|
NADHARIYA ZA UHAKIKI WA FASIHI YA KISWAHILI (PROF. T.S.Y. SENGO)
Nadhariya za fasihi
Nadhariya ya Nadhariya
Kwa mujibu wa Sengo, nadhariya ni….Wazo kuu,fikira kuu,mwongozo mkuu….wa mtu au watu (jamii), wa pahala fulani,wakati fulani, kwa sababu fulani.
Tunamtaka MWAAFRIKA ajisimamishe, ajiamini, ajiendeshe, aache mchezo, asikubali kuwa mume haramu, mke haramu, mtumwa, kijakazi…..wa mtu fulani kwa jina la uhisani, ufadhili, uwekezaji mgeni, tajiri, mume wa waume, jike la wake, n.k. Hayo maoni hatuyataki. Hii inaweza kusemwa ni NADHARIYA au ni FALSAFA.
- Nadhariya ya Mtu – Utu
Kwa Afrika na mwaafrika, utu ndicho kitambulishi cha uungwana, ustaarabu,hekima,busara,fikra,mawazo na hadhari za mtu. Ujenzi wa wahusika katika kazi za ubunifu, maudhuwi ya kazi hizo hupewa kipaumbele na umuhimu hasa katika ujumbe na falsafa nzima ya kazi hiyo. Mtu – kwao. Tukisema Afrika, ndilo bara letu. Mengine yapo na watu wa huko, wana yao. Kimsingi utu unatakiwa uwe mmoja. Tafauti ni za kihulka, kitabiya na kimazingira. Kwa nadhariya hii Sengo anasisitiza kujali utu katika utunzi na uhakiki wa kazi za fasihi. Mtunzi hana budi kuwajali waAfrika na kuzijali jadi za muAfrika katika utunzi na kinyume chake ni kutojali utu wa muAfrika.
- Mtu – Kwao, Ukwao wa Mtu, Asokwao…..
Ni nadhariya inayompima mtu kwa asili ya kizazi chake, kuzaliwa na kulelewa kwake,mbeko zake kwa watu wengine – wakubwa kwa wadogo. Mtu – kwao; mtu na wazazi wake,mtu na asili yake,mtu na ukoo wake,mtu na kabila lake,mtu na mazingira yake,mtu na taifa lake. Mtu na hisiya ya kuzaliwa na kulelewa kwake,kufanyiwa na kushukura kwake. Aso – kwao ni yule asiye kisogo,aso macho na uwezo wa kukisoma kisogo na kuyaona mengi alokwishafanyiwa kabla na watu mbalimbali. Mtovu wa utu na shukurani. Kila mtu ana asili yake na hiyo sharti iwe chimbuko hasa la fasihi yake, mtunzi anayeshabikiya ya nje na kuacha ya ndani ni sawa na msaliti wa jamii yake.
- Taalimu ina kwao,Utamaduni una kwao,fasihi ina kwao;
Taalimu ina kwao; Taalimu ni kweli. Kweli ni dhanna. Kweli ni sifa. Kweli ya kitaalimu hupatikana kwa utafiti. Utafiti hufanywa na watu. Kila kweli ina asili na wakati wake na mazingira yake kwa kila jamii. Taalimu ya kiungwana kwao ni kwa waungwana,hawezi kuja mgeni na kumfunza mwenyeji kweli batili isiyoendana na wenyeji na hata hao wenyeji wakijifunza hayo ya wageni iwe ni kwa kuwajuwa tu hao wageni lakini sio kujifunza na kuyaona bora kuliko yao.
Utamaduni una kwao; mwanataalimu akutanapo na nadhariya yoyote, hasi, chanya, chapwa, sharti aitafutiye KWAO. Utamaduni wa jamii ya watu ni utambulishi wa jamii hiyo. Jamii ina eneo la kijiografiya katika ardhi. Watu wake wana mapisi marefu katika eneo hilo. Na kila jamii ni jamii ya mchanganyiko, tangu hapo hadi leo. Si jambo la Kihore atokaye Maragori tena ya Kenya au Okenyo wa Kisumu au Kakaibagarura wa Kiziba kuamuwa kuwa watoto wake sasa wamekuwa Wachina, Wajapani, Wangoni ati kwa kuwa wamezaliwa na kusema Kichina,Kijapani au Kingoni. Utamaduni wa watu na utambuzi wao si lugha tu kama sivyo mmbwa wote wa Waingereza wangekuwa Waingereza. Mchaga hawezi kuwa Mhaya kwa kuweza tu kusema Kihaya. Hivyo, jiografiya, mapisi(historiya), damu (biolojia), jadi, utamaduni, mila, desturi, ada, lugha, kawaida, mazoweya, mavazi na sanaa kwa ujumla ndio humpa mtu u UKWAO.
Fasihi ina kwao
Ili mtu aielewe fasihi simulizi ya jamii yoyote sharti akujuwe jamii hiyo inakoishi, utamaduni wao, mila na ada zao, lugha yao, n.k. fasihi ya Kiswahili kwao ni Uswahilini, Pwani ya Afrika Mashariki. Jiografiya ya Jumuiya ya Waswahili inaanziya Kismayu hadi Pemba asili ya Msumbiji kaskazini na visiwa vya Kilwa, Mafia, Unguja, Tumbatu, Pemba ya leo, Mombasa au Mvita, Lamu na Pate hadi visiwa vya Ngazija/Comoro.
Waswahili wana jadi zao katika viambo vyao, makaazi yao, vijiji vyao, miji yao, n.k. Wapare kama Wachaga wapo hawapo, pale uendapo kwao ukimtafuta Mchaga huambiwa huyu Mrombo, yule Mmachame, yule Mkibosho, Mmarangu, Muhimo, Msanyajuu, n.k. Kadhalika Mmakanya, Msangi na Nathaeli Mmbaga mwenye kikabila chake ndani ya Upare. Hivyo, jadi, Sanaa, kazi, mila, desturi, lugha na kawaida zina kwao, kila jamii ina zao na hakuna moja iliyo bora dhidi ya yenziye.
Vielezeya vya fasihi ya jamii yoyote ile ni:
(i) Jamii; kwao fasihi ni jamiini
(ii) Taalimu maalumu; fasihi ni taalimu kama zilizvyo taalimu nyingine kama uhandisi na udaktari
(iii) Taalimu ya maneno mateule; maneno ya ishara za jamii, maneno kama pombe, nguruwe, kanisa, kimada, hawara…… hayatajwi kwa fakhari Uswahilini, hasa katika maeneo ya kina Sheikh.
(iv) Ujumi wa jamii ambamo ndimo baharini mchotwamo ubunifu na upambifu wa hali na majambo.
(v) Ubunifu
(vi) Sanaa – usanii
(vii) Umbuji na umahiri wa lugha na wa uwezo wa kuyatumiya maneno kisawasawa.
(viii) Mvuto wa kusomeka
(ix) Mafumbo tata au tatanishi
(x) Semi za ndani na semi za barabarani
(xi) Maneno mateule (kwa mukhtasari, fasihi ina mambo matatu muhimu na yasemwayo, na tamu/ladha ya ujumi wa baina ya hayo mawili. Fasihi ilizayo Ujerumani yaweza kuchekesha sana Afrika. Ukwao wa jamii ndiyo bahari ya fasihi na fasihi ya jamii ndiyo mvuwa za mchomo, vuli, za mbaazi, na za masika za kuineemesha jamii kiutamaduni na kimaisha. Mtu kwao. Watu na yao. Na haya yote huanza na wale waliomzaa, pale alipozaliwa kwa asili ya uzazi wa damu yake.
- Nadhariya ya Ndani – Nnje
Mtafiti, mwalimu au mhakiki wa fasihi ya jamii fulani, ili aweze kuitafiti, kuifundisha au kuihakiki ni shuruti aimanye vizuri. Kuijuwa fasihi ya watu ni muhimu kwanza kuwajuwa wenyewe, utamaduni wao, mila zao, ada na desturi zao, bahari yao ambayo ndiyo chemchem ya ishara na dhanna zao. Ndani ni ndani. Mambo ya jamii sharti yazingatiye kweli za ndani za jambo. Mvaa suti ya kung’aa na ndani ana gagulo, hajavaa, sawa na mtu alofunga kilemba cha mita kumi na tano lakini ndani mwa uvaaji, maboga na muhogo vyaonekana ndani ya mawingu na kitumbuwa cha wavaaji viyoo viko ndani ya barafu ya sharubati, vyengine viko juu ya paji la uso au utosini mwa mtembezaji.
Utamaduni wa vyakula, mavazi, uwadilifu, imani ya dini, ucha – mungu, ujenzi, n.k. ni moja kati ya vitu vya ndani vya fasihi ya jamii ya watu fulani. Si kwa fasihi tu bali kwa mambo mengi yanayofahamika, vizuri zaidi kwa nadhariya ya ndani nnje.
- Nadhariya ya Ukhalisiya
Penye ukame, huzungumzwa njaa, kutopatikana kwa maji na taabu za kukosa vitu fulani fulani.Hayazungumzwi mafuriko ya kawaida. Penye kiliyo, ni nadra sana kuchezwa ngoma ila kwa Jaluwo ndiyo jadi yao kuliya kwa ulevi na dansa la rumba au samba, bampingi au shekisheki. Penye ndowa na harusi, hapachurwi kwa wanga kuanguwa kiliyo. Mradi hali halisi ya pahala au ya jambo huwa ndiyo msingi wa matukiyo au hali fulani. Halipo la kupitwa na wakati, hakuna fikira au mawazo potofu (kuna fikira au mawazo tafauti).
Ukhalisiya wa kiuchumi, hali, wingi wa kina mama dhidi ya kina baba, ukhalisiya binafsi wa utu, wa hulka na tabiya, wa kuzaliwa huo ndio humuongoza mtu katika utunzi wa kazi yake ya fasihi.
Ukhalisiya wa miktadha na mandhari ya kazi ya fasihi umejikita katika kweli zote ziihusuzo kazi hiyo.
Ukhalisiya wa kutumia lugha ya watu kufundishiya yao – leo CIVICS – URAIYA kufundishwa kwa lugha ya kigeni hali wafundishwao hawaijuwi lugha hiyo ya kigeni, hapo hapana ukhalisiya bali kuua uzalendo wa watoto hao kwa kuwalazimishiya lugha isiyo kujifunza yao. Ukhalisiya ni NADHARIYA pana na kubwa. Isipelekwe Ulaya wala Marikani, isomwe viamboni, vijijini, mitaani na itumike kwa upana wake.
- Nadhariya ya Kiislamu
Nadhariya hii inajikita katika kuelekeza watunzi na wahakiki wa kazi za fasihi kutunga na kuhakiki kwa kuzingatiya mafundisho na makatazo ya dini ya Kiislamu. Prof. Sengo katika nadhariya hii anasema; ….. Msanii, mbunifu, mwandishi, mtunzi, mhakiki mtumiyaji wa nadhariya hii ya Kiislamu, anatakiwa ashike adabu zake, afyate mkiya wake, akiri miya fil-miya kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muumba na mwendeshaji mmoja tu wa yote na vyote. Akibuni hubuni kutokana na uumbizi wa Allah. Kama ni riwaya, isiwe na ufuska wala mashizi katika starehe za muktadhani wala katika dhanna ya maendeleo kuwamo makasino, mabaa, madansa, madawa yoyote ya kulevya n.k. Kulewa, kuiba, kuzini, kufanya ujasusi, ufisidi, dhuluma n.k. yakiwemo iwe ni katika sababu za mtu kuadhibiwa kwa kufanya mambo hayo na isiwe kuyashabikia. Hii si nadhariya ya kubabaishia maisha bali ni ya uhakika wa maisha ya kivuli, ya duniani nay a ukweli wa maisha ya kudumu Peponi au Motoni.
- Nadhariya ya Utambulishi
Fasihi inatambulisha sanaa za jadi za utamaduni wa jamii. Kila fasihi ina kwao. Hivyo utambulishi wa utamaduni – bahari ya fasihi – na fasihi-mvuwa imwagayo maji baharini, hutambulikana kama mzingiro mzima wa mila na desturi, ada na kawaida, ujenzi na ukaazi, utoto na usheza, nyago na nyagizi, jando, ngoma, starehe na pumbazi, ndowa na harusi, mavazi na hisiya, mapambo na pambizi, kupika, kupakuwa, kuandika chakula na kukila, kazi na ndima za kigosi, safari za anga, maji, ardhini, usiku, mchana na za kuruka kwa nyungo na mitungi. Nadhariya hii inatufundisha juu ya dhanna ya watu kwa yao. Kila watu ni watu kwao. Jamii zikishatambuu haya, sharti na zenyewe zibakiye hai kama jamii.
- Nadhariya ya kimaudhuwi/kidhamira
Hii ni nadhariya kongwe sana na imetumiwa pia na wahakiki wakongwe kama Sengo na Kiango.
Sengo, anasema…Dhamira si dhamiri. Kwa hiyo msomaji asisome maneno ya mtunzi au mwandishi yanayoazimiya kadhaa nay eye akayachukuliya kuwa yaliyomo ni kadha wa kadha kutokana na hiyo kadhaa. Dhamira ni sehemu ya maudhuwi na maudhuwi ni yale yasemwayo na maandishi ya kazi ya fasihi. Dhamira ya mtunzi ya asili yaweza kuwa ni mgogoro wa wanandowa; maandishi yakatowa dhamira kadhaa juu ya kugongana wenyewe kwa wenyewe. Baada ya neno na neno, katikati, ndani na nnje ya maneno, mishororo, huwa mwapatikana visa na mikasa ya ajabu!
Aghalabu,mhusika mkuu, hubeba dhamira kuu na tajribu imetupa walimu fursa ya kumpima mtunzi au mwandishi kwa hayo yenye uzito kuwa ni yake yeye na huyo msemaji mkuu ni mwakilishi wake. Kuna kazi ambazo humpa nafasi huyo mtu aitwaye, “mpumbavu” kusemasema ya kipumbavu, kumbe hayo ndiyo kweli aliyoikusudiya mbunifu ama yale yanayodhihirika na ubunifu wenyewe.
Nadhariya hii ni kuu, nzito na muhimu sana. Kazi ya fasihi isipokuwa na yale mazito yasemwayo, huwa si kazi ya kuzingatiwa. Ama yawayo yawe kama maji ya mawaga au manyunyu yasiyojaza hata kikombe, hayo si maji ya mvuwa ya kifasihi inayoweza kukabidhiwa kokwa ardhini ikainywesha, ikaishibisha, ikaifungisha hadi kuifungulisha, ikaota, ikameya, ikachipuwa na kukuwa. Kwa wafanyao mitihani, ni swali la lazima kwa kila kitabu, kwa kila mtihani; wimbo unasema nini, riwaya yambaje, natiki inaeleza nini n.k.
- Nadhariya ya fani
Kazi ya fasihi inasema nini, lipi, yepi, mwenziwe ni kazi hiyo ya fasihi yambaje, yasema vipi, kwa namna, mbinu, mtindo, lugha …. ipi? Duniya kusemwa ni ni jifa, mti mkavu, duniya, hadaa, nazi ama yai, na maisha ya mja kusemwa si lolote, si chochote, moto mkali, mtihani, hidaya, tunu, balaa….. Ni katika kupambika kwa fani ya usemaji. Uhodari wa kuitumiya lugha katika maandishi kunategemeya umahiri na umbuji wa hiyo lugha inayotumika. Fani ya lugha humudiwa na wenye lugha yao, ukitaka kukijuwa Kiswahili sharti uwajiye wenyewe Wapwani, ama kwa usuhuba ama kwa utafiti.
Tamathali za usemi kama zilivyoainishwa, sitiari, tashbiha, tashihisi, kejeli, vijembe…… n.k zinatokana na mtu kukuliya katika utamaduni wa viambo/mitaa ya lugha. Kiswahili kipana. Pemba kuna utajiri mwingi wa lugha ya Kiswahili ambao unauhitaji watafiti wa lugha kwenda kuufanyiziya kazi. Lugha ya sawasawa ikimkaa mtu, hasiti kuzimudu beti za kila bahari za arudhi ya Kiswahili asiliya, insha kabila zote, baruwa za kuliwaza na kupoza, posa pamoja na tungo aina aina za kila utanzu na vijitanzu – hakuna la kipera wala kapera. Kiswahili hakijashindwa wala hakishindwi ila kwa wanaotaka kukifisidi.
- Nadhariya ya Dhima (Role) na kazi (Function)
Dhima ni wajibu. Kinyume chake ni jukumu, dhima ni kufanya lile litakiwalo. Dhima yamdai mtu kutimiza wajibu kwa jamii yake. suala la dhima si suala la orodha. Kuwa fasihi inafundisha, inaleya, inaonya, inaadibu, inaelekeza …. suala ni kwa vipi haya yanafanyika na kazi za fasihi zenyewe tafauti na kuonywa mtoto kwa kofi au fimbo? Utanzu wa ushairi kama vile wimbo au nyimbo, unaposemwa unafundisha, basi hufanya kazi zake hivi;
Wimbo Unaofundisha
Mwanangu kuwa usome,upende ujitahidi
Upate kazi uchume,ulipe na hizo kodi
Uzae wana utume,haya usiyakaidi
(TSYMS – ZNZ 18/04/08)
Unaleya
Mume wangu nakuomba,unisamehe ya jana
Mimi kwako ni mtamba,fahali ni lako jina
Kuleya ndowa ni kwamba,huba kusikilizana
Shairi linaloadibu
Unajiita katibu,Mtendaji wa Baraza
Kazi yako kuratibu,si mambo kujazajaza
Yafaa ujitanibu,acha watu kubamiza
U mtu wa bezabeza,wizara yakuadhibu
Utenzi unaoelekeza
Bi Fulani wanipenda
Kama kokwa kuipenda
Ama kisamvu kufunda
Kwanza kaa ufikiri
Nami piya nakuwaza
Moyoni wanikwaruza
Machoni wanipendeza
Hili jambo nalikiri
Tazama umri wangu
Mashavu na mvi zangu
Si mbali usoni kwangu
Kukuowa si vizuri
Ni huruma kukutoka
Edani nije kuweka
Mpweke utapwekeka
Hilo nahisi khattari
Likiwa ni la Qahari
Mwenyewe Akikhiyari
Nafsi inasubiri
Kwa ndowa iso fakhari
(TSYMS – SUZA 18/04/08)
Kama ni hadithi fupi, insha au riwaya, natiki ama utungo wowote basi kudondowa maneno, aya moja au mbili, huyafupisha yasemwayo lakini kwa ushahidi wa kazi zenyewe za fasihi kuthibitisha la Mussa la Mussa, la Issa la Issa na la Firauni la Firauni. Tukisema tu, fasihi inafundisha, kila somo lafanya hivyo, mapisi yanafundisha, elimunafsi au ushunuzi unafundisha, sayansi ama ulimbe unafundisha na asofunzwa na mamiye, hufundishwa na ulimwengu. Kinafundishwa nini? Kinafundishwa vipi?
Kazi ni kazi. Si kazi ya fasihi kuubadili Ulimwengu. Kazi ya fasihi kama dhima ni kuyaweka mambo uwanjani, Wachina wataelezeka uchina wao kwa kichina chao kwa ile fasihi yao hasa, na kwa lugha nyengine yoyote kwa manufaa ya hao wenye lugha hiyo kuwasoma na kupata fununu ya Wachina walivyo.
Kazi ya fasihi kilugha ni kumshawishi atakae kupata umahiri na umbuji wa lugha. Kamwe, fasihi haimfundishi mtu asiyetaka, lugha yoyote. Kama dhanna ya kazi ina nguvu, Afrika ndipo pahala pake. Hivyo ni juu ya walimu wa fasihi kutumiya mbinu mpya kushadidiya kwamba kila kifaacho katika fasihi, kwa manufaa ya jamii kitumiwe ili jamii nzima ijifunze kukitumiya. Kazi mojawapo ya fasihi, kwa kupitiya ubunifu ni kuwahamasisha na kuwahimiza wanafunzi watokezee kuwa watunzi na waandishi bora zaidi kuliko wa huko nyuma kwa vile wana wana vigezo, vyanzo na nyenzo zifaazo zaidi kuliko za zama za utangulizi.
- Nadhariya ya Ushunuzi, Kero la Moyo, Hisiya za
Nafsi
Ili mtu apate ahuweni wa lile limkeralo, hapati pumbao wala pumuo, ila atowe pumzi zake kwa kutunga kitu-kiwe “kishada”, cha lulu na marijani, nudhumu, beti mbili tatu n.k. Mwalimu naye asomeshaye fasihi, na mwalimu wake mhakiki wa kazi za fasihi, raha yao ni kuyapa maneno fasili zao zinazotokana na ushunuzi nafsiya, kero za nyoyo au mioyo yao na vile wanavyojihisi. Mbinu hii ya hisiya, ndiyo iliyowatia kortini kina Sengo au Kiango (1973), kwa kudaiwa kutokana na HISI ZETU ati walisema FASIHI NI HISI. Hisiya za kila mtu ni maumbile ya kila mja. Mhakiki hamalizi kila kitu anapohakiki kazi ya fasihi. Pale anapoishiya yeye ndipo mwisho wa tamu na chungu yake, mwisho wa hisiya zake, hana tena. Hali hiyo isiwe sababu ya kumkwaza mhakiki wa pili na wa tatu, kufanya yao kwa uwezo wao. Waliokuja “kulima” wenzao, “kuwaponda”, karibu wote walikuwa wasungo wa lugha na fasihi, kisha ni mabega, hayakufika yakavikiuka vichwa; ni nazi, zilizojipiga mabweni, zilijipasuwa zenyewe.
Hisiya ni mbinu ya kiungwana, wasomi, wahakiki, waachiwe kazi, kwa kutaka ama bila ya kutaka, kwa kuweza ama bila ya kuweza; kila mmoja afanye anachotaka, anachoweza, kulingana na vionjo vyake na vile vilivyomzaa na kumleya.
- Nadhariya ya Kiujumi
Kwa miyaka mingi, wanafasihi wa Uswahilini na wale wa fasihi kwa lugha ya Kiswahili, wamezowezwa kuzisoma kazi za fasihi kwa (i) kutazama maudhuwi-dhamira kuu na dhamira ndogo ndogo (ii) kutazama fani-lugha, mitindo mbalimbali, tamathali mbalimbali,miundo n.k. Nadhariya hii inatuelekeza tuanze kuzamiya mbizi ujumi-kwa maana ya ladha-tamu au chungu-ya kazi ya fasihi. Kuitazama kazi nzima na jinsi inavyomvutia msomaji kuisoma si mara moja wala mbili bali kila akimaliza, hupenda aisome tena na tena. Uhodari wa kubuni kitu au jambo hadi kikaonekana kwa macho au kikatamanika na ulimi, puwa na kuchekewa au kuliliwa na moyo, macho na kuhisika kwa hisiya zote hadi mkono au mguu ukatamani kugusa, huu ndiyo ubunifu wa kiujumi.
Mfano wa swali:
Bila kanuni fasihi isingekuwa na tanzu zinazofahamika. Ijadili kauli hii huku ukitoa mifano toka riwaya au tamthiliya zozote ulizosoma.
JIBU:
Ni kweli kwamba kazi yoyote ya fasihi isingeweza kutambulika tanzu zake na wala kuainishika kirahisi. Katika fasihi kanuni zinazotawala ni zile za kinadharia ambazo humuwezesha mtunzi au msomaji kubaini na kubainisha kazi ya fasihi iliyo mbele yake. Kwa minajili ya swali hili nitatalii mojawapo ya fasihi andishi kama ifuatavyo.
Kanuni ya maudhui, kwa kuzingatia maudhui yanayojitokeza katika riwaya tunaweza kuzigawa riwaya katika tanzu mbili ambazo ni riwaya dhati na riwaya pendwa.
Riwaya dhati ni zile zote ambazo maudhui yake huegemea kwenye kuifanya jamii iwe bora zaidi kimaudhui, kimaadili, kisiasa, kiuchumi na kifikra. Mifano ya riwaya dhati ni kama vile “ Wasifu wa Siti Binti Saad,” “ Vuta N’kuvute,” “ Kufikirika,” na “ Zawadi ya Ushindi”
Riwaya pendwa ni zile ambazo maudhui yake huegemea kwenye masuala ya mapenzi,ujasusi,upelelezi na ujambazi. Ni riwaya ambazo hazina mchango katika kulinda na kutetea maadili ya jamii zaidi sana zinalenga kupata pesa, mifano ya riwaya pendwa ni kama vile, Mzimu wa Watu wa Kale, Simu ya Kifo, Tutarudi na Roho Zetu, Machozi Jasho na Damu, Mkimbizi, n.k
Kanuni ya ukweli ni kanuni inayododosa ukweli kuhusu maisha ya wanadamu na jinsi anavyoyakabili mazingira yanayomzunguka kwa kigezo hicho tunapata riwaya za Ksaikolojia ambazo huwa zinasawiri maisha ya jamii. Riwaya hizi hutumia wahusika kuonesha jinsi mwanadamu anavyokabiliana na mazingira yake na kuyashinda au kushindwa na anaposhindwa huacha maswali mengi nyuma yake ambayo kila mmoja wa wasomaji atapata majibu yatakayompa ukweli. Mfano ni riwaya ya Rosa Mistika ambapo “Rosa” anapitia mazingira magumu yanayodhihirisha ubinadamu wake na mwisho anajiua na kuacha maswali juu ya kwanini amefanya hivi au vile. Kwa upande wa riwaya za kifalsafa hizi ni zile zinazolenga kutoa majibu ya maswali magumu katika jamii kwa kuonesha jinsi wahusika wanavyopambana hadi kupata suluhisho mfano riwaya ya Kiu ya Haki mhusika mkuu Mzee Toboa pamoja na kupatwa na shuruba nyingi alisimamia kweli na kila mtu akapata haki yake (Sikujua ambaye ndiye muuaji wa Pondamali akatiwa hatiani na kufungwa). Riwaya hizi kwa ujumla zinatoa majibu ya kisaikolojia na kifalsafa kuhusu maisha na ukweli wake.
Kanuni ya mabadiliko; hii inaelekeza utunzi wa riwaya kwa kuzingatia uhalisia wa maisha ya historia ya jamii. Nchini Tanzania kanuni hii inazigawa riwaya katika vipindi mbalimbali kama vile kipindi cha uhuru ambacho kinachukua riwaya zilizotungwa kufurahia mafanikio hewa katika jamii mfano riwaya ya Ndoto ya Ndalia na Nyota ya Rehema hizi ni riwaya ambazo zilianza kuyaona mafanikio makubwa na yenye neema hata kabla inayotokea.
Kipindi kilichofuata ni kile cha mfumo wa siasa ya ujamaa na kujitegemea na kuanzishwa kwa vijiji vya ujamaa, hapa watu walihubiriwa kuwa mafanikio yako vijijini kwenye kilimo kuliko mjini. Riwaya ya Shida ni kielelezo cha mahubiri hayo na kipindi hiki pia kilikuwa na riwaya za kihakiki na zilizokosoa mfumo wa siasa uliopo kwa mfano riwaya ya Njozi za Usiku na Njozi Iliyopotea ni baadhi ya riwaya zilizokosoa utunzi wa kikasuku.
Kipindi cha vita vya Kagera kiliibua riwaya za ujenzi wa jamii mpya zilizolenga kuhamasisha uzalendo kwa jamii. Mfano riwaya ya Zawadi ya Ushindi ambayo inaonesha jinsi vijana kama Sikamona wakijitoa muhanga kwenda vitani kupigana kwa ajili ya ukombozi wa nchi yao dhidi ya uvamizi wa nduli Iddi Amin wa Uganda.
Kipindi cha mwisho ni kile cha kulegezwa kwa masharti na ujio wa uhuru wa soko huria na mwingiliano mkubwa wa kijamii. Kipindi hiki kina riwaya kama Makuwadi wa Soko Huria, Almasi za Bandia, Babu Alipofufuka, Kufikirika na Kusadikika. Kwa ujumla riwaya ni utanzu wenye kanuni zake ambazo kwazo wasomaji huweza kuziainisha na kuzibainisha katika makundi mbalimbali.
|