ETIMOLOJIA YA NENO ' AGHALABU/AGHLABU' NA 'NADRA' - Printable Version +- JIFUNZE KISWAHILI (https://jifunzekiswahili.co.tz) +-- Forum: My Category (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=1) +--- Forum: Majadiliano ya Wadau wa Kiswahili (https://jifunzekiswahili.co.tz/forumdisplay.php?fid=16) +--- Thread: ETIMOLOJIA YA NENO ' AGHALABU/AGHLABU' NA 'NADRA' (/showthread.php?tid=2025) |
ETIMOLOJIA YA NENO ' AGHALABU/AGHLABU' NA 'NADRA' - MwlMaeda - 01-05-2022 HII NDIYO ETIMOLOJIA YA NENO ' AGHALABU/AGHLABU' NA 'NADRA' Neno aghalabu/aghlabu katika lugha ya Kiswahili ni kielezi chenye maana ya mara nyingi, kwa kawaida, mara kwa mara. Mifano: 1. Nyota nyingi aghalabu/aghlabu huonekana usiku. 2. Watu wanaofanya mazoezi, aghalabu/aghlabu huwa na afya njema. Katika lugha ya Kiarabu, neno hili aghalabu/aghlabu (soma: aghlabu/aghlaba اغلب) ni nomino yenye maana zifuatazo: 1. Mtu mwenye shingo nene. 2. Mnyama simba. 3. Mwenye nguvu. 4. Mara nyingi. Neno nadra katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo: 1. Nomino: [Ngeli: i-/zi-] uchache wa vitu au mambo kwa nadra mara chache sana. Mfano : Tunaonana kwa nadra siku hizi. Methali: Heri huenda mara kwa mara kwa wajasiri, nadra huenda kwa walegevu. 2. Kivumishi : -a uchache, haba, kidogo sana, -siyopatikana kwa urahisi. Mfano : Siku hizi asali ni nadra sana kupatikana. Katika lugha ya Kiarabu neno ' nadra ' ( soma: naadiratu/naadiratan/naadiratin نادرة/ nadiratun ندرة) lina maana zifuatazo: 1. Kinachopatikana kwa uchache sana, mfano: kitaabun naadirun. 2. Kitu kulichoadimika. 3. Jambo au kitu kinachotokea mara moja moja. Kinachodhihiri ni kuwa neno aghalabu/aghlabu ( soma: aghlabu/aghlaba اغلب) lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno aghalabu lilichukua maana ya ' mara nyingi' na kuziacha maana zingine, kama ambavyo neno ' nadra ' ( soma: naadiratun/naadiratan/naadiratin نادرة/nadiratun/nadiratan/nadiratin ندرة) lilipoingia katika Kiswahili lilichukua maana ya ' mara chache' na kuziacha maana zingine. Shukran sana. Khamis S.M. Mataka. |