Neno afkani katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo:
1. Nomino: [Ngeli: a-/wa-] mtu mwenye uwezo mdogo wa akili.
2. Nomino: [Ngeli: u-/u-] ugonjwa wa moyo. (Chanzo: Kamusi Kuu ya Kiswahili).
3. Nomino: [i-/i-] ugonjwa wa moyo (Chanzo: Kamusi ya Karne ya 21).
4. Kivumishi: -enye wehu, -enye upungufu wa akili.
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili afkani (soma: afkaanu أفكان) ni nomino inayotokana na kitenzi cha Kiarabu afika افك (افك:ضعف عقله وصار سفيها- imedhoofu akili yake na amekuwa safihi )
Kinachodhihiri ni kuwa neno afkani ( soma: afkaanu افكان) lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno afkani lilichukua maana ya 'wehu' na kuacha maana zingine.
Tanbihi: Kisarufi, Kamusi Kuu ya Kiswahili na ile ya Kamusi ya Karne ya 21 zimetoa ngeli mbili tofauti kulihusu neno (nomino) afkani kwa maana ya 'ugonjwa wa moyo'.
Posted by: MwlMaeda - 01-06-2022, 07:59 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
“OWENI WAKE WAWILI” ✏Oweni wake wawili
Au wanne kamili
Dada hawaihimili
Hali waliofikia. ✏Kila nyumba ina wari
Na wajane na vigori
Tupangeni mashauri
Twende kujichukulia. ✏Uma uko taabani
Na huku watu wazini
Hala hala ya jamani
Allah ameweka njia. ✏Wanawake wako wengi
Tena wapo kila rangi
Hili jambo la msingi
Lazima kufatilia. ✏Hebu tuokoe uma
Tuwaoe kina mama
Tuwafanyie huruma
Wapi watakimbilia. ✏Hal wao wakazini
Wapate kwenda motoni
Sie tuna kazi gani
Mijicho twawatolea. ✏Wana wake ni neema
Aliotupa Karima
Iko nyingi kwenye uma
Ni yetu masuulia. ✏Na dada waache wivu
Huo sio uwerevu
Wenzenu pao pakavu
Mume wajitafutia. ✏Leo hawa wasichana
Mara nne ya vijana
Yani wale wavulana
Nini watajifanyia. ✏Hapa leo yadhihiri
Hekima yake Ghafuri
Alipotoa amri
Ya wengi kujiolea. ✏Haya haya anzieni
Kuanzia thnateni
Haluwa isahanini
Na Shekhe kahudhuria. ✏Na thulatha na rubaa
Sikia ewe abaa
Madamu sio sabaa
Waweza kujiolea. ✏Tumwa ewaoa tisa
Na Mola alituasa
Kwamba yeye ni qabasa
Tuwe twamfatilia. ✏Ela Mola ehadidi
Kwenye uma Muhamadi
Wane wasiwe zaidi
Hekima yake Jalia. Sheikh Juma Al Mazrui
Posted by: MwlMaeda - 01-06-2022, 07:54 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
Shaaban Robert aliona kwamba maisha ya binadamu hayana maana yoyote iwapo hayana lengo la maisha baada ya kifo cha mwanadamu. Aliona kwamba kila tendo jema ni kidato kimoja cha ngazi inayotupeleka mbinguni.
SHAABAN Robert aliona kwamba maisha ya binadamu hayana maana yoyote iwapo hayana lengo la maisha baada ya kifo cha mwanadamu. Aliona kwamba kila tendo jema ni kidato kimoja cha ngazi inayotupeleka mbinguni.
Mara nyingi, mashairi yake kuhusu jambo hili yamo katika manung’uniko kuhusu kuharibika kwa ulimwengu. Kwake, maisha ni kitu kisichotegemeeka. Anajaribu kutueleza kutotegemeeka huku kwa maisha katika mashairi mbalimbali.
Shairi “Hubadilishana Zamu” katika kitabu chake ‘Ashiki Kitabu Hiki’ linaonyesha raha na balaa za maisha – maisha ya kumpokonya mwenye nacho huku yule asiyekuwa na chochote, ghafla akajikuta amepata. Mshairi anasema:
Wadogo kuwa wakuu, kwa watu ndio tabia,
Na wa chini kuwa juu, ni jambo la mazoea,
Mwenendo wao ni huu, wanao kama sheria,
Watu duni na wakuu, katika hii dunia.
Katika dunia hii, ya machungu na matamu,
Na rafiki na adui, na mepesi na magumu,
Viumbe walio hai, hubadilishana zamu,
Lakini hawatambui, kwa uchache wa fahamu.
Katika shairi hili, maisha yamesawiriwa kama jambo lisiloweza kutegemeeka. Ingawa hivyo, mshairi analalamika na kustaajabia jinsi wanadamu wasivyoweza kufahamu mambo yanayotokea kila siku, ya wenye navyo kuwa mafukara huku mafukara wakijikuta wamepanda ngazi ya utukufu na kuwa matajiri wa kutajika.
Baadhi ya mashairi ya Robert yanaonyesha utupu wa maisha yaliyojawa na hofu, kiwewe pamoja na wasiwasi. Kutokana na kutotegemeeka kwa maisha, mshairi anauona uokovu ukitoka kwa Mwenyezi Mungu pekee. Kwa sababu hii, mtazamo wake hautofautiani sana na jumla ya washairi wengine walioandikia mashairi katika kipindi cha historia ya uwepo wake. Shairi “Mbinguni” kutoka katika kitabu ‘Kielelezo cha Fasili’ ni sala ya Robert, akiuombea ulimwengu. Moja ya beti zake unasema:
Tutakase kila mtu, na nafsi kung’arisha,
Toa uchafu na kutu, madhila na mshawasha,
Kuwa huru kila kitu, twazidi kukukumbusha,
Kwamba ndio haja yetu, katika haya maisha,
Katika kila msitu, na bahari ya maisha,
Lakini kusudi letu, E Mwenyezi kamilisha.
Shairi hili ni maombi ya Robert asikate tamaa katika maisha ya duniani na ya ulimwengu wa pili kama inavyodhihirishwa na maneno “E Mwenyezi kamilisha”. Vilevile anaomba dhambi ziyeyuke ili wanadamu wawe waadilifu na kuuona wema daima ukiushinda uovu.
Wakati uo huo, anapoomba maisha yenye baraka na thawabu, mshairi anazungumzia uzuri wa dunia, lakini tena katika misimgi ya kidini. Shairi “Dunia Njema” kutoka katika kitabu ‘Ashiki Kitabu Hiki’ linadokeza hivi:
Dunia nzuri, ina mambo yake,
Yana fahari, ya peke yake,
Juu sayari, ni taa zake,
Chini johari, ardhi yake.
Zulia lake, nyasi kijani,
Na maji yake, mvua mbinguni,
Kushuka kwake, milele shani,
Na sifa zake, Mola Manani.
Katika beti hizi, mshairi anazungumzia dunia na ulimbwende uliomo ndani yake. Mambo haya ni ya fahari kuu na anayaeleza kwa njia ya kutamanisha. Ingawa hivyo, mshairi anatukumbusha kuwa uzuri huu ni hisani aliyotendewa mwanadamu na Mungu wake. Kwa sababu dunia ni pambo la tunu, mwanadamu anashauriwa amsifu na daima kumwabudu Mungu kwa kumpambia dunia nzuri ambayo ni makazi yake. Ili kufanikiwa kufikisha ujumbe wake kwa binadamu, Mungu huwapa wanadamu ufunuo wenye ukweli.
Kweli inayozungumziwa na mshairi katika nyingi za tungo zake inaweza kugawanywa mara mbili: Kweli kama inavyodhihirika hapa duniani na kweli ya ulimwengu wa pili. Kweli ya duniani inahusu uhusiano baina ya mwanadamu na mwanadamu mwenzake ilhali kweli ya pili inahusu ukaribu wa binadamu na Mungu wake. Kweli ya pili ndiyo inayosisitizwa sana na mshairi katika utunzi wake. Kweli ya aina ya kwanza inajitokeza katika shairi “Kweli” katika kitabu chake ‘Pambo La Lugha’ linalosema:
Siche kweli kuisema, hata kwa mfalme,
Ingawa inauma, sema kweli atazame,
Kweli ina heshima, wajibu wa mwanamume,
Uongo una lawama, ufukuzeni uhame.
Kweli ina thawabu, wametumia mitume,
Japo wamepata tabu, wamerithi ufalme,
Na waliowaadhibu, hawakumbukwi kamwe,
Kweli ina thawabu, kila mtu aseme.
Tunaweza kuitilia shaka kweli hii inayozungumziwa na Robert na kudadisi iwapo ni sharti useme kweli wakati wowote na mahala popote. Kweli kama hii ina hatari yake na huenda ikamtia mtu matatani, hasa asipojiandaa vilivyo kukabiliana na watu ambao hawapendi ukweli usemwe. Kwa sababu hiyo, ni lazima kila msema-kweli ajitahadhari ili kukabiliana vilivyo na athari zozote za watu wasiouthamini ukweli.
Kwa upande mwingine, shairi “Kweli” kutoka katika kitabu ‘Insha na Mashairi’ linasisitiza kweli inayoambatana na misingi ya kidini:
Kweli luluye Jalali, fahariye bwana Mungu,
Mtenzi huwa imara, sababu kweli kamili,
Kitu hiki cha busara, kinatangua batili.
Kweli luluye Jalali, fahariye bwana Mungu,
Mtenda hili amini, huaminiwa mahali,
Ana zawadi peponi, mtu aliye na kweli.
Katika beti hizi, kweli inaambatanishwa na utukufu wa peponi. Mshairi anaitazama kweli kama ngazi mojawapo inayotufanya tupate kiingilio cha ufalme na utakaso.
Neno *ahadharau* katika lugha ya Kiswahili ni *nomino [Ngeli:i-/zi-]* yenye maana zifuatazo:
1. Rangi ya kijani.
2. Yenye rangi ya kijani kibichi.
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *ahadharau* si neno la Kiarabu bali ni mseto wa maneno mawili ya Kiarabu.
Sarufi ya Kiarabu imeweka jinsia katika nomino, viwakilishi na vivumishi vya Kiarabu. Kwa mfano, rangi nyeupe ikikusudiwa kwa jinsia ya kiume huitwa abyadh (soma: *abyadhwu* *ابيض* ) na ikikusudiwa kwa jinsia ya kike huitwa *baydhaa* (soma: *baydhwaau* *بيضاء* ). Hivyo hivyo, rangi nyeusi itakuwa *aswadu/sawdaau* , nyekundu itakuwa *ahmaru/hamraau,* njano itakuwa *aswfaru/swafraau* na rangi ya kijani ni *akh-dhwaru* (kwa jinsia ya kiume) na *khadhw-raau* (kwa jinsia ya kike).
Sasa neno *ahadharaau* ni neno jipya ambalo unaweza kulirejesha kwenye mseto wa maneno mawili ( *akhdhwaru na khadhwraau* ).
Kwamba wamechukua herufi *a* katika neno *akhdhwaru* wakaliweka mwanzoni mwa neno *khadhwraau* na kupata neno jipya *akhdhwaraau* ambalo walipolitohowa kwa kuondoa herufi (k) kutoka (kh/خ) na herufi (dhw ض) wakaifanya herufi (dh/ذ) wakapata neno jipya la Kiswahili *ahadharau*.
Kinachodhihiri ni kuwa neno *ahadharau* limechukua maana ya maneno *akhdhwaru* na *khadhwraau* katika lugha ya Kiarabu.
HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO ' AGHALABU/AGHLABU' NA 'NADRA'
Neno aghalabu/aghlabu katika lugha ya Kiswahili ni kielezi chenye maana ya mara nyingi, kwa kawaida, mara kwa mara.
Mifano:
1. Nyota nyingi aghalabu/aghlabu huonekana usiku.
2. Watu wanaofanya mazoezi, aghalabu/aghlabu huwa na afya njema.
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili aghalabu/aghlabu (soma: aghlabu/aghlaba اغلب) ni nomino yenye maana zifuatazo:
1. Mtu mwenye shingo nene.
2. Mnyama simba.
3. Mwenye nguvu.
4. Mara nyingi.
Neno nadra katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo:
1. Nomino: [Ngeli: i-/zi-] uchache wa vitu au mambo kwa nadra mara chache sana.
Mfano : Tunaonana kwa nadra siku hizi.
Methali: Heri huenda mara kwa mara kwa wajasiri, nadra huenda kwa walegevu.
2. Kivumishi : -a uchache, haba, kidogo sana, -siyopatikana kwa urahisi.
Mfano : Siku hizi asali ni nadra sana kupatikana.
Katika lugha ya Kiarabu neno ' nadra ' ( soma: naadiratu/naadiratan/naadiratin نادرة/ nadiratun ندرة) lina maana zifuatazo:
1. Kinachopatikana kwa uchache sana, mfano: kitaabun naadirun.
2. Kitu kulichoadimika.
3. Jambo au kitu kinachotokea mara moja moja.
Kinachodhihiri ni kuwa neno aghalabu/aghlabu ( soma: aghlabu/aghlaba اغلب) lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno aghalabu lilichukua maana ya ' mara nyingi' na kuziacha maana zingine, kama ambavyo neno ' nadra ' ( soma: naadiratun/naadiratan/naadiratin نادرة/nadiratun/nadiratan/nadiratin ندرة) lilipoingia katika Kiswahili lilichukua maana ya ' mara chache' na kuziacha maana zingine.
Posted by: MwlMaeda - 01-05-2022, 07:37 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
Hino naswaha twajipa, Mbaruku ni amana
Tumwombe hatwendi kapa, Mola wetu Subhana
Awape na wasotupa, pengine wao hawana Tupawapo si kuhepa, na mato kuyakodoa
Tumwombe Mola kwa hapa, mwenye sifa ziso doa
Awape na wasotupa, nao wapate kutoa Ukipawa fanya pupa, wewe nawe kupeana
Si nofu hata kifupa, na Mngu atakuona
Atawapa wasokupa, na hali mutafanana Tusijitie kishipa, kumfunzia Rabbana
Ukata kutoogopa, kupata ni kupanana
Awape wasiotupa, nao waanze kupana
Mkata hutapatapa, funguni simuondoe
Muombee kutokopa, Allaah amfungulie
Awape na wasokupa, ili na wao watoe Wenye roho za kupapa, kijito kiwaepuke
Madeni wasiolipa, Mwenyezi awatunuke
Awape wasiotupa, hasadi iwaondoke Sitaguwe wa kuwapa, Bwana Mngu si fakiri
Omba dua iso dupa, duwara iduru dori
Awape wasiotupa, kwani Mngu ni tajiri