FASIHI SIMULIZI
Fasihi Simulizi ni utanzu wa fasihi ambao unawakilisha sanaa ya lugha inayopitishwa kutoka kwa kizazi hadi kizazi kwa njia ya maneno/masimulizi ya mdomo.
Kwa hiyo, fasihi simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa njia ya masimulizi ya mdomo na vitendo bila maandishi. Fasihi simulizi hurithiwa kutoka kizazi kimoja na kingine.
Fasihi simulizi ni fasihi ya awali zaidi, kwani ilianza wakati binadamu alipoanza kutumia lugha kama chombo cha mawasiliano katika jamii ndipo alipoanza kutumia nyimbo, methali, vitendawili n.k.
SIFA ZA FASIHI SIMULIZI
- Hupitishwa kwa njia ya mdomo
- Ufanisi wa sanaa katika fasihi simulizi hutegemea uwezo wa msimulizi, au wahusika
- Masimulizi yake yanaweza kuathiriwa na mazingira, hisia na hali
- Ni mali ya jamii. Hakuna mtu fulani anayemiliki sanaa katika fasihi simulizi.
- Inaweza kubadilika kutoka kizazi hadi kizazi, au mazingira mbalimbali kwa sababu hutegemea kumbukumbu ya msimulizi.
- Aghalabu huwa na funzo fulani
UMUHIMU WA FASIHI SIMULIZI
- Kuburudisha – Hufurahisha na kuchangamsha hadhira
- Kunasihi- kutolea mawaidha na kuonyesha mwelekeo unaotarajiwa katika jamii
- Kuelimisha watu kuhusu vitu mbalimbali hasa mazingira yao
- Kutambulisha jamii – jamii mbalimbali husifika kutokana na sanaa zao katika fasihi simulizi kama vile nyimbo
- Kuhifadhi na kudumisha utamaduni wa jamii
- Kuunganisha watu – huleta watu pamoja
- Kukuza lugha – fasihi huimarisha lugha kwa kuwa hutumia mbinu mbalimbali za lugha.
- Kuliwaza – hutoa huzuni na kuleta matumaini.
- Kupitisha muda – wakati mwingine fasihi simulizi hutumika kupitisha muda.
VIPENGELE VYA FASIHI SIMULIZI
- Msimuliaji (fanani)
Huyu ni mtendaji wa tukio la kifasihi mbele ya hadhira. Tukio laweza kuwa kutamba hadithi, kuimba wimbo au kutoa kitendawili au methali. Huyu ni muhusika anayesana kazi ya fasihi.
- Hadhira
Hawa ni walengwa wa kazi ya fasihi ambao husikiliza na kutazama kinachotendwa na fanani. Hadhira hushiriki kwa namna fulani kwenye kile kinachotendwa iwe ni kuitikia wimbo au kupiga makofi, kutingisha kichwa au mwili. Hadhira humsaidia fanani kujitathimini juu ya kile anachokitenda na mbinu ya utendaji anayoitumia.
- Mandhari
Hapa ni mahali ambapo matukio ya kifasihi yanatendekea. Mandhari huweza kuwa uwanjani, kichakani, chini ya mti mkubwa au mlimani.
- Tukio
Hili ni tendo au tukio linalotendwa na fanani kifasihi. Tendo hili laweza kuwa usimuliaji hadithi, vitendawili, kuimba au kutoa methali.
TANZU NNE ZA FASIHI SIMULIZI
- Hadithi (visakale, ngano, visasili na vigano)
- Ushairi (tenzi, ngonjera, shairi, nyimbo)
- Semi (nahau, mafumbo, methali, vitendawili)
- Sanaa ya maonyesho /maigizo (vichekesho, majigambo)
UHAKIKI
Nini maana ya uhakiki wa kazi fasihi simulizi?
Uhakiki wa fasihi simulizi ni kazi au kitendo cha kutafakari, kuchambua na kufafanua kazi ya fasihi simulizi ili kuweka bayana maadili na ujumbe uliomo katika kazi ya fasihi.
MHAKIKI
Huyu ni mtu anayejishughulisha na uhakiki wa kazi za fasihi zilizotungwa na wasanii wengine wa fasihi.
VIGEZO VYA UHAKIKI
- Ukweli wa mambo yanayoelezwa
Mhakiki wa kazi za fasihi simulizi atajiuliza, je ni kweli jambo linaloelezwa linafanyika katika jamii inayozungumzwa.
Kwa mfano:
Kama mhakiki wa fasihi simulizi anahakiki ngonjera inayohusu ubakaji inabidi ajiulize je kweli kuna ubakaji katika jamii inayomzunguka.
- Uhalisia wa watu, mazingira na matukio katika jamii.
Mhakiki wa kazi za fasihi simulizi atalingalisha Wahusika waliotumiwa, mazingira na matukio katika kazi hiyo ya fasihi simulizi na hali halisi katika jamii.
Kwa mfano: kama hadithi inahusu ulevi, mhakiki inabidi ajiulize. Je katika jamii husika tabia ya ulevi ipo.
- Umuhimu wa kazi hiyo kwa jamii husika lazima uzingatiwe
Mhakiki atachunguza jambo ambalo linazungumziwa kwenye hiyo kazi ya fasihi simulizi kama lina umuhimu na kuelimisha jamii. Jambo linalozungumziwa linaweza kuwa la kweli lakini halina umuhimu kwa jamii hiyo kwa kipindi hicho.
Mhakiki wa kazi za fasihi simulizi huzingatia vipengele vikuu viwili vya kazi ambavyo ni: –
Fani (umbo la nje la kazi ya fasihi)
Hili linatia ndani vipengele vyake ni muundo, matumizi ya lugha, mtindo, mandhari na wahusika.
Maudhui (umbo la ndani la kazi ya fasihi)
Linatia ndani dhamira, ujumbe, mafunzo, migogoro na falsafa
UHAKIKI WA USHAIRI WA FASIHI SIMULIZI
Katika fasihi simulizi ushairi ni fungu lenye kujumuisha tungo zote zenye kutumia mapigo kwa utaratibu maalum, mapigo hayo hupangwa kwa muwala wa urari wa vina na mizani. Baadhi ya fani za ushairi huambataniswa na muziki wa ala na wakati mwingine hupata mizani yake kutokana na mipangilio ya ala.
VIPENGELE VYA FANI KATIKA USHAIRI
- MUUNDO
Mashairi yana miundo tofauti tofauti ikitegemeana na ufundi wa mshairi husika. Katika muundo tunaangalia kile kinachooneshwa kwa nje.
Kwa mfano: - Mgawo wa vipande
- Kiitikio / mkarara/ kibwagizo
- ldadi ya mistari katika kila ubeti
- ldadi ya beti katika shairi zima
Hivyo, katika mashairi tuna miundo tofauti tofauti ambayo hutumiwa kuainisha kwa mujibu wa idadi ya mistari kwenye kila ubeti muundo huu ndio unatupa mashairi ya tathnia/mistari 2 tathlitha/mistari 3 Tarbia/mistari 4 Takhmisa/mistari 5.
- MTINDO
-Mashairi ya fasihi simulizi yamejengwa na mitindo mingi katika utungaji
Mtindo tunaangalia vipengele kama vifuatavyo:
-Urari wa vina pamoja na ulinganifu wa mizani au ushairi unaofuata sheria za urari wa vina na mizani ni mashairi ya kimapokeo. - Mizani…. Idadi ya silabi ambazo zipo katika kila mstari
- Vina……. Silabi zenye mlio unaofanana
-Mtindo wa Pindu ambapo silabi mbili (2) za mwisho wa mstari hurudiwa rudiwa mara kadhaa, Kwa mfano kama mstari wa kwanza unaishia na neno “fahamu” basi mstari wa pili pia utaishia na silabi “mu” -Mashairi ya masivina {gum au mauve}
Haya ni mashairi yasiyofuata urari wa vina na mizani
- HISIA
Hapa tunajiuliza maswali yafuatayo: –
Ni hisia zipi zinazowasilishwa na ushairi huo?
Kwa mfano; Hisia za huzuni, hisia za furaha, hisia za kukatisha tamaa, hisia za kuchekesha, hisia za kuudhi, hisia za kuogopesha au hisia za ujasiri.
Kwa ukawaida mshairi anapoandika shairi huanza yeye mwenyewe kupatwa na hisia fulani ambazo hujaribu kuzitoa kwa njia ya ushairi ili ziwasilishwe kwa hadhira.
- UTENDAJI
Katika utendaji tunaangalia vipengele kama vile mtindo na utendaji. Unatendwa na mtu mmoja au watu wengi, mmoja kwa mmoja au mtu akijibizana na kundi la watu kadhaa kwa zamu.
Pia ni muhimu kuzingatia mbinu za utendaji, kama vile malighati ukariri au majibizano/ngonjera na uimbaji.
Muktadha/mazingira
Ushairi unaimbwa wapi? Wakati gani na kwa hadhira ya aina gani? Watendaji akina nani, wazee, vijana, wanawake/ wanaume
- WAHUSIKA
Ushairi wa fasihi simulizi kwa kawaida ina wahusika, fanani na hadhira. - Fanani huwa wanatumika na mtunzi kufikisha ujumbe unaokusudiwa kwa hadhira.
- Fanani kwa kawaida anaweza kuwa muimbaji, waghanaji n.k
- Tanzu za fasihi simulizi zinatumia hadhira kama vile waitikiaji, Jukumu kubwa la waitikiaji ni kumpumzisha fanani hasa mwimbaji.
Kwa upande mwingine, ngonjera huwa na wahusika pande mbili ambapo huwa na malumbano kati yao. Dhumuni huwa ni kutoa ujumbe fulani mhusika mmoja anaweza kusema jambo moja kutoka ubeti na mwingine kulijibu jambo hili.
- MATUMIZI YA LUGHA
Lugha ni malighafi ya ushairi. Lugha inayotuwa ni ile iliyokusudiwa kuinua hisia fulani kwa hadhira husika.
Matumizi ya lugha katika ushairi kuna ya aina tofauti tofauti. Uteuzi wa maneno au msamiati lazima ufuate kile unachozungumzia.
Uteuzi wa maneno(msamiati). Mambo ya kutilia maanani hapa kuhusiana na msamiati na ushairi ni: – - Matumizi ya maneno ya kale/zamani ili kuleta ulinganifu wa vina na mizani.
- Uendelezaji wa msamiati ili kuwepo uhusiano wa vipindi tofauti tofauti vya kihistoria na pia kukejeli jambo au hali fulani.
- Kutumia maneno yaliyobuniwa na msanii husika.
- Kutumia maneno ya kawaida yenye muundo usiokuwa wa kawaida.
- Kutumia tamathali za semi
KUNA AINA MBALIMBALI ZA SEMI
Ni mbinu inayotumika kulinganisha vitu viwili bila kutumia viunganishi.
Kwa mfano, Mfalme ni simba
Kukipa kitu kisichokuwa na uhai uwezo wa kutenda kama binadamu.
Ufananishaji wa kitu au jambo kwa kutumia maneno kama vile mithili ya, kama, mfano, au viunganishi
Ni kurudia kurudia maneno, silabi, sentensi hii ni katika kusisitiza maudhui na upambaji wa lugha.
Ni kumpa mtu sifa isiyofanana na jinsi alivyo.
MBINU NYINGINE ZA KISANAA.
Taswira
Haya ni maelezo ambayo hutumika kuunda picha ya kitu, hali, wazo au dhana fulani akilini mwa msomaji au msikilizaji.
Ni mbinu ambayo msanii anatumia katika kazi yake ya fasihi kwa lengo la kuwakilisha wazo, dhana ya kitu kingine
Mfano; neno “Ua” …. Huashiria mpenzi/ mwanamke mzuri(mrembo)
Tafsida
Ni kutumia lugha iliyo fasili siyo kali ili kuficha ukali au uchafu wa maneno machafu au yanayokarahisha yasitumike moja kwa moja.
Pia msanii hutumia misemo na nahau; hii ni katikaharakati za kuipamba kazi yake ya fasihi simulizi na pia katika kutajirisha maelezo yake.
Matumizi ya methali
Msanii hutumia methali katika ushairi kwa lengo la kupitishia hekima pia zinatumiwa ili kujenga kejeli kuhusu masuala tofauti tofauti ya jamii.
UHAKIKI WA MAUDHUI YA USHAIRI WA FASIHI SIMULIZI
VIPENGELE VYA MAUDHUI KATIKA USHAIRI WA FASIHI SIMULIZI: –
MAUDHUI
Maudhui katika kazi ya fasihi ni jumla ya mawazo yote yanayozungumzwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Maudhui hujumuisha mawazo pamoja na mafunzo mbalimbali yaliyomsukuma msanii hadi akatunga na kusanii kazi fulani ya kifasihi. Vipengele vya maudhui ni pamoja na dhamira, migogoro, falsafa ujumbe na msimamo.
Dhamira
hili ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Senkoro anataadharisha maana hii isichanganywe na maudhui kwani dhamira ni sehemu tu ya maudhui na aghalabu dhamira kuu ndio hujenga kiini cha kazi ya fasihi. Dhamira zimegawanyika katika makundi mawili, kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo.
Wasanii wa ushairi wameonesha dhamira mbalimbali kama
Migongano ya kitabaka, Mapenzi na ndoa, mwanamke na nafasi yake katika jamii, maadili tofauti tofauti ya jamii, ukombozi, ujenzi wa jamii mpya n.k
Ujumbe na maadili
mwandishi anapoandika kazi yake huwa na ujumbe ambao hutaka uifikie jamii aliyoikusudia. Ujumbe katika kazi fasihi ni mafunzo mbalimbali ambayo hupatikana baada ya kusoma kazi ya fasihi. Katika kazi ya fasihi dhamira kuu hubeba ujumbe wa msingi na dhamira ndogondogo hubeba ujumbe ambao husaidia kuujenga au kuupa uzito zaidi ujumbe wa msingi
Falsafa
Falsafa ni msimamo na mtazamo wa mwandishi katika kazi yake, ama imani na mwelekeo wake kuhusu maisha.
Msimamo
katika kazi ya fasihi, mawazo, mafunzo na falsafa ya msanii hubainisha msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Msimamo ni ile hali ya mwandishi kuamua kufuata na kushikilia jambo fulani. Jambo hili huweza kukataliwa na wengi lakini akalishikilia tu. Msimamo ndio huweza kuwatofautisha wasanii wawili au zaidi wanaoandika kuhusu mazingira yanayofanana.
UHAKIKI WA MAIGIZO
Maigizo (drama)
Ni sanaa inayotumia watendaji kuiga tabia au matendo ya watu na viumbe wengine ili kiburudisha na kutoa ujumbe fulani. Maigizo ni sanaa inayopatikana katika makabila mengi. Drama (maigizo) ya kiafrika huambatana na ngoma mtambaji wa hadithi au matendo ya kimila. Kwa mfano jando na unyago, yapo maigizo yanayofungana na michezo ya watoto, uwindaji, kilimo, na kadhalika
VIPERA VYA MAIGIZO
Haya ni maigizo ya jukwaani ambapo watendaji huiga maneno na matendo ya wahusika na kuyasema wakiwa kwenye jukwaani. Jukwaa hutayarishwa ili kuiga mazingira ya tamthilia au tukio wanaloliigiza.
Sifa za Michezo ya Kuigiza
- Huwa na wahusika ambao huwakilishwa na watendaji.
- Hufanyika kwenye jukwaa mbele ya hadhira
- Huhitaji kumbukumbu ili kukumbuka maneno ambayo mhusika anapaswa kusema katika jukwaa
- Vitambaa au mwangaza hutumiwa ili kuashiria kubadilika kwa mazingira au wakati
- Hutumia mbinu za lugha kama vile chuku, tanakali za sauti, tamathali na nyinginezo
- Hujumulisha aina nyingine za sanaa kama vile ushairi na nyimbo.
Umuhimu wa Michezo ya Kuigiza
- Huburudisha
- Huelimisha
- Hukuza uwezo wa kukumbuka kwa watendaji
- Miviga
Miviga ni sherehe mbalimbali katika jamii fulani. Watu hujumukika na sherehe hizi kulingana na tamaduni zao. Watu mbalimbali katika jamii huwa na majukumu tofauti tofauti. Miviga huandamana na nyimbo, vyakula na mawaidha kutoka kwa wazee. Mifano ya miviga ni kama vile Sherehe za ndoa, mazishi, tohara n.k
Sifa za miviga
- Huandamana na nyimbo zinazohusiana na sherehe hiyo kwa mfano nyimbo za mazishi, ndoa n.k
- Ngoma mbalimbali huchezwa
- Huwa na vyakula vya kienyeji
- Aghalabu kina mama hupewa kazi za upishi na burudani
- Wazee hutoa mafunzo, mawaidha kwa vijana
Umuhimu wa miviga
- Huleta jamii pamoja na kuunganisha watu katika jamii
- Watu hupata mafunzo kutoka kwa wazee katika jamii
- Hudumisha tamaduni katika jamii
- Huburudisha – kwa mfano sherehe zinapohusisha nyimbo na michezo ya kuigiza
- Huliwaza – kwa mfano wakati wakati wa huzuni kama vile mazishi
- Ngomezi
Ngomezi ni sanaa ya ngoma. Midundo tofauti tofauti ya ngoma hutumika kuwakilisha ujumbe au maana fulani. Ngoma zilitumika sana kabla ya teknolojia ya barua na simu. Wataalam wa ngoma walipiga ngoma kwa milio mbalimbali kufahamisha jamii kwa jambo fulani limefanyika kwa mfano kuingia kwa adui, moto, mtoto anapozaliwa n.k
Sifa za ngomezi
- Hutumia midundo mbalimbali ya ngoma kupitisha ujumbe fulani
- Huhitaji mtaalam wa ngoma
- Maana ya midundo mbalimbali hubadilika kutoka kwa jamii moja hadi nyingine, hivyo basi ni vigumu kwa jamii-adui kutambua ujumbe wake
Umuhimu wa Ngomezi
- Kupitisha ujumbe
- Kutahadharisha jamii dhidi ya adui
- Kuburudisha
- Kuhifadhi tamaduni za jamii
- Malumbano ya Utani
Malumbano ya utani ni mashindano ya kuongea jukwaani baina ya watu wa makundi au jamii mbili ambayo hutumia kejeli na chuku kukejeli tabia mbaya katika jamii au kundi fulani. Watu husimama jukwaani na kushindana kwa maneno.
Sifa za Malumbano ya Utani
- Hutumia mzaha na vichekesho
- Hutumia kinaya na kejeli ili kuangazia ukweli fulani katika jamii
Umuhimu wa Malumbano ya Utani
- Kurekebisha mambo mabaya katika jamii
- Kuburudisha
- Kupitisha muda
- Ulumbi
Ulumbi ni uwezo wa kipekee wa kuzungumza mbele ya hadhira. Mtu mwenye uwezo huo wa kipekee wa kuzungumza jukwaani huitwa mlumbi. Walumbi husifika sana kwa kuzungumzia mambo yanayoathiri jamii.
Sifa za Mlumbi
- Ana uwezo wa kushawishi watu kuhusu ujumbe anaopitisha.
- Huwa mkwasi wa lugha anayeifahamu vizuri lugha yake.
- Hutumia lugha ya kuvutia na kumakinisha hadhira
- Anaifahamu sana hadhira yake na maswala yanayoiathiri.
- Ni kiongozi.
Umuhimu wa Ulumbi katika jamii
- Kuhamasisha jamii kuhusu mambo yanayowakabili.
- Kuunganisha watu watekeleze jambo fulani kwa pamoja
- Kuburudisha
- Soga (Mazungumzo)
Soga ni mazungumzo baina ya watu wawili au zaidi ambayo aghalabu huwa hayana mada maalum. Aghalabu soga huwa na vichekesho vingi, mzaha na kejeli. Nia yake huwa kuburudisha na kupitisha wakati.
Sifa za Soga
- Soga huwa na vichekesho na mzaha mwingi
- Mada hubadilikabadilika kutoka wakati mmoja hadi mwingine
- Haihitaji taaluma yoyote ya kisanaa
- Inaweza kufanyika mahali popote – njiani, sebuleni, katika vyumba vya burudani n.k
Umuhimu wa Soga
- Kupitisha wakati hasa watu wanaposubiri jambo fulani lifanyike kama vile chakula kiive
- Kuburudisha
- Kuunganisha jamii
- Vichekesho
Vichekesho ni aina ya sanaa ya fasihi simulizi ambayo watu hutoa vihadithi vifupi au sentensi zenye uwezo wa kuwafanya wasikilizaji wacheke. Vichekesho huhitaji ubunifu mwingi ili kutaja jambo litakalowavunja bavu hadhira.
Sifa za Vichekesho
- Huwa na uwezo wa kutekenya hisia hadi mtu acheke.
- Aghalabu vichekesho huwa vifupi
- Hutumia mifano ya vitu vinavyojulikana wazi na hadhira katika mazingira/mandhari yao.
- Hutumia mbinu ya kejeli na chuku sana.
Umuhimu wa Vichekesho
- Kuburudisha
- Kupitisha wakati
- Maonyesho ya Sanaa
Maonyesho huhusisha watu wa jamii au kundi fulani wanaoonyesha taaluma, ujuzi au sanaa yao kwa watazamaji. Kwa mfano maonyesho ya kilimo, maonyesho ya kitamaduni n.k Mazingira katika maonyesho haya huwa ni maeneo halisi na wahusika wake huwa watu halisi katika familia.
Mifano ya Sanaa ya Maonyesho
a) Maonyesho ya Kilimo
Katika maonyesho haya, wakulima kutoka sehemu mbalimbali huonyesha bidhaa zao za kilimo kama vile vyakula, mifugo, mbegu na kadhalika. Nia ya maonyesho ya kilimo huwa ni kuwaelimisha watu kuhusu mbinu bora za ukulima.
b) Maonyesho ya Kisayansi
Haya ni maonyesho ya mbinu mpya za kisayansi na teknolojia.
c) Maonyesho ya Kitamaduni
Jamii mbalimbali huonyesha utamaduni wao mbele ya hadhira kama vile nyimbo za kitamaduni na sherehe nyingine
d) Maonyesho ya Kibiashara
Katika maonyesho ya kibiashara, bidhaa mpya huonyeshwa kwa hadhira. Kampuni mbalimbali hujitokeza kufahamisha hadhira kuhusu bidhaa zao mpya.
Sifa za Sanaa ya Maonyesho
- Huwa na matangazo kusifia bidhaa, mbinu au mawasilisho mbalimbali
- Aghalabu huwa na mashindano ambayo washiriki hushinda zawadi mbalimbali
- Wahusika huwa watu halisi katika jamii
- Hutumia mazingira halisi badala ya kutumia jukwaa
Umuhimu wa Sanaa ya Maonyesho
- Kufahamisha watu kuhusu bidhaa na mbinu mpya
- Kuburudisha
- Kuleta watu pamoja
UHAKIKI WA MAIGIZO
- FANI
Uhakiki wa fani katika maigizo unajihusisha na ufundi uliotumiwa. Ufundi huu unajumuisha mambo kadhaa kama ifuatavyo, tendo au tukio.
Katika Sanaa ya maigizo lazima kuwe na tukio ambalo hubebwa kama kiini au chanzo cha utunzi huo.
Tendo au tukio huwa ndio kishawishi cha fanani wa maigizo husika, kwa sababu hiyo katika maigizo lazima pawe na tendo linalotendeka, yaani tendo linalorihidhishwa katika umbo la vitendo vikitendwa.
- WAHUSIKA
Katika maigizo kuna wahusika wa aina kuu mbili - Watendaji
- Watazamaji/hadhira
Watendaji
Hawa ni wasanii wanaotumia vipaji vyao ili kuonesha dhana fulani kwa hadhira.
Wasanii hawa hutumia mbinu tofauti tofauti ili kuvutia hisia kwa hadhira hasa kwa kutumia viungo vya miili yao.
Katika Sanaa ya maigizo kuna watendaji wakuu na watendaji wadogo.
Watendaji wakuu ndio wabebaji wa kiini cha dhamira kuu na maanaau lengo la igizo lenyewe, watendaji hawa huonekana tokea mwanzo wa onesho hadi mwisho wa onesho. Matendo yote kwenye igizo hujengwa kumhusu yeye.
Watendaji wadogo hawa kwa kawaida hujitokeza hapa na pale katika onesho husika kwa lengo la kukamilisha onesho hilo.
Watendaji hawa husaidia kuunda dhamira fulani katika igizo vilevile husaidia katika kumjenga mtendaji mkuu katika igizo.
Watazamaji (hadhira)
Katika muktadha huu watazamaji humaana watu walio kusanyika kwa lengo la kutazama igizo lolote lile.
Watazamaji hawa wanahisi, wanasikia, wanatafakari ili kuweza kutoa uhakiki wa vipengele tofauti tofauti vya igizo hilo
Kwa kawaida hadhira huwa na uhuru wa kudadisi, kushiriki kwa kucheza kuimba na kupiga vigelegele kuhusiana na igizo wanalolitazama.
Katika igizo lolote hadhira ndio huwa wahakiki wa kwanza wa igizo hilo. Hadhira huakiki igizo la mtendaji kwa kutazama vitendo, mwenendo na vitabia anavyovifanya mtendaji katika jukwaa la Sanaa.
- MANDHARI
Mandhari humaanisha mahali popote ambapo watendaji hutumia kuonesha onesho lao.
Mfano: – - Uwanjani
- Barabarani
- Nyumbani
- Porini
- Jukwaani.
Katika jukwaa mtendaji, huwa huru kutenda, kuingia na kutoka jukwaani bila wasiwasi wowote.
Hapo kale michezo mingi iliigizwa nje na waigizaji walikuwa wakiangalia sana umuhimu wa jukwaa kwani jukwaa liliwekwa sehemu yoyote ile kama vile uwanjani au shuleni.
- MUUNDO
Muundo katika maigizo humaanisha mpangilio wa igizo lenyewe yaani umbo lake lilivyogawanyika kwenye sura au maonyesho au mtiririko wa matukio na msuko wa igizo husika.
Matukio huwa na uwezekano wa kufanana moja kwa moja au yanaweza kuwa na uchangamano ambao huusisha kwenda mbele na kurudi nyuma/msuko changamani
- MTINDO
Mtindo ambao hutumiwa na maigizo ni mtindo wa dayolojia, dayolojia ni majibizano kati ya wahusika waliopo kwenye jukwaa. Ni jambo la muhimu kwamba mazungumzo hayo siyo maongezi au majibizano kwa ajili ya kujibizana tu bali mazungumzo lazima yaendane na tendo kuu katika maigizo. Mazungumzo ndiyo nguzo kuu ya kukidhi maudhui na dhamira katika igizo.
- MATUMIZI YA LUGHA.
Nyenzo kuu ya maigizo ni Lugha. Dhamira na maudhui haviwezi kuwasilishwa na kufikishwa kwa watazamaji pasipo kutumia lugha.
Uchunguzi pamoja na matumizi ya lugha ni muhimu katika uhakiki wa maigizo yote.
- Matumizi ya methali
Methali hutumika katika maigizo kwa lengo la kupitisha hekima, kuunda kejeli kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo jamii, kuunda mandhari ya kitamaduni ya kuaminika kuhusu jamii fulani.
- Misemo na nahau
Jinsi misemo na nahau inavyotumika katika kazi ya fasihi hushabiana sana na matumizi ya methali.
Misemo na nahau hutumika katika kutambulisha mazingira maalum yanayotumiwa katika igizo au kujulisha hadhira wakati na wahusika katika kazi ya fasihi inayoshughulikiwa.
Hii ni kwasababu msemo huzuka na kutoweka kutokana na hali tofauti tofauti za kimazingira.
Misemo, misimu, nahau kwa kawaida huzaliwa, hukua na kufa kwahiyo matumizi yake katika kazi ya fasihi nayo hutegemeana sana na uhai wa misemo, nahau na misimu iliyotumika.
Kwa upande mwingine misimu na nahau hutumiwa kwa njia ya kupendezesha kazi ya fasihi na pia katika kuainisha wahusika na lugha zao. Vilevile wasanii hutumia kutayarisha maelezo yao.
- Tamathali za semi.
Tamathali za usemi ni maneno ambayo hutumiwa na wasanii wa fasihi ili kutia msisitizo, nguvu na maana katika kazi zao, hali kadhalika kuboresha mtindo wa kazi zao. Wakati mwingine huwa na lengo la kupamba kazi ya fasihi na kuongeza utamu wa lugha.
Kuna aina nyingi zatamathali za usemi kama ifuatavyo;
- Tafsida
Tafsida hutumika ili kupunguza ukali wa maneno au matusi katika usemi
Mfano:
-Kujisaidia au kwenda haja badala ya kunya au kukojoa.
-Kuaga dunia badala ya kufa n.k
- Kejeli /stihizai
Kejeli ni mbinu ya sanaa inayotumia maneno kudharau au kukemea kitendo au mtu fulani. Kejeli inawezatumia maneno ya madharau yanayojitokeza moja kwa moja au yaliyofichika.
Tofauti kuu kati ya kejeli na kinaya ni kwamba kinaya hutumia maneno kumaanisha kinyume chake - Kama wewe ndiye mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe na utuokoe sisi.
- Mwalimu Manyumba ndiye anayetoa hotuba leo; itabidi tubebe mablanketi.
- Dhihaka
Hii ni tamathali ya dharau na yenye lengo la kumweka mtu katika hali duni kupita kiasi, lakini kwa kutumia mbinu ya mafumbo
Mfano:
“Angela alikuwa msichana msafi na mrembo sana. Ndiyo sababu kila, mara alipaka mafuta yaliyonukia na kukaribisha nzi walioleta matatizo makubwa”.
- Sitiari
Ni tamathali inayolinganisha matendo, vitu au tabia ya vitu vyenye maumbile tofauti bila kutumia viunganishi linganishi
Kwa mfano:
-Maisha ni moshi
-Pesa ni maua
-Penzi upepo
-Misitu ni uhai
- Tashbiha
Tamathali inayolinganisha vitu kwa kutumia maneno kama vile mfano wa, kama, mithili ya , sawa na , n.K
Kwa mfano;
-Ana sauti tamu sawa na ya chiriku
-Ana maringo kama twiga
-Ananyata mithili ya kinyonga
-Ana ng’ang’ania kama kupe.
- Tashihisi
Tamathali hii huvipa vitu sifa walizonazo binadamu (hupewa uwezo walionao binadamu)
Kwa mfano:
-Mvua iliponyesha misitu ilipiga makofi
-Mawimbi yalitabasamu kwa upepo wa kusi.
- Mubalagha
Hii hutia chumvi kuhusu uwezo wa viumbe, tabia zao na hata sifa zao kwa lengo kuchekesha au kusisitiza
Kwa mfano:
-Loo! Hebu muangalie mrembo yule! Ana mlima wa kiuno.
-Tulimlilia Nyerere hadi kukawa na bahari ya machozi
-Mrembo yule hubeba kila aina ya silaha na huwatia wazimu wanaume wote anaokutana nao.
- Metonimia au Taashira
Katika tamathali hii jina la sehemu ya kitu kimoja au la kitu kidogo kinachohusiana na kingine kikubwa hutumiwa kuwakilisha kitu kamili.
Kwa mfano:
-Jembe huwakilisha mkulima
-Kutabasamu huwakilisha furaha
-Mvi huwakilisha uzee
-Kalamu huwakilisha mwanafunzi / msomi.
- Taniuba (Antonomasia)
Hizi ni tamathali ambazo kwayo jina la mtu binafsi hutumiwa kwa watu wengine wenye tabia, mwenendo, hali au kazi sawa na ya mtu huyo.
Kwa mfano:
-Yesu – mkombozi
-Yesu wa kwanza wa Afrika alikuwa Kwame Nkrumah
-Nyerere alikuwa Yesu wa kwanza Tanzania
- Msisitizo bayana
Hii hutumika kusisitiza maana ya sentensi kwa kutumia kinyume
Kwa mfano: - Mwanadamu anaweza kupanga, Mungu akapangua
- Alikuwa binti mzuri, ukimwona kwa mbali huwezi kutambua anakuja au anakwenda.
- Ritifaa
Hizi ni tamathali za semi ambazo mtu huzungumza na kitu au mtu ambaye anamfikiria tu.
Mf. Baba umetutoka umetuachia majonzi
- Tabaini
Huu ni usemi unaosisitiza jambo kwa kutumia maneno yanayokinzana.
Mfano. Ni mrefu si mrefu, mfupi si mfupi.
- Takriri
Ni mbinu ya kurudia rudia maneno kwa ajili ya kusisitiza jambo.
Mfano. Maisha ni magumu jamani ni magumu.
- Mdokezo
Ni mbinu ya kukatiza maneno katika sentensi.
Mf. Unasema alitaka ……………..
Tahtiti
Ni mbinu ya kuuliza maswali kwa swali ambalo jibu lake linafahamika na unafanya hivyo kwa lengo la kusisitiza jambo au kuleta mshangao.
Mf. Ndio umekuja? (ikiwa unamuona mtu amekuja)
- Nidaa
Huu ni msemo unaoonesha kushangazwa kwa jambo fulani. Msemo huu huambatana na alama ya mshangao. Mf. Loh! hii ni hatari.
- Mjalizo
Ni mfululizo wa maneno usio na viunganishi. Mf. Nilikaa nikasubi nikachoka nikaamua kuondoka kwenda nyumbani.
- Tanakali sauti/ Onomatopia
Ni mbinu ya kuiga sauti za milio mbalimbali. Milio hii ni ya wanyama, vitu n.k
Kwa mfano: – - Alitumbukia mtoni chubwi!
- Alidondoka sakafuni puu!
- Taswira
Ni picha zinazojitokeza ndani ya mawazo ya msomaji au msikilizaji wa kazi ya fasihi. Matumizi mazuri ya taswira na ishara hutegemea ufundi wa yanayomzunguka yeye na jamii yake pamoja na historia za maisha azijuazo.
Aina za Taswira
(i)Taswira za hisia
Taswira hupenyeza hisia na kuzigandisha akilini mwa msomaji au msikilizaji na kunasisha ujumbe wa mwandishi. Taswira hizi hushughulikia hisi za ndani, na kuweza kumfanya msomaji au msikilizaji awe na wasi wasi aone woga, apandwe na hasira, ahisi kinyaa, n.k
mfano:
Akadharau! Siwezi na sitaweza kula chakula kama hicho! Rojorojo nyororo kama limbwata, mfano wa kohozi lenye pumu, liingie katika koo langu lililozoea chipsi kuku, kuku wa kumimina na wa mrija
-Maelezo kama hayo humfanya mtu akinahi na kutaka kutapika mara akisoma rojorojo, kunyororoka mfano wa kohozi lenye pumu.
(ii)Taswira za mawazo / kufikirika
Taswira hizi zinatokana na mawazo yanayohusu mambo yasiyoweza kuthibitika. Mambo kama kifo, pendo, uchungu, fahamu, sahau, raha n.k
Mfano:
Kifo, kifo umefanya nini? Umeninyang’anya penzi langu bila huruma? kumbuka, nilimpenda nikapoteza mpaka fahamu, kifo ukazidi kunidunga sindano ya usingizi?
(iii)Taswira zionekanazo
Kwa kawaida hizi ni picha ambazo hujengwa kwa kutumia vielelezo tunavyovijua vile vinavyofahamika katika maisha yetu ya kila siku.
Mfano:
Dakika haikupita mijusi wawili waliokuwa wamebebana walipita haraka sana. Midomo yao ilikuwa myekundu sana. Ghafla walikutana na nyoka aliyeonekana mnene hasa sehemu za tumboni. Hapana shaka alikuwa amemeza mnyama.
UCHESHI
Ucheshi ni mbinu ya kifani ambayo hutumiwa na watambaji fasihi simulizi kwa nia tofauti. Kama ilivyo katika baadhi ya kazi za fasihi andishi, vivyo hivyo katika fasihi simulizi, ucheshi hutumiwa kuwa kipumuo, hasa baada ya matukio ya kutisha, au maelezo marefu yenye kuwachosha wasikilizaji.
Upeo/ kelele katika maigizo
Hii ile hali inayokidhi haja ya hadhira inayopokea kazi hiyo ya fasihi katika sehemu hizi watazamaji hupata majibu muhimu ambayo igizo au onesho linakuwa imeyachelewesha kwa kutumia mbinu mbalimbali kama vile tabaruki, mbinu rejeshi n.k
Sehemu hizi mara kadhaa husisimua watazamaji waigizo kwa hali ya juu sanakatika maigizo, watendaji huunda migogoro ambayo hujitokeza na kukua sambamba na kazi zikuavyo. Kipeo hutokea pale wanapotoa suluhisho la mgogoro katika onesho au igizo.
Kwa upande mwingine uamuzi huwa sehemu fulani ya igizo au onesho na kipeo hutegemea watazamaji wanaohusika. Wakati mwingine inawezekana kusiwe kabisa na kipeo katika onesho au igizo fulani.
Maudhui
Ni jumla ya mawazo yote yanayozungumziwa pamoja na mtazamo wa mwandishi juu ya mawazo hayo. Katika maigizo ni mambo yote ambayo yamebeba matukio na vitendo katika katika igizo. Tunaweza kupima nafasi ya maigizo katika jamii kutokana na maudhui yake.
Maudhui huoneshwa katika vipengele vifuatavyo: –
(a) Dhamira
Ni mawazo/mambo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Huweza kuwa dhamira(wazo) kuu yaani jambo lililokusudiwa kiutunzi na ambalo mjadala wake umeteka igizo nzima au
dhamira ndogondogo zinazosaidia kuijenga dhamira kuu au kujitegemea zenyewe.
Dhamira hutokana na jamii, ni zao la jamii kwa vile msanii hutunga kazi fulani ya fasihi kutokana na maisha ya jamii anamoishi msanii.
Dhamira huweza kutokana na mambo mbalimbali ya kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi. mfano; Uongozi mbaya, dhuluma, unyonyaji, mmomonyoko wa maadili, uzembe kazini, ugumu wa maisha, ukoloni mamboleo n.k
(b) Falsafa
Ni msanii na jamii inaamini lipi ni ukweli wa kujikomboa au kujikwamua kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na hata kifikra. (mwelekeo wa imani ya mwandishi).
Mfano. Falsafa inaweza kutuaminisha kuwa mwanamke si chombo duni ikiwa na kusudio la kuamini kuwa viumbe wote ni sawa.
© Ujumbe na maadili
Ujumbe katika maigizo ni yale mafunzo mbalimbali tunayoyapata baada ya kuona na kusikia igizo /onesho fulani.
Ujumbe huambatana na maadili mbalimbali.
(d) Migogoro
Ni matatizo anayoyajadili msanii katika kazi yake yatokanayo na jamii anamoishi kwa njia ya uhusiano anaoufuma kisanaa kati ya wahusika anaowatumia katika kutunga kazi ya fasihi. Kupitia matatizo hayo msanii huibusha mivutano baina ya wahusika ili kuliainisha tatizo fulani katika jamii. (Ni mivutano na misuguano mbalimbali katika kazi ya fasihi inayoibua matatizo yaliyomo katika jamii ya msanii wa kazi ya fasihi.)
Yafuatayo ni muhimu yachunguzwe katika kujadili migogoro: –
i. Aina ya mgogoro (wahusika wa mgogoro)
Aina ya mgogoro yaweza kuwa wa kinafsia unapomuhusu mtu binafsi, wa mtu na mtu endapo unahusu watu wawili, wa mtu na jamii iwapo mtu anatatizana na jamii au wa jamii na jamii iwapo jamii mbili zinatatizana juu ya jambo fulani. Aina hizi za mgogoro zaweza kuwa katika nyanja yoyote ya kimaisha kama kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni n. k
ii. Chanzo cha mgogoro.
Mgogoro huo ulisababishwa na nini? chanzo chake nini? ni ipi sababu ya kutokea mgogoro huo?
iii. Mgogoro unawakilisha matatizo gani katika jamii.
iv. Suluhisho la msanii/ jinsi ulivyomalizika kitabuni.
v. Tathmini yako kuhusu suluhisho la msanii.
vi. Pendekeza suluhisho la kufaa linaloweza kutumiwa kama ufumbuzi wa matatizo kama hayo iwapo suluhisho la msanii halifai au hakuwa ametoa suluhisho lolote.
|