Posted by: MwlMaeda - 01-10-2022, 08:35 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
KIFO
Kifo kimekuwa siri, aijuwaye Mwenyezi
Kaficha Mola Jabbari, hakutaka kiwe wazi,
Huja pasipo habari, fumbo hili hatuwezi,
Leo yule kesho mimi, kila nafsi itakufa.
Kifo hakina fulani, kuchaguwa kama nazi,
Alipangalo Manani, binadamu huliwezi,
Wote wake ikhiwani, Muumbaji mwenye enzi,
Leo yule kesho mimi, kila nafsi itakufa.
Kifo kipo ujinini, hakinacho ubaguzi,
Mbinguni na aridhini, atabakia Mwenyezi,
Kaenda Suleimani, na Muhammad kipenzi,
Leo yule kesho mimi, kila nafsi itakufa.
Kifo huja kitandani, kiwa tele usingzi,
Hakina habari gani, japo hili umaizi,
Kifo hakijui nani, mjomba wala shangazi,
Leo yule kesho mimi, kila nafsi itakufa.
Kifo hujuwa Dayani, Mola aliye mlezi,
Kichwa naye kaburini, msizione tungizi,
Ati champata nini, hamtamwona mtunzi,
Leo yule kesho mimi, kila nafsi itakufa.
Kifo kipo kila nafsi, hukifichi kwa irizi,
Chozi lanitoka Rasi, kuandika sikuwezi,
Kaditama nisihasi, niliache simulizi,
Leo yule kesho mimi, kila nafsi itakufa.
Posted by: MwlMaeda - 01-10-2022, 08:29 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
WASIA Naapa kwa nyota tano, angani zinoelea
Na kwa huu muagano, niuyako narejea
Ushike wasia huno, ambao nakumegea
Kifo chaninyemelea, yashike yangu maneno
Kuno kunena kwa wino, mosi kinywa chalemea
Yamepukutika meno, na fizi kunilegea
Udenda kumwaga kuno, wema ‘siche nitendea
Kifo chaninyemelea, yashike yangu maneno
Ndoa ni maridhiano, huyuno ‘metuletea
Ufakiri siyo neno, ata ungaselelea
Usitembeze kiuno, viwavi kujiletea
Kifo chaninyemelea, yashike yangu maneno
Mazishi ya jumatano, juma lililopotea
Kisa’che ndiyo mguno, mwenzio kujifyelea
Sitaki wende hivino, waambe sijakulea
Kifo chaninyemelea, yashike yangu maneno
Chukua wangu mfano, nisiloona umbea
Simcha wa malumbano, na ovyo kujisemea
Madhila yakiwa mno, Mola namuelekea
Kifo chaninyemelea, yashike yangu maneno
Busara yake mavuno, wema ukuongezea
Pamwe hekima vivino, amani ukuletea
‘Kiabudu mivutano, dhiki utaogelea
Kifo chaninyemelea, yashike yangu maneno
Ikiwa mfarakano, ndoani umetokea
Yaepuke mapambano, lengo usirudi bea
Samahani huwa chano, hasira zinapomea
Kifo chaninyemelea, yashike yangu maneno
Kutetemeka mkono, ambavyo wajionea
Ni kwakuja kwake yuno, uhai ‘nojibebea
Kutokwa roho ndo kuno?, sina cha kuongezea
Kifo chaninyemelea, yashike yangu maneno
Neno kadhia katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo:
1. Nomino: [Ngeli: i-/zi- ] jambo linalofanyika.
2. Nomino: [Ngeli: i-/zi-] tukio lililojiri.
3. Nomino: [Ngeli: i-/zi-] mkasa uliomfika mtu.
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili kadhia *(soma: *qadhwiyyatu/qadhwiyyatan/qadhwiyyatin قضية ) ni nomino yenye maana zifuatazo:
1. Hukumu itolewayo na chombo cha kutoa maamuzi.
2. Suala linalobishaniwa na lilifikishwa kwa jaji/majaji kwa ajili ya kusikilizwa na kutolewa hukumu.
3. Mambo yanayohusu tapo maalumu katika jamii; qadhwiyyatun siyaasiyyat قضية سياسية kadhia ya kisiasa, qadhwiyyatun ijtimaaiyyat قضية اجتماعية kadhia ya kijamii, qaadhwiyatu Filistwiin قضية فلسطين kadhia ya Palestina.
Kinachodhihiri ni kuwa neno kadhia (soma: *qadhwiyyatu/qadhwiyyatan/qadhwiyyatin قضية )ilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno kadhia lilibeba maana ya jumla ya tukio lililojiri au jambo linalofanyika.
Posted by: MwlMaeda - 01-10-2022, 06:35 AM - Forum: Ushairi
- No Replies
SINA NAFUU
Kula mie ninakula, bila kula sijilazi,
Langu tatizo kulala, japo ni mema malazi,
Najaribu Ila wala, siupati usingingizi,
Yananitesa mapenzi, mwenzenu sina nafuu.
Daima ninamuwaza, mwendani wangu lazizi,
Vile ananipuuza, ninakonda siku hizi,
Hata nikimueleza, hunita mie mpuzi,
Yananitesa mapenzi, mwenzenu sina nafuu.
Ashiki mwili mzima, kuhimili siiwezi,
Jamani nisijezima, inikatike pumzi,
Msione nalalama, hali yangu sijiwezi,
Yananitesa mapenzi, mwenzenu sina nafuu.
Usiku wa katikati, ninakesha kama mwizi,
Nadhani sina bahati, au tatizo ujuzi,
Moyo wangu hatihati, yanimwagika machozi,
Yananitesa mapenzi, mwenzenu sina nafuu.
Kiwa kuna matibabu, inifae hiyo dozi,
Niondokewe taabu, niwe kama mwaka juzi,
Leo yanayonibu, kusimulia siwezi,
Yananitesa mapenzi, mwenzenu sina nafuu.
Ninazidi kuteseka,vile sina muuguzi,
Wengine wananicheka, eti mie siyawezi,
Donda limenifumuka, maumivu hayapozi,
Yananitesa mapenzi, mwenzenu sina nafuu.
Neno amiri katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo:
1. Nomino: [Ngeli: a-/wa-, wingi: maamiri ] mtoto wa mfalme; mwana mfalme.
2. Nomino: [Ngeli: a-/wa-] kiongozi mwenye mamlaka ya kutoa amri.
Mfano: kiongozi mkuu, amiri jeshi mkuu: mtu mwenye cheo kikubwa kijeshi anayetoa mwongozo kwa wanajeshi wengine walio chini yake.
2. Kitenzi si elekezi: amir.i anza kufanya jambo; anzisha ( Minyumbuliko : amiria, amirika, amirisha, amiriwa.)
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili amiri(soma: amiirun/amiiran/amiirin امير) ni nomino inayotokana na kitenzi cha Kiarabu amura أمر ameamrisha , lenye maana: mwenye kutoa amri.
Maana zingine za neno (amiri) katika Kiarabu ni:
1. Mfalme
2. Mtoto wa mfalme.
3. Mtawala.
4. Mshauri.
5. Jirani.
6. Lakabu ya kiongozi wa Waislamu, amiru al-Muuminiina (soma: Amirul Muuminiina Kiongozi Mkuu wa Waislamu امير المؤمنين ).
Kinachodhihiri ni kuwa neno amiiri (soma: amiirun/amiiran/amiirin امير ) lilipoingia katika Kiswahili na kutoholewa kuwa neno amiri lilichukua baadhi ya maana zake kutoka Kiarabu na kuziacha maana zingine.
Neno *halmashauri* katika lugha ya Kiswahili lina maana zifuatazo:
1. *Nomino: [Ngeli: i-/zi-]* kikundi cha watu waliochaguliwa au kuteuliwa kufanya kazi ya kuwa watawala, watunga sheria, washauri au kuelekeza jambo fulani.
2. *Nomino: [Ngeli: i-/zi-]* chombo cha kiutawala katika wilaya au mji.
2. *Nomino: [Ngeli: i-/zi-]* kundi la watu waliochaguliwa au kuteuliwa kuelekeza utendaji wa shughuli fulani.
Katika lugha ya Kiarabu, neno hili *halmashauri* ni naneno mawili ya Kiarabu yaliyowekwa pamoja; neno *ahlu* (soma: *ahlu/ahla/ahli اهل)* lenye maana ya *watu, -enye,* na neno *mashauri* (soma:*mashuuratun /mashuuratan/mashuuratin* *مشورة* ) pia *mash-wara* (soma: *mash-waratun/mash-waratan/mash-waratin مشورة)* lenye maana zifuatazo:
1. Kinachotolewa nasaha kwa rai au namna nyingine.
2. Ushauri.
3. Nasaha, muongozo.
Kinachodhihiri ni kuwa maneno haya mawili *ahlu mashuurat/mash-warat* yaliipoingia katika Kiswahili na kutoholewa, neno jipya la Kiswahili *halmashauri* lilipatikana.
Katika lugha ya Kiarabu neno *shuuraa شورى* linatumika kwa kisawe cha maneno *mashuurat مشورة* na *mash-warat مشورة* na hupatikana misamiati *ahlu al-shuuraa* (soma: *ahlush shuraa اهل الشورى washauri)* na *majlis al-shuuraa* (soma: *majlisush shuraa مجلس الشورى baraza la ushauri; bunge).*