kitenzi hicho.
Aina za Vitenzi
- Vitenzi Halisi
- Vitenzi Visaidizi + Vitenzi Vikuu
- Vitenzi Vishirikishi
- Vitenzi Sambamba
Vitenzi Halisi
Hivi ni vitenzi vinavyorejelea kitendo moja kwa moja. Vitenzi halisi vinapoambatanishwa na vitenzi vidogo katika sentensi, huitwa vitenzi vikuu.
k.m: soma, kula, sikiza - Waziri Mwasimba aliwasili jana kutoka ng’ambo.
- Kawia atapikia wageni.
- Funga mlango wa dirisha.
Vitenzi Visaidizi
Vitenzi visaidizi hutangulia vitenzi halisi (vitenzi vikuu) katika sentensi ili kuleta maana inayokusudiwa kulingana na wakati au hali.
k.m: -kuwa, -ngali, - Jua lilikuwa limewaka sana.
- Bi Safina angali analala
Vitenzi Vishirikishi
Vitenzi vishirikishi hutumika kuelezea hali iliyopo au mazingira. Kuna aina mbili za vitenzi vishirikishi:
- a) Vitenzi Vishirikishi Vipungufu – havichukua viambishi vyovyote.
k.m: ni, si, yu - Kaka yako ni mjanja sana.
- Huyo si mtoto wangu!
- Paka wake yu hapa.
- b) Vitenzi Vishirikishi Vikamilifu – huchukua viambishi vya nafsi au ngeli. Vitenzi hivi vinaweza kusimama peke yake au vinaweza kufuatiliwa na vitenzi vikuu.
k.m: ndiye, ndio, ndipo - Sanita ndiye mkurugenzi wa kampuni
- Huku ndiko kulikoibiwa
MUUNDO WA VITENZI
Kwa kuzingatia muundo wa vitenzi, tunaweza kuweka vitenzi katika aina zifuatazo:
- Vitenzi vya Silabi Moja
- Vitenzi vya Kigeni
- Vitenzi vya Kibantu
Vitenzi vya Silabi Moja
Hivi ni vitenzi vyenye silabi moja pekee. Ili kuleta maana kamili, vitenzi hivi huambatanishwa na kiungo KU- katika kauli ya kutenda. Kama vitenzi vingine, vitenzi vya silabi moja vinaweza kunyambuliwa.
k.m: soma, kula, sikiza
- -cha – kucha – jua linapochomoza asubuhi k.m kumekucha
- -fa – kufa – kuacha kupumua, kupoteza uhai k.m amekufa
- -ja– kuja – fika mahali hapa k.m nimekuja
- -la– kula – kutia chakula mdomoni k.m anakula
- -nya– kunya – kutoa mabaki ya chakula toka tumboni k.m mtoto amekunya
- -nywa– kunywa – kutia kinywaji kama vile maji au maziwa mdomoni k.m ninakunywa uji
- -pa– kupa – kumkabithi/kumpatia mtu kitu k.m amenipa pesa
- -pwa– kupwa – kujaa hadi pomoni – k.m kisima kimekupwa maji
- -twa– kutwa – jua linapozama magharibi na usiku kuingia k.m kumekutwa
- -wa– kuwa – kutokea katika hali au mahali fulani k.m alikuwa
Vitenzi vya Kigeni
Hivi ni vitenzi vyenye asili kutoka kwa lugha nyingine badala ya Kibantu. Baadhi ya lugha hizo ni Kiarabu, Kizungu, Kireno, Kihispania n.k. Vitenzi hivi havifuatilii muundo wa kawaida wa vitenzi vya Kiswahili ambavyo huishia kwa sauti -a. Badala yake, vitenzi hivi huishia kwa sauti nyingine kama vile -e, i, -o, na u
k.m: haribu, tubu, shukuru, salimu, thamini, amini, samehe, baleghe
Vitenzi vya Kibantu
Hivi ni vitenzi vyenye asili ya Kibantu na ambavyo huishia kwa sauti -a. Kitengo hiki hujumuisha asilimia kubwa zaidi ya vitenzi vya Kiswahili
k.m: simama, shika, tembea, beba, soma, lia
Vivumishi (V)
Kiingereza
Adjectives
Vivumishi au visifa ni maneno yanayotuelezea zaidi kuhusu nomino. Aghalabu vivumishi hutanguliwa na nomino. - AINA ZA VIVUMISHI
- Vivumishi vya Sifa
- Vivumishi Vimilikishi
- Vivumishi vya Idadi
- Vivumishi Visisitizi
- Vivumishi Viashiria / Vionyeshi
- Viwakilishi Viulizi
- Vivumishi Virejeshi
- Vivumishi vya KI-Mfanano
- Vivumishi Vya A-Unganifu
Aina za Vivumishi
Vivumishi vya Sifa
Hivi ni vivumishi ambavyo hutoa sifa ya kitu, mtu, mahali, n.k
k.m: kizuri, kali, safi, mrembo - Yule mama mweusi hupika chakula kitamu.
- Mvulana mkorofi aliadhibiwa na mwalimu kutokana na tabia zake mbaya.
- Sauti nzuri humtoa nyoka mkali pangoni
Vivumishi Vimilikishi
Vivumishi hivi hutumika kuonyesha nomino inamiliki nyingine. Mizizi ya vivumishi hivi huundwa kulingana na nafsi mbalimbali ( -angu, -ako, -ake, -etu, -enu, -ao).
k.m: changu, lako, yake, kwetu, vyenu, zao - Nitatumia talanta zangu kwa manufaa ya taifa letu.
- Aliweka kitabu chako sebuleni mwako
- Katosha amepata nguo yake miongoni katika sanduku lao.
Vivumishi vya Idadi
Hutueleza zaidi kuhusu kiasi, au idadi ya nomino. Kuna aina mbili za vivumishi vya idadi.
a) Idadi Kamili
hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino.
k.m: tatu, mbili, kumi - Msichana mmoja amewauwa nyoka wawili
- Siku kumi zimepita tangu Bi Safina alipojifungua watoto watatu
b) Idadi Isiyodhihirika
huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja idadi kamili
k.m: chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani - Watu wachache waliohudhuria mazishi ya Kajuta walikula chakula kingi sana.
- Baba yao alikuwa mateka kwa miaka kadhaa.
Vivumishi Visisitizi
Husisitiza nomino fulani kwa kurudia rudia kivumishi kiashiria
k.m: yuyu huyu, wawa hawa, kiki hiki, papo hapo, mumu humu, - Jahazi lili hili
- Wembe ule ule
- Ng’ombe wawa hawa
Vivumishi Viashiria / Vionyeshi
Vivumishi viashiria hutumika kuonyesha au kuashiria nomino kulingana na mahali.
Karibu
hapa, huyu, hiki, hili, huku, haya, ule, wale, pale
Mbali kidogo
hapo, huyo, hiyo, hicho
Mbali zaidi
pale, lile, kile
- Msichana huyu ni mkubwa kuliko yule
- Jani hili la mwembe limekauka
- Tupa mpira huo
Viwakilishi Viulizi
Vivumishi viulizi hutumika kuuliza swali.
Baadhi ya vivumishi viulizi huchukua viambishi vya ngel
k.m: -ngapi?, -pi? - Ni walimu wangapi wamefukuzwa? – kuulizia idadi
- Je, ni dawati lipi lenye funguo zangu?
Kunavyo vivumishi viulizi vingine ambavyo havichukui viambishi vyovyote.
k.m: wapi?, gani?, nini?, vipi? - Unazungumza kuhusu kipindi gani?
- Je, mmefika mahali wapi? – kuulizia mahali
Vivumishi Virejeshi
Hivi ni vivumishi ambavyo hurejelea nomino. Vivumishi hivi vinaweza kuwa vivumishi vya O-rejeshi au vivumishi viashiria vinapotumika kurejelea nomino.
k.m: ambaye, ambao, ambalo, ambacho, - Msichana ambaye alikuja ni Sheila
- Sauti ambayo uliisikia ilikuwa ya Mzee Kasorogan
Vivumishi vya KI-Mfanano
Vivumishi vya KI- ya Mfanano hutumika kulinganisha sifa ya nomino na hali au tabia nyingine. Vivumishi hivi hutanguliwa na nomino, kiunganishi cha A-unganifu na huchukua kiungo KI.
k.m: wa kifalme, za kijeshi, ya kitajiri, n.k - Chifu wa Vikwazoni anaishi maisha ya kimasikini
- Chali anapenda kusikiliza mziki wa kizungu
- Bi Naliza huvulia mavazi ya kifalme.
Vivumishi Vya A-Unganifu
Vivumishi hivi hutuelezea zaidi kuhusu nomino kwa kuonyesha kitu kinachomiliki nomino hiyo. Huundwa kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na kiambishi -a cha a-unganifu, kisha nomino
k.m: cha, la, kwa, za, ya - Watoto wa mwalimu mkuu wana tabia nzuri
- Chai ya daktari imemwagika
Viwakilishi (W)
VIWAKILISHI
Kiingereza
Pronouns
Viwakilishi vya Nomino ni maneno yanayotumika badala ya nomino. Kiwakilishi hakiwezi kuambatanishwa na nomino inayorejelewa. - AINA ZA VIWAKILISHI
- Viwakilishi vya Nafsi
- Viwakilishi Viashiria
- Viwakilishi Visisitizi
- Viwakilishi vya Sifa
- Viwakilishi vya Idadi
- Viwakilishi Viulizi
- Viwakilishi Vimilikishi
- Viwakilishi Virejeshi (O-Rejeshi)
- Viwakilishi Vya A-Unganifu
Aina za Viwakilishi
Viwakilishi vya Nafsi
Viwakilishoi hivi hutumika kwa niaba ya nafsi kwa umoja na kwa wingi.
k.m: mimi, wewe, yeye, sisi, nyinyi, wao
NAFSI
UMOJA
WINGI
Nafsi ya Kwanza
Mimi
Sisi
Nafsi ya Pili
Wewe
Ninyi/Nyinyi
Nafsi ya Tatu
Yeye
Wao
- Sisi tuliwatangulia nyinyi kufika hapa.
- Mimi si mjinga kama vile yeye anavyofikiria
Viwakilishi Viashiria
Viwakilishi viashiria (vionyeshi) hutumika badala ya nomino kwa kutumia kuonyesha nomino inayorejelewa bila kuitaja.
k.m: huyu, yule, hapa, n.k - Hiki hakina maandishi yoyote.
- Hao hawajui tofauti ya viwakilishi na vivumishi
- Tumekuja hapa ili kuwaburudisha kwa nyimbo tamu tamu.
Viwakilishi Visisitizi
Husisitiza nomino inayowakilishwa kwa kurudiarudia kiashiria chake.
k.m: yuyu huyu, wawa hawa, kiki hiki, papo hapo, mumu humu, - Zizi hizi ndizo zilizovunjika wiki jana
- Yule yule aliyekamatwa juzi, ameiba tena.
Viwakilishi vya Sifa
Husimama badala ya nomino kwa kurejelea sifa yake.
k.m: ‘-eupe, -zuri, -tamu, -embamba, -rembo, safi’ - Vyekundu vimehamisha
- Warembo wamewasili.
- Kitamu kitaliwa kwanza.
Viwakilishi vya Idadi
Hutumika kusimama badala ya nomino kwa kurejelea idadi yake.
- a) Idadi Kamili– hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino.
k.m: ‘saba, mmoja, ishirini’ - Wawili wamepigwa risasi na polisi leo jioni.
- Alimpatia mtoto wake hamsini kununua chakula
- b) Idadi Isiyodhihirika– huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja idadi kamili
k.m: ‘chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani’ - Tutazungumza na wachache kabla ya kuanzisha maonyesho yetu.
- Kadhaa zimeripotiwa kupotea.
Viwakilishi Viulizi
Viwakilishi viulizi hutumika kwa niaba ya nomino katika kuulizia swali.
Baadhi ya viwakilishi viulizi huchukua viambishi vya ngeli
k.m: ‘ -ngapi?, -pi?’ - Vingapi vinahitajika? – kuulizia idadi
- Zipi zimepotea?
Kunavyo viwakilishi viulizi vingine ambavyo havichukui viambishi vyovyote.
k.m: ‘wapi?, gani?, nini?, vipi?’ - Gani imefunga bao hilo?
- Wapi hapana majimaji?
- Yule mvulana alikupatia nini?
- Uliongea naye vipi? – kuulizia namna
Viwakilishi Vimilikishi
Viwakilishi hivi hurejelea nomino kwa kutumia vimilikishi.
k.m: ‘-angu, -ako, -ake, -etu, -enu, -ao ‘ - Kwetu hakuna stima.
- Lake limekucha.
- Zao zimeharibika tena
Viwakilishi Virejeshi (O-Rejeshi)
Hutumia O-rejeshi kurejelea na kusimamia nomino
k.m: ‘ambaye, ambao, ambalo, ambacho, huyo, yule’ - Ambalo lilipotea limepatikana.
- Ambaye hana mwana, aeleke jiwe
Viwakilishi Vya A-Unganifu
Huwakilishi nomino kwa kutaja kinachomiliki nomino hiyo. Huundwa kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na kiambishi -a cha a-unganifu, kisha nomino nyingine
k.m: ‘cha, la, kwa, za, ya’ - Cha mlevi huliwa na mgema
- Za watoto zitahifadhiwa.
Vielezi (E)
Kiingereza
Adverbs
Vielezi ni maneno yanayotoa habari zaidi kuhusu kitendo kilivyofanyika. Pia vielezi hutoa habari zaidi kuhusu hali, vivumishi au vielezi vingine. - AINA ZA VIELEZI
- Vielezi vya Mahali
- Vielezi vya Wakati
- Vielezi vya Idadi
- VIelezi Vya Namna
Aina za Vielezi
Vielezi vya Mahali
Vielezi vya mahali hutoa habari kuhusu mahali ambapo kitendo kilifanyika. Aghalabu vielezi hivi huundwa kwa kutumia jina la mahali au kwa kuongeza kiungo -NI mwishoni mwa neno linaloashiria mahali.
k.m: nyumbani, kazini, shuleni - Mtoto huyo hajatulia nyumbani tangu alipotoka Mombasa.
- Msipitie sokoni mkienda kanisani.
Vielezi vya Wakati
Huelezea zaidi kuhusu wakati kitendo kipofanyika
k.m: jioni, jana, asubuhi, saa saba, mwaka juzi - Mzee Kasorogani amesema kwamba ataoga mwaka ujao
- Musa alilazimishwa kuchimba mtaro saa sita usiku
- Kisaka na Musa watakutana kesho
Vielezi vya Idadi
Vielezi vya idadi hutulezea kitendo kilifanyika mara ngapi
a) Idadi Kamili
Vielezi vya Idadi Kamili hutaja idadi kamili ya mara ngapi kitendo kilifanyika.
k.m: mara mbili, siku mbili kwa juma, mara kumi - Gibi alimzaba kofi mara tatu na kisha akakimbia.
- Daktari alimwagiza mama huyo achukue dawa mara tatu kwa siku na arudi hospitalini siku mbili kwa mwezi
b) Idadi Isiyodhihirika idadi jumla
Vielezi vya Idadi Isiyodhirika huelezea kiasi ambacho kitendo kilifanyika bila kutaja kiasi kamili
k.m: chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani - Mwizi wa kuku alipigwa mara kadhaa kabla ya kuokolewa na polisi.
- Yeye hunipigia simu mara kwa mara
VIelezi Vya Namna
Huelezea jinsi au namna kitendo kinavyofanyika. Kitendo kinaweza kufanyika kwa namna mbalimbali. Hivyo basi kuna aina mbalimbali za vielezi vya namna:
a) Vielezi vya Namna Halisi
Hutufahamisha jinsi kitendo kinavyofanyika kwa kutumia maneno halisi (bila kuambatanishwa na maneno mengine au viambishi vingine).
k.m: vizuri, ovyo, haraka - Kioo cha bibi harusi kilianguka na kuharibika vibaya
- Mama alipika chakula upesi
- Amepigwa kalamu kwa kufanya kazi kiholela
b) Vielezi vya Namna Hali
Hutufahamisha hali ambayo kitendo kilifanyika. Vielezi hivi hujihusisha na tabia ya kitu/mtendaji wa kitendo
k.m: kwa furaha, kwa makini, - Bibi harusi aliingia kanisani kwa madaha
- Mtoto alilia kwa maumivu mengi
c) Vielezi vya Namna Kitumizi/Ala
Hutoa habari kuhusu kifaa, ala au mbinu iliyotumiwa kufanya kitendo fulani
k.m: kwa kisu, kwa jembe, kwa meno, kwa moto, kwa maji - Mkulima aliangusha mti mkubwa kwa shoka
- Mzee huyo alimpiga mke wake kwa bakora kabla ya kuchoma nguo zake kwa makaa
d) Vielezi Vikariri
Husisitiza kitendo kinavyofanyika kwa kutaja kielezi kinachorejelewa mara mbili mfululizo.
k.m: haraka haraka, ovyo ovyo, juu juu - Polisi walipoingia, wezi walitawanyika haraka haraka.
- Wanafunzi wengi hufanya kazi yao ovyo ovyo
e) Vielezi vya Ki-Mfanano
Vielezi mfanano hutumia KI-mfanano kuelezea kitendo kinavyofanyika kwa kulinganisha.
k.m: kitoto, kiungwana, - Babake huongea kiungwana.
- Harida hutembea kijeshi
f) Vielezi Viigizi
Vielezi hivi huigiza sauti au mlio wa kitu, kitendo kitendo kilipofanyika kwa kutumia tanakali za sauti
k.m: tuli, chubwi, tifu, chururu - Mwanafunzi alitulia tuli mwalimu alipomzaba kofi pa!
- Kaswimu aliangusha simu changaraweni tifu na kujitumbukiza majini chubwi
g) Vielezi vya Vielezi
Vielezi hivi hutumika kuelezea kielezi kingine. Hivyo basi, hutanguliwa na kielezi badala ya kitendo
k.m: sana, kabisa, hasa, mno - Mamake Kajino alitembea polepole sana.
- Chungu kilivunjika vibaya kabisa
h) Vielezi vya Vivumishi
Hutoa habari zaidi kuhusu kivumishi
k.m: sana, kabisa, hasa, mno - Yeye ni mrefu sana
- Mtoto wake ana tabia nzuri mno
Viunganishi (U)
Kiingereza
Conjunctions
- Viunganishi ni maneno yanayoutumika kuunganisha, kulinganisha au kuonyesha uhusiano wa dhana mbili au zaidi.
Aina za Viunganishi
Zifuatazo ni aina mbalimbali za viunganishi kulingana na matumizi yake
A-Unganifu
Kiatu cha Mzee Sakarani kimepasuka.
KWA (umilikaji wa mahali)
Mbinguni kwa kuna makao mengi.
na
Baba, mama na watoto huunda familia kamili.
pamoja na
Mwizi aliiba runinga pamoja na redio
fauka ya, licha ya
Fauka ya mapigo yote, Kafa alikatakatwa kwa kisu.
zaidi ya, juu ya
Unataka nini tena zaidi ya mema yote niliyokutendea?
pia, vilevile
Alimpiga mkewe na bintiye vilevile
mbali na
Mbali na hayo nitakujengea nyumba ya kifahari.
aidha
Keti akitoka shuleni atapika. Aidha atampelekea nyanya sukuma wiki.
wala (kukanusha)
Ndege wa angani hawalimi wala hawapandi.
lakini, ila
Ongea nayeilausimwambie mipango yetu.
bila
Tasha aliondoka bila kusema lolote.
bali
Sitawaacha kama mayatima bali nitawatumia msaidizi.
kinyume na, tofauti na
Jana kulinyesha kinyume na utabiri wa hali ya hewa.
ingawa, ingawaje
Nitamtembelea ingawa sijui nitamwambia nini.
japo, ijapokuwa
Nakuomba upokee nilichokileta japo ni kidogo sana.
ilhali
Fungo zimepotea ilhali zilikuwa zimewekwa vizuri.
minghairi ya
Waliendelea kutenda dhambi minghairi ya kuhubiriwa kanisani.
dhidi ya
Vita dhidi ya gonjwa hilo vingali vinaendelea.
ili
Hanna aliumizwa ili asikumbuke aliyoyaona.
kwa, kwa vile
Emili alinyamaza kwa vile kugombana na rafikize.
kwa maana, kwa kuwa
Aria alipigwa na butwaa kwa maana mpenzi wake aligeuka kuwa mwalimu wake.
kwani
Melisa alijificha kwani hakutaka kuonekana na Spensa.
kwa minanjili ya
Chali alitembea mwendo huo wote kwa minanjili ya kuongea na Katosha.
maadam
Wanawake katika familia hiyo hawali maini maadam mama mkongwe alilaani maini katika familia hiyo.
madhali
Madhali sote tuko hapa, tunaweza kuanzisha mkutano mapema
basi, hivyo basi
Umekula ng’ombe mzima, hivyo basi huna budi kumalizia mkia.
kwa hivyo
Alipatikana na makosa ya kumnajisi bintiye, kwa hivyo akahukumiwa miaka kumi gerezani.
ndiposa
Mama Kelele alipenda kuongea sana, ndiposa wakamkata midomo.
kama, sawa na
Kunywa pombe ni kama kujichimbia kaburi mwenyewe.
kulingana na
Mwalimu Makunza hafanyi kazi kulingana na maadili ya shuleni.
kuliko, zaidi ya
Talia ni mfupi kuliko Nuru
vile
Mganga Daimoni hutibu vile alivyofunzwa na Mganga Kuzimu.
- Kuonyesha Kitu kimoja kama sehemu ya kingine
kati ya
Vitatu kati ya vitabu hivi vimepigwa marufuku.
miongoni mwa
Miongoni mwa walioachiliwa, ni Ngiri na Mende.
baadhi ya
Baadhi ya wasichana kutoka Vikwazoni hawaheshimu miili yao.
mojawapo
Mojawapo ya maembe uliyochuma yameoza.
- Kuonyesha Kitu kufanyika baada ya kingine
kisha
Soma mfano huu kisha usome sentensi ifuatayo.
halafu
Alichukua kisu halafu akatokomea gizani.
- Kuonyesha Kitu kufanyika badala ya kingine
badala ya
Mapepo yalimchukua Shakawa badala ya bintiye
kwa niaba ya
Mama Roga alitoa hotuba kwa niaba ya mumewe.
labda, pengine
Sina pesa leo, labda uje kesho.
ama, au
Ama Anita au Katosha anaweza kuja.
huenda
Huenda kesho ikifika, Mungu atende miujiza.
bora, muradi
Sitakuuliza bora tu usichelewe.
ikiwa, iwapo
Ikiwa huna jambo muhimu la kusema, nyamaza.
Vihisishi (I)
Kiingereza
Injections
Vihisishi ni maneno yanayotumika kuonyesha hisia kama vile hasira, furaha, mshangao, kusifia, kushangilia n.k. Vihisishi hutambulishwa katika sentensi kwa kuambatanishwa na alama ya mshangao (!). Kihisishi kimoja kinaweza kutumika kutoa hisia tofauti kulingana na muktadha.
Mifano ya Vihisishi
Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya maneno yanayotumika kuonyesha hisia. Hata hivyo, maneno mengine yoyote yanaweza kutumika kama vihisishi, kulingana na mukhtadha. k.v Potelea mbali!
Kihisishi
Mfano katika Sentensi
Hisia
Lo!
Lo! Maajabu ya Musa haya!
mshangao
Salaale!, Masalaale!
Salaale! Angalia watu wote hawa waliofika mahali hapa!
mshangao
Kumbe!
Nilidhani wewe ni rafiki yangu. Kumbe!
mshangao
Po!
Sijawahi kuona kijana mjeuri kama wewe. Po!
hasira
Ng’o!
Omba msamaha utakavyo, lakini unachoka bure. Ng’o!
kiburi
Hata!
Bwanake hakumwachia chochote! Hata!
kusifia, kupuuza
Akh!, Aka!
Mtoto mpumbavu huyu! Akh!
hasira, kukashifu
Ah!
Ah! Sikuyaamini macho yangu.
mshangao
Ala!
Ala! Umefika tayari!
mshangao
Haha!
Haha! Umenivunja mbavu, bwana!
kicheko
Ehee!, Enhe!
Enhe! Endelea, ninaipenda sana hadithi hiyo!
kuitikia
Hmmm!
Hmmm! Chakula kitamu hicho!
kuitikia, kusifia
Ebo!
Ebo! Tabia gani hiyo.
kukashifu, hasira
Kefule!
Kefule! Umenifedhehesha sana.
hasira
Wee!
Katamu alinegua kiuno na kucheza kwa madaha. Wee! Wavulana wakaduwaa.
kusifia
La!, Hasha!
La! Sitaki kusikiliza upuuzi wako tena.
kukataa
Hoyeee!
Wamama wote, hoyee! Hoyee!
kushangilia
Huraa!
Huraa! Tumeshinda.
kushangilia
Vihusishi (H)
Kiingereza
Prepositions
Vihusishi ni maneno yanayotuarifu zaidi kuhusu uhusiano wa nomino na mazingira yake. - AINA ZA VIHUSISHI
- Vihusishi vya Mahali
- Vihusishi vya Wakati
Aina za Vihusishi
Vihusishi vya Mahali
mbele ya, nyuma ya
Kuna mzoga nyuma ya jengo hilo.
chini ya, juu ya
Joto lilipozidi, watoto waliketi chini ya mti ule.
kando ya
Kando ya mito ya Babeli ndipo tulipoketi.
karibu na, mbali na
Fisi aliambiwa asile mifupa karibu namtoto yule.
Vihusishi vya Wakati
kabla ya
Ni vizuri kusali kabla ya kula chakula.
baada ya
Watoto safi hupiga meno mswaki baada ya kila mlo.
|