MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MyBB Internal: One or more warnings occurred. Please contact your administrator for assistance.
MASHAIRI YA SHAABAN ROBERT YANAVYOJADILI DINI NA BINADAMU

Thread Rating:
  • 0 Vote(s) - 0 Average
  • 1
  • 2
  • 3
  • 4
  • 5
MASHAIRI YA SHAABAN ROBERT YANAVYOJADILI DINI NA BINADAMU
#1
Shaaban Robert aliona kwamba maisha ya binadamu hayana maana yoyote iwapo hayana lengo la maisha baada ya kifo cha mwanadamu. Aliona kwamba kila tendo jema ni kidato kimoja cha ngazi inayotupeleka mbinguni.
SHAABAN Robert aliona kwamba maisha ya binadamu hayana maana yoyote iwapo hayana lengo la maisha baada ya kifo cha mwanadamu. Aliona kwamba kila tendo jema ni kidato kimoja cha ngazi inayotupeleka mbinguni.
Mara nyingi, mashairi yake kuhusu jambo hili yamo katika manung’uniko kuhusu kuharibika kwa ulimwengu. Kwake, maisha ni kitu kisichotegemeeka. Anajaribu kutueleza kutotegemeeka huku kwa maisha katika mashairi mbalimbali.
Shairi “Hubadilishana Zamu” katika kitabu chake ‘Ashiki Kitabu Hiki’ linaonyesha raha na balaa za maisha – maisha ya kumpokonya mwenye nacho huku yule asiyekuwa na chochote, ghafla akajikuta amepata. Mshairi anasema:
Wadogo kuwa wakuu, kwa watu ndio tabia,
Na wa chini kuwa juu, ni jambo la mazoea,
Mwenendo wao ni huu, wanao kama sheria,
Watu duni na wakuu, katika hii dunia.
Katika dunia hii, ya machungu na matamu,
Na rafiki na adui, na mepesi na magumu,
Viumbe walio hai, hubadilishana zamu,
Lakini hawatambui, kwa uchache wa fahamu.
Katika shairi hili, maisha yamesawiriwa kama jambo lisiloweza kutegemeeka.  Ingawa hivyo, mshairi analalamika na kustaajabia jinsi wanadamu wasivyoweza kufahamu mambo yanayotokea kila siku, ya wenye navyo kuwa mafukara huku mafukara wakijikuta wamepanda ngazi ya utukufu na kuwa matajiri wa kutajika.
Baadhi ya mashairi ya Robert yanaonyesha utupu wa maisha yaliyojawa na hofu, kiwewe pamoja na wasiwasi. Kutokana na kutotegemeeka kwa maisha, mshairi anauona uokovu ukitoka kwa Mwenyezi Mungu pekee. Kwa sababu hii, mtazamo wake hautofautiani sana na jumla ya washairi wengine walioandikia mashairi katika kipindi cha historia ya uwepo wake. Shairi “Mbinguni” kutoka katika kitabu ‘Kielelezo cha Fasili’ ni sala ya Robert, akiuombea ulimwengu. Moja ya beti zake unasema:
Tutakase kila mtu, na nafsi kung’arisha,
Toa uchafu na kutu, madhila na mshawasha,
Kuwa huru kila kitu, twazidi kukukumbusha,
Kwamba ndio haja yetu, katika haya maisha,
Katika kila msitu, na bahari ya maisha,
Lakini kusudi letu, E Mwenyezi kamilisha.
Shairi hili ni maombi ya Robert asikate tamaa katika maisha ya duniani na ya ulimwengu wa pili kama inavyodhihirishwa na maneno “E Mwenyezi kamilisha”. Vilevile anaomba dhambi ziyeyuke ili wanadamu wawe waadilifu na kuuona wema daima ukiushinda uovu.
Wakati uo huo, anapoomba maisha yenye baraka na thawabu, mshairi anazungumzia uzuri wa dunia, lakini tena katika misimgi ya kidini. Shairi “Dunia Njema” kutoka katika kitabu ‘Ashiki Kitabu Hiki’ linadokeza hivi:
Dunia nzuri, ina mambo yake,
Yana fahari, ya peke yake,
Juu sayari, ni taa zake,
Chini johari, ardhi yake.
Zulia lake, nyasi kijani,
Na maji yake, mvua mbinguni,
Kushuka kwake, milele shani,
Na sifa zake, Mola Manani.
Katika beti hizi, mshairi anazungumzia dunia na ulimbwende uliomo ndani yake. Mambo haya ni ya fahari kuu na anayaeleza kwa njia ya kutamanisha. Ingawa hivyo, mshairi anatukumbusha kuwa uzuri huu ni hisani aliyotendewa mwanadamu na Mungu wake. Kwa sababu dunia ni pambo la tunu, mwanadamu anashauriwa amsifu na daima kumwabudu Mungu kwa kumpambia dunia nzuri ambayo ni makazi yake. Ili kufanikiwa kufikisha ujumbe wake kwa binadamu, Mungu huwapa wanadamu ufunuo wenye ukweli.
Kweli inayozungumziwa na mshairi katika nyingi za tungo zake inaweza kugawanywa mara mbili: Kweli kama inavyodhihirika hapa duniani na kweli ya ulimwengu wa pili. Kweli ya duniani inahusu uhusiano baina ya mwanadamu na mwanadamu mwenzake ilhali kweli ya pili inahusu ukaribu wa binadamu na Mungu wake. Kweli ya pili ndiyo inayosisitizwa sana na mshairi katika utunzi wake. Kweli ya aina ya kwanza inajitokeza katika shairi “Kweli” katika kitabu chake ‘Pambo La Lugha’ linalosema:
Siche kweli kuisema, hata kwa mfalme,
Ingawa inauma, sema kweli atazame,
Kweli ina heshima, wajibu wa mwanamume,
Uongo una lawama, ufukuzeni uhame.
Kweli ina thawabu, wametumia mitume,
Japo wamepata tabu, wamerithi ufalme,
Na waliowaadhibu, hawakumbukwi kamwe,
Kweli ina thawabu, kila mtu aseme.
Tunaweza kuitilia shaka kweli hii inayozungumziwa na Robert na kudadisi iwapo ni sharti useme kweli wakati wowote na mahala popote. Kweli kama hii ina hatari yake na huenda ikamtia mtu matatani, hasa asipojiandaa vilivyo kukabiliana na watu ambao hawapendi ukweli usemwe. Kwa sababu hiyo, ni lazima kila msema-kweli ajitahadhari ili kukabiliana vilivyo na athari zozote za watu wasiouthamini ukweli.
Kwa upande mwingine, shairi “Kweli” kutoka katika kitabu ‘Insha na Mashairi’ linasisitiza kweli inayoambatana na misingi ya kidini:
Kweli luluye Jalali, fahariye bwana Mungu,
Mtenzi huwa imara, sababu kweli kamili,
Kitu hiki cha busara, kinatangua batili.
Kweli luluye Jalali, fahariye bwana Mungu,
Mtenda hili amini, huaminiwa mahali,
Ana zawadi peponi, mtu aliye na kweli.
Katika beti hizi, kweli inaambatanishwa na utukufu wa peponi. Mshairi anaitazama kweli kama ngazi mojawapo inayotufanya tupate kiingilio cha ufalme na utakaso.
Mwl Maeda
Reply


Forum Jump:


Users browsing this thread: 1 Guest(s)