MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
FASIHI YA KISWAHILI NADHARIYA NA UHAKIKI: MUHADHARA WA TANO

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
FASIHI YA KISWAHILI NADHARIYA NA UHAKIKI: MUHADHARA WA TANO
#1
MUHADHARA WA TANO
          DUA
Haya ni maombi ya kawaida kwa mizimu mahususi kwa ajili ya kupata mafanikio yanayotegemewa na muombaji.
Mfano:
–   Dua fulani au kuomba mtu fulani apate rehema
(i)         TABANO
Ni manuizo ya maneno kama ya kiganga yasemwayo wakati wa shughuli ya kuzindika au kwa ajili ya kutaka mizimu au miungu ibariki uganga huo.
Mfano:
–   Wazee wetu…mwanenu kaja leo na hiki kidogo kuwataka radhi zenu….nawaomba mumpokee na kumkubalia maombi yake.
(ii)       MASIMULIZI
Ni fasihi yenye kusimulia habari fulani. Masimulizi huwa na sifa zifuatazo:
–   Mpangilio mahususi
–   Wahusika
–   Mandhari
–   Lugha ya kimaelezo
–   Utambaji
–   Maudhui ya kweli au ya kubuni yenye funzo fulani
Masimulizi yanaundwa na tanzu mbalimbali kama vile:
v Hadithi za kubuni; Hadithi hizi huweza kuwa:
(i)         Ngano au vigano
Hadithi za kimapokeo zitumiazo wahusika kama wanyama,mazimwi na watu katika kuonya na kuadibu kuhusu maisha.
(ii)       Ishara
Ni hadithi ambazo maana yake ya wazi huwakilisha maana ingine iliyofichika.
Mfano:
–   Kusadikika ni ishara kuhusu utawala wa mabavu wa kikoloni.
(iii)     Mbazi
Hadithi itolewayo kama kielelezo cha kufafanulia hadithi inayosimuliwa.
Mfano:
–   Mafundisho ya Yesu katika Biblia aliyafafanua
kwa kutumia hadithi ndani ya masimulizi.
Ipo mbazi kuhusu kisa cha mtego wa panya, mbazi hii inasimuliwa hivi; …. siku moja katika nyumba fulani panya aligundua kuwa ametegewa mtego na kwa kuwa hakuweza kuutegua alienda kuomba msaada kwa ng’ombe lakini ng’ombe alikataa akidai kuwa huo ni mtengo wa panya yeye haumuhusu. Panya hakuchoka akapiga hodi kwa mbuzi na kumlilia shida yake, mbuzi naye akamjibu kama alivyojibu ng’ombe kuwa huo ni mtego wa panya wala haunihusu. Hatimaye panya akamwendea jogoo na kueleza yote lakini jogoo naye alimkataa panya na kumkejeli kuwa huo mtego hamhusu yeye jogoo. Baada ya kugonga mwamba panya akakosa amani akihofia mtego ulioitwa.. “ …wa panya..” kwa kweli siku nzima ile panya hakuweza kujipatia riziki akihofia mtego. Usiku ulipofika baba mwenye nyumba alishituliwa na mkewe akiambiwa kuwa mtego umefyatuka na bila shaka panya atakuwa amenaswa. Baba yule akakurupuka na kuuendea mtego huku akipuuza hadhari ya mkewe kuwa asiende giza giza, alienda huku akijifariji kuwa panya hawezi kumdhuru chochote……alipoufikia mtego ule akapeleka mkono ili auchukue na kumsulubu panya aliyewasumbua kitambo. La haula! Kumbe hakuwa panya, mzee yule akarudi nyuma haraka huku akiagiza mkewe amletee taa haraka. Baada ya taa kuletwa ikabainika mtego ulinasa nyoka na hivyo mzee yule aliumwa na nyoka yule…..ghafla hamkani ikaingia ndani ya nyumba kutafuta dawa ya kumponya mzee mwenye nyumba. Muda si muda mzee yule alikata roho kwa kuzidiwa na sumu ya nyoka na nyumba ikawa na msiba. Siku ya kwanza wageni wachache ikabidi achinjwe jogoo kupata kitoweo. Siku ya pili wageni ni wengi kiasi ikabidi achinjwe mbuzi ili kukidhi mahitaji. Baada ya maziko siku ya tatu na kumaliza tanga akachinjwa ng’ombe.
Funzo:
Hivi ule mtego ulikuwa wa panya,ng’ombe,mbuzi,kuku au baba mwenye nyumba? Mbazi hii inasadifu umuhimu wa kushirikiana kuokoa mambo ambayo yakiharibika yataathiri wengi.
(iv)       Mchapo
Ni hadithi fupi aghalabu husimuliwa kwa watu wanaofahamu historia ya jambo linalotolewa mchapo huo.
Mfano:
–   Kawawa alipoambiwa afunike kikombe ughaibuni ili asiendelee kutiliwa chai hali ametosheka.
–   Mchapo wa kuchapwa viboko kwa Samwel Sitta baada ya kuongoza wanafunzi wenzake kudai siagi akiwa chuo kikuu.
(v)         Hekaya
Ni hadithi ndefu na yenye kuzingatia matukio machache ya kusisimua na ya kustaajabisha. Msuko wake hauchangamani na wahusika huwa ni wachache na bapa.
Mfano:
–   Hekaya za Abunuwasi, Alfu-lela Ulela
Moja wapo ya hekaya za Abunuwasi ni hii:
“ Abunuwasi baada ya kutofurahishwa na utawala wa mfalme wake aliamua kupanga njama za kumpa adhabu mfalme wake huyo, basi siku moja Abunuwasi akapika wali wake na ulipoiva akaufunua ili upoe naye akaendelea na shughuli zingine,baada ya muda akarudi na kukuta nzi wamejaa kwenye chakula chake. Hapo abunuwasi akazua kisa kuwa nzi wamekula harufu yote ya wali wake hivyo akamwendea mfamle ampe waraka utakaomruhusu (Abunuwasi) kuwaua nzi popote atakapowaona. Mfalme bila kujua akampa Abunuwasi waraka huo. Abunuwasi kisha kupata waraka huo akachonga rungu kubwa maalumu kwa kazi ya kuwasaka na kuwaua nzi. Siku moja mfalme akawa na karamu nyumbani kwake iliyohusisha wananchi wake wote akiwemo Abunuwasi. Katika karamu hiyo Abunuwasi alihudhuria na akaketi karibu kabisa na mfalme huku akiwa na rungu lake. Muda si muda huku sherehe ikiendelea ghafla Abunuwasi akainua lile rungu lake na kulishusha kwa nguvu kichwani kwa mfalme, mfalme alianguka palepale na kupoteza maisha. Walinzi wa mfalme walipomshika Abunuwasi akawatolea waraka wenye saini ya mfalme ukisomeka kuwa Abunuwasi ameruhusiwa kuua nzi popote atakapowaona. Basi hapo Abunuwasi akawaambia kuwa lengo lake halikuwa kumdhuru mfalme bali kumsulubu nzi aliyetua kichwani kwa mfalme huyo.”
(vi)       Salua
Ni kipengele cha kimasimulizi kinachojumuisha tanzu za kihistoria zenye kusimulia habari za zamani. Baadhi ya tanzu zake ni:
v Visakale
Ni masimulizi yanayohusu matukio yaliyopita ya kale/zamani kuhusu mashujaa wa kabila au taifa yenye kuchanganya chuku na historia.
Mfano:
–   Hadithi za Liyongo,Mkwawa,n.k
v Mapisi
Ni maelezo ya historia bila kutia maneno ya kubuni. Ni historia halisi ya mtu au kitu au jambo pasipokutiwa chuku.
Mfano:
–   Mapisi ya Tanganyika- mapisi ya historia ya kweli.
v Tarihi
Ni maelezo au jedwali la matukio muhimu na tarehe zake. Hutokea zaidi katika maandishi na huhusu matukio ya kihistoria.
v Nasaba/shajara/potifolio
Ni orodha ya wazee au wahenga wa mtu kuanzia baba,babu na wengine waliotangulia. katika baadhi ya makabila kila mtu hupaswa kufahamu majina ya wahenga wake hadi kizazi fulani.
Mfano:
–   Prof. Sengo anaweza kutaja orodha ndefu ya wahenga wake tangu kizazi cha kwanza hadi cha sasa alichopo yeye. (Tigiti-Yusuf-kibwana-Semindu-Mnyagatwa-Sengo)
–   Watu wengi wenye kuendeleza historia za makabila yao hupenda kutumia majina zaidi ya mawili (mf; John-Joseph-pombe-magufuli)
v Kumbukumbu
Ni maelezo ya matukio muhimu yanayohusu mtu binafsi au jamii ya watu. Fani za wasifu ni aina ya kumbukumbu.
Mfano:
–   Wasifu wa Siti Binti Saad
–   Dereva wa kwanza Tanganyika
–   Uhuru wa watumwa.
(vii)     Visasili
Ni hadithi za kale zenye kuwakilisha imani na mtazamo wa jamii unaohusiana na asili ya ulimwengu na mwenendo wake.
AINA ZA VISASILI
v Visasili vya usuli
Hivi ni visasili vinavyojaribu kuelezea asili ya chimbuko la taifa fulani au wanadamu kwa ujumla.
Mfano:
–   Hadithi ya wayahudi ya kuumbwa kwa ulimwengu na kutokea kwa mwanadamu (Adam na Hawa) ni mfano mzuri wa kisasili cha usuli. Baadhi ya visasili vya usuli hasa Afrika huelezea asili ya mila na desturi fulani ya jamii.
v Visasili vya ibada na dini
Visasili hivi huhusu matendo ya ibada na imani mbalimbali za dunia na mara nyingi hutungwa kisanaa (kuigizwa) katika ibada hizo.
Mfano:
–   Katika ibada za kikristo Ekaristi (kula pamoja chakula cha bwana) ni maigizo ya chakula cha mwisho alichokula Yesu Kristo na wanafunzi wake kabla ya kusulubiwa.
NB:
– Madhehebu ni makundi ya watu wanaoongozwa
na imani fulani.
–     Dini-ni kikundi cha waamini wenye
kufuata utaratibu fulani katika
kumuabudu mungu wao.
v Visasili vya miungu na mizimu
Hivi hupatikana zaidi katika mataifa yenye miungu wengi kama vile Asia, Ulaya ya kale na Misri ya kale.
Hapa Afrika visasili hivi hupatikana kwa wingi katika lugha ya Wayoruba (Nigeria) na katika falme zinazozunguka ziwa victoria (Nyanza).
  1. Maigizo (Drama)
Ni utendaji unaohusisha uigaji wa tabia na matendo ya watu au viumbe uli kuburudisha na kutoa ujumbe kwa njia ya sanaa. Drama za ki-Afrika huambatana na ngoma, utambaji, hadithi, nyimbo na matendo ya kimila kama jando na unyago. Drama nyingi hutumia maleba maalumu (mavazi maalumu) yanayovaliwa na waigizaji ili kuficha uhalisia wao.
AINA ZA MAIGIZO
(i)         Maigizo ya watoto
Watoto wanapocheza mara nyingi huigiza matendo ya kimaisha wanayoyaona katika jamii zao kama vile kulima,kupika,harusi,vita, n.k
Maigizo ya aina hiyo ni sanaa za maonesho zenye kuburudisha na kuwaelimisha watoto pamoja na kukuza vipaji vyao vya ubunifu.
(ii)       Maigizo ya misibani
Maigizo haya hufanywa na watani au wajukuu wa marehemu na huhusiana na maisha, matendo na tabia za marehemu. Maigizo haya hufanywa ili kuwapunguzia wafiwa huzuni na kutoa mafundisho kwa watu waliopo msibani kuhusiana na tabia za marehemu.
Mfano:
–   Kama marehemu alikuwa na tabia mbaya waigizaji/ watani wanaweza kuigiza kwa njia ya kejeli au dhihaka juu ya tabia hiyo.
(iii)     Maigizo ya kwenye sherehe/kidini
Sherehe nyingi za kijadi na kidini huambatana na maigizo mfano; kusimika viongozi huweza kuambatanishwa na kuvishwa aina fulani ya mavazi na kukalishwa katika viti vya asili,kusemewa baadhi ya maneno,kutemewa mate ya Baraka pamoja na kupewa vinywaji fulani kama ishara ya jambo husika.

Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)