Mwandishi
Sephania Kyungu
Simu: 0756719643
Gmail: Sephaniakyungu1996@gmail.com
Iks UDSM 2019
@masshele swahili.
Iksiri
Katika makala hii tumeabili maana ya tafsiri, historia ya tafsiri hususani katika kazi za fasihi, pia tumeeleza maana ya ulinganishi au fasihi linganishi. Aidha, katika kiini cha makala hii tumechambua changamoto anuai ambazo zinawakumba wafasiri wa kazi za kibunifu pamoja na athari za kazi hizo zinazotafsiriwa katika uga wa fasihi linganishi.
1.0 Utangulizi
Tafsiri, Mwansoko (2015) anaeleza kwamba ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi lugha nyingine. Mwansoko (k.h.j) akimnukuu Catford (1965) anasema kuwa kutafsiri ni kuchukua mawazo yaliyo katika maandishi kutoka lugha moja (lugha chanzi) na kuweka badala yake mawazo yanayolingana kutoka lugha nyingine (lugha lengwa).
Anaendelea kueleza kuwa ili kufanikisha tafsiri ni lazima uzingatie mambo mawili ambayo ni: mawazo yanayoshughulikiwa ni sharti yawe katika maandishi na si vinginevyo, pia ujumbe/mawazo katika lugha chanzi na lugha lengwa sharti yalingane.
Kwa hakika hakuna tafsiri iliyosawa kabisa na matini lengwa ndiyo maana Catford akadai sharti yalingane na siyo mawazo sawa, hii inatokana na changamoto za kiisimu, mtindo, historia, utamaduni na tofauti ya semi na tamathali za semi. Changamoto hizi ndizo zilizochambuliwa katika kiini cha makala haya.
Kwa ujumla fasili ya Mwansoko (k.h.j) imeeleza mambo yote ambayo ni ya msingi katika fasili ya tafsiri.
1.1 Historia ya Tafsiri ya Fasihi
Mwansoko (2015) na Mshindo (2010) wanadai kuwa kumbukumbu zinaonyesha kwamba kutafsiri kulianzia zamani sana hata kabla ya Kristo. Wanaendelea kueleza kuwa sayansi na taaluma nyingi zilianzia Misri kwenye miaka ya 3000 na zaidi kabla ya kuzaliwa Kristo zilienea mataifa ya Ulaya kwa njia ya tafsiri kupitia kwa wataalamu wa Kiyunani. Wataalamu wa Ulaya walitafsiri kwa Kilatini vitabu kutoka kwenye ulimwengu wa Kiislamu vilivyokuwa vimetafsiriwa kwa Kiarabu kutoka kwa Wayunani na kuvipeleka kwao Ulaya na kuchota maarifa yaliyokuwamo ndani yake.
Wanaendelea kueleza kuwa kazi nyingi za kutafsiri ziliibuka karne ya 12 na kushika kasi karne ya 19 na 20. Katika karne iliyopita matini nyingi zilizotafsiriwa zilikuwa za kidini, fasihi, sayansi na falsafa.
Karne ya 20 inajulikana kama karne ya tafsiri kutokana na wimbi kubwa la tafsiri. Mwansoko (2015) anaeleza kuwa Hamziyya ni utenzi wa Kiarabu uliotungwa karne ya 13, anaendelea kwa kusema kuwa karne ya 19 Wamisionari walitafsiri vitabu vingi vya Kikristo kwa Kiswahili na baadhi ya lugha za makabila makubwa ya Tanzania.
Wakati wa ukoloni maandiko mengi ya fasihi ya Ulaya na Asia yalitafsiriwa kwa Kiswahili. Kwa mfano:
Hekaya za Abunuasi
Alfu – Lela – Ulela
Robinson Krusoe na Kisawe Chake
Baada ya uhuru wazalendo walichovya katika tafsiri. Kwa mfano Nyerere alitafsiri tamthiliya mbili ambazo ni Mabepari wa Venisi na Juliasi Kaisari.
1.2 Fasihi Linganishi
Kabla ya kufasili dhana ya fasihi linganishi ni vema tukaanza kwa kueleza dhana ya ulinganishaji. TUKI (2014) ulinganishaji ni kufanya tathimini ya vitu viwili au zaidi ili kujua ubora, kufanana na kutofautiana kwa vitu hivyo.
Hivyo, mlinganishaji anapotaka kufanya shughuli hii sharti awe na ujuzi wa vitu vilinganishwavyo, kuwepo kwa vitu viwili vinavyolinganishwa na kuwepo kwa kigezo au vigezo maalumu vya kulinganisha.
Aidha, fasihi linganishi Boldor (2003) akimrejelea Campbell (1926) anaeleza kuwa ni taaluma inayochunguza uhusiano uliopo baina ya fasihi mbili au zaidi nje ya mipaka ya kitaifa kwa njia ya kulinganisha mfanano na msigano. Kwa ujumla, tunaweza kusema kuwa fasihi linganishi ni taaluma inayojishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa uhusiano na usigano uliopo baina ya fasihi mbili au zaidi zinazohusisha vipengele tofauti vya kiutamaduni, itikadi, historia n.k.
2.0 Kiini
Katika sehemu hii tumeangazia changamoto zinazomkabili mfasiri wa matini za kifasihi na athari zake katika ulinganishaji. Katika sehemu hii tutaanza kwa kuangazia changamoto za kutafsiri matini za kifasihi.
2.1 Changamoto za Kiisimu
Massamba (2004) anadai kuwa isimu ni taaluma ya ufafanuzi, uchambuzi na uchunganuzi wa lugha kwa kutumia mbinu za kisayansi.
Anaendelea kueleza kwamba lugha zote duniani zina msingi wa kipekee katika vipengele vyake kiisimu (fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki) hutofautiana.
Hakuna lugha mbili au zaidi ambazo zina muundo unaofanana kiisimu. Mutie (1997) akimnukuu Newmark (1990) anasema kwamba matatizo yanayohusiana na tafsiri yatakwisha pale muumano wa kiisimu utakapowasilishwa katika nadharia ya tafsiri.
Kwa hiyo, kukosekana kwa muumano wa kiisimu kati ya lugha chanzi na lugha lengwa ndiyo unaosababisha changamoto katika kutafsiri matini za kifasihi. Mathalani, riwaya, tamthiliya na ushairi.
2.1.1 Changamoto y Leksia
Fekih (2018) anadai katika kiwango hiki, tunatazama maneno na msamiati iliyotumiwa na mwandishi wa matini chanzi na visawe vyake katika matini lengwa. Aidha, katika kiwango hiki cha leksia kuna changamoto za aina mbalimbali ambazo mara nyingi hujitokeza wakati wa kutafsiri matini za kifasihi, ambazo ni:
Matumizi ya visawe visivyo sahihi, changamoto hii inasababishwa na kutokuwepo na muumano mzuri katika lugha chanzi na lugha lengwa ama athari au upungufu wa mfasiri husika. Changamoto hii inajidhihirisha katika tafsiri ya Robinson Crusoe.
Kwa mfano:
Na.
Matini Chanzi
Ukurasa
Matini Lengwa
Tafsiri Sahihi
01.
Sand bar
6-8→16-19
Mwambani
Fungu la mchanga
02.
Mountainous waves
6→16
Mawimbi makubwa
Milima ya mawimbi
03.
Tossed
6→17
Likainua
Likarusha
04.
Thirty foot
6→17
Futi ishirini
Futi thelethini
05.
Good swimmer
6→18
Muogeleaji hodari
Muogeleaji mzuri
Chanzo cha tafsiri sahihi TUKI (2014)
Kwa ujumla, changamoto ya tafsiri katika kiwango cha leksia unajidhihirisha kuwepo kwa uteuzi mbaya wa visawe kutoka katika matini lengwa jambo ambalo huondoa uzuri wa kazi ya fasihi.
Matini za kifasihi zinafungamana sana na utamaduni hivyo, mfasiri anapaswa kuzingatia utamaduni wa jamii ya matini chanzi pia ubunifu wa msanii.
Matumizi ya kisawe kimoja katika maneno zaidi ya moja, hii ni changamoto nyingine katika kutafsiri kazi za fasihi.
Kwa mfano, katika tafsiri ya riwaya ya Robinson Crusoe kisawe kimoja kinatumika kurejelea leksia zaidi ya moja katika matini lengwa. Tatizo hilo linapotosha maana pia, huwafanya hadhira kutatanika katika kupata ujumbe uliokusudiwa.
Mathalani, neno land katika (Uk. 6) lilijitokeza mara mbili na kulitafsiri kwa maneno tofauti tafsiri moja “nchi kavu” (Uk. 17) na tafsiri ya pili “ufukoni” (Uk. 18).
Pia, neno land limejitokeza (Uk. 33) na mfasiri kalitafsiri kama “kisiwa” katika (Uk. 33).
Hivyo, matumizi ya kisawe kimoja kurejelea maneno zaidi ya moja katika matini inasababisha upotofu wa maana. Ikiwa kisawe kinarejelea maneno zaidi ya moja katika matini lengwa husababisha hadhira ishindwe kuelewa kisawe kipi ni sahihi na hata kushindwa kupata maana iliyokusudiwa.
Neno la jumla kulitafsiri kimahususi na neno mahususi kulitafsiri kimajumui, hii ni changamoto kubwa katika kutafsiri matini za kifasihi. Kwa mfano, katika Robinson Crusoe, mfasiri neno bonds katika (Uk. 62) mfasiri alitafsiri kama “kamba” (Uk. 66) wakati bonds linajumuisha kitu chochote ambacho kinatumia na kufungia kama vile “kamba”, “mnyororo”, “pingu” au “waya”. Aidha, neno mahususi hutafsiriwa kama neno majumui. Kwa mfano, neno crew (Uk. 51) mfasiri kalitafsiri kama “watu” (Uk. 49) wakati neno crew linarejelea wafanyakazi wa melini. Kwa maana hiyo, tafsiri iliyotolewa ni ya kiujumla kwani si kila mtu anaweza kuwa mfanyakazi wa meli lakini kila mfanyakazi wa meli huwa mtu.
Katika changamoto hizo hapo aidha husababishwa na kukosekana kwa kisawe katika matini lengwa au udhaifu wa mfasiri mwenyewe.
2.1.2 Changamoto za Kisintaksia
Feki (2018) anadai kuwa katika kiwango hiki kuna changamoto katika mjengeko wa tungo kati ya lugha chanzi kwenda lugha lengwa, hii inatokana na ukweli kwamba kila lugha ina mjengeko wake wa tungo.
Mathalani, katika Bwana Myombekere na Bi Bugonoka na Ntulanalwo na Bulhwali.
“…tena watoto wasipokuwapo husingizia kwa mbwa.” (Uk. 435)
“Siri isiyokuwemo na jamaa yako atashitukia kifo.”
Chanzo, Mwansoko (2015)
Bila shaka maneno yaliyoandikwa kwa hati ya italiki yanaleta mushkili katika muundo wa sentensi. Ingawa hatuna matini chanzi ya Kikerewe lakini tunaweza kubashiri kuwa maneno yaliyowekwa kwa hati ya italiki ama yanaweza kuondolewa kabisa au kubadilishwa maumbile endapo kungetumika sintaksia ya Kiswahili.
“…tena kama watoto hawapo, husingizia mbwa.”
“Siri isiyokuwemo jamaa yako atashitukia kifo.”
Chanzo, Mwansoko (2015)
Changamoto kama hizi katika kutafsiri matini za kifasihi zinatokana na athari za lugha ya kwanza ya mfasiri. Hii ni changamoto kubwa katika matini nyingi, si tu katika Bwana Myombekere na Bi Bugonoka na Ntulanalwo na Bulhwali bali hata kazi zingine mathalani, Robinson Crusoe.
Hii inatokana na ukweli kwamba hakuna umahiri mkamilifu katika lugha mbili.
2.1.3 Kiwango cha Semantiki
Semantiki ni kipengele cha kiisimu kinachochunguza maana katika lugha, kipengele hiki hutafiti maana za maneno katika tungo (Habwe na Karanja, 2004). Fakih (2018) anadai kwamba inapofanyika tafsiri ya matini chanzi kwenda matini lengwa huwa tunahawilisha maana na ujumbe uliokuwepo ndani katika matini chanzi kwenda matini lengwa. Kwa mfano, katika riwaya ya Robinson Crusoe.
Na.
Matini Chanzi
Matini Lengwa
Tafsiri Sahihi
01.
Sand bar
Mwambani
Fungu la mchanga
02.
Tassed
Likainua
Likarusha
03.
Thirty foot
Futi ishirini
Futi thelathini
04.
Dragged
Lilinichukua
Liliniburuta
05.
Jagged
Jabali kubwa
Jabali lenyeincha
Chanzo cha Tafsiri sahihi ni TUKI (2014)
Matokeo ya changamoto hii ni kupotosha maana na ujumbe wa matini chanzi na hata kuondoa ushikamani wa maana na ujumbe wa matini hizo.
2.2 Changamoto za Kiutamaduni
Utamaduni ni mkusanyiko wa mila na desturi za jamii inayotumia lugha moja mahususi kama njia ya mawasiliano (Newmark, 1988), kwa kuongezea zaidi Wanjala (2011) naye anasema kuwa zinatofautiana katika utamaduni na hili ni tatizo kwa mfasiri kuliko tofauti za kiisimu. Kwa mfano, katika riwaya ya Robinson Crusoe, changamoto za kiutamaduni zimejitokeza kwa kukosekana ulinganifu katika kiwango cha neno. Hali hii imetokana na matini lengwa imekosa usawa wa moja kwa moja kwa neno lililojitokeza katika matini chanzi. Hivyo, mfasiri hulazimika kuweka maneno yanayokidhi ujumbe katika mawasiliano kwa hadhira pokezi ijapokuwa maneno hayo siyo msamiati halisi iliyotumika katika matini chanzi.
Mfano 1:
Matini Chanzi
Matini Lengwa
Brandy
Mvinyo
Rum
Mvinyo
Wine
Mvinyo
Chanzo, Fakih (2018)
Tukichunguza katika kifani hicho hapo tunaona kwamba neno brandy, rum na wine ni aina ya pombe ambazo zinapatikana katika utamaduni wa lugha chanzi kwa vile katika utamaduni wa jamii ya lugha pokezi hakuna aina hiyo ya pombe kama hizo husababisha mfasiri kuzipa kisawe cha aina moja, ambacho ni “mvinyo”. Changamoto hii inaikumba kazi nyingi za tafsiri hususani zile fasihi kwani hufungamana sana na utamaduni.
Mfano 2: Song of Lawino – Wimbo wa Lawino
Majina ya mimea: Lugoro, Ober, Lyamo, Ocuga, Omar, Lakara n.k.
Majina ya ngoma: Otele, Moko, Ogodo, Bwola, Orok, Lacucuka n.k.
Majina ya majira: Ager, Pato, Kot, Ondunge n.k.
Mavazi maalumu: Odiye, Lacomi n.k.
Hata mwandishi aliyaacha hivyo katika katibu cha Song of Lawino ingawa kitabu hicho alikitafsiri yeye mwenyewe kutoka katika lugha ya Kiacholi ambayo ndiyo aliyokuwa ametumia kwanza. Maneno hayo yalishindwa kutafsiriwa kwenda lugha nyingine kutokana na ufungamano wa moja kwa moja na kabila la Waacholi.
Chanzo, Mtesigwa (2015)
2.3 Changamoto ya Mtindo
Masoko (2015) mtindo ni changamoto kubwa katika tafsiri, anasema mtindo ndiyo unatia uhai, utamu wa hadithi, hii pia si kavu ina ukwasi mwingi wa tamathali za semi. Kwa mfano, katika riwaya ya Bwana Myombekere na Bi Bugonoka na Ntulanalwo na Bulhwali.
“Njoo ukale na mgeni, apate kula vizuri, sababu ugali wa kula pekee yako, kama umezao kula pamoja na wengine, huwezi kushiba vizuri, hapana.” (Uk. 221)
“…hakuweza tena kuzidi kutamani kuwa na maisha mendi hivyo duniani hapana.” (Uk. 590)
Katika mifano hiyo hapo, ingawa tunaweza kusema kuwa mbinu hii inasisitiza ukiushi, lakini pia ni tabia ya Kikerewe kuwa na vikanushi katika sentensi. Hali hii imehifadhi uasili wa matini chanzi na kupuuza mtindo wa matini lengwa ambayo ni ya Kiswahili.
2.4 Changamoto za Misemo, Nahau, Methali na Vitendawili
Mwansoko (2015) kwa kawaida misemo au tamathali za semi, nahau, methali na vitendawili husukwa kwa kutumiwa kwa kufungamana sana na utamaduni wa watu fulani. Anaendelea kueleza kuwa uchoraji wa dhana zinazowakilishwa na mafungu haya ya maneno siyo tu hufanywa kwa usanii wa hali ya juu bali pia mila, desturi, imani, historia, mazingira na falsafa ya watumiaji wa lugha wanaohusika. Hali hii husababisha changamoto kubwa kwa mfasiri pindi anapotaka kufanya kazi yake.
Kwa mfano:
Nahau
Kata mbuga.
Mkono wa birika.
Kuongea kwa herufi kubwa.
Methali
Mpanda ngazi hushuka.
Haraka haraka haina baraka.
Nazi mbovu ni harabu ya nzima.
Vitendawili
Mzungu wangu daima hubebwa na watumishi 4.
Wazungu wawili wanachungulia dirishani.
Kuku wangu anatagia mibani.
Tamathali za Semi
Ujana ni maji ya moto (sitiari)
Kwa mujibu wa Kihore (1991) anaeleza kwamba mafungu haya yana changamoto mbili. Changamoto ya kwanza ni kupatikana kwa visawe vyake kimuundo vya mafungu kama haya katika matini lengwa na kupatikana kwa visawe mwafaka vya dhana au maana yake katika lugha lengwa. Aidha, Mwansoko (2015) anajaribu kueleza namna ya kutanzua changamoto hii ambapo anadai kuwa mfasiri hana budi kutafuta misemo yenye maana zinazokaribiana na zile zilizomo katika matini chanzi bila kuzingatia muundo wake. Hii inatokana na ukweli kwamba katika tafsiri kitu kinachoangaliwa sana ni maana na si muundo.
3.0 Athari za Tafsiri katika Ulinganishaji
Katika sehemu hii tutaangazia athari za tafsiri katika ulinganishi, hususani katika uga wa fasihi.
3.1 Tafsiri Imesaidia katika Kuibuka kwa Nadharia ya Fasihi Linganishi
Ponera (2014) anaeleza kuwa lengo la nadharia ya fasihi linganishi ni kuchunguza na kufanana na kutofautiana kwa kazi ya fasihi ya Tanzania na kazi za mataifa mengine hasa Amerika na Ulaya hususani katika vipengele mbalimbali hasa vya kiutamaduni pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kwa hiyo, kutokana na maelezo hayo ni wazi kuwepo kwa kazi nyingi za mataifa ya nje zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili na zile ambazo hazijatafsiriwa, ni sababu tosha ya kuanzisha nadharia hii mpya ya fasihi linganishi. Mfano wa kazi zilizotafsiriwa ni:
Mkaguzi wa Serikali
Mkaguzi Mkuu wa Serikali
Mfalme Edipode
3.2 Tafsiri Inaathiri katika Ulinganisho wa Utamaduni
Newmark (1988) anaeleza kuwa utamaduni ni mkusanyiko wa mila na desturi za jamii moja inayotumia lugha moja mahususi kama njia ya mawasiliano. Tafsiri inaathiri katika ulinganishaji kwani inatusaidia kufanya ulinganishi kati ya jamii/taifa au bara katika kipengele cha utamaduni. Kwa mfano:
Song of Lawino - Wimbo wa Lawino
Majina ya Mimea:
Logoro, Ober, Lyanno, Ocuga, Labwor Omar, Lakura n.k
Majina ya Ngoma:
Otole, Moko, Ogodo, Bwola, Orak, Lacucuku n.k.
Vyeo vya Watu, Miungu:
Odure, Agik, Alyker, Ojebu, Nyandyang n.k.
Chanzo, Mtesigwa (2015)
Katika kifani hicho, tunaona mfasiri ameshindwa kufasiri maneno hayo ambayo ni ya utamaduni wa Kiacholi kwenda Kiswahili, hii inatupa ushahidi kuwa utamaduni wa Kiacholi na Kiswahili haufanani.
3.3 Tafsiri Imesababisha Kuongezeka kwa Kazi za Fasihi kwa Kiswahili
Mulokozi (2017) anaeleza kwamba fasihi kwa Kiswahili ni fasihi iliyotafsiriwa kutoka taifa lingine. Tafsiri imesaidia kuibuka kwa kazi za fasihi kwa Kiswahili ambazo kwa hakika zimesaidia sana kuongezeka kwa tafiti za fasihi linganishi. Kwa mfano, utafiti wa Fekih (2018) na Serem (2018).
3.4 Tafsiri Imesaidia Kuenea kwa Fasihi ya Kiswahili Ulimwenguni
Tafsiri imesababisha kuenea kwa fasihi ya kiswahili ulimwenguni kwa mfano Kasri ya Mwinyi Fuadi Dei Sklaverei de Gewiize. Kazi nyingine kama vile Uhuru wa Watumwa kwenda Kiingereza, Rose Mistika, Bwana Myombekere na Bi Bugonoka na Ntulanalwo na Bulhwali. Hizi ni baadhi ya kazi zilizotafsiriwa kwenda mataifa mengine, hivyo na kusaidia kukuza shughuli ya ulinganishaji katika uga wa fasihi.
4.0 Hitimisho
Ulinganishi ambao kwa kiasi kikubwa unategemea taaluma ya tafsiri pia una athari hasi kubwa hususani kwa lugha lengwa na kwa utamaduni wa lugha lengwa. Kwa mfano, baadhi ya tabia ambazo ni za asili ya Kiafrika au utamaduni wa Mwafrika leo haupo tena kama zamani. Hii ni kutokana na athari za kazi zilizotafsiriwa kusomwa na watu wengi na kuona kama utamaduni huo ndiyo faafu kwao kuliko tamaduni zao za awali.
MAREJELEO
Fekih, A. H. (2018). “Changamoto za Kutafsiri Riwaya: Mifano kutoka Tafsiri ya Riwaya ya Robinson Crusoe” Tasnifu ya Uzamili: Chuo Kikuu Huria. (Haijachapishwa)
Habwe, J. na Karanja, P. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.
Kihore, Y. M. (1991). “Miundo ya Kisarufi Katika Tafsiri: Matatizo na Utatuzi” Makala Yaliyotolewa Katika Semina ya Mafunzo kwa Wafasiri wa Kiswahili. Dar es Salaam 16 – 21.
Massamba, D. P. B. (2004). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI.
Mshindo, H. B. (2010). Kutafsiri na Tafsiri. Zanzibar: Chuo Kikuu cha Zanzibar.
Mulokozi, M. M. (2017). Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili: Kozi za Fasihi Vyuoni na Vyuo Vikuu. Dar es Salaam. KAUTTU.
Mutie, E. K. (1997). Sanaa katika Tafsiri: Matatizo na Athari Zake. Tasnifu ya Shahada ya Umahiri: Chuo Kikuu cha Nairobi.
Mwansoko, H. J. M. na Wenzake (2015). Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu. Dar es Salaam: TUKI.
Newmark, P. (1988). A Text of Translation. London: Prentice Hall.
Ponera, A. S. (2014). Utangulizi wa Fasihi Linganishi. Dar es Salaam: Karljamer Print Technology.
Serem, S. P. (2018). “Uhakiki Linganishi wa Fani katika Tasnifu Mintarafu ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (Mwakusaka, 1979) na Mkaguzi wa Serikali (Madumulla, 1999).” Tasnifu ya Uzamivu: Chuo Kikuu cha Moi. (Haijachapishwa).
TUKI (2014). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaamu: TUKI.
Wanjala, S. F. ((2011). Misingi ya Ukalimani na Tafsiri. Serengeti: Serengeti Educational Publish.
Masshele/kiswahili
|