Niliwahi kueleza katika makala zangu za hapo awali na kusisitiza kuwa bado wako waandishi wengi wanaoendelea kufanya makosa ya hapa na pale bila kuzingatia ufasaha na usanifu wa lugha ya Kiswahili. Nilitilia mkazo katika uandishi hasa kwa upande wa sintaksia, mofolojia na semantiki katika Kiswahili. Niliwasihi waandishi wawe makini wanapoandika makala na taarifa za matukio mbalimbali. Watumie lugha sanifu na iliyo fasaha ili wasomaji wapate habari zilizo sahihi na za ukweli. Waandishi wasio makini wanaporuhusu neno ajari (malipo ya muda wa ziada-ovataimu) na ajali (tukio lenye kuleta madhara ambalo linatokea ghafla) kutumika bila uangalifu hupotosha maana iliyokusudiwa.
Katika makala ya leo nitajikita zaidi katika matumizi ya Kiswahili kwa watangazaji redioni na pia kwenye runinga.
Redio na runinga zimeanzishwa kwa lengo la kuelimisha, kuburudisha na kutoa taarifa kwa wananchi wa ngazi zote kuanzia watoto hadi watu wazima. Katika vyombo hasa vile vinavyoanzishwa na watu binafsi wako baadhi ya wafanyakazi ni vijana ambao baadhi yao hawakupatiwa mafunzo ya kutosha katika suala zima la utangazaji na hasa katika matamshi ya maneno, lafudhi sahihi ya Kiswahili, usomaji habari kwa kituo na kutilia mkazo maneno kulingana na misingi ya Kiswahili. Watangazaji wengi vijana wameathirika kutokana na lugha za asili na hivyo hutamka maneno kama vile wanazungumza lugha zao kikabila. Wako baadhi wanatamka maneno ya Kiswahili kwa kutumia lafudhi ya lugha za kigeni kama Kiingereza au Kiarabu. Hawatambui kuwa Kiswahili kina mpangilio wake wa matamshi ya maneno ambao ni fauti na lugha nyingine. Baadhi yao hawatambui ni wapi wanapotakiwa kuweka mkazo katika neno. Kwa mfano tukitamka neno ‘barabara ni tofauti na bara’bara. ‘Barabara (ni nomino), ni njia pana ya magari. Mkazo unakuwa katika silabi ya pili wa neno hilo. Hata hivyo, neno bara’bara (ni kielezi) na mkazo unakuwa katika silabi ya tatu ya neno hilo. Ni neno hili linaeleza jambo kuwa ni sawasawa kabisa au bila kasoro. Tunapokubali jambo tunasema barabara, naam, hasa, sawa. Maana ya tatu ya barabara ni aina ya ndege kama hondohondo. Kama mtangazaji hataweza kutambua tofauti za matumizi ya neno barabara atawababaisha na kuwakanganya wasikilizaji wake.
Ili kuwaweka watangazaji wa habari wawe katika hali ya kuridhisha, hasa katika matumizi fasaha na sanifu ya Kiswahili, wanatakiwa waanze kupata mafunzo ya lugha tangu waiwa katika madarasa ya awali, shule za msingi na sekondari kwa kuanzia na walimu. Walimu wanatakiwa kupatiwe mafunzo katika stadi zote za lugha kama kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika. Stadi hizi zinasomeshwa katika vyuo vya ualimu katika somo la lugha kwenye darasa na pia katika maabara. Matamshi sahihi ya Kiswahili yanatakiwa kufundishwa. Wanafunzi wengi kutoka vijijini wanatoka nyumbani kwao na hawajui Kiswahili cha kuridhisha. Wako wengine hata Kiswahili cha kuzungunza hawajui kabisa. Walimu wanatakiwa kuanza kuwafundisha kwa kutumia mbinu za ufundishaji hatua kwa hatua. Wanaanza na stadi za kusikiliza, kuzungumza, baadaye kusoma na kuandika. Stadi hizi hujengeka kwa walimu ili kuwa mfano bora wa kuigwa. Ni kawaida kwa walimu kufanya uchunguzi wa matatizo yanayowakabili watoto wanapoanza kujifunza Kiswahili. Watambue herufi zinazowatatiza wenyeji wa eneo la shule wanakotoka wanafunzi kwa maana lugha zao za asili ili zifahamike. Kwa mfano, wako wazungumzaji wanaochanganya herufi kama /l/ na /r/, /b/ na /p/, /z/ na /s/, /z/na /dh/, n.k. Mwalimu akifahamu tatizo hili itakuwa ni rahisi kuwasaidia wanafunzi wake tangu mwanzo. Wakufunzi vyuoni wanapaswa kuwaandaa wanachuo wao katika taaluma ya fonolojia kwa kutumia maabara za lugha (Language Laboratories). Ni bahati mbaya kuwa baadhi ya wakufunzi wa vyuo vya ualimu hawana ujuzi wa kutosha katika suala la fonolojia na mofolojia na sarufi kwa jumla. Vilevile baadhi ya vyuo hivi havina maabara kabisa. Mpaka sasa haijulikani ni hatua zipi zitachukuliwa ili kila chuo cha ualimu kiwe na maabara yake ya lugha. Hili ni tatizo kubwa ambalo linawathiri walimu wengi wa Daraja la A wanaoandaliwa kwenda kufundisha katika shule za msingi baada ya kumaliza mafunzo yao.
Katika vyuo vya uandishi wa habari suala la lugha halitiliwi mkazo kwa kiwango kinachotakiwa. Upo ushahidi tosha kuwa katika redio na kwenye runinga watangazaji wana udhaifu mkubwa wa lugha. Inasikitisha kuwasikia watangazaji wakikiboronga Kiswahili bila woga. Hawatambui kuwa taifa zima la Tanzania na hata nchi za jirani zinasikiliza redio zetu kama mfano wa kuigwa. Pamoja na matamshi na lafudhi isiyoridhisha, watangazaji wengi siyo makini. Nina maana kuwa wanazungumnza kama wako mtaani au kijiweni wakati sivyo.
Wako watangazaji wanaojitetea wakisema kuwa wanatangaza katika redio inayohudumia nchi za Afrika Mashariki kwa maana ya Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Kwa hiyo wanatumia lugha inayoeleweka katika nchi hizo ambayo ni Kiingereza. Wanachofanya ni kuwa wanachanganya Kiswahili na Kiingereza wakisema eti wakitumia Kiswahili baadhi ya wasikilizaji hawaelewi vizuri basi iwe ni Kiswahili na siyo vinginevyo.
Pamoja na udhaifu uliopo, yafaa vyombo vya habari viimarishwe katika kutoa mafunzo ya lugha. Vianze kwa kutoa mafunzo ya kujinoa katika utangazaji. Hii ina maana kuwa mafunzo yatolewe kwa walio kazini (in service trainng) kwa kipindi kifupi. Kozi hii inaweza kuandaliwa katika chuo kimojawapo cha uandishi wa habari kama ‘Tanzania School of Journalism (TSJ)’. Chuo hiki kina walimu waliobobea katika taaluma ya uandishi wa habari na pia kina vifaa vya kutosha vya kushughulikia taaluma hii. Wataalamu wa lugha wataweza kualikwa kutoa mihadhara ili kuinua kiwango cha watangazaji hawa.
Eneo la pili la kushughulikia ni kuhuisha mitalaa wa kufundisha waandishi wa habari kwa kuongezea vipengele vya sarufi ambavyo ni muhimu katika utangazaji. Mtalaa huu uwashirikishe wawakilishi wa wakufunzi kutoka katika vyuo mbalimbali vya uandishi wa habari pamoja na mabingwa wa sarufi kutoka katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hapa wako mabingwa ambao wanaweza kutumika kwa upande wa kuhuisha mtalaa wa uandishi wa habari uwe wa aina moja kwa vyuo vyote vya uandishi wa habari. Inashangaza kuona kuwa vyuo binafsi vinavyoanzishwa havina maandalizi ya kutosha kwa maana ya kuwa na walimu waliobobea katika uandishi wa habari, somo la Kiswahili na pia na vifaa vya kufundisha lugha. Matokeo yake ni kujidhalilisha wenyewe na pia nchi yao.
Jambo la msingi ni kuwatahadharisha watangazaji hasa katika runinga mpya zinazoanzishwa kuacha kuchanganya lugha ya Kiingereza wanapotangaza. Baadhi yao wanadhani kuwa kuweka maneno ya Kiingereza ni ufahari wakati sivyo. Yako maneno mengi ya Kiswahili yanayoweza kutumiwa na watangazaji wa aina hii. Hawa nawaita ni limbukeni.
Nikirejea katika suala la taaluma ya uandishi na utangazaji wa habari, napenda kushauri wahusika kuwa habari ni silaha muhimu sana katika maendeleo ya nchi. Ndiyo maana inasemekana kuwa ni muhimili wa nne katika nchi baada ya mihimili mingine kama Serikali, Bunge na Mahakama.
Kitivo cha Elimu/ Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Kijamii
Idara ya Kiswahili
Kozi: Kis 300; Mofolojia ya Kiswahili
Kazi ya Muhula
Mada: Mchango wa mofolojia katika taaluma nzima ya isimu.
Chaka Jumaa Ngombeko
Muhula: Agosti-Disemba, 2015
UTANGULIZI.
Isimu hushughulikia uchunguzi wa lugha mbalimbali kwa kutumia misingi ya kisayansi. Matawi ya isimu kama fonetiki, fonolojia, semantiki, mofolojia na sintaksia ndiyo huifanya isimu kuonekana kuwa sayansi ya lugha kulingana na majukumu mbalimbali yanayofanywa na matawi haya katika lugha.
Fonetiki huchunguza sauti za lugha ya binadamu; nayo fonolojia huchunguza jinsi sauti hizo huweza kuunganishwa na kuunda maneno yenye maana na baadaye mofolojia huangalia maneno yaliyoundwa miundo yake na kuzalisha maneno zaidi.
Mofolojia ni taaluma ya isimu ambayo ina jukumu la kuchunguza maneno ili kuelewa maumbo yake yalivyo (Mgullu, 1999).
MCHANGO WA MOFOLOJIA KATIKA TAALUMA NZIMA YA ISIMU.
Matthews (1991, Uk3) Mofolojia ni tawi la isimu linaloshughulika na ustadi wa maumbo ya maneno na jinsi maumbo hayo yanavyotumika katika miktadha mbalimbali ya matumizi ya lugha. Jukumu la neno husika katika sentensi hubainika vyema kulingana na uhusiano baina ya maneno mengine katiaka tungo. Kwa mfano: Jumaa amefika chuoni. Jumaa ni kiima kwani ndilo neno linalohusika na utendaji ilhali amefika chuoni ni kiarifu kwani sehemu hii inatoa maelezo juu ya kiima.
Maneno ni maumbo katika lugha yanayojisimamia. Maneno yenye maumbo sahili huwa na mofu moja tu; hayawezi kukatwakatwa na kutoa mofu zingine. Mofu hizi ni mofu huru. Kwa mfano baba, mama.Kwa upande mwingine maneno yenye maumbo changamani huwa na mofu zaidi ya moja; yaani kiambishi awali, mzizi na kiambishi tamati. Kwa mfano;
Mtangazaji {M+tangaz+a+ji}
{M}-kiambishi awali cha kunominisha;
{-tangaz-} mzizi wa nomino
{-a-} kiambishi tamati endelezi
{-ji} kiambishi tamati cha kunominisha
Bauer Laurie (2003, Uk 91), taaluma ya mofolojia imegawanywa katika matawi mawili; mofolojia ya minyambuliko ya maneno na mofolojia ya uundaji wa maneno. Mofolojia ya minyambuliko ya maneno husaidia kupatikana kwa maumbo mbalimbali ya leksimu ilhali mofolojia ya uundaji wa maneno husaidia kupatikana kwa leksimu mpya. Maneno yanapoundwa husaidia katika kuboresha mawasiliano baina ya binadamu. Watumiaji wa lugha hutafuta njia mbalimbali ili kupata maneno yanayotosheleza mawasiliano yao. Hivyo basi mofolojia imejenga isimu-jamii.
Matthews (1991, Uk9) mofolojia ni tawi la kisarufi linalochunguza maumbo ya ndani ya maneno. Mofolojia hutilia maanani sarufi ambayo ndiyo sehemu muhimu ya kila lugha. Sarufi ndiyo uti wa mgongo wa kila lugha hapa duniani. Bila sarufi lugha haiwezi kuwa na muundo sanifu unaokubalika na wenye kueleweka na watumiaji wake. Mofolojia huangalia hijai. Mofolojia huhakikisha maneno yameendelezwa vizuri. Ni sehemu hii ndiyo inaonyesha jinsi mofolojia huchunguza muundo wa maneno ambayo yameundwa kwa kutegemea taaluma ya fonolojia.
Matthews (1991, Uk 63) mofolojia pia huonyesha mifanyiko mbalimbali ya maneno katika lugha. Kwa mfano nomino huweza kuundwa kutokana na vitenzi, kiwakilishi, vivumishi, kielezi. Katika lugha ya Kiingereza maumbo ya nomino hutokana na maumbo ya vitenzi yanapoongezewa mofu –ion-. Kwa mfano:generate-generation.
Katika lugha ya Kiswahili aina ya neno huweza kubadilika linapoambishwa au kunyambuliwa. Kwa mfano: nomino msomi inaweza kuzalisha maneno kama kisomo, masomo, somea, someka, kusomeka.
Mofolojia huhusika na utambuzi wa mofu, mofimu, shina, mzizi na alomofu katika neno. Dhana hizi ambazo zilizalishwa na taaluma ya mofolojia husaidia katika taaluma nzima ya isimu ambapo dhana hizi huleta maana katika maneno ya lugha. Maana inayopatikana katika maneno ya lugha ndiyo semantiki.
Mgullu (1999), mofu ni umbo la neno ambalo huwakilisha mofimu na ambalo hudhihirika kifonolojia. Mofu ni sehemu halisi ya neno ambayo ina maana.
Mtangazaji (M+tangaz+a+ji)
{M} kiambishi awali cha kunominisha;
{-tangaz-} mzizi wa nomino
{-a-} kiambishi tamati endelezi
{-ji} kiambishi tamati cha kunominisha
Kumekuwa na swala la kuainisha lugha hasa katika karne ya Ishirini. Hapo mwanzo kulikuwa na haja ya kuelewa lugha ya kilatini na Kigiriki. Uelewa wa lugha zingine uliendelea kukua pia; ndipo lugha zikaanza kuainishwa kifamilia. Katika taaluma ya mofolojia lugha zinaainishwa kulingana na muundo wa maneno ya lugha hizo. Kigezo hiki cha kimofolojia kinatupatia lugha ambishi na tenganishi (Matthews, 1991 uk3-4). Hii husaidia kutofautisha miundo ya maneno ya lugha mbalimbali. Hivyo basi mofolojia inasaidia kuelewa miundo ya maneno ya lugha. Pia wanaohitaji kujifunza lugha za kigeni huweza kujifunza kwa urahisi wanapoelewa muundo wa maneno ya lugha hiyo.
Mgullu (1999, Uk 12), lugha ambishi ni ile lugha ambayo maneno yake huambishwa viambishi mbalimbali ambavyo huwakilisha maana mbalimbali; kwa mfano lugha ya Kiswahili- Neno: PIGA
Anapiga
Atapiga
Alipigia
Alipigiwa
Matthews (1991, Uk 20) Lugha tenganishi ni ile aina ya lugha ambayo maumbo ya maneno yake huonekana tu kama mofu moja moja. Mfano ni Kituruki, Kichina na Kiingereza.
Maumbo ya maneno ya lugha tenganishi hayaambishwi wala kunyambuliwa. (Mgullu, 1999 Uk 12). Kwa mfano katika lugha ya Kiingereza;
With,
Rice.
Matthews (1991, Uk 19), mofolojia imeleta mchango mkubwa katika isimu nzima. Mofolojia ni kiungo muhimu katika isimu. Mofolojia imeweka wazi masuala muhimu kuhusu maumbo ya maneno katika lugha zote duniani. Mofolojia imeweza kusaidia wanaisimu kutambua mofu, mofimu, na alomofu katika kuchunguza miundo ya maneno katika lugha.
Kwa mfano; viambishi katika lugha ya Kiingereza hupatikana mwishoni mwa mzizi wa neno kwa sababu mara nyingi huonyesha dhana ya wingi; kama –s, ies, ren, (child-children). Katika lugha ya Kiswahili mara nyingi mzizi wa neno hutanguliwa na mofu ambayo ni kiambishi awali na kisha kufuatiwa na kiambishi tamati. Haya ni yale maneno ambayo yana mofu tegemezi. Kwa mfano:
-end-
naenda
Siendi
Endea
Endeleza
Hivyo basi mofolojia imesaidia kujua maumbo ya maneno ya lugha mbalimbali.
Matthews (1991, Uk 19-20) mofolojia inaeleza jinsi maneno katika lugha yanavyobadilika hasa kimaendelezo jinsi muda unavyosonga. Hapa mofoloia hujikita kuangalia mabadiliko ya maneno katika lugha husika kwa kuzingatia vipindi vya kihistoria. Mahitaji ya kimatumizi ya maneno husika katika lugha ndiyo husukuma wanajamii kubadili dhana za kimatumizi ya maneno fulani kulingana na wakati huo. Kwa mfano; neno girl (gyrle) hapo kale lilikuwa linamaanisha mtoto wa kiume au wa kike lakini likafinyika kimaana na leo hii linarejelea tu mtoto wa kike.
Katika lugha ya Kiingereza kipashio –pter- kiliazimwa kutoka lugha ya Kigiriki kikiwa kinamaanisha unyoya feather au ubawa wing. Kipashio hiki kimetumika kuunda neno helicopter ambapo kifaa hiki kina tabia sawa na dhana ya kipashio hicho (Katamba na Stonham, 2006 Uk.22) Hivyo basi mofolojia imesaidia kueleza historia ya maneno katika lugha.
Matthews (1991, Uk 37) mofolojia husaidia katika kupeana njia mbalimbali za uundaji wa maneno katika lugha. Hii ni kwa sababu kila lugha inakua kulingana na mahitaji ya jamii yake. Kila lugha inahitaji maneno mapya yaundwe kila siku kwa sababu jamii mbalimbali hutagusana kila siku. Ili kurahisisha mawasiliano lazima kuwe na maneno yanayoweza kusaidia kurahisisha mawasiliano ya watu wa jamii hizo tofauti. Pia maneno yanaweza kuundwa ili kupeana majina vitu vigeni; yaani vitu vinavyovumbuliwa kila siku kupitia teknolojia. Kuna njia kama mwambatano, kutohoa, kubuni, akronimu. Maumbo ya maneno yanayoundwa hutegemea mazingira ya jamii na sheria inayothibiti uundaji wa maneno katika lugha hiyo. Hivyo basi mofolojia husaidia kuchagua njia mwafaka ya uundaji wa maneno kulingana na mazingira husika.
Mofolojia pia inadhihirisha uhusiano uliopo baina ya lugha moja na nyingine. Lugha nyingi duniani zinategemeana katika mawasiliano. Wenyeji wa lugha mbalimbali hulazimika kukopa maneno ya lugha za kigeni ili kusaidia katika mawasiliano. Mofu za kigeni zinapoingizwa katika lugha fulani husahihishwa na kufuata muundo wa maneno ya lugha husika kulingana na sheria ya uundaji wa maneno wa lugha hiyo. Hivyo basi mofolojia imesaidia lugha nyingi kuingiza mofu za kigeni na kukuza lugha hizo na kurahisisha mawasiliano (Katamba na Stonham, 2006 Uk. 78-79).
Taaluma ya mofolojia hueleza ni kwa nini majina mengine huwa na maumbo yale yale katika dhana ya umoja na wingi. Majina kama maziwa, mchanga, maji hubaki vivyo hivyo kimaandishi katika umoja na wingi. Mofolojia imerahisisha kueleweka kwa hali hii kwani majina mengine huwa tu na dhana ya wingi au umoja katika akili za wazungumzaji. Mofolojia hutumia mofu kapa kuonyesha umoja au wingi wa majina kama hayo.
Kwa mfano:
Wingi umoja
Maziwa Ømaziwa
Mofolojia ndiyo chanzo cha kujifunza msamiati. Wanafunzi hutumia elimu ya mofolijia ili kutambua maana ya maneno yanayoibuka kila wakati. Mofolojia huwa na sheria ambazo humwongoza msemaji kuongeza umilisi katika lugha.
Mofolojia humhamasisha mwanafunzi kuhusu uandishi na usomaji bora katika lugha. Mwanafunzi huweza kujua namna ya kuandika maneno na maumbo yake mbalimbali.
Msomaji anapotambua sheria ya uundaji wa maneno katika lugha na jinsi ya kuandika na kusoma maneno humrahisishia kusoma matini mbalimbali na kuzielewa vizuri. Mofolojia husaidia kujua maana ya maneno inayonuiwa katika mawasiliano ndani ya lugha. Maana ya maneno huenda yakabadilika kutegemea mazingira yalimowekwa. Maneno yanapowekwa pamoja na maneno mengine katika tungo huweza kuwa na maana. Hivyo basi mofolojia imejenga semantiki na sintaksia na kuifanya isimu nzima ikue (Nagy, Carlisle & Goodwin (2013).
Maneno huweza kuwekwa katika makundi yaani ngeli. Nomino hugawanywa na kuainishwa kimakundi kulingana na sarufi; kila kundi likiwa na mabadiliko ya aina moja ya viambishi vya umoja na wingi (Kihore na wenzake, 2003).Mofolojia ndiyo imechangia kuainisha ngeli kisintaksia kwani maana ya maneno yanayofafanuliwa na taaluma ya mofolojia ndiyo huongoza uanishaji wa majina kisintaksia.
Marejeleo:
Bauer Laurie (2003), Introducing Linguistic Morphology: 2nd Edition. Edinburgh. Edinburgh University Press.
Katamba Francis and Stonham John (2006), Modern Linguistics Morphology: New York. PALGRAVE MACMILLAN.
Kihore na wenzake (2003), Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: TUKI
Matthews P. H (1991), Morphology (Second Edition): United Kingdom. Cambridge University Press.
Mgullu R. S. (1999), Mtalaa wa Isimu: Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi. Longhorn Kenya Ltd.
Nagy, W. E., Carlisle, J. F, & Goodwin, A. P. (2013). Morphological Knowledge and Literacy Acquisition. Journal of Learning Disabilities, 47(1) 3–12. DOI: 10.1177/0022219413509967.
Fasili: -0-rejeshi ni kiambishi cha mtenda au mtendwa ambacho hujitokeza katika kitenzi au amba- ili kuonesha dhana ya urejeshi. Urejeshi huo hufuata mfumo wa upatanishi wa kisarufi yaani mfumo wa ngeli. Ngeli ni utaratibu wa kupanga majina ya Kiwahili katika makundi yanayofanana. Kiambishi hiki hujiegemeza kwenye kiambishi ngeli cha nomino iliyotajwa.
Viambishi vya –o- rejeshi ni kama vile -ye-, -o-,
-cho, -mo-, -vyo-
Kwa mfano:
Mtu a-li-ye-iba
Watu wa-li-o-iba
Katika mifani (i) na (ii) -ye- na -o- ndivyo vinavyoitwa viambishi vya -o- rejeshi.
Katika -o- rejeshi vitenzi hubeba viambishi ngeli vyenye kiangami -o- isipokuwa kama nomino iliyotajwa ni ngeli ya kwanza umoja. Urejeshi wa ngeli hiyo hutumia -e- badala ya
-o-. Hivyo, -ye- ni -o- rejeshi kwa kwa inaangukia kwenye ngeli ya kwanza (YU/A-WA) hata kama haina -O-
Swali: Taja mazingira matatu ya kisarufi ya utokeaji wa -o- rejeshi katika tungo. Kiambishi cha -o- rejeshi hujitokeza katika mazingira yafuatayo:
Mosi hujitokeza kabla ya mzizi wa kitenzi.
Kwa mfano:
Mzizi wa kitenzi ni -li-; kiambishi -ye-kimejitokeza kabla ya mzizi wa kitenzi na ndivyo ilivyo katika mfano wa ii ambapo mzizi wa kitenzi ni -imb-, hivyo kiambishi rejeshi –vyo- kimejitokeza kabla ya mzizi huo.
Pili, -o- rejeshi hutokea baada ya mzizi wa kitenzi. Mfano (ii) -j- ndiyo mzizi wa kitenzi, kirejeshi –o- kimejitokeza baada ya mzizi wa kitenzi.
Mwisho –o- rejeshi hujitokeza katika shina amba-. Shina hili huongezewa viambihi vya -o- rejeshi na kupata neno lionyeshalo urejeshi. Hapa tunapata maneno kama ambalo, ambaye, ambacho, nk. haya ndiyo mazingira ya utokeaji wa -o- rejeshi. Zifuatzo ni dhima tano za -o- rejeshi:
TANGULIZI. Maana ya unyambulishaji Massamba (2009:105), unyambulishaji ni utaratibu wa kupachika viambishi kwenye mizizi ili kuunda maneno mapya. Unyambulishaji ni mbinu ya uundaji wa maneno,hivi kwamba viambishi mbalimbali huambikwa kwenye mzizi husika na kuunda neno jipya.(Matinde,2012:119). Unyambulishaji ni utaratibu katika lugha wa kupachika au kuongeza viambishi kwenye mzizi wa neno ili kuunda maneno mapya. Kwa mfano, kuunda nomino kutokana na vitenzi kwa kutumia viambishi. Maneno mapya yanayoundwa hapa huwa ya kategoria nyingine (Masebo,2012:127). Hivyo basi tunaweza kusema kwamba unyambulishaji ni aina ya uambishaji unaosababisha neno kutoka katika kategoria moja hadi nyingine. Unyambulishaji wa nomino Habwe na Kalanje (2004),wanadai kuwa unyambulishaji wa nomino ni hali ya kuunda nomino kutoka kuwa kategoria nyingine za maneno huitwa unominishaji. Nomino za Kiswahili zinaweza kuundwa kutokana na vitenzi, vivumishi na hata kutokana na nomino moja hadi nyingine. Hivyo basi, unyambulishaji wa nomino ni hali ya kuweka viambishi vinyambulishi kwenye mzizi wa neno ambao hupelekea neno hilo kuhama kutoka kategoria moja kwenda kategoria nyingine ambayo ni nomino. Nomino. Ni neno linalotaja kitu, kiumbe, hali, dhana au tendo kama kiti,ndege na furaha. (Massamba, 2009:68). Unyambulishaji wa nomino hufanyika kama ifuatavyo; Kinominishi {o} kinaweza kunominisha vitenzi vya Kiswahili katika mazingira yafuatayo; Kwa mfano vitenzi vya kibantu vinavyoishia na kiambishi tamati {-a} {Mzizi} + {-o} Mfano, Kitenzi mzizi nomino Tenda tend +o tendo Andika andik + o andiko Jenga jeng + o jengo Pamba pamb + o pambo Hata hivyo, kuna baadhi ya vitenzi vya kibantu ambavyo huishia na kiambishi tamati {-a} ambavyo vikiambikwa viambishi tamati {-o} haviwezi kubadilika na kuwa nomino. Kwa mfano kitenzi ;Lowa,tembea. Pia kiambishi cha unyambulishi {-o} huweza kunyambulisha nomino kwa kuambatana na kinyambulishi {-i} au {-li}. kwa mfano; {mzizi} + {-i/-li-} + {-o} Kitenzi mzizi nomino Kaanga kaang + i + o kaangio Chuja chuj + i + o chujio Kaa ka + li + o kalio Mazingira mengine kiambishi kinyambulishi {o} huweza kunominisha kitenzi pale ambapo huambatana na mofimu {e}. {mzizi} + {-e-} + {-o} Kwa mfano; Kitenzi mzizi nomino Fyeka fyek + e + o fyekeo Chekecha chekech + e + o chekecheo Pia unyambulishaji wa nomino huweza kutokea kwa kuambika kiambishi {M-/Mw-} mwanzoni kabla ya shina la kitenzi na kiambishi cha unyambulishi {-ji} baada ya mzizi wa neno. Kiambishi tamati {-ji} cha unominishaji ambacho huonesha mtu anayetenda kitendo kama kazi yake ya kila siku. {M/Mw-}+{shina-T}+{-ji} Mfano kitenzishinanomino Baka m + baka + ji mbakaji Chezam + cheza + ji mchezaji Imba mw+imba+ji mwimbaji Omba mw +omba + jimwombaji Nomino zenye mofolojia yenye kiambishi awali {ku}, ambacho hutumiwa kuunda nomino. Kiambishi hiki {ku} huwekwa mbele ya shina la kitenzi na hubadili kitenzi kuwa nomino. {Ku-} + {shina-T} Mfano, Kitenzi shina nomino imba ku + imba kuimba Cheza ku + cheza kucheza Lia ku + lia kulia Piga ku + piga kupiga Nomino zenye mofolojia yenye kiambishi awali {u} cha unominishaji , mzizi wa kitenzi na kiambishi tamati {vu/fu} cha unominishaji. Huonyesha mtu au watu walio katika hali fulani. {u} + {MZIZI} + {vu/fu} Mfano:- Kitenzi Mzizi Nomino Tulia u + tuli + vu Utulivu Vumilia u + vumili + vu Uvumilivu legea u + lege + vu Ulegevu Nomino zenye mofolojia yenye kiambishi awali {ki} cha unominishaji katika umoja au {vi} katika umoja , mzizi wa kitenzi na kiambishi tamati {o} kiambishi hiki huweza kuleta dhana ya kitu/ kifaa kinachotumika kutenda kitendo. {Ki/ Vi} + {MZIZI} + {o} Mfano:- Kitenzi Mzizi Nomino Funika ki + funik + o kifuniko/vifuniko Pima ki + pim + o kipimo/vipimo Tua ki + tu + o kituo/vipimo Kiambishi kinyambulishi {-a} Ikiwa kitenzi huishia kwa irabu i au u irabu hizo hubadilika na mahali pake huchukuliwa na kiambishi tamati {a} hivyo husababisha kitenzi kubadili kategoria yake na kuwa nomino. Yaani, {mzizi} + {a} Mfano, Kitenzi mzizi nomino Hoji hoj + a hoja Faidi faid + a faida Heshimu heshim + a heshima Unyambulishaji katika vitenzi Rubanza Y.I (1996), unyambulishaji wa vitenzi ni upachikaji wa mofimu fuatishi katika vitenzi. Kitenzi ni neno ambalo huarifu tendo linalofanyika. TUKI (2012). Mgullu (2012),anadai kuwa katika lugha ya Kiswahili vitenzi vinaweza kuundwa kutokana na vivumishi. Kwa mfano; Refu refusha Fupi fupisha Bora boresha Safi safisha Pia mara chache sana nomino zikinyambuliwa huunda vitenzi, Masebo (2012:134). Kwa mfano; Nomino Kitenzi Taifa taifisha Sulubu sulubisha Ratiba ratibu Hata hivyo kuna idadi ndogo ya vielezi vikinyambuliwa vinaweza kutumikakatika kuunda vitenzi. Kwa mfano; Kielezi Kitenzi Haraka harakisha, harakishwa, HITIMISHO. Unyambulishaji wa maneno katika lugha ni muhimu sana katika ukuaji wa lugha kwani hupelekea kuongezeka kwa misamiati katika lugha. MAREJELEO. Habwe na Karanja, (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Foenix Publishers. Massebo (2012). Nadharia ya Lugha Kiswahili 1,kidato cha 5&6.Dar Es salaam: Nyambari Matinde, S. (2012), Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia, kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo Mgullu, (2012), Fonetiki, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn Publishers. Nyangwine Publishers. TUKI (2012). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar Es salaam: Oxford University Press. Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.
Sarufi finyizi ni nadharia ya kisarufi ambayo inaangazia utaratibu wa kuchunguza lugha ulio na unyumbufu wa mielekeo tofauti inayowezeshwa na ufinyizi wake. Sarufi finyizi imekuwa ikikua ndani ya nadharia ya hapo awali ya sarufi zalishi tangu miaka ya tisini. Hasa hujikita katika kueleza sifa za kijumla ambazo lugha ya mwanadamu huwa nazo.
Nadharia hii ilianzishwa na mwanaisimu wa Kimarekani na mwenye asili ya Uyahudi Noam Chomsky. Katika sarufi finyizi, Chomsky anaiwasilisha sio hasa kama nadharia bali kama utaratibu wa uchunguzi wa lugha. Nadharia hii ilijitokeza kwa mara ya kwanza mwaka wa 1993 kupitia kazi yake Chomsky “A minimalist program for linguistic theory.“
Hata hivyo, nadharia hii aliiweka wazi mwaka wa 1995 katika chapisho lake “The Minimalist Program.” Baadhi ya watu waliowahi kuirejelea na kuizungumzia nadharia hii ni kama vile Webelhuth (Tah) (1995), Brody (1995), Cook na Newson (1996), Radford (1997) miongoni mwa wengine.
Sarufi finyizi ni maendelezo na uboreshaji wa nadharia ya sarufi zalishi iliyoanzishwa na Chomsky mwenyewe alipoizungumzia kwa mara ya kwanza mwaka wa 1957 katika chapisho lake “Syntactic Structures.’
Sarufi zalishi ilianza hasa kwa kutofautisha dhana mbili kuu ambazo ni umilisi lugha na utendaji lugha. Pia ilitambulisha muundo nje na muundo ndani. Muundo ndani uliwakilisha umilisi nao muundo nje ukawakilsha utendaji.
Kufuatia sarufi finyizi, dhana ya muundo ndani iliondolewa ikabaki ile ya muundo nje pekee. Aidha vinadharia vilivyoongoza uchanganuzi wa sentensi viliondolewa na vikageuzwa kuwa kanuni za kisintaksia katika sarufi finyizi. Jambo hili linaangaliwa kuwa na umuhimu wa kuifanya nadharia ya lugha kuwa na uwekevu zaidi na urahisi kuliko sarufi panuzi ya awali.
Sarufi finyizi inajikita katika kuendeleza malengo ya sarufi zalishi ambayo yanahusisha kuandaa sintaksia bia ya lugha. Hii ina maana ya sarufi ambayo inajumlisha kanuni zinazoweza kudhihirika katika lugha yoyote ya mwanadamu. Hivyo basi, sarufi ya kijumla inayoeleza sifa zinazopatikana katika lugha zote za mwanadamu inazingatia maongozi maalum. Haya ni pamoja na sifa ya kuwa na ufafanuzi toshelevu, uasilia wa lugha inayochunguzwa, upekee wa lugha ya mwanadamu na ujumla wa tanzu zote za lugha. Pia utumiaji wa vipengee vichache vyenye utoshelevu (ufinyizi) na urahisi au wepesi wa kueleweka.
Aidha, sarufi finyizi inalenga kutafuta uhusiano kati ya nadharia ya isimu na tanzu nyinginezo za lugha kama vile miundo ya fasihi na falsafa ya lugha.
Nadharia ya sarufi finyizi inajikita katika imani kuwa kunayo idadi maalum ya sheria ambazo hufanya kazi kwa lugha zote za mwanadamu. Pia inashikilia kwamba kuna mseto wa sifa unaoweka msingi wa mfumo anaopata mtoto mzawa wa lugha fulani na ambao unamwezesha kuipata lugha kwa urahisi.
Chomsky (1995) anahoji kwamba yapo maswali yazuliwayo na sarufi finyizi tu ila majibu yake yanaweza kufafanuliwa katika nadharia yoyote. Kwake, swali muhimu zaidi kati ya yote ni lile linaloulizia sababu za lugha ya mwanadamu kuwa na sifa inazodhihirika kuwa nazo. Hivyo basi, sarufi finyizi inaandaa mtazamo mahsusi wa misingi ya sintaksia katika sarufi ya lugha. Katika hali hii, sarufi finyizi inapolinganishwa na mifumo mingineyo inatazamika kama nadharia.
Mhimili mwingine muhimu wa sarufi finyizi ni kuwa utendaji wa lugha miongoni mwa watu ni ishara tosha inyothibitisha mfumo komavu ulio na mpangilio maalum. Suala hili linaelekeza kwamba mfumo wa lugha umeingiliana na kurandana na kanuni nyepesi ya matumizi yake au kuhimiliwa ama na kiungo au kitivo fulani maalum katika ubongo wa binadamu. Hii ni kumaanisha kwamba sarufi finyizi inajiegemeza katika dai eti sarufi bia inajumlisha muundo toshelevu unaofanikisha mahitaji ya ufahamu na yale ya kimatamshi.
Katika mtazamo wa kinadharia na muktadha wa sarufi zalishi, sarufi finyizi inaainishwa kama mtazamo wa kanuni na sheria unaoangaliwa kuwa kielelezo cha upeo wa nadharia ambayo imekuwa ikikuzwa na kuendelezwa na isimu zalishi tangu miaka ya themanini. Mtazamo huu unachokieleza ni kuwepo kwa mseto maalum wa sheria zinazotumika katika lugha zote. Sheria hizi zikishirikishwa kwa miundo fulani ya kanuni zenye idadi mahsusi hueleza sifa za mfumo wa lugha ambao mtoto mzawa wa lugha hiyo huja kupata.
Sarufi finyizi inatambulisha jumla ya kategoria nane za maneno ambazo zinagawika katika matapo mawili. Tapo la kwanza ni lile la kileksia na la pili ni lile la kisarufi
Tapo la kileksia linahusisha kategoria za maneno ambazo zinawakilisha maana msingi au maana za kileksia. Kategoria hizi ni tano kama ifuatavyo:
i) Nomino
ii)Kitenzi
iii) kivumishi
iv)kielezi
v)Kielezi
Tapo la kisarufi huwa na kategoria za maneno ambayo hayawakilishi maana ya kimsingi. Maneno haya huwa na umuhimu wa kuendeleza maana ya maneno ya kileksia. Kategoria hizi za kisarufi ni tatu:
i)Kibainishi
ii)Kishamirishi
iii) Kipatanishi
Kutokana na maelezo haya, ni wazi kuwa sarufi finyizi inatumika kufafanua na kuchanganua sentensi za Kiswahili. Sarufi finyizi inatambulisha sentensi sahili kama kishazi huru na kuchukulia utanzu wa sintaksia kuwa msingi zaidi.
Urahisishaji wa jinsi ya kuchanganua sentensi kwa kuondoa muundo ndani na muundo nje huenda una manufaa lakini itachukua muda kujenga uzoevu wa hatua zilizopendekezwa. Pia kuondolewa kwa vile vinadharia na kupunguzwa kumeondoa utata pamoja na kutupilia mbali dhana ya x-baa na ile nadharia ya utawala na ufungamanisho.
Japo sarufi finyizi ilipata uungwaji mkono na wasomi wanaisimu, kunao waliipinga mwishoni mwa miaka ya tisini. Kwa mfano, David E. Johnson na Shalom Lappin katika jarida la Natural Language and Linguistic Theory wanadai kuwa sarufi finyizi haikutokana na mtazamo wa kisayansi na hivyo haikuwa na malengo yoyote ya kiusomi bali ni dhana iliyotokana na Chomsky kutaka tu kujidai na kunadhifisha nadharia ya awali ya lugha.
Wanadai kuwa kukubalika kwa sarufi finyizi hakukuwa na manufaa au ishara zozote za mapinduzi ya kisayansi katika isimu ila ni kutokana na nafasi na mchango wa hapo awali wa Chomsky katika taaluma ya isimu.
Kutokana na hali ya nadharia hii kuendeleza sarufi bia, ni wazi kwamba sarufi finyizi hutumika kueleza vipengee vya lugha yoyote ya mwanadamu.
MATUMIZI ya lugha rasmi aghalabu hutegemea matukio, wakati, idadi ya walengwa, uhusiano baina ya mzungumzaji au mwandishi na hadhira yake pamoja na uwezekano wa habari kuwa ama za kibinafsi au kwa ajili ya umma.
Katika kuchunguza lugha, wanaisimu hutumia misingi ya kisayansi kama zifanyavyo sayansi nyingine. Maswala katika isimu huelezwa kwa udhahiri usio na utata wowote.
Hoja huelezwa bila kuleta vuguvugu lolote la kimaana.
Habwe na Karanja, (2003) wanaeleza kuwa utaratibu na uwazi ni dhana zinazokaribiana sana. Bila kuwa na uwazi ni vigumu kuwa na utaratibu na kinyume chake.
Utaratibu ni kufanya jambo kwa mpangilio mzuri wenye kubainika na aghalabu unaweza kuhusisha wakati, idadi, umuhimu na hata ukubwa.
Katika kushughulikia na kuelewa lugha mwanaisimu hujikuta akiwa na kazi ya kutimiza majukumu ya kueleza maana na asili ya lugha, kuchambua muundo wa lugha, kueleza uhusiano kati ya lugha na asasi nyingine za mwanadamu na kuibua nadharia mbalimbali za lugha.
Hizi ndizo sifa bainifu ambazo kwa mara nyingi hutuelekeza katika uwezo wa kutofautisha lugha zinazotumika katika kudumisha mawasiliano ya kila siku miongoni mwa wanajamii.
Umilisi (langue) ni ujuzi alionao mjua lugha kuhusu lugha yake. Ni ujuzi alio nao mjua lugha ambao upo katika ubongo wake. Ujuzi huo huhusu kanuni zinazotawala lugha hiyo husika.
Ujuzi huu humwezesha kutambua sentensi sahihi, zisizo sahihi na kupambanua sententi zenye utata. Ujuzi huo humwezeha kupuuza makosa ya kiutendaji katika mazungumzo kama vile kuteleza kwa ulimi, kukatisha sentensi n.k.(Rubanza, 2003).
Utendaji (parole) ni kile asemacho mjua lugha katika muktadha wa mawasiliano ikiwa ni pamoja na makosa ya kiutendaji ya bahati mbaya na yale ya kukusudiwa. Vilevile tunaweza kusema ni udhihirikaji wa ujuzi wa lugha alionao mjua lugha.
Uamilifu au utumizi (functionalism) ni elimu inayohusu muundo wa lugha kwa kurejelea kazi zake za kijamii katika mawasiliano.
Inamchukulia mtu binafsi kama kiumbe-jamii na kuchunguza namna anavyojifunza lugha na kuitumia katika mawasiliano na wanajamii wenzake.
Urasmi
Urasmi (formalism) ni elimu ya maumbo dhahania ya lugha na mahusiano yake ya ndani. Huzingatia maumbo ya lugha kama uthibitisho wa kimalimwengu bila kuzingatia namna jamii inavyowasiliana.
Uelezi ni mtazamo ambao huelezea ukweli wa lugha jinsi ilivyo na inavyotumika na jamiilugha husika.
Na siyo namna inavyotakiwa kutumika. Isimu elezi haiweki kanuni ngumu au sheria ngumu zozote zinazotokana na mawazo ya mtu juu ya lugha fulani bali huelezea lugha kwa kuangalia namna lugha hiyo inavyojidhihirisha yenyewe.
Huelezea sheria na kanuni ambazo mzungumzaji mzawa ameziweka kichwani na zinazoakisi uwezo wake wa lugha. Kwa kifupi, haielezi wala kuagiza namna mtu anavyotakiwa kutumia lugha bali namna lugha ilivyo na inavyotumika na wamilisi wa lugha hiyo.
Kanuni za Usahihi
Uelekezi ni mtazamo unaojaribu kuweka kanuni za usahihi wa namna watu wanavyotakiwa kutumia lugha.
Katika misingi hii, lugha rasmi hutumika pakubwa tunapokuwa waangalifu zaidi katika mazungumzo yetu.
Kadri uangalifu unavyozidi kudhihirika katika mazungumzo fulani ndivyo yanavyopata nafasi kubwa zaidi kutambuliwa kuwa rasmi.
Mfumo rasmi wa lugha huzingatia matumizi ya mseto wa sentensi changamano na sahili zenye kuwasilisha maana kamilifu.
Kwa mujibu wa Joos (1961), lugha rasmi haina madakizo au mapambo na aghalabu inahusishwa na kujitambulisha kwa wageni. Hujiepusha na urudiaji isipokuwa tu pale ambapo msisitizo unahitajika. Katika kukwepa udondoshaji, lugha rasmi huzingatia kanuni zote za kisarufi na usahihi.
Lugha rasmi ni aina ya mawasiliano yanayotumika katika mazungumzo na maandishi yaliyo rasmi kama vile kwenye mazingira ya afisini, mahakamani, uwasilishaji wa maazimio, maagizo, miongozo, nyaraka muhimu za kiserikali, hati za idara mbalimbali, matangazo ya kisheria au makala ya kitaaluma.
Katika matumizi ya lugha hii, usahili na ukweli wa mambo yanayojadiliwa ni kigezo muhimu sana kuzingatiwa. Mfumo wa lugha unaotumika katika matini ya kisheria kwa mfano, ni ule unaosisitiza kabisa usahili wa lugha ili kujaribu kuzuia ufafanuzi unaogongana na sheria hizo.
Aidha, mawasiliano katika shughuli rasmi hayafanywi ovyo tu bila ya kufuata mpangilio maalum wa matukio. Badala yake, huzingatia mtiririko maalum unaokusudia kuleta ukamilifu wa maana.
Lugha huhusisha matumizi ya zana za kiisimu zinazofanana au kulingana katika kuelezea mambo. Mathalan, tuandikapo barua za kiafisi, aghalabu tunajikuta tukitumia ‘klishe’ zilezile zilizokwisha kushamiri katika mawasiliano mengi ya namna hii. Fomu za kujazwa na wahusika ni mfano mzuri zaidi.
Mazungumzo yoyote rasmi hupangwa kabla ya kuwasilishwa ili kuepuka uradidi na urejeshi mwingi. Ni mpangilio huu wa hali ya juu ndio unaoipa lugha hii jina lake.
Kuna matumizi ya istilahi maalum zinazohusu masuala ya afisini au kidiplomasia. Aidha, vyeo au nyadhifa za wahusika mbalimbali hutajwa. Huzingatia uwazi kwa kuepuka matumizi ya misimu, nahau, mafumbo au lahaja.
Kwa ujumla, lugha rasmi ni namna ya mawasiliano katika nyanja za utawala, uendeshaji wa uongozi na masuala ya kisheria.
Mawasiliano haya yanaweza kutekelezwa ama kwa njia ya maandishi au mazungumzo.
Matumizi ya viungo au miondoko ya mwili pia ni mbinu ya mawasiliano iliyo na viwango vyake vya urasmi.
Kwa mfano, katika mahojiano kwa minajili ya kutafuta ajira, matumizi fulani ya viungo vya mwili yanaweza kumdhihirisha msailiwa kama asiyependezwa na kazi hiyo, asiye mwaminifu, aliye na mtazamo hasi, asiye msikivu au aliye na wasiwasi au kiasi fulani cha aibu.